UHURU 08.09.2005

 

 

 

Dk. Salmin amnadi Rais Karume na kusema:

·        Wazanzibari msichague watu wanaoomba ‘kula’

·        Bali wagombea wa CCM wanaotaka kuwatumikia

·        Awaasa wampigie Karume kura zote za ndiyo

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

WAZANZIBARI wametahadharishwa kuwa makini katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutowapigia kura wanaoomba 'kula', badala ya kuomba kazi ya kuwatumikia wananchi.

Ushauri huo ulitolewa mjini hapa kwenye viwanja vya Kibandamaiti, unaojulikana pia kwa jina la uwanja wa Demokrasia, na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Zanzibar, Dk. Salmin Amour.

Amewaasa Wazanzibari katika uchaguzi mkuu ujao kuichagua CCM kwa kumpigia kura zote Amani Abeid Karume na wagombea wote wa CCM wa ubunge, uwakilishi na udiwani ili CCM iendelee kudumisha mafanikio ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

"CCM ni chama cha watu wote, kisicho na ubaguzi, cha masikini na matajiri. CCM ndiyo inayojali maslahi ya wote na kuleta maendeleo. Ichagueni CCM iendelee kuongoza nchi," alisema Dk. Salmin katika mkutano huo uliyohudhuriwa na maelfu ya wana CCM na wananchi.

 "Ndugu wana-CCM na wananchi kwa utaratibu wetu kila baada ya miaka mitano viongozi wote akiwemo rais, wabunge, wawakilishi na madiwani hurejea kwenu kuja kuomba ridhaa ya kuongoza. Lakini uchaguzi unapofika wapo wanaoomba kura na wanaoomba 'kula'.

 "Jihadharini na msiwachague wanaoomba 'kula. Chagueni CCM inayoomba kura, kwa maana ya kuomba kazi ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wote," alisema Dk. Salmin katika mkutano huo wa kampeni kumnadi mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Rais Amani Abeid Karume.

 Alirudia kuwatahadharisha Wazanzibari wasiuchague upinzani kuongoza nchi, kwa sababu wanayapinga Mapinduzi na wanakerwa na maneno 'Mapinduzi Daima'.

 Alisema Mapinduzi Daima maana yake ni kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi na nchi yao, lakini wapinzani wanaibadilisha maana hiyo kwa kusababisha kuchukiana, kuumizana, kusumbuana na kuuana.

 "Hiyo siyo maana ya Mapinduzi Daima. Mapinduzi Daima maana yake ni kuleta maendeleo ya haraka kwa nchi na wananchi wake," alifafanunua na kuongeza "wanaokuja kwenu kuomba kuchaguliwa kwa chuki hawafai, hawajaiva".

 

 

 

 

Lwakatare wa CUF aonja ‘joto ya jiwe’

·        Mkutano wake Bukoba wakosa watu

·        Wamiminika kwa mgombea wa CCM

Na Angela Sebastian, Bukoba

MGOMBEA wa ubunge jimbo la Bukoba mjini kupitia tiketi ya chama cha CUF, Wilfred Lwakatare jana alijukuta akipigwa butwaa baada ya mkutano wake aliokuwa ameuandaa katika kata ya Ijuganyondo kukimbiwa na watu na kwenda katika mkutano wa kampeni wa mgombea wa CCM, Khamisi Kagasheki.

Lwakatare alijikuta mkutano wake unahudhuriwa na viongozi wa wilaya wa CUF na watu wachache mno tofauti na ilivyozoeleka ambapo hujaa umati wa watu, mashabiki na wafuasi wake.

Hali hiyo iliyomtisha Lwakatare ilitokea katika viwanja vya kata ya Ijuganyondo nje kidogo ya mji wa Bokoba.

Wafuasi hao wa CUF kuukimbia mkutano huo kulitokana na mgombea wa CCM wa jimbo hilo, Kagasheki kuteka kundi kubwa la wananchi katika mkutano wake uliofanyika katika viwanja vya Kibeta alikozaliwa Lwakatare.

