UHURU 10.09.2005

 

 

 

Mauaji ya kinyama ya kisiasa D'Salaam

Na Esther Katua

WATU watatu, akiwemo Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi, tawi la  Midizini  Manzese,  Dar es Salaam, Mwajuma Nyanza (53) wamekufa baada ya nyumba yao kuchomwa moto usiku wa kuamkia jana, katika tukio ambalo linahisiwa ni la kisiasa.

Wengine waliokufa ni watoto Mwajuma Rashid (16) na Sambali Lusian (11). 

Majeruhi, ambao hadi jana jioni hali zao zilikuwa mbaya wakiwa wamelazwa hospitali ya Muhimbili, ni mtoto David John (3) na Asha Rashid (13). Nyanza alifariki jana jioni akipatiwa matibabu Muhimbili.

Kamanda wa polisi mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, alikaririwa jana jioni na chombo kimoja cha habari akithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtu mmoja anahojiwa na polisi, huku uchunguzi ukiendelea.

Tibaigana alisema kwamba chanzo cha moto ni petroli inayosadikiwa kumwagwa kupitia mlango.

Akizungumaza na mwandishi wa habari hii katika eneo la tukio,   mtoto wa marehemu, ambaye pia ni mjumbe wa shina la CCM  eneo hilo, Nia Shabani (28) alidai tukio hilo limefanywa na wafuasi wa chama cha  CUF.

Alidai   siku mbili zilizopita kulifanyika mkutano wa kampeni za CCM eneo la Midizini  na  wakati mama yake akirejea nyumbani baadhi ya wafuasi wa CUF walikuwa wakimkebehi na kumwambia watamwonyesha kwa kuipenda 'Yeboyebo', wakiwa na maana ya CCM.

Alidai juzi mama yake akitokea kwenye kikao cha CCM alifuatwa kwa karibu na vijana watatu, hali iliyomtia hofu, na kwamba vijana hao walimfuata hadi nyumbani kwake na baada ya yeye kuingia ndani walipitiliza, ndipo saa chache baadaye nyumba ilichomwa.

Nia alidai kuwa majirani walimfuata nyumbani kwake na kumweleza habari za moto saa nane usiku na kudai kuwa waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walifungiwa mlango kwa nje kabla ya kuchomwa moto.

"Niliambiwa mlango ulikuwa umefungwa kwa nje, ndiyo maana walishindwa kutoka, mmoja alikufa hapa hapa, mmoja amefariki mapokezi Muhimbili," alidai.

Akizungumza eneo la tukio, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya  Taifa  ya CCM, Salum Londa, alisema kitendo kilichotokea si cha kiungwana na kwamba kwa mtindo huu unaofanyika Watanzania hawawezi kujenga nchi ya amani na umoja.

"Huu siyo uungwana, siwezi kuongea zaidi, taifa  haliwezi kujengwa hivi, hili si jambo la kujenga umoja hata siku moja", alisema Londa.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama, Luteni mstaafu Yusuf Makamba, alisema bado ni mapema kuzungumzia chochote kwenye tukio hilo.

" Hatuwezi kusema ni wanasiasa au  vinginevyo. Hatuwezi kuzungumza chochote kwa sasa hadi polisi wafanye uchunguzi wao. Hivyo tunasubiri  taarifa ya polisi", alisema Makamba.

 

 

Wapuuzeni wanaodai CCM inawadharau viongozi wake, asema Mapuri

Na Mwandishi  Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi kimewataka Watanzania kuwapuuza  baadhi ya wagombea urais wa upinzani wanaopanda mbegu za fitina kwa kudai kwamba CCM inawadharau viongozi wake akiwemo Makamu Mwenyekiti (Bara), John Malecela.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Omar Ramadhan Mapuri alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba mjini Dar es Salaam jana.

Mapuri alisema baadhi ya wagombea urais wa upinzani na hasa CUF wamekuwa wakieneza mbegu za fitina kwamba CCM imewadharau Malecela na Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Salim Ahmed Salim ndiyo maana hawakuteuliwa katika mchakato wa kuwania nafasi ya kugombea urais kupitia CCM.

Alisema CUF wanadai kuwa CCM haikumpitisha Malecela kwa kuwa ni mzee na ilimbagua Dk. Salim kutokana na rangi yake.

Mapuri alisema CUF na wengine wameishiwa sera na wameanza kutangaza sera za ubaguzi kwa lengo la kujenga fitina ndani ya CCM.

Katibu alisema Malecela hakujaza fomu ya kuomba kuteuliwa kwa hoja ya uzee na wala Dk. Salim hakujaza fomu ya kuomba kuteuliwa kwa hoja ya rangi yake.

Mapuri alisema CCM ilifanya uteuzi wake wa haki na kila mwenye macho aliona na kwamba kama Dk. Salim alikuwa amebaguliwa kwa rangi yake asingefika hata Chimwaga, tena akashika nafasi ya pili.

