UHURU 12.09.2005

 

Mrema apoteza mvuto Arusha hadi kuomba apigiwe makofi

Na Omari Shaaban, Arusha

MGOMBEA urais wa kwa tiketi ya Chama cha TLP, Augustine Mrema, jana aliwachekesha wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwa kila mara kuwaomba wampigie makofi wakati alipokuwa akiwahutubia.

Mrema ambaye yuko mjini hapa kwa mikutano ya kampeni ya chama chake alikuwa akiwaomba wananchi wafanye hivyo kutokana na kuhutubia muda mrefu bila kupigiwa makofi, hali iliyoonyesha hakuwa na mvuto wala jipya kwao.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja maarufu vya NMC mjini hapa, Mrema pia alitumia muda mwingi kuwakandia wagombea wenzake wa upinzani, hususan Freeman Mbowe wa CHADEMA na Profesa Ibrahimu Lipumba wa CUF.

Alisema miongoni mwa wagombea wote wa upinzani ni yeye pekee ndiye anayestahili kuchaguliwa kuongoza nchi kwa kuwa Mbowe na Lipumba hawana uzoefu kama alionao yeye.

“Lipumba alishindwa kufanya kazi wakati akiwa na nafasi ya kufanya hivyo. Mbowe hana uzoefu wowote wa kuongoza zaidi ya biashara ndogo ya hoteli,” alisema Mrema.

“Hawana cha kuwaambia wala kuwaletea maendeleo zaidi ya mimi tu," alisema Mrema kwenye mkutano huo na kuongeza kuwa mbali ya yeye wengine ni vibaraka na wabinafsi na hawafai kuwa viongozi wa nchi.

 Mrema ambaye aligeuza jukwaa hilo kuwa sehemu ya malumbano badala ya kunadi sera aliwashambulia kwa maneno viongozi wa dini kwa kuwaita kuwa ni 'wanafiki', jambo lililofanya baadhi ya waliokuwa wakimsikiliza kukerwa na kuanza kuondoka.

Kutokana na Mrema kuwa akirudiarudia mambo na kuelezea mengine yaliyoonekana kuwakera wananchi, wachache waliobaki waliendelea kumsikiliza, ingawa walionekana kukerwa na kauli zake.

Hali hiyo ilimfanya Mrema baada ya kuhutubia kwa muda mrefu kuwaomba wananchi hao walau wampigie makofi. “Nipigieni makofi basi,” aliomba Mrema.

 

 

 

 

 

Karume aviagiza vyombo vya dola kudhibiti vurugu 

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar Amani Abeid Karume, amewaagiza wakuu wa mikoa na vyombo vyote vya usalama Zanzibar, kuchukua hatua za haraka kuhakikisha vurugu zinazojitokeza kwenye misafara ya kampeni inadhibitiwa.

Alitoa agizo hilo jana katika mkutano wa kampeni za urais wa Zanzibar uliyofanyika kijiji Cha Bumbwini Makoba, wilaya ya Kaskazini B mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema wakuu wa mikoa yote ya Unguja na Pemba, makamanda wa polisi wa mikoa na wakuu wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama lazima wakutane na kupanga mikakati ya kuwasaka wote wanaohusika na kushambuliwa kwa misafara ya kampeni ya CCM.

Rais Karume ambaye ni mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM alitoa agizo hilo baada ya Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Foum Mati Foum, kueleza kuwa wanachama wa CCM wa mkoa wake waliyokuwa wakitoka kwenye mkutano wa kampeni juzi, uliyofanyika Uzini, walishambuliwa na mwanachama mmoja kuchomwa kisu.

Hilo ni tukio la pili la misafara ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi kushambuliwa na watu wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa CUF. Siku tatu zilizopita msafara wa CCM ulishambuliwa kwa mawe ulipokuwa ukitoka kwenye kampeni katika kijiji cha makunduchi, mkoa wa Kusini Unguja, na kusababisha kijana mmoja kujeruhiwa mdomo na gari husika kuvunjwa kioo.

“Sitaki kuja kuelezwa sijui imekuwaje, kuna nini… lugha hiyo sitaki kabisa kuisikia, ni lazima tuwasake wote wanaohusika na vitendo hivyo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria,” alisema Karume huku akishangiliwa na maelfu ya wana CCM na wananchi waliyofurika kwenye mkutano huo.

