UHURU 15.09.2005

 

MAGUFULI AWAAMBIA WANANCHI JIMBO LA TEMEKE:

Kinamama wahimizwa kuhakikisha wagombea wanawake wanashinda

Serikali kujenga miundombinu ya reli mikoa ya Kusini - Sheni

Serikali imepania kuona mtumishi anastaafu akiwa na nyumba

John Komba aipa salamu CHADEMA Kigoma

CUF yageuzia kampeni zake katika makanisa

CCM yapinga uchokozi wa mgombea wa CUF Kilombero

Kagasheki aahidi kufungua kituo cha redio, gazeti

Tanzania kufikia malengo ya  pili ya milenia mwakani - Mkapa

Mwanga mpya wa maendeleo Kigoma Mjini

 

 

MAGUFULI AWAAMBIA WANANCHI JIMBO LA TEMEKE:

Na Mwandishi Wetu

WANANCHI wa majimbo ya wilaya ya Temeke wametakiwa kuwachagua wabunge na madiwani wa CCM ili serikali ikamilishe ujenzi wa barabara katika majimbo hayo.

Waziri wa Ujenzi, John Magufuli alisema hayo juzi jioni katika mkutano wa kampeni ya kuomba wananchi wawachague wagombea wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao. Majimbo ya uchaguzi wilayani humo ni Temeke na Kigamboni.

Magufuli alisema wabunge na madiwani wa upinzani nchini wamekuwa hawajui kushirikiana na serikali katika masuala ya maendeleo na hivyo kusababisha maeneo yao mengi kukabiliwa na matatizo ya maji, elimu na hata barabara kuliko maeneo mengine nchini.

Mkutano huo wa kampeni ulifanyika kwenye uwanja wa ‘Mbonde yangu Macho’ Tandika mjini Dar es Salaam, ambapo alikuwa akiwanadi mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, Ubunge wa jimbo la Temeke, Abbas Mtemvu na mgombea Udiwani kata ya Tandika, Zena Mgaya.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Mattson Chizi na Katibu wa Umoja wa Vijana Mkoa,  Mussa Matoroka.

Magufuli alisema wilaya ya Temeke inakabiliwa na ubovu wa barabara kwa kipindi kirefu kwa sababu ya migongano ya mawazo kutoka kwa wabunge na madiwani wa upinzani.

Kipindi kilichopita Mbunge wa jimbo la Temeke alikuwa Khadija Kusaga wa CCM, lakini jimbo la Kigamboni alikuwa Frank Magoba wa CUF ambaye baada ya kutambua kasoro aliamua kurudi CCM mwaka huu.

“Wilaya ya Temeke yenye majimbo mawili haijaungana, inagawanyikagawanyika kisiasa, kwani jimbo moja linakwenda upinzani na kata zingine zinakwenda upinzani na kusababisha mivutano ya maendeleo,” alisema na kuwaomba wananchi wa Temeke kuwachagua wagombea wote wa CCM ili serikali itekeleze majukumu yake.

Alisema serikali ya CCM, mwaka huu, kwa nia nzuri, imetenga sh. bilioni 2.4 ili kukarabati barabara za mkoa wa Dar es salaam zikiwemo za wilaya ya Temeke, lakini wilaya hiyo inaweza kukosa ikiwa wananchi wataendelea kuchanganya CCM na wapinzani, kwani kazi ya wapinzani ni kupinga maendeleo.

Kufuatia kauli hiyo, vijana wengi waliofurika waliahidi kuwachagua wabunge, madiwani na Rais kupitia CCM jambo ambalo naye Magufuli aliamua kuahidi kwamba Wizara yake itatoa sh. milioni 100 kwa ajili ya kuongezea ukarabati wa barabara za wilaya hiyo peke yake ikiwa watatekeleza mambo hayo.

Waziri aliwafurahisha zaidi wananchi waliofurika alipowaeleza CCM inaahidi kwamba ikipata madaraka itajenga daraja la Kigamboni, kwani tayari mipango imekamilika na kwamba kampuni nne za China zimechukua michoro ya daraja hilo ili kutathimini tayari kwa kuanza ujenzi.

Daraja hilo litagharimu zaidi ya sh. bilioni 30 ambazo alisema zipo tayari kwa kazi hiyo.

“Daraja hilo litakuwa na njia nne, njia ya baiskeli na ile ya wapita kwa miguu,” alisema na kuongeza kwamba litakuwa na urefu wa mita 600.

Alisema kama wananchi wa Temeke watawachagua wagombea wote wa CCM, serikali pia kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM itakamilisha ujenzi wa barabara ya Kilwa kwa gharama ya sh. bilioni 16 katika kipindi chake cha miaka mitano ijayo.

Waziri Magufuli ambaye amepita bila kupingwa kwenye jimbo la Biharamulo Mashariki aliwataka wakazi wa wilaya ya Temeke kuwachagua wagombea wote wa CCM ili kuondoa kasoro zilizojitokeza kipindi kirefu na kwamba kinachotakiwa ni kuwachagua wagombea wote wa ubunge na madiwani kupitia CCM.

