UHURU 19.09.2005

 

 

Msiwape nafasi wapinzani waharibu uchaguzi - Karume
Na Abubakar Rajab, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amewaambia wananchi kutokuwapa nafasi wapinzani kuharibu na kuchafua uchaguzi mkuu.
Rais Karume aliyasema hayo jana alipowahutubia wananchi huko Dole, mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni mfululizo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi ujao.
Alisema imekuwa kawaida ya wapinzani kulalamikia matokeo mara baada ya kushindwa katika uchaguzi wa vyama vingi tokea kuanza  mwaka 1995.
Rais Karume alisema wapinzani wanaelewa vyema kuwa hawana nafasi ya kushinda  katika uchaguzi huu wa mwaka 2005, hivyo wanajaribu kuandaa mbinu za kuharibu  uchaguzi huo.
"Wanafahamu vizuri sana kuwa watashindwa uchauguzi hivyo wanajaribu kuandaa  ugomvi, ili waharibu uchaguzi, lakini CCM inawapelekea salamu kuwa hatuna  haja ya ugomvi na wasituharibie ushindi wetu," alisema Rais Karume katika mkutano huo uliohudhuria na maelfu ya wanachama wa CCM na wapenzi.
Rais Karume alieleza kuwa wapinzani hao katika uchaguzi wa mwaka 1995 na mwaka 2000 mara baada ya kushindwa ambapo walijaribu sana kuzivuruga, walikimbilia nchi za nje kulalamika kuhusu uchaguzi ambao wao ndiyo walioleta vitendo vya kuuharibu.
Aliwashangaa viongozi hao kwa kujifanya hivi sasa wanajali shida za wananchi ambapo kwa kipindi chote cha nyuma hawakujishughulisha  chochote katika matatizo na maendeleo ya wananchi.
Rais Karume alisema kutokana na kuwa mbali na wananchi pamoja na nchi, hivi sasa wanazungumzia vitu ambavyo havipo kabisa nchini vikiwemo uchakavu wa barabara na ufungwaji wa uwanja wa ndege.
Alisema kauli hizo kutolewa na mtu anayegombea uongozi wa nchi ni aibu kutokana na ubora wa miiundombinu ya Zanzibar kujulikana na  kila mwananchi na hata wageni wanaoitembela Zanzibar.
"Sasa wenzetu hawa wameshindwa, tuliyajuwa zamani hayo wanashindwa kwa sababu badala ya kukaa na kutengeneza sera na ilani yao anazungumza vitu visivyoingia akilini, uwanja wa ndege wa Zanzibar haujawahi kufungwa
hata siku moja na na ndege zinatua kila siku tena ndege kubwa kubwa kutoka mashirika tofauti duniani," alisema Rais Karume katika mkutano huo uliohudhuriwa na halaiki ya wanachama na wapenzi wa CCM.
Rais Karume alisema viongozi wa Chama hicho wanapita kupakaza maneno ya uongo kwa wananchi ambapo wiki iliyopita timu ya chama hicho kikiongozwa na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad walidai wameongea na wamiliki
wa mahoteli na baadaye kutangaza matatizo yao.
Rais Karume alisema hii si kazi yao... si kazi ya chama cha siasa na kamwe hawahusiki na kujua
matatizo wakati hawakusaidia kitu chochote katika kuanzisha vitega uchumi hivyo.
Alieleza kuwa kuna mafanikio dhahiri ya Serikali katika kipindi kilichopita ambapo alieleza kuendelea na azma hiyo ya maendeleo ya  haraka katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwemo kuimarisha elimu ya fani zote.
Alisema Serikali itatilia mkazo elimu zote zikiwemo ufundi na amali pamoja na elimu rasmi ambayo CCM imepindukia malengo katika kutekeleza Ilani yake ya mwaka 2000.



