UHURU 18.09.2005
Viongozi wa dini walaani mauaji ya Manzese
Ni wa kiislamu na kikristo
Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa dini za kikristo na kiislamu wametoa tamko la kulaani ya mauaji ya watu watano yaliyotokea Manzese Midizini, Dar es Salaam, na kuwataka wanasiasa kufanya kampeni za amani.
Tamko hilo lilitolewa jana walipokutana katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu nchini (TEC), Kurasini, kwa kushirikana na wadau wa usalama mkoani Dar es Salaam, kujadili amani ya nchi kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Mauaji katika Kata ya Midizini, Manzese yaliwakuta Katibu Mwenezi wa CCM Tawi la Midizini na motto wake na wajukuu zake ambao vifo vyao vilitokana na nyumba yao kuchomwa moto usiku wa manane.
Watu waliouawa ni Katibu Mwenezi Mwajuma Nyanza (53), Mwajuma Rashid (16), Sambali Luciani (11), Daniel John (3) na Asha Rashid (13).
Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, akiwasilisha mada kikaoni kuhusu hali ya usalama mkoani, alisema uchunguzi wa polisi hadi sasa haujapata ushahidi kuthibitisha tukio hilo ni la uhalifu wa kisiasa.
Tibaigana alisema vigezo vya upelelezi wa polisi haviongozwi na yanayosemwa mtaani, bali vielelezo vinavyopatikana kupitia upelelezi. Kwa mujibu wa Tibaigana, katika tukio la Manzese, watu sita walishatiwa mbaroni na polisi, mmoja aliachiwa na watano waliobaki wameshafikishwa mahakamani.
Tamko lililosomwa na Mratibu wa Programu ya Haki za Binadamu ya Jumuia ya Kikristo nchini (CCT), Hubert Lubyana, lilisema:“ Tunatoa wito kwamba kampeni za siasa ziendeshwe kwa kufuata taratibu na kanuni kama zinavyosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”
Mkutano huo uliongozwa na Askofu mstaafu Elinaza Sendoro na ulifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Baraka Konisaga, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba.
Wengine waliohudhuria ni viongozi mbalimbali wa dini, akiwemo mwenyekiti wa mtandao huo wa viongozi wa dini katika kutafuta amani mkoani Dar es Salaam, Sheikh Ali Hamisi kutoka Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA) na maaskofu kadhaa.
Akitoa hoja mkutanoni hapo, Askofu Alex Malasusa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alisema uzoefu umeonyesha kuwa mara kwa mara kinapofikia kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu, kuna mazoea ya kutokea matukio ya namna hiyo.
Askofu Malasusa alimsifu Kamanda Tibaigana kwa kufanya kazi katika mtazamo wa kitaalamu zaidi, kuliko katika mtazamo wa kisiasa au mingine inayofanana nayo.
Kwa upande mwingine, mkuu wa wilaya ya Ilala, Seif Mpembenwe, alisema uzoefu alio nao mkoani Dar es Salaam, hasa wilayani Temeke, ikiwemo katika uchaguzi wa mwaka 2000, baadhi ya misikiti na makanisa yamekuwa yakitumika mno kuhubiri siasa.
Mpembenwe, huku akitumia mifano ya uzoefu wake wa kushiriki vita kama askari, alisema kuwa kuna haja ya wanasiasa kutowatumia viongozi wa dini na viongozi hao nao wawe macho kutotumiwa. Hoja hiyo nayo imo katika tamko la viongozi hao wa dini.
Akifungua mkutano huo, Askofu Sendoro ambaye ni mwenyekiti wa taifa wa mtandao huo wa kidini ulioanzisha nyendo zake mwaka 2001, alisema kikao cha jana kiliitwa makusudi kukutanisha viongozi wa kidini kuzunguzia mustakabali huo, kutokana matukio ya kihalifu yanayoripotiwa kuhusishwa na kisiasa.
Baadhi ya maeneo yanakotokea matukio hayo kwa mujibu wa Askofu Sendoro ambaye ni mstaafu wa KKKT, Karatu, Dar es Salaam na Shinyanga na Zanzibar. Pia wamaezimia kuwaita viongozi wa kisiasa ili kukutana nao.
