UHURU 17.10.2005
Mbowe ataka vijana wawe watumwa nje?
Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Freeman Mbowe amewashawishi Watanzania, hasa vijana, kurudi kuwa watumwa nchi za nje kwa madai kwamba Tanzania ni nchi ya dhiki.
Akihutubia mkutano wa kampeni juzi mjini Dar es Salaam, Mbowe alionekana kuwashawishi waliohudhuria mkutano wake huo ili waamini kuwa wataishi maisha bora zaidi wakichuliwa kwenda kuwa watumwa nchi za nje, akidai kwamba Tanzania ni nchi ya dhiki.
Mbowe alitoa ushawishi huo na kusababisha baadhi ya vijana wachache kuunga mkono kauli yake kwa kuonyoosha vidole alipowataka kufanya hivyo iwapo waliiona kauli yake ni barabara. Alikuwa anahutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe.
“ …Enzi zile walikuwa watu wakipandishwa meli kuchukuliwa kwenda kuwa watumwa nchi za nje…kitendo hiki tukilichukia sana… lakini sasa jamani nchi hii ilivyo na dhiki eti mkiambiwa mchukuliwe kwenda kuwa watumwa hivi sasa si mtakubali?” alisema Mbowe.
“…nasema hivi sasa kina mama, vijana na wazee wanateseka na kuishi kwa dhiki…hebu wanaokubali kuwa afadhali kuchukuliwa kwenda kuwa watumwa nchi za nje wanyooshe mikono” alisema Mbowe.
Baada ya kutamka hivyo, waliokuwa wakimsikiliza walionyesha kuduwaa kwanza, lakini kwa kuwa waliokuwa mbele ya jukwaa karibu wote walikuwa wanachama au mashabiki wa Chadema ilibidi wanyooshe mikono hali iliyoashiria kutotaka kupinga kauli ya mgombea wao.
Mkapa na Guebuza wazindua ujenzi wa Daraja la Umoja
Na Maura Mwingira, Masasi
RAIS Benjamin Mkapa
RAIS Benjamin Mkapa na mwenzake, Armando Guebuza wa Msumbiji jana waliweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma litakaloziunganisha nchi hizi mbili na kuwataka wananchi wa pande zote kulitumia kujikomboa kiuchumi.
Jiwe la msingi kwa upande wa Tanzania liliwekwa katika kijiji cha Mtambaswala, katika Wilaya mpya ya Nanyumbu, na baadaye wakavuka upande wa pili wa mto na kuweka jiwe katika kijiji cha Nagomane, katika mkoa wa Cabo Delgado, Msumbiji Sherehe ya uwekaji mawe ya msingi iliyohudhuriwa na wananchi toka pande mbili za Tanzania na Msumbuji, ilitanguliwa na utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja hilo uliofanywa kati ya makatibu wakuu wa Wizara za Ujenzi na Mkandarasi toka Kampuni ya China – Geo huku wakishuhudiwa na Marais Mkapa na Guebuza.
Gharama ya ujenzi wa daraja hilo hadi kukamilika inakadiriwa kuwa dola za Marekani milioni 29.9. Tayari Tanzania na Msumbiji zimekwishatenga fedha kupitia bajeti zao dola milioni 8 kila moja.
Kuanza kujengwa kwa daraja hilo kunakamilisha kiu na dhamira na utashi wa kisiasa ulioonyeshwa na Rais Mkapa na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano, ambao mwaka jana walitia saini mkataba wa ushirikiano wa kulijenga daraja hilo kwa kutumia fedha za kodi ya wananchi badala ya kutegemea wahisani ambao ilibainika hawakuwa tayari kufadhili ujenzi huo.
Pia kuanza kwa ujenzi kunakamilisha ndoto ya waasisi wa mataifa haya mawili, marehemu Julius Nyerere na Samora Mashel ambao mwaka 1975 waliamua kulijenga daraja hilo kwa kutumia mapato ya serikali zao.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi ya Tanzania, daraja hilo linatarajiwa kukamilika katika miezi 36 ijayo.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Mkapa alitoa changamoto kwa wananchi na Msumbiji kuwa ujenzi wa daraja hilo uwe ni kichocheo cha kuamsha ari miongoni mwao ya kujikomboa kiuchumi ili kuupiga vita umaskini.