MALECELA AWEKA BAYANA:
Wana-CCM wanaohujumu Chama waitwe ili wasutwe
Asema walioshindwa uteuzi wasiwe na nongwa mioyoni mwao
Na Thomas Mtinge, Kisarawe
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara), John Malecela amesema baadhi ya wana-CCM wanaofanya hujuma baada ya kushindwa kwenye vikao vya uteuzi wa Chama, waitwe kwenye vikao husika ili wasutwe.
Malecela alisema japokuwa katika baadhi ya maeneo kunaonekana hakuna kambi, lakini baadhi ya walioshindwa wanaonekana kuwa na nongwa mioyoni mwao, hivyo kukihujumu chama.
“Kuna baadhi ya wana-CCM wakishakosa kura za maoni, basi inakuwa nongwa. Matatizo sasa yapo kwa viongozi siyo wananchi. Wapo baadhi wanasema eti bora wawapigie wapinzani… wanaofanya hivyo waitwe kwenye vikao na kusutwa. Kambi hakuna sasa zilizopo zipo mioyoni mwa watu na hizo ni nongwa waache,” alisema Malecela.
Makamu Mwenyekiti aliyasema hayo juzi katika kijiji cha Manerumango alipokuwa akizindua rasmi kampeni za CCM kwa ajili ya jimbo hilo ambalo Athumani Janguo aliteuliwa kuwania ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM.
Malecela alisema kama msingi wa kukubali matokeo haujawekwa imara, siku zijazo hali itakuwa mbaya na kuwa ni jukumu la viongozi wa Chama sasa kuwaita wanaofanya nongwa na kuwasuta bila kuwaonea aibu ili kukomesha hali hiyo.
“Wapo wana-CCM ambao wakikosa kuteuliwa katika kura za maoni kuendeleza nongwa katika mioyo yao kutokana na kuwa na tama na uroho wa kupata madaraka utadhani wamezaliwa wakiwa viongozi,” alisema Malecela huku akishangiliwa na wananchi waliofurika katika uwanja huo.
Aliwaagiza vijana wa CCM kuanzia sasa kutembea vifua mbele badala ya kuwaacha vijana wa vyama vya upinzani wakifanya hivyo na kusababisha vurugu.
“Vijana mpo? Vijana wa CCM kwa vipi kukiwa na wapinzani wachache wanafanya fujo kwenye mikutano yenu mnawaangalia tu, sasa umefika wakati na ninyi kutembea vifua mbele badala ya kuwaachia wapinzani kutamba,” alisema Malecela na kuongeza kuwa: “Amani katika nchi hii italindwa kwa gharama yoyote.”
Malecela pia aliwataka wananchi kujihadhari na wanasiasa na viongozi wa dini wanaochanganya mambo hayo mawili kwa wakati mmoja na kuwa wanaofanya hivyo wanastahili kutengwa.
“Mtu anayepeleka siasa katika nyumba za ibada mtoeni, hafai. Misikiti na Makanisa yatumike kwa malengo yake ya kuwapeleka watu mbinguni sio mambo ya siasa na duniani,” alisema Malecela ambaye alishangiliwa sana na watu waliohudhuria mkutano huo.
“Niwaulizeni wananchi. Sheikh akisema jambo mnaitikia amina, Mchungaji akitoa mahubiri kanisani mnaitia amina, huko ndiyo mahali kwake ili kujiandaa kwenda mbinguni. Katika jukwaa la siasa unaeleza sera ili upate madaraka ya uongozi wa dola,” alisema Malecela.
Katika mkutano huo, Malecela pia alielezea kushangazwa na baadhi ya viongozi ambao wana uchu wa madaraka na wasiotaka kushindwa na wengine jambo alilolisema kuwa lisilokubalika kwa jamii.
“Kuna mwana-CCM mmoja amefanya mambo ya ajabu sana, tulidhani ni mwenzetu kumbe sio. Mwaka 1995 alishindwa kura za maoni tukampa na mwenzake akakubali. 2000 alishindwa tena tukampa, mwenzake akakubali, safari hii kashindwa tena, hataki kukubalia matokeo, ni jambo la kushangaza,” alisema Malecela bila kumtaja na kuwa kiongozi huyo kwa uchu wake wa madaraka siku ya mwisho ya kurudisha fomu asubuhi alichukua za CHADEMA na jioni za CUF ambapo matokeo yake alichelewa kuzirudisha.
Makamu Mwenyekiti alisema CCM ni jabali hivyo matatizo madogo kama hayo wanayokumbana nayo hayawezi kuwateteresha.
Malecela pia aliwataka wananchi wa Mkoa wa Pwani mwaka huu kuwa na mshikamano kuliko ilivyotokea kipindi kingine kwa kuwachagua wagombea wa CCM kwa kuwa hata mgombea wa Chama wa Urais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete anatokea mkoani humo.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu wananchi wa mkoa huo hawana budi kuweka historia ya ushindi wa CCM tofauti na miaka ya nyuma kwa kujivunia mgombea huyo wa urais kutoka mkoani kwao .
Malecela alisema CCM ni Chama kinachowajali na kuwaletea maendeleo wananchi, hivyo endapo kitachaguliwa tena kitaendelea kudumisha amani na utulivu uliopo sasa.
“Hakuna Chama kingine cha siasa kinachoweza kufanananishwa na CCM. CCM imeonyesha mifano hai ya kuwaletea maendeleo hivyo kichagueni ili kiweze kuleta mambo makubwa zaidi,” alisema Malecela.
Malecela aliifananisha CCM na mtoto alieonyesha uadilifu na utiifu mbele ya wazazi wake baada ya kulima shamba na kisha kurudi kwao kuwaomba mbegu ya mazao kwa ajili ya kupanda katika shamba hilo, tofauti na vyama vingine ambavyo vina mashamba yasiyolimwa.
“Nataka niwaulize… hivi baba anapokuwa na watoto wawili ambao wote ni wakulima, lakini kati yao mmoja shamba lake limelimwa na mwingine limejaa magugu, wanapokwenda kwa baba yao kuomba mbegu ni yupi atakayepewa haraka? alihoji Malecela huku wananchi wakimjibu kwamba atapewa aliyeanza kulima.
Malecela alisema kwa misingi hiyo wananchi hawana haja ya kupoteza mbegu zao katika msitu usiolimwa na badala yake wazipeleke katika shamba lililolimwa ili ziweze kustawi vizuri, akimaamisha CCM.
“Maendeleo yoyote yale yanapatikana kwa jasho… bila kutoa jasho maendeleo hayawezi kupatikana. Unapotaka kuwa na mwanamke mzuri lazima utoke jasho huwezi kumpata hivi hivi tu,” alisema Malecela akimaanisha kwamba wapinzani wasitegee kupata ushindi kwa njia ya mkato pasipo kuonyesha njia ya kuwaletea wananchi maendeleo kwanza.
Kwa upande wake, Janguo aliwaomba wananchi wa jimbo hilo wampe tena ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo ili aendeleze mafanikio alioyaanza na kumalizia yale mengine alioyaahidi.
Alisema endapo atachaguliwa atahakikisha miundombinu katika jimbo hilo inaboreshwa na kuimarisha zaidi ili kuwapa unafuu wananchi wake. “Katika kipindi kilichopita mmeona mafanikio ya kimaendeleo jinsi yalivyopatikana na hili halina ubishi kwa sababu mnajionea wenyewe.
Janguo alisema katika kipindi kijacho atahakikisha mshikamano na ushirikiano uliopo sasa baina ya serikali ya CCM na wananchi vinadumishwa zaidi katika kutoa kipaumbele kwa kuboresha huduma za jamii.


