UHURU 13.09.2005

 

 

 

KIKWETE ANGURUMA UINGEREZA NA KUSEMA:

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete amesema kuwa kipaumbele cha Tanzania kwa sasa ni kuondoa umasikini na sio kugombea ujumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kikwete ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alisema hayo jana alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mjini London, Uingereza akiwa njiani kuelekea New York, Umoja wa Mataifa.

Alisema hoja ya Tanzania siyo kukimbilia ujumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bali ni kupigania katika majukwaa mbalimbali, yakiwemo vikao vya kimataifa namna ya kuondoa umasikini.

Kikwete amekwenda kuungana na Rais Benjamin Mkapa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi kuhusu utekelezaji mchakato wa maendeleo ya malengo ya milenia ambayo yanatilia mkazo uondoaji umasikini.

Alisema mkutano uliopita wa wakuu wa nchi ulizungumzia namna ya kupambana na umasikini ambapo ilionekana kwamba zinahitajika dola za Marekani bilioni 50 kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoendelea kila mwaka kupambana na umasikini.

Kikwete alisema mkutano wa New York utatathmini utekelezaji wa yale waliyokubaliana. Mkutano wa mwisho kuhusiana na masuala ya umasikini ulifanyika Mexico.

Kuhusu nchi za Nigeria, Misri na Afrika Kusini kugombea nafasi ya ujumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Kikwete alisema kwa kuwa nchi zote zinatoka Afrika, Tanzania haitakuwa na upande wowote zaidi ya kuiunga mkono itakayochaguliwa.

Alifafanua kwamba ni muhimu kwa bara la Afrika kuwa na mwakilishi katika baraza hilo, hasa kwa kuwa mabara mengine tayari yana wawakilishi, kwa mfano, bara la Ulaya linawakilishwa na Uingereza, Ufaransa na Urusi, na Ujerumani nayo hivi sasa inataka nafasi hiyo. Kwa bara la Asia, Waziri Kikwete alisema China ni mjumbe na wakubwa pia wanataka Japan iingizwe.

Wakati huo huo, wakuu wa nchi na serikali zaidi ya 170 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) watakutana kuanzia kesho Makao Makuu ya Umoja huo, New York, Marekani.

Pamoja na mambo mengine kwenye mkutano huo utakaomalizika Ijumaa wiki hii, wakuu hao watajadili uimarishaji wa umoja huo likiwemo Baraza Kuu, Baraza la Uchumi na masuala ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, John Hendra alisema mkutano huo utatoa fursa kwa wakuu wa nchi hizo kutoa maamuzi kuhusu kutokomeza umasikini, kuimarisha haki za binadamu, kupambana na ugaidi na kusaidia ujenzi mpya wa nchi zilizokuwa kwenye vita.

Hendra alisema agenda za mkutano huo zimezingatia mapendekezo kadhaa yanayotekelezeka ambayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan kwenye ripoti yake “Katika Uhuru Mpana: Kuelekea maendeleo, Usalama na haki za Binadamu kwa Wote” aliyoitoa Machi, mwaka huu.

Inakadiriwa watu bilioni moja wanaishi katika dimbwi la umasikini, ambapo watu 20,000 wanakufa kila siku kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika. UN imeweka Malengo ya Maendeleo ya Milenia ikiwa ni pamoja na kupunguza umasikini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015.

Kwa mujibu wa mpango huo, nchi za Umoja wa Ulaya (EU) zimeahidi kutoa msaada kwa nchi masikini duniani ikiwemo kuzifutia madeni ya zaidi ya sh. trilioni 40 kama ilivyotangazwa na nchi nane zilizoendelea zaidi duniani (G-8) Julai, mwaka huu.

Hendra alisema katika mkutano huo pia wakuu hao watajadili suala la kuongeza wajumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuwa chombo chenye ushirikishwaji zaidi kulingana na hali ya uanachama wa umoja huo kwa hivi sasa.