Alisema ni matarajio yake kwamba watendaji wakuu wa serikali zote mbili katika ngazi ya taifa, mikoa na wilaya watafanya hima kutayarisha mipango ya maendeleo ya uwiano katika ngazi hizo kwa lengo la kuzalisha kwa wingi na kuongeza ushirikiano wa kibiasahra na uhusiano wa kitamaduni kati ya wananchi wa pande hizo mbili.
“Kwa vyama vya CCM na FRELIMO, ambavyo bado ninaamini vingali ni vya ukombozi na ikiwa hizi ni zama za kuchochea kukua kwa uchumi na kuupiga vita umaskini, natoa wito wa kuendelea na wajibu wenu wa kihistoria wa kuwaandaa wananchi kushiriki na kufanya kazi kwa bidii katika kutekeleza mipango ya maendeleo itakayopangwa,” alisisitiza Rais Mkapa.
Aliahidi kuwa kwa vile serikali ya Tanzania ndiyo iliyopewa jukumu la kusimamia kazi ya ujenzi wa daraja hilo itakuwa makini kutekeleza vipengele vyote vilivyokubaliwa katika mkataba na kwamba itaendelea kila mwaka kutenga fedha katika bajeti yake hadi ujenzi utakapokamilika.
Kwa upande wake, Rais Guebuza alisema anajisikia mwenye faraja sana kona wananchi wa pande hizo mbili wakijumuika kama dada na kaka katika sherehe hiyo.
Alisema hivyo ndivyo Afrika inavyotakiwa kujengwa. “Afrika ambayo wananchi wake wanajisikia wameungana na mipaka yao inakuwa wazi,” alisema.
Alitoa mwito kwa serikali hizo mbili kuwatia moyo wafanyabiashara wa pande zote mbili kulitumia daraja hilo kufungua milango ya biashara na uwekezaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi wa Tanzania, John Magufuli, alisema awali kuwa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa mita 720 litakuwa na njia ya waendao kwa miguu na waendesha baiskeli. Alisema kuwa katika upande wa daraja hilo kutajengwa barabara yenye urefu wa kilomita tano kwa kiwango cha lami.
Magufuli alisema barabara ya Mtwara – Masasi hadi kijiji cha Mtambaswala linakoanzia daraja hilo sasa haitakuwa ya mkoa bali barabara kuu ambayo itajengwa kwa lami.
Alisema serikali ya Japan imeonyesha nia ya kuijenga barabara hiyo ambayo itaungana na ya Tunduru kwenda Songea hadi Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa. Ujenzi wa barabara hizo na Daraja la Umoja ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa uendeshaji wa Ukanda wa kibiashara wa Mtwara.
Baada ya sherehe hiyo, Marais Mkapa na Guebuza walikwenda katika eneo la Naliendele mjini Mtwara kuweka mashada ya maua katika makaburi walimozikwa wanajeshi waliopigana katika vita vya kuikomboa Msumbiji.
Rais Guebuza aliondoka hiyo jana kurudi Msumbiji na Rais Benjamin Mkapa yuko mjini Mtwara ambapo leo ataagwa rasmi na wananchi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, shughuli itakayofanyika kwenye uwanja wa Umoja, mjini Mtwara.
Kikwete aahidi dawa kwa uharamia Ziwa Victoria
Na Florian Kaiza, Nansio
MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete
MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amewaonya majambazi katika Ziwa Victoria, hasa visiwa vya Ukerewe na Sengerema, kwamba endapo atachaguliwa mwisho wao utakuwa mwakani.
Alisema moja ya mikakati atakayotumia ni kuimarisha jeshi la polisi katika uendeshaji wa doria za ziwani nyakati zote.
Kikwete alisema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Gertruda Mongela, mjini Nansio, Ukerewe.