Wakati huo huo, watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CUF wameanza fujo ambapo juzi walilishambulia gari la Katibu Mwenezi wa CCM Bukoba Mjini, Hassan Mnyonge na kulipasua vioo wakati akitokea Ijuganyondo katika shughuli za Chama.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Bukoba Mjini, Cosmas Kasangani alibainisha hayo jana wakati wa mkutano wa kampeni za kuwanadi wagombea wa CCM katika viwanja vya Kibeta nje kidogo ya hapa.

Baadhi ya viongozi wa CUF walipoulizwa juu ya tukio hilo walikana na kudai kuwa hawajahusika na tukio hilo la kuvunjwa vioo kwa gari hilo la kiongozi wa CCM.

Aidha, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, David Saibul alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema kuwa hana taarifa yoyote na kwamba hayo ni majungu ya mitaani.

Akihutubia katika mkutano huo, Kagasheki alisema kuwa endapo atachaguliwa atafunga mtambo wa kuzuia radi katika shule ya msingi Kibeta ambapo mwaka huu ilisababisha mauaji ya watoto tisa kwa mkupuo.

Ahadi hiyo ilitokana na wananchi kudai kuwa mbunge aliyekuwepo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita hakuweza kuliona hilo na aliwadanganya kwa kuwaambia  atawafungia mtambo huo ambapo mpaka sasa wanafunzi na walimu wa shule hiyo wako shakani pindi mvua inaponyesha.

 

 

 

 

Ngawaiya: Keenja amepata fedha Benki ya Dunia kuibadili Manzese

·        Asihi wananchi kutoziacha kwa kumchagua mwingine

·        Evodi Mmanda asema Lipumba alishindwa kazi Ikulu

Na Mwandishi  Wetu

ALIYEKUWA mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini kupitia Tanzania Labour Party (TLP), Thomas Ngawaiya amesema mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo (CCM) Charles Keenja amepata msaada wa fedha toka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuiendeleza Manzese.

Ngawaiya ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika jana kwenye kiwanja cha Manzese Madizini aliwaonya wananchi kutokubali kuzipoteza fedha hizo ambazo zimelenga kuibadili Manzese kuwa kama Ulaya.

Alisema vyama vya upinzani ni sawa na gari lenye rangi mpya, lakini injini yake imechakaa na kufafanua kuwa wapinzani wana rangi mpya, lakini wamechakaa na hivyo hawezi kulisukuma gurudumu la maendeleo.

Ngaiwaya alisema jogoo la miaka 10 haliwiki na alimfananisha mgombea urais wa TLP, Augustine Mrema sawa na jogoo la miaka 10 ambalo halina thamani zaidi ya kuchinjwa.

Akimpigia kampeni Keenja alisema kuwa mgombea huyo ambaye ni Waziri wa Kilimo na Chakula amefanya kazi kubwa kiasi cha kuifanya Tanzania isikumbwe na baa la njaa.

Ngawaiya alisema Keenja amefanya mambo mengi tangu akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Jiji hadi Waziri na nafasi zote hizo amezitumikia vizuri na anastahili kupewa tena ubunge.

Alisema kuwa alianza kufanya kampeni kwa ajili ya wagombea ubunge wa CCM, Moshi Vijijini, Vunjo na sasa yuko Ubungo na kazi hiyo ataendelea hadi mwisho.

Naye aliyekuwa mwanasheria wa NCCR-Mageuzi, Evodi Mmanda akihutubia mkutano huo wa kampeni alisema kuwa Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alikuwa mshauri wa uchumi wa Rais, alishindwa kuifanya kazi vizuri.

Alisema Profesa Lipumba hakuwa mshauri mzuri wa masuala ya uchumi ndiyo maana alikimbia na kwamba hivi sasa amejiunga na vikundi vya vijana wanaotembea na mapanga ‘shashasha'.

