UHURU 17.09.2005

 

 

Watano kortini kwa mauaji ya Manzese

Na Gabriel John

MGANGA wa kienyeji ni miongoni mwa watu watano waliofikishwa mahakamani mjini Dar es Salaam jana kwa mashitaka ya mauaji ya kada wa CCM na familia yake.

Watu hao watano wanatuhumiwa kuhusika na  mauaji ya  aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi Tawi la Midizini, Manzese na wenzake wanne ambao vifo vyao vilitokana na nyumba yao kuchomwa moto usiku wa manane.

Mwendesha Mashitaka Kamishna Msaidizi wa Polisi, Patrick Byatao aliwasomea mashitaka ya mauaji mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Francis Mutungi.

Byatao aliwataja washitakiwa kuwa ni Mganga wa kienyeji Rashid Ally (44), Juma Rajabu (25), Hassan Kassim (37), Kassimu Salum (55) na Juma Hamis (31), wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Alidai mbele ya Hakimu Mutungi kuwa mnamo Septemba 9, mwaka huu, saa 8 usiku, washitakiwa waliwauwa Katibu Mwenezi Mwajuma Nyanza (53), Mwajuma Rashid (16), Sambali Luciani (11), Daniel John (3) na Asha Rashid (13)  katika eneo la Manzese, Midizini.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji kwa kuwa husikilizwa na Mahakama Kuu. Kesi hiyo itatajwa Septemba 30, mwaka huu.

 

 

 

Kikwete avunja ngome za CHADEMA, CUF Kigoma

Na Bashir Nkoromo, Kigoma

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete

amezisambaratisha ngome muhimu za vyama vya CHADEMAna CUF baada ya jumla ya wanachama 199 wa vyama hivyo kumkabidhi kadi zao na kuhamia CCM, wakati wa mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika jana katika uwanja wa Lake Tanganyika mjini hapa.

Katika mkutano huo ambao ulihuduriwa na maelfu ya

wananchi katika uwanja huo, wanachama 125 wa CHADEMA kutoka kutoka mji mdogo wa Gungu ambao

ni ngome muhimu ya mgombea ubunge wa chama hicho jimbo la Kigoma Mjini, Dk. Walid Kabourou walitangaza

kukihama chama hicho na kumkambidhi kadi zao Kikwete.

Wakati CHADEMA ikipata pigo hilo, CUF kilipata pigo la baada ya wanachama wake 74 kutangaza mbele ya Kikwete kuwa tawi lililokuwa la chama hicho la Bangwe eneo la Kigoma Mjini kuanzia sasa litakuwa la CCM ambapo walimkabidhi kadi zao kwa mgombea huyo wa Urais naye akawapatia kadi mpya za CCM.

Akizungumza mbele ya Kikwete mmoja wa wanachama hao wa CUF, Ephraim Nicholaus alisema, yeye na wenzake

wameamua tawi lao kuligeuza la CCM  baada ya kuchoka na ahadi hewa za viongozi wa juu wa chama hicho.

Naye Daudi Kasoma alisema, yeye na wenzake wa Gungu wameamua kukihama CHADEMA kwa sababu ahadi zote alizotoa Dk. Kabourou wakati akigombea Ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini kuwa watapatiwa umeme wa uhakika na maji, hakuna alichoweza kukitekeleza hadi leo.

Akihutubia mkutano huo, Kikwete alisema wananchi mkoani Kigoma hawana sababu ya kuwapa wapinzani kura

katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, kwa sababu wao kazi yao ni kulalamika huku wakiwa hawajui wanachotaka.

Kikwete akiwahakikishia wananchi wa Kigoma kwamba mpango wa mji wa mkoa huo kuwa na umeme wa uhakika

tayari imekamilika kwa kuwa sasa umefika Urambo.

Alisema hawezi kutamba sana kuwa ameufanikisha yeye, lakini akawaahidi kwamba akiwa rais atasimamia kwa

uwezo wake wote na kuhakikisha umeme huo unafika mapema iwezekanavyo.

Kikwete alisema, vilevile ujenzi wa daraja la Mto Malagarasi na barabara ya urefu wa kilometa  90

kupitia daraja hilo vitajengwa.

Aliwahakikisha wananchi wa mkoa huu kwamba, akiwa rais ataendeleza juhudi zinazofanywa na CCM hadi sasa

kuhakikisha mkoa wa Kigoma unaweza kufikiwa kutoka maeneo mengine ya nchi kwa barabara za lami.

