UHURU 12.10.2005

 

 

 

Mabalozi si majaji, Karume awapasha wapinzani

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MABALOZI wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini si majaji wala mahakimu wa malalamiko yanayowasilishwa kwao na viongozi wa vyama vya upinzani.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ambaye alisema viongozi wa upinzani Zanzibar wanawaweka mabalozi katika hali ngumu kuwafanya wawe majaji wanapokwenda kuwalalamikia.

Rais Karume aliyasema hayo alipowahutubia wananchi na wapiganaji katika sherehe ya uwekaji wa jiwe la msingi la hospitali mpya ya kijeshi inayojengwa Bububu, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

“Wapinzani wamekuwa na utamaduni wa kuanzisha vurugu na baadaye kukimbilia kwa mabalozi kwenda kulalamika.Tabia hii inawaweka mabalozi katika hali ngumu kwani hii si kazi yao kuwa majaji na mahakimu,” alisisitiza Rais Karume.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya juhudi kubwa kujenga taasisi za kuimarisha utawala bora, ukiwemo uimarishaji wa uhuru wa mahakama ili kutumiwa kama taasisi ya demokrasia.

Karume alisema anashangazwa na mtindo wa viongozi wa wapinzani Zanzibar kukimbilia kwa baadhi mabalozi kila wanapoanzisha vurugu wakati ndani ya nchi kuna taasisi za kidemokrasia zenye jukumu la kuimarisha utawala bora.

Akitoa mfano wa tukio la vurugu lililotokea mwishoni mwa wiki Mahonda, Zanzibar, Rais Karume alisema: “Kama wapinzani wanahisi wamenyimwa haki yao basi wangekwenda mahakamani kushitaki na si kwa mabalozi kwani mahakama ndiyo taasisi inayotoa haki....muhimu ni kuwepo maelewano na uhusiano mzuri na si vurugu.”

Rais Karume alikumbusha kuwa Zanzibar kwa ridhaa za wananchi wenyewe imeanzisha mfumo wa demokrasia ambapo viongozi wa kisiasa wanatakiwa kunadi sera na si vurugu.

“Ndani ya mfumo huo hakuna nafasi ya ugomvi... tunapingana kwa sera, lakini hatupigani,” alisisitiza Rais Karume.

Karume aliishukuru serikali ya Ujerumani kwa msaada mkubwa waliotoa kugharamia ujenzi wa hospitali hiyo ya kijeshi ambayo hadi kumalizika kwake imekisiwa kugharimu Sh bilioni1.6.Jengo hilo la hospitali linatarajiwa kumalizika Agosti mwakani.

Mapema, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Wolfgang Ringer alisema kuwa moja ya masharti ya msaada huo ni kwamba hospitali itatoa huduma kwa wapiganaji na wananchi.

 

 

Mangula ahimiza umakini wa vyama kuteua mawakala

Na Mwandishi Wetu, Moshi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Philip Mangula, amesema ni vyema vyama vya siasa viwe makini vinapoteua mawakala wake wa uchaguzi ili kuondoa hofu ya kuibiwa kura na hivyo uchaguzi wa mwaka huu kufanyika kwa amani na utulivu.

Alisema madai kwamba CCM itaiba kura ni kisingizio cha kuamsha fujo baada ya matokeo kwa kuwa wapinzani wanajua watashindwa.

Mangula alisema kwa utaratibu mzuri uliowekwa na tume za uchaguzi, si rahisi kwa chama chochote kuibiwa kura.

Akifafanua hilo, Mangula aliwapandisha jukwaani watu wawili waliowahi kuwa mawakala kutoa ushuhuda kuhusu isivyo rahisi kuibiwa kura katika chumba cha kuhesabia.

Katika mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Himo, Vunjo, mkoani Kilimanjaro, Mangula alimnadi mgombea ubunge kupitia CCM, wa jimbo la Vunjo, Aloyce Kimaro.

Alisema wanaoeneza porojo za kuibiwa kura huku wakijua wana fursa ya kuweka mawakala kulinda kura zao zisiibwe ni waongo na wazushi.

Kuhusu hoja kwamba watasindikiza masanduku ya kura ili zisiibwe, Mangula alisema huko ni kupoteza muda kwani kura zitahesabiwa kituoni na mawakala wa kila chama watatia saini fomu maalum kukubali matokeo.