Rais Karume alisema suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao, na usalama wa nchi hauna mjadala na kwa hilo ‘hakuna muhali’. “Muhusika awe mdogo kabisa katika makundi hayo, au mkubwa kabisa lazima washughulikiwe, na kufikishwa katika vyombo vya sheria”.

Alisema wapinzani ni walalamishi, wanawachokoza wana CCM ili wachokozeke wajibu vitendo vyao hivyo wapate njia za kulalamika kuwa wanaonewa. Aliwataka wana CCM wasikubali kuchokozeka na waendelee kudumisha amani na utulivu, kwani hiyo ndiyo sifa ya Chama cha Mapinduzi. 

Aliwataka wana CCM na wananchi wote kuendelea kuichagua CCM, kwani ndicho chama kinachojali amani na utulivu na kuwaongoza wananchi kujiletea maendeleo. Alitahadharisha kuwa kuchagua upinzani ni kukwamisha maendeleo, kwani maendeleo hayawezi kupatikana katika mazingira ya fujo na vurugu.

 

 

 

Lipumba atakiwa asipoteze muda kwa kuishambulia CCM

Na Godfrey Mhando, Lindi

BAADHI ya wakazi wa mkoa wa Lindi wamemtaka mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuacha na kampeni za kukishambulia Chama Cha Mapinduzi, badala yake atumie muda mwingi kuelezea sera za Chama chake.

Walisema hayo mbele ya waandishi wa habari walipohojiwa wakati wa Mkutano wa kampeni wa Profesa Lipumba ili kujua ni mambo gani waliyoyasikia kwa mgombea huyo alipohutubia kwenye uwanja wa Ilulu mjini hapa jana.

Miongoni mwa wakazi waliohojiwa ni pamoja na Said Mohammed Bakari ambaye pia alisema Profesa Lipumba alipoteza muda mwingi kuelezea mambo ya CCM na mgombea wake, lakini hakueleza yeye atawafanyia nini wananchi akipata Urais.

Bakari ambaye alisema ni mwanachama wa CHADEMA alisema Profesa Lipumba hakuweza kuelezea sera za chama chake, tofauti na mgombea wa CCM ambaye alieleza wazi kwamba CCM ikipata uongozi itahakikisha inakamilisha ujenzi wa barabara ya lami na kuongeza kasi ya masuala ya utalii mkoani Lindi.

Naye Hamadi Makupa aliyejitambulisha kuwa ni mwanachama wa CCM alisema Lipumba alitumia muda mwingi kutukana CCM badala ya kueleza mipango ya maendeleo itakayotekelezwa na chama chake.

Makupa alisema mgombea huyo alipwaya katika masuala ya mvuto kwa watu na kwamba wakati wote alizungumza mambo ambayo utekelezaji wake ni mgumu.

Awali, akihutubia wakazi waliohudhuria mkutano wake kwenye uwanja wa Ilulu Profesa Lipumba, alisema atawashangaa sana watu wa Lindi ikiwa watamnyima kura za urais wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.

Profesa Lipumba alisema yeye ndiye msomi mzuri wa masuala ya uchumi na kwamba hivi sasa ni mashauri wa uchumi katika nchi kadhaa za nje.

Alisema anao uwezo wa kutatua matatizo ya uchumi wa Watanzania na kwamba  Watanzania watakuwa watu wa ajabu ikiwa hawatamchagua.

Hata hivyo, Profesa Lipumba ambaye aliwahi kuwa mshauri wa masuala ya uchumi wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi kutokana nao ushauri wake alisababisha mfumuko wa bei ufikie zaidi ya asilimia 30.

 

 

 

 

 

Dk. Sheni: Huduma ya maji salama kufikia asilimia 65 vijijini, 90 mijini

Ramadhani Mkoma, Nachingwea

SERIKALI imetoa sh.milioni 200 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa maji wa Mbwinji, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake katika kuhakikisha wananchi wa wilayani hapa wanapata maji safi na salama.

Hayo yalielezwa juzi na Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ali Mohammed Sheni, wakati akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Sokoine mjini Nachingwea.

Dk. Sheni ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma za maji

vijijini na mijini.