Alisema hoja ya uzee nayo imekuwa ikipingwa hata na mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete kwamba CCM itaendelea na wazee na nchi bila wazee inaweza kuwaka moto.

Mapuri aliwataka wana-CCM kutokubali kurudishwa nyuma kwa hoja ya kibaguzi na kwamba wapinzani wenyewe walikuwa wakiwatolea macho wana-CCM ambao hawakuteuliwa kugombea.

Alisema iwapo CCM ingekuwa na viongozi wabaya wapinzani wasingeweka milango wazi kwa wana-CCM walioachwa kuteuliwa katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani.

Kuhusu hoja ya CUF ya kuipa siku saba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa iwe imehakiki daftari hilo kwa kutumia wataalamu wa nje, Mapuri alisema huko ni kutoa vitisho na kuingilia uhuru wa ZEC.

Mapuri alisema kuwa mgombea urais wa CUF Seif Sharif Hamad na mgombea urais wa CCM Amani Abeid Karume walikubaliana kuwa waiache ZEC ifanye kazi zake bila kuingiliwa.

Alisema kinachoshangaza Maalim Seif baada ya kutoka kwenye mazungumzo hayo akageuka na kutoa siku hizo saba na baadaye kwenda nje kufanya mkutano na vyombo vya habari vya nje.

Mapuri alisema tabia ya CUF kupenda mambo ya nje ni dalili za kupenda kutawaliwa na kwamba hali hiyo inatia wasiwasi kama chama hicho kitaweza kutawala bila kufuata amri  ya nje kama kilivyozoea.

Alisema CCM inakubaliana na ZEC kwamba daftari litakaguliwa ndani ya nchi na wataalam wa nje wanaweza kutumika kama kutakuwa na haja, lakini kwa sasa ZEC imesema ina uwezo wa kumalizia kazi ya uhakiki wa daftari hilo.

 

 

Malecela: Nitahakikisha uaminifu wangu kwa CCM hautiliwi shaka

Na Bashir Nkoromo, Dodoma

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara), John Malecela, ameweka nadhiri kwamba atahakikisha uaminifu wake kwa CCM na taifa hautiliwi shaka hadi anakwenda kaburini.

Nadhiri hiyo aliitangaza jana mbele ya mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye kijiji cha Mvumi kilichopo katika jimbo la Mtera, Dodoma vijijini.

“Nduguzanguni nawahakikishieni, uaminifu wangu kwaChama Cha Mapinduzi na taifa letu nitahakikisha hautatiliwa shaka hadi nakwenda kaburini” alisema Malecela ambaye alikuwa ni miongoni mwa wanachama kumi walioomba ridhaa ya CCM kuwania Urais.

Akizungumza baada ya kunadiwa na Kikwete kwenye mkutano huo, Malecela ambaye anawania Ubunge, alisema CCM haina sababu ya kushindwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, kwa sababu ndiyo ‘baba lao’.

Malecela aliwataka wananchi wa jimbo la Mtera na Watanzania wote kwa jumla kumpigia kura Kikwete na kuahidi kumpa ushirikiano mgombea huyo wa Urais pindi akishika kiti hicho.

Malecela alisema CCM tayari imekwishalima shamba na wapinzani bado wana pori tupu, hivyo la maana ni kuipa CCM mbegu (kura) ili sasa ipande katika shamba hilo kwa kuwa wakiwapa wapinzani mbegu hizo itabidi walime kwanza shamba.

“Hivi nduguzanguni mimi nina shamba nililokwisha lilima na mwenzangu ana pori tupu nani mtampa mbegu?” Malecela aliuuliza umati wa wananchi kwenye mkutano huo ambao ulilipuka “mbegu tutakupa weweee!”

Akimnadi kwenye mkutano huo, Kikwete alimsifu Malecela kuwa ni lulu katika CCM na nchi kwa jumla kutokana na uwezo wake katika masuala ya siasa na uongozi thabiti.

“Huyu ni mzee anayetegemewa mno na CCM, taifa na hata Bunge, hivyo ni vema kabisa mhakikishe ndugu wananchi wa jimbo hili mnamchagua,” alisema Kikwete huku akishangiliwa.

Kikwete aliahidi kuutumia vilivyo uwezo wa Malecela akifanikiwa kushika kiti cha urais. “Wazee kama hawa ni muhimu kuwa nao karibu katika uongozi… ndiyo watu muhimu wa kuegemea ili uweze kupata ushauri mzuri wakati yanapotokea matatizo,” alisema Kikwete.

Kuhusu wapinzani, Kikwete alisema wananchi wasiwachague kwa sababu hawana la msingi la kuifanyia nchi ambapo hadi sasa wameshalieleza kwa sababu wanajua wasilotaka, lakini wanalotaka hawalijui.

