UHURU 09.10.2005

 

Mgombea mwenza Chadema atelekezwa hospitali Dar

Ni Jumbe Rajabu Jumbe

Kapooza mkono na mguu

l Kulazwa Hindu Mandal

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha siasa cha Chadema kinadaiwa kumtelekeza mgombea mwenza wake wa urais wa Tanzania, Jumbe Rajabu Jumbe, ambaye amepooza mkono na mguu na kulazwa hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam.

Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema ni Freeman Mbowe.

Mke wa mgombea mwenza huyo, Mama Jumbe, akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, alisema Chadema ilitoa sh. 100,000 tu kati ya zaidi ya sh. 800,000 zilizotumika kwa ajili ya kumuuguza mgombea mwenza huyo ambaye bado yuko hospitali.

Mama Jumbe alisema kwa mara ya kwanza alipougua na kulazwa hospitalini hapo, viongozi wa Chadema walilipa sh. 100,000 na walimweleza kuwa chama hakina pesa na ruzuku wanayopata ni ndogo kutosheleza mahitaji ya chama.

Habari zinasema Jumbe, ambaye kwa mara ya kwanza alizidiwa akiwa kwenye kampeni na Mbowe, mkoani Kagera na kulazimika kurejeshwa Dar es Salaam kwa matibabu, hajawahi kutembelewa na kiongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho, akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mama Jumbe alisema kuwa mara ya kwanza mumewe alipolazwa katika hospitali hiyo akitokea Kagera, walilipa sh. 500,000, ambapo Chadema ilichangia sh. 100,000, huku sh. 400,000 zikiwa zimechangwa na wanafamilia.

Alisema baada ya Jumbe kuwa ametolewa hospitali, Okotba 2, mwaka huu alizidiwa na kupoteza fahamu ambapo alirudishwa Hindu Mandal na amelazwa hadi sasa.

Mwandishi wa habari hii alipotembelea hospitalini hapo jana, alimshuhudia Jumbe akiwa hawezi kuzungumza wala kufumbua macho, akiwa analishwa kwa kutumia mpira uliowekwa puani.

Mama Jumbe alisema walipomfikisha hospitalini hapo walilazimika kulipa ada ya kulazwa hospitali ya sh. 150,000 na gharama za X-Ray ya kichwa sh. 150,000.

Alisema walilipa gharama za matibabu ambazo ni sh. 39,000 na gharama nyingine za usafiri na kwamba katika gharama za sasa walilazimika kukopa sh. 200,000 kutoka kwa mpangaji wa nyumba yao.

Mama Jumbe alisema kuwa kwa sasa hawana deni hospitalini hapo, isipokuwa walilo nalo ni la mpangaji wao, na alimtaja kiongozi wa Chadema kwa jina moja la Shija, kuwa ndiye anayemtembelea.

Alisema X-Ray aliyopigwa imeonyesha kuwa ana kitu kama tone la damu lililoganda kwenye ubongo na kwa sasa amepooza mkono na mguu. Muda wote yuko chini ya uangalizi wa familia yake na madaktari.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Shaibu Akwilombe, akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, alisema ni kweli Jumbe amelazwa na jana ilikuwa siku ya tano, na kuwa “hali yake inaendelea vizuri”.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa chama hakimsaidii mgombea mwenza huyo, alisema: "Mimi ndiyo nakusikia wewe", na kuongeza kuwa habari hizo si za kweli.

Hata hivyo, baadhi ya watu wa karibu na mgombea mwenza huyo wamehoji kitendo cha Mbowe kutumia mamilioni ya shilingi kukodi helikopta kwa ajili ya 'mbwembwe' za kampeni, na kumwacha 'makamu wa rais' wake akitaabika hospitali.

Walidai kuwa kama kweli Mbowe ana hoja ya kuwasaidia Watanzania masikini, inakuwaje amtelekeze mgombea mwenza, na kuhoji kama kadiriki kumtekelekeza mwenzake ndani ya chama chake, atashindwaje kuwatelekeza Watanzania.

Helikopta anayotumia Mbowe imekodiwa Kenya, na habari zinasema Chadema inalipa dola za Marekani 1,200 kwa saa (karibu sh. milioni 1.3).

Helikopta hiyo kwa saa tisa siku inatumia sh. milioni 9.1, na kwa siku 30 itatumia sh. milioni 273.

 

 

Chadema yakimbiwa na mgombea ubunge wake

Ajiunga na CCM

Alikuwa pia mwenyekiti wake mkoa wa Moro

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Chadema mkoa wa Morogoro, David Mgesi ambaye alikuwa akiwania ubunge wa jimbo la Morogoro Kusini kupitia chama hicho, amehamia CCM jana kwa tuhuma za kuepuka migogoro inayofukuta kwa kasi kubwa ndani ya Chama hicho..

