UHURU 16.09.2005
CCM Zanzibar yashinda rufani zote za pingamizi
Ziliwekwa na wapinzani kwa wagombea uwakilishi, udiwani
Na Khatib Suleiman, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi kimeshinda rufani za pingamizi zote zilizowekwa na vyama vya upinzani dhidi ya wagombea wake katika nafasi za uwakilishi na udiwani.
Rufani hizo zilikatwa dhidi ya wagombea wa nafasi hizo katika kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, baada ya rufani hizo kukosa ushahidi.
Taarifa iliyotolewa jana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa vyombo vya habari, Tume imetupilia mbali rufani aliyowekewa mgombea
uwakilishi wa jimbo la Amani, Ali Denge Makame, na wagombea wa CUF ambao walidai mgombea huyo bado ni mfanyakazi wa serikali huku akiwa wakala wa ZEC.
Baada ya kusikiliza rufani hiyo, ZEC imegundua kuwa Denge aliomba ruhusa kutoka kwa mwajiri wake kwa mujibu wa barua nambari AT/TMV/C 20/C./VOL.111/145 ya Agosti Mosi, 2005, hivyo alistahiki kugombea uwakilishi kama alivyofanya.
Katika rufani nyingine iliyowasilishwa na mgombea uwakilishi jimbo la Kitope kwa tiketi ya CUF, Hassan Khatib Ameir, aliyeomba mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, Mshimba Makame Mbarouk, jina lake lifutwe katika orodha ya wagombea.
Pingamizi ya mgombea wa CCM iliwekwa baada ya kuonekana hakuna maelezo ya kina ya kutosheleza ikiwemo tarehe ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi na mahali pa kazi kinyume na kifungu cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984, vifungu 49 (1) (a) na (b).
ZEC ilisema baada ya kuridhika na utetezi wa mrufaniwa licha ya kukosekana taarifa hizo na maelezo yaliyomo katika fomu ya utetezi, inatosha kabisa kumtambua na hivyo kumtangaza mgombea Mshimba wa CCM kuwa mgombea halali wa jimbo la Kitope.
Rufani nyingine iliyotupwa ni ile iliyowasilishwa na Haji Ameir Haji wa CUF kupinga uteuzi wa mgombea wa CCM wa uwakilishi jimbo la Kwahani, Ali Suleiman kwa madai kwamba amedanganya katika fomu zake za uteuzi kwa kusema elimu yake ni ya kidato cha nne, huku vielelezo vya kuthibitisha elimu yake hiyo vikiwa havitoshelezi.
ZEC ilitupilia mbali rufani ya pingamizi hiyo baada ya mgombea huyo kutoa cheti cha mtihani wa taifa cha kumaliza elimu ya kidato cha nne mwaka 1988, ambacho kilisainiwa Machi 18, 1989.
Aidha, katika pingamizi ya rufani hiyo mgombea wa CUF alishindwa kuwasilisha kielelezo chochote cha kuthibitisha madai yake dhidi ya mrufaniwa, na hivyo ZEC kumtangaza rasmi Ali Suleiman kuwa mgombea halali wa uwakilishi jimbo la Kwahani kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi.
Chama cha JAHAZI ASILIA kilimuwekea pingamizi mgombea uwakilishi katika jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman, na kutaka jina lake liondolewe katika orodha ya wagombea kwa madai kwamba watu waliomdhamini walighushi saini.
Baada ya kufanya uchunguzi wa kina, Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilibaini kwamba madai
hayo siyo ya kweli na hivyo mgombea huyo ambaye ni Waziri wa Elimu wa Zanzibar, kuruhusiwa kuendelea na kampeni za kuwania uwakilishi katika jimbo hilo ambalo alipita bila ya kupingwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya ZEC, tayari wagombea walioshinda pingamizi zao kwa sasa wapo huru kuendelea na kampeni zao za uwakilishi na udiwani katika majimbo ya uchaguzi zinazoendelea kote Unguja na Pemba.