Mmanda alisema kuwa Profesa Lipumba badala ya kufikiria njia za kukuza uchumi amekuwa akitoa kauli za kuashiria shari kwa kuwachochea vijana.

Akimzungumzia Mrema, Mmanda alisema kuwa Mrema alifukuzwa kazi na Rais Ali Hassan Mwinyi kwa utovu wa nidhamu na hivyo hana sifa ya kuwa kiongozi wa nchi hii.

 

 

Wapinzani wanaoshawishi watu kuichukia CCM wamekosa fadhila

·        Mama Salma Kikwete asema ndiyo iliyowalea kisiasa kufikia walipo

Na Mwandishi Wetu

TABIA ya wapinzani ya kuwashawishi wananchi kuichukia CCM ni dalili zinazodhihirisha jinsi viongozi hao walivyokosa fadhila kwa Chama ambacho kimewalea.

“Msiwasikilize kwa sababu wanawadanganya,” alisema Mke wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Mama Salma Kikwete.

Mama Salma ambaye alikuwa akihutubia umati wa wanawake waliohudhuria mkutano uliofanyika jana jimbo la Ukonga, alisema wapinzani wanaichukia CCM kutokana na kukosa fadhila, kwani ndiyo iliyowasomesha na kisha kuwakuza katika medani za kisiasa.

Mkutano huo ulioandaliwa na Jumuia ya Wanawake (UWT), mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa ni sehemu ya ziara yake iliyoandaliwa na UWT kwa lengo la kuwahamasisha wanawake kuipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu ujao ambapo ziara hiyo inaendelea leo, wilayani Kinondoni.

Alisema pamoja na kampeni mbaya wanazoendesha dhidi ya CCM, wapinzani hawapaswi kuchaguliwa kuendesha nchi, kwani kufanya hivyo ni kukaribisha vurugu.

Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Taifa, Zakia Meghji alisema wapinzani hawayaoni mafanikio yaliyoletwa na serikali za CCM kwa vile wana boriti za macho.

Alitoa mfano ambapo alisema tofauti na madai yao kuwa uchumi wa nchi umedidimia, ukweli ni kwamba unaendelea kukua mwaka hadi mwaka ambapo alisema mwaka huu umepanda kwa asilimia 6.7 dhidi ya asilimia 3.6 kwa mwaka 2000.

 

 

Mwinyi awaasa wana-CCM kutowakataa wagombea

·        Kufanya hivyo ni sawa na  kujimaliza  kwa mabomu ya kujitoa muhanga

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

 MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, Ali Hassan Mwinyi, amewaomba wana-CCM kutowakataa wagombea walioteuliwa na chama kusimama kwenye uchaguzi mkuu ujao, na kusema kufanya hivyo ni sawa na kukiangamiza chama.

 "Kuwakataa wateule hao ni sawa na wanaojitoa muhanga kwa kujifunga mabomu, unajiua mwenyewe na kukiua chama chako," alisema Mzee Mwinyi katika mkutano wa kampeni za mgombea urais wa Zanzibar mjini hapa jana.

 Mkutano huo wa kwanza wa kampeni kwa mgombea urais wa Zanzibar, baada ya CCM kuzindua kampeni zake Pemba Jumatatu iliyopita, ulifanyika uwanja wa Kibandamaiti, mjini hapa maarufu kama uwanja wa Demokrasia.

 Makamu Mwenyekiti huyo mstaafu alisema wanaofanya uteuzi wa wagombea ni Chama cha Mapinduzi ambacho kinaoongozwa na binadamu, inawezekana viongozi wakafanya makosa, lakini wasamehewe kwa wagombea hao wateule kukubaliwa kwa mara ya mwisho.