Alisema kwa kuwa kila wakala wa chama ataondoka na fomu iliyotiwa saini na kila chama, haitakuwa rahisi kwa mtu yeyote kubadilisha matokeo na hivyo hakuna uwezekano wa kura kuibwa.

 

 

Mkapa ahimiza kuharakishwa kuanzishwa kwa shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa amesema kuwa ana matumaini makubwa kwamba umuhimu wa kufufuliwa jumuiya ya Afrika Mashariki, safari hii, utaharakisha kuanzishwa kwa shirikisho la kisiasa la nchi hizo.

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya chakula cha jioni alichoandaliwa na mwenyeji wake Rais Mwai Kibaki wa Kenya. Rais Mkapa ambaye anarejea nchini leo, alikuwa Kenya kwa ziara ya kikazi.

Alisema marais waliowatangulia Rais Kibaki na yeye, waliweka mazingira mazuri na imara ya kuanzishwa kwa shirikisho la kisiasa.

Rais Mkapa alisema msingi wa shirikisho hilo umeshaanzishwa ambapo marais hao na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, wameongeza nguvu kwa kuanzisha umoja wa forodha.

"Historia ni mwalimu mzuri. Haishangazi leo tunajenga Jumuiya mpya ya Afrika Mashariki kwa uangalifu na tahadhari, kutokana na mafunzo ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.

"Kuvunjika kwa jumuiya ya awali ilikuwa hasara kubwa kwetu," alisema na kusisitiza kuwa juhudi ziwepo zitakazodhibiti uvunjaji wa jumuiya hii mpya.

Aliwataka viongozi wa Kenya na Uganda, pamoja na mrithi wake katika Serikali ijayo ya Tanzania, kuendeleza mchakato huo.

Rais Mkapa aliusifu ushirikiano alioupata kutoka kwa viongozi wenzake wa Afrika Mashariki na nchi jirani na kusema kwa pamoja walionyesha mshikamano katika Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola na hata katika masuala ya kimataifa katika utawala bora, maendeleo, ulinzi na usalama.

Aliipongeza Serikali ya Kenya na watu wake kwa hatua waliyopiga katika kuimarisha uchumi wa nchi hiyo, mshikamano wa kisiasa walionao na amani.

Rais Mkapa alisema kama nchi zinazoendelea, lazima viongozi na wananchi wakabiliane na changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kujenga taifa la kisasa.

Rais alishukuru kwa kutunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa katika Chuo Kikuu cha Kenyatta na kusema hiyo inaonyesha wanafunzi wa chuo hicho na Serikali ya Kenya wanavyotambua mchango wake katika kuhudumia watu kisiasa na kijamii.

Katika ziara hiyo, Rais Mkapa aliongozana na mkewe, Anna Mkapa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Abdulkadeer Shareef, na Naibu Waziri wa Afya wa Zanzibar, Sultan Mugheiry.

 

 

Maadhimisho ya upunguzaji maafa leo

Na Furaha Omary

LEO ni siku ya kuadhimisha upunguzaji wa maafa Duniani.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (SERA), William Lukuvi, jana, ilisema lengo la siku hii ni kuwafanya wananchi waelewe kuhusu maafa na madhara yake.

Waziri Lukuvi alisema Baraza la Umoja wa Mataifa hutoa kauli mbiu kwa wananchi kwa madhumuni ya kuwasisitiza mambo ya kuzingatia katika mwaka huo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Matumizi ya vyombo vya fedha vya mitaji midogo na vya kinga ya jamiii katika kupunguza hatari za maafa duniani," alisema Lukuvi.

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu imetokana na ukweli kuwa shughuli za uzuiaji, upunguzaji na kukabili maafa zinahitaji rasilimali za kutosha.

Alisema kwa sasa Tanzania inatishiwa na majanga ya magonjwa ya milipuko, maradhi ya mifugo, ukame, mafuriko, matetemeko ya ardhi, ukimwi, moto, ajali za vyombo vya usafiri na viwandani na migogoro ya kijamii.