Tanzania yasisitiza mkutanoni UN:
Haitaki kuona amani Burundi inavurugwa
Kisingizio kukwamisha utawala wa kidemokrasia kisikubaliwe
Na Mwandishi Maalum, New York
TANZANIA imesisitiza kuwa haitakuwa tayari kuona mchakato uliofanikisha kupatikana kwa utawala wa kidemokrasia, amani na utulivu nchini Burundi unavurugwa kwa kisingizio cha ina yeyote kile.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais Benjamin Mkapa wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano uliokuwa umeitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Anan ili kupokea taarifa ya mchakato wa amani ya Burundi na kujadiliana namna ya kuisaidia nchi hiyo.
“Sisi sote kutoka nchi za Maziwa Makuu na wale wote waliowezesha na kusaidia kukamilika kwa amani na demokrasia nchini Burundi, tunajisikia fahari sana na tumepata matumaini.
“Vilevile, kwetu sisi tulioshuhudia kuapishwa kwa Rais mpya wa Burundi, tunakumbuka hisia na matumaini ya kuanza kwa awamu mpya ya amani na utangamano walioonyesha wananchi wa Burundi. Sisi sote tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa matarajio ya wananchi hao yanatimizwa,” alisema Rais Mkapa.
Alisema Tanzania na kama ilivyokwisha ahidi huko nyuma itakuwa tayari na iko tayari kusaidia katika kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu uliopatikana nchini Burundi hauhujumiwi kwa namna yeyote ile.
Rais Mkapa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa juhudi za kuleta amani kwa nchi za Maziwa Makuu alisema kila kiongozi wa nchi za Maziwa Makuu anafahamu namna hali ya amani ilivyo bado tete nchini Burundi pamoja na changamoto zinazoikabili nchi hiyo.
Aliainisha maeneo sita ambayo ni muhimu katika kuendeleza amani ya Burundi kuwa ni pamoja na jumuia ya kimataifa kutimiza ahadi zao za kusaidia Burundi.
Alisema kuwa eneo lingine ni kusaidia ulinzi wa viongozi wapya, kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuwataka kikundi cha PALIPEHUTU-FNL kutambua kwamba hawana njia mbadala isipokuwa kujiunga katika mchakato wa amani ya nchi yao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Anan aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kwamba dhamira ya jumuia ya kimataifa ni kusaidia serikali mpya ya Burundi ili iweze kujijenga upya.
Alisema kuwa taratibu zote za kuisaidia nchi hiyo zitafanywa kwa kushirikiana na serikali mpya ya Burundi.
Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini aliunga mkono kauli ya Rais Mkapa kuwa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na wale waliochangia kufanikisha kupatikana kwa demokrasia na amani nchini Burundi hawatakubali kuona mafanikio hayo yanavurugwa kwa namna yeyote.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Rais Mwai Kibaki (Kenya), Rais Levy Mwanawasa (Zambia), Rais Piere Nkurunziza (Burundi), Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi (Ethiopia) na mwakailishi wa serikali ya Uholanzi aliyeahidi kuwa atahakikisha kikundi cha PALIPEHUTU-FNL kinashiriki meza ya mazungumzo. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Abdulkadri Shareef naye alihudhuria.
Msome: Hiki si kipindi cha kuwatambia walioshindwa
Na Angela Sebastian, Bukoba
lNi katika kura za maoni
CHAMA Cha Mapinduzi kimesema huu siyo wakati wa wagombea wake katika Uchaguzi Mkuu ujao kuwatambia walioshindwa katika kura za maoni.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Oganaizesheni , Jackson Msome, alisema huu ni wakati wa kujenga mshikamano kati ya wagombea, wanachama na wakereketwa wa Chama ili kukiwezesha kushinda katika uchaguzi ujao.
Msome aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na makatibu wa wilaya zote mkoani Kagera, katika
Ukumbi wa mikutano wa CCM Mkoa.
Alisema wagombea walioshindwa katika kura za maoni nao wasinune wala kukisaliti Chama hasa wakati huu ambao kampeni zinaendelea.
Alieleza kuwa ili chama cho chote cha siasa kishinde uchaguzi, kinahitaji kuwa na wagombea bora, Ilani ya Uchaguzi inayotekelezeka na mikakati mizuri ya kampeni.