 Mzee Mwinyi ambaye aliomba msamaha wa makosa yaliyofanyika katika vikao vya Chama kwa kuwateua wagombea wasiyokubalika kwa wananchi, ambao alisema ni wachache, na kuwaomba wana CCM na wananchi kuwapigia kura na kuwachagua kwa mara ya mwisho.

 "Wana CCM hawajifungi mabomu na kujitoa muhanga ili afe na chama chake. Hiyo siyo sifa ya mwana-CCM," alisisitiza na kuwaomba wana CCM na wananchi kumchagua mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume na wasaidizi wake wote, akimaanisha wabunge wawakilishi na madiwani wa CCM.

 Alisema kumchagua rais peke yake hakutoshi, kwani rais anakuwa na wasaidizi wake, na wasaidizi hao ni wabunge, wawakilishi na madiwani.

 "Tuwape voti (kura) zetu zote Amani na wake wote, ili amalize ngwe ya kuleta maendeleo ya haraka katika nchi," alisema Mzee Mwinyi ambaye alionekana kuuvuta umati uliyohudhuria mkutano huo kutokana na hotuba yake nyepesi kwa lugha ya kawaida na kutoa mifano ya hapa na pale.

 Alisema Rais Amani ambaye anawania kutetea kiti chake hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu, amefanya mengi na kuleta maendeleo makubwa Zanzibar ambayo kila mwananchi anayashuhudia.

 Alisema maendeleo hayo yakiwemo ujenzi wa barabara za lami, ongezeko la shule za msingi na sekondari, vyuo na nyumba za maendeleo za Michenzani mjini Zanzibar, ni muendelezo wa Mapinduzi ambayo lengo lake ni kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi na nchi.

 

Karume asema kila wilaya visiwani kuwa na sekondari

·        Ni shule zitakazoandaliwa kukabili changamoto ya wakati wa sasa

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

MGOMBEA urais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, amesema Wazanzibari wakiipa ridhaa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, serikali atakayoiongoza itajenga shule ya sekondari katika kila wilaya Unguja na Pemba.

Alisema sekondari hizo kila moja itakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 4,000, watakaoandaliwa kielimu kukabiliana na changamoto ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ili waweze kuendesha maisha yao ya baadaye.

Rais Karume alitoa ahadi hiyo jana katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni katika kisiwa cha Unguja, uliyofanyika viwanja vya Kibandamaiti, unaojulikana pia kwa jina la uwanja wa Demokrasia, uliopo Mikunguni mjini hapa.

Alisema serikali atakayoingoza itaendelea na juhudi zake za kuimarisha sekta ya elimu, ikiwa pamoja na kujenga na vyuo vya ufundi, ili kuwaandaa vijana watakaoshindwa kuendelea na elimu ya juu wafunzwe kazi mbalimbali za ufundi zitakazowajengea uwezo wa kujiajiri.

Rais Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliuambia umati uliyohudhuria mkutano huo kuwa CCM ambayo ndiyo Baba wa demokrasia nchini, ilikubali kuanzisha mfumo wa vyama vingi ili vyama vishindane kwa sera, hoja na ilani, lakini wapinzani wameugeuza mfumo huo kuwa uadui na ugomvi.

Alisema katika kuongoza nchi, CCM imefanya makosa mengi ambayo yamesahihishwa, lakini miongoni mwa kosa kubwa ililofanya ni kuwakubali ‘wale' akimaanisha watu waliyokuwa ama wenye asili ya upinzani kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 katika CCM.

"Tulikosea kuwachukua wale tukawapa dhamana, wengine wakafika hata kuwa mawaziri kiongozi. Lilikuwa kosa lile," alisema na kuongeza kwa sababu hawakuwa na nia ya dhati ya kushirikiana kuleta maendeleo ya nchi na watu wake.

Alisema kama wangekuwa na uchungu wa nchi na wananchi wake, baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa 1995, wasingetembea dunia nzima kuitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea vikwazo Zanzibar.

