UHURU 09.09.2005

 

 

 

Kikwete kuendeleza makao makuu Dodoma

Na Bashir Nkoromo, Dodoma

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete ameahidi kuendeleza ujenzi wa Makao Makuu Dodoma.

Kikwete alitoa ahadi hiyo jana alipohutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Alisema ataendeleza ujenzi wa makao makuu Dodoma ambayo ni ya nchi, kwa kuwa sababu zilizofanya uamuzi huo bado zina umuhimu ule ule hadi sasa.

Akielezea Ilani ya Uchaguzi, Kikwete alisema awamu ya nne ya uongozi wake, suala la elimu ni miongoni mwa mambo atakayoyapa kipaumbele cha hali ya juu.

Alisema, hata hivyo, atachofanya ni kuongeza kasi na ubora zaidi katika nyanja ya elimu kwa kuwa kazi nzuri imekwishaanza kufanywa na serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa na matunda yanaonekana.

Kikwete alisema, wakati Mkapa anaingia madarakani mwaka 1995, idadi ya wanafunzi waliokuwa katika shule za msingi ilikuwa milioni 3.5, lakini sasa imeongezeka na kufikia milioni 7.5, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi milioni nne.

Alisema, kwa upande wa shule za sekondari idadi ya watoto nayo imeongezeka kutoka wanafunzi 190,000 wakati Rais Mkapa anaingia madarakani mwaka 1995 hadi 520,000 hivi sasa.

Kutokana na juhudi za kuboresha sekta ya elimu nchini, hali ya madarasa karibu yote katika shule za msingi hapa nchini ni mazuri na yale ambayo bado yako katika hali mbaya mipango ya kuyaboresha ipo mbioni.

Alisema katika uongozi wake atajikita zaidi katika kuhakikisha kiwango kilichofikiwa kinaongezeka zaidi na zaidi ili kikidhi mahitaji ya wakati wa sasa.

Mgombea huyo alisema katika jitihada hizo, serikali yake itaboresha elimu ya sekondari na vyuo vya elimu ya juu ili viweze kumudu kupokea wanafunzi wengi inavyowezekana.

Alisema, kutokana na nia yake hiyo thabiti, Watanzania hawana budi kuipa kura CCM na kumfanya aongoze dola kwa kuwa hawana sababu ya kufanya kinyume chake.

Alisema, CCM ndicho chama pekee chenye mwelekeo na kwamba vyama vya upinzani bado havijaweza kuwa mbadala wa CCM kwa miaka mingi ijayo.

Bila kuvitaja KIkwete alisema, baadhi ya vyama hivyo vimekuwa vikijinadi kwa misingi ya ukabila au udini bila kujali kwamba kutumia njia hizo kunyakua uongozi katika siasa ni jambo hatari.

Aliwataka wananchi pamoja na kumchagua yeye, wahakikishe pia kwamba wanawachagua wagombea wa ubunge na udiwani wanaowania kwa tiketi ya CCM.

Mapema, kabla ya kuhutubia mkutano huo ambao ulifurika maelfu ya wananchi, asubuhi Kikwete alikwenda katika wilaya mpya ya Bahi ambako alihutubia mkutano mwingine wa hadhara.

Leo anaendelea na ziara yake katika jimbo la Mtera ambako ndiko Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), John Malecela anakowania Ubunge.

 

 

 

Wapinzani hawana nia ya kujenga nchi, bali kuvuruga

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Rais Amani Abeid Karume, amesema wapinzani hawafai kukabidhiwa nchi kwa sababu hawana nia ya kujenga isipokuwa kuvuruga.

Alisema siku zote wapinzani na hasa chama cha CUF, kimekuwa wakiukaji wakubwa wa makubaliano yanayofikiwa na Chama cha Mapinduzi na serikali zake.

Rais Karume aliyasema hayo jana katika mkutano wake wa kampeni uliyofanyika Makunduchi, mkoa wa Kusini Unguja.

Akitoa mfano wa ukiukaji huo ambao aliueleza lengo lake ni kuivuruga nchi na kukwamisha maendeleo ya wananchi, alisema Muafaka wa CCM na CUF umeweka misingi mizuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki, lakini chama hicho sasa kinakiuka ili kujenga mazingira ya vurugu kwenye uchaguzi.