Mgesi alitangaza uamuzi wake wa kukihama mbele ya waandishi wa habari alipokutana nao ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mjini Dar es Salaam, ambako alipokewa na mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete.

Kikwete, ambaye jana hiyo alitimiza miaka 55 tangu kuzaliwa, waandishi wa habari walimwimbia wimbo wa ''Happy Birthday to you'' na alisema alitarajia kufuturu na watoto yatima jioni.

Kabla ya wimbo huo aliipokea kadi ya Mgesi na kumshukuru kwa kutambua ubaya wa Chadema.

Hafla hiyo iliongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula na kushuhudiwa na wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Abdulrahman Kinana, Salome Joseph Mbatia, Omar Ramadhan Mapuri na Jackson Msome.

''CHADEMA inakabiliwa na mgogoro mkubwa unaofukuta kutokana na ubinafsi wa kukumbatia fedha nyingi zilizotolewa msaada na chama cha upinzani cha Uingereza cha Conservative na zingine kutoka Norway,'' alisema Mgesi.

Chama cha Conservative cha Uingereza ndicho kilichounda serikali iliyokuwa ikiitawala Tanganyika wakati wa ukoloni hadi ilipopata uhuru.

Alisema yeye alipokuwa mwenyekiti wa mkoa alishiriki kuandaa bajeti ya uchaguzi kwa chama hicho na kwamba ilifikia sh. bilioni tatu, lakini baada ya kupokea misaada kutoka kwa wahisani, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, hataki tena kuonana na wenzake.

''Baada tu ya magari, pikipiki na baiskeli kufika, uongozi wa Chadema taifa ulikata mawasiliano na wala sijui fedha walizopokea zinatumika kwa kitu gani,'' alisema.

Alisema ameamua kuachana na kuwania ubunge na uanachama wa Chadema kwa sababu baadhi ya wagombea wa udiwani na ubunge mkoani Morogoro wameanza kulalamikia tabia ya uongozi wa chama hicho kitaifa kuwanyima fedha za kampeni.

Katibu Mkuu wa CCM, Mangula ,akizungumza kwenye hafla hiyo alionyesha kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya vyama vya upinzani kutaka kuwarudisha wakoloni nchini.

Alishangaa pia kuona nchi kama Norway ikitoa misaada kwa siri kusaidia upinzani nchini.

 

 

 

CCM imekodi ndege kwa safari ya mgombea mwenza Tabora

 

MGOMBEA mwenza wa urais kupitia CCM, Ali Mohamed Sheni.

 

Na Seleman Bitala, Mwanza

CHAMA Cha Mapinduzi kimeeleza kimekodi ndege kwa safari ya mgombea mwenza wa urais Tanzania kwa tiketi ya CCM mkoani Tabora, Dk. Ali Mohammed Sheni kwa kutumia ndege ya serikali.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Kamishina wa Tume ya Uchaguzi Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu Harun Mahundi, alipojibu swali la Edward Mboje wa UDP katika mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dola na

serikali katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela uliofanyika kwenye ukumbi wa jiji.

Mboje katika kipindi cha maswali baada ya kupokea taarifa ya Tume kuhusu hali ya kampeni alilalamikia taarifa hiyo kuwa ya upande mmoja na

kwamba sio sahihi kwa sababu katika uzinduzi wa kampeni zake Wilaya ya Nyamagana CCM walitumia magari ya serikali na wakuu wa Wilaya wakiwepo ili hali kwenye kampezi za vyama pinzani hawaendi hivyo kutovitendea haki vyama vya hivyo.

Mbali ya kutumia magari na rasilimali za serikali kwa safari za kampeni zao CCM pia alidai wamekuwa wakitumia Ndege za serikali, suala ambalo kamishna alisema tayari alipokea malalamiko kama ilivyosikika katika baadhi ya vyombo vya habari na kwenye kikao cha maadili cha Tume CCM walionyesha listi za kukodi ndege hiyo.

"Hivi sasa ndege za serikali zinakodishwa kwa yeyote anayeweza kulipia gharama zake awe mfanyabiashara ama chama chochote lakini hakuna chama chochote kinachoruhusiwa kutumia magari na rasilimali nyingine za serikali kufanyia kampeni," alifafanua Kamishna Mahundi.

