UHURU 14.09.2005
Sijaona chama pinzani dhidi ya CCM – Mkapa
Darasa la Saba nchini wafanya mtihani leo
Dk. Sheni asisitiza haja ya serikali mbili kwa Watanzania
Ngawaiya awaambia wananchi wasipoteze muda kwa upinzani
TAMWA yaomba wagombea kuepuka lugha za kashfa
Matanki ya maji Mwanza kujengwa karibuni
Msumbiji yausifu mfumo wa muundo wa serikali za mitaa
Sijaona chama pinzani dhidi ya CCM – Mkapa
Asema si kwa Tanzania Bara tu, bali hata Visiwani
Awaambia Watanzania Marekani, CCM itashika dola
Na Maura Mwingira, New York, Marekani
RAIS Benjamin Mkapa amesema hadi sasa hajaona chama chochote chenye mwelekeo wa kutoa upinzani kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), si kwa Tanzania Bara, bali hata Visiwani.
Mkapa ambaye alikuwa akizungumza juzi hapa na Watanzania wanaoishi Marekani alisema ana uhakika kuwa CCM na mgombea wake katika nafasi ya Urais, Jakaya Kikwete pamoja na nafasi za ubunge na udiwani ndio watakaoshika uongozi wa dola, kauli iliyowafurahisha Watanzania hao.
Akielezea zaidi kuhusu hali ya kisiasa pamoja na kampeni za uchaguzi zinazoendelea, Rais aliwaeleza Watanzania hao ambao walijitokeza kwa wingi kuungana naye kuwa hali ilikuwa ni nzuri.
Rais alitumia mazungumzo hayo na Watanzania ambao aliwapatia nafasi ya kuuliza maswali, kwamba ingawa wako mbali na nyumbani, lakini wasiache kudumisha uzalendo wao, kujenga moyo wa kupendana na kuiombea nchi yao katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi huo.
Mkapa alisema kuwa matukio ya vurugu za kisiasa yaliyotokea Januari 26 na 27, mwaka 2001 Tanzania Visiwani, hususani Pemba, yalikuwa ni matukio mabaya katika kipindi cha uongozi wake na ambayo hataweza kuyasahau katika maisha yake yote.
"Katika kipindi cha uongozi wa miaka 10, ni matukio yale ya Januari 26 na 27, yalikuwa mabaya katika uongozi wangu… ni matukio ambayo sitaweza kuyasahau, sitaweza kuyasahau kwa sababu kwanza sikuamini kwamba yangeweza kutokea. Huu haukuwa utamaduni wetu, na si utamaduni wa Watanzania, natumaini kuwa tumejifunza na hayatajirudia tena," alisisitiza Rais.
Alikuwa akijibu swali kutoka kwa kijana Shabani aliyetaka kufahamu ni wakati gani ambao ulikuwa mgumu kwake na ni wakati gani ulikuwa mzuri kwake katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake.
Rais alisema kuwa kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiandika na wanaendelea kuandika kupitia mtandao wa ‘Internet’ kuwa watu waliopoteza maisha yao wakati wa matukio yale walikuwa ni watu ambao hawakuwa na hatia kana kwamba hawakuvunja sheria yoyote.
“Watu hawa wanaandika tu kwamba wale watu waliopoteza maisha hawakuwa na kosa lolote, wanasahau kuwa wale watu walivunja sheria za nchi, walikuwa na mapanga na visu, lakini pia walimchinja askari, lakini hili la kuchinjwa askari haliandikwi kwenye mtandao na hii si haki kabisa… wale walipoteza maisha walikuwa wamevunja sheria," alisisitiza.
Akizungumzia ni kipindi gani kililchokuwa kizuri kwake, Rais alijibu kuwa ni ile siku ambapo mashirika ya fedha ya kimataifa ya IMF na Benki ya Dunia yalipompelekea taarifa kuwa Tanzania ilikuwa imetimiza masharti ya kufutwa kwa nusu ya madeni kupitia mpango wa HIPC.
"Hiki kilikuwa kipindi cha furaha sana kwangu, nilifurahi kwa sababu nilitambua na kuamini kuwa yale mageuzi makubwa ya kiuchumi tuliyokuwa tumeyafanya na kuyasimamia yalikuwa yamekubalika kwa wakubwa hawa… unajua tabu ya wakubwa hawa daima wamekuwa wakituona sisi Waafrika kama malofa, tusiojua kitu, walafi, wala rushwa na wababaishaji, lakini walikuja kukiri kuwa sisi ni watu makini na wakatufutia nusu ya madeni yetu yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni tatu katika kipindi cha miaka 20.