Kuhusu amani, Kikwete aliwataka wananchi hasa wa mkoa wa Kigoma kuenzi kwa kuchagua viongozi bora ambao

wanapatikana CCM kwa kuwa uongozi mbovu ndiyo chanzo cha migogoro na vita kama ilivyo kwa jirani wa mkoa huo Burundi na Rwanda.

Akizungumzia hali ya amani iliyorejea nchini Burundi baada ya kufanya uchaguzi mkuu na kumpata rais mpya,

Kikwete alisema, wakimbizi hawataswagwa kurejea kwao lakini watarejea huko kwa taratibu zilizopo.

Kikwete alisema, akiwa rais atahakikisha ushirikiano baina ya nchi za Burundi na Rwanda unaimarika zaidi,

lakini akaonya kuwa isiwe katika kutatua migogoro ya vita lakini iwe ya masuala ya uchumi.

Baada ya mkutano huo, Kikwete aliyewasili mkoani hapa jana, alikwenda katika mji mdogo wa Uvinza ambako

alitarajiwa kuhutubia mkutano wa kampeni na baadaye kurejea Kigoma kupumzika.

 

 

Lowassa: Kifo cha upinzani kimewadia

Na Omari Shaaban, Monduli

MGOMBEA ubunge katika jimbo la Monduli kwa tiketi ya CCM, Edward Lowassa, amezindua kampeni zake za kuwania kiti hicho mbele ya umati mkubwa wa watu, ambao aliwaeleza kuwa kifo cha vyama vya upinzani kimewadia.

Katika uzinduzi huo uliofanyika juzi kwenye uwanja wa michezo wa Mto wa Mbu, alisema hakuna utawala utakaoweza kuwaletea maendeleo wananchi jimboni humo na Tanzania zaidi ya Chama cha Mapinduzi.

Umati huo wa watu uliyokuwa umevalia fulana za Lowassa na za mgombea urais  kupitia CCM, Jakaya Kikwete, na wengine wakiwa wamevaa migolole ya kimasai, Lowassa alisema kwa tathmini ya uchaguzi kwenye jimbo lake hakuna mpinzani atakayepata kura hata moja kutokana na maendeleo yaliyoletwa na CCM, na anaweza hata kuanza kusherehekea ushindi.

"Nafikiri kwa hali ninayoiona... hakuna mpinzani atakayepata kura hapa za urais, ubunge wa udiwani. Mnaonaje tukianza kusherehekea ushindi wa kishindo... ama tungoje kwanza," aliuliza umati huo uliitikia kwa nguvu 'tuanzee'.

Akihutubia umati huo, ambao katika historia ya Monduli hauwajahi kutokea, alisema hana sababu ya kuanza kutoa ahadi kwa kuwa kila kitu kinaendelea kutekelezwa kama kilivyopangwa kwa maendeleo ya wananchi wa Monduli na Tanzania kwa jumla.

Huku akishangiliwa mara kwa mara, alisema wananchi wana kila sababu ya kuichagua CCM, kwa kuwa imeleta na inaendelea kuleta maendeleo Monduli, na hivyo basi, aliwataka kuhakikisha CCM inapata ushindi wa 'Kimbunga' ili iwe fundisho kwa wapinzani.

Lowassa ambaye ni Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo, alitumia muda huo pia kuwaomba na kuwataka wananchi kutokuwa na hasira kutokana na maneno mabaya yanayotolewa na wapinzani wanaotembelea mkoa wa Arusha na jimboni humo, kwa kuwa hiyo ni kawaida yao.

 

"Ndugu wananchi nyie si mnafahamu kabisa kwamba CCM haina muda wa malumbano zaidi ya kutekeleza ahadi zake? Nyie waacheni hata wakiongea maneno ya kuwakera kiasi gani... msighadhibike ni kawaida yao," Lowassa aliwasihi wananchi hao.

Alisema CCM itaendelea kutekeleza mipango endelevu ya maendeleo kwa wananchi katika awamu ya nne ya urais inayokuja, na hivyo wananchi waendelee kufaidi matunda ya CCM na wakipe kura zote za ndiyo.

Katika mkutano huo, vikundi mbalimbali vya sanaa vilihudhuria uzinduzi huo, akiwemo msanii kutoka Mwanza Vicky Kamata na wengineo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na mkuu wa wilaya Monduli, Kapteni Malle, mwenyekiti wa CCM mkoa, Yona Nko, katibu Nurdin Babu pamoja na watu maarufu wa ndani na nje ya Arusha.