Alisema kwamba atawawezesha wananchi kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao, hasa wavuvi, ambao alisema wataundiwa utaratibu utakaowapa fursa ya kupata mikopo yenye masharti nafuu.
Naye Thomas Mtinge anaripoti kuwa Kikwete amesema atahakikisha anaunda serikali yenye mchanganyiko wa watu wenye maarifa na uzoefu mbalimbali, na si lazima kuwe na vijana wenye umri mdogo.
Alisema atakaowateua iwapo ataunda serikali lazima wawe wanaipenda nchi kwanza, wenye utaifa, wachapa kazi na wenye huruma kwa wanyonge na kwamba wanawake pia watakuwemo.
Kikwete aliyasema hayo juzi katika kipindi maalum cha mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star cha mjini Mwanza mara baada ya kuhutubia umati mkubwa kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM uliyofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba.
Mgombea huyo alikuwa akihojiwa na waandishi waandamizi Nathan Lwehabura na Nkwabi Ng’wanakilala.
Hata hivyo, alisema kwa sasa hajafikiria sana suala la kuunda serikali bali anachokifanya ni kuhakikisha kwamba CCM itashinda katika uchaguzi huo.
Alisema suala la kuunda serikali halina shida kwa sababu kazi hiyo hataifanya peke yake bali kwa kushirikiana na viongozi wenzake ambao pia wana uzoefu na upeo mkubwa wa kutoa maamuzi kama hayo.
Aliyeiba mtoto amuomba RPC amuombee msamaha asiachike kwa mumewe
Na Selina Wilson,Kibaha
MWANANMKE aliyekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga wa kiume katika hospitali ya Tumbi mjini Kibaha amemwomba Kamanda wa polisi mkoani Pwani amwombee msamaha kwa mumewe Ayoub Kabalata ili asimwache.
Vumilia Jacob (25) alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akihojiwa na kamanda huyo wa polisi wa mkoa Ally Mbilikira kuhusiana na wizi huo ambao yeye mwenye alikiri.
Akibubujikwa na machozi, Vumilia alisema anaomba asamehewe kwa kuwa kitendo alichofanya ni cha kinyama na cha aibu na ni dhambi kubwa mbele za Mungu lakini hakuwa na nia mbaya kwa mtoto huyo wa Sofia Mohamed Mkazi wa Vikuge wilayani Kibaha.
"Kamanda naomba unisamehe na nipo chini wa miguu yako nakuomba uniombee msamaha kwa mume wangu asije akaniacha kwa kosa hili nililofanya kwani nampenda sana na ninapenda kuwa na mtoto lakini sijabahatika kumpata," alisema mwanamke huyo.
Hata hivyo, kamanda Mbilikira alisema pamoja na kukiri kosa lake ni lazima ufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini sababu za kuiba mtoto huyo na baadae atafikishwa mahakamani huko ndiko watatoa uamuzi .
Kamanda Mbilikira alimuuliza mume wa mwanamke huyo Kabalata kwamba ni kwanini alikuwa akitoa huduma za maziwa na kuhudumia mzazi wakati ana uhakika mkewe hakuwa na ujauzito, na kwa nini hakuripoti polisi.
Kabalata alieleza kwamba alishinikizwa na wazazi wake ambao waliamini kuwa mtoto huyo ni wake na lazima awajibike vinginevyo wangempeleka polisi.
Alisema kutokana na vitisho alilazimika kutoa huduma lakini alikuwa na shaka juu ya mtoto huyo wa kiume.
Aliongeza kuwa hayuko tayari kuendelea kuishi na mwanamke huyo kwa ni amemsababishia balaa na kumtia aibu kubwa huko kwao wanakoishi na maeneo yote anakojulikana.
Kabalata alimtaka mkewe huyo aendelee na ustaarabu wake kwani yeye ameshapata mwanamke mwingine anayeishi naye.