 


Mvuto wa Kikwete wavuta wapinzani 725 Karagwe
Ni wa vyama vya CUF, TLP na Chadema
Na Bashir Nkoromo, Karagwe
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi Jakaya Kikwete amezoa wanachama 725 toka vyama vya CUF, TLP na Chadema katika Kata ya Nkwenda, alipokuwa njiani kuelekea wilaya ya Karagwe.
Wananchi wa kijiji hicho ambapo pia ndipo ilipo Kata hiyo walikusanyika kwa wingi kiasi cha kumfanya mgombea ahutubie huku akiwa amesimama juu ya gari ili aweze kuonekana kwa wananchi wote waliohudhuria mkutano huo wa kampeni.
Kwenye mkutano huo wanachama 101 kutoka CUF, 415 kutoka TLP na 199 kutoka Chadema walirudisha kadi zao na kujiunga na CCM.
Akihutubia mkutano huo, Kikwete alisema serikali yake itaendelea amani na mshikamano ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kikwete alisema ataboresha zaidi suala la elimu kwa kuhakikisha inakidhi haja kwa kuongeza idadi ya madarasa, vifaa na idadi ya wanafunzi.
Alisema pia ataboresha suala la afya kwa kuongeza idadi ya zahanati na zenye vifaa vya kutosha kwa ajili ya kusaidia wananchi.
Kuhusu suala la umeme, mgombea huyo wa CCM alisema kuwa serikali yake itafanya kila njia kuhakikisha tatizo la nishati hiyo linakwisha katika mkoa wa Kagera.
Alisema pia serikali yake itasaidia kuongeza soko la zao la kahawa na kuhakikisha bei inaongezeka ili ajira kwa vijana nayo iongezeke.
Wakati Kikwete na msafara wake ambao ulikuwa ukitokea Ngara kwenda Karagwe ulipata mapokezi makubwa katika kila kijiji vikiwemo vya Nyamsa, Nyaishozi na Omurushaka ambako kote huko kulikuwa na umati mkubwa wa watu.
Alimnadi mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Kyerwa, Eustas Katagira kwamba ndiye chaguo la CCM. Kikwete pia alimtawaza Katagira kuwa Kamanda wa Vijana wa wilaya ya Karagwe.
Akiwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma, Kikwete alipata mahudhurio makubwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika juzi, na wananchi wa wilaya hiyo wameeleza kuwa mkutano wake wa kampeni umevunja rekodi kutokana na wingi wa watu.
Mkutano huo wa ulifanyika kituo cha Vijana na kuhudhuriwa na maelfu ya watu ambao walionyesha bashasha na shauku kubwa ya kumuona na kumsikiliza Kikwete.