Msafara wa Lowassa ulianzia njia panda ya makao makuu ya Monduli kuelekea Mto wa Mbu ukiwa na magari zaidi ya 50, pamoja na wapanda baiskeli na pikipiki huku kukiwa na nyimbo za kampeni.

 

 

Kikwete avunja ngome za CHADEMA, CUF Kigoma

Lowassa: Kifo cha upinzani kimewadia

Mgombea udiwani aahidi maendeleo

Na Igamba Libonge, Kilombero

MGOMBEA udiwani kata ya Ifakara, Horitensia Mbalahami, awataka wananchi wa kata ya hiyo wamchague ili aweze kuwatetea na kuwaletea maendeleo  kwa ajili kuboresha barabara za mitaa na elimu kwa watoto.

Hayo aliyasema jana wakati wa kampeni zake kwenye kata hiyo wakati alipokuwa akijinadi na kuomba kura kupitia tiketi ya CCM mjini Ifakara.

Mbalahami ambaye ni mwanamke pekee kugombea udiwani katika wilaya hiyo alisema kama wananchi wakimchagua atajali jinsia zote kwa kuwatetea na kusaidia sana yatima ambao kwa sasa wapo wengi wilayani humo.

Alisema kwa upande wa wanawake atajitahidi kuwainua, kwani ameona kuwa wanawake wana uchungu mkubwa dhidi ya watoto, hususan kwenye elimu kwani yeye alikuwa mwalimu katika kata hiyo na baadae kuacha na kufanya biashara.

"Mkinichagua nitaendeleza kuhamasisha kuwapeleka shule watoto yatima ambao wazazi wao walifariki kwa magonjwa mbalimbali, hususan janga hili la Ukimwi," alisema.

Aliendelea kusema kuwa atahamasisha kuendelea kwa ujenzi wa shule za awali na kumalizia shule ambazo zilianzishwa na diwani aliyemaliza muda wake.

Aidha, katika ahadi hizo alisema atahamasisha ujenzi wa madarasa mengi zaidi na nyumba za walimu pamoja na kujenga shule za sekondari za kata, hasa ikizingatiwa kuwa kata hiyo kutokuwa na shule ya sekondari kutokana na wananchi kutokuwa mwamko.

Aidha, Mbalahami alisema atahakikisha kata hiyo inajiwekea mipango thabiti ya kukabiliana nha tatizo la maji, hasa kutokana na kinamama wengi kuteseka kwa kuyafuata umbali mrefu.

Alisema atajitahidi kufanya mbinu za kufuatilia tatizo hilo kwa karibu na kuweza kufanikisha kuleta maendeleo hayo kwa kushirikiana na jamii ya kata hiyo na halmashauri ya Wilaya.

 

 

 

Murad aonya viongozi wasiotekeleza majukumu

Na Prosper Kulita, Mvomero

MGOMBEA ubunge jimbo la Mvomero, Suleiman Sadiq Murad, amesema ugumu wanaopata baadhi ya wagombea wa udiwani katika kata mbalimbali za wilaya hiyo wakati huu wa kampeni, unatokana na baadhi ya viongozi wa CCM na watendaji wa serikali kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika ziara ya kampeni iliyofanyika katika kata za Kanga, Dihongoya na Mhonda.

Alisema uzembe huo wa kushindwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ndiyo unaowapa ugumu wagombea wa sasa na kutoa mwanya wa kukua kwa ongezeko la upinzani katika kata husika jambo ambalo linawafanya baadhi ya wagombea wawe na wakati mgumu kuuzika kwa wananchi.

"Kwa kipindi kijacho cha uongozi chama hakitawafumbia macho viongozi wazembe wa CCM na serikali ambao wamekuwa kiini cha kukwamishwa kasi ya maendeleo katika jimbo letu," alisema Sadiq.

Aliongeza kusema kuwa viongozi hao wanapaswa kujirekebisha haraka ili fagio la chuma lisiwapitie katika kipindi cha awamu ya nne ya serikali ya CCM ambayo imedhamiria kutekeleza ilani yake kwa vitendo na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa Watanzania.

Pia, aliwataka wananchi kufahamu juu ya maana ya maisha bora kwa kila Mtanzania na kuachana na propaganda za wapinzani za kusema kuwa watawajaza pesa mifukoni ili kujikwamua na umaskini.