“Mkiwaona wanapitapita hapa kutafuta ubunge hawana lolote ni waganga njaa tu ambao wanaona wajaribu kwenye ubunge labda wataponea huko njaa zao,” alisema Kikwete.

Akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Kikwete alisema, kazi kubwa itakayofanywa na uongozi wake akiwa rais ni kuhakikisha kasi ya kukuwa kwa uchumi inaongezeka ili kuboresha maisha ya wananchi.

Kikwete alisema, ili kufikia lengo hilo serikali yake itahakikisha yanafanyika mapinduzi makubwa katika kilimo kwa kuwawezesha wakulima kutumia zana bora na kupata pembejeo kwa wakati na kwa gharama wanazoweza kuzimudu.

Alisema, vilevile itafanyika mikakati ili wananchi hasa vijana na kinamama wawezeshwe kwa kupata mitaji itakayowafanya wajiajiri wenyewe katika shughuli zao.

Kikwete anatarajiwa kuendelea na ziara yake ya kampeni leo katika wilaya ya Kondoa kabla ya kurejea mjini Dar es Salaam.

 

 

Vodacom yashukuru Watanzania kuwafikisha walipo kibiashara

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania, Romeo Kumalo, amewashukuru Watanzania kuwa ndio chanzo kikuu cha kuwafikisha walipo sasa kibiashara. 

Romeo aliyasema hayo juzi jioni katika Hoteli ya Slipway, Msasani Dar es Salaam, ambapo kampuni hiyo ilizindua toleo jipya la matangazo ya kibiashara kwa kutumia ubunifu wa nchini.

“Ni Watanzania wenyewe waliotuwezesha kuwa kama tulivyo leo,” alisema Kumalo na kunukuu kibwagizo chake: “Taifa moja lenye mtandao mmoja”.

Alitaja mazingira yaliyotumika kuandaa matangazo hayo ya picha na televisheni, ni katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Pwani na Zanzibar.  

Kwa mujibu wa Kumalo, kampuni hiyo imedhamiria kuwanufaisha Watanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Vodacom Afrika Kusini na makao makuu yake nchini Uingereza.

Hafla hiyo ilipambwa na burudani ya muziki katika hoteli hiyo iliyo katika ufukwe wa bahari Hindi.

Vodacom ni kati ya kampuni nne zinazotoa huduma zas simu ya mkononi. Nyingine ni Mobitel, Zantel na Celtel. Zamani ilikuwepo Tritel, lakini haipo tena katika biashara.

 

 

Serikali inachukua hatua za kuboresha utendaji TAMISEMI

Na Peter Orwa

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI), Diotrephes Mmari, amesema serikali inachukua hatua ya kuboresha utendaji wa Serikali za Mitaa, kwa kuajiri watalamu wapya na wahasibu kupelekwa mafunzoni.

Mmari, alitoa taarifa hiyo jana, katika kikao maalum cha Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini, katika hoteli ya Kunduchi Beach, kujadili jukumu la sekretarieti za mikoa katika kusimamia utendaji wa halmashauri.

Meneja Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Utendaji wa Serikali za Mitaa nchini, Alfred Kabagile, alidokeza kuwa ajira hizo mpya ni sehemu ya mkakati wa kuboresha nguvu kazi katika mfumo wa serikali za mitaa, kwani ilionekana kuna udhaifu.

Kwa mujibu wa Kabagile, serikali imetangaza nafasi mpya za ajira ya wataalamu 138, ambapo baadhi ya nafasi hizo zimeshaanza kutangazwa magazetini.

Aidha, mafunzo maalum ya wahasibu ni mahsusi kwa wahazini wa wilaya ambao hawana sifa ya kuwa na shahada ya juu inayotambulika na Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Fedha (NBAA), yaani CPA.

Kwa mujibu wa Mmari, mpango wa kurekebisha muundo na utendaji wa serikali za mitaa unalenga kuiletea ufanisi, ili ielekeze huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu. Utekelezaji huo upo katika awamu ya pili unaojulikana kama “Mpango wa Kati”.

Alisema juhudi hizo zimefanyika kutokana na udhaifu uliojitokeza katika maeneo ya uwajibikaji, ujuzi na elimu ya watendaji wake.

Mmari, alitoa mfano wa utafiti uliowahi kufanywa kuwa asilimia 60 ya wananchi kuwa hawaridhiki na utendaji wa serikali za mitaa, kulinganisha na kiwango cha asilimia 25 wa serikali kuu kupitia vigezo hivyo hivyo.

Makatibu Tawala waliokutana kuanzia jana, katika kikao cha siku mbili walitarajia kujadili mkakati huo wa utekelezaji ambao umeshaidhinishwa na serikali, kutokana na muundo wa ofisi zao kuwa ndio sekretarieti inayosimamia halmashauri ya miji yao.