Serikali ijayo kukamilisha vitambulisho vya uraia
Na Abihudi Saideya na Ramadhani Mkoma, Ludewa
MGOMBEA Mweza wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed ShenI amesema serikali ya CCM ya awamu ya nne itakakikisha inakamilisha mpango wa kuwapatia Watanzania vitambulisho vya uraia.
Akihutubia katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana mjini Ludewa, Dk. Sheni alisema kutolewa kwa vitambulisho hivyo kutaviwezesha vyombo vya dola
kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
Alisema pamoja na kutolewa kwa vitambulisho vya uraia, serikali itaangalia namna ya kuimarisha sheria za
uhamiaji ili kulinda haki za Watanzania.
Dk. Sheni aliwaomba wananchi wamchague mgombea Urais wa CCM, Jakaya Kikwete, wagombea Ubunge na Udiwani kwa tiketi ya CCM akisema CCM ndicho Chama chenye uwezo wa kuendeleza amani iliyopo nchini.
Akiwa amefuatana na viongozi wa CCM kwenye mkutano huo, alisema Serikali ya CCM ikiendelea kuwa madarakani itawahamasisha wananchi na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Mbinu zitakazotumika kuwawezesha wananchi ni utoaji wa elimu ya uzalishaji na mitaji ya kuendeshea miradi ya maendeleo, alisema na kuongeza kuwa serikali itajenga
mazingira mazuri yatakayowawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Viongozi wa CCM waliofuatana na Dk. ShenI kwenye ziara yake ya kampeni Mkoani Iringa ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Pindi Chana, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa na viongozi
wengine wa Chama wa mkoani humo.
Mapema akitoa taarifa ya hali ya Chama mkoani, Katibu wa CCM wa mkoa Constantine Malyagili alisema jumla
ya madiwani 47 wa CCM wamepita bila kupingwa katika kata mbalimbali za mkoa huo.
Malyagili alisema wilaya iliyoongoza kwa kupitisha madiwani wengi ni Mufindi ambayo madiwani wake 19 hawakupata wapinzani.
Wilaya zingine ambazo wagombea wa CCM wamekosa wapinzani na idadi ya kata kwenye mabano ni Ludewa (12), Makete (9), Njombe (5) na Iringa Vijijini wawili.
Malyagili alisema CCM mkoani Iringa kinatarajia kupata ushindi mkubwa katika majimbo yote 11 ya ubunge na viti vingi vya madiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka
huu.
Pia, alisema wana-CCM na wananchi mkoani humo wamempongeza Dk. Sheni kwa kuchaguliwa kuwa mgombea mwenza wa kiti cha urais kupitia CCM na akaongeza kuwa
kuteuliwa kwake kunadhihirisha anavyokubalika ndani ya Chama na wananchi kwa jumla.
Kesho, Dk. Sheni ataendelea na ziara ya kampeni katika wilaya ya Makete mkoani Iringa.


 