Alisema kuwa hoja ya maisha bora kwa kila Mtanzania inamaanisha kuboresha huduma za kijamii ili ziweze kupatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu pamoja na kujenga mazingira ambayo yatawezesha kila mananchi kupata ajira iwe ya sekta rasmi au isiyo rasmi.

Alitolea mfano wa mafaniko ya CCM jimboni humo katika miaka mitano iliyopita ambayo imeweza kufanikiwa kujenga zahanati 11 na shule tano za sekondari na kuboresha shule zote za msingi katika wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na miuondo mbinu.

 

 

 

 

‘Wingu’ la wanachama wa vyama vya upinzani lamiminika CCM Mbinga

Ni zaidi ya watu 230, wakiwemo wagombea udiwani wa upinzani

Na Ramadhan Mkoma, Mbinga

WINGU la wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani kuhama vyama vyao limeendelea kutanda, kufuatia hatua ya wanachama 232 wakiwemo wagombea wawili wa viti vya udiwani kuhamia CCM.

Wanachama hao wa jimbo la Mbinga Magharibi, walitangaza kuvikimbia vyama vyao juzi katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katika kijiji cha Tingi.

Katika mkutano huo mgombea mwenza wa kiti cha urais kupitia CCM, Dk. Ali Mohammed Sheni, alikuwa akihutubia wananchi waliofurika kwenye

mkutano huo.

Wagombea wa udiwani waliojitoa ni Mayola Mpangala wa CUF kutoka kata ya Matili na Bruno Kapinga wa CHADEMA kutoka kata ya Mkumbi jimboni humo.

Viongozi wengine wa kambi ya upinzani waliotangaza kujiunga na CCM ni Valerian Ndimbo ambaye ni Katibu wa CUF wilaya ya Mbinga na Katibu Mwenezi wa chama hicho wilayani humo, Cathbert Murusi.

Mbali na kujitoa, viongozi hao walikabidhi bendera mbili na mihuri miwili ya vyama hivyo (CUF na CHADEMA) na baadaye kula kiapo sambamba na wanachama wengine wa upinzani waliojiunga na chama tawala cha CCM.

Sambamba na wapinzani hao kuvihama vyama yao, mkutano huo ulifana licha ya mgombea kiti cha ubunge wa jimbo hilo, Kapteni mstaafu John Komba kutokuwepo.

Komba ambaye ni msanii mashuhuri aliripotiwa kuwa mkoani Kigoma na kikundi chake kwa ajili ya kampeni za mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Kutokana na hilo, Dk. Sheni alilazimika kumuombea kura Kapteni Komba kutoka kwa wananchi hao waliojitokeza kwa wingi katika mkutano huo hali iliyoonyesha mapenzi waliyonayo na CCM na mshikamano waliokuwa nao.

Vikundi vya ngoma na wana kwaya waliokuwa wamevalia sare zisizopungua kumi tofauti viliupamba kwa kiwango kikubwa mkutano huo.

Wasanii hao walimvutia Mgombea Mwenza hatua iliyomfanya yeye na ujumbe wake kuamua kutembea na kuangalia ngoma na kwaya zilizokuwa zikichezwa katika viwanja hivyo kabla ya kupanda

jukwaani.

Mbali na wasanii hao, wananchi waliohudhuria mkutano huo walikuwa wamevalia sare zenye picha za Kikwete na Komba hali iliyozidi kupamba sura ya mkutano huo. Walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kusifu mafanikio ya CCM pamoja na kusisitiza kupewa kura kwa wagombea wa CCM.

Awali, aliweka jiwe la msingi wa ujenzi wa madarasa matatu ya shule ya sekondari Tingi inayojengwa kwa nguvu za wananchi wakisaidiwa na serikali.

Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Sheni aliwataka wananchi hao kutohadaika na ahadi za wapinzani ambao aliwaelezea kuwa ni wachanga na wasiostahili kupewa uongozi wa dola. Dk. Sheni alisema vyama vya upinzani vina miaka 13 umri ambao alisema mdogo kuweza kukabidhiwa dola.

Alisema hilo linatokana na ukweli kwamba uongozi haufanyiwi majaribio na kuwataka wananchi kukipa kura CCM ili kiendeleze mazuri iliyoaanzisha tangu taifa hili kupata uhuru.

Katika mkutano huo, Dk. Sheni mbali ya kuombea kura Kapteni Komba pia alimnadi mgombea wa jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo na diwani wa kata ya Tingi, Yasinti Wero. Pia aliwaombea kura madiwani wengine wa jimbo hilo.