VETA kujenga chuo cha kilimo na ufugaji
Na Lauden Mwambona, Singida
MAMLAKA ya vyuo vya ufundi nchini (VETA) inatarajia kujenga chuo cha kufundishia masuala ya kilimo na ufugaji mkoani Singida ili kuwezesha wakulima na wafugaji kufanya kazi zao kitalaamu.
Chuo hicho kitajengwa mkoani hapa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na kwamba tayari maandalizi ya awali kutafuta eneo la kujenga chuo hicho yanayendelea kutekelezwa.
Hata hivyo, gharama za ujenzi wa chuo hicho bado hazikupatikana mara moja, lakini chuo hicho kitalenga kutoa mafunzo ya ufugaji na kilimo cha kisasa zaidi.
Mkurugenzi wa VETA kanda ya kati Hidegardis Bitegera alipoulizwa juu ya suala hilo akiwa Singida kuhudhuria maonyesho ya bidhaa za viwandani yaliyoandaliwa na Shirika la viwanda vidogovidogo (SIDO) wiki iliyopita, alisema ni kweli mpango huo upo mbioni na kwamba taarifa zaidi zinaweza kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Kasungu.
Mkuu wa Mkoa Halima hakuweza kupatikana kutokana na kutingwa na ugeni uliokuwepo mwishoni mwa wiki, lakini Ofisa mmoja wa mkoa alikiri kuwepo kwa mpango huo na kuongeza kwamba VETA inahitaji hekta 100 ili kujenga chuo hicho.
Alisema Oktoba 10, mwaka huu, Mkuu wa mkoa huo akiwa na Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo Profesa Juma Kapuya na Mkurugenzi Mkuu wa VETA walifanya kikao mjini Singida ili kujadili suala hilo ambalo kimsingi limekubaliwa.
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema miaka kadhaa iliyopita VETA iliomba hekta 33.5 ili kujenga chuo kidogo cha aina hiyo, lakini sasa inaomba hekta 100 ili kujenga chuo kikubwa ambacho kitakuwa cha kisasa na huduma mbalimbali za utalaamu wa ufugaji na kilimo.
VETA kwa sasa ina vyuo 20 vikiwemo vyuo 10 vikubwa ambavyo vinafundisha mambo mbalimbali ya ufundi yakiwemo uashi, useremala, ujenzi wa barabara, masuala ya hoteli, uchoraji na masuala ya kilimo yanafundishwa kwa uchache katika vyuo vidogo vodogo.
Mkurugenzi wa VETA kanda ya kati alitoa mfano wa vyuo vidogovidogo vya kilimo na ufugaji kuwa ni kile cha Makutupora ufundi ambacho ofisi yake ilisaidia kukipatia chuo hicho ng'ombe wa maziwa wawili na madume matatu pamoja na vifaa mbalimbali vya ufugaji.
Ngawaiya: Kutomchagua Keenja ni sawa na kukataa maendeleo
Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya ameomba wananchi wa Ubungo kumchagua Charles Keenja kuwa mbunge wao na wasipofanya hivyo ni kukataa maendeleo.
Akihutubia mkutano wa kampeni wa ubunge uliofanyika juzi Kimara Mwisho, Ngawaiya alisema Keenja anagombea tena ubunge katika jimbo hilo ili kumalizia kazi aliyoifanya kwa maendeleo ya wananchi na siyo kwa manufaa binafsi.
Ngawaiya alisema Keenja ameonyesha kwa vitendo kuwa ni mtumishi wa watu kutokana na mambo mengi aliyoyafanya tangu alipokuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam na sasa Mbunge na Waziri wa Kilimo na Chakula.
Alisema alipokuwa Tume ya Jiji alifanya maajabu kwa kujenga barabara katika sehemu mbalimbali za jiji ambazo wananchi walikata tamaa kuwa hazitajengwa kamwe.
Mbali na kujenga barabara, alisema, Keenja alijenga mfumo wa uwajibikaji na utendaji kazi katika Jiji ambao unafuatwa hadi sasa ili kuleta maendeleo ya wananchi.