Wakuu hao kwa mujibu wa Hendra pia watajadili mapendekezo ya kuanzisha chombo kipya cha Baraza la Haki za Binadamu ambalo halitajishughulisha na masuala ya siasa pekee.

 

 

 

Watano mbaroni kwa mauaji ya Manzese

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Omar Ramadhan Mapuri amesema watu watano wamekamatwa hadi sasa kuhusiana na mauaji ya watu watano wa familia moja Manzese mjini Dar es Salaam yaliyotokea mwishoni mwa wiki.

Sambamba na watu hao kukamatwa Waziri Mapuri alisema amesikitishwa na kitendo cha waandishi wa habari kupigwa hadi kuumizwa na askari Magereza.

Mapuri aliyasma hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusiana na kitendo cha askari Magereza wa Ukonga kuwapiga Christopher Kidanka wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Mpiga picha wa The Citizen, Mpoki Bukuku.

Akizungumzia tukio la ajali ya moto iliyotokea Midizini, Manzese, Waziri alisema watu watano wamekamatwa hadi sasa kuhusiana na tukio hilo lililoua watu watano na kwamba uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea na watakaokamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Tayari Chama Cha Mapinduzi, mkoa wa Dar es Salaam, kimeishutumu CUF kwa kula njama zilizosababisha kifo cha kinyama cha Kada wa CCM, Mwajuma Nyanza (53) na wanafamilia wake wanne, Manzese Midizini.

Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Mattson Chizi, alisema kuwa vifo hivyo vilitokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako majeruhi hao walikimbizwa kupata matibabu na kuwa ndilo hitimisho la chokochoko za CUF zilizoanza muda mrefu dhidi ya marehemu.

Chizi alisema marehemu Nyanza alifanyiwa fujo nyingine siku chache kabla ya unyama huo na aliripoti katika kituo kidogo cha polisi Manzese, lakini katika mazingira ya kutatanisha, watuhumiwa walikamatwa, na muda mfupi baadaye waliachiwa.

Alisema  watuhumiwa  walionekana kuranda mtaani na kumtisha waziwazi kwamba watalipiza kisasi. Waliokamatwa na kufikishwa  polisi walikuwa wanne, alieleza.

Aliwataja  marehemu kuwa ni wajukuu wawili Mwajuma Rashidi (16)  na David John (3) na mwanawe Mwabai Lucian (11)  aliyebakia hospitali ni mjukuu mwingine, Asha Rashidi (13)

Kuhusu suala la waandishi wa habari na askari Magereza ni kwamba lilitokea wakati waandishi hao walipokwenda Ukonga ambako jeshi la Magereza lilikuwa likifanya oparesheni ya kuwahamisha waliokuwa wafanya kazi wa lililokuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) kwenye nyumba tisa ambazo jeshi la Magereza lilizinunua kutoka Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC).

Mapuri alisema kuwa jeshi la Magereza walizinunua nyumba hizo mwaka 2002 kwa ajili ya wafanyakazi hao na tangu kipindi hicho wamekuwa wakifanya suluhu ya kibinadamu ya kuwataka watu hao kuhama kwenye nyumba hizo.

Alisema nyaraka zote zinaonyesha Magereza ndiyo wenye haki ya nyumba hizo na kwamba waliwaandikia barua ya kuwataka wahame na ndipo mmoja wao alipoita waandishi wa habari.

Mapuri aliwatahadharisha wananchi na waandishi wa habari kuwa makini na maeneo ya kijeshi kwamba siyo maeneo ya kwenda bila idhini yao.

 

 

 

Maandishi ya kashfa Msikiti wa Mtoro yafutwa

Na mwandishi Wetu

MAANDISHI kwenye ukuta wa choo cha Msikiti wa Mtoro, Kariakoo mjini Dar es Salaam yaliyokuwa yakiikashifu CCM na Rais Benjamin Mkapa yamefutwa.