Bariadi waaswa kupuuza uongo wa John Cheyo
Na Peter Katulanda, Bariadi
WANANCHI wa Wilaya ya Bariadi wametakiwa kupuuza uongo wa mgombea ubunge wa chama cha UDP, John cheyo na badala yake wawachague wagombea wa CCM ili wajipatie maendeleo.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na mgombea ubunge wa CCM katia jimbo la Bariadi Mashariki, Danhi Makanga wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM
uliofanyika Lugulu wilayani hapa.
Makanga alisema Bariadi imechezewa kitapeli na UDP kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita tofauti na yeye aliporudi CCM na kuwaletea maendeleo kwa kuboresha
miundombinu chini ya serikali ya CCM.
Huku akishangiliwa na umati mkubwa, Makanga alisema UDP inaendeshwa na
ukoo wa kina Cheyo na kwamba anamfananisha na suruali iliyokatwa na kuwa kaptura kwa maana ya kushindwa kwake katika ugombea wa urais na ubunge
mara nne.
“Cheyo ni muongo wa mchana, amefilisika kisiasa ndiyo maana anawadanganya eti mkimchagua ataongeza bei ya pamba, na kujenga barabala na shule… ana pesa
gani wakati hata nyumba yake imepigwa mnada?” Alihoji Makanga.
Alieleza kwamba wanachi wasikubali hata kidogo kudanganywa na kutapeliwa Naye, kwani mustakabali wa wilaya hiyo unategemea uchaguzi wao kwa 
kuichagua CCM ambayo ndio inayojenga barabara, shule na zahanati.
“Kama anataka kunyanyua bei ya pamba mpeni stoo aweke kapani (mzani) na kununua pamba hata kwa bei ya sh. 500 kwa kila kilo. CCM ndio inaweza kuwajengea barabara na shule, lakini siyo UDP,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Shinyanga, Charless Gishuli akizindua kampeni hiyo na kuwanadi wagombea  wa CCM alisema kuwa CCM haiandikii mate, bali inaandika kwa vitendo na kama wana Bariadi wanataka maendeleo waichague CCM.
“Najua Kikwete hana mpinzani, wanamsindikiza tu, lakini wana Bariadi uongozi ni sawa na gari halichanganywi vipuri. Chagueni CCM na siyo wabunge wa
kwenda kwenye posho,” alisema Mwenyekiti huyo.
Katika uzinduzi huo, CCM pia ilimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Diwani wa Kata ya Lugulu, Bulima Kiloya, mgombea
ubunge Viti Maalum Joyce Nhamanilwa na wagombea wengine wa kata mbalimbali.


… UDP yazidi kumomonyoka
Yakimbiwa na wanachama wake tegemeo
Na Peter Katulanda, Bariadi
MZIMU wa mmomonyoko katika chama cha UDP unazidi kumuandama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, John Cheyo baada ya wanachama wake tegemeo kuhama
na kujiunga  CCM.
Pigo hilo ambalo ni jingine tena katika chama hicho lilitokea Jumamosi iliyopita katika uwanja wa Sabasaba mjini hapa wakati wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Mpasuko huo ulitokea muda mfupi baada ya aliyekuwa kada wa UDP, Abel Kitebo alipoelezea kile alichodai kuisha kwa UDP kutokana na kuongozwa ki-ukoo.
“Mimi haikuwa rahisi kutoka UDP, lakini nilipoona kimekosa dira na kuongozwa na ukoo ilibidi nitoke na kurudi kwenye Chama chenye sera za kweli,” alieleza
Kitebo.
Siku moja akiwa na Cheyo kwenye gari alikatazwa na kiongozi huyo asifungue kioo kwa madai kwamba wananchi wakimuona watamsumbua kuomba pesa kwa
kuwa aliahidi kuwajaza mapesa na hajafanya hivyo na kuongeza kuwa waliobaki UDP wanangoja nini kama si kuongozwa na ukoo.
Kufuatia maneno hayo punde wanachama 14 wakiwemo 11 wa UDP, CUF mmoja na wawili wa Chadema walianza kurudisha kadi zao kwa mgombea wa CCM, Chenge.
Akihutubia mkutano huo, Chenge alisema wananchi wasicheze bahati nasibu kwa kuchagua vyama vya upinzani, kwani uongozi sio mahali pa kujipima kama maabara.
Chenge alisema upendo wake kwa wananchi wa Bariadi umemlazimu kuja nyumbani kuomba ridhaa yao awatumikie, kwani wilaya hiyo kwa miaka 10 imewafanya wananchi wake kuishi kama wako jela kwa kukosa maendeleo.
“Masuala ya maendeleo ni magumu sana, lakini nawaahidi tutashirikiana kuyaleta iwapo mtanichagua. Bariadi imeachwa nyuma kimaendeleo sababu
ya kuwa jela ya UDP,” aliongeza.
Akimpigia debe mgombea ubunge wa jimbo la Bariadi Mashariki (CCM), Danhi Makanga, Chenge alisema kipindi kifupi alichorudi CCM na kuchaguliwa kuwa mbunge ameleta maendeleo kwa kuboresha barabara na 
sasa alikuwa akitafuta ufumbuzi wa tatizo la uhaba wa maji.
Wanachama waliorudisha kadi ni pamoja na Ndakama Bugeye, Masumbuko George wa CUF, UDP ni Paul Jacob, Makoye  Nyabulula, Kwandu Sanagu na Makoye
Nhigo ambaye alikuwa mpiga debe wa Cheyo.
Wengine ni Sulwa Kingi, Rashid Juma, Sagude Mangu, Shinyanga Nkundi, Mazuye Zephania, Njile Stephen, Mitambe Shambano na Joseph Limbe wa Chadema.