Katibu Mkuu huyo wa TAMISEMI, pia alisema ripoti za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali imebaini kuwa kwa kiasi kikubwa kuna matumizi yasiyo sahihi ya fedha za serikali zilizoidhinishwa katika bajeti.

Mmari, alisema kuwa mpango wa mabadiliko hayo katika awamu ya kwanza uligharimu sh. bilioni 32 na awamu ya pili, inayotarajiwa kukamilika mwaka 2008 inakadiriwa itatumia sh. bilioni 70. Zaidi ya asilimia 90 ya mradi unagharamiwa na wafadhili.

Leo Makatibu Tawala hao, wanatarajiwa kusikiliza na kujadili ripoti ya mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo wa serikali ya mitaa kama yalivyofanyiwa mchanganuo na wataalamu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wengine wanaohudhuria mkutano huo ni watendaji waandamizi kutoka Wizara za Maji na Maendeleo ya Mifugo, Kilimo na Chakula na Ushirika la Masoko. Pia, wapo wataalamu wa kigeni na kutoka kutoka katika Mradi wa Programu wa Mabadiliko katika Serikali za Mitaa.

Kwa mujibu wa mkakati uliopo, watendaji wote wa programu hiyo baada ya mradi kumaliza kazi yake wataunganishwa katika wizara husika na Halmashauri zake kuitumikia ili ujuzi wao utumike huko.

Hivi karibuni, katika hotuba yake ya kufunga warsha ya namna hiyo, kuhusu mabadiliko ya utendaji ndani ya Serikali za Mitaa huko Bagamoyo, Mmari alisema kuanzia sasa kutakuwepo ufuatiliaji wa karibu wa uwajibikaji kwa wakuu wa idara walio chini ya ofisi yake.

 

 

 

 

Mbowe amiminia sifa kibao Rais Mkapa

Na Omari Shaaban, Arusha

MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, amesema kuwa rais wa sasa anayemaliza muda wake wa Tanzania, Benjamini Mkapa, hakuwa mtu hatari wala mbinafsi kwenye uongozi wake.

Mbowe aliyazungumza hayo jana kwenye mkutano wake na wananchi, katika uwanja wa NMC, mjini hapa wakati akijinadi apewe ridhaa ya wananchi ya kuwa rais wa Tanzania kupitia CHADEMA.

Huku kukiwa na watu wachache anaowahutubia uwanjani hapo alisema, kuwa uongozi wa rais Mkapa ulikuwa mzuri kwa kuwa ulikuwa haubagui mtu wa kumpa madaraka ya kiutawala na uongozi.

“Mkapa siyo mtu hatari kwa watanzania wala mbinafsi… au siyo wananchi? Kwa hiyo basi tuangalie uchaguzi huu utakuwaje, na wala hakuweka ndugu zake kwenye nafasi za nchi,” alisema.

Mgombea huyo urais wa CHADEMA,  ambaye aligeuza jukwaa uwanja wa kuwateta viongozi mbalimbali wenzake wa upinzani na wa CCM, badala ya kunadi sera zake, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kuondoka kwenye mkutano huo bila hata ya kuendelea kumsikiliza.

 

Mbowe kama hilo halitoshi katika mkutano huo alishindwa kabisa kunadi sera zake za uongozi wake na kuanza kuwashambuliwa viongozi wa dini kama vile maaskofu.

“Nawashangaa maaskofu nao kuingilia masuala ya kisiasa… wanadhubutu kusema kuwa mmoja wa wagombea urais wa nchi hii ni chaguo la Mungu… si mtaji mnafahamu. Wananchi nichagueni mimi niwe rais wenu,” alilalama mgombea huyo.

Alisema kuwa akiwa rais wa Tanzania, atabadilisha miundo mbinu ya uongozi na kwamba hakutakuwa na baadhi ya nyadhifa ambazo kwa sasa zipo, huku wananchi ‘kiduchu’ waliokuwa wakimsilikiza walionyeshwa kushangazwa na kauli hizo.

Hata hivyo, siyo tu kwenye mkutano wake tu wa jana uliohudhuriwa na watu wachache, bali hata kwenye mikutano yake aliyofanya wilayani Arumeru, eneo la Kikatiti ilikosa watu kabisa.

Wananchi kadhaa wakilizungumzia hilo, walisema kuwa ni kutokana na wagombea wa upinzani kushindwa kunadi sera zao na badala yao wamekuwa wakitoa maneno ya kashfa na ya chuki ambayo wananchi hawanufaiki nayo.

Mbowe aliingia mjini hapa siku nne zilizopita kwa ajili ya kujinadi kwa wananchi ili apate ridhaa yao kumchagua awe rais wa Tanzania kupitia CHADEMA, kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.