Pia jana alikuwa na mkutano katika jimbo la Namtumbo na kumnadi mgombea wake Vita Kawawa katika mkutano uliofanyika katika kijiji cha Luchili. Leo anaendelea na kampeni wilayani Ludewa, mkoani Iringa.

 

 

 

CCM Mkoa yasikitishwa kuuawa mashabiki wake

Na Rashid Mussa, Mtwara

CHAMA Cha Mapinduzi mkoani Mtwara kimesikitishwa na taarifa ya kuuawa kwa mashabiki wake Masasi na mwingine katibu tawi kujeruhiwa vibaya huko Newala pamoja na vitisho kwa kiongozi mmoja wa chama kutokana na ushabiki wa kisiasa.

Akitoa salamu za kuwafariji wafiwa wa marehemu Jofrey Malingonya 30 wa mjini Masasi, Katibu wa CCM mkoa Anna Magowa alisema Chama kinalaani vitendo vya ushabiki wa kisiasa vinavyotishia usalama wa maisha ya watu na kuvunjika kwa amni na utulivu katika jamii.

Katibu huyo alitoa salamu hizo juzi nyumbani kwake marehemu eneo la Rest mjini Masasi akiongoza uongozi mzima wa wilaya hiyo uliyokwenda kuwapa pole wafiwa wa kifo hicho cha ghafla kilichohusishwa na ushabiki wa kisiasa.

Alisema Chama kimeshtushwa na kifo cha shabiki wake huyo na kujeruhiwa kwa kipigo katibu wake tawi la Nyanyambachi Newala, Shaibu Ulaya mkaazi wa kijiji cha Tengulengu wilayani humo katika tukio lingine la ushabiki wakisiasa.

Aidha, alisema Chama kimefadhaishwa sana na kushangazwa na vitisho vinavyotolewa na watu wasiyojulikana wanaodaiwa kuwa Waislamu kwa katibu mwenezi wa Chama wa mkoa Msham Nayopa kuwa siku zake za kuishi zinahesabika.

Anna alisema Chama kina imani kubwa na vyombo vya dola kuwa vitafanya kazi yake kisheria na kuhakikisha wote wanohusika katika matukio yote haya wanachukuliwa hatua za kisheria haraka ili kulinda usalama wa maisha ya watu.

Aliahidi kuwa yeye mwenyewe ataongoza uongozi wote wa CCM mkoa kuhakikisha haki inatendeka na kwamba wanohusika wote wanapatikana na kutiwa mbaroni.

Kamanda wa Polisi wa mkoa, Rahma Othaman alikiri kutokea kwa matukio hayo na kwamba upelelezi mkali unaendelea hadi jana aliyehusika na mauji ya masasi alikuwa bado kukamatwa.

Alisema mtu huyo Mohamed Mfaume alitoweka mara baada ya tukio hilo ambapo anadaiwa kuwa katika ugomvi huo alimpiga mwenziwe kwa chuma kichwani na kumwacha akigalagala chini katika hali mbaya hadi kufa papo hapo.

Alifafanua kuwa watu hao wawili ni majirani kama ilivyo katika tukio la Newala, ambapo walikuwa wakizozana kwa ubishi wa CCM itashinda mwaka huu.

Aidha, kwa mujibu wa tamko la maandishi lilitolewa juzi na kusambazwa mjini hapa linadai kuwa, siku za kuishi Nayopa zinahesabika kutokana na matamshi yake aliyoyatoa katika mkutano wa hadhara ya kuwa hata Mungu hakulinganisha katika uumbaji.

Katika tamko hilo linalodai ni la Waislam manispaa ya Mtwaa wanamshutumu kwa kuhusisha vingozi wa juu wa CCM kuwa ndiyo waliyomtuma kumtukana Mwenyezi Mungu.

Inasemekana Nayopa alitoa kauli ya kumhusisha Mwenyezi Mungu wakati wa kunadi wagombea wa CCM huku akitumia jukwaa vizuri kujibu hoja mbalimbali  za kejeli na kashfa zinazotolewa na wapinzani wa jimbo hili kwa chama na yeye binafsi kutokana na wadhifa wake.

Wapinzani wanadaiwa kumkashifu sana katika mikutano yao ya kampeni katibu huyo  anaonekana kuwa mwiba kwao kwa nguvu  hoja anazotoa katika kuinadi CCM na badala ya kumjibu kwa hoja wengi wanaweweseka na kumkashifu yeye binafsi na Chama.