Akijibu swali lake la pili ambalo lililalamikia baadhi ya vyama kukosa Ruzuku, Mahundi alisema Tume haitoi ruzuku bali Msajili wa Vyama vya Siasa kwa sifa zinazotakiwa ili usajili wa vyama vya siasa visigeuzwe kuwa miradi ya kujipatia pesa, mfumo ambao sio wa Tanzania peke yake bali dunia nzima kwa kupishana vigezo vya sifa stahili kulingana na mazingira ya nchi husika.

Ili vyama hivyo viweze kupata ruzuku alivitaka vijenge hoja zitakazo mshawishi Msajili wa Vyama aridhike kubadili utaratibu wa sasa unaowanyima ruzuku wale wasiofikisha sifa zinazokubalika.

Akijibu swali la Alfred Samson kutoka TADEA ambaye alilalamikia vyombo vya habari hasa TV kuwa na upendeleo katika kuonyesha na kutangaza habari za wagombea huku wakiipa CCM muda mrefu kuliko vyama vingine, alisema vyombo visivyo milikiwa na serikali viko nje ya uwezo wa tume yake, lakini makubaliano yaliyoko ni kutangaza bila kuegemea upande wowote.

"Kwa mujibu wa kanuni na masharti ya kufanya kampeni, CHAMA chochote cha siasa hakiruhusiwi kufanya kampeni kwenye luninga bali kwenye mihadhara ya majukwaa na nyumba hadi nyumba".Alisema.

Vyama vilivyohudhuria mkutano huo vilikuwa TLP, UDP, DP, NCCR, CCM, CUF, TADEA na CHADEMA ambavyo havikufika kwa kuwa havina ofisi mjini Mwanza. Vyama hivyo ni CHAUSTA, NLD, FORD, PPT-MAENDELEO na DEMOKRASIA MAKINI.

 

Watakiwa kumuandalia ‘mazishi ya heshima’ Kabourou kutokana na kifo cha kisiasa

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

WANACHAMA na wakereketwa wa CCM katika jimbo la Kigoma mjini, wametakiwa kumuandalia 'mazishi ya heshima’ ya kisiasa mbunge wa jimbo hilo anayemaliza muda wake Dk.Walid Aman Kabourou, ambaye anagombea tena nafasi.

Mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Peter Serukamba, aliwaambia wapiga kura wa jimbo hilo katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika katika eneo la Katonga Migazini juzi.

Serukamba alisema mwisho wa enzi za Dk. Kabourou kuendelea kuwa mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini umewadia, kwani ana hakika ya kumshinda katika uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo amelifananisha na 'kifo' cha kisiasa cha mbunge huyo.

Alisema dalili za Kabourou kushindwa katika uchaguzi ujao zimeshajionyesha kufutia mbunge huyo kutumia muda wake mwingi kuwa nje ya nchi kuliko kuzunguka jimboni mwake kuomba kura.

Mgombea huyo aliwataka wana CCM katika jimbo hilo kumuandalia 'mazishi' ya heshima Dk. Kabourou wakati wa 'kifo' chake hapo Oktoba 30 mwaka huu, siku ambayo Watanzania watapiga kura kuwachagua wabunge, madiwani na rais wa nchi.

"Mwanamume akiwa 'anakufa' msaidieni 'afe' kiume kwa heshima, na kwa sababu 'kifo' cha Kabourou kimewadia, tumuandaliea 'mazishi' ya heshima hapo oktoba 30 mwaka huu," alisema Serukamba.

Mgombea huyo amemtaka Dk. Kabourou awaeleze wananchi wa jimbo hilo ubunge wa Afrika umewasidia kwa kiasi gani wananchi hao tangu alipochaguliwa kuwa katika nafasi hiyo, kutokana na maneno kutoka kwa wananchi hao yakieleza kuwa ubunge huo hauna manufaa yoyote kwao.

Serukamba alisema kuwa tofauti na wabunge wenzake waliofanya vitu vya kuonekana, Dk. Kabourou amekuwa akijinufaisha kwa posho anazolipwa anapohudhuria vikao katika bunge hilo bila kuwasaidia wananchi wake.

Alitoa mfano wa mbunge wa Kisarawe, Athumani Janguo wa CCM, ambaye alitoa kompyuta 80 kwa shule za sekondari zilizoko katika jimbo.

Sambamba na hayo mgombea huyo amewaahidi wananchi wa kata hiyo ambao wengi wao ni wavuvi, kuwafanya wafaidi na kutumia kikamilifu fursa ya Ziwa Tanganyika lililopo katika eneo lao.

 

Ngawaiya: CHADEMA inawapotosha wananchi Thomas Ngawaiya

Na Rodrick Makundi, Moshi

 

 

Thomas Ngawaiya

MPIGA debe mkuu wa CCM katika jimbo la Moshi vijijini, Thomas Ngawaiya, amedai kauli iliyotolewa na mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo haina ukweli, ila imelenga kuwapotosha wananchi ili wasiipigie kura CCM.