Kamanda Tibaigana akioanisha hali ya siasa na uchaguzi, alivishangaa baadhi ya vyama vya siasa kuwa na tabia ya kupiga wapenzi wa vyama vingine wanapoenda katika miktutano yao na kusema huko ni kuwanyima haki na polisi inaposhuhudia hali hiyo itawachukulia hatua mara moja.
Kwa upande mwingine, Tibaigana ambaye wakati wote alikuwa anajitambulisha kama mtaalamu wa masuala ya usalama, aliwaonya baadhi ya mashabiki wanaotumuia vibaya mazingira ya umma kukweza matakwa yao kisiasa, kisha inapotokea matatizo wanakimbilia polisi waache mara moja. Alitoa mfano wa nyumba ya wakazi wengi wenye itikadi tofauti.
Wakati huohuo, Tibaigana jana alitumia fursa hiyo kukanusha madai yaliyozushwa dhidi yake kutokana kukaa kwake katika jukwaa juu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya CCM kitaifa, kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, kwamba yeye ni shabiki wa Chama Cha Mapinduzi.
“Licha ya kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais (Benjamin Mkapa) ni Rais. Urais wake hauondoki, hivyo mimi nilikuwa pale kumsindikiza. Mimi ni kiongozi na kukaa kwangu juu ni halali, lakini wasisahau mimi ni mpiga kura…halafu nikikaa pale askari wangu wananiona hivyo wanafanya kazi,” alisema Tibaigana.
Alivielekezea ‘kidole’ vikundi vinavyotoa elimu ya uraia kwamba huenda kazi zao hazijafanikiwa na ndiyo maana uelewa wa kutofautisha majukumu unakuwa mdogo na akaongeza: “Sasa itakapokuwa chama kingine kimenikaribisha sijui watasemaje?”
Wanyonge watarahisishiwa kupata mikopo - Kikwete
Na Bashir Nkoromo, Kasulu
MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, amesema serikali yake itatengeneza utaratibu utakaowezesha wanyonge kupata mikopo.
Kikwete, ambaye jana alikuwa mkoani hapa kwa siku ya pili, alisema mkakati huo umelenga kuwawazesha vijana na wanawake kujiajiri.
Mgombea huyo wa CCM alisema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Umoja, mjini hapa.
Alisema kufanya hivyo kutawawezesha vijana ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali kuweza kupata mikopo ambayo itawawezesha kuboresha shughuli zao kama kilimo, ususi na shughuli zingine mbalimbali zinazokwama kutokana na mitaji midogo.
Kikwete aliutaja utaratibu ho kuwa ni pamoja na kuthaminisha mali walizo nazo wanyonge kama nyumba au mashamba ili ziweze kuwa dhamana ya kupata mikopo benki.
Akizungumzia matatizo yanayoukabili mkoa wa Kigoma, alisema anayafahamu kuwa ni ukosefu wa umeme wa uhakika, maji na barabara na tayari kuna utaratibu wa kuyatatua.
Kikwete alisema akiwa rais atahakikisha vitu vyote hivyo vitatu vinashughulikiwa, ambapo mipango yake imeanza kufanyika
Ataka wakome kusingizia miradi ya serikali ni yao
Na Angela Sebastian, Bukoba
WAPINZANI wametakiwa kutotumia miradi iliyotekelezwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi cha serikali ya awamu ya tatu kama sera zao katika mikutano yao ya kampeni.
Imeelezwa kuwa hali hiyo imejitokeza katika mikutano ya baadhi ya viongozi wa upinzani kutumia miradi iliyotekelezwa na CCM katika serikali ya awamu ya tatu kwamba kelele za viongozi wao bungeni na wawakilishi wao (madiwani ) katika halmashauri ya wilaya ndizo zimesasababisha miradi hiyo kutekelezeka.
Waziri wa Nchi katika ofisi ya Rais na Utawala Bora, Wilson Masilingi, aliyasema hayo jana alipokuwa anahutubia katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni katika jimbo la Muleba Kusini ambapo amesimamishwa
tena kugombea ubunge.