Alisema wilaya zingine zitakazofaidika na mradi huo ni Newala, Masasi na vijiji vya jirani. Alisema kijiji cha Mbwinji kina hifadhi kubwa ya maji na kwamba iwapo mradi huo utakamilika utapunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la maji safi na salama.

Kwa mujibu wa Dk.Sheni lengo la Serikali ni

kuhakikisha huduma za maji vijijini zinaimarika na kufikia asilimia 65 kutoka asilimia 53 na mijini inafikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2010.

Dk. Sheni, alisema licha ya kiasi hicho pia kuna sh. milioni 264 nyingine zitakazoongezwa kuboresha miradi ya maji wilayani hapa. 

Alisema iwapo wananchi watakipa ridhaa kwa mara nyingine Chama Cha Mapinduzi kuongoza dola, kitafanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuanzisha viwanda vya usindikaji kwa ajili ya kuinua soko la mazao ya Tanzania, ikiwemo korosho.

Mbali na usindikaji ambao alisema utakwenda sambamba na kukaribisha wawekezaji katika sekta hiyo, kilimo cha umwagiliaji katika mashamba madogo madogo kitapewa kipaumbele.

Aliongeza kuwa Serikali itarejesha mashindano ya wakulima ili kutoa changamoto kwao kuongeza uzalishaji.

Dk.Sheni aliwataka wananchi kuichagua CCM ili iweze kuendeleza mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tatu chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wakulima wilayani humu kwa kuongeza  uzalishaji wa zao la ufuta kutoka tani 814 mwaka jana hadi 913 mwaka huu.

Mapema, akizungumza katika mkutano huo, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 30 ambaye pia ni Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Kuondoa Umasikini) Edgar Maokola  Majogo, aliwataka wana -Nachingwea kuwachagua wagombea wa CCM katika nafasi zote akiwemo Mathias Chikawe, anayegombea ubunge wa jimbo hilo, ili kuongeza kasi ya maendeleo ya jimbo hilo.

 

 

 

 

 

Mapuri ataka wanachama  CCM  kuwa wavumilivu

Na Thomas Mtinge

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wanachama wake kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa kifo cha kinyama cha Katibu wake wa Itikadi na Uenezi wa Tawi la Midizini, Manzese, Mwajuma Nyanza na baadhi ya watu wa amilia yake.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Omari Ramadhan Mapuri alitoa wito huo wakati akitoa salamu za rambirambi za Chama nyumbani kwa marehemu kabla ya mazishi Manzese, Dar es Salaam juzi.

Mapuri alisema msiba huo ni mkubwa na ni wa kitaifa na kuwaita marehemu hao kuwa mashujaa wa kupigania ushindi wa CCM.

Alisema wana-CCM lazima wawe watulivu na kudumisha amani na kuiachia Serikali iendelee kufanya uchunguzi ili kubaini watu waliofanya uhalifu huo ambao aliuita kuwa ni wa kishenzi na kinyama.

Kwa mujibu wa Mapuri, pamoja na kwamba hadi sasa haijafahamika kama tukio hilo ni la kisiasa au la, lakini ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa lina uhusiano wa kisiasa.

"Kila mtu anajua kama tukio hili linahusiana na masuala ya kisiasa...hata mimi najua hivyo, lakini tuiachie Serikali ifanye kazi yake," alisema.

Alisema marehemu Mwajuma alikuwa mpiganaji hodari wa CCM na kuhakikisha Chama kinafanikiwa kupata ushidi katika uchaguzi wote dhidi ya wapinzani.

"Unyama huu unatokana na wivu na ukweli kwamba marehemu hakuna mtu asiyemjua kama alikuwa mtu mwenye kukipenda Chama na kukipigania kwa nguvu zake zote ili kishinde," alisema Mapuri.

Hata hivyo, alisema siasa za namna hiyo ni mbaya na hazifai na kwamba hata CCM sasa imekuwa ikivulia lakini kutokana na tukio hilo uvumilivu unaanza kupungua.

Alisema anashangaa kuona viongozi hao hao hivi karibuni kutangaza kwamba wangefuata nyayo za CCM za kufanya kampeni za kistaarabu na za utulivu na amani, lakini sasa wanageuka na kuanza kufanya vitendo vya kinyama.

"Ni hao hao karibuni tumewasikia wakiahidi kufanya kampeni za kistaraabu, amani na utilivu...lakini kumbe ahadi zao hazikuwa za vitendo bali ni maneno tu.