Alisema katika Muafaka huo vyama vimekubaliana kuweka ofisi ya Muendesha Mashitaka, kurekebisha Tume ya Uchaguzi iwe huru na wao ndiyo waliyotoa mapendekezo hayo na kutaka wajumbe wa vyama wawekwe kwenye Tume.

"Lakini ajabu ya mwaka, sasa wajumbe wao ndiyo wamekuwa wa kwanza kuigeuka Tume na viongozi wao kuishutumu Tume," alisema Rais Karume na kusisitiza kuwa viongozi wao siku zote wamekuwa hawana nia njema zaidi ya kuvuruga.

Alisema viongozi na vyama vya aina hiyo havifai kupewa uongozi wa nchi.

Rais Karume alisema CCM pekee na wagombea wake ndiyo wanaofaa kuchaguliwa kwa kura zote za wananchi, kwa sababu kimefanya mengi ya maendeleo ya nchi na wananchi wake, ikiwa pamoja na kujenga barabara za kisasa, kujenga shule, kuondoa kero za maji safi na salama na kuimarisha huduma za afya, hasa vijijini.

Alisema CCM ikichaguliwa kuongoza tena nchi, itapiga vita ajira mbaya za watoto.

Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema ajira mbaya zinazokatazwa ni zile za kuwaajiri watoto mashambani na kwenye kazi mbaya.

Alisema mtoto kupewa kusaidia kazi ndogo ndogo za nyumbani, siyo ajira inayokatazwa.

Rais Karume ataendelea na mikutano yake ya kampeni kesho, ambapo atafanya mkutano Uzini, wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja.

 

 

Mkapa: Mchakato wa Helsinki utumike kwenye siasa za ndani

Na   Mwandishi   Wetu

RAIS Benjamin Mkapa amesema kuwa changamoto iliyopo kwa viongozi duniani ni kuufanya mchakato wa Helsinki utumike kwenye siasa za ndani ya nchi.

Aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa mwisho wa mchakato wa Helsinki unaofanyika Helsinki, Finland kwa ajili ya kuwasilisha ripoti ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya dunia na utekelezaji wake. Nakala ya hotuba ya Rais Mkapa ilipataka mjini Dar es Salaam.

Mkapa alisema anaamini kuwa njia pekee ya kutekeleza mikakati ya ufumbuzi wa matatizo ya dunia ni kwa wananchi wa nchi zote masikini na tajiri kuzibana serikali zao ili ziwajibike ipasavyo.

Alisema iwapo siasa za ndani ya nchi zitatekelezwa kwa mujibu wa mchakato huo na fedha zikawepo, utekelezaji wa mikakati na ufumbuzi wa matatizo hayo utawezekana.

Mkapa alisema kama wananchi wa mataifa tajiri watazibana serikali zao, misaada kwa nchi masikini itaongezeka hata mara tano ya kile walichoahidi kuchangia. Mataifa makubwa yanachangia asilimia 0.7 ya pato la Taifa kwa mwaka.

Rais Mkapa alisema kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 33, zinazotumiwa na mataifa makubwa kununua vipodozi na manukato.

Alisema ripoti ya Maendeleo ya Milenia imeeleza kuwa nchi za Afrika zinahitaji dola kati ya bilioni 20 na 25 kila mwaka kwa ajili ya maendeleo.

Rais Mkapa alitaka utashi wa kisiasa uhamasishwe  kati ya nchi na watu wake kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati ya kutatua matatizo ya dunia.

 

 

Kikwete aonya mabadiliko katika serikali hayafanywi kwa majaribio

Na Bashir Nkoromo, Gairo

WATANZANIA wameonywa kuepukana na fikra kuwa mabadiliko ya serikali yanaweza kufanywa kwa majaribio kama kubadilisha mboga.

Onyo hilo lilitolewa juzi mjini hapa na mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na umati wa wananchi katika uwanja wa CCM jimboni humo mkoani Morogoro majuzi.

“Wananchi tambueni mtu anachoweza kubadilisha bilatahadhari yoyote ni mboga… leo bamia, kesho mlenda keshokutwa nyama au maharage, lakini kwa serikali haifai kabisa, kwani kudhani unaweza kufanya hivyo unaweza kupata madhara yasiyokwisha,” alisema Kikwete.

Hivyo, Kikwete aliwaasa Watanzania kuendelea kuichagua CCM kwa kuwa inaaminika kutokana na kwamba tayari imekwisha tekeleza ahadi zake nyingi katika awamu zake zote za uongozi.