Masilingi aliitaja miradi wanayoitumia wapinzani kujitangaza kuwa ni elimu, barabara, maji, miradi ya ujenzi wa zahanati na miundo mbinu.
"Naomba niwaleleze wananchi wa jimbo la Muleba kuhusu barabara inayotengenezwa kutoka Katobago ambayo wamekuwa wakiitumia kuwa wao ndo walioomba pesa kwa
ajili ya kuitengeneza.
“… Si kweli pesa niliomba mimi mwenyewe kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya na mkoa wa Kagera kwa kupitia ubalozi wa nchi ya Japan; tukapewa kiasi cha sh. milioni 126 ambapo zilikuwa hazitoshi kumaliza kutengeneza barabara hiyo," alisema Masilingi.
Alisema kuwa baada ya kupata msaada huo alimwomba balozi wa China nchini kumpatia mkandarasi aliyetengeneza barabara ya Muhutwe - Kagoma ili aweze kusaidia kutengeneza barabara hiyo.
"Sasa hiyo kama si mafaniko ya CCM ni nini? Halafu watu wanatoka pembeni na kusema kuwa ni jitihada zao kutokana na kitu kinachooneka? Na kwa hali hii naomba kura zenu kwa wagombea wote wa CCM kuanzia urais hadi udiwani," alisema Masilingi.
Aliwashauri wananchi wa jimbo hilo kutotukanana na wapinzani wala kujibizana nao maana hiyo si sera ya CCM, ila wawasikilize na kuzichambua sera zao na kuona
kuna ukweli gani na kuwauliza maswali.
Alitoa shukrani kwa waliokuwa wagombea katika kura za maoni, Khalid Kahuza na Juma Mtatya, kushiriki kumuunga mkono katika ufunguzi wa mkutano wa kampeni.
Na Maura Mwingira
RAIS Benjamin Mkapa alirejea nchini jana kutoka New York, Marekani ambako alikwenda kuhudhuria mkutano wa maadhimisho ya miaka 60 ya Umoja wa Mataifa.
Akiwa katika mkutano huo, Rais Mkapa alipata fursa ya kuhutubia na kusisitizia nchi wanachama kutekeleza ahadi walizozitoa miaka mitano iliyopita walipokuwa wakipitisha tamko la Malengo ya Maendeleo ya Millenia.
Rais Mkapa alisema kuwa hakuwahi kufikiria kuwa taasisi hiyo yenye heshima kubwa duniani inaweza kuwa na matatizo, si matatizo ya kutokubaliana kuuondoa umaskini, lakini kuwa na nia ya dhati ya kuupunguza umaskini angalau kwa nusu ifikapo mwaka 2015.
Alisema ingekuwa vema kwa nchi zinazoendelea kila moja ikafanyiwa tathmini kama nchi badala ya kufanya tathmini ya jumla, kaitka kuona kama nchi hizo zina mfumo wa utawala na uwezo wa kutumia misaada ziliyopewa.
Viongozi wengine waliozungumza katika mkutuno wa Baraza la Usalama na Umoja wa Mataifa ni Rais George Bush wa Marekani na Waziri Mkuu Tony Blair wa Uingereza, ambao wote kwa nyakati tofauti walisema kuwa wanaunga mkono juhudi zilizoanzishwa na Rais Benjamin Mkapa na kuzuia machafuko katika Afrika.
Kwa ujumla viongozi wote waliozungumza baada ya Rais Mkapa kuzungumza katika kikao cha Baraza la Usalama, walisisitiza kuunga mkono kwa bara la Afrika katika kila eneo, hasa la kuzuia machafuko na kuongezewa misaada.
Akiwa New York Rais pia alizungumza katika uzinduzi wa Tume ya Kimataifa itakayoratibu urasilimishwaji wa kisheria mali za wanyonge. Rais Mkapa ni miongoni mwa wajumbe wa Tume hiyo, ambayo wenyeviti wenza wake ni Madeleine Albright na Profesa Hernando de Soto.