"Kweli mapambano yapo lakini ni ya kutaka kutafuta dola na  si kutoana roho," alisema Mapuri.

Mapuri alisema CCM itaendelea na msimamo wake wa kufanya kampeni za amani na utulivu ili kuwapa wananchi fursa ya kuhudhira mikutano hiyo na kusikiliza sera bila kuwepo bughudha za aina yoyote.

Alisema dawa ya wapinzani ni wananchi kuwanyima kura katika Uchaguzi Mkuu ujao ili iwe fundisho kwao kutokana na vitendo hivyo vya kinyama.

Katika msiba huo CCM ilitoa sh. laki tano kwa ajili ya rambirambi na kuahidi kuisaidia familia hiyo kwa hali na mali baada ya kumalizika kwa msiba.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kinondoni Abraham Mihewa, alisema CCM katika wilaya hiyo imeupokea msiba huo kwa mshituko mkubwa.

Aliiomba Serikali kufanya uchunguzi wake haraka ili kuwabaini watu waliohusika na tukio hilo na kuwachukulia hatua.

Viongozi wengine waliyohudhuria katika mazishi hayo ni pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Mattson Chizi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salum Londa, mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo Charles Keenja, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Aaron Mwaikambo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Athuman Mdoe.

 

 

 

 

 

CUF wavamia kwa mgombea ubunge wa CCM Bukoba

Na Angela Sebastian, Bukoba

KUNDI la watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa  CUF wamevamia nyumba ya mgombea kiti cha Ubunge kupitia CCM Khamis Kagasheki wakiwa na marungu, ngoma na mawe na kuporomosha matusi ya nguoni wakidai jimbo hilo ni ngome yao.

Tukio hilo lilitokea jana saa 12.30 jioni katika eneo la National Housing mjini Bukoba  ambapo wafuasi hao wa CUF waliokuwa wamevalia sare za chama chao walikuwa wakitokea katika mkutano wa kumnadi mgombea wao Wilfred Lwakatare katika kata ya Kashai mjini hapa.

Imedaiwa kuwa watu hao walipofika katika eneo anakoishi Kagasheki waliamua kuanza kupiga ngoma huku wakitoa matusi na kashfa kwa mgombea huyo.

"Kwa kweli hatuwezi kuvumilia vitendo kama hivi vya kuhatarisha maisha yetu na familia zetu, hawa CUF wanatafuta uchokozi sio kwamba wanafanya Kampeni," walilalamika baadhi ya wananchi waliokuwa eneo la tukio.

Wananchi hao walidai kuwa Lwakatare ametumia mgomgo wao kujipatia maisha bora ambapo mpaka sasa ana gari zuri na kuwa anawarubuni tena ili aweze kuboresha maisha yake binafsi.

Wakati huo huo, Meneja wa kampeni wa CCM jimbo Bukoba Mjini, Medard Mushobozi amedai wapo baadhi ya wana CUF wanaosema Septemba 19, mwaka huu atakapowasili mgombea Urais wa CCM Jakaya Kikwete watafanya fujo wakiwa wamevalia sare za CCM.

"Wapo watu wameandaliwa kuja kufanya fujo wakati Kikwete atakapowasili Bukoba. Watavalia sare za CCM, tuna wakaribisha maana ugonjwa siku hiyo na matibabu hapo hapo," alisema Mushobozi.

 

 

 

 

 

Mama Salma Kikwete asisitiza ajira kuongezeka

Na Prosper Kulita na Latifa Ganzel, Morogoro

MKE wa mgombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Salma Kikwete juzi alianza mkutano wake kukinadi Chama kwa staili ya aina yake baada ya kuongoza uombaji dua kwa wanawake kwa dini ya kiislamu.

Pia sala ya dini ya kikristo ilitolewa na mmoja wa akina mama iliyofunga mkutano mkoani hapa akiwataka kuvunja makundi na kukipigia debe CCM ili kishinde kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Salma ambaye yuko katika ziara ya kampeni kuwanadi wagombea wa CCM alifika kwenye ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Forest Hill mjini hapa akiwa ameongozana na Waziri wa Maliasili na Utalii Zakhia Meghji na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.