Hali ya kuwepo kwa maandishi hayo ambayo sambamba na kuikashifu CCM, pia yalikuwa yanakisifu chama cha CUF na viongozi yaligundulika mwishoni mwa wiki iliyopita na kuripotiwa kwenye gazeti la Mzalendo juzi.

Haikuweza kufahamika maandishi hayo yalifutwa lini, lakini mwandishi wa habari hii alipoingia kwenye choo hicho jana saa saba alikuta maandishi hayo yakiwa yamefutwa huku ukuta ukiwa mweupe na kung’ara tofauti na ulivyokutwa mwishoni mwa wiki.

Kufutwa kwa maandishi hayo, pia kumesaidia kukiweka choo hicho katika hali ya usafi zaidi, kwani ukuta wake ambao ulikuwa na ukungu mwekundu uliotumika kuandika kashfa hizo umesafishwa.

Maneno  hayo ambayo yalikuwa yameandikwa sehemu za kulia na kushoto mwa ukuta huo ni pamoja na ‘CCM inawabugudhi Waislamu’, ‘Mkapa fala’, ‘CUF chama dume’, ‘Lipumba mwanamme’, na kwamba muhusika alifanikiwa kuyaandika kwa kuchora herufi zinazounda maneno hayo kwenye ukungu mwekundu uliokuwa umetapakaa ukutani mwa sehemu ya ndani ya choo hicho.

Mengine ni ‘Chagueni CUF’, ‘CUF yes’, ‘CCM hiyoo’ na ‘Seif mshindi’ yote yakipingana na kauli zilizowahi kutolewa na  baadhi ya viongozi wa msikiti huo kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea ambao waliahidi kutoruhusu msikiti huo kutumika kukihujumu au kukifanyia kampeni chama chochote cha siasa.

Katika kuhakikisha azma hiyo, kabla ya kuanza kwa mbio za kugombea urais na wabunge kujinadi, Imamu wa Msikiti huo wa Mtoro, Sheikh Khalifa Khamis aliwahi kukutana na kuzungumza na baadhi ya wagombea urais wa vyama kadhaa na kuwauliza mambo mbalimbali, ikiwemo kuwataka waeleze msimamo wao kuhusu hatma ya Waislamu endapo watafanikiwa kuingia madarakani.

 

 

 

 

 

 

Ngome za CUF Kilwa zasambaratika

Na Rashid Musa, Kilwa Masoko

 NGOME  za chama cha Civic United Front (CUF) wilayani Kilwa ziko taabani kufuatia kampeni kali yenye mafanikio ya CCM inayoendelea kuzoa makundi ya wanachama na viongozi maarufu wa chama hicho.

Mafanikio hayo katika majimbo yote mawili ya Kilwa Kusini na Kaskazini yanatokana na wananchi kuwashtukia wapinzani na sera zao za ulaghai na vurugu na CCM kuwasimamisha wagombea wanaokubalika katika nafasi zote.

Wananchi kadhaa waliohojiwa katika miji ya Kilwa Masoko na Kivinje inayodaiwa kuwa ngome kuu ya  CUF walisema CCM itaibuka na ushindi mkubwa kutokana na wagombea wake kukubalika na jamii.

CCM kimesikia kilio cha wananchi wa wilaya hiyo cha  kuwaweka wagombea wanaotokana na matakwa yao wenyewe katika majimbo yote mawili.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa wilaya Amin  Mwaya alisema  asilimia  85 ya madiwani na wabunge wawili wa zamani wameachwa na wananchi wenyewe kupitia kura za maoni zilizopigwa.

Alisema hatua hiyo na Halmashauri Kuu ya Taifa kuwateuwa wagombea walioongoza katika kura hizo za maoni kumedhoofisha ngome kuu ya upinzani hasa katika jimbo la Kilwa Kusini ambako CUF ilijichimbia tangu uchaguzi uliopita.