Alisema viongozi wa aina hiyo hawafai kuchaguliwa kuiongoza nchi hii, kwa sababu hawajali maendeleo ya wanaotaka kuwaongoza ila wanajali maslahi yao binafsi.

"Tuliwakubali na kuwaita tushirikiane, kumbe tulifanya makosa. Walikuja kutuchafulia chama chetu na nchi yetu," alisema Karume bila ya kutaja jina la mtu yeyote.

Aliwaambia wananchi kuwa Chama cha Mapinduzi na wagombea wake, akiwemo yeye anayewania kutetea kiti cha rais wa Zanzibar, ndiyo wanaofa kuchaguliwa kwa sababu CCM imeonyesha miaka yote iliyoongoza nchi kuwa inajali maslahi na maendeleo ya Wazanzibari wote.

Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya mengi ya maendeleo ikiwemo kujenga barabara, shule, zahanati na hospitali, nyumba za maendeleo na kutoa elimu na matibabu bila malipo kwa kila mwananchi ili kila mmoja apate mafanikio na maendeleo katika maisha yake.

Alisema pia imeinua pato la kila mwananchi hadi sasa kuwa kati ya sh. 290,000 hadi 340,000, wakati makusanyo ya mapato ya serikali yameongezeka kutoka kati ya sh. milioni 800 na bilioni 1.2 kwa mwezi hadi sasa kufikia sh. bilioni 3.6 kwa mwezi.

Alisema makusanyo hayo yamekuwa kutokana na serikali ya awamu ya sita kusimamia vizuri makusanyo na matumizi ya mapato ya serikali, hali ambayo imeiwezesha Serikali ya mapinduzi Zanzibar kuimarisha huduma za jamii, ikiwemo kugharamia ujenzi wa barabara.

Leo Rais Karume anaendelea na mikutano yake ya kampeni katika mkoa wa Kusini Unguja, katika kijiji cha Makunduchi.

  

Usawa katika biashara ni muhimu kuliko nafasi Baraza la Usalama

·        Ni kauli ya Rais Mkapa alipozungumza na Rais wa Finland

Na Maura Mwingira, Helsinki-Finland

RAIS Benjamin Mkapa amesema pamoja kuwa ni haki kwa Bara la Afrika kupata nafasi ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) jambo la msingi kwake lingekuwa bara hilo kushinikiza upatikanaji wa fursa sawa katika soko la kimataifa.

Mkapa alisema ni muhimu  kupigania kupatikana haki katika dunia hii yenye ushindani mkubwa wa utandawazi na kushinikiza mataifa tajiri  kuyafuta madeni yake kwa nchi maskini na kuongeza misaada.

Aliyasema  hayo jana  wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Serikali ya Tanzania na Finland. Upande wa Finland ujumbe uliongozwa na Rais Tarja Hoalonen.

Mazungumzo  hayo yaligusia maeneo mbalimbali yakiwemo ya ushirikiano, changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa hususani utekelezaji wa malengo ya milenia, uhusiano kati ya Jumuia ya Ulaya na bara la Afrika na marekebisho ya muundo wa Umoja wa Mataifa.

"Ni kweli tunataka nafasi ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini kwa mawazo yangu na haya ni yangu binafsi, nadhani kwetu na kwangu kipaumbele chetu hasa kingekuwa kupigania mambo ya msingi ambayo yataongeza kasi ya kubadilisha hali ya maisha ya watu wetu", alisisitiza  Mkapa.

Rais Mkapa yuko Finland kwa ziara rasmi ya siku nne kwa mwaliko wa Rais Tarja ambapo ataitumia ziara hiyo kuagana na viongozi wa Serikali ya Finland na wananchi  na kuwashukuru kwa ushirikiano na misaada ya kimaendeleo ambayo nchi hiyo imetoa kwa Tanzania katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 ya ushirikiano huo.