"Lengo la ziara hii ni kuonana na ninyi ili niwaeleze neema inayokuja na matumaini ya maisha bora kwa Serikali ya awamu ya nne kupitia CCM katika kupambana na umaskini kwa kuwa ninyi mnaushawishi mkubwa kwenye jamii na mkafanye kazi hiyo ili Chama chetu kishinde uchaguzi ujao," alisema Salma.

Akitaja neema hiyo itakavyopatikana alisema tatizo la ajira litatatuliwa na sekta kuu tatu ambazo ni ajira serikalini, katika sekta binafsi na ile ya kujiajiri ambayo mwananchi atawezeshwa kupata mitaji kwa mikopo ya  mashariti nafuu sana ukilinganisha na sasa ambpo mikopo hiyo imekuwa ikiwaingiza matatizoni badala  ya

kuwatatulia matatizo.

"Sikilizeni kina mama kuhusu watu kuajiriwa serikalini ongezeko hilo litahusisha sana Wizara ya Elimu na Afya ambapo vijana na kina mama wengi watapewa mafunzo maalumu ya ualimu, unesi na madakitari na watakao faulu  wataajiriwa moja kwa moja," aliongeza.

 

Alisema kundi lingine litakalo toa ajira ni sekta binafsi ambapo viwanda vingi vikiwemo vya kusindika mazao hasa  vijijini vitaongezwa ambapo vijana wataweza kuajiriwa na kulipwa ujira unaolingana na hali ya maisha.

Mama Salma aliwataka akinamama hao kuwa na umoja, mshikamano na kuvunja makundi yaliyokuwepo awali kwa kuwa sasa muda wa kulumbana umepita na kuwa kilichobaki ni kutafuta ushindi wa kimbunga wa mafiga matatu.

"Mkiwachagua Rais, mbunge na diwani wa CCM mtawezesha kwa kiwango kikubwa kuharakisha hayo yote niliyowaelezeni kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu lakini kama mtachanganya utekelezaji wake utakuwa mgumu kwa kuwa sera na mipango inatofautiana,"alisema.

 

 

 

 

Kuweni macho na ahadi hewa za wapinzani- Karume

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

WAZANZIBARI wameshauriwa kuwa macho na vyama vya upinzani vinavyoomba kuchaguliwa kwa kutumia ahadi hewa, zikiwemo za kuongeza mishahara ya wafanyakazi mara mbili ya mishahara inayotolewa sasa.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume, alisema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema ahadi ya kuongeza mishahara na wakati huo huo mgombea huyo akiahidi kupunguza kodi, hiyo ni kuonyesha kwa kiasi gani asivyojua taratibu zinazoendesha uchumi.

Alikuwa akizungumzia ahadi iliyotolewa juzi na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Seif Shariff Hamad, ambaye alisema akichaguliwa ataongeza mishahara ya kima cha chini kutoka sh. 50,000 hadi 100,000 kwa mwezi, na wakati huo huo atapunguza kodi kwa bidhaa zote zinazoingizwa nchini isiwe zaidi ya asilimia 10.

Rais Karume alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina wafanyakazi wapatao 30,000 ambapo mfanyakazi mmoja kwa mshahara wa sh. 50,000 kwa mwezi anachagiwa na watu 33.

Alisema kwa taratibu za kiuchumi ikiwa mfanyakazi mmoja anachangiwa mshahara wake na watu 33, na Zanzibar ina watu milioni moja, wafanyakazi 30,000 mishahara yao itatachangiwa na watu 970,000.

“Bwana mdogo anaposema ataongeza mishahara, hizo fedha atazitoa wapi?” aliuliza Rais Karume.

Aliwataka Wazanzibari kuwa makini na ahadi hewa za aina hiyo, alizoziita ni ‘ndoto za alinacha’ na kusema kutakuwa na njia mbili tu ambazo zitakazomuwezesha mgombea huyo wa CUF kutekeleza ahadi yake hiyo.

Ya kwanza alisema, ama ana mawazo ya kuvunja Muungano na kuanzisha Benki Kuu na baadaye kuchapisha fedha zake, hali ambayo alisema ikitokea uchumi wa Zanzibar utaanguka na fedha yake haitakuwa na thamani kiasi cha kibiriti kuweza kuuzwa kwa sh. 1,000, kama ilivyowahi kutokea nchini Uganda, wakati wa utawala wa Nduli Idi Amin.