 

 

 

Karume azungumzia utekelezaji wa ujenzi taasisi za mafunzo

RAIS wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amesema Serikali ya Mapinduzi itahakikisha kuwa programu zote za miradi ya ujenzi wa taasisi za mafunzo zinatekelezwa kwa wakati.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi mara tu baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo la Elimu Mbadala, linalojengwa katika mtaa wa Rahaleo mjini Zanzibar.

Karume alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuhakikisha kuwa vyuo vikuu vinaimarishwa, shule za msingi na sekondari na vituo vya elimu mbadala vinajengwa ili kuendelea kutoa fursa ya elimu kwa watoto nchini.

Maendeleo ya elimu Zanzibar yamefikia hatua nzuri ya kuridhisha na hakuna budi kutumia hatua iliyofikiwa ili kuendeleza maeneo mengine ya maendeleo, alisema Rais Karume.

Rais Karume alikemea tabia ya upinzani ya kubeza na kupotosha ukweli juu ya maendeleo ya elimu. "Kigezo kinachoweza kutumika ili kupima maendeleo ya elimu Zanzibar inafaa kulinganisha maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar na yale yaliyofikiwa na nchi jirani."

Aliendelea kusema kuwa Zanzibar hatuko nyuma katika kukamilisha Malengo ya Milenia hasa kwa upande wa elimu ya lazima. "Hakuna nchi jirani ambayo imeweza kufikia Malengo ya Milenia kwa upande wa elimu ya msingi," alisisitiza Rais Karume.

Mapema, Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo, Haroun Ali Suleiman alisema katika hatua za kuimarisha maendeleo ya sekta ya elimu Zanzibar, Serikali itachukua juhudi za kuipitia na kuirekebisha sera ya elimu kwa kuzingatia haja ya kuongeza maslahi ya walimu na watendaji wengine.

Waziri Haruon alisisitiza juu ya ukweli wa maana halisi ya elimu bila malipo. Alisema serikali haitaruhusu wanafunzi kufukuzwa au kusimamisha wanafunzi kwa sababu kwamba hawajalipa ada.

Aliendelea kusema kuwa hakuna jambo jipya katika sera za upinzani kwa kusema kuwa watafanya elimu iwe bure, kwa sababu Serikali ya Mapinduzi imetangaza elimu bila ya malipo tokea mwaka wa 1964.

Mapema ilielezwa kuwa mradi wa ujenzi wa jengo la Elimu Mbadala unaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB). Hadi kukamilika kwake jengo hilo litagharimu jumla ya sh. 620,917,300 kati ya hizo, SMZ itachangia sh. 136,601,806 na ADB itachangia jumla ya sh. 484,315,494.

Jengo hilo linatarajiwa kukamilika Januari 10, 2006. Lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kuwasaidia watoto wanaozurura mitaani na waliokosa fursa ya kujiunga na shule kwa sababu moja au nyengine, hasa watoto wa kike waliopata mimba mapema au ndoa za mapema.

 

 

 

Msiwachague wanaojinadi kwa udini - Sheni

Na Ramadhani Mkoma, Liwale

MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Sheni, amewataka Watanzania kutokuwachagua viongozi wanaojinadi kwa misingi ya udini.

Dk. Sheni alisema hayo juzi alipohutubia maelfu ya watu  katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya elimu Liwale, mkoani Lindi katika siku ya kwanza ya kampeni mkoani hapa.

Alisema Tanzania haina dini isipokuwa wananchi wana dini zao na kwamba kila mtu ana imani yake ambayo haiwezi kuingiliwa na mtu yeyote.

"Serikali haina dini, lakini imetoa haki kwa watu wake kuabudu dini zao bila kuingiliwa na kulazimishwa. Iweje wanasiasa wasimame na kuhubiri dini kuhusisha na chama fulani?" alihoji.

Dk. Sheni aliongeza kuwa: "Watu wa namna hii wakija kuhubiri dini badala ya siasa wakataeni, kwani hawawafai. Kila mtu yuko huru kuishi na kuabudu dini aipendayo."

Mgombea mwenza pia aliwataka wananchi kutambua kuwa dini na siasa ni vitu viwili tofauti na kwamba hata madhehebu ya dini husajiliwa na Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali wakati vyama vya siasa husajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Awali, akimkaribisha mgombea mwenza, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Lindi, Dk. Ali Mohamed Mtopa alisema baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wanajinadi kwa kuchanganya dini na siasa.

Alisema hali hiyo inawafanya baadhi ya wafuasi wao kuhubiri siasa katika misikiti, hatua ambayo huhatarisha mshikamano wa kitaifa.

Dk. Mtopa alitoa mfano wa baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kukataa picha za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati huchangisha fedha zenye sura ya kiongozi huyo muasisi wa taifa.