Mbunge huyo wa zamani aliyejiunga na CCM akitokea TLP, alisema katika Wizara ya Kilimo na Chakula Keenja ameiweka sekta ya kilimo kwenye chati ya juu tofauti na iliyokuwa zamani.
Alisema hivi sasa serikali imetangaza kuwa ina akiba ya chakula ya kutosha pamoja na ziada inayouzwa nje ya nchi, yote hiyo ikiwa juhudi ziliyofanywa na Keenja.
“Yote hii inaonyesha kwamba Keenja ni lulu kwa hiyo kumchagua ni sawa na kuokota dhahabu katikati ya Kariakoo, jambo ambalo halitatokea daima,” alisema.
Katika nafasi ya ubunge, Ngawaiya alisema Keenja kwa kushirikiana na madiwani amehakikisha adha ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi imepungua. Pia alisema huduma mbalimbali kama vile elimu, afya na miundombinu vimeimarishwa katika miaka mitano iliyopita jimboni humo.
Kwa upande wake, Keenja aliwaomba wananchi kumchagua tena ili kutekeleza ahadi zake alizozitoa nyingi zikiwa zimeshaanza kufanyiwa kazi.
Alitaja ahadi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule za sekondari kila kata kama inavyoeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, huduma za maji na afya karibu na wananchi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa maendeleo ya jamii, Wanawake na Watoto, Dk. Asha Rose Migiro, mgombea udiwani wa Kimara Mahmoud Mringo na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Kleyst Sykes.
Kagasheki atoa ahadi ya gari la wagonjwa hospitali ya mkoa
Mrema aponda matumizi ya helikopta kwenye kampeni
Na Peter Orwa, Bukoba
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Balozi Khamis Kagasheki, ameahidi iwapo atachaguliwa ataanza kazi kwa kuwapatia wananchi hao gari la wagonjwa la kisasa, katika Hospitali ya Mkoa iliyopo mjini hapa.
Kagasheki alitoa ahadi hiyo juzi jioni katika mkutano wa kampeni, uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Hamgembe, ambapo umati ulifurika kumsikiliza, huku akimtaka mbunge anayemaliza muda wake Wilfred Lwakatare (CUF) aache kuwalaghai wapiga kura wake.
"Gari hili litafika kwa huduma ya wananchi na kutakuwepo na simu, ukipiga unajibiwa," alisema Balozi Kagasheki.
Siku hiyo pia kulikuwa na mikutano mingine ya kampeni mjini hapa, ambapo mgombea Urais wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alikuwa katika uwanja wa Uhuru na Lwakatare alikuwa katika eneo la Kagondo.
Huku akishangiliwa na watu, mwanadiploamasia huyo mstaafu ambaye pia ni mfanyabishara wa mjini hapa, alisema pia anatazamia kuleta mabadiliko ya kuboresha vifaa katika hospitali hiyo.
Alisema ameshaanza kufanya mambo mengine ya maendeleo kabla ya hata kuchukua fomu za ubunge, ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa kigeni kuona uwezekano wa kuboresha uwanja wa ndege wa mjini hapa, ambapo hadi sasa hauna lami.
Alikishangaa chama cha CUF kubeza juhudi zake hizo, huku akitaka vyama vya siasa mjini hapa kutotumia chuki na kejeli badala yake sera ndiyo itawale na wananchi wapate chaguo lao sahihi Kagasheki alimtaka mbunge anayetoka madarakani- Lwakatare, awape wananchi haki yao kwa kuwaleza wananchi wa jimbo hilo, amewafanya nini, badala ya kuendesha siasa za chuki na fujo.
" Nasema bwana mdogo (Lwakatare) awaeleze vitu gani amefanya katika miaka mitano hii na si kuweka vipeperushi," alisema na kuongeza: "Kiongozi yeyote anachaguliwa kutokana na rekodi yake nasema bwana mdogo huyu naye achaguliwe kwa rekodi yake.
"Wapo wabunge katika mkoa huu wameandika vitabu kuonyesha wamefanya kitu gani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa mfano Dk. Kamala (Diodorus) ameandika kitabu kuhusu mambo aliyoyafanya kama mbunge wa Nkenge.