Mwaka 2000,  CUF ilipata nguvu katika jimbo la Kilwa Kusini baada ya vikao vya juu vya Chama  kumuengua Hasnein Gulamaabbasi Dewji aliyeongoza katika kura za maoni.

Katika kinyang’anyiro cha mwaka huu, Dewji  ameteuliwa na Chama baada ya kupata ushindi mkubwa katika kura za maoni.

Kufuatia kuteuliwa kwake kugombea jimbo hilo matawi imara ya vyama vya upinzani yanaanguka kwa kukosa wanachama wanaorudi kwa kasi na ari mpya kabisa.

Miongoni mwa waliorudi katika kipindi hiki cha kampeni ni pamoja na Wenyeviti wa matawi na Serikali za vijiji na Diwani wao wa zamani wa Kata ya Kilwa Masoko mjini Said Alumas.

Alumasi ambaye amerudi na mamia ya wanachama na kuidhoofisha kabisa ngome ya CUF mjini hapa alisema kurudi kwake CCM kumemaliza ngome ya upinzani na atahakikisha CUF inakufa kabisa katika mji huu kwa kuwa anajua siri zao zote za ulaghai wanazotumia.

Bibi kizee wa miaka zaidi ya 80, Nasifu Hasani mkazi wa Kilwa Kivinje alisema kilichowakatisha tamaa wananchi ni kwamba  upinzani eneo hilo ni vurugu  na ulaghai mkubwa kama uliojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Jimbo la Kilwa Kusini ndiyo iliyonekana kuwa ngome ya CUF kwa mikoa ya Mtwara na Lindi ambapo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa walipata asilimia 28.2 ambayo ni kubwa ukilinganisha na ushindi waliopata upinzani wilaya zingine katika mkoa hii.

Hali hii ya CUF ilifanya kuwa na mategemeo makubwa katika jimbo hili lakini kadri kampeni inavyopamba moto ndivyo chama hicho kinavyozidi kudorora kwa watu wengi kurudi CCM.

 

 

Karume: Mwekezaji kiwanda cha Mahonda kapatikana

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

RAIS  Amani Abeid Karume amewahakikishia wananchi wa Bumbwini kwamba ajira katika kiwanda cha sukari Mahonda itarudi  kwao kwa sababu mwekezaji ameshapatikana.

Karume alitoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wa kampeni mwishoni mwa wiki kwa kuwaambia wananchi wa Bumbwini ambao baadhi yao walikuwa wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Mahonda kabla ya kufungwa.

Alisema  kiwanda hicho kimeshapata mwekezaji na kinatarajiwa kufufuliwa na kuanza kazi baada ya muda siyo mrefu.

“Ajira zilizopotea zitarudi kiwanda kitakapoanza kazi. Na si ajira tu bali hata wakulima watafaidika kwa kulima miwa, kwa sababu kiwanda kitanunua miwa kutoka kwa wakulima,” alisema huku akishangiliwa.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa  tiketi ya CCM,  amesema akichaguliwa kuiongoza tena Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu ujao, Serikali yake itawekeza zaidi katika sekta ya kilimo ili kuboresha maisha ya wakulima.

“Tutaendelea na mpango wa kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, ili mkulima aboreshe maisha yake kwa kupata mavuno mazuri ya uhakika,” alisema katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katika kijiji cha Bumbwini Makoba, juzi.

Alisema katika mpango huo wa kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, Serikali itajitahidi kusambaza pia teknolojia ya umwagiliaji wa matone kwa wakulima wa mazao ya kawaida.

Mgombea huyo ambaye anatetea kiti chake, alisema wananchi wengi wa Bumwibini na Zanzibar ni wakulima, ambao hawana budi kuendelezwa na kuwawekea mazingira bora zaidi ya kuendesha kilimo chenye manufaa kwao.

Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Bumbwini ambayo iko katika hali mbaya, alisema ujenzi wake utaanza hivi karibuni na kinachosubiriwa ni kwa mfadhili, Benki ya Maendeleo ya Afrika kuteua mkandarasi wa kufanya kazi hiyo.