Alisema, tayari CCM imekwishajijengea uaminifu mkubwa kwa wananchi kutokana na kuonyesha nia na uwezo wake wa kuboresha maisha ya wananchi na kuifanya nchi kuwa tulivu.

Kikwete alisema, kinachofuata sasa ni wananchi kuipa tena ridhaa CCM ili chini ya uongozi wake iweze kuendeleza pale awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa itakapokuwa imekomea.

Alisema, kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, uongozi wake wa awamu ya nne umelenga zaidi kuongeza kasi ya uchumi wa nchi ili maisha ya wananchi yawe ya neema zaidi.

Kikwete alisema, chini ya uongozi wake CCM itahakikisha katika awamu ya nne, vijana na wanawake wanawezeshwa ili waweze kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira za serikali.

Alisema, watu wa kada hiyo serikali yake itafanya mikakati ya kuwawezesha kupata mitaji kutokana na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuanzisha biashara zao.

Kikwete alisema, kwa kuwa benki si rafiki wa masikini zinapenda matajiri tu, serikali yake itaweka mpango huo wa mikopo nafuu na pia kurasimisha mali za wananchi wakiwemo wa vipato vya chini ili ziweze kuwa dhamana ya kupata mikopo.

Alisema, vilevile serikali yake itaweka mkakati kamambe wa kuboresha huduma za afya ikiwa ni kwa kufuata nyayo za mikakati iliyofanikisha uboreshwaji wa elimu ya msingi kupitia mpango wa MMEM.

Kikwete alisema, pia elimu ya sekondari nayo itaboreshwa na vyuo vikuu kuongezwa ili viweze kuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi zaidi.

Kuhusu miundombinu, Kikwete alisema, serikali yake itahakikisha katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya uongozi wake barabara kuanzia Korogwe, Handeni, Mziha, Mvomero, Kilosa hadi Mikumi inajengwa ili kuwa kichocheo cha maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo.

Baadaye Kikwete aliwanadi wagombea Ubunge wa majimbo ya Gairo, Mikumi na Kilosa na kuwamwagia sifa huku akiwasisitiza wananchi kuwapa kura za ndiyo wagombea hao kupitia tiketi ya CCM.

Alisema, mgombea wa Gairo, Ahmed Shabiby, Mustafa Mkullo wa Kilosa na Christopher Liamba wa Mikumi ni watendaji bora ambao kila mmoja ana medani ya kutumainiwa katika kuboresha uchumi wa majimbo hayo.

Mapema kabla ya kufika Gairo, Kikwete alikuwa tayari amezungumza na wananchi waliokuwa wakizuia msafara wake katika maeneo mbalimbali wakati akitokea mjini Morogoro.

 

 

Dk. Sheni asema hakuna chama mbadala wa CCM

Na Ramadhani Mkoma, Liwale

MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Sheni, amewataka Watanzania kuichagua CCM kuendelea kuongoza kwa kuwa hakuna chama mbadala kinachoweza kushika nafasi yake.

Dk. Sheni alisema hayo jana alipokuwa akiwasalimia wananchi katika vijiji vya Nangano, Kibutuka na Kiangara waliokuwa wakisubiri kuuona msafara wake katika ziara ya kampeni wilayani Liwale, Lindi.

Alisema vyama vya upinzani ni sawa na wapita njia, hivyo kuvichagua ni sawa na kupoteza muda kwani havina uwezo wa kufanya mambo ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

“Naomba msihadaike na ahadi zisizotekelezeka za wapinzani. Chama Cha Mapinduzi hakina mbadala hivyo endeleeni kukichagua ili kiweze kuongoza nchi na kuwaleteeni maendeleo,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba CCM ni chama pekee chenye sera sahihi, ilani na viongozi waadilifu tofauti na vyama vingine ambavyo havina ilani sahihi.

Pia, alisema licha ya kutokuwa na Ilani, sera madhubuti, vyama vya upinzani havina historia ya kuongoza kama ilvyo CCM, hivyo kuwataka wananchi kutosumbuka kuvipa kura ili kuingia madarakani.