 

 

 

Wahariri kutathmini wanavyotoa nafasi kwa wagombea wanawake

Ni katika vyombo vyao vya habari

Na Mwandishi Wetu

WAHARIRI 40 kutoka vyombo vya habari vya redio, televisheni na magazeti hapa nchini wanakutana jijini Dar es Salaam leo kutathmini jinsi vyombo vyao vinavyowapa nafasi wagombea wanawake.

Mkutano huo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), utafanyika katika hoteli ya Peacock kuanzia saa sita mchana. 

Taarifa ya TAMWA kwa vyombo vya habari ilisema lengo la mkutano huo ni kuwapa fursa wahariri kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu jinsi ya  kuwawezesha wanawake wa vyama vyote vya siasa wanaogombea nafasi za udiwani, ubunge na urais  wapate fursa zaidi ya kunukuliwa na vyombo vya habari wakati wanaendesha shughuli zao za kampeni.

Ilisema TAMWA inaamini kuwa vyombo vya habari vina mchango muhimu na wa pekee katika kuelimisha, kuhamasisha na kushawishi wananchi  kutekeleza mambo yanayowezesha taifa kupiga hatua  kubwa ya maendeleo  kwa kuzingatia usawa wa jinsia.

Hivyo, katika taarifa hiyo TAMWA ilisema kwamba inaamini kuwa vyombo vya habari vikiweza  kuwapatia wananchi habari za wagombea wote wanawake  na wanaume, wapiga kura watapata fursa  ya kuwafahamu vyema wagombea wote na hivyo ifikapo siku ya uchaguzi Oktoba 30, 2005 wataweza kuchagua mgombea wanayeamini atakuwa kiongozi bora.

Lakini, TAMWA ina hofu  kuwa endapo vyombo vya habari havitafanya kazi ya ziada  kutangaza habari za wanawake wanaogombea, hasa kwenye majimbo  ili wapiga kura wawafahamu mapema, huenda nchi yetu ikashindwa kufikia lengo la kupata asilimia 30 ya wanawake wabunge baada ya uchaguzi mkuu.

Taarifa hiyo ilisema hali hiyo inaweza kulitia  taifa   aibu kwa sababu serikali imetia saini Azimio la  Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ambalo linataka nchi wanachama kuwa na angalau asilimia 30 ya wanawake kwenye ngazi za maamuzi ikiwa ni pamoja na  bungeni kabla ya mwisho wa 2005.

Serikali, mwaka jana  ilitia saini azimio la Umoja wa Afrika linalohimiza nchi wanachama kuhakikisha kuwa  katika kila chombo cha maamuzi  kunakuwa  na idadi  ya wanawake asilimia 50.

 

 

 

Serikali yatoa changamoto kwa maofisa mipango miji

Sumaye ataka watenge maeneo maalum kwa shughuli za walemavu

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU Frederick Sumaye amewataka watendaji wa serikali wanaohusika na mipango miji kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za watu wenye ulemavu.

Sumaye alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Umoja wa Wafanyabiashara wenye ulemavu mjini Dar es Salaam.

“Wito wangu kwa wataalamu wetu katika nyanja mbalimbali, hususan wale wa mipango ni kuwa kila mara tunao wajibu wa kuzingatia mahitaji maalum ya walemavu kwenye mipango yetu,” alisema Sumaye.

Aliwataka walemavu kutofanya biashara kwenye maeneo yenye shughuli maalum kama vile barabarani au kwenye njia za watembea kwa miguu.

Sumaye alisema, hata hivyo, Jiji la Dar es Salaam bado linakabiliwa na tatizo la mpangilio mzuri wa shughuli za biashara na kuongeza kuwa pamoja na upungufu huo ni lazima mapungufu yaendelee kurekebishwa.

Alisema haitoshi kutoa elimu na kutumia sheria kukataza kufanya biashara kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, bali pia kuna wajibu wa kuweka mpangilio mzuri na kutenga maeneo maalum kwa wafanyabiashara.

“Katika kufanya hivyo ni wajibu wa Mamlaka mbalimbali kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za watu wenye ulemavu.

“Hatuwezi kuzungumzia dhana ya kuwapa walemavu nafasi kama hatuchukui hatua za dhati za kuwajengea mazingira yatakayowawezesha kujitegemea,” alisema.

Sumaye aliwataka walemavu kuchukua mikopo inayotolewa na mabenki na kuwaasa waache hofu ya kuchukua mikopo kwa ajili ya maendeleo yao.