Rais Karume alisema njia ya pili inawezekana labda ameahidiwa kupewa fedha pahala, njia ambayo aliuliza kama ni hivyo atapewa fedha hizo kwa mkataba gani. Alimtaka kiongozi huyo wa CUF, ikiwa ni hivyo aeleze makubaliano ya kupatiwa fedha hizo ili wananchi wajue.  

Aliwaambia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni kuwa kazi ya kubadilisha uchumi wa nchi kuwa bora si ‘safari’ ya siku moja au mwaka mmoja, bali ni ya muda mrefu inayohitaji mipango na taratibu za kiuchumi zinazoeleweka.

Alisema Chama cha Mapinduzi ndicho peke kinachofaa kupewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi, kwa sbabau ya sera zake zinazojali maslahi ya wananchi na kuwaletea maendeleo, kama ambavyo kimekuwa kikifanya tokea nchi ilipopata uhuru.

 

 

 

 

 

CCM Morogoro Mjini yapata sare kwa vijana

Na Prosper Kulita, Morogoro

CHAMA Cha Mapinduzi wilaya ya Morogoro Mjini kimepatiwa msaada wa mashati zaidi ya 50 yenye thamani ya sh. 250,000 na Kamanda wa Umoja wa Vijana Kata ya Sabasaba ili yaweze kuwasaidia vijana walio katika mapambano ya kuleta ushindi wa kishindo wa CCM.

Msaada huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Kamanda wa Umoja wa Vijana Kata hiyo ya Sabasaba, Joe Mzuwanda katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Kiwanja cha Ndege katika Manispaa ya Morogoro.

Akitoa msaada huo, kamanda huyo alisema kuwa lengo la kutoa mashati hayo ni kuhakikisha kuwa vijana wa CCM walio katika kampeni wanakuwa katika sare nzuri ya  kukinadi na kuzinadi sera za CCM na hatimaye ushindi wa kishindo uweze kupatikana.

Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni mwenyeikiti wa CCM wilaya ya Morogoro mjni Fikiri Juma alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa Chama katika uongozi wa nchi wananchi wasifanye kosa kuchagua viongozi wa vyama vya upinzani kwa kuwa miongoni mwao wamejaa uroho wa madaraka.

Alisema kuwa hilo liko wazi na ndiyo maana baadhi yao wameamua kujipa aina tofauti za uongozi mpaka kufikia hatua ya kugombana wenyewe kwa wenyewe.

"Wewe ona mtu huyo ni katibu wa chama halafu ni mhasibu bado anataka udiwani na ubunge sasa huyo ni mwema kwenu wananchi? Angalieni aina ya uongozi ndani ya CCM ukiwa diwani basi na vingine waachie wenzako si kila kitu wewe hao tunawaita bwana mimi," alisema Fikiri.

Juu ya demokrasia, mwenyekiti huyo alisema kuwa anaamini ni CCM pekee ndiko kuna demokrasia ya kweli ambayo inawafanya wagawane uongozi kila mara ambapo hakuna wakati kulisikika kuwa wana CCM wameanza kulumbana mpaka kufikia kupelekana mahakamani kwa ajili ya uongozi.

Katika mkutano huo Chama Cha Mapinduzi Morogoro Mjini kilikuwa kikiwanadi wagombea wa nafasi za udiwani na ile ya ubunge ambaye ni Dk. Omari Mzeru.

 

 

Dk. Sheni awataka wananchi waachane na ahadi za wapinzani

Na Abihudi Saideya, Nachingwea,

MGOMBEA Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya CCM Dk. Ali Mohamed Sheni amesema ahadi za vyama vya upinzani kuwa vitatoa bure huduma za jamii ni za uongo na hazitekelezeki.

Akihutubia mikutano ya mikubwa ya kampeni jana katika Wilaya za Ruangwa na Nachingwea mkoani Lindi Dk. Sheni alisema katika dunia ya leo hakuna Serikali yenye uwezo wa kutoa kila kitu bure.

Lakini akasema anashangazwa na ahadi zinazotolewa na vyama vya upinzani kuwa vitakuwa vinatoa bure huduma za afya, maji na elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.

Bila kutaja vyama hivyo, Dk. Sheni ambaye alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa Sheikh Ally Mohamed Mtopa, na viongozi wengine wa CCM aliwataka wananchi wasiyumbishwe na hadaa za aina hiyo.