"Wananchi wanaweza kutambua sababu na mbinu za matishio haya, lakini kutokana na ukosefu wa rasilimali au utaratibu wa kujiwekea kinga za kijamii wamekuwa wakishindwa kupunguza madhara yanayowatishia mara kwa mara," alisema

Pia aliwataka wananchi kutumia vyombo vya fedha vya mitaji midogo na kinga ya kijamii ambavyo vilithibitishwa kuwa na manufaa katika nchi kama silaha dhidi ya umaskini na njaa.

Lukuvi alisema watu wenye kipato cha chini wataweza kufikia vyombo hivi na hivyo kufanya maendeleo ambayo hupunguza madhara ya maafa hasa katika kuwapa wanawake uwezo wa kupunguza umaskini. Siku hii huadhimishwa kila Jumatano ya pili ya 0ktoba.

 

 

Kanda ya Ziwa kuwa wazalishaji wakubwa wa mpunga - Kikwete

Na Dunia Mzobora, Kahama

MGOMBEA urais wa wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete, amesema Serikali ya CCM itahakikisha mikoa ya kanda ya Ziwa inapewa nafasi ya kuwa mzalishaji mkubwa wa mpunga.

Kikwete alitoa ahadi hiyo juzi katika mkutano wa kampeni uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Kahama, walioonyesha wazi nia ya kuipatia CCM ushindi wa kishindo dhidi ya vyama vya upinzani, katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwezi huu.

Alisema Serikali ya CCM inaeleza wazi katika Ilani yake kuwa itatoa fursa kwa ajili ya wakulima kuzalisha kwa wingi mazao na kwamba kwa Kanda ya Ziwa, mpango umeandaliwa ili kuwawezesha kuwa wazalishaji wakubwa wa zao la mpunga.

Alisema chini ya mpango huo, serikali itahakikisha inawapatia wataalamu wa kutosha wa kilimo cha umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi.

Katika ziara yake hiyo, Kikwete ambaye pia anawanadi wagombea wa udiwani na ubunge amezidi kuvutia wananchi na wapinzani kujiunga na CCM na kuahidi kuwa serikali atakayoiunda ikiwa atachaguliwa, itahakikisha wakulima wanapewa fursa nzuri ya kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara kwa nia ya kuwaondolea umaskini.

Alisema chini ya mpango huo, Wilaya ya Kahama itanufaika na umwagiliaji kupitia mradi wa maji wa Ziwa Victoria utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 170, utakapokamilika.

Sambamba na mpango huo, Kikwete alisema serikali ya CCM katika ilani yake inaelezea wazi kuwa imedhamiria kuondoa tatizo la mbolea na pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa kutoa ruzuku ili waipate kwa gharama nafuu na kwa wakati unaohitajika.

Hiyo alisema, itawasaidia wakulima kutoelemewa na mzigo wa gharama za kilimo na kwa kufanya hivyo kutawafanya wakulima waweze kupata faida kwa mazao yao.

"Ninafahamu matatizo ya wakulima hususan kuhusu suala la mbolea, tutatoa ruzuku kwa mbolea ili wakulima waweze kumudu gharama yake," alisema Kikwete akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika kumsikiliza.

Kuhusu watoto yatima na wasiojiweza, Kikwete alisema watahakikisha wanapatiwa msaada wa kusoma kwa kutumia fedha za serikali badala ya kutegemea wahisani na vyama vya kujitolea.

Alisema Serikali ya CCM inatambua kuwa walemavu, watoto yatima na wasiojiweza ni Watanzania na wanahitaji kunufaika na matunda ya nchi yao kama walivyo wananchi wengine.

Alisema mpango maalumu umeandaliwa ili watoto yatima na wasiojiweza waweze kuishi na kusoma katika mazingira ambayo hawatajiona kuwa wanyonge badala yake watajiona sawa na watoto wenzao.

Kikwete katika mkutano wake uliyofanyika juzi wilayani Nzega, aliwapokea wanachama wapya 603 waliyojiunga na CCM kutoka vyama vya upinzani.

Pia alipohutubia mkutano wa kampeni mjini Kahama, juzi hiyo hiyo, mgombea huyo wa urais kupitia CCM alimpokea Mwenyekiti wa CHADEMA wa wilaya hiyo, Simon Ngeleja, ambaye amekihama chama hicho na kurejea CCM.