Naye mgombea udiwani wa kata ya Tandika kupitia CCM, Zena aliwataka wasiwachague wagombea kupitia upinzani ili kuondokana na uongo uliokithiri.

Alisema mgombea wa udiwani kupitia CUF, Saleh Msoka amewadanganya wananchi wa Temeke kwamba akipata udiwani ataweka taa za umeme kwenye barabara zote za Tandika jambo ambalo ni uongo.

“Maendeleo ya kata ya Tandika yalisimama kutokana na kiongozi wetu, diwani kupitia CUF ambaye hakutaka kuwa na ushirikiano wala hakushiriki kazi za maendeleo, na mpaka sasa hajaanza kampeni, bali anazungumza na waandishi wa habari wa gazeti la Alasiri kwamba ataweka umeme barabara zote,” alisema huku akionyesha gazeti lililoandika kauli hiyo.

Naye Mgombea Ubunge jimbo la Temeke, Mtemvu aliwataka wakazi wa Temeke kuacha kurukia basi wasilolijua linakwenda wapi kwa kumchagua Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye mkoani kwake wote walimkataa kwa kukinyima chama chake ubunge hata udiwani.

Wakati huo huo, Waziri Magufuli alisema juzi hiyo kwamba serikali imeamua kujenga daraja jipya kwenye Mto Ruvu ili kuondokana na kero inayotokana na daraja la sasa ambalo ni dogo.

Akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka mipango ya serikali kujenga daraja hilo, Magufuli alisema  tayari sh. bilioni 3.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na kwamba hivi sasa michoro ipo tayari.

Alisema tenda itaitishwa wakati wowote kujenga daraja hilo ili kuondokana na kero.

“Ukarabati unaoendelea sasa katika daraja hilo unalenga kuliimarisha tu lililopo, lakini ujenzi wa daraja jipya utafanyika,” alisema.

Nitaendeleza ujenzi wa makaazi ya wananchi - Karume

Na Khatib Suleiman, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar Amani Abeid Karume amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea na kazi za ujenzi wa nyumba za kisasa kwa ajili ya makazi ya wananchi wake ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kushiriki katika kazi za uwekaji wa zege katika nyumba za Michenzani Jengo la Mwisho, alisema kwamba suala la makazi ni muhimu kwa mwananchi yeyote hivyo serikali yake itaendelea  kulipa kipaumbele.

“Ujenzi wa nyumba za Michenzani unafanywa kwa kutumia nguvu za wananchi na misaada kamwe iwe ni nguvu za ziada tu,” alisema Karume ambapo ujenzi wa Nyumba za Michenzani kwa sasa upo katika hatua za mwisho kumalizika.

Karume alisema mara baada ya kumalizika kwa ujenzi wa jengo hilo unaotazamiwa kukamilika mwakani, shughuli za kazi za ujenzi zitaendelea katika majengo ya nyumba za maendeleo huko Mpapa, ambazo kwa muda mrefu zimeachwa bila ya kushughulikiwa.

Kwa sasa ujenzi wa nyumba za Michenzani unafanywa kwa kutumia mafundi na wataalamu wa Idara ya Majenzi wakishirikiana na wapiganaji wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo Valantia, Mafunzo, pamoja na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na KMKM.

 

Nyumba za maendeleo za Michenzani pamoja na nyumba kama hizo ziliopo vijijini Unguja na Pemba zilianzishwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume kwa ajili ya wananchi wazalendo kupata makaazi bora ya kisasa kama inavyosema Ilani ya Chama kilichoongoza Mapinduzi ASP.

ASP katika Ilani yake iliyopitishwa mwaka 1958 ilisema kama  kitafanikiwa kushika hatamu ya kuongoza nchi, basi kitajenga nyumba za kisasa za maendeleo kwa ajili ya wananchi wake waweze kuishi katika makaazi bora ya kisasa na kuachana nyumba za vibiriti.

Hata hivyo, ujenzi wa nyumba hizo mara baada ya kufariki kwa hayati Abeid Amaan Karume mwaka 1972, ujenzi wake ulisimama  na baadhi ya majengo yaliyoachwa kugeuka magofu ya kujificha wahalifu wakiwemo wezi katika mitaa ya jirani.

Rais Karume alipoingia madarakani alitoa ahadi ya kuhakikisha  anamaliza ujenzi wa nyumba hizo na wale waliovunjiwa nyumba zao katika maeneo hayo waweze kupata makaazi kwa kufidiwa nyumba zao kama alivyotoa ahadi zake hayati Abeid Karume wakati wa ujenzi wa nyumba hizo.

Wakati huo huo, Rais Karume amesisitiza kwamba wananchi waliokodishwa nyumba za maendeleo hawaruhusiwi kukodisha wala kuziuza kwa watu wengine.

Alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari mara tu baada ya kushiriki katika kazi ya ujenzi wa taifa hapo Michenzani, mjini Unguja.