Aliwashauri watendaji wa CCM wahakikishe mikutano ya kampeni inahusisha makundi yote muhimu katika jamii na pia kufungua mashina ya wakereketwa.
Msome alisema jumuia za chama nazo ziwajibike kikamilifu katika kuendesha kampeni za kistaarabu zinazozingatia sheria.
Vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea katika kata na majimbo mbali ya CCM ni CUF, CHADEMA, TLP, CHAUSTA, NCCR-MAGEUZI na UDP.
Mgombea udiwani wa UDP alalamikia viongozi wa kitaifa
Adai wamemwacha ‘solemba’ na sasa anajigharamia kampeni
Na Igamba Libonge, Kilombero
MGOMBEA udiwani wa chama cha UDP katika kata ya Lumemo wilayani Kilombero, Yahya Tungupo ameulalamikia uongozi wa chama chake kwa kushindwa kumpatia vifaa na fedha ili aweze kuendesha kampeni katika kata hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Tungupo amedai toka aanze kampeni zake katika kata hiyo Septemba 5, mwaka huu ameshindwa kupatiwa vifaa muhimu vya kampeni hivyo kuamua kuachana kampeni hadi atakapokabidhiwa vifaa hivyo.
Alivitaja vifaa ambavyo kama angevipata kampeni zake zingeenda vizuri kuwa ni Kipaza sauti, mabango ya chama chake ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe.
Tungupo alisema toka aanze kampeni amekuwa akijigharamia mwenyewe bila uongozi wa wilaya kumsaidia na yeye alijipangia siku 12 tu katika kampeni zake katika vijiji sita vya kata hiyo.
Aidha, Tungupo pia aliulalamikia uongozi wa UDP Taifa kwa kuwasahau wagombea wa udiwani kwa kujigharamia wao wenyewe kwa kuwa wakuu hao wanagombea ubunge katika majimbo mbalimbali hivyo bajeti yote wamejiwekea wenyewe.
"Kwa sababu wao wanagombea ubunge, bajeti yote wamejiwekea wenyewe wamesahau kwamba ili chama kiendelee kinatakiwa kipate asilimia tano ya kura na sisi wa chini ndio wenye uwezo wa kuwapa hizo asilimia iweje watusahau?" alihoji Tungupo.
Hata hivyo, mgombea huyo alisema anasikitishwa na tabia ya uongozi wa UDP wilaya kwa kumpiga chenga, kila anapotaka kukutana nao ili kuwasilisha ombbi lake la kupatiwa vifaa aendelee na kampeni.
Hata hivyo, mwandishi wa habari hii alipoutafuta uongozi wa wilaya ili kuthibitisha suala hilo, hakuweza kumpata kiongozi yoyote kwa madai kila mmoja yupo katika shughuli zake za kifamilia.
Wapinzani wahutubia abiria vituo vya mabasi
Ni kutokana na mikutano kukosa watu
Na Rashid Mussa, Mtwara
MIKAKATI ya wapinzani kusaka kura mkoani Mtwara inazidi kugonga ukuta kutokana na mikutano yao mingi ikiwemo ya viongozi wa kitaifa kukosa watu hata kuwafanya mahali pengine kuhutubia abiria kwenye vituo vya mabasi.
Katika hali inayoonyesha kukata tamaa baadhi ya viongozi hao badala ya kunadi sera na ilani zao, wamejikuta wakitoa kashfa na kejeli kwa wananchi na serikali jambo ambalo linawafanya watu kuendelea kususia mikutano yao.
Miongoni mwa waliokatishwa tamaa ni pamoja na mgombea Urais kupitia chama cha CUF, Ibrahim Lipumba ambaye katika mikutano yake ya kampeni licha ya mingi kukosa watu, mjini Masasi alijikuta anahutubia kituo kikuu cha mabasi cha mji huo na wengi kudai kuwa alisababisha kero kwa wasafiri.
Watu waliyohudhuria mikutano yake walisema mgombea huyo wa CUF alitumia muda wake mwingi kuwakejeli na kuwakashifu wananchi wa mkoa huu na kutilia mkazo sana ‘ilani yake’ ya kuuza ndege ya serikali.