Pamoja naye, mwenyekiti huyo wa zamani wa CHADEMA alirejea CCM akiwa na wanachama wengine 308 wa chama hicho na kufunga kabisa ofisi ya Chadema wilaya ya Kahama.

 

 

 

CCM ikishinda hospitali ya Pasua kuwa ya wilaya

Na Mwandishi Wetu, Moshi

MGOMBEA ubunge jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi, Elizaberth Minde, amesema iwapo CCM itapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza, itahakikisha hospitali ya Pasua inapewa hadhi na kuwa ya wilaya.

Alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa kampeni uliofanyika Boma Mbuzi katika Kata ya Pasua, mjini Moshi.

Mgombea huyo alisema hilo linatokana na ukweli kwamba uboreshaji wa hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuifanya iwe ya wilaya uko ndani ya CCM na serikali yake.

Akihutubia katika mkutano huo uliofurika mamia ya wakazi wa kata hiyo, Elizaberth alisema mafanikio na maendeleo kama hayo yanawezwa kufanywa na CCM tu kwani ndiyo chama pekee chenye sera na ilani sahihi zinazolenga katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Mgombea huyo alisema juhudi hizo zitakwenda sambamba na uimarishaji wa huduma za maji katika maeneo ya Matindigani, Relini na Boma Mbuzi.

Alisema katika kudhihirisha ukweli kwamba CCM imekuwa ikiwajali wananchi wake imekuwa ikitoa bure huduma mbalimbali kwa wazee na watu wasiojiweza.

Mgombea alitoa mfano wa huduma za afya na maji ambayo wazee wamekuwa wakipewa ndoo nane za maji bure kwa siku, hatua aliyosema kwa kiwango kikubwa imewapunguzia adha ya kutafuta maji.

Aliwasihi wananchi kutochagua vyama ambavyo mbali ya kutokuwa na serikali havina sera na ilani sahihi zinazolenga kuwaendeleza wanachi kwa ujumla.

Katika mkutano huo, baadhi ya wanachama kutoka kambi ya upinzani waliojiunga na CCM hivi karibuni walielezea kusikitishwa kwao kwa kupoteza muda wao wakiwa katika kambi hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Nicodemus Massatu, kutoka CHADEMA, alikifafanisha CCM na kisiki na kuwataka wapinzani kuacha ndoto ya kuking'oa madarakani.

" CCM ni kisiki cha mpingo kama Ndesamburo (Mbunge wa Moshi Mjini kupitia CHADEMA), Lipumba na wenzake wanasubiri CCM kiondoke madarakani, basi waendelee kusibiri miaka 100 ijayo," alisema Massatu na kuongeza yeye aliamua kurejea baada ya kuona ataendelea kuzeeka kama ataendelea kuwa na ndoto hizo.

Alisema hilo linatokana na umahiri wa CCM uliokifanya kishinde katika chaguzi zote zilizopita.

Massatu aliwasihi wananchi wa jimbo la Moshi Mjini kutoendelea kufanya makosa kwa kuchagua upinzani kama wanataka maendeleo ya kweli.

Alisema CHADEMA hakina serikali na hivyo wananchi wasitarajie maendeleo kwani kipaumbele kitaendelea kutolewa kwa majimbo yanayoshikiliwa na CCM.

Massatu alisema chini ya uongozi wa CHADEMA, jimbo la Moshi Mjini limeendelea kuwa nyuma kimaendeleo licha

ya rasilimali zilizopo huku mbunge wake akiendelea kutoa ahadi hewa kwa wananchi.

Alisema wakati umefika kwa wananchi kutoendelea kuchagua viongozi wanaotanguliza maslahi yao na badala yake wachague viongozi kutoka vyama vyenye uwezo, sera na ilani sahihi zinazolenga katika kuwaletea maendeleo wananchi kwa ujumla.

Katika mkutano huo, Elizaberth alimnadi mgombea wa Udiwani wa kata ya Pasua, Godfrey Mwangamilo, na kuwataka wananchi kumchagua ili kukamilisha falsafa ya mafiga matatu.

Pia alihitimisha mkutano huo kwa kwenda kusalimiana na wanachama wa upinzani waliohudhuria mkutano huo na

kuwaomba kura zao. Wengi walionekana kuvutiwa na 'staili' hiyo na kuonyesha kumkubali mgombea huyo, ambaye katika uchaguzi uliopita hakupita katika jimbo hilo. Mbunge wa sasa wa jimbo hilo ni Philemon Ndesamburo kutoka CHADEMA.