Aliyejiengua NCCR asema wapinzani ni wababaishaji
Na Naftali Siwonike, Iringa
ALIYEJIENGUA chama cha NCCR Mageuzi katika nafasi ya ukatibu mwenezi mkoa wa Iringa na kurejea CCM, David Butunini amesema vyama vya upinzani ni vyama vya wababaishaji.
Butinini aliyasema hayo katika mkutano wa kampeni za mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM jimbo la Iringa Mjini, Monica mbega katika mtaa wa Magari Mabovu kata ya Kitanzini Miyomboni juzi.
Alisema kuwa hakuna mgombea wa chama chochote cha upinzani katika jimbo la Iringa na mkoa wa Iringa ambaye anaweza kumfikia yeye kwa kuwepo ndani ya upinzani kwa kipindi kirefu na tena si kwa chama hicho
Tu, bali amekwishapita katika vyama mbali mbali vya upinzani mkoani hapo.
Lakini pamoja na kuwepo ndani ya vyama hivyo vya upinzani, amekwishatambua uzuri na ubaya wa vyama hivyo vya upinzani ambapo chuki, fitina, ubinafsi, masengenyo na kila aina ya uovu ndio uliopo ndani ya
Vyama hivyo na hiyo ndio sababu ya yeye kuondoka katika upinzani na kurejea CCM.
Hivyo aliwataka wananchi kuepuka kudanganywa na wapinzani kuwa watawafanyia maendeleo wakati wenyewe
hata ofisi hawana, hayo maendeleo watayafanikishaje kwa wananchi.
Butinini aliwataka wananachi kutowabeza wagombea wa CCM kuanzia diwani, mbunge na rais, kwani sera za Chama cha Mapinduzi zipo wazi na matunda yamekwishaonekana kwa kiasi kikubwa.
"Ninataka kuwaelezeni kuwa CCM ndiyo yenye sera za kweli na zilizo wazi… hakuna udini wala ubaguzi ndani ya CCM tofauti na vyama vya upinzani," alisema.
Alibainisha kuwa kutokana na kuwepo kwa mwelekeo mbovu, upinzani utabaki kuwa wasindikizaji wa CCM hadi kufa, na kuwataka wananchi kuepuka kufanya majaribio ya
Uongozi, kwani hata kama majaribio yanahitajika basi yawe kwa CCM sio chama kingine.
Akiongea katika mkutano huo, Monica alisema kuwa pamoja na kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano ameweza kufanya mengi mazuri, lakini upo uwezekano wa jimbo la Iringa kuendelea kupata mafanikio makubwa iwapo wananchi wataiweka CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, alisema mafaniko hayo hayatakuwepo kama mfumo wa mafiga matatu hayataundwa iwapo wananchi hawatawachagua madiwani, wabunge na rais kutoka CCM.
Alisema kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano, jimbo hilo limeweza kupata mafaniko makubwa ya miundombinu tofauti na jimbo hilo lilipokuwa likiongozwa na kiongozi wa chama cha NCCR Mageuzi mwaka 1995.