Rais Mkapa aliwasili New York juzi kwa ajili ya kuhudhuria mkutano mkuu wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa.
Hafla hiyo ya Rais kuagana na Watanzania, pia ilihudhuriwa na Mama Anna Mkapa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete ambaye pia alitambulishwa na Rais kama Rais Mtarajiwa na pia alishiriki katika kujibu baadhi ya maswali kutoka kwa Watanzaia hao.
Aidha, katika msafara huo wamo pia Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk. Abdulkadir Shareef, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Umaskini) Edgar Maokola- Majogo,Katibu Mkuu Ofisi Rais (Mipango na Ubinafsishaji), Enos Bukuku.
Darasa la Saba nchini wafanya mtihani leo
Kidato cha Pili Visiwani nao wafanya mitihani
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai amesema kuwa jumla ya wanafunzi 502,152 wa darasa la saba nchini kote wanafanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi leo, ambao utachukua siku mbili.
Hotuba ya Waziri Mungai aliyoitoa jana usiku na nakala ya hotuba yake kutumwa kwa vyombo vya habari ilisema idadi hiyo inajumuisha wasichana 243,927 sawa na asilimia 49 na wavulana 258,225 ambao ni sawa na asilimia 51.
Alisema watahainiwa wa mwaka huu walianza darasa la kwanza mwaka 1999 wakiwa 737,564, na kwamba idadi yao ilipungua hadi kufikia wanafunzi 235,412 sawa na asilimia 32 kutokana na sababu mbalimbali.
Habari kutoka Zanzibar zinasema kwamba, mitihani ya kitaifa ya kidato cha pili na darasa la saba imeanza Unguja na Pemba chini ya ulinzi mkali.
Vikosi vya Ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar viliimarisha ulinzi katika shule zote ambazo wanafunzi wamekuwa wakifanya mitihani yao.
Ofisa mmoja wa Wizara ya Elimu,Utamaduni na Michezo ambaye hakupenda kutajwa kwa jina, alikiri kuimarishwa kwa ulinzi katika shule zote ambazo wanafunzi wamekuwa wakifanya mitihani ya kitaifa kwa lengo la kudhibiti vitendo vyote vya wizi wa mitihani.
Ulinzi umeonekana kuimarishwa zaidi katika shule za sekondari za Haille Selasie, Forodhani pamoja na Vikokotoni ambapo hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingia katika eneo hilo.
Aidha, walinzi katika maeneo hayo walionekana kuanzia sehemu za ndani hadi nje ya shule hizo ambapo katika kipindi hiki shule zote za serikali zimefungwa ili kutoa nafasi ya utulivu kwa
wanafunzi hao kufanya mitihani yao.
Katika mitihani ya mwaka jana jumla ya wanafunzi 56 walifutiwa matokeo yao ya Wizara ya Elimu,utamaduni na michezo baada ya kuhusishwa na vitendo vya udanganyifu ambavyo huathiri sana uwezo wa wanafunzi katika masomo yao.
Jumla ya wanafunzi 37,031 wa kidato cha pili na darasa la saba wanafanya mitihani yao muhimu Tanzania ambapo kwa upande wa kidato cha pili watakaofanikiwa wataendelea na masomo yao ya kidato cha tatu na wale watakaoshindwa watalazimika kununuwa mitihani ya kidato cha nne, kwani hadi sasa mwisho wa elimu ya lazima kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kidato cha pili.
Dk. Sheni asisitiza haja ya serikali mbili kwa Watanzania
Wanazungumzia serikali hawaitakii nchi mema
Na Ramadhani Mkoma, Tandahimba
MGOMBEA Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Sheni, amesema Muungano wa serikali mbili ndio sahihi na Watanzania wanaowaza serikali tatu hawaitakii mema nchi.
Dk. Sheni aliyepokewa kwa shangwe mjini hapa juzi jioni, alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika kijiji cha Kitangali wilayani Newala na kuhudhuriwa na mamia ya watu.
Aliwashangaa wanaowaza kuelekea serikali tatu na kusema hata dunia mwelekeo wake ni katika kuungana zaidi.
Mgombea huyo Mwenza ambaye pia ni Makamu wa Rais, alisema Watanzania wajifunze adha na balaa la mgawanyiko kwa kutoa mfano wa baadhi ya nchi ambazo hazina serikali kwa miaka 13 sasa.
Ziara hiyo pia iliendana na kumbo dhidi ya kambi ya upinzani ambapo jumla ya wanachama 398 kutoka kambi ya upinzani walivihama vyama vyao na kujiunga na CCM. Waliojiunga kutoka Newala walikuwa 215. Vyama vilivyopata pigo hilo ni UPDP, CUF, TLP, na NCCR Mageuzi.
Katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Chakawa, Dk. Sheni aliwataka wananchi kuichagua CCM akiifananisha na jungu kuu linalopika wali mzuri na kufanya watu wamshagilie.
Katika safari yake hiyo, alifuatana na wagombea ubunge wote akiwemo Kapteni (Mstaafu) George Mkuchika (Newala), Dustan Mkapa (Nanyumbu), Raynald Mrope (Masasi) na Selemani Kumchaya (Lulindi).
Dk. Sheni, alieleza kwa kina mafanikio ya CCM mkoani Mtwara kuwa ni pamoja na kuwezesha kuchangia pato la taifa, kwa asilimia 3.8 na nguvu kazi yao imetoa mchango wa sh. bilioni 3.9.
Mchango mwingine kwa mujibu wa Dk. Sheni ni ongezeko la uzalishaji wa mazao ya uvuvi kutoka tani 49,107 mwaka 2003 hadi 51,214 za sasa. Korosho zilizovunwa zimefikia tani 51,214 mwaka juzi kutoka 49,107 wastani wa awali.
Aidha, kwa upande wa elimu kitaifa alisema wanafunzi wa kike wanaoijunga na vyuo vikuu waliongezeka kutoka 5,513 mwaka 2000 hadi 11,782, ada ya shule za msingi kufutwa na kwa sekondari za umma kupunguzwa kwa asilimia 50.
Kwa upande mwingine, alisema huduma za afya na chanjo kwa watoto ziliboreka kufikia asilimia 90 kutoka 30. Alisema yote hayo ni kutokana na mafanikio ya sera bora za CCM.
Juzi jioni alipowasili mjini Tandahimba, Dk. Sheni alikuwa kivutio cha pekee kutokana na watu kujaa barabarani kuanzia vijijini alikopita katika mikutano ya kampeni, ili wamsalimie au walau wamuone hata pale usiku ulipoingia.
Dk. Sheni, alikuwa akiwasili akitokea wilaya za Masasi na Newala, ambapo alicheleweshwa na wananchi mbalimbali waliosimamisha msafara wake kumsabahi na walimshangilia kwa vifijo ikiwa ni ishara ya kukubalika kwa CCM.
Miongoni mwa vijiji alikokuwa akisimamishwa na wananchi ni pamoja na Nambunga, Chihanga na Kitangali.
Ngawaiya awaambia wananchi wasipoteze muda kwa upinzani
Na Mwandishi Wetu, Korogwe
ALIYEKUWA Mbunge wa TLP, jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, Thomas Ngawaiya amewataka wananchi wa Korogwe wasipoteze muda kuwachagua wapinzani kwa sababu hawana uwezo wa kuongoza.
Ngawaiya ambaye alihama TLP na kujiunga CCM mwezi uliopita, tangu wakati huo amekuwa akisaidiana na viongozi wa CCM kuwanadi wagonbea katika mikutano ya kampeni zinazoendelea.
Kauli hiyo aliitoa juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge Korogwe Mjini, Joel Bendera kwa tiketi ya CCM.
Alisema wapinzani hawana uwezo wa kushinda katika uchaguzi mkuu ujao na kwamba endapo wananchi watawachagua wapinzani watapoteza muda wao na kuzorotesha maendeleo na kwamba hata wenyeviti wa serikali za mitaa karibu asilimia 85 ni CCM.
Ngawaiya alieleza matumaini yake kwamba zaidi ya asilimia 85 ya wabunge wote katika uchaguzi ujao watatoka katika CCM, na kwamba hata wananchi wakichagua wapinzani hawatakuwa na uwezo wa kuunda serikali kwa kuwa watakuwa na wabunge wachache.
Alisema kutokana na ukweli kwamba asilimia kubwa ya wenyeviti wa serikali za vijiji ni wa CCM, hiyo ni dalili tosha kwamba serikali ijayo itakuwa ni ya CCM.
Mbunge huyo wa zamani kwa tiketi ya chama cha upinzani alikiri kuwa kutokana na kambi ya upinzani kutokuwa na nguvu bungeni, wapinzani wamekuwa wakishindwa kujenga hoja na kupewa uzito unaostaili.
Alisema kuwa yeye amewahi kuwa mbunge wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya TLP, lakini hoja za wapinzani zimekuwa zikishindwa kutekelezeka kutokana na kukosa kuungwa mkono na wabunge wa CCM na hivyo wapiga kura wao kukosa huduma muhimu.
Ngawaiya alisema baadhi ya viongozi wa kambi ya upinzani wanataka kujaribu tena huku wakijua wazi hawataweza kushika madaraka ya nchi.