Alisema si jambo la busara na kinyume na mkataba wa makabidhiano kati ya aliyekodishwa na mkodishaji ambaye ni serikali kwa mtu aliyekodi nyumba hizo kuchukua maamuzi yake binafsi ya kuuza nyumba hizo za maendeleo bila idhini ya Serikali.

 

Kinamama wahimizwa kuhakikisha wagombea wanawake wanashinda

Na Omari Shaaban, Arusha

WANAWAKE wametakiwa kuhakikisha wanawake wenzao waliogombea kwenye nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba wanashinda nafasi zao.

Akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa Chama cha Mapinduzi, mjini hapa, mke wa mgombea urais kupitia CCM, Salma Kikwete alisema wanawake wapewe kipaumbele kwa kuwa ndiyo muhimili wa familia na nchi.

Alisema kuwa mwanamke ni muhimili mkubwa katika familia na ndiye msimamizi wa shughuli zote za nyumba, kwa hiyo anastahili kuongoza na kuwa na madaraka ya kiutawala na uongozi ili mafanikio na maendeleo ya nchi yapatikana kwa haraka.

Mama Kikwete aliwataka wanawake, kuvunja makundi yao yaliyojitokeza wakati wa mchakato wa kampeni za kura za maoni, na wakati wa kugombea nafasi mbalimbali katika chama ili wahakikishe ushindi wa kishindo kwa CCM unapatikana.

"Sote tunajua CCM, itashinda... lakini ushindi tu hautoshi, tunataka kushinda kwa kishindo kikubwa ili iwe fundisho kwa wapinzani ambao hawana sera za maendeleo," alisema Mama Kikwete.

Aidha, katika mkutano huo ambao aliufanya kwenye wilaya za Arusha na Arumeru, alisema kila mwana-CCM analo jukumu kubwa la kuhakikisha wagombea wote wa CCM, wanashinda kwenye uchaguzi bila ya kujali tofauti zilizopo.

Katika mkutano huo Mama Kikwete alitumia fursa hiyo pia kuwanadi mgombea Urais wa CCM, Jakaya Kikwete, wabunge wa Arumeru na Arusha Mjini.

Mama Salma jana alimaliza ziara yake ya siku mbili mkoani Arusha, ambayo ilikuwa na lengo la kuwahamasisha kinamama kuhakikisha kuwa CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

 

 

Serikali kujenga miundombinu ya reli mikoa ya Kusini - Sheni

Na Ramadhani Mkoma, Mtwara

MGOMBEA Mwenza wa kiti cha Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohammed Sheni, amesema iwapo Chama kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, kimenuia kujenga miundombinu ya reli, ikiwemo katika mikoa ya Kusini ya Mtwara na Ruvuma.

Katika mikutano ya hadhara iliyofanyika juzi wilayani Tandahimba na jioni mjini Mtwara, Dk. Sheni alisema kuwa mikakati hiyo iliyoanishwa katika Ilani ya uchaguzi, reli hiyo inalenga kuunganisha bandari za Mtwara na mji wa Songea, hadi bandari ya Mbambabay, pwani ya Ziwa Nyasa.

Alisema, ujenzi wa reli pia utahusisha miji ya Arusha itayaounganishwa na Musoma, Isaka hadi Kigali Rwanda. Kwa mujibu wa Dk. Sheni, lengo hilo ni kuboresha miundombinu ya usafiri nchini.

Mgombea mwenza huyo na Makamu wa Kwanza wa Rais alisema pia kwamba mkakati huo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo katika maeneo ya ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Uboreshaji wa bandari ya Kigoma nao upo katika mkakati huo.

Dk. Sheni, alitaja juhudi nyingine za kitaifa zitakazokuwa na manufaa makubwa kati ya nchi hizo mbili ni ujenzi wa daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji kupitia mkoani Mtwara.

Alisema, serikali ya CCM kupitia ilani yake ya uchaguzi ambapo si kipindi kirefu wananchi wanatarajia kupata umeme wa gesi, kutoka mradi wa Mnazi Bay mkoani humo.

Sambamba na hiyo, alisema katika kuwa serikali yake inalenga katika kuleta maji yatakayohudumia wananchi wa mkoani hapa, kwa kiwango cha asilimia 90 kwa wananchi wa mjini na asilimia 65 ya wale wa vijijini. Alitaja vyanzo vitakavyotoa maji hayo ni Mahuta, Namkunya na Kitangara vyote vya mkoani hapa.

Katika mkutano wa mjini haoa uliyofanyika katika eneo la Mikindani, uliohudhuriwa na umati wa watu, aliwanadi mgombea ubunge wa Mtwara Mjini, Mohamed Sinani, na diwani wa mjini hapa, Selemani Mtakila jumla ya wanachama wapya 120 walijiunga na CCM na wanawe kutoka vyama vya upinzani.

Aliviponda vyama vya upinzani kwa kuzunguka kunadi sera hewa azizosema zina kauli za ‘nita’ na ‘tuta’ tofauti na CCM inayotangaza ahadi za wazi na mifano hai. Alisema kwa ulaghai huo umewaweka hadharani kuwa watu waliokosa uzalendo.