"Karamagi (Nazir) ameandika ripoti ya kazi yake. Chato, (John) Magufuli, ameandika ripoti ya kazi yake, lakini ripoti ya Bukoba Mjini tumetafuta lakini wapi!"
Alimshutumu Lwakatare kwa kuwahadaa wapiga kura wake kuwa alisaidia kuwezesha wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata mafao yao na ujenzi wa hoteli ya Workguard ya mjini hapa.
Balozi huyo, alisema kama mgombea mbunge ana haki ya kumkosoa mwenzake, hivyo alihoji tabia ya Lwakatare,
kufanya kampeni za kulala katika kila kata mwaka 2000 alipokuwa anawania ubunge na kufanya hivyo tena mwaka huu, huku miaka ya katikati kuadimika hadi kampeni nyingine. Wakati huo huo, mgombea Urais kwa tiketi ya TLP, Augustine Mrema, juzi alielekeza mashambulizi kwa mgombea Urais wa Chadema, Freeman Mbowe, akisema helikopta anayoitumia haina maana yoyote kwa maisha ya Mtanzania na nafasi ya Urais.
"Mtu atakuja na helikopta'pata-pata-pata, sawa! Unapoenda kuchagua si helikopta, ila ni maisha yako," alisema Mrema na kudai kuwa hadi sasa yeye ndiyo anaongoza katika kukubalika katika mbio za Urais.
Katika hali iliyozua kicheko kutoka kwa waliohudhuria mkutano huo katika uwanja wa Uhuru, walimshangaa, alipowaorodhesha wanaofuatia "kwa mbali" kuwa ni Jakaya Kikwete (CCM), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Mbowe. Aliwaponda waliobaki kwa kauli "hata siwajui".
Mrema pia aliwashukuru wananchi kutokana na kile alichokitaja kama "kumvalisha nguo" kutokana na watu kutarajia kuwa asingepata watu kusikiliza mkutano wake. Hata hivyo mkutano huo haukuhudhuriwa na watu wengi, wala hakukuwa na shamshamra zaidi.
Walioshindwa kura za maoni waambiwa hawana sababu ya kuendelea kununa
Na Angela Sebastian, Bukoba
MJUMBE wa Kamati Utekelezaji ya Jumuia ya Wazazi mkoa wa Kagera Juma Mutatya alisema wanachama ambao hawakufanikiwa kupitishwa katika kura za maoni hawana sababu ya kununa.
Mutatya aliyasema hayo juzi katika mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge katika jimbo la Muleba kaskazini kupitia tiketi ya chama hicho Ruth Msafiri katika viwanja vya kata Mayondwe.
Alisema yeye alikuwa mmoja wa wagombea wa kiti cha ubunge kupitia CCM katika jimbo la Muleba Kusini lakini hakuchaguliwa . Alisema kuwa watu hao walikuwa na haki ya kusikitika kwa sababu hawakufanikiwa ila wangeyachukulia matokeo hayo kama jambo la kawaida na kuungana na wenzao wa CCM na sio kukimbilia vyama vingine.
Alisema kuwa yeye alifuatwa na Mzee Christopher Ngaiza anayegombea katika jimbo hilo kupitia CHADEMA na kumweleza kuwa kwakuwa wameshindwa katika kura za maoni kwa hiyo wahamie CHADEMA .
"Kwa sababu mimi sitaki unafiki maana CCM ilinisomesha mpaka sasa mafanikio haya niliyo nayo ni CCM, nilimjibu kuwa kushindwa katika kura za maoni sio kununa na kukimbilia vyama vingine kilichopo nikujiunga na wenzetu ili tuweze kuipatia CCM ushindi wa kishindo" alieleza Mutatya.
Wakati huo huo, Katibu Mwenezi wa CCM mkoani Kagera Medard Mushobozi aliwaeleza wananchi kuwa uchaguzi si lelema na si mchezo wa kulala ni sawa na vita kwa hiyo amewashauri kupigana kikamilifu ili waweze kushinda kwa kishindo kwa kuwapata viongozi kupitia CCM.