"Viongozi hawa katika misikiti pia huhubiri siasa wakiwataka waumini wao kutokuichagua CCM kwa madai eti ni chama cha makafiri," alisema.

Katika hatua nyingine, Dk. Sheni aliwataka wananchi kuendelea kuichagua CCM iendelee kuongoza nchi kwa kuwa ina ilani na sera zenye mwelekeo wa maendeleo.

Alisema katika awamu ya nne ya serikali chini ya CCM, sekta ya kilimo itapewa kipaumbele ili kuwawezesha Watanzania walio wengi, ambao shughuli yao kuu ni kilimo kunufaika nacho na hatimaye kuondokana na umaskini.

 

Mwinyi asema uongozi  hapewi mtu ili ajifunze

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

RAIS mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, amesema uongozi si kitu cha kumpa mtu kujifundishia.

“Uongozi hupewa mtu mwenye uzoefu, mstahiki, muadilifu na mchapakazi,” alisema Mzee Mwinyi katika mkutano wa kampeni uliyofanyika uwanja wa Bopa, Makunduchi, juzi.

Alikuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni za Chama cha Mapinduzi, kumnadi mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Mzee Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM, aliuambia umati uliyofurika kwenye mkutano huo kuwa ‘mtu mwenye sifa hizo tumeshampata…’ na kabla hajamtaja jina wana-CCM na wananchi waliojazana kwenye uwanja huo walitamka kwa pamoja ‘Amani’ na Mzee Mwinyi akawaambia ‘barabaraa… mmenipunguzia kazi’.

“Nimefurahi leo mmekuja kuthibitisha kuwa Amani ndiye kiongozi wetu kwa miaka mitano ijayo,” aliuambia umati huo ambao ulimuhakikishia kuwa siku ya uchaguzi Oktoba 30, mwaka huu, wananchi wote wa Makunduchi na mkoa wa Kusini Unguja, watampa kura zao zote mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.

Rais huyo mstaafu wa Jamhuri ya Muungano alisema baada ya kumpa kura Amani katika uchaguzi mkuu ujao, wapiga kura wasisahau kuwa rais huchaguliwa na wasaidizi wa kumsaidia kuifanya kazi atakayopewa na wananchi, hivyo pia wawapigie kura wagombea wa CCM wa ubunge, uwakilishi na udiwani.

Alisema kwa kuwachagua wagombea wote wa CCM watamrahisishia Rais Amani Abeid Karume katika kutekeleza kazi ya kuwaongoza Wazanzibari na Watanzania kujiletea maendeleo yao na ya nchi yao.

Mzee Mwinyi aliwaomba Wazanzibari waliojiandikisha kupiga kura, kutofanya makosa ya kuchagua kiongozi atakayeingia Ikulu kwenda kujifunza uongozi, hali ambayo aliieleza kuwa itakuwa ni sawa na kucheza bahati nasibu.

Alisema mtu katika kujifunza anaweza akafanya vizuri ama vibaya, na akifanya vibaya wananchi ndiyo watakaojuta na kujilaumu.

Hakuna sababu alisema, wananchi kucheza bahati nasibu hiyo wakati Rais Amani Abeid Karume, ameshaonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza na ameiletea Zanzibar maendeleo makubwa katika miaka minne tu ya uongozi wake.

“Nasema miaka minne kwa sababu mwaka wa kwanza wa utawala wake kulikuwa na rabsha zilizosababisha hata askari wenu akachinjwa, au mmesahau?” aliuliza na kujibiwa ‘hatujasahau’.

“Mambo yale yalimshughulisha na yalimpotezea muda hadi yalipomalizwa kwa kufikiwa Muafaka mwaka 2001. Hivyo mwaka mzima ulipita hivi hivi. Miaka minne iliyosalia ndiyo amefanya kazi ya kuleta maendeleo yote haya mnayoyaona ya kujenga barabara, shule, hospitali na kuleta maji,” alisema

Alisema ikiwa katika miaka minne ameweza kuleta maendeleo makubwa kiasi hicho, ‘nakuombeni ndugu wananchi mumchague tena aongoze kwa miaka mitano ijayo, amalize ngwe. Alete maendeleo makubwa zaidi’.

 

 

CCM pekee ndiyo chama kisichochakaa, asema Karume

 kwa sababu kina demokrasia ya kubadili uongozi

Vingine sura ni zile zile tangu vilipoanzishwa

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

WAZANZIBARI wameombwa kukichagua Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo kwa sababu ndicho chama pekee Tanzania kisichochakaa, au kuwafanya wananchi wakichoke.

Kauli hiyo ilitolewa Makunduchi juzi na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume, alipohutubia mkutano wa kampeni.

Alisema CCM haichoki au kuwafanya wananchi waichoke kwa sababu ni chama kinachojibadilisha na kujisahihisha kila baada ya muda.