Dk. Sheni alisema CCM pekee ina historia ya ukombozi wa uhuru wa nchi. Kwa maana hiyo, kuichagua CCM ni kuendelea kudumisha maendeleo yaliyopatikana tangu enzi za uhuru.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Sheni aliwasisitiza wananchi kutokuwa na sababu ya kuchagua wapinzani kwa wana ahadi za uongo huku viongozi wao wakiwa na chuki na ghilba.

“Hamna sababu ya kuchagua wapinzani kuongoza nchi. Lakini wakija wasikilizeni na muwaulize wamefanya nini mpaka wakaomba uongozi wa dola,” alisema.

Mgombea mwenza huyo alisema CCM inaomba tena ridhaa ya kuongoza nchi ili kuendeleza mengi mazuri iliyofanya na itakayoyaanzisha katika awamu ijayo ya uongozi.

Sababu nyingine, kwa mujibu wa Dk. Sheni ni kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo, kwa mfano, elimu kama ambavyo imefanya kwa kujenga shule sita za sekondari wilayani Liwale. Alisema hiyo yote ni kutokana na sera bora na zinazotekelezeka chini ya CCM.

“Wapinzani ni wababaishaji tu hawana lolote kwani wanatoa ahadi za uongo. Lakini wakija wasikilizeni, kwani ndiyo demokrasia, bali msiwape kura,” alisisitiza.

Jana jioni, Dk. Sheni ambaye ameongozana na mkewe, Mama Manamwema Sheni, alitarajiwa kuhutubia mkutano wa kampeni katika Viwanja vya Elimu Liwale.

 

 

Mgombea urais upinzani asifia mawaziri wa CCM

Na Rodrick Makundi, Moshi

MGOMBEA urais kupitia chama cha PPT-Maendeleo, Anna Senkoro amewamwagia sifa mawaziri Edward Lowasa, John Magufuli na Mark Mwandosya kutokana na utendaji mzuri wa kazi kwenye wizara zao.

Anna alisema kuwa hatua hiyo ndiyo iliyowawezesha wagombea Magufuli na Mwandosya wa nafasi za ubunge kwenye majimbo yao kupita bila kupingwa ili waweze kuendeleza ufanisi wao wa kiutendaji katika wizara na serikali kwa jumla.

Aliyasema hayo jana wakati alipokutana na waandishi mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani hapa kwa ajili ya kampeni za chama hicho.

Akielezea juu ya viongozi hao wa ngazi za uwaziri katika serikali ya awamu ya tatu alisema tangu wamekabidhiwa kuongoza wizara hizo hawajakumbwa na kashfa zozote na kwamba wanayo nafasi kubwa ya kueleza wananchi kile wanachotaka kuwatendea kwa ajili ya maendeleo.

Kufuatia umakini wao katika shughuli za kiserikali, mgombea huyo alisema kwamba iwapo atachaguliwa na wananchi kuwa rais atahakikisha mawaziri hao wanakuwa miongoni mwa mawaziri watakaokuwa kwenye baraza atakalounda katika serikali yake.

Aidha, aliongeza kwamba yeye binafsi hajaona wala kusikia kashfa zozote kuhusiana na viongozi hao ama doa kuhusiana na vitendo vya rushwa ambavyo vinawakabili wananchi na viongozi wengi hapa nchini.

Katika hatua nyingine mgombea huyo alisema kuwa iwapo atafanikiwa kuchaguliwa atahakikisha anaunda chombo huru cha kuzuia rushwa nchini ambacho kitasimamiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Alisema ameamua kuwa na mkakati huo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa katika maeneo mengi ya nchi na ambavyo vimeonekana kushamiri kwa kasi katika kila kona, hususan wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Anna alidai katika baadhi ya sehemu ambazo amekuwa akipita baadhi ya wananchi wamekuwa wakimwomba rushwa ili aweze kupata kura nyingi wakati wa uchaguzi, jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi katika suala zima la elimu ya uraia.

Pia, alisema kuwa pamoja na mikakati mingine chama hicho kimedhamiria kuunda chombo ambacho kitatetea maslahi ya wanahabari nchini ambao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu.

Alisema hadi sasa hakuna chama ambacho kimezungumzia jinsi ya kutetea maslahi ya waandishi wa habari nchini, ambapo wamekuwa hawathaminiwi pamoja na kuonyesha mchango wao mkubwa kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa siasa na serikali.