Aliwaeleza viongozi wa umoja huo kuwa ni wajibu wao kutochoka kuonana na viongozi na watendaji wa serikali ili kwa pamoja waweze kuweka mazingira ya kutatua kero zinazokwamisha juhudi za walemavu.

 

 

 

Rais Mkapa amwondoa mkuu wa wilaya Lindi

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa amemwondoa madarakani aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Luhozyo Siwale.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Dar es Salaam jana na Idara ya Habari (MAELEZO) ilisema kuwa Siwale ameondolewa kazini tangu juzi kutokana na sababu za kiafya.

Wakati huo huo, Rais Mkapa amemteua Profesa Apollinaria Pereka wa Chuo Kikuu cha Kilimo, Sokoine kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Dar es Salaam jana na MAELEZO ilisema kuwa uteuzi huo umefanyika kufuatia kumaliza muda wa baraza hilo tangu Juni 11, mwaka huu ambapo mwenyekiti wake alikuwa Profesa Cleophas Migiro.

Kabla ya uteuzi huo Apollinaria alikuwa Profesa katika fani ya mifugo katika Chuo Kikuu cha Sokoine na pia amewahi kufanya kazi katika vyuo mbalimbali vya kilimo vikiwemo vya Uyole, Mbeya na MATI cha Tengeru, Arusha.

Katika hatua nyingine Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Juma Ngasongwa amewateua wajumbe tisa watakaounda Baraza hilo.

Wajumbe hao ni Godfrey Mkocha, Said Nkya, Christine Kilindu, Kanali Nsa Kaisi na Francis Mutungi.

Wajumbe wengine ni Salma Ebrahim, Dk. Romwald Mbwasi, Shaweji Abdallah na Daimon Mwakyembe ambaye ni Mkurugenzi wa TBS.

 

 

 

 

 

 

 

Mlezi wa TLP Mvomero ajiunga CCM

Na Prosper Kulita, Mvomero

MLEZI wa chama cha Tanzania Labour (TLP) Wilaya ya Mvomero, Christian Makundi ni miongoni mwa wanachama wa vyama zaidi ya vinne walioamua kujiengua na vyama hivyo na kujiunga na CCM.

Wanachama hao 20 walirudisha kadi hizo mbele ya mgombea ubunge katika jimbo la Mvomero, Suleiman Sadiq, wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea huyo wa CCM katika Kata za Mhonda, Dohongoya na Kanga wilayani humo.

Chama kilichopoteza  wanachama wengi ni TLP ambayo wanachama wake 11 walikikimbia, wakati Chadema kilipoteza wanachama watano, NCCR-Mageuzi wanachama watatu na CUF watatu.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mvomero, Abdallah Mtiga, alisema kurejea CCM kwa wanachama hao wa vyama vya upinzani,  kumewafanya kuvunja ngome ya wapinzani katika maeneo hayo ambayo alisema kwa asilimia kubwa yalikuwa yameshikwa nao.

Alisema kurejea kwa wanachama hao pia kumetokana na CCM wilayani humo kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2000 kwa zaidi ya asilimia 89, na hivyo kuifanya kuwa wilaya pekee katika Mkoa wa Morogoro uliyovuka lengo la utekelezaji wa ilani.

Mgombea ubunge wa jimbo la Mvomero, Sadiq alisema moyo wa wananchi kushiriki katika shughuli za maendelo umepungua kutokana na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kuwashawishi wananchi wasishirki katika shughuli hizo.

Alisema hali hiyo inawafanya wananchi wanaoshabikia vyama vya upinzani kushindwa kuchangia maendeleo katika jamii wanamoishi jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma mchakato wa maendeleo.

Alisema lazima vyama hivyo vibadilike na kuanza kuwashawishi wananchi waweze kushirki kikamililifu katika shughuli za maendeleo badala ya wao kuwa vikwazo kwa kigezo cha kupaka matope CCM.

"Matusi ya wapinzani kwa wana CCM yanayotolewa katika mikutano ya kampeni yapuuzwe kwa kuwa vyama hivyo  ni vichanga kisiasa," alisema na kutolea mfano wa vyama hivyo kuwa sawa na mtoto mdogo.

 

 

 

'Kuomba kura sawa  na kuomba ajira'

Na El-hadji Yuusuf, Tabora

KUOMBA  kura katika kampeni za uchaguzi mkuu ujao ni sawa na kuomba ajira, hivyo ni muhimu waombaji kura kuanisha uzoefu, elimu, mafanikio na mipango yao kwa jamii ili kuwezesha kupatikana kwa viongozi bora.