Juzi mgombea ubunge wa Chadema, Anthony Komu, alikaririwa akidai kumtaka Ngawaiya kurejesha sh. milioni 60 za wananchi, alizopewa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo wakati akiwa mbunge.

Katika kauli hiyo pia mgombea huyo wa Chadema, alidai Ngawaiya anapaswa kurejesha fedha hizo kwani baada ya kuhama upinzani na kuhamia CCM, alishindwa kuleta maendeleo katika jimbo hilo.

Ngawaiya akizungumzia madai hayo, alisema mgombea huyo wa Chadema hana hoja ya msingi, kwani fedha alizozitaja ni sehemu ya mshahara wake wa ubunge katika kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, alisema mgombea huyo hana hakika na Anachokizungumza, kwani serikali ilimpa Ngawaiya zaidi ya milioni 100 zikiwa mshahara, na fedha za maendeleo zinatolewa na serikali kuu kwa halmashauri husika.

"Fedha za maendeleo hutolewa kwa mkurugenzi wa halmashauri ambaye anakuwa na jukumu la kuzigawa kwa madiwani ili ziende kufanya shughuli za maendeleo, na sio kama alivyodai mgombea huyo," alisema Ngawaiya.

"Labda hafahamu kwamba serikali pia haitoi fedha kwenye halmashauri bila ya kurejesha mahesabu ya matumizi ya fedha ambazo zimetolewa mwanzo, na anayerejesha mahesabu hayo ni mkurugenzi kwa kuainisha shughuli za maendeleo ambazo halmashauri imefanya," aliongeza.

Katika hatua nyingine alidai kuwa wakati akiwa mbunge jimbo la Moshi vijijini, aliwaletea wananchi wa kata ya Mabogini maendeleo, ikiwemo ununuzi wa darubini yenye thamani ya sh. milioni 1.8, na kusaidia kuondoa kero za wananchi kufuata huduma katika hospitali ya Mawenzi mjini hapa.

Pia alisema aliwezesha ujenzi wa choo katika soko la Nkoringa kata ya Kibosho, chenye thamani ya zaidi ya

Sh. milioni tano, pamoja na uchagiaji wa zaidi ya sh. milioni 11 katika shule za msingi na sekondari kwenye jimbo hilo.

Ngawaiya aliongeza kuwa kauli ya mgombea huyo imelenga kuipaka matope CCM, pamoja na kushawishi wananchi wasiipigie kura jambo ambalo alimshauri aachane na siasa za malumbano badala yake anadi sera za chama chake.

Alisema huu ni wakati wa kila chama cha siasa kunadi sera zenye lengo la maendeleo na sio kutumia majukwaa ya kisiasa kupakana matope.

"Mtu anayetakiwa kurejesha fedha za serikali ni yeye maana alisomeshwa na serikali na hajawafanyia wananchi lolote, kwa hiyo hafai kuwa mbunge maana akipewa nafasi hiyo atakuwa anatafuta maendeleo yake na sio ya wananchi," alidai Ngawaiya.

Kwa upande mwingine aliwataka wananchi wa kata ya Mabomgini kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Cyrill Chami, ambaye ni mmoja wa watendaji serikalini na aliye na uzoefu wa uongozi.

Alisema mgombea huyo amekuwa akimshauri rais masuala mbali mbali ya kuiuchumi na amekuwa akitambua hali ya maisha ya Tanzania, ikiwemo kutafuta njia za kuyatatua kwa kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

 

TUICO yashauri rais ajaye akutane na wafanyakazi

Na Pendo Mangala, Dodoma

CHAMA cha Wafanyakazi wa Viwanda Biashara, Taasisi za Fedha huduma na ushauri (TUICO), kimemshauri na kumuomba rais ajaye, kuweka utaratibu wa kukutana na wafanyakazi kila baada ya miezi minne kama ilivyokuwa kwa Rais Benjamin Mkapa.

Ushauri huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa TUICO Taifa, Bonifaces Mkakatisi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye semina ya Kamati ya Utendaji na Baraza Kuu la chama hicho, kwa lengo la kuwaelimisha sheria mpya za kazi iliyofanyiwa marekebisho na Bunge mwaka jana.

Mkakatisi alisema endapo rais ajaye ataweka utaratibu huo wa kukutana na wananchi kila baada ya miezi mnne utasaidia kutatua matatizo mbali mbali ambayo wafanyakazi wamekuwa wakikumbana nayo kama lile ambalo limekuwa likilalamikiwa sana ya wafanyakazi la kukatwa kodi.