Aliwaambia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni uliokuwa umepambwa na rangi za njano na kijani, kuwa kilichochelewesha ujenzi wa barabara hiyo ambayo ilikuwemo katika ahadi za uchaguzi wa mwaka 2000, ni kuhama kwa makao makuu ya benki hiyo kutoka Abidjan, Ivory Coast, kwenda Tunisia.

Alisema benki hiyo ililazimika kuhamisha makao makuu yake kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast, hali ambayo ilichelewesha benki hiyo kuidhinisha fedha za mradi huo pamoja na mingine ikiwemo ya barabara ya Kiembesamaki/Fumba.

“Hiyo ndugu wana CCM na wananchi, ndiyo athari ya vita,” alisema na kuongeza: “Ndiyo maana tunawaomba muendelee kuichagua CCM inayodumisha amani na utulivu, na kuviepuka vyama vinavyohubiri shari na ugomvi.”

Aliwaomba wananchi kuendelea kukipa ridhaa Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza kwa sababu ndicho kinachoongoza katika kuleta maendeleo na ni chama pekee kinachotoa ahadi na kutekeleza.

Mapema Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliwataka wana CCM kutolipiza kisasi kwa vitendo vinavyofanywa na wapinzani kushambulia misafara yao wanaporejea kutoka katika mikutano ya kampeni.

“Vitendo vyao ni dalili kuwa wapinzani wameishiwa, na tutaingia Ikulu kwa muziki,” alisema Mzee Mwinyi.

Aliwasihi wana CCM, wapenzi wake na wananchi wapenda amani, wasikubali kuchokozeka kwa vitendo hivyo na kufanya kama wapinzani wanavyofanywa kwani hicho ndicho wanachokitafuta ili ‘uchaguzi uharibike’.

“Nakuombeni wananchi, na hasa wana CCM tuwe watulivu, tusiige vitendo vyao. Tufuate sheria za nchi,” alisema Mwinyi.

 

 

 

 

 

 

 

Salamu mpya ya Kikwete hii hapa

Na Bashir Nkoromo, Dodoma

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amesema baada ya CCM kuwa ‘mambo poa’ sasa ni ‘mambo Bomba’.

Kila anaposalimia wananchi katika mikutano yake ya kampeni kwa kutumia salamu inayoishia na swali ‘Mambooo?’ iliyoasisiwa na Rais Benjamin Mkapa, Kikwete amekuwa akisisitiza sasa wasiitikie  ‘poaa’ bali  waseme ‘bombaa’.

Kikwete: “Salaam Alaykum, Tumsifu Yesu Kristo, Mambooo?”

Wananchi: Poaaa!

Kikwete: Hapana, msiseme poa semeni ‘bombaa’ kwa sababu  CCM mambo yamezidi baada ya kuwa poa sasa ni bombaa.

Salamu ya “Salaam alaykum,  Mambo?” iliyoasisiwa na  Rais Mkapa tangu wakati wa kampeni zake za kuwania Urais mwaka 1995, imekuwa ikipendwa na wananchi kwa kuwa haibagui dini na pia inawagusa vijana.

Mvuto wa salam hiyo ulionekana  wakati Kikwete alipokuwa akihutubia mikutano yake ya kampeni katika mikoa ya Morogoro na Dodoma  wiki iliyopita.

 

 

 

 

 

 

 

NBC Ltd kuwapatia mikopo wafanyabiashara wadogo

Na Mwandishi Wetu

BENKI ya NBC Ltd inakusudia kuboresha kwa kuanzisha mpango kabambe wa kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wale wa kati ifikapo mapema mwezi ujao, imeelezwa.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Christo De Vries alipozungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam.

Vries alisema licha ya kuwa NBC Ltd inaongoza kwa utoaji mikopo kwa wafanyabiashara wa kada hiyo, wanakusudia kuimarisha huduma hiyo ambapo maelezo ya kina yatatolewa mapema mwezi ujao.