Alifafanua kwamba  hali duni ya maisha ya Waafrika haiwezi kubadilika kwa kupata nafasi katika baraza hilo, na wala hali hiyo haikusababishwa na kutokuwamo ndani ya baraza.

Alihoji kuna maana gani kupigania nafasi ya kudumu katika baraza hilo, huku watoto wa Kiafrika wakiendelea kupoteza maisha kabla ya kufikia umri wa miaka mitano.

Rais Mkapa alisema hali hiyo itabadilika tu kwa kushinikiza Bara la Afrika litendewe haki kwa kupatiwa fursa sawa katika kila eneo na kwa mataifa tajiri kutekeleza ahadi zao za kusaidia bara hili.

Alisema kuwa pamoja na kutafuta haki kutoka kwa mataifa tajiri katika mambo ya msingi kwa maendeleo ya Afrika, lakini pia nchi za Afrika zina uwezo wa kutekeleza malengo ya maendeleo ya milenia hususani katika elimu na afya ifikapo mwaka 2015 na kuwa kinachotakiwa ni utashi wa kisiasa na kujituma.

Kwa upande wake, Rais Tarja pamoja na kusifu hali ya uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi mbili na watu wake, alisisitiza kuwa kuna kila sababu ya mataifa tajiri na mataifa yanayoendelea kushirikiana katika kutekeleza na kufuatilia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti ya Tume ya Kimataifa kuhusu athari za utandawazi katika masuala ya kijamii ili kujengea hali bora ya maisha kwa kila mtu.

Aliahidi  kuwa Finland itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania na hususani katika kupigania na kutetea haki na fursa sawa za kimaendeleo kwa nchi za Afrika.

Alisema Finland inajivunia uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania  na kwamba umekuwa mfano wa kuigwa na itauendeleza.

Pamoja na kuwa na mazungumzo na Rais  Halonen, Rais pia alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Matri Vanhanen, Naibu Spika, Marku Kiski, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Jiji la Helsinki Rakel Hiltunen ambaye alimkabidhi tuzo ya heshima ya jiji hilo na kisha akaweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya mashujaa.

 Rais pia alipata nafasi ya kuagana na Watanzania wanaoishi  Finland. Leo atahutubia mkutano wa mwisho wa mchakato wa Helsinki.

 

 

Mgombea ubunge Ngorongoro amwombea kura Kikwete

·        Tayari yeye amepita bila kupingwa

Na John Shija, Ngorongoro

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Ngorongoro kupitia CCM, Saning’o Ole Tilele amesema mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete katika jimbo hilo atapata ushindi wa kishindo.

Ole Tilele alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika mwishoni mwa wiki eneo la Matambo wilayani Ngorongoro na ulihudhuriwa na viongozi wengine wa CCM mkoa.

Mgombea huyo ambaye amepita bila kupingwa alisema hayo alipokuwa akimnadi mgombea urais wa CCM Jakaya Kikwete katika uzinduzi huo wa kampeni.

Alisema ana imani kubwa na wananchi wa jimbo hilo kuwa watamchagua mgombea urais aliyesimamishwa na Chama Cha Mapinduzi ili atekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kuwaletea maendeleo.

Uzinduzi huo uliongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Yona Nnko ambaye aliongozana na Katibu Mwenezi wa CCM mkoa, Novatus Makunga waliwataka wananchi hao wasichague wapinzani kwa kuwa siyo watu waadilifu.

Hata hivyo, mwenyekiti Nnko ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwapongeza wananchi wa Ngorongoro wa kumpitisha mgombea huyo bila kupingwa ikiwa ni ishara kwamba wana imani kubwa na wagombea waliopitishwa na CCM.

Aliwataka wananchi kutofanya makosa siku ya uchaguzi na kuzitumia kura zao kwa kuwapa wagombea wa CCM.

Naye Makunga aliwaambia wananchi kuwa kipindi hiki siyo cha kukubali kudanganywa na wapinzani na kuwaeleza wananchi hao kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ndiyo nguzo ya maendeleo.