Jana, Dk. Sheni alitarajiwa kuanza ziara mkoani Ruvuma kuendelea na kampeni zake kwa ajili ya kuinadi CCM katika uchaguzi mkuu ujao. 

 

 

Magufuli: Serikali imepania kuona mtumishi anastaafu akiwa na nyumba

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli amesema serikali imepania kuona kila mtumishi anastaafu akiwa na nyumba aliyonunua kipindi cha kazi.

Alisema wapinzani wanapinga kuwauzia nyumba watumishi wa serikali kwa sababu wanataka wastaafu bila ya kuwa na nyumba ya kuishi.

Magufuli alitoa ufafanuzi huo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa 'Mbonde yangu macho' wilayani Temeke ambapo alikuwa akiwaomba wananchi kuwapigia kura za ndio wagombea wote wa CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.

Alisema mpango huo hauathiri utendaji wa serikali, bali unawanufaisha wafanyakazi na kwamba serikali imepania kuona kila mfanyakazi anastaafu akiwa na nyumba aliyonunua kipindi cha kazi.

“Wakati serikali ilipopata uhuru ilikuwa na nyumba 6,000 nchini kote ambazo zilijengwa na wakoloni na nyumba hizo ziliendelea kudumu na kuisababishia serikali itenge fedha kila mwaka za kukarabati,” alisema.

Alisema kufuatia matatizo hayo, serikali iliwahi kuunda tume mara tatu ili kutafuta mbinu za kuondokana na suala la kutenga fedha za kukarabati nyumba zake za zamani bila kujenga mpya.

“Suluhisho limepatikana kipindi cha Rais Benjamin Mkapa ambaye ameongoza vizuri serikali ya CCM na kubuni mtindo wa kuwauzia wafanyakazi wakati serikali inaendelea kujenga nyingine,” alisema.

Magufuli alisema pamoja na kuuza nyumba hizo, serikali pia imejenga nyumba zingine 12,000 ambazo zinaendelea kuuzwa na kwamba mwaka huu imepanga kujenga nyumba zingine 600.

Alisema serikali pia kwa sasa inajenga nyumba nne kila mkoa ambazo pamoja na kwamba wataishi wafanyakazi wake, lengo ni kuwauzia ili kujenga nyingine.

Aliwataka wapinzani wakosoe kasoro zinazotokana na utekelezaji na wala siyo kukosoa mpango wa kuwauzia wafanyakazi, kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kutaka wabaki na umaskini daima.

Katika kipindi cha kampeni baadhi ya wagombea wa Urais wakiwemo Freeman Mbowe wa CHADEMA na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF wamekuwa wakiahidi kuwanyang'anya nyumba watumishi wa serikali waliouziwa.

 

 

John Komba aipa salamu CHADEMA Kigoma

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

MKURUGENZI wa kikundi cha uhamasishaji cha TOT, Kapteni John Komba juzi aliuteka mkutano wa mgombea ubunge wa CCM na kusababisha hotuba iliyokuwa ikitolewa na mgombea

huyo kusimama kwa karibu dakika 10.

Hali hiyo ilifuatia kiongozi huyo kulakiwa kwa shangwe nderemo na vifijo na wana-CCM mara baada ya kuingia

kwenye eneo ulipokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni wa kumnadai mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini

Peter Serukamba uliokuwa ukifanyika eneo la Kidarajani Mwanga mjini kigoma.

Kiongozi huyo mara baada ya kuteremka kwenye gari la mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Azim Premji alijikuta

akibebwa juu juu na wana-CCM waliohudhuria mkutano huo huku wakiimba nyimbo za hamasa za TOT bila kujali umbo

kubwa la kiongozi huyo.

Kapteni Komba aliwasili mkoani juzi jioni kwa ndege akitokea Dar es Salaam tayari kwa kumsindikiza

mgombea Urais wa CCM, Jakaya Kikwete anayetarajiwa kuanza ziara ya kampeni mkoani humo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Komba alisema kuwa ametangulia kusafisha njia kwa ajili ya mgombea Urais wa CCM, Kikwete.

Komba alisema kuwa hiyo ni salamu kwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Walid Kabourou kwamba

zama zake zimekwisha na akae chonjo, kwani jimbo hilo linachukuliwa na CCM kwa mwaka huu.

 

 

 

 

 

CUF yageuzia kampeni zake katika makanisa

Na El-hadji Yuusuf, Tabora

CHAMA cha CUF kimeanza kutumia makanisa katika kufanya kampeni za uchaguzi mkuu, ikiwa ni jitihada zake za kuwarubuni Watanzania kuwa chama hicho hakiegemei katika dini ya Kiislamu pekee.

Taarifa zilizopatikana mjini hapa jana zimebaini kuwa chama hicho kinatumia Kanisa la Leedmed Pentekoste la mjini hapa kwa ajili ya kuendeshea kampeni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

Taarifa hizo ambazo zimethibitishwa na Mwinjilisti wa Kanisa hilo, Yassin Ramadhan "Mlokole" ambaye pia ni mgombea wa udiwani kupitia chama hicho, katika kata ya Mbugani, alisema kuwa CUF kutumia kanisa hilo katika kampeni si kosa.