“Ni CCM pekee inayobadilisha sura za viongozi wake kila baada ya miaka 10. Viongozi waliopo sasa wengi wao hawakuwepo wakati wa Mzee wetu, Mzee Mwinyi. Na mimi kutokana na demokrasia ya chama chetu mkinipa ridhaa ya kuendelea, baada ya miaka mitano kitanipumzisha,” alisema Rais Karume.

Alisema ni kutokana na kubadilika huko kila baada ya muda, Chama cha Mapinduzi kimekuwa chama cha watu, kutokana na wanachama wake kuwa na nafasi ya kuchagua na kuchaguliwa katika uongozi wake.

Alisema kutokana na demokrasia hiyo ya CCM baada ya miaka mitano ijayo inawezekana kabisa vijana wengi wakawa viongozi katika chama chao, tofauti na vyama vingine ambavyo miaka nenda rudi sura za viongozi ni zile zile.

Rais Amani ambaye yumo katika kufanya kampeni za kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 30 mwaka huu, aliuambia umati wa maelfu ya watu walihudhuria mkutano wake kuwa si vyema Wazanzibari wakacheza bahati nasibu katika uchaguzi ujao.

Alisema CCM na wagombea wake ndiyo wanaofaa kuchaguliwa katika uchaguzi huo kwa sababu wameshaonyesha uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi, na rekodi yake ya kulinda haki za binadamu.

Alisema akichaguliwa kuendelea kuongoza Zanzibar kwa miaka mitano ijayo, atahakikisha kuwa viongozi wa kuchaguliwa ndiyo watakaopewa nafasi za kuongoza.

Wapinzani alisema, na hasa chama cha CUF hawafai kupewa uongozi wa nchi kwa sababu viongozi wake wameshaonyesha tabia za udikteta na kusababisha ghasia na kuhatarisha amani nchini.

Alisema viongozi hao wa upinzani wamekuwa na mkakati wa kuleta vurugu kwa muda mrefu tokea walipoingizwa katika uongozi wa chama na serikali kati ya mwaka 1977 na 1987.

Rais Karume alisema baadhi ya viongozi hao ndiyo waliyosababisha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa wakati wa utawala wa awamu ya pili iliyoongoza na Aboud Jumbe Mwinyi na hao hao ndiyo waliyosababisha vurugu za Januari 26 na 27.

Aliwaambia wana CCM na wananchi waliyohudhuria mkutano huo kuwa kuwachagua viongozi kama hao kuongoza nchi ni kuiweka rehani nchi, kwa sababu hawana nia ya kuongoza kwa kujenga nchi, bali nia yao ni kuvuruga nchi.

Aliwaomba Wazanzibari kuwachagua wagombea wa CCM wa urais wa Zanzibar, Jamhuri ya Muungano, ubunge, uwakilishi na udiwani ili kuwa na hakika ya kudumisha amani na utulivu, na hivyo kuendelea kuwaongoza wananchi katika kujiletea maendeleo yao na nchi yao.

Alisema CCM imeshadhihirisha uwezo wake wa kuleta maendeleo kwa wananchi, kwani imefanya kazi kubwa katika miaka mitano iliyopita ya kuimarisha miundo mbinu kwa kujenga barabara kadhaa kwa kiwango cha lami Unguja na Pemba, kufufua ujenzi wa nyumba za maendeleo zilizokwama kwa miaka kadhaa, kujenga zahanati mijini na vijijini na kuimarisha sekta ya elimu.

Alisema akichaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao, atahakikisha vyuo vitatu vipya vya ufundi vinajengwa ili vijana watakaoshindwa kuendelea na elimu ya juu, wapate elimu ya ufundi itakayowafanya wajiajiri.

Alisema chuo kimoja kimeshaanza kujenga Rahaleo mjini Zanzibar, na vingine vitajengwa Mkokotoni Unguja na Vitongoji, kisiwani Pemba.

Aliwaambia Wazanzibari waendelee kuichagua CCM kwa sababu kwa kufanya hivyo ni kuwa na uhakika wa maendeleo, lakini wakicheza bahati nasibu kwa kuchagua upinzani ni kuweka rehani maendeleo na amani na utulivu wa nchi yao.

 

 

 

Ngeze ataka walioshindwa kura za maoni waache kununa

Na Angela Sebastian, Karagwe

MWENYEKITI wa CCM mkoa wa Kagera Pius Ngeze amesisitiza kwamba wana-CCM ambao hawakupitishwa katika kura za maoni hawana sababu ya kununa.

Ngeze alisema katika mkutano wa kampeni jimbo la Kyerwa juzi kuwa watu hao walikuwa na haki ya kusikitika kwa sababu hawakufanikiwa, ila wanapaswa kuyachukulia matokeo hayo kama jambo la kawaida na kuungana na wenzao badala ya  kukimbilia vyama vingine.