Akihutubia mkutano huo, mgombea wa kiti cha ubunge kupitia tiketi ya CCM katika jimbo la Muleba Kaskazini Ruth Msafiri aliwaomba wananchi kumpa kura ili aweze kutatua matatizo ya wananchi wa jimbo hilo.
Ruth alisema wakati huu wananchi wanapaswa kuangalia kiongozi anayefaa katika kuwaletea maendeleo ya jimbo na sio yule anaye shinda akipiga kelele bila kufanya lolote.
Tuondoe tofauti zetu ili CCM ishinde – Chami
Na Rodrick Makundi,MoshiMGOMBEA ubunge wa Moshi Vijijini kupitia CCM,Dk.Cyril
Chami amewataka wanachama katika jimbo hilo kusahau tofauti zao na wamchague kwa kuwa ana uhakika wa kuwawakilisha bungeni kwa umakini zaidi.
Alisema kwamba wakati wa kampeni wapinzani wamekuwa wakijenga hoja kwamba katika jimbo hilo wabunge wake wote ni kutoka sehemu moja hivyo kuna kila sababu ya kuchagua mtu wa eneo jingine.
Kufuatia hoja hiyo ya wapinzani Dk.Chami aliwataka wananchi kutambua kwamba wabunge waliotangulia walikuwa wa upinzani na vyama vyao havikuwawezesha katika kuwaletea wananchi wao maendeleo.
Alisema kwamba hiyo ni hoja ya kuwashawishi wananchi wa Moshi vijijini wasichague CCM na badala yake wawape tena wapinzani ambao kwa miaka kumi iliyopita hawakuweza kufanikisha shughuli za maendeleo kwa wananchi wao.
Akitolea mfano kwa wabunge Thomas Ngawaiya aliyekuwa mbunge kupitia TLP na Ngotolainyo kupitia NCCR-Mageuzi,ni wabunge waliopigiwa debe na Augustine Mrema aliyekuwa kiongozi wao na baada ya kuingia madarakani waliachwa wakihangaika wenyewe na hata kukosa fedha kwa ajili ya kutekeleza ahadi zao.
Alisema hivi sasa wananchi hao wanapaswa kutambua kwamba waliojitokeza kuwania kugombea katika jimbo hilo wakati wa kura za maoni hivi sasa wako naye bega kwa bega kuhakikisha kwamba CCM inashinda Oktoba 30,mwaka huu.
"Nikiingia bungeni sitaenda kama mbunge wa Kibosho nitaenda kama mbunge wa Moshi vijijini, wapinzani wanatumia hiyo hoja lakini ieleweke CCM hatuna zamu ya kupeana uongozi kwa maana ya maeneo," alisema Dr.Chami.
"Hili liko wazi, Ngawaiya ni mtu wa karibu sana anakuwa nami kila kona na hata Gaudience aliyeshiriki kura za maoni amehamasisha vijana wake kuichagua CCM, Mkuu wa Wilaya ya Rombo naye ameahidi kutoa ushirikiano wa kuipigia debe CCM ili ishinde,Orauya naye hivyo hivyo," aliongeza Chami.
Pia alipongeza jitihada zilizofanywa na mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo Ngawaiya na kwamba aliwezesha kuleta maendeleo na jukumu lake baada ya kushinda ni kuendeleza maendeleo hayo.
Aliwataka wanachama wa jimboni humo kutambua kuwa hoja za wabunge wa chama kimoja bungeni ndizo zinazopewa uzito hasa wabunge wanapowasilisha hoja za kuboresha miundombinu kwenye majimbo yao.
"Pato la serikali linatokana na kodi za wananchi bila kujali chama na pato hilo haliwezi kutosheleza kila sehemu,maamuzi ya ugawaji wa pato hilo yanafanywa na bunge hivyo idadi kubwa ya wabunge ndiyo inayofanya hoja za maendeleo kutekelezwa," alimalizia.