Yassin alisema: “Kanisa hili ni mali yangu, nimelijenga mwenyewe, vifaa kama spika ni mali yangu… hivyo hakuna sababu ya watu kuhoji kuhusu matumizi yake.”

Aliongeza kuwa kanisa ni ukumbi kama zilivyo kumbi nyingine, hivyo kutumiwa na CUF isiwe sababu ya watu kuhubiri kuwa chama hicho kinaendesha sera za kidini.

Alisema kuwa CUF itaendelea kutumia vifaa vya Kanisa ambavyo si dhambi kuvitumia kwa wakati huu, na pia itaendelea kutumia kanisa hilo kwa ajili ya kuendeshea vikao mbalimbali vya chama, alisisitiza Mwinjilisti Ramadhani.

Hivi karibuni wazee na wanachama wa vyama vingine vya siasa vya mjini hapa, walilalamika kuwa kuna baadhi ya vyama vimekuwa vikitumia nyumba za ibada katika kampeni jambo ambalo ni hatari kwa umoja wa kitaifa.

Wazee hao walitoa malalamiko yao, katika ziara ya Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Sheni, alipofanya ziara ya kampeni mjini hapa mwanzoni mwa mwezi huu.

 

 

 

CCM yapinga uchokozi wa mgombea wa CUF Kilombero

Na Igamba Libonge, Kilombero

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kilombero kimelaani tabia ya mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF kuvamia mara kwa mara mikutano ya kampeni ya CCM katika jimbo hilo.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kilombero Luteni Makame Makame alisema mgombea wa CUF katika jimbo hilo Kassim Mtaalam ameanzisha kampeni za fujo kwa kuvamia mikutano ya CCM na kugawa vipeperushi na magazeti ya CUF katika mikutano yao huku akielewa kuwa ratiba haimruhusu.

Makame alisema mgombea huyo alianza fujo zake Septemba 12, mwaka huu kwa kufanya kampeni huku akigawa vipeperushi katika kata ya Idete wakati akielewa siku hiyo eneo hilo alitakiwa azungumze mgombea udiwani CCM na yeye ratiba ilionyesha alipaswa kuzungumza katika kata ya Kibaoni.

Alisema katika kuingilia kampeni hizo, wana-CCM hawakumfanya lolote na usiku wa siku hiyo mgombea huyo alifanya tena kampeni katika kata ya Mchombe wakati kisheria, muda wa usiku hauruhusiwi kufanya kampeni.

Katibu huyo alisema juzi Mtaalam alifanya kampeni katika kata ya Mlimba huku akielewa siku hiyo eneo hilo alitakiwa kufanya kampeni mgombea ubunge wa CCM, Castor Ligallama na yeye alitakiwa kufanya kampeni katika kata ya Kisawasawa.

Makame alibainisha kuwa wao kama CCM hawapendi kuona chama cha CUF kikiendesha kampeni chafu kwa kuingilia kampeni zao kwa kugawa mabango na vipeperushi na kudai kuwa huo ni kama uchokozi na wanachama wakichoka wanaweza kumfanyia fujo mgombea huyo.

Aliomba vyama vyote vya siasa wilayani humo kufuata taratibu zilizopangwa na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kilombero ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kutokea kwa baadhi ya wafuasi wa vyama.

 

 

Kagasheki aahidi kufungua kituo cha redio, gazeti

Na Angela Sebastian, Bukoba

MGOMBEA ubunge katika jimbo la Bukoba mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Khamis Kagasheki amesema endapo atachaguliwa pamoja na mambo mengine ataanzisha Mpango Maalum wa kufungua radio na gazeti la Bukoba ili kuutangaza mkoa wa Kagera, hususani Bukoba mjini.

Kagasheki alisema hayo juzi katika uwanja wa Rwamishenye ulioko mjini Bukoba wakati wa mkutano wa

Kampeni za CCM.

Alisema kuwa vyombo hivyo vya habari vitasaidia kuutangaza mkoa  na kuchapisha habari nyingi

zinazohusu mkoa huo.

Mgombea alisema mkoa huo ni tofauti na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa ambayo ina radio na magazeti

yake ambapo imeweza kusaidia sana kupata taarifa mbali mbali za wakati huo huo.

“Hiyo itasaidia hata waandishi wa mkoa huu kukusanya habari nyingi, kujitegemea katika maisha yao ya baadae

na hivyo kuondokana na umaskini,” alisema.

Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na maelfu ya watu alisema kuwa kama atachaguliwa ataanzisha mpango

maalum ya kuwawekea mazingira mazuri na vijana waendesha baiskeli na pikipiki (Asecdo) ikiwa njia

mojawapo ya kuwasaidia vijana kujiajiri na kuondokana na umaskini.