 

UWT, UVCCM yawahakikishia wagombea wa Chama ushindi

Na Naftali Siwonike, Iringa

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) mkoani hapa, umewapa matumaini makubwa ya kushinda kwa kishindo wagombea wote wa CCM mkoa wa Iringa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, Katibu wa Umoja wa Vijana mkoa, Bajoji Zakaria, alisema kujitokeza kwa wagombea wa upinzani katika majimbo na kata, kunaipatia CCM ushindi kutokana na jinsi ambavyo wananchi walivyokuwa na msimamo wa kutopoteza muda wao kuchagua vyama visivyo na ofisi kuongoza nchi.

Alisema hakuna sherehe isiyokuwa na washangiliaji, hivyo anaamini vyama vya upinzani ni 'washangiliaji' wa wagombea wa CCM, ikiwa ni pamoja na kuyaeleza ambayo CCM imeyafanya kwa kipindi chote toka nchi ipate uhuru mwaka 1961.

"Naamini wanapita na kuyanadi mafanikio ya CCM na kujitokeza kwao ni ishara kuwa CCM imefanya mengi, na kwa kuwa wanahitaji kuja kugombea miaka 200 ijayo, ni vyema wakawa wanapita kujua jinsi ambavyo siasa ilivyo, ila si kwa kupewa uongozi," alisema.

Aliwataka wananchi kutoyumbishwa na wagombea wa vyama vya upinzani, kwani kazi waliyopewa ni kujitangaza kama wapo, lakini si kupewa uongozi.

Zakaria aliwataka pia vijana kundelea kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha hakuna hata kura moja

inayokwenda kwa mgombea wa chama cha upinzani, wala inayoharibika, kwa kupita kuwanadi wagombea wa CCM.

Alisema kuwa kupingwa kwa wana CCM katika baadhi ya majimbo mkoani hapo ni mbegu ya fitina na chuki

iliyopandikizwa na wapinzani kwa lengo la kuipaka matope CCM kuwa imesimamisha wagombea wasio kubalika, ambapo mbinu hiyo imepitwa na wakati na katika

kuhakikisha kuwa wagombea wote wa CCM wanakubalika wapinzani wasubiri Oktoba 30, waone ushindi

utakaopatikana katika majimbo hayo.

Katibu wa UWT mkoa wa Iringa, Asha Kipangula, alisema kwa kuwa wanawake ndio wenye majukumu makubwa ya kulea familia, UWT mkoa wa Iringa imejipanga kuhakikisha hakuna hata kura moja itayopotea.

Kipangula alisema katika majimbo mawili ya mkoa wa Iringa, Iringa Mjini na Njombe ambayo yamesimamisha wagombea wanawake, watahakikisha wagombea hao wanashinda.

Mbali ya wagombea hao alisema kuna wanawake wamegombea katika kata sita za mkoa huo, na amewataka wanawake na wananchi wote kuhakikisha wanawapa

kura zao wagombea wote wa CCM.

 

Pemba watakiwa kuipa ushindi CCM

Na Bashir Nkoromo, Pemba

WANANCHI Kisiwani Pemba wametakiwa kuipa kura nyingi CCM katika uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa mwezi huu, kama shukurani kwa iliyoyafanya katika awamu zake za uongozi zilizopita.

Hayo yalisemwa juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mazingira na Ushirika wa Zanzibar, Mohammed Aboud, wakati akitoa elimu ya uraia kwa wapiga kura, katika eneo la Kiwani na Mkanyageni, mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema katika awamu ya sita ya uongozi wa CCM chini ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, CCM imefanikiwa kuondosha kero kuu zilizokuwa zikiikabili Pemba, ikiwemo miundombinu ya barabara na bandari.

Aboud aliwapa wananchi mfano wa kero zilizoondoshwa kuwa ni pamoja na kujengwa kwa kiwango cha lami barabara za Mkoani-Chake Chake, Mtuhaliwa-Chokocho, Chake Chake-Wesha, Machomanne-Vitongoji, Kilindi-Micheweni, na barabara kuu inayounganisha Chake,Ole na Konde.