Akihutubia mkutano huo, mgombea wa CCM katika jimbo la Kyerwa, Eustace Katagira aliwaomba wananchi kumpa kura ili aweze kusaidiana nao kutatua matatizo katika jimbo hilo ambalo alidai limekuwa yatima kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Katagila alisema kuwa wakati huu wananchi wanapaswa kuangalia kiongozi anayefaa katika kuwaletea maendeleo ya jimbo hilo na siyo yule anayeshinda akipiga kelele bila kufanya lolote.

Wakati huo huo, baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Karagwe wamekishauri Chama kubadili utaratibu unaotumika sasa wa kura za maoni katika kupata wagombea wa nafasi za ubunge na madiwani.

Ushauri huo waliutoa walipohojiwa na mwandishi wa habari hii katika viwanja vya Mabira katika jimbo la Kyerwa ambapo CCM ilikuwa ikizindua kampeni za kumnadi mgombea ubunge, Eustace Katagira.

"Kura za maoni zinatugawa na kutuharibia malengo yetu ambapo hutufanya kuwapigia wale ambao majina yao hukataliwa kurudishwa kutoka katika uchaguzi wa kura za maoni," walieleza wananchi hao.

"Chama chetu kisipoangalia upya suala hilo na kubadilisha utaratibu, tutajikuta tunapoteza majimbo mengi na hivyo kuchukuliwa na upinzani," walisema.

 

CHADEMA ndiyo iliyovamia shina la wakereketwa wa CCM’

Na John Shija, Monduli

CHAMA Cha Mapinduzi wilayani Monduli imekishutumu CHADEMA kwa kuvamia shina la wakereketwa katika kijiji cha Makuyuni na kuleta vurugu

Katibu wa CCM wilayani Monduli, Allan Kingazi alikanusha madai ya viongozi wa CHADEMA kuwa wana-CCM ndiyo waliovamia mkutano wa chama hicho na kuharibu gari na baadaye kumjeruhi mtu mmoja.

Alisema kuwa kauli hizo za viongozi wa CHADEMA ni propaganda iliyolenga kutafuta kura za huruma kutoka kwa wananchi baada ya kubaini kuwa hawataambulia chochote wilayani humo.

Kingazi alieleza kuwa msafara huo wa mgombea wa urais kupitia CHADEMA ndiyo uliofanya fujo kwa kuvamia tawi la wakereketwa wa CCM Makuyuni na kuanza kung'oa bendera kabla ya kuanza kufanya mkutano wake katika shina hilo, hali ambayo ilisababisha wana-CCM waliokuwa hapo kuhamaki na kuwafukuza.

Hata hivyo, Katibu huyo wa CCM alieleza kuwa hakukuwa na gari iliyoguswa na wakereketwa hao wala mtu aliyejeruhiwa, kwani polisi waliokuwa katika kizuizi cha barabara walifika katika eneo la tukio na kuzima vurugu za msafara wa CHADEMA.

Kingazi alisema baada ya fujo hizo zilizosababishwa na CHADEMA kutulia, ndipo msafara huo wa chama hicho ulipoondoka na kuelekea Mto wa Mbu ambapo ulikutana na wenzao baadaye kurejea Makuyuni ambapo waliendesha mkutano wao katika uwanja unaohusika na mikutano bila ya kuingiliwa

“Hawa watu wamezoea kuzua uongo na nchi kamwe haiwezi kuongozwa na uongo wa kitoto namna hii, kila mtu Makuyuni anafahamu nini kilichotokea, wanataka kuleta hadithi ya mtu anayempiga mwenzake ngumi halafu anawahi polisi kwenda kufungua mashtaka,” alisema Kingazi.

Akifafanua, alisema hakuna gari lolote lililovunjwa vioo wala mtu yeyote aliyejeruhiwa kama wanavyodai viongozi wa CHADEMA, kwani hata suala lililoripotiwa Kituo cha Polisi halionyeshi kuharibiwa kwa mali wala kujeruhiwa kwa mtu.

Kingazi aliwataka CHADEMA kueleza wazi mtu huyo aliyelazwa yupo katika hospitali gani badala ya kuudanganya umma wa Watanzania baada ya kubaini kuwa hivi sasa wamebanwa wilayani Karatu na kukuta hali hiyo walipoingia Monduli.

Baadhi ya magazeti ya jana yaliandika kwamba wanaCCM waliovaa sare za kijani walivamia mkutano wa CHADEMA na kuharibu gari la matangazo lenye namba za usajili T 167 AJE kuharibu mlango wa gari hilo na kipaza sauti na kuchana bendera za chama hicho.

Pia, ilidaiwa katika vurugu hizo MC wa CHADEMA aliyekuwa katika gari hilo aliyetajwa kwa jina la Elisifa Ama alivunjwa mkono.