 

 

 

Mahita aonya wanasiasa wanaotisha wananchi

Na Rodrick Makundi, Same

WANANCHI wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutambua kwamba Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ambayo imewanufaisha.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Vicky Nsillo Swai, aliyasema hayo juzi  kwenye uzinduzi wa nyumba zilizojengwa na polisi kwa ajili ya makazi ya askari  wanaofanya kazi kwenye vituo vya polisi wilayani Same.

Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa nyumba hizo za polisi ambazo zitasaidia kuboresha maisha ya askari hao hivyo kuwawezesha kufanya kazi katika hali ya uhuru.

“Tunazindua nyumba hizi naomba mtambue kwamba hii ni kazi nzuri iliyofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wetu Benjamin Mkapa na mnajua serikali inashikiliwa na kina nani? Alisema Mwenyekiti huyo huku wananchi wakijibu kuwa inashikiliwa na CCM.

Alimpongeza Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Inspekta  Jenerali  Omar Mahita kwa usimamizi mzuri katika kuhakikisha kwamba askari wanapata makazi bora ili waweze kufanya kazi zao katika hali bora.

Kwa upande wake,  Mahita amevitaka vyama vya siasa nchini vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu, kuacha siasa za uchochezi ambazo zinaweza kusababishia kuvuruga.

Mahita alisema pamoja na jeshi lake hawataruhusu chama chochote cha siasa kutumia majukwaa kuwatisha wananchi ili wawapigie kura wakati wa kampeni na muda wa upigaji wa kura utakapowadia.

“Siingii kwenye siasa lakini ningependa mfahamu, ndiyo maana nayasema haya sasa, sisi polisi hatutaruhusu chama chochote cha siasa kinachoshiriki uchaguzi mwaka huu kutumia fursa wakati wa kampeni kuwatisha wananchi,” alisema Mahita.

 Mapema akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya polisi wilayani Same, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo na Mipango Makao Makuu ya polisi Kamishna Msaidizi wa polisi Vicent Matama alisema ujenzi huo umegharimu kiasi cha sh. 342,205,135.

Alisema ujenzi wa nyumba hizo zipatazo 12, ulianza Juni mwaka jana na kukamilika Oktoba 31, mwaka huo na kuwa kukamilika kwa ujenzi huo ni moja ya utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 344 nchini katika kipindi cha miaka mitano.

Matama alisema kuwa ujenzi wa nyumba za polisi nchini ulifanywa katika awamu ya tatu ambapo nyumba hizo zimejengwa katika miji ya Kiteto, Ukonga, Chake Chake, Pemba, Kunduchi, Dodoma, Hai, Babati, Kateshi na Same.

 

 

 

‘Wapinzani wataleta kero sio maendeleo’

Na Omari Shaaban, Arumeru. 

WANACHAMA, mashabiki wa CCM na wananchi wametakiwa kutowachagua viongozi wa vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, kwa kuwa wataleta kero na siyo maendeleo. 

Pia wameelezwa kwamba wapinzani kazi yao ni kuiga sera safi pamoja na Ilani ya CCM katika kampeni zao kwa kuwa hawana ubavu wa kutengeneza zao zinazotekelezeka kama za CCM.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,  Sifa Swai aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa CCM, Jeremiah  Sumari jimbo la Arumeru Mashariki uliofanyika Kikatiti, Arumeru. 

Akimnadi kwa wananchi mgombea huyo, Sifa Swai alisema Sumari ni chaguo la CCM,  ambalo litawaletea maendeleo ya haraka wananchi wa jimbo hilo na hivyo wampe kura za ndiyo na siyo kuwapa wapinzani ambao watarudisha nyuma maendele.

Alisema wapinzani wanaojaribu kugombea ubunge jimbo hilo, hawana lolote la kuwaambia wananchi, zaidi ya malumbano, fitina na uzushi na kuwaomba wananchi kuwapa wagombea wa CCM kuanzia madiwani, wabunge na rais kura.

Katibu wa CCM Mkoa, Nurdin Babu katika uzinduzi huo alisema gurudumu la maendeleo litasonga mbele zaidi katika  jimbo hilo, kutokana na mgombea wake kuwa mpenda maendeleo. 

Alisema wananchi na wanachama wa CCM, wavumilie tu endapo kampeni za wapinzani  zitakuwa za matusi na kashfa, badala ya kutangaza sera na ilani zao za uchaguzi kwa kuwa CCM ni kisiwa cha amani na utulivu. 

