UHURU
11.09.2005
Mwana-CCM apigwa na wafuasi wa CUF
Ni mkazi wa Kilosa
Na Mwandishi
Wetu
MKAZI wa kijiji cha Magole, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Ahmed Muya (50)
amewalalamikia wafuasi wa chama cha CUF kwa kumpiga na kumjeruhi
kwa tuhuma za kuwa mwanachama wa CCM.
Muya alitoa malalamiko hayo jana alipofika ofisi za gazeti hili, mtaa wa Lumumba,
mjini Dar es Salaam, akitokea
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikopata matibabu ya kurekebishwa uso wake
baada ya kupigwa na wafuasi wa chama hicho, nao wakazi wa kijijini hapo,
Septemba 4, mwaka huu.
Pamoja na kulalamika, aliiomba serikali kupitia polisi, kuwashughulikia kwa
karibu wanachama wa CUF wanaotaka kuharibu amani nchini kwa kuanzisha vita
“vya visu na nondo’.
Alisema siku ya tukio, saa 2 asubuhi alikuwa akihangaikia maandalizi ya harusi
ya mtoto wake, Zuhura Ahmed na kwamba alipita eneo ambalo wanachama wa CUF
walikuwa wanafanya matayarisho ya mkutano wao.
''Wafuasi wa CUF waliikamata baiskeli yangu kwa nyuma na kudai kwamba mimi
nilisababisha wakose umeme kutoka kwa mtu waliyekuwa wakimwomba ili wautumie
kwenye mkutano wao,'' alisema.
Muya alisema kabla hajajibu hoja alipigwa usoni kwa nondo iliyosababisha aanguke
na baadaye kusaidiwa na wananchi wema kupelekwa kwenye vyombo vya dola.
Alisema wana-CUF hao walijigamba kwa kutamka maneno ya ''wanaume, yeee, mapanga,
shashasha'' na kwamba hata hivyo
wanakijiji walijitokeza na kumpeleka Polisi kituo cha Dumila alikopata PF3 ili
kutibiwa kwenye zahanati ya Dumila.
Zahanati ya Dumila walishauri aende hospitali kubwa kwa vile alikuwa amevunjika
mataya na kwamba ndipo alipoamua kufika Dar es Salaam ambako ndugu yake anafanya
kazi hospitali ya Temeke.
Hata hivyo, alisema, madaktari wa Temeke walishauri apelekwe moja kwa moja
Muhimbili ambako alichunguzwa na hatimaye kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha taya
kwa saa 3.50 mfululizo.
Alisema taarifa alizopata kutoka Dumila ni kwamba watuhumiwa walikamatwa na
kufikisha mahakamani, na kwamba wameachiwa kwa dhamana.
''Pamoja na kunipiga, pia waliiba simu yangu, '' alisema.
Salma Kikwete ahimiza kura kwa CCM
Prosper Kulita na Latifa Ganzel, Morogoro
MKE wa wa mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Mama
Salma Kikwete amesema sera nzuri zinazotekelezeka kwa urahisi ni sababu kubwa
inayowafanya wanachama wa vyama vya upinzani kujirudi na kujiunga na CCM.
Salma aliyatamka hayo mjini hapa
juzi wakati wa ziara yake ya siku
ya moja ambayo iliandaliwa na UWT makao makuu
kuwahamasisha wanawake kukipigia debe Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi
mkuu wa rais, wabunge na madiwani,
mwezi ujao.
Akizungumzia uchaguzi mkuu, Salma amewataka
wanawake wa Morogoro kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuipatia CCM
ushindi mkubwa na kuendelea kuongoza nchi.
Mke wa mgombea urais alikumbusha kwamba wanawake
ndiyo nguzo namba moja katika mapambano ya CCM na ndiyo maana hata viongozi
wakuu wa Chama wameandaa ziara hiyo.
Akizungumzia mikopo ya wanawake,
alieleza matumaini yake kwamba serikali
ya CCM awamu ya nne itaandaa utaratibu
mzuri zaidi ambao utawawezesha wanawake kukopa na riba kupunguzwa ili
iwasaidie katika kupunguza umaskini.
Mwenyekiti wa UWT, mkoa wa Morogoro, Hawa Mbaruk, awali alimtaka Salma kutambua
kuwa uwingi wa wanawake waliojitokeza kukutana naye kwenye mkutano huo
ni dalili ya kuwepo kwa ushindi
mkubwa wa CCM katika uchaguzi mkuu.