Aliwaambia wananchi waepuke uongo wa baadhi ya wahisani na wanaojiita watoa elimu ya uchaguzi ambao wamekuwa wakipita kwa wananchi kuwaeleza kuwa wasipoiondoa CCM madarakani hakuna mabadiliko.

 

CCM yaonya wananchi Bukoba kutochanganya dini na siasa

Angela Sebastian, Bukoba

MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi wa Wilaya ya Bukoba ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo Alhaj Ahmed Lugusha amewashauri wananchi wa Wilaya hiyo kutochanganya dini na siasa wakati wa kupiga kampeni zao.

Mlezi huyo wa wilaya alitoa tahadhari hiyo juzi katika viwanja vya Kashai mjini hapa, wakati wa mkutano wakampeni za kumnadi mgombea wa CCM jimbo la Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki.

Alisema kuwa Katiba ya Tanzania haina udini, kwa hiyo aliwashauri wananchi hao kuwachagua watu wanaostahili kwa kutazama uwezo na jinsi gani wanaweza kupiga vita umaskini na kuleta maendeleo.

Alisema kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kuingiza masuala ya udini katika masuala ya kisiasa, jambo ambalo ni sumu ya maendeleo.

"CCM haina dini kwa hiyo msiingize dini katika serikali au chama kwa maana, hali ya kushabikia na kuchanganya dini na siasa inaweza kusababisha uvunjifu wa amani,” alisema.

Naye Katibu wa CCM wa Wilaya ya Bukoba Mjini, Cosmas Kasangani aliwashauri wananchi wa jimbo hilo kutorudia kufanya makosa waliyoyafanya mwaka 2000 ya kumchagua mgombea wa CUF.

Kasangani alikilinganisha kitendo hicho kuwa ni sawa na na mtu aliyekurupuka na gaguro, huku akiwa amesahau shati nyumbani.

"Bukoba Mjini tukiendelea kukumbatia upinzani tusitarajie kupata maendeleo kama yalivyo majimbo mengine ambayo yananeemeka na sera za CCM kupitia viongozi waliopatika na kupitia chama hicho," alieleza Kasangani.

Akihutubia katika mkutano huo, Kagasheki aliwaomba wananchi wa Jimbo hilo kulinganisha sera za vyama wanavyotaka kuvichagua na kuacha kujiingiza katika uchochezi ambao unaweza kusababisha kuvunja amani na utulivu wa mkoa na nchi kwa jumla.

Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Robert Bahati aliwaasa wananchi kwamba ili maendeleo yapatikane kwa haraka Bukoba Mjini hawana budi kuwachagua madiwani, mbunge na Rais wanaogombea kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi.

  

Wagombea ubunge majimbo ya Tanga kutatua tatizo la ajira

Na Hussein Semdoe, Kilindi

WAGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya CCM mkoani Tanga wameahidi kushirikiana na serikali kutatua tatizo la ajira kwa vijana endapo watachaguliwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao.

Maneno hayo yametamkwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na aliyekuwa mwenyekiti wa wabunge mkoa wa Tanga, Dk. Abdallah Kigoda wakati akizindua kampeni za ubunge na madiwani katika kijiji cha Msente juzi.

Dk. Kigoda mwenyewe ambaye ni mgombea wa jimbo la Handeni alisema jimbo la Kilindi na mkoa mzima wa Tanga ni mkoa wa Chama cha Mapinduzi.

“Ni matumaini yetu kuwa wananchi wote mkoani Tanga mtachagua wagombea wa CCM tena kwa ushindi wa kishindo na mgombea wetu wa Urais Jakaya Kikwete mtamchagua kwa kura nyingi,” alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliofurika katika mkutano huo.