"Hatua hii itafanyika na kufanikiwa kwa kuunga mkono na kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa kada hiyo. Maelezo zaidi yatatangazwa karibuni," alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema watakaofaidika ni pamoja na wafanyabiashara wanaoanza shughuli zao na wale ambao wanaendelea nazo.

Vries alisema kada hiyo ya wafanyabiashara ni muhimu sio tu hapa nchini, bali duniani kote kwa jumla kwa kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya uchumi.

Alifafanua kuwa kwa Tanzania, wafanyabiashara wadogo na wakati wanachangia katika kutoa ajira na ukuzaji uchumi katika maeneo ya mijini na vijijini na kuwa robo tatu ya uchumi wa taifa unachangiwa na kada hiyo ambayo pia inatoa asilimia 20 ya ajira zote.

NBC Ltd ni miongoni mwa benki kubwa ambayo ina matawi 33 huku kukiwa na mashine za kuchukulia fedha 45 katika maeneo mbalimbali nchini.

Vries alisema utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ulikuwepo, lakini sasa benki hiyo imepanga kuboresha zaidi ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa watu kuwa benki hiyo ni kwa wateja wakubwa tu.

"NBC kwa sasa ni miongoni mwa benki zinazoongoza katika utoaji mikopo kwa wafanyabiashara wadogo na wakati hapa nchini," alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo.

 

 

 

 

 

Mazingira bora ya biashara yamepanua sekta binafsi

Na Mwandishi Wetu

UBORESHAJI wa mazingira ya biashara nchini, umewezesha kupanuka kwa sekta binafsi na ukuaji wa haraka wa uchumi.

Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Programu ya Uimarishaji na Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara Tanzania (BEST), Dk. Stergomena Tax-Bamwenda wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wadau wa sekta ya biashara kwenye Taasisi ya Utafiti wa Upunguzaji Umaskini (REPOA), Mikocheni, Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ya wiki moja yanahusu matumizi ya sheria na kanuni bora katika biashara, na tathmini juu ya kanuni hizo katika uboreshaji wa mazingira ya biashara.

Alisema mabadiliko yaliyofanywa katika marekebisho ya uchumi nchini, yamewavutia wawekezaji wengi na hivyo kuwezesha kuanzishwa kwa miradi midogo na ya kati (SMEs) pamoja na sekta binafsi kuwa mhimili katika ukuaji wa uchumi.

"Serikali inatambua kwamba mafanikio katika maendeleo yanategemea mazingira bora yanayowezesha kupanuka kwa sekta binafsi.  Kwa maana hiyo, serikali inatambua na inaendelea na jukumu lake la kuhakikisha kuwepo kwa sera na kanuni bora,” alisema.

Kwa upande wa BEST, Dk. Stegormena alisema programu yake imelenga kuhakikisha biashara inaendeshwa bila kuwepo kwa umangimeza na urasimu.

Kuhusu mafunzo yaliyoanza jana, Ofisa Mtendaji Mkuu huyo alisema wakufunzi watapata uelewa juu ya matumizi ya sheria na kanuni zinazowezesha kuboreshwa kwa mazingira ya biashara hapa nchini.

Alisema mafunzo hayo ni nyenzo muhimu ambayo itawawezesha kushiriki kikamilifu katika upangaji wa sera na kanuni katika nyanja za biashara.

"Mafunzo haya yatasaidia uandaaji wa kanuni ambazo zitakuwa kichocheo cha maendeleo ya sekta binafsi pamoja na kulinda maslahi ya uchumi, jamii na mazingira ya wadau mbalimbali na taifa kwa jumla," alisisitiza.

Kutokana na umuhimu huo, Dk. Stegormena aliwahimiza washiriki kutumia fursa hiyo kuchanganua masuala mbalimbali yatakayosaidia uboreshaji wa mazingira ya biashara pamoja na matumizi ya kanuni bora miongoni mwa wadau.