Huku akishagiliwa na wakereketwa wa CCM pamoja na wananchi waliokuwa wamefurika katika mikutano hiyo, Dk. Sheni alisema CCM ndicho Chama kinachotoa ahadi za uhakika na hakina mashaka juu ya kukubalika kwake.

Aliwaomba wananchi wamchague mgombea Urais Jakaya Kikwete, wabunge na madiwani wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu kwa kuwa mafanikio ya utekelezaji wa Ilani zake katika Uchaguzi zilizopita unaonekana wazi.

Baadhi ya mambo aliyoyataja ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa shule za msingi toka milioni 3.5 mwaka 1995 hadi milioni 7.5 mwaka 2005, wanafunzi wa sekondari 190,000 hadi 520,000, wanafunzi vyuo vikuu

7,785 hadi 32,681 katika kipindi hicho.

Pia alisema serikali imepanua mtandao wa barabara za lami ikiwa ni pamoja na kujenga daraja la Mkapa kwenye Mto Rufiji, ambalo limeunganisha mikoa ya Kusini na sehemu nyingine za Tanzania.

Dk. Sheni alisema mafanikio zaidi yamepatikana katika sekta za mawasiliano ya simu ambayo yameenezwa katika mikoa ya kusini na sehemu nyingine za Tanzania.

Akinukuu vipengele kadhaa vya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010, Dk. Sheni aliwaambia wananchi waliohudhuria mikutano hiyo kuwa CCM itaboresha hali ya uchumi na kutoa kipaumbele katika kukabiliana na matatizo ya wanawake, vijana, wazee na walemavu.

Katika mikutano hiyo iliyopambwa kwa mavazi ya njano na kijani wanachama 580 wa vyama vya upinzani walirejesha kadi za vyama hivyo, na kujiunga Chama Cha Mapinduzi. Wanachama hao walitoka vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CHAUSTA, TLP na UDP.

Pia, wanachama wapya 152, waliokuwa hawajaingia katika vyama vya siasa, wajiunga na CCM katika wilaya ya Nachingwea.

Baadaye jioni wakiwa katika mazungumzo, Wazee wa Nachingwea  walimwambia Dk. Sheni kuwa wananchi wa Wilaya hiyo wamekuwa karibu na CCM tokea enzi za kupigania uhuru wa Tanganyika na nchi nyingine kusini mwa Afrika, hivyo wataipatia CCM ushindi wa kishindo.

Walisema wimbi kubwa la wanachama wanaojitoa katika vyama vya upinzani ni mwanzo wa jitihada zinazofanywa na wazee kusambaratisha upinzani katika wilaya hiyo.

Kesho kutwa, Septemba 12, Dk.Sheni anatarajiwa kuendelea na ziara ya kampeni za uchaguzi mkoani Mtwara baada ya kukamilisha ratiba yake mkoani Lindi.

 

 

 

Karume amtaka Maalim Seif alaani vurugu

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

RAIS Amani Abeid Karume, amemtaka mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, kulaani vitendo vya ugomvi na vurugu vinavyotokea katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu.

Alisema asipolaani vitendo hivyo na kuwakataza wafuasi wake kuacha vurugu na uchokozi, yeye na viongozi wenzake watabeba jukumu la vitendo hivyo na ndiyo watakaowajibika.

Rais Karume ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, alitoa onyo hilo jana kufuatia tukio la juzi la kushambuliwa kwa mawe gari ya abiria iliyokuwa imewapakia wanachama wa Chama cha Mapinduzi, waliyokuwa wakitoka kwenye mkutano wa kampeni wa CCM katika kijiji cha Makunduchi.

Kaika tukio hilo lililotokea jioni, kijana mmoja alijeruhiwa vibaya mdomoni kwa kupigwa jiwe na kioo cha gari hiyo kuvunjwa. Inaaminika kuwa waliyofanya shambulio hilo ni wafuasi wa CUF.

Karume ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni huko Uzini, wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja, alisema CCM na CUF vimefikia makubaliano ya kuendesha kampeni za kistaarabu, kulinda na kudumisha amani na utulivu, kutokashifiana na kuwazuia mashabiki wake na vitendo vitakavyosababisha chuki, ugomvi na uhasama.