Katika mkutano huo viongozi mbalimbali wa CCM Mkoa walikuwepo ambao ni pamoja na wagombea wanawake Viti maalum, Dk. Aisha Kigoda, Mwatumu Mahiza, mgombea Ubunge wa Jimbo la Bumbuli, William Shelukindo na mgombea wa Kilindi Beatrice Shelukindo.

Akizungumza katika uzinduzi huo mgombea ubunge Jimbo la Bumbuli, Shelukindo aliwataka wana Kilindi kumchagua Jakaya Kikwete na kusema upinzani hauna mtandao vijijini ukilinganisha na CCM.

Mgombea wa Kilindi, Beatrice alisema: ''Tutashirikiana wote kwa pamoja ili tuweze kuleta maendeleo wilayani kwetu''.

Katibu Mwenezi wa CCM wilayani Kilindi, Fikirini Masokola katika mkutano huo alitangaza majina ya wagombea sita 6 wa udiwani kwa tiketi ya CCM waliopita bila kupingwa katika kata zao kuwa ni Mussa Semdoe (Jaila,) Yoona Moono (Saunye), Rashidi Lunga (Mkindi), Mapombe Tupilo (Pagwi), Clement Chamoto ( Tunguli) na Ramadhani Luswago (Lwande).

Wanachama 27 wa vyama vya CUF, CHADEMA na NCCR, walirudisha kadi za vyama hivyo kwa kumkabidhi Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Taifa Dk. Kigoda na kujiunga na CCM. 

 

 

 

‘Wapinzani watoe elimu ya uraia kwa wanachama wao’

Ni mwito uliotolewa na mjumbe wa NEC-CCM

Na Mwandishi Wetu

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye amevitaka vyama vya upinzani nchini kuiga utaratibu wa CCM wa kufundisha wanachama wake masuala ya uraia ili Watanzania wengi waweze kuona umuhimu wa kushiriki katika masuala ya demokrasia na uchaguzi wa viongozi.

Nnauye alitoa wito huo jana alipohojiwa na waandishi wa habari kwenye mkutano ulioandaliwa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kuwaeleza maafisa wa vyama vya siasa juu ya kitengo maalum cha msaada wa pamoja wa nchi za Ulaya katika masuala ya kutoa elimu ya uraia wakati wa uchaguzi.

Vyama vyote 18 vilivyosajiliwa vilituma wawakilishi wake kwenye mkutano huo ambapo kwa upande wa UNDP washiriki walikuwa Margie Cook na Richard Klein.

Alisema CCM inao mpango wa kutoa elimu ya uraia kwa wanachama wake, jambo ambalo kama litafanywa na vyama vyote vya upinzani litasaidia kuwaelimisha Watanzania wengi juu ya umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi wa kidemokrasia.

“Vyama vya upinzani visilaumu Serikali juu upungufu wa elimu ya uraia nchini, kwani ni jukumu lao kuitoa wakati wote na siyo kuomba kura wakati wa uchaguzi pekee,” alisema.

Alisema vipo vyama vya upinzani ambavyo tangu vilipoandikishwa havijatoa hata semina kwa wanachama wake juu ya masuala ya uraia, jambo ambalo ni hatari na kwamba kinachotakiwa ni kwa vyama vya upinzani kuiga malengo mazuri ya CCM .

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Zanzibar Khalifa Khalifa akielezea uzoefu wake katika masuala ya elimu ya uraia nchini, alishauri elimu hiyo itolewe na serikali na asasi zisizo za kiserikali wakati wote.

Khalifa alitoa mfano wa asasi 13 za Zanzibar ambazo alisema ndizo zinazoshiriki kutoa elimu ya uraia wakati Zanzibar ina asasi zisizopungua 200.

Hata hivyo, Ofisa Uchaguzi wa CUF Hussein Masauni  aliwaambia waandishi wa habari kwamba  suala la elimu ya uraia linatakiwa kutatuliwa na serikali iliyopo madarakani kwa madai kwamba ndiyo yenye wajibu. Mkutano huo ulimalizika jana.