Wengi wanashangaa mpango huo wa kung’angania kuuza mali ya serikali iliyopatikana badala ya kuiongeza ama kubuni mikakati mingine ya kukuza mapato ya serikali.
Wananchi hao walihoji iwapo atauza ndege na kutumia fedha zake umasikini kwa Watanzania utakuwa umekwisha, na kama bado watauza mali gani tena?
Kwa mujibu wa maoni ya wananchi wengi waliohojiwa katika majimbo yote saba ya mkoa huu, kukosa mwelekeo kwa upinzani kukosa wasikilizaji kunatokana na vyama hivyo kuonekana wakati wa uchaguzi tu na baada ya hapo vinakuwa kama havipo, kuiachia CCM ikijiimarisha zaidi hasa vijijini.
Aidha, katika mikutano hiyo Lipumba amekuwa akielezea mambo kwa jazba, hasira na kutumia lugha za kejeli na kashfa kwa wananchi.
Mgombea mwenza wa Urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Sheni aliyemaliza ziara yake mkoani hapa juzi aliwataka wananchi kuwa wavumilivu na kuwaomba kuondoka salama katika mikutano mara lugha chafu kwao na serikali inapoanza kutolewa ili kuepusha shari.
Alisisitiza umuhimu wa vyama vyote kufanya kampeni ya kistaarabu kwa kuzingatia kushindanisha sera na ilani badala ya matusi na kashfa kwa wananchi na serikali iliyopo madarakani, lugha ambazo zinaweza kuamsha hasira na vurugu miongoni mwa jamii.
Dk. Sheni ambaye mikutano yake ilivuta maelfu ya watu na hata kufanya ratiba kuvurugika mara kwa mara kutokana na umati wa watu kufurika njiani kote alikopita, aliwapongeza wananchi wa mkoa huu kwa kuiunga mkono CCM na kuihakikishia ushindi wa kimbunga.
CCM kufufua viwanda vya mbolea nchini
Na Ramadhan Mkoma, Songea
MGOMBEA Mwenza wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapindizi, Dk. Ali Mohammed Sheni, amesema iwapo
wananchi wataipa ridhaa CCM kuendelea kuwa madarakani kitakahikisha kinafufua viwanda vya mbolea
nchini ikiwa ni pamoja na kukaribisha wawekezaji katika sekta hiyo.
Dk. Sheni aliyasema hayo juzi katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Soko la
Peramiho 'A', mkoani Ruvuma, ambako anaendelea na kampeni baada ya kuhitimisha kampeni zake mkoani Mtwara.
Alisema juhudi hizo zitakwenda sambamba na kuongeza rukuzu ya mbolea ili kuhakikisha wakulima wa Ruvuma na
mikoa mingine wanapata mbolea nyingi na kwa bei nafuu.
Mbali na mbolea, Dk. Sheni alisema viwanda vidogo vidogo kwa vya ukoboaji wa nafaka, vitaanzishwa ili
kuwapunguzia mzigo kinamama na hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli zingine za kiuchumi.
Alisema mikakati hiyo ni sehemu ya maandalizi iliyojiwekea serikali ya awamu ya nne katika kufanya
mapinduzi makubwa ya kilimo nchini.
Pia, alisema ujenzi wa viwanda vya kutengenezea zana za kilimo utatiliwa mkazo katika kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa zaidi na wananchi wanaondokana na matumuzi ya jembe la mkono.
Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na mamia ya wakaziwa Peramiho, Dk. Sheni alisema msingi wa kutoa
kipaumbele katika suala zima la mbolea unatokana na ukweli kwamba wakulima wa mkoa huo ni watumiaji wazuri wa mbolea.
Dk. Sheni alitoa mfano kuwa katika kipindi cha mwaka 1995, wananchi hao walitumia wastani wa tani 42,139
ikilinganishwa na mwaka huu ambapo wametumia tani 141,328.
Pia, Dk. Sheni aliwapongeza wananchi wa mkoa Ruvuma kwa kuongeza ulizalishaji katika mazao ya biashara kutoka
tani 28,513 mwaka 1995 hadi tani 45,415 kwa mawaka huu.