CCM yasema haina sababu ya kuiba kura
Yasema inao wanachama ‘kibao’ watakaoipigia
Na Khatib Suleiman, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi kimesema hakina sababu ya kuiba kura kutoka kwa wapinzani kwa sababu kinao wanachama wa kutosha wa kukiwezesha kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Akihutubia wananchi pamoja na wafuasi wa CCM katika mkutano wa kampeni katika uwanja  wa Kiembesamaki wilaya ya Magharibi, mgombea wa nafasi ya Uwakilishi katika jimbo la  Kiembesamaki kwa tiketi ya
CCM, Mansoor Yussuf Himid alisema CCM imejizatiti kushinda ili kushika hatamu tena ya kuongoza dola.
''CCM itashinda na haina sababu ya kuiba kura katika uchaguzi mkuu... hiyo ni hofu ya wapinzani dhidi ya uchaguzi kuu,” alisema
Mansoor ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na mweka hazina wa CCM Zanzibar.
Mansoor alisema wapinzani wameingiwa na hofu kubwa na kiwewe cha kushindwa uchaguzi mkuu na sasa moja ya sababu yao kubwa wanayoitumia ni uwezekano wa kuibiwa kwa kura na CCM jambo ambalo si kweli.
Mapema Mansoor alipongeza uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutaka majina ya wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura kuhakikiwa hapa hapa nchini kwa kuwashirikisha wataalamu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) pamoja na wale wa Tume ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (NEC).
Alisema uamuzi huo ni wa kijasiri na unaostahiki kupongezwa kwa sababu majina ya wapiga kura kuhakikiwa na wataalamu wa kigeni ni aibu, hatua
ambayo inaonesha kwamba Watanzania bado hawajaweza kujiendesha wenyewe katika shughuli zao.
Mapema, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mjini Magharibi Yussuf Mohamed aliwataka wanachama na wafuasi wa CCM kuwachaguwa wagombea wa
nafasi ya Uwakilishi, Ubunge pamoja na Udiwani wagombea wa Chama Cha Mapinduzi ili wapate nafasi ya kuwaletea maendeleo.
Alisema Chama Cha Mapinduzi kimefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka mitano ikiwemo utekelezaji mzima wa Ilani ya CCM, na hivyo sasa wagombea hao wapo kwa ajili ya kuomba kura waweze kukamilisha kazi iliyobaki.
Wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Kiembesamaki katika nafasi ya Ubunge ni Omar Yussuf Mzee na kwa upande wa nafasi ya Uwakilishi ni
Mansour Yussuf Himid ambaye pia ni Waziri wa Nchi, anayeshughulikia Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi.




Kikwete: Tutayashughulikia majambazi ipasavyo
Ni kwa kuhakikisha amani nchi jirani
Na Bashir Nkoromo, Ngara
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi Jakaya Kikwete amesema Serikali yake italishughulikia suala la ujambazi kwa kuhakikisha nchi jirani zenye vita zinarejesha hali ya amani ili wakimbizi warejee kwao.
Kikwete alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Posta mjini hapa kwa kueleza kuwa kushamiri kwa ujambazi kunatokana na wakimbizi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiingia na silaha na kujihusisha na uhalifu.
Alisema katika uongozi wake atahakikisha anazungumza na taasisi husika ili kukomesha vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na wakimbizi wasio waaminifu.
Kikwete alisema Serikali pia itahakikisha amani inapatikana katika sehemu zenye migogoro ili kuwezesha wakimbizi kurejea makwao.
Alisema hata kama wakimbizi wataondoka wote, lazima ifanyike operesheni zaidi kwa kuwa baadhi ya silaha zitakuwa zimebaki na kutumika katika vitendo vya uhalifu.
Kikwete pia alisema Serikali itawezesha wananchi ili waweze kupata mikopo katika taasisi za fedha ambapo mali walizonazo zitarasimishwa ili kutumika kupatia mikopo.
Alitoa changamoto kwa wananchi wa hapa kuwa ili yote hayo yafanikiwe lazima wachague CCM kwa kuwa upinzani hauna dhamana wala anuani. Kikwete alisema suala la amani ni matunda ya sera sahihi za CCM.



Mrema atamba wakimchagua tena Arusha wataendelea kufaidi
Na Omari Shaaban, Arusha.
MGOMBEA ubunge kupitia CCM, Felix Mrema, wa jimbo la Arusha Mjini amezindua kampeni zake za kuwania jimbo hilo kwa mbwembwe  na kuwataka wananchi kumchagua tena ili waendelee kuyafaidi matunda ya maendeleo ya CCM kama yanavyoonekana kwenye jiji la Arusha.

Huku akishangiliwa na umati mkubwa watu kwenye uuwanja wa Mbauda Kata ya Sombetini alisema katika mipango hiyo ni kuhakikisha kila kata inakua na shule ya sekondari na kwamba mpango ulikwisha anza na sasa ni umaliziaji tu na tayari zaidi ya kata nane zina shule ya sekondari.
Mrema alisema hakuna chama chenye Ilani zinazotekelezeka kama CCM  na hivyo kuwataka wananchi kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo ili wananchi waendelee kula matunda ya Chama ya maendeleo na wananchi kujinyanyua kiuchumi kama iliyo sasa.
Mrema alisema wapinzani hawana lolote walilolifanya katika nchi hii zaidi ya malumbano na majungu na kwamba hata wakichukua nchi itakuwa hivyo hivyo na matokeo yake kuwagawa Watanzania ambao wamedumu kwenye amani kwa miaka mingi chini ya Serikali ya  CCM.