Akiwahutubia wananchi waliofurika kwenye uzinduzi huo, mgombea ubunge Sumari aliwataka wananchi kumpa kura za ndio kwa kuwa ni mwenzao katika maendeleo ya jimbo hilo. 

Alisema wakimpa kura,  jimbo hilo litamaliza  matatizo yaliyopo kama vile, maji, huduma za afya pamoja na kutafuta soko la bidhaa za wakulima ndani na nje ya nchi.

Sumari alisema atahakikisha Kikatiti inakuwa na soko kubwa kwa ajili wa wafanyabiashara na wakulima ambao hilo ni moja ya kero zao.

 Uzinduzi huo ulihudhiriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Eliasi Wawa-lali, mgombea ubunge Arumeru Magharibi Elisa Mollel na madiwani wa jimbo hilo na viongozi wengine

 

 

Kuwa mwana-CCM si mkataba wa kupata uongozi - Kataraia

Na  Peter Katulanda, Mwanza

KUWA mwanachama wa  CCM si mkataba wa kupata uongozi au ubunge na kamwe Chama hakina sababu ya kurudisha jina la mgombea asiyefaa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mwanza Mjuni Kataraia mwishoni mwa wiki mjini Sengerema wakati akizumgumza na viongozi wa Chama wa Wilaya za Magu, Sengerema, Kwimba na Misungwi.

Alisema mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM umeishapita na kamwe huu si wakati wa kulumbana na kuendeleza makundi  kwa sababu za kushindwa katika kura za maoni ama kutoteuliwa licha ya kuongoza kwenye kura hizo.

“Mwana CCM wa kweli akishindwa, baada ya uteuzi anavunja kambi yake na kumuunga mkono  mteule. Uana-CCM si mkataba wa uongozi wowote,” alisema.

Kataraia alifafanua kuwa wagombea walio katika  madaraka licha ya kushindwa katika kura za maoni siyo kwamba hawafai kuteuliwa kugombea tena na kuwa Chama kuwarudisha hakikufanya  makosa.

“Nimeshangaa kuona kila tulipopita upinzani wa mgombea wetu wa ubunge jimbo la Buchosa uko ndani ya CCM kipindi hiki cha kampeni si cha kutambiana ni cha kuungana na kushirikiana ili CCM iibuke na ushindi katika ngazi zote,” alisisitiza.

Kauli hiyo ya Kataraia imekuja baada ya hali iliyojitokeza katika vijiji vya Bukokwa na Itabagumba jimboni Buchosa wilayani Sengerema ambapo baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM baada ya kura za maoni hawajavunja kambi zao.

 

 

 

Serikali ya awamu ya nne itafanya makubwa

Na Idefonce Mgimba, Tukuyu

 MGOMBEA   wa jimbo la Rungwe Magharibi Profesa  David Mwakyusa amewahakikishia wananchi kupatikana kwa maendeleo makubwa katika miaka mitano ijayo ya Serikali ya awamu ya nne ya CCM.

Profesa  Mwakyusa alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa kampeni za CCM katika Kata ya Kyimo ambapo mamia ya watu walihudhuria na kuonyesha imani kwa CCM na kuahidi kumpigia kura za kishindo mgombea urais  Jakaya Kikwete, mbunge na wagombea wa udiwani wa CCM.

 Mwakyusa alionyesha mshangao kwa kitendo cha aliyemshinda katika kura za maoni, Afwilile Mwakijungu ambaye sasa amehamia TLP na kuchukua fomu ya ubunge kupitia chama hicho kwani alisema kwa misingi ya demokrasia hakutarajia kuwa angehama kwa kuwa chaguo la wengi ndilo angelichukulia kuwa ni mkondo sahihi wa demokrasia.

Hata hivyo, Profesa  Mwakyusa ambaye anatetea nafasi hiyo alisema Serikali ya CCM imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa njia ya kushirikisha nguvu za wananchi na kwamba ili matarajio ya wananchi yafikiwe katika kipindi kifupi kijacho. 

Aliwataka wananchi kuwapuuza wapinzani wanaotoa orodha ya mambo mengi ambayo hayajatekelezwa kwani katika kipindi cha miaka mitano Serikali ya CCM iliahidi katika Ilani yake kutekeleza mambo kadhaa na pia kutoa nafasi kwa wananchi katika maeneo husika kutekeleza miradi kulingana na vipaumbele vyao.