Akizungumzia chanjo, Dk. Sheni alisema mkoa wa Ruvuma ulifanya shughuli hiyo kwa ufanisi mkubwa kwa kutoa chanjo hiyo kwa alisimia 92.4 kwa mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 75 kwa mwaka 1995.
Dk. Sheni alisema mafanikio hayo yote yanatokana na usimamiaji mzuri wa shughuli za kimaendeleo chini ya
uongozi wa CCM.
Alisema kutokana na hilo, wananchi wana kila sababu ya kuendelea kuichagua CCM ili iendeleze mazuri ambayo
imekuwa ikiyafanya katika kipindi chote cha utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi.
Katika mkutano huo, Dk. Sheni alimnadi mgombea wa kiti cha ubunge wa jimbo la Peramiho, Jenister Mhagama na
mgombea kiti cha udiwani wa kata ya Maposeni, Dominick Mahundi.
Akizungumza katika mkutano huo, Jenister alisema iwapo atashinda kiti hicho atahakikisha anatekeleza kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005/2010.
Kikwete aandaliwa mapokezi makubwa mkoani Kigoma leo
Na Jumanne Gange, Kigoma
CHAMA Cha Mapinduzi mkoani Kigoma kimeandaa mapokezi makubwa kwa ziara ya mgombea Urais, Jakaya Kikwete atakapowasili leo asubuhi katika uwanja wa ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Katibu Mwenezi wa CCM mkoani Kigoma, Mussa Chowo
alisema kuwa maandalizi yote ya kumpokea Kikwete yamekamilika na hivyo kuwataka wananchi mkoani kigoma
kujitokeza kwa wingi Akitoa ratiba ya ziara hiyo, Chowo alisema baada ya kuwasili Kikwete atakwenda wilaya ya Kigoma Vijijini kata ya Uvinza na kufanya mkutano wa kampeni na baadae kurudi siku hiyo hiyo wilaya ya Kigoma Mjini atakapofanya mkutano wa hadhara kuanzia saa nane mchana katika uwanja wa mpira wa Lake Tanganyika
Aliongezea kuwa baada ya kumaliza mkutano huo wa
kampeni katika wilaya ya Kigoma mjini, kesho atakwenda wilayani Kasulu na kufanya mkutano wa kampeni na baada ya kumaliza siku hiyo hiyo.
Baada ya mkutano huo, KIkwete ataelekea wilayani Kibondo kufanya mkutano wa kampeni na kumalizia kampeni hizo katika tarafa ya Kakonko na baadaye kuelekea mkoani Kagera.
Makamba aagiza sungusungu kuimarishwa Dar
Na Thomas Mtinge
MWENYEKITI wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Dar es Salaam, Yusuf Makamba, amewaagiza watendaji kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la ulinzi wa sungusungu katika maeneo yao.
Agizo hilo la Makamba limekuja siku chache huku kukiwa kumeripotiwa matukio mbalimbali ya uhalifu mkoani humu.
Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na la kuchoma moto nyumba ya Katibu wa Uenezi na Siasa wa tawi la CCM Midizini, Mwajuma Nyanza na kusababisha kifo cha watu watano akiwemo Mwajuma.
Makamba ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa akizungumza na makatibu tarafa na maofisa watendaji wa kata za Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam katika ukumbi wa Arnatoglou jana.
Alisema maofisa hao wa kata pamoja na mambo mengine yanayowakabili, wana jukumu la kusimamia na kuhakikisha amani na utulivu vinapatikana katika maeneo yao hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 30, mwaka huu.
Makamba alisema endapo amani na utulivu vitatoweka, jiji la Dar es Salaam halitakalika na wananchi watashindwa kufanyakazi maofisini na hata mashambani.
Alisema suala la ulinzi mkoani humo halina mjadala kwa sasa na lazima kila mtu ashiriki kikamilifu ili kupambana na vitendo vya uhalifu ambao vimeonekana kushamiri.
"Kuanzia sasa watendaji lazima msimamie suala la ulinzi wa sungusungu na kama kuna mtu hataki kufanya hivyo basi aandike barua mapema," alitahadharisha Makamba.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, alieleza umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu baina ya polisi na watendaji hao katika kukabiliana na hali hiyo.