Katika kuhakikisha jiji la Arusha linakuwa kwenye hadhi ya kimataifa, Mrema alisema wananchi wawachague viongozi wa CCM na kwamba Urais wampe Jakaya Kikwete na ubunge yeye na madiwani wa CCM, ili mipango iliyopangwa ya jiji la Arusha kuwa la kimataifa zaidi iendelee.
Alisema kipindi hiki siyo cha malumbano, bali ni kujenga ushirikiano na umoja ndani ya CCM, ili kuhakikisha ushindi wa kishindo unapatikana.
"Jamani wananchi siyo kwamba tunataka ushindi tu...bali tunataka wa kishindo ili wapinzani waogope...na kukitambua kuwa CCM, inakubalika na wananchi ndicho chama chao cha maendeleo," alisema Mrema na kushangiliwa na umati huo wa watu huku ukisema: "Utapata kura wewe na Kikwete".
Baada ya hotuba hiyo Mrema aliwanadi kwa wananchi madiwani wa CCM, waliochaguliwa kwa kura za maoni na wale wa viti maalumu ambao walikuwa wakishangiliwa na kukubaliwa na umati huo pindi wanaponadiwa.
Mkutano huo ulihudhuriwa  Peter Kisamo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mwenyekiti CCM mkoa, Yona Nnko na Katibu wa Mkoa, Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fulgence Saria, pamoja na viongozi wengine waalikwa.

 



Dk. Sheni asema mapambano dhidi ya ukimwi kuimarishwa
Na Ramadhani Mkoma, Makete
MGOMBEA Mwenza wa kiti cha urais Dk. Ali Mohammed Sheni amesema Serikali ya awamu ya nne itandeleza mapambano dhidi ya ukimwi kwa  kuongeza bajeti ya dawa za kurefusha maisha.
Dk. Sheni aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja wa Mabehewani. Kata ya Iwawa, wilayani Makete.
Alisema ukumwi ni tatizo kubwa nchini na kwamba iwapo CCM itapewa ridhaa ya kuendelea kushika dola itakakikisha inapambana na ukimwi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.
Dk. Sheni alisema hilo linatokana na ukweli kwamba hali ya ugonjwa wa ukimwi nchini na hasa wilayani Makete ni ya kutisha.
"Takwimu za hapa si nzuri...na hesabu zake mnazijua," alisema Dk. Sheni katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wakazi ya kata hiyo wakiwemo kina mama na watoto na kuongeza:                   " Tusifanye mchezo na maradhi ya ukimwi tupambane kweli kweli".
Pia  Dk. Sheni aliwataka wananchi kutowanyanyapaa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kwa kuwa ni sehemu ya jamii.
Alisema takwimu zilizopo za wakazi wa wilaya hiyo wanaofikia 105,000 ni za hatari na zinatisha na hivyo kuna kila sababu ya kuchukua hatua mahususi katika kukabiliana na tatizo hilo.
Kutokanan na hilo alisema Serikali ya awamu ya nne itahakikisha inapambana vilivyo katika kupunguza maambukizi ya ukimwi ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya dawa za kurefusha maisha kwa waathirika.
Mbali na Makete alisema hali ya ukimwi kitaifa ni
mbaya na hivyo kuna kila sababu ya kwa jamii kwa ujumla kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya ukimwi.
Alisema kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, Kitengo cha Kupambana na Ukimwi,  hadi Desemba mwaka 2003, jumla ya watu milioni 1.8 wanaishi na ukimwi.
Kwa mujibu wa Dk. Sheni idadi hiyo ni kubwa kwa Taifa lenye watu wanaofikia milioni 35.
Dk. Sheni alisema katika kukabiliana na makali ya ugonjwa huo Serikali ilishaanza kuwa hudumia
waathirika 44,000 kwa kuwapa dawa za kurefusha maisha na kwamba idadi hiyo itaongezwa kulingana na uzito wa tatizo.
Akizungumzai mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa katika kipindi  cha miaka 10 ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi. Dk. Sheni alisema sekta ya afya  ni miongoni mwa sekta ambazo hudum zake ziliboreshwa.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Osmund Kapinga alisema kwa sasa idadi ya vifo vinavyotokana na ukimwi vimepungua kutoka kifo cha mtu moja kwa siku hadi kifo cha mtu mmoja kwa siku saba au wiki mbili.
Alisema hilo linatokana na kusambazwa kwa elimu ya kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na utoaji wa ushauri nasaha.