Mapokezi makubwa yamsubiri Mama Kikwete Mbeya kesho
Na Idefonce Mgimba, Mbeya
MKE wa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Salma Kikwete, atafanya ziara ya ya kampeni ya siku mbili mkoani Mbeya kuanzia kesho.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa CCM wa mkoa wa Mbeya, Sylvester Kikungwe, zilisema kuwa Salma atapokewa katika mpaka wa Mbeya na mkoa wa Rukwa saa tatu asubuhi katika kijiji cha Mkutano, wilayani Mbozi ambapo jioni atakutana na wajumbe wa mabaraza ya UWT wa wilaya zote mkoani Mbeya.
Wengine katika mkutano huo, utakaofanyika katika ukumbi wa Benjamin Mkapa hapa ni wagombea wote wa udiwani kupitia viti maalum na wa majimbo, wazee wa Jiji la Mbeya ambao watawawakilisha wazee wenzao wa wilaya za mkoa wa Mbeya, wanawake kutoka kata zote Jijini Mbeya na viongozi wa ngazi mbalimbali za CCM wakiwemo mabalozi nyumba kumi.
Kikungwe alisema katika mkutano huo wa kampeni ya kukinadi Chama Cha Mapinduzi kwa ngazi ya Rais, wabunge na madiwani, Salma ataelezea umuhimu na nafasi ya mwanamke katika kufanikisha kampeni ya uchaguzi mkuu ujao ili kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi.
Akiwa mkoani Mbeya, kwa mujibu wa Kikungwe, Salma atakwenda wilayani Mbarali ambapo atakuwa na mkutano na wakazi wa wilaya hiyo watakaokutana mjini Rujewa kabla ya kuelekea mkoani Iringa kwa madhumuni kama hayo.
Kama ilivyokuwa wakati wa ziara ya mgombea urais, Jakaya Kikwete, akiwa katika ziara ya kampeni mkoani Mbeya ambapo alipata mapokezi makubwa kuwahi kupokewa kiongozi yeyote wakati wa kampeni, Salma ameandaliwa mapokezi makubwa na tayari kabla ziara yake iliyopangwa ianze leo kuahirishwa hadi kesho, mazungumzo katika mitaa mbalimbali jijini yanamtaja "Salma" "Mama Kikwete" ni CCM.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mkoani Mbeya unaonyesha kuwa upinzani una kazi ngumu ya kupata ushindi katika viti, hasa vya ubunge, kutokana na kutokuweka mtandao wa kutosha wa kukubalika, wakati kwa upande wa urais vyama hivyo havina nafasi.
Hali hiyo imeonyeshwa na mapokezi makubwa aliyopata Kikwete wakati wa ziara yake ya kampeni ambapo kila alikopita alielezwa kuwa hakukuwa na ulazima wa yeye kupoteza muda kupiga kampeni kwa kuwa tayari alishapata tiki ya kuingia Ikulu tangu alipotangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi Mkuu wa Chama mjini Dodoma.
Mwapachu aahidi kuimarisha uvuvi Tanga
Na Hamida Khalid, Tanga
MGOMBEA wa nafasi ya ubunge Jimbo la Tanga kupitia Chama Cha Mapinduzi, Bakari Mwapachu, amesema akichaguliwa tena atahakikisha anaimarisha sekta ya uvuvi pamoja na kuboresha mazingira yatakayosaidia kuwavutia wawekezaji.
Mwapachu alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Tangasisi, kijiji cha Machui.
Alisema katika kutimiza ahadi yake hiyo tayari ameshafanya mazungumzo na wafadhili mbalimbali ambao wamekubali kuja kuwekeza, hali itakayosaidia kuboresha maisha ya watu wa Tanga.
Kuhusu nia yake ya kuwania kiti hicho cha ubunge kwa mara nyingine, Mwapachu alisema kuwa hafanyi hivyo kwa lengo la kuboresha maslahi yake wala kutaka uwaziri ila anafanya hivyo ili kuweza kuwainua wananchi wa Jiji la Tanga kiuchumi na kuwaondoa katika umasikini.
Alisisitiza kuwa Jiji hilo lina rasilmali nyingi ambazo kama zikitumiwa vizuri na wananchi kuwezeshwa wataweza kupiga hatua za haraka katika maendeleo ambapo ili kufikia hatua hiyo alitoa mwito kwa wapigakura kutofanya makosa kwa kuwachagua wapinzani, watu aliosema kuwa wengi wao hawana uchungu wa kweli na maendeleo ya nchi hii.