Alitoa mfano kwamba nchini Kenya vyama vya upinzani viliungana na kufanikiwa kuchukua madaraka ya nchi, lakini hivi sasa kila kukicha ni matatizo matupu na migogoro isiyomalizika.
Ngawaiya alisema vyama vingine havina wanachama hata 1000, lakini ndio hao wanaodai kuwa wakishinda nchi itakuwa na mabadiliko wakati wakijua wazi hawana uwezo wa kuunda serikali.
Ngawaiya akimzungumzia mgombea huyo, alisema Bendera ni mbunge mzoefu na amejitahidi kuleta maendeleo ya wananchi wa Korogwe ikiwa ni pamoja na kufanikisha wananchi kurejeshewa hekta zaidi ya 4000 na serikali ili waweze kuendesha shughuli zao za kilimo.
Alisema wananchi wa wilaya ya Korogwe hivi sasa wanapata maji safi na salama ya kunywa, barabara zimekuwa nzuri na huduma nyingine za kijamii zimeboreshwa.
TAMWA yaomba wagombea kuepuka lugha za kashfa
Hasa kwa wanawake wanaogombea nafasi za urais, ubunge na udiwani
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewaomba watu wote wanaogombea kuhakikisha kuwa wanaepuka kutumia lugha za kuwakashifu na kuwadhalilisha wanawake wanaogombea nafasi za udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi mkuu.
Taarifa iliyotolewa na TAMWA jana ilisema kampeni zinazozaa uchaguzi huru na unaozingatia demokrasia ya kweli na kwamba wanawake na wanaume wana haki ya kuwa viongozi kamwe hazitumii lugha zinazochochea udhalilishaji wa mtu kutokana na maumbile yake, bali huchochea mijadala juu ya masuala yanayogusa maisha ya wananchi walio wengi.
“Tunawaomba Watanzania wawapime wagombea wote wanawake na wanaume kwa hoja watakazozitoa ili kuona nani anafaa kuchaguliwa kuwa kiongozi kutokana na hoja anazozitoa kama zinalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kujiletea maendeleo yao,” ilisema taarifa.
Aidha, taarifa imewaomba wananchi kuwa macho na kuwapuuza wale wote wanaotoa lugha za kuwachafulia wanawake wanaogombea nafasi za ubunge udiwani na Urais.
TAMWA imesema inaamini kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki na wenye kuleta viongozi wazuri wa kuendeleza taifa endapo wagombea wote na mashabiki wao watajiepusha kutumia vitisho na lugha zinazolenga kuwakatisha tamaa, kuwabeza na kuwadhalilisha wanawake.
“Tungependa pia kuwahakikishia Watanzania wote kuwa TAMWA haifungamani na chama chochote cha siasa, bali inahamasisha na kuwatia shime wanawake wa vyama vyote wanaogombea katika uchaguzi mwaka huu ili waweze kufanya kampeni zao kikamilifu na bila bughudha,” imesisitiza taarifa.
Matanki ya maji Mwanza kujengwa karibuni
Na Peter Katulanda, Mwanza
CHAMA Cha Mapinduzi kimesema ujenzi wa matanki na chujio la maji la kisasa jijini hapa ni moja ya miradi itakayokamilishwa na Serikali ya awamu ya nne iwapo CCM itachaguliwa tena kushika dola.
Mradi huo utawawezesha wakazi wa jiji la Mwanza na vitongoji vyake vyenye uhaba wa maji kupata maji safi na salama.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambaye pia ni Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo Edward Lowassa alitoa ahadi hiyo juzi alipozindua rasmi kampeni za CCM Wilaya ya Nyamagana kwenye uwanja wa shule ya msingi Mirongo.
Lowassa alisema CCM ndiyo Chama pekee kinachoweza kuwavusha wananchi kutoka kwenye hatua moja kwenda nyingine kubwa zaidi kwani kimeishakaa Ikulu kinajua jinsi ya kuwasaidia.
Alisema CCM inaomba tena ridhaa ya kuchaguliwa kwa sababu Ilani yake inatekelezeka na kuiwezesha nchi kuwa tulivu yenye mshikamano, amani, maendeleo na kusifika hadi nje kwa demokrasia nzuri.
"Nimekuja kwa furaha sana kwani wana Mwanza mmeona tuliyofanya awamu ya tatu, tutafanya makubwa zaidi awamu ya nne tupeni kura zote," alieleza Waziri huyo na kuongeza: "Mpeni kura zote Kikwete awe Rais, mpeni kura Masha awe mbunge wa
Nyamagana, wapeni na madiwani mzidi kujipatia maendeleo."