Alisema kujengwa kwa barabara hizo kumefungua kisiwa cha Pemba na kuwafanya wananchi kupata fursa ya kuuza bidhaa zao hasa za kilimo, na kurahisisha usafiri wa kawaida baina ya watu wa sehemu moja hadi

nyingine, tofauti na zamani.

Aboud alitaja pia bandari zilizoboreshwa na kuwa sasa zinafanyakazi ni za Mkoani, Wesha na Wete, ambazo aliwaambia wananchi hao kwamba zimepanua uwezo wa wakazi wa Pemba, kusafirisha na kupokea bidhaa

kwa urahisi, na kwamba kwa ufupi zimefungua milango ya biashara.

Waziri huyo alisema, mbali na miundombinu hiyo ya barabara na bandari, pia uongozi wa Karume umeliondosha tatizo sugu la umeme lililokuwa likikikabili kisiwa cha Pemba miaka nenda miaka rudi, na sasa umeme unapatikana maeneo yote kisiwani humu.

Kuhusu kero ya uhaba wa majisafi na salama, Mohamed Aboud, alisema kwa sasa tatizo hilo limepunguzwa kwa kiasi kikubwa baada ya serikali ya CCM kulipunguza ambapo sasa asilimia 75 ya wakazi wake wanapata maji ya uhakika.

Alisema katika kuondoa tatizo la uhaba wa maji, serikali ya CCM imeweka matangi makubwa ya maji katika maeneo ya Machomanne, Wete, Chake Chake, Mtambile, Mkoani na Uweleni.

Waziri alisema katika hali iliyokuwa haitarajiwi, serikali ya awamu ya sita ya Karume, imefikisha maji hadi katika visiwa vya Kojani, Fundo na Kisiwapanza, ambako alisema sasa nako wanapata maji safi na salama.

Kuhusu amani na utulivu, waziri huyo alisema serikali ya awamu ya sita ya CCM chini ya Karume, imefanikiwa kujenga maelewano makubwa baina ya wananchi kwa wananchi, na wananchi na serikali.

Alisema sasa serikali ipo katika hatua nyingine kubwa za kuhakikisha kisiwa kinajitosheleza kwa chakula katika msimu wote, na alifafanua kwamba kwa sasa

sehemu kubwa ya chakula kisiwani hasa matunda na mchele inatoka Tanzania Bara.

Waziri huyo wa kilimo alisema wakati kilimo kinaboreshwa, pia upo mradi wa kuboresha uvuvi na mazingira, na miradi hiyo yote imekwishapatiwa fedha na ipo katika hatua za awali kutekelezwa.

 

 

Mkullo: Nitaishauri serikali kutoa mikopo ya riba nafuu kwa vijana

Na Stan Likomawagi, Kilosa

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya CCM, Mustafa Mkullo, amewahakikishia vijana katika jimbo Kilosa, kuwa akichaguliwa ataishauri serikali kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana.

Mkullo aliwambia vijana katika mkutano wake wa kampeni katika kijiji cha Mvumi, wilayani Kilosa, kuwa iwapo watamchagua atashirikiana na uongozi wa wilaya kutafuta mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya vikundi vya biashara vya vijana kama moja ya mikakati ya kufuta umasikini na kuinua uchumi wa vijana.

Alisema cha msingi kwa vijana katika kipindi hiki ni kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao, kwa kumchagua yeye kuwa mbunge.

Hata hivyo, aliwashauri vijana hao kuunda vikundi vya biashara badala ya kusubiri mikopo kwa mtu mmoja mmoja.

Alisema upatikanaji wa mikopo hiyo kwa vijana utakuwa rahisi endapo vijana wataunda vikundi vya uzalishaji mali katika sehemu zao, ili kuwarahisishia kupata mikopo hiyo kutoka taasisi zinazotoa mikopo.

Alisema suala la kuvikopesha vikundi vya uzalishaji mali mikopo yenye riba nafuu ni moja ya utekelezaji wa sera na ilani ya CCM ya kufuta umasikini kwa Watanzania kwa kupitia mpango wa MKUKUTA.

Aliwashauri wakazi wa jimbo la Kilosa, kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuwasemea wananchi, badala ya kuchagua viongozi wasio na uwezo wa kuwasemea kero zao bungeni.