Alisema kuwa pia atashirikiana na viongozi wengine kutetea makundi yaliyoanzisha miradi au biashara ya

kujipatia kipato mfano vikundi vya kinamama kwa kuwapatia mikopo midogo ya kujiendeleza.

 

 

Tanzania kufikia malengo ya  pili ya milenia mwakani - Mkapa

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa amewaeleza viongozi wa nchi mbalimbali duniani kwamba Serikali ya Tanzania imewekeza katika elimu ambapo sasa inatoa elimu ya msingi bure.

Hayo yamo kwenye hotuba ya Rais Mkapa aliyoitoa jana katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani na nakala ya hotuba yake kupatikana mjini Dar es Salaam.

Alisema hadi kufikia mwakani Tanzania itakuwa imeweza kuyafikia malengo ya pili ya maendeleo ya milenia ikiwa mbele kwa miaka tisa kabla ya muda uliopangwa.

Rais Mkapa alisema hayo alipokuwa akielezea umuhimu wa mataifa makubwa kutimiza ahadi zao za kuzisaidia nchi masikini.

Alisema mataifa yalioendelea lazima yatimize ahadi  ili kuwezesha utekelezaji wa kuboresha maendeleo kwa kutumia misaada hiyo.

Rais Mkapa aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanaishughulikia migogoro inayoibuka katika baadhi ya nchi kabla haijaleta madhara.

Alisema inapoanguka ndege yenye abiria 100 kila mtu anakimbilia kutafuta ufumbuzi wake na kujua chanzo chake lakini viongozi wanasahau kwamba kila siku watoto 30,000 wanakufa kwa njaa.

Rais Mkapa alisema kuwa suala la umasikini limekuwa likipangiwa mikakati kwa miaka mingi na aliwataka viongozi hao kuanza utekelezaji.

Wakati huo huo, Rais Mkapa amesema Umoja wa Mataifa (UN)  umekuwa na msaada mkubwa katika kutatua matatizo ya Ukanda wa Maziwa Makuu.

Rais Mkapa alisema hayo alipokuwa akihutubia Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba kwa kutumia ushirikiano huo ni wajibu kuanisha mambo muhimu ya kuimarisha UN na wajibu wake wa kupambana na ugaidi na  matatizo mengine ya migogoro inayosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

 

 

 

 Mwanga mpya wa maendeleo Kigoma Mjini

Na Dunia Mzobora

MCHAKATO wa wanaowania kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini kote ulimalizika vyema na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wamepatikana.

Ulikuwa mchakato wa kuwapata madiwani, wabunge na wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Kimsingi, ni mchakato ulioendeshwa kwa msingi wa uwazi na demokrasia ya hali ya juu, hali iliyoonyesha kuwa CCM ni chama kikomavu na kinachozingatia matakwa ya wananchi.

Hata hivyo, lengo la makala  hii siyo kujadili namna wagombea wa nafasi mbalimbali walivyopatikana, kwani hilo limekwisha, hasa ikizingatiwa kuwa wana-CCM sasa wako ‘vitani’ kuhakikisha wanashinda katika nafasi hizo na hivyo kushika dola.

Kwa maana hiyo, makala hii inajaribu kuwakumbusha wananchi wa jimbo la Kigoma Mjini kwanini ni muhimu sasa kumchagua mgombea wa jimbo hilo kupitia CCM, Peter Serukamba.

Nikiwa mzaliwa wa mkoa wa Kigoma, ninafahamu kwa mapana na marefu jinsi jiografia ya mji huo, hasa jimbo hilo la Kigoma Mjini ilivyo, watu wake na miundombinu iliyopo.

Kwa kweli Kigoma, na hasa jimbo lenyewe halina eneo kubwa sana kijiografia, ukiachilia mbali vitongoji vyake kadhaa vilivyotapakaa hapa na pale. Kwa maneno mengine ni eneo unaloweza kusema ni la kimjimji hivi.

Ni jimbo linaloundwa na vitongoji mbalimbali kama vile eneo la Kigoma Mjini ambalo lina mchanganyiko wa shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara na ofisi za idara mbalimbali za serikali.

Katika miaka ya nyuma, eneo hilo la Kigoma mjini lilikuwa linakaliwa na wafanyabiashara wa Kiasia, na wananchi wengine wachache, hasa maofisa wa ngazi za juu serikalini.

Aidha, kuna maeneo ya Mwanga, Ujiji, Bangwe, Gungu, Buhanda, Kahabwa na Kibirizi. Na katika maeneo haya ipo pia mitaa kadhaa.

Kwa mfano, maeneo kama Ujiji yana vitongoji kadhaa kama vile Kasingirima, Kitongoni, Buzebazeba, Bogogwa, Majengo, Mnarani; huku Mwanga ikiwa na mitaa kama vile Majengo Mapya, Vamia, Sido n.k.