Alisema wafanyakazi wamekuwa wakiilalamikia serikali kwa utaratibu uliowekwa wa kuwakata kodi wafanyakazi, wakati wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipata faida kubwa kwa mwezi hawakatwi kodi.

Katibu huyo alisema utaratibu huo unachangia kudumaza juhudi za wanafakazi katika kujiondoa na umaskini kutokana na kwamba ni wafanyakazi wachache wanaolipwa mishara kwa kima cha juu.

Hata hivyo, aliwalalamikia wamiliki wa kampuni mbali mbali wanaonunua baadhi ya kampuni na viwanda hapa nchini, kwa kutoa ahadi za kuviendeleza, lakini baada ya muda viwanda hivyo wanavitelekeza bila ya serikali kuchukua hatua yoyote.

Alisema mbaya zaidi ni ile tabia ya ubaguzi ya kuwaajiri wafanyakazi wengi kutoka nje ya nchi na kuwalipa mishahara mikubwa kwa madai kuwa Watanzania hawana uwezo, hata kama itabainika kuwa wapo walio na uwezo kuliko wa wafanyakazi kutoka nje.

Akifungua semina hiyo, Mwenyekiti wa TUICO taifa, Omary Ayubu, aliwataka wajumbe kuwa makini wakati wa majadiliano ya sheria hiyo, ili wakawaelimishe ipasavyo wanachama katika matawi yao na hatimaye waielewe vizuri ili itakapoanza kutumika isiwe mpya kwao.

Alisema pamoja na kwamba bado sheria hiyo ina mapungufu, wanachotakiwa ni kuisoma na kuielewa, na baadaye baada ya kupokelewa watakuwa na haki ya kulalamikia vipengele ambavyo vitakuwa haviwapi haki.

Aliwataka kuacha malumbano na migogoro mbali mbali ndani ya chama ili kuungana kwa pamoja katika kukiendesha chama hicho na hivyo kiwe mfano kwa wengine na waweze kuvutwa nacho ili kutetea maslahi ya wafanyakazi.

Sheria hizo zilizofanyiwa marekebisho ni pamoja na sheria ya taasisi za kazi ya mwaka 2004 na sheria ya ajira na uhusiano kazini.

 

Aonya uuzwaji holela shahada za kupigia kura

Prosper Kulita, Morogoro

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Kingorwila Dumba Omary Manispaa ya Morogoro ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuingilia katika uuzwaji holela wa shahada za kupigia kura unaofanyika katika baadhi ya vijiji vinavyounda kata hiyo.

Dumba alitoa kilio hicho mbele ya mgombea ubunge wa jimbo la Morogoro mjini Dk. Omary Mzeru, wakati wa mkutano wa kampeni ulifanyika katika kijiji cha Tubuyu.

Alisema kumekuwepo na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamekuwa wakifika katika vijiji vinavyounda kata hiyo ambapo wamekuwa wakiwarubuni wananchi kwa kununua shahada hizo kwa shilingi 5000 .

Alisema kutokana na zoezi hilo haramu anaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuinglia kati na kuzuia oezi hilo hilo ili kuweza kunusuru hali ya upigaji kura katika siku za usoni na katika uchaguzi wa mwaka huu.

Hata hivyo aliwasifu wananchi walioonyesha moyo wa uzalendo kwa kukataa kuuza shahada zao, ambapo alisema kuwa shahada hiyo ni moja ya heshima kwa Mtanzania ambapo pia inatumika kukutambulisha katika sehemu nyingi ambazo utahitajika kutoa kitambulisho endapo utakuwa huna.

Akihutubia wananchi katika kijiji hicho Dk. Mzeru alisema wananchi watunze shahada zao na wasikubali kurubuniwa na mtu wa aina yeyote na endapo watajitokeza watoe taarifa kwa uongozi wa kijiji na hata polisi ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema utaratibu wa kununua shahada unadhihirisha jinsi gani vyama hivyo visivyo na uhakika wa kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambapo alisema kwa staili hiyo CCM itaendelea kuongoza nchi.

Wakati huo huo wananchi hao walishikwa na butwaa pale kaka wa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CUF Mahiku Maharagande alipopanda jukwaani kunadi sera za CCM huku akimwelezea mgombea wa CF kuwa ni mtu anaependa madaraka bila kujali anatakiwa kuyagawa kwa wananchi.

Mbarala Maharagande ambae pia ni katibu wa CUF wilaya ya Morogoro Mjini anawania nafasi za ubunge jimbo la Morogoro mjini na pia udiwani katika kata ya Sultan Manispaa ya Morogoro.