Alisema kuwa mapokezi makubwa kama hayo yanadhihirisha kuwa CCM ina wapenzi,
mashabiki na wakereketwa ambao wako nyuma katika kila tukio ambalo linafanyika.
Mama Salma alikuwa amefuatana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya
Taifa ya CCM, Zakia Meghji, na wagombea ubunge viti maalum, wakiwemo
Shamim Khan, Lucy Mayenga, Lucy Nkya na Margareth Mkanga.
CCM Tabora ‘yawapigia debe’ wagombea ubunge
Na El-hadji Yuusuf, Kaliua
CHAMA Cha Mapinduzi kimesema kuwa kinatarajia kupata ushindi mkubwa katika
uchaguzi mkuu ujao kutokana na CCCM kukubalika kwa Watanzania wengi.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Tabora, Juma Nkumba,
aliyasema hayo juzi mjini Kaliua,
alipokuwa akizindua kampeni za uchaguzi mkuu katika jimbo la Urambo Magharibi.
Alisema kuwa CCM imekuwa ikitekeleza ahadi zake kwa wananchi, kila inapoahidi
kufanya jambo na kuwa uamuzi huo umewezesha kuondoa matatizo mengi yaliyokuwa
yakiwakabili wananchi katika jimbo hilo.
Nkumba alisema kutokana na msimamo huo wa CCM, wananchi katika jimbo hilo
wanatakiwa waendelee kuiamini na kuwachagua wagombea wake katika ngazi zote ili
waweze kutekeleza sera nzuri za CCM ambazo lengo lake ni kuleta maendeleo.
Aliwataka wananchi wamchague Profesa Juma Kapuya kuwa mbunge wa jimbo hilo,
kutokana na uwezo mkubwa wa kuhimili kazi anazopewa na
Rais, ambazo zimekuwa fahari ya Tanzania na wakazi wa jimbo hilo.
Mwenyekiti alionya kwamba kuchagua kiongozi wa majaribio ni hatari, kwa sababu
wakazi wa jimbo hilo wanaweza kujikuta wakiwachagua watu ambao hawana sifa na
hivyo kurejesha nyuma maendeleo yaliyokwisha patikana.
“Wapinzani bado ni wachanga na wanahitaji kulelewa kwanza, hivyo kuwakabidhi
madaraka ni sawa na kukubali mtoto wa miaka 13 aongoze nyumba yenye baba na
mama,” alisema Mwenyekiti.
Nkumba alikumbusha kwamba serikali
ya CCM inatarajia kujenga barabara ya lami itakayopita katika
jimbo hilo, kupeleka huduma za maji safi katika mji wa Kaliua na kupeleka
simu za mkononi kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano kwa wakazi wa jimbo hilo.
Mwenyekiti pia aliwataka wakazi wa jimbo la Urambo Mashariki wamchague Samwel Sitta, kuwa mbunge wa jimbo hilo, kwa kuwa
ni kiongozi mwenye uwezo, mbunifu na mwaminifu ambaye anaweza kuwatumikia
wakazi wa jimbo hilo kwa uaminifu mkubwa.
Alisema kuwa rekodi ya utendaji wa Sitta ni nzuri, hivyo kumpoteza ni sawa na
kupoteza lulu ambayo Mwenyezi Mungu amewatunukia watu wa wilaya hiyo.
Masasi wasema sera za CUF ni kivuli cha za CCM
Na Godfrey Mhando, Masasi
BAADHI ya wananchi mjini Masasi, mkoani Mtwara,
wamesema kwamba mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,
hana sera mpya .
Wamesema pamoja na Profesa Lipumba kupinga sera za CCM, lakini
imebainika kwamba sera anazozitangaza
kwamba atazitekeleza chama chake kikiingia madarakani ni marudio ya sera
ambazo CCM hivi sasa inazitekeleza.
Mpaka sasa hakuna chama cho chote cha siasa
ambacho kimetoa mgombea urais mwenye uwezo, nguvu ya umma na
sera bora zenye kuzingatia maslahi ya umma
kama Jakaya Kikwete, wamesema.