Alisema kuwepo kwa ushirikiano kutasaidia kwa kiasi fulani kufichua mbinu za uhalifu zinazofanywa na raia wasio wema.
Hata hivyo, Tibaigana alisema kumekuwa na taarifa kwamba baadhi ya wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya kata wamekuwa wakikiuka taratibu za utoaji vibali vya matumizi ya silaha.
Alisema baadhi ya wajumbe hao wamekuwa wakidiriki kutoa kibali cha kutumia silaha 'kinyemela' bila wajumbe wenzao kujua hata kama mtu huyo hastahili kupewa.
"Si kwamba nawashutumu, bali baadhi yenu mmekuwa mkichukua fedha kwa watu wanaoomba kibali na kuvisaini bila ya wenzenu kujua lakini katika muhtasari mnaandika majina ya wajumbe wote kuwa wamehudhuria, kumbe si kweli," alisema Tibaigana.
Alisema njama hizo zimegundulika na ushahidi upo na hivyo kuwataka watendaji hao kuachana na tabia hiyo kwani ni hatari kwa maisha yao.
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)kimekusanya ya sh. 96,228,200 kwa ajili ya kuwawezesha wanahabari wanawake kupata elimu ya Chuo Kikuu kuanzia mwaka huu wa masomo.
Ofisa Mipango wa TAMWA, Irene Bwire alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Ananilea Nkya.
Irene alisema fedha hizo ni makusanyo yalitokana na chakula cha usiku kilichoandaliwa Septemba 2, mwaka huu katika viwanja vya Karimjee na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Frederick Sumaye.
Alisema kiasi kilichopatikana hadi sasa ni asilimia 64 ya lengo la TAMWA la kukusanya sh. milioni 150 hadi ifikapo Desemba 31, mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza azma yake ya kusomesha wanahabari wanawake Chuo Kikuu wasiopungua 35 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Irene alisema katika makusanyo hayo sh. 25,071,200 ni fedha taslimu na sh. 71,157,000 ni ahadi zikiwepo za taasisi nne ambazo kila moja imejitolea kusomesha mwanahabari mwanamke mmoja Chuo Kikuu kwa muda wa miaka mitatu.
Alizitaja taasisi zilizotoa ahadi ya kusomesha mwanahabari mmoja kwa miaka kwa miaka mitatu ni Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais (Umasikini), Mamlaka ya Elimu nchini na Hoteli ya Protea Courtyard.
Irene alisema michango mingine iliyopatikana kwa viwango tofauti ni kutoka wizara mbalimbali, vyama vya siasa, wanasiasa binafsi, taasisi, mashirika ya umma, benki, hoteli, mashirika ya kijamii, na watu binafsi.
Alisema benki ya CRDB pamoja na kutoa fedha taslimu sh. Laki tano pia imeondoa gharama za malipo ya kutuma fedha kwenye akaunti ya TAMWA kwa watu wa mikoani.
Irene alisema jumla ya wananchi 37 walichangia sh. 5,000 kila mmoja, wananchi 111 kila mmoja walichangia sh. 10,000, wananchi tisa waliahidi kuchangia kila mmoja sh. 15,000, wananchi 77 waliahidi kuchangia sh. 20,000 kila mmoja, wengine 118 waliahidi kuchangia sh. 50,000 kila mmoja.
Aliwataja wengine kuwa ni wananchi 45 waliahidi kuchangia sh. 100,000 kila mmoja, wananchi 26 waliahidi kuchangia sh. 200,000 kila mmoja, wananchi watatu wameahidi kuchangia sh. 300,000, wananchi wengine watatu sh. 400,000, waliochangia sh. 500,000 ni watu 25 na waliochangia kati ya sh. m cilioni moja hadi mbili ni watu tisa.
Irene alisema kuwa lengo bado halijatimia na aliwaomba wananchi waendelee kuichangia TAMWA kiasi chochote kwenye akaunti ya TAMWA namba 01J2027600600 iliyopo CRDB tawi la Azikiwe jijini Dar es Salaam au kuwasiliana na simu namba 022 22115278 au 0744 365214 au barua pepe tamwa@raha.com