Akieleza mradi huo wa ujenzi wa matanki alisema Tanzania imepata mkopo wa sh. bilioni 54 kutoka Umoja wa Ulaya kwa ajili ya ujenzi wa matanki hayo katika milima ya Nyashana, Nyasaka, Bugarika, Capripoint na Ibanda Mkolani ambalo kila moja itakuwa na ujazo wa lita 27,000.
Kazi nyingine katika mradi huo ni kuweka chujio la maji la kisasa,
kujenga magati 167 ya jamii katika maeneo mbalimbali ambayo wananchi watapata maji kwa bei nafuu na kufanya matengenezo ya mashine ya maji ya Capripoint au kuweka mpya.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Nyamagana kwa tiketi ya CCM Lawrance Masha alisema wana CCM na wananchi kwa ujumla watumie haki yao ya kupiga kura kwa kuichagua CCM kwani ndicho chama pekee kitakacho waletea maendeleo.
Alieleza kwamba endapo watachagua wagombea wa vyama vya upinzani watabaki bila maendeleo na alitolea mfano Kata ya Mirongo iliyokuwa na diwani wa CUF ambayo imekosa Sekondari ya kata wakati kila kata imejenga sekondari yake.
"Wapinzani wanachonga sana juu yangu eti sijui Kiswahili kwa kuwa nimesoma Marekani. Huo ni wivu, nipeni kura niwe mbunge wenu tushirikiane kuleta maendeleo kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya," alisema Masha huku akishangiliwa na umati ulioudhuria.
Pia katika mkutano huo Lowassa aliwanadi Anthony Diallo mgombea ubunge wa jimbo la Ilemela, madiwani wa kata 12 na wagombea wa Viti Maalum.
Msumbiji yausifu mfumo wa muundo wa serikali za mitaa
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Msumbiji imeusifu mfumo na muundo wa serikali za mitaa nchini, kuwa unatoa fursa ya demokrasia kwa wananchi wa chini kuwa na sauti pia kunufaika kisiasa.
Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa Nchi hiyo anayeshughulikia Serikali za Mitaa na Utawala wa Umma, Lucas Chonera, katika ziara ya kujifunza nchini kuhusu mabadiliko yanayoendelea nchini katika mfumo wa serikali za mitaa na utumishi wa umma, akiongoza ujumbe wa watu wanane.
Chonera, alisema hayo baada ya kupata maelezo ya kina kutoka kwa wataalamu wanaoshughulikia mradi wa mabadiliko katika mfumo wa serikali ya Tanzania, ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Deotrophes Mmari.
Kwa mujibu wa Waziri Chonera, ziara hiyo ni ya kujifunza kutokana na nchi hiyo nayo kuwa katika mabadiliko kama hayo.
Miongoni mwa waliyoelezwa ni pamoja na jinsi serikali za mitaa ambazo ziliingia katika mabadiliko mwaka 1996 kunuia kufanya mabadiliko, hasa katika maeneo makuu, ambayo ni pamoja na utawala, ubora wa nguvu kazi na matumizi ya fedha.
Meneja wa mradi wa mabadiliko ya serikali za mitaa, Alfred Kabagile, alisema jana kuwa tayari mabadiliko hayo ambayo yako katika awamu ya pili, pia yanaangalia katika namna ya kuwepo kwa mabadiliko ya katiba yatakayoipa serikali hizo za mitaa nguvu zaidi.
Alisema moja ya maeneo ya udhaifu bado ni kwanba, serikali hizo za mitaa kwa kupitia halmashauri zinamudu kuchangia asilimia 10 tu ya bajeti zake. Mpango wa mabadiliko hayo yanatarajiwa kukamilika mwaka 2008.
Naye Meneja mradi wa maboresho ya serikali za mitaa nchini, Cosmas Takule, alisema katika mwaka ujao wa fedha jumla ya dola za Marekani milioni 24 ambayo ni sawa na zaidi ya sh. billion 26 na hadi kumalizika kwa mradi itagharimu zaidi ya sh sh. bilioni 65.
Waziri Chonera, alisema kutokana na mafunzo aliyoyapata nchini, kuwa umefika wakati kwa viongozi wa nchi za Kiafrika kubuni utaratibu wa kujifunza kutoka miongoni mwao badala ya kukimbilia Ulaya.
Ujumbe huo ambao uko nchini tangu juzi leo unatarajiwa kutembelea Ofisi ya Rais Utawala Bora na kupata mafunzo zaidi kuhusu maboresho yanayoendelea katika sekta ya utumishi wa umma, baada ya kupata maelezo ya kina katika mfumo wa serikali za mitaa.