Vilevile, yapo maeneo mapya yaliyozuka karibuni ambapo kutokana na ongezeko la watu, nyumba nzuri za kuishi zimejengwa, ingawa katika miaka ya nyuma, maeneo hayo yalikuwa mapori yaliyotumika kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Maeneo hayo ni pamoja na Masanga, ambapo zamani kulikuwa na mwamba mkubwa uliokuwa chimbuko la mawe na kokoto za ujenzi, lakini sasa ni mji mkubwa uliojengwa nyumba nzuri na za kisasa za kuishi sambamba na maeneo kama vile Mlole, vilima vya Bangwe n.k.

SIASA ZA VYAMA VINGI

Tanzania kama nchi nyingine nyingi duniani sasa, inaendesha siasa zake chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Huu ni mfumo wa ushindani.

Kimsingi, mfumo huu unashindanisha vyama vingi vya siasa kwa minajili ya kushinda uchaguzi na kisha kuunda serikali. Hapa nchini, mfumo huu ulianzishwa rasmi mwaka 1992.

Lakini tangu kuanzishwa kwa mfumo huu, tayari nchi yetu imekwishafanya uchaguzi mkuu unaoshirikisha vyama vingi mara mbili, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1995 na wa pili mwaka 2000.

Kwenye uchaguzi huo, Chama cha Mapinduzi kiliweza kuibuka na ushindi wa kishindo katika nafasi ya urais, na nafasi za ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa bahati mbaya, jimbo la Kigoma Mjini ni miongoni mwa majimbo machache sana nchini ambayo kwa nyakati tofauti katika vipindi hivyo lilitwaliwa na chama cha upinzani, CHADEMA.

Ushindi wa CHADEMA katika jimbo hilo ulipokewa kwa ‘shangwe’ na ‘vifijo’ kubwa na wakazi wa Kigoma, wengi wakiamini kwamba sasa wananchi watapata maendeleo makubwa… kwamba Kigoma imepata mkombozi, Dk. Amaan Walid Kabourou.

Chambilecho, Waswahili walinena: ‘Usichokijua ni sawa na usiku wa giza’. Sasa wananchi wa jimbo hilo wako gizani… wanatazama, lakini wako katika mwanga hafifu usio na matumaini. Mwanga wa kibatari, koroboi!

VYAMA VINGI NA HUDUMA ZA JAMII

Jambo ambalo wananchi wanapaswa kujifunza ndani ya mfumo wa demokrasia ya siasa za vyama vingi ni kwamba upo uhusiano mkubwa baina ya Chama tawala na usambazaji wa huduma za kijamii katika majimbo.

Katika mfumo huu wa sasa, uchaguzi wa viongozi, hasa rais, wabunge na madiwani unafananishwa na jinsi mwili wa binadamu unavyofanya kazi. Kiungo kimoja kikikatwa, mwili hauwezi kufanya kazi yake barabara.

Vivyo hivyo, wananchi wanapochagua mbunge wa jimbo kutoka chama cha upinzani, kwa maana nyingine wanakuwa wamekata sehemu moja ya kiungo cha mwili, na hivyo mwili kushindwa kufanya kazi ipasavyo. 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete anasema katika kampeni zake kuwa anataka wananchi wachague ‘mafiga matatu’ ili chungu kiweze kukaa vizuri mekoni.

Mkewe, Salma naye anakwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba ni ‘mafiga matatu’ ndiyo yanayoweza kuivisha mboga na watu wakala na kushiba. Hawa ni pamoja na rais, wabunge na madiwani.

HUDUMA ZA JAMII KIGOMA

Oktoba, mwaka jana nilipata safari ya kikazi mkoani Kigoma, ambapo nilikaa kwa takriban wiki mbili hivi. Nilitumwa na mwajiri wangu, Uhuru na Mzalendo kwa kazi maalum.

Katika safari yangu hiyo, nilibahatika kutembelea maeneo mbalimbali ya mji wa Kigoma, pamoja na wilaya ya Kasulu, mji ambao niliutembelea karibu miaka 20 iliyopita, lakini ni miongoni mwa wilaya zinazopiga hatua kubwa kimaendeleo.

Hata hivyo, nikiwa katika shughuli zangu, hasa katika maeneo ya Kigoma mjini na vitongoji vyake nilikuwa nikichunguza baadhi ya mambo na kustaajabu kutokana na jinsi mji  ulivyokuwa ‘umebadilika’.

Kwa maneno rahisi yanayoweza kuuelezea mji wa Kigoma ni kwamba mabadiliko hayo ni kutokana na ‘kuzeeka’. Mji ambao wananchi wake walikuwa hawana matumaini… ukiwaangalia unaona dhahiri walikuwa wamekatishwa tamaa na ahadi za mbunge aliyemaliza muda wake… ahadi za CHADEMA!

Nakumbuka kwa mara ya kwanza wakati mbunge huyo alipoingia madarakani, kama nilivyosema awali, wananchi walimshangilia kwa ‘shangwe’ wakijua kuwa ‘mkombozi’ angeyetoa asali na maziwa amekuja. Walimwona Dk. Kabourou kama Masiha aliyekuja kuwakomboa!