Alisema wananchi wawe macho na wagombea wanaowaomba kura kwa kutoa ahadi ya kuwaletea maendeleo ya haraka kana kwamba kila kitu wanaweza kukifanya wenyewe pasipo kushirikisha nguvu za wananchi na kuwa ahadi za namna hiyo mara zote huwa hazitekelezeki.

 “Tulipoanza kazi za kupunguza kero za wananchi mara baada ya kuchaguliwa miaka mitano iliyopita ilikuwa kama utani. Tulisema kwamba matatizo ni mengi, kero ni nyingi, hatuwezi kuziingia zote kichwa kichwa ili kuziondoa; tukasema elimu kwanza na kwa kipindi cha miaka mitano tumeweza kujenga shule ya sekondari kila kata na tayari tumefungua 11 kati yake,” alisema.

 Alisema, hiyo ilitokana na CCM kutoa ahadi zinazotekeleza na Serikali ya CCM  kuhakikisha kuwa inaondoa kero za wananchi moja baada ya nyingine  lakini kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya Andagile Mwakasendo alisema wananchi wanapaswa kuwa macho na wanachama wanaotafuta kuungwa mkono katika chama kimoja na wanapokosa wanakwenda chama kingine kuitafuta nafasi ile ile na kuwa hao nia yao ni kutafuta maslahi binafsi na siyo ya  wananchi.

 

 

 

 

 

 

Karume azungumzia utekelezaji wa ujenzi taasisi za mafunzo

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amesema Serikali ya Mapinduzi itahakikisha kuwa programu zote za miradi ya ujenzi wa taasisi za mafunzo zinatekelezwa kwa wakati.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi mara tu baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo la Elimu Mbadala, linalojengwa katika mtaa wa Rahaleo mjini Zanzibar.

Karume alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuhakikisha kuwa vyuo vikuu vinaimarishwa, shule za msingi na sekondari na vituo vya elimu mbadala vinajengwa ili kuendelea kutoa fursa ya elimu kwa watoto nchini.

Maendeleo ya elimu Zanzibar yamefikia hatua nzuri ya kuridhisha na hakuna budi kutumia hatua iliyofikiwa ili kuendeleza maeneo mengine ya maendeleo, alisema Rais Karume.

Rais Karume alikemea tabia ya upinzani ya kubeza na kupotosha ukweli juu ya maendeleo ya elimu. “Kigezo kinachoweza kutumika ili kupima maendeleo ya elimu Zanzibar inafaa kulinganisha maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar na yale yaliyofikiwa na nchi jirani.”

Aliendelea kusema kuwa Zanzibar hatuko nyuma katika kukamilisha Malengo ya Milenia hasa kwa upande wa elimu ya lazima. “Hakuna nchi jirani ambayo imeweza kufikia Malengo ya Milenia kwa upande wa elimu ya msingi,” alisisitiza Rais Karume.

Mapema, Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo, Haroun Ali Suleiman alisema katika hatua za kuimarisha maendeleo ya sekta ya elimu Zanzibar, Serikali itachukua juhudi za kuipitia na kuirekebisha sera ya elimu kwa kuzingatia haja ya kuongeza maslahi ya walimu na watendaji wengine.

Waziri Haruon alisisitiza juu ya ukweli wa maana halisi ya elimu bila malipo. Alisema serikali haitaruhusu wanafunzi kufukuzwa au kusimamisha wanafunzi kwa sababu kwamba hawajalipa ada.

Aliendelea kusema kuwa hakuna jambo jipya katika sera za upinzani kwa kusema kuwa watafanya elimu iwe bure, kwa sababu Serikali ya Mapinduzi imetangaza elimu bila ya malipo tokea mwaka wa 1964.

Mapema ilielezwa kuwa mradi wa ujenzi wa jengo la Elimu Mbadala unaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB). Hadi kukamilika kwake jengo hilo litagharimu jumla ya sh. 620,917,300 kati ya hizo, SMZ itachangia sh. 136,601,806 na ADB itachangia jumla ya sh. 484,315,494.

Jengo hilo linatarajiwa kukamilika Januari 10, 2006. Lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kuwasaidia watoto wanaozurura mitaani na waliokosa fursa ya kujiunga na shule kwa sababu moja au nyengine, hasa watoto wa kike waliopata mimba mapema au ndoa za mapema.