Mwana-CCM aliyejitambulisha kwa jina moja la Ndumbaro,
alisema Lipumba pamoja na uprofesa wake, hakuna kipya katika sera
anazozinadi kwa kuwa ni kurejea sera ambazo CCM hivi sasa inazitekeleza.
Ndumbaro alisema sera za elimu ya msingi na afya bora kwa jamii ndizo ambazo CCM
inazitekeleza sasa hivi, na hakuna kitu kipya ambacho CUF itawaletea Watanzania.
Mwananchi mwingine
aliyetambulika kwa jina moja la Clitus alisema kwamba hadi sasa sera za
CUF zina mwelekeo wa kutaka madaraka kwa nguvu kutokana na chama
hicho kutamka kwamba hakitayapokea matokeo ya kushindwa katika uchaguzi mkuu
ujao.
Alisema hali hiyo inaonyesha kwamba
chama hicho, ambacho Lipumba anakiongoza hakiafiki muafaka, na kuna hatari
kwamba kikipata madaraka kitaingiza nchi katika machafuko.
Akiwa mjini Mtwara juzi watu
waliojitokeza katika mkutano kwenye uwanja wa Mashujaa
walionyesha kutoshangazwa na hoja alizotoa katika mkutano wake wa kampeni
na wengine wakisema 'hana jipya'.
Jana mchana Lipumba aliondoka mjini Mtwara
kwenda Lindi ambapo
alisimama katika vijiji vya Mnolela na Mnazi Mmoja katika tarafa ya Mingoyo.
Jioni alitarajiwa kuhutubia mkutano
katika viwanja vya Ilulu.
Leo anatarajiwa kuendelea na kampeni zake katika maeneo mbali mbali ya Lindi
Vijijini na wilaya ya Kilwa kabla ya kesho kuendelea na ziara yake katika wilaya
ya Rufiji na Mkuranga, mkoani Pwani.
UVCCM yateua makatibu
Na Mwandishi
Wetu
UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM), umefanya uteuzi wa makatibu wapya wa mikoa na
wilaya nchini, taarifa kwa vyombo vya habari iliyopatikana jana imeeleza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotiwa saini na Katibu Uhamasishaji na Chipukizi
ya UVCCM, Dk. Diodorus Kamala, Kamati ya Utekelezaji imewateua Abdubakari Ghati
kuwa katibu wa mkoa wa Mwanza na Saad Kusilawe, Mbeya.
“Pamoja na uteuzi huo, kamati ya Utekelezaji pia imempangia kituo cha kazi
Barnabas Essau mkoa wa Singida,” ilisema taarifa .
Kwa upande wa wilaya, walioteuliwa na wilaya zao katika mabano ni Judith Mlela (Tabora
Mjini), Said Yasin Said (Kisarawe) na Philbert Ngemela (Muleba).
Umoja huo Alhamisi na Ijumaa
iliyopita, ulikuwa na semina maalum
kwa watendaji wake, chini ya Mwenyekiti wa Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi, juu ya
mikakati ya kuipatia CCM ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
Kamala aliwataja washiriki wa semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam,
kuwa ni wenyeviti na makatibu wa UVCCM wa mikoa na wilaya zote za Tanzania na
wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Umoja huo.
Majambazi yaua Katibu wa UVCCM
Na Esther Katua
KATIBU wa UVCCM wilaya ya Mkoa
Kusini Pemba, Rajab Kheri Rajab, amefariki baada ya kujeruhiwa kwa risasi
ubavuni na majambazi waliovamia nyumba ya wageni
ya Bondeni, iliyopo Magomeni Morocco, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia juzi.
Taarifa kutoka Umoja huo zilisema tukio hilo lilitokea saa saba na nusu usiku
wakati Rajab na wenzake wakiwa katika nyumba hiyo wakiangalia televisheni.
Kwa mujibu wa taarifa, majambazi yalivamia
na kuanza kurusha risasi zilizompata Rajab ubavuni wakati mjumbe wa
kamati ya Utekelezaji ya vijana
Taifa, Mohamed Abrahamani Mwinyi, alijeruhiwa
mkono wa kulia.
Alisema walikimbizwa hospitali ya Muhimbili, lakini Rajabu alifariki juzi
mchana wakati Mwinyi alitibiwa na kuruhusiwa.
Maiti ya Rajab, ambaye alikuwa mjini Dar es Salaam kwa semina ya UVCCM,
ilisafirishwa juzi kupelekwa
Zanzibar.