UHURU 21.09.2005

 

 

 

Kikwete awasihi wananchi kuendelea kuichagua CCM

Na Bashir Nkoromo, Musoma

MGOMBEA wa Urais kupitia CCM  Jakaya Kikwete, jana aliwasihi wakazi wa  mkoa wa Mara kuwachagua madiwani, wabunge na yeye mwenyewe  awe Rais kupitia CCM ili nchi iendelee kuwa ya amani , utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Kikwete alisema zipo dalili za baadhi ya wagombea wa upinzani kuwa na nia ya kuigawa nchi kwa masuala ya udini na ukanda ama ukabila jambo ambalo ni hatari kwa umoja wa kitaifa nchini.

Alisema Baba wa Taifa Marehemu Julius Kambarage Nyerere alijenga msingi imara wa Taifa na kwamba msingi huo ulizidi kuimarishwa na serikali za awamu ya pili na ya tatu na kwamba CCM imedhamiria kuimarisha zaidi umoja huo katika awamu yake ya nne.

‘’Mkinichagua mimi kuwa Rais na wabunge pamoja na madiwani wote kupitia CCM, nina uhakika wa kuzungumza lugha moja na kufanya kazi kwa ufanisi’’ alisema.

Mgombea huyo ambaye alifika Mkoani Mara na kulakiwa na umati wa watu , akitokea Kagera  alisema serikali ya awamu ya nne itakuwa na kazi moja kubwa ambayo ni kukuza uchumi ambao msingi wake umejengwa na serikali ya Rais Benjamin Mkapa.

Katika kutekeleza kazi hiyo, alisema serikali yake itatengeneza sera ya mikopo nafuu kwa wananchi wengi ili waweze kupata mikopo katika vyombo mbalimbali vya fedha.

Kikwete ambaye pia ni Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa aliwasihi wananchi wa mkoa wa Mara kwenye majimbo yote yakiwemo ya Musoma mjini na vijijini, Tarime na  Mwibara  kujiandaa kumchagua yeye  Oktoba 30, mwaka huu pamoja na wabunge na madiwani wote wanaogombea kupitia CCM

Awali akiwasili mkoani Mara, umati wa watu ukiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba ulifurika kumpokea  kwa maandamano makubwa ambayo baadhi ya wananchi walisema yalivunja rekodi  ya wagombea wengine waliopita huko.

Kama kawaida wanachama karibu 50 wa vyama vya upinzani walijikuta wakitupa kadi zao hadharani na kuomba kujiunga CCM ili waendelee kulinda amani na utulivu wan chi.

Mgombea wa Urais Kupitia CCM , Kikwete , leo anatarajia kuwasili mkoa wa Singida kuendele na kampeni za kuomba kura kwa wananchi mbalimbali.

 

 

 

Dk. Sheni aasa dini zisitumike kuendeleza chuki na uhasama

Na Dunstan Bahai, Dodoma

MAKAMU wa Rais, Dk. Ali Mohamed Sheni amesema kwamba imani za dini zisitumike kuendeleza chuki na uhasama bali ziwe za kudumisha amani na utulivu.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akiweka jiwe la msingi la Msikiti wa mjini hapa katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Benjamin Mkapa, Sheikh Mkuu Mufti Issa Shaaban bin Simba na wawakilishi wa Libya ambao ndiyo wafadhili wakubwa wa ujenzi huo.

Msikiti huo utakapokamilika utagharimu sh. bilioni sita na utakuwa na uwezo wa kuchukua waumini 3,000 kwa wakati mmoja.

Mafanikio ya ujenzi huo yanatokana na mikakati ya Rais Mkapa ambapo Kiongozi wa Libya Muammar Gadaffi amekubali kugharamia ujenzi huo na kwamba hiyo anatoa kama zawadi kwa Rais Mkapa kutokana na jitihada zake za maendeleo ya Bara la Afrika.

Mufti Simba alieleza kwamba msikiti huo ni wa aina yake, utakaokuwa na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja na afya na elimu.

Alisema msikiti huo umepewa jina la Rais Gaddafi kama shukrani kwake kwa kutoa msaada huo.

Dk. Sheni katika hotuba yake alisema kwamba ujenzi wa msikiti huo ni ishara kuwa Serikali inathamini uhuru wa raia wake wenye dini mbalimbali na uhuru wa kuabudu ingawa Serikali yenyewe haina dini.