Lakini, bila kutambua kwamba kulikuwa hakuna uhusiano baina ya CHADEMA na serikali iliyopo madarakani, na hivyo kuifanya mambo kuiharibikia Kigoma… hakuna maji, japo Ziwa Tanganyika lipo umbali wa kutupia macho!

Kutokana na CHADEMA kutokuwa na sera za kushirikisha watu katika shughuli za maendeleo, wananchi wa jimbo hilo wamebaki wanalia kwenye kikaango cha moto… walikubali ghilba na hadaa sasa wamehadaika.

Huduma nyingine za kijamii ambazo zilihitaji ushawishi wa mbunge ni pamoja na ujenzi wa shule, usafi wa mazingira, upandaji miti katika maeneo ya wananchi, achilia mbali barabara katika mitaa na masuala ya umeme wa gridi ya Taifa.

Mji wa kihistoria wa Ujiji, umebaki mahame kiasi kwamba hivi sasa, kwa mfano, nyumba ikianguka si rahisi kujengwa tena kutokana na hali ya umasikini iliyowakumba wananchi wake, hali iliyowafanya wengi wao kukimbilia miji mingine.

Kimsingi, wananchi wa jimbo hilo la Kigoma Mjini walikosa kiungo madhubuti cha kuwaunganisha na serikali yao ili kutumia fursa na rasilmali mbalimbali zilizomo mkoani kujiletea maendeleo, hasa ikizingatiwa kuwa Kigoma ni mkoa uliojaa utajiri wa hali ya juu.

MGOMBEA WA CCM PETER SERUKAMBA

Wakati nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu, huku kampeni za wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi zikipamba moto, wananchi wa jimbo la Kigoma Mjini wanapaswa kujiuliza maswali yafuatayo.

             Hivi wamefaidika nini na uwakilishi wa mbunge aliyepita katika kuwaletea maendeleo?

            Alijihusisha vipi katika kuwahamasisha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo, kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo mkoani?

            Nini mchango wa mbunge aliyepita katika kuhimiza shughuli za maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji na barabara katika jimbo hilo?

            Alijihusishaje kuhakikisha kinamama na vijana wanapatiwa mikopo yenye masharti nafuu kutoka taasisi za fedha na serikali?

            Je, ni ahadi zipi alizowaahidi wananchi wa jimbo hilo zilizoweza kutimizwa kwa kipindi chote cha miaka mitano iliyopita?

Kwa jinsi ninavyofahamu, majibu ya maswali hayo yatakuwa kichocheo kikubwa kwa wananchi wa jimbo hilo kuachana na upinzani na kukichagua Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Hiyo ni kwa sababu, mbunge aliyemaliza muda wake hakufanya lolote kuwawezesha wananchi wa jimbo hilo kutumia fursa zilizomo kuwaletea maendeleo, zaidi ya kuanzisha ‘mradi’ wa vijana na wazazi wao kuoga pamoja ‘bichi’ ya Ziwa Tanganyika eneo la Burega kwa kauli mbiu ya ‘Aifola… Aifola’.

Hivyo basi, wananchi wa jimbo hilo wakifunguka macho na kutambua uhusiano uliopo baina ya maendeleo na ‘mafiga matatu’, ni dhahiri kwamba watamchagua Peter Serukamba kuwawakilisha kwenye bunge lijalo.

Na hilo ni jambo lililo wazi iwapo wananchi wataondoa tofauti zao za kiitikadi na kidini, na pia kuumwa na jimbo lao kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo licha ya rasilmali lukuki zilizomo.

Tukichague Chama cha Mapinduzi… tumchague Serukamba kwa maendeleo ya Kigoma Mjini, kwani licha ya kuwa ndiye mwanga mpya wa matumaini, lakini pia ndiye atakayekuwa kiunganishi cha serikali ya Chama tawala na wananchi.

Ni rahisi kwa hoja za Serukamba zinazohusu mchakato wa maendeleo ya wananchi wa jimbo lake bungeni kupewa kipaumbele na serikali, kuliko kama ilivyokuwa kwa mbunge aliyepita.

Hoja za mbunge aliyepita kamwe zisingeweza kutiliwa maanani, kwa sababu kwa kiasi kikubwa zingekuwa zinakinufaisha zaidi chama chake kuliko Chama tawala ambacho, kimsingi, ndicho chenye serikali na huo ndio ukweli wenyewe.

Wananchi wa jimbo la Kigoma mjini kukaa miaka kumi mkishuhudia maendeleo yakiwapita ni jambo la kujiuliza mara mbili mbili, kwani muda huo hausubiri na wala haurudi nyuma, bali unazidi kusonga mbele.

Ni lazima sasa wananchi wabadilike na waone kwamba suala la maendeleo, hasa katika kuimarisha na kuboreshwa kwa huduma muhimu za kijamii ni jambo la lazima.

Hata hivyo, njia mojawapo ya kuhakikisha hayo yanafanikiwa ni kukipa hadhi hiyo Chama cha Mapinduzi, ambacho kimedhamiria bila shaka yoyote kuondoa kadhia hiyo jimboni humo kupitia mgombea wake Serukamba.