"Huu si wakati wa kujaribisha uongozi...ni wakati wa kusukuma mbele maendeleo, hapa mtawaona wengi wanakuja, wengine bado ni wanafunzi wametoka shule wanawarubuni, likizo zao zikiisha wanaondoka kwenda masomoni nje ya nchi," alisema Mwapachu na kueleza kuwa yeye ndiye hasa anayejua uchungu wa watu wa Tanga.
Kwa upande mwingine, Mwapachu aliwataka wana CCM kuvunja kambi zao ili kuwezesha Chama kupata ushindi wa kishindo na kuongeza kuwa wote watakapokubali na kuwa kitu kimoja ndipo watakapoweza kupata baraka za Mwenyezi Mungu katika uchaguzi wa mwaka huu.
Kwa upande wake mgombea nafasi ya udiwani kupitia CCM wa kata ya Tangasisi, Mwakisua Kingi, alisema kuwa Viongozi wa vyama vya siasa wanaowakataza Wananchi kuchangia maendeleo wanapaswa kuogopwa kama Ukimwi kwa vile watu hao hawaitakii mema nchi hii.
Mwakisua, ambaye alikuwa akiomba kura ili aweze kutetea kiti chake, aliwataka wananchi kutokubali kurubuniwa na baadhi ya wanasiasa kutakiwa kutoshiriki kuchangia shughuli za maendeleo na amewataka kuunga mkono jitihada za uongozi wa CCM chini ya Rais Benjamin Mkapa kutokana na maendeleo yaliyofikiwa.
Nitainua elimu jimboni K’mbero - mgombea
Na Igamba Libonge, Kilombero
MGOMBEA ubunge jimboni Kilombero kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Castor Ligallama, ameibuka na sera ya kuinua elimu ya ufundi kwa wakazi wa wilaya hiyo pindi atakapochaguliwa.
Ligallama aliyasema hayo hivi karibuni wakati akiomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo katika mikutano yake ya kampeni katika viwanja vya shule ya Jongo, mjini Ifakara.
Alisema akichaguliwa atahakikisha kuwa vijana waliomaliza elimu ya msingi na kukosa nafasi ya kuendelea na sekondari watapata fursa ya kujiunga na chuo cha ufundi kinachotarajiwa kuanzishwa hivi karibuni katika tarafa ya Mang’ula.
Aliendelea kusema kuwa Chuo hicho kitakuwa cha kwanza kumilikiwa na watu binafsi wilayani hapa na kinatarajiwa kuwa Mang’ula baada ya kukinunua kiwanda cha Mang’ula Machine Tools (MMT).
Mgombea huyo alisema kuwa pindi Chuo kikianzishwa kitaweza kusaidia vijana wengi wanaokosa elimu katika wilaya za Kilombero na Ulanga kutokana na upungufu mkubwa wa vyuo katika wilaya hizo.
Pia Ligallama aliwaomba wananchi wote jimboni humo kumpa kura na kuahidi kwamba kila kata, kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kila mita 400 akina mama watakuwa wakipata maji safi na salama kwa kupitia visima vitakavyochimbwa kwa kushirikiana na wananchi wenyewe pamoja na wafadhili.
Alisema maji hayo yatakuwa kwa kiwango cha asilimia 60 kwa wakazi wa mijini na asilimia 40 itakayobaki ni kwa wakazi wa vijijini ambao watakuwa wananufaika kwa miradi ya umwagiliaji katika kilimo.
Pia Ligallama alisema kuwa kama akifanikiwa kushinda atawashawishi vijana kuanzisha vikundi kwa ajili ya kuendesha SACCOS ili kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi pamoja na kuondokana na umaskini kwa kupata mikopo.
Wana-CCM wanaounga mkono wapinzani Mbeya waonywa
Na Idefonce Mgimba, Mbeya
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Mbeya, Sylvester Kikungwe, ameonya kuwa viongozi wanaoshindwa kuondoa makovu ya kura za maoni na kuhujumu kampeni za CCM watachukuliwa hatua kali.