Hayo yameelezwa na Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Tabora Mjini, Dk. Ahmed Kassim Aziiz, hivi karibuni, katika uzinduzi wa kampeni za kuwania udiwani kwa tiketi ya CCM katika Kata ya Kanyenye, mjini hapa.

Dk. Aziiz alisema katika kampeni, wakati wa kuomba kura jamii inapaswa kuwapima wagombea kwa kuzingatia uzoefu, elimu, mafanikio na mipango yao kwa kuwa kuomba uongozi ni kuomba kazi, hivyo vigezo hivyo ni muhimu vikazingatiwa daima.

Aliwataka wananchi wawapime wagombea na vyama vyao kwa vigezo hivyo ambapo alisema kuwa CCM inajivunia uzoefu wa miaka 40 ya kuongoza Serikali ikiwa ni pamoja na mafanikio lukuki yanayoonekana sambamba na mipango madhubuti na makini iliyowekwa katika kuboresha uchumi.

Alisema CUF imekuwa ikidai kuwa haki sawa kwa wote, lakini haiwatendei haki wananchi wa Zanzibar, wenye asili ya bara kutokana na kuwakatalia kupiga kura wakiwa Zanzibar kwa madai kuwa si Wazanzibar, ambapo alidai kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya kimsingi.

Naye, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Juma Abdallah, alisema ushindi wa chama ama wagombea katika uchaguzi hautokani na ubabe, matusi, na maneno ya kebehi bali unatokana na kukubalika kwa sera, msimamo na mipango ya chama husika.

Aliwahimiza wananchi wahudhurie kwa wingi katika mikutano ya kampeni ya uchaguzi ili kuwasikiliza wagombea na kuwapima uwezo wao kupitia sera, uzoefu, elimu, mafanikio na mipangilio.

Katika uzinduzi wa kampeni hizo katika kata hiyo, William Maswa Sizya, alinadiwa rasmi kugombea nafasi ya udiwani kwa tiketi ya CCM, ambapo ameelezwa kuwa mtumishi mwaminifu.

 

 

 

Serukamba asema Serikali ya mseto ni ndoto kwa sasa

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

MGOMBEA ubunge katika jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya CCM, Peter Serukamba, amesema ni ndoto kuundwa kwa Serikali ya mseto kwa sasa kutokana na hali ya upinzani ilivyo nchini.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika Soko la Buzebazeba Ujiji mjini hapa, mgombea huyo alisema serikali ya mseto inawezekana iwapo tu wapinzani wanaweza kupata kura zinazokaribiana na zile itakazopata chama tawala.

Alisema kuwa uwiano wa asilimia zaidi ya 75 za CCM na zinazobaki wanagawana wapinzani ni ndoto kwao kuweza kuundwa kwa serikali ya mseto jambo linaloonyesha kwamba vyama hivyo havikubaliki hata kwa wananchi.

Serukamba alisema jambo kubwa linalofanya vyama vya upinzani kukosa kuungwa mkono ni kwa sababu havina sera zilizo wazi zinaweza kukubaliwa na wananchi ambazo zitawahakikishia matatizo yao yanaweza kutatuliwa.

Mgombea huyo amewataka wapiga kura kuchagua kiongozi ambaye yuko tayari kujituma na kuwaondolea kero zao badala ya kuchagua kiongozi atakayegeuka kama mtalii anayezunguka dunia nzima pasi na kusikiliza matatizo ya wananchi wa jimbo lake.

Maneno ya mgombea huyo yamekuja siku chache kufuatia majigambo ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Dk.Walid Kabourou ambaye anatamba kuwa ni mbunge pekee wa kambi ya upinani aliyetembea nchi nyingi duniani.

Sambamba na hilo Mgombea huyo alisema elimu pekee haitoshi kumfannya mgombea awe kiongozi mzuri bali anatakiwa awe na hekima ili aweze kuwatumikia wananchi.

Naye mpiga debe mkuu wa mgombea huyo, Azim Premji, amewahoji wapinzani kuwa kinawauma nini kwa baadhi ya wagombea ubunge wa CCM kuachwa kwenye mchakato wa kura za maoni wakati wenyewe walioachwa hawasemi.

Premji ambaye aliwahi kuwa mbunge wa jimbo hilo alisema vikao vya chama ndivyo  vyenye uamuzi wa mwisho na wana CCM wamekubaliana navyo na kwamba hao wanaopiga kelele wanataka nini kama si kiherehere.