Alisema inaonekana wanakiuka 'mkataba' huo na 'tunamsubiri (Seif Shariff Hamad) na viongozi wenzake walaani vitendo hivyo na kuwakataza wafuasi wao waache vurugu. Wasipofanya hivyo watawajibika,' alisema.

"Tumesema tunataka amani, lakini kwa vitendo hivi tumechoka. Lazima tujuane sasa huko tunakokwenda," alisema Rais Karume ambaye alionyesha kukerwa na kitendo hicho cha uchokozi wa wazi wazi.

Aliema CCM ni chama cha wastaarabu na wavumilivu, ndiyo kimewaita CUF na kuzungumza nao juu ya umuhimu wa kutafuta na kulinda amani ya nchi yetu na kuongeza 'lakini kumbe wenzetu walikuwa wakifuata posho tu. Kama hawakufuata posho tu, kwa nini wanakiuka mkataba wetu?'

Aliwataka Wazanzibari kutowapigia kura wapinzani kwa sababu ni vyama visivyojali amani na utulivu, hali ambayo itaiingiza nchi katika vurugu vikishika hatamu za dola.

Aliwataka waichague CCM ambayo ndiyo muhimili mkubwa wa amani, utulivu na maelewano nchini.

 

 

 

 

Rais Mkapa ampongeza Rais Mubarak kwa ushindi wa kishindo

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa amemtumia salaamu za kumpongeza Rais wa Misri Hosni Mubarak kwa ushindi mkubwa aliopupata katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika hivi karibuni.

Taarifa iliyotyolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilisema Rais Mkapa alimpongeza Rais Mubarak kwa kupata ushindi unaomuhakikishi kuendelea kuiongoza nchi ya Misri na watu wake.

Rais Mkapa alimuhakikishia Rais Mubarak kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Misri kwa maslahi ya nchi zote mbili.

Matokeo ya uchaguzi nchini Misri yalitangazwa juzi ambapo Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Rais Mubarak kwamba ni mshindi baada ya kupata asilimia 88.6 ya kura zote zilizopigwa.

 

 

 

 

Mzalendo yapongezwa kufichua kampeni za matusi Msikiti wa Mtoro

Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya waumini wanaoswali Msikiti wa Mtoro jijini Dar es salaam wamelipongeza gazeti la Mzalendo kwa kufichua  kampeni za matusi zinazofanywa kwa kuandikwa kwenye kuta za  vyoo vya msikiti huo.

Gazeti la Mzalendo toleo la  Septemba 11, mwaka huu  liliandika  habari iliyosema ’Ukuta wa Msikiti wa Mtoro wageuzwa ubao wa siasa’ kwa kuandika maneno yanayokashifu CCM na Rais Benjamin Mkapa huku yakisifu CUF  na viongozi wake.

Mwandishi wa gazeti hilo alishuhudia ukuta wa choo kimoja cha Msikti huo ukiwa umeandikwa maneno mengi ya kuisifu CUF na kuwakashifu viongozi wa Serikali hususani Rais Mkapa.

Muumini aliyedai ni mmoja wa wanaoswali  msikitini hapo alisema  kwa  njia ya simu jana kwamba maandishi ya kashfa dhidi ya CCM na Serikali yake  kwenye kuta za choo cha msikiti huo zinawakera wengi.

‘’Kwa kweli tunapongeza kufichua mambo haya,  kwani inaelekea hata vyombo vya dola vinaachia achia kashfa ambazo zitahatarisha amani ya nchi,’’ alisema muumini huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdallah alisema matusi kwenye vyoo hivyo yaliandikwa mwishoni mwa mwezi uliopita na kwamba kwa bahati mbaya wapo viongozi wa msikiti ambao wanapenda kuzungumzia masuala ya CUF na CCM msikitini jambo ambalo linawakwanza wengine.

‘’Sisi tunakwenda msikitini kuswali, lakini wapo vingozi wanaoanza kuzungumzia masuala ya CUF  ni safi na kukashifu waziwazi viongozi wa CCM jambo linalowaondoa wengi,’’ alisema.

Muumini huyo alisema maandishi kama hayo pia yapo kwenye misikiti kadhaa  ya jijini ukiwemo msikiti mmoja maarufu uliopo eneo la  Ilala.