Katibu wa CCM alieleza hayo jana wakati akihojiwa na ‘Uhuru’ ofisini kwake baada ya kupatikana habari kuwa kuna baadhi ya wanachama wa CCM na viongozi katika majimbo ya Mbeya, Rungwe Magharibi na Mbarali wanawapigia kampeni za chini chini wagombea wa upinzani.
Kikungwe alisema kwa sasa kinachofanyika ni kuwaondoa katika kamati za kampeni viongozi na wanaoonekana kuwa bado wanaendekeza makovu ya machungu ya kushindwa katika kura za maoni ili wasipunguze kasi ya kampeni ya wagombea katika kila ngazi.
"Kwa hiyo tunawashauri na kuwataka viongozi na watendaji wa ngazi zote kuondoa makovu ya kura za maoni ili tuungane katika kukitafutia Chama chetu ushindi wa kishindo.
"Wale wanaoonekana kuendeleza makovu ya kura za maoni hatutaendelea kuwavumilia bali tutawaondoa kwenye kamati za kampeni pasipo kujali nafasi zao katika kata wilaya na hata mkoa," alisema.
Akitoa mfano, alisema tayari mkoa umeshaagiza kuchukuliwa hatua mara moja viongozi wa CCM waliomdhamini aliyekuwa mbunge wa jimbo la Lupa ambaye sasa amehamia CUF, Njelu Kasaka, ikiwemo kusimamishwa uanachama wakisubiri maamuzi ya vikao vya juu.
Tayari aliyekuwa mjumbe wa Halmashauri ya CCM ya mkoa wa Mbeya akiwakilisha Jumuia ya Wazazi toka wilaya ya Chunya, Douglas Mpemba, ambaye alikuwa miongoni mwa wana-CCM kadhaa waliomdhamini Kasaka kugombe ubunge kupitia CUF. amesimamishwa uanachama.
Akielezea sababu halisi za Mpemba kusimamishwa uanachama, Katibu wa CCM wa wilaya ya Chunya, Clemence Mponzi, amesema kuwa kiongozi huyo alikuwa na makosa kadhaa ikiwemo kushabikia upinzani, hususan CUF kwa kumsindikiza mgombea wake, Njelu Kasaka kugombea ubunge siku ya uteuzi Agosti 21, 2005.
Kosa jingine ni kumdhamini Kasaka kwenye fomu zake, jambo ambalo kulingana na kanuni na maadili ya CCM, halikustahili kufanywa na mwanachama wa CCM wala kiongozi.
Kikungwe alisema chama mkoani Mbeya kimekuwa imara na kinafanya uchunguzi wa kina kuona madai ya kuwa kuna baadhi ya viongozi wanawashabikia wagombea wa upinzani.
Chama mkoa, kwa mujibu wa Kikungwe, wajumbe wa kamati ya utendaji mkoa wanaanza ziara Jumatano ijayo kwa kutembelea wilaya zote mkoani kuratibu kampeni za wabunge na madiwani.
Kumekuwepo tuhuma kuwa kiongozi wa Jumuia moja ya CCM ngazi ya mkoa anafanya kampeni za chini chini kwa nia ya kumwangusha mgombea wa CCM ili kutoa nafasi kwa mgombea wa upinzani katika jimbo la Rungwe Magharibi, ambalo linatetewa na Profesa David Mwakyusa wa CCM.
Kulingana na taarifa hizo kiongozi huyo wa jumuia anampigania mgombea wa TLP, Afwilile Mwakijungu, ambaye kabla ya kuingia TLP alipambana na Profesa Mwakyusa katika kura za maoni ndani ya CCM na kushindwa.
KIkungwe alisema kuwa amefikishiwa mara kadhaa malalamiko hayo, lakini alisema bado anayafanyia uchunguzi kujua ni nani na kama kweli hilo lipo ili kama ikibainika achukuliwe hatua kali za kinidhamu.
"Bado sijaamini kama hilo linaweza kufanywa na kiongozi wa juu katika kamati yangu ya siasa, lakini hata hivyo tunalifanyia uchunguzi na ikiwa atabainika hatutajali dhamana yake ndani ya chama tutamchukulia hatua kali hata ikiwezekana kumsimamisha uanachama," alisema Kikungwe.