Aliwataka Waislamu kuhakikisha imani yao ya dini haitumiki kuendeleza masuala na maslahi yasiyodumisha amani na utulivu.

Mwakilishi wa Jumuia ya ya Kiislamu ya Kimataifa kutoka Libya Sheikh Ammar Hareba alisifu demokrasia iliyopo nchini na hasa wakati wa kupishana madaraka, utaratibu aliosema unafanywa kwa amani na utulivu.

Alisema Rais wa Libya amefurahishwa na jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Mkapa kwa nchi yake na Afrika kwa ujumla hivyo  amelazimika kumpa zawadi ya msikiti huo.

 

 

 

 

 

 

Mrema aibukia MAELEZO na majigambo kibao

Achekesha waandishi kuwa ‘ameshakuwa Rais’

Atembea mitaani na shahada ya chuo kikuu

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya TLP, jana alikuwa ‘kichekesho’ katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), alipoibuka kwa majigambo kuwa kampeni zinamnyookea na kujitambulisha kuwa ‘ameshakuwa Rais’.

Mrema alitoa hoja hiyo, akidai ahadi alizopewa na wananchi wa Chalinze waliomuahidi kumpa Urais. Pia alidai amepata mapokezi makubwa alipokuwa huko Kibaha, juzi.

“Mwaka huu nitafanya maajabu,” alisema Mrema ambaye aliomba apigiwe makofi kutokana na wananchi kumhakikishia kuwa Rais mapema, kabla ya kampeni kwisha. 

Kiongozi huyo wa TLP, aliibuka na madai lukuki ikiwa ni pamoja na kuwatoa gerezani zaidi ya wafungwa wanaotumikia vifungo, wakiwemo waliohukumiwa katika kesi za kubaka, huku akitaja baadhi ya majina.

Mrema jana, pia alitimiza ahadi yake ya kutoa sh. 200,000 kwa waandishi wa habari wanaodaiwa kwamba walipigwa na askari magereza hivi karibuni. Pesa hizo zilipokewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wapigapicha za Habari, Juma Dihule.

“Mimi Augustine Lyatonga Mrema, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Natoa mchango wa sh. laki mbili…” alitamka Mrema na kuongeza: “Wembe ni ule ule, tutabanana hadi kieleweke”.

Baada ya simulizi ndefu, Mrema aliibua cheti cha shahada yake kutoka Chuo Kikuu cha Western Pacific, na kuwaonyesha waandishi waliokuwa wakiangua kicheko wakati wote, ambapo alidai wanaomuonea gere ndiyo wanaokibeza kuwa kina walakini wa kutambulika.

Baada ya kumalizika mkutano wake, ofisa habari wa MAELEZO alitoa nafasi ya maswali kwa waandishi wa habari, lakini Mrema alisimama na kutamka huku akianza kufungasha vilivyo vyake: “Mumuulize Rais maswali ya nini?”

Kwa mujibu wa Sheria za nchi, Rais hutangazwa rasmi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutokana na matokeo ya kura zilizopigwa, ambapo katika uchaguzi huu ni Oktoba 30.

Hii si mara ya kwanza kwa Mrema kuibuka na vituko vinavyohusiana na shahada yake ya chuo kikuu na hoja ya kutaka apigiwe makofi, lakini suala la kujitangaza Rais na kutaka kuungwa mkono na waandishi wa habari ‘kuisusia CCM’ ni hatua mpya.

 

 

 

 

Salma Kikwete: Wanawake hakuna tena kama CCM

Na Idefonce Mgimba, Mbeya

MKE wa mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM)  Salma Kikwete amesema kutokana na CCM kuonyesha uwezo na nia ya kujali maslahi ya wanawake, hawana haja ya kushabikia vyama vya upinzani.

Salma alitoa kauli hiyo jijini Mbeya juzi alipokutana na mamia ya wanawake waliokusanyika katika kampeni za ndani anazoendelea kuzifanya nchini kote kwa nia ya kuwahamasisha wanawake kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi.

"CCM imeonyesha na kudhamiria kuwakomboa wanawake hasa katika kuwashirikisha katika vyombo vya maamuzi jambo ambalo kimsingi ni kujali maslahi yao na hivyo wanaoshabikia upinzani wanapotoka," alisema Salma huku akishangiliwa na mamia ya wanawake hao.

Aliwataka wanawake wa ngazi zote kuwashawishi wanawake wenzao ambao bado wanashabikia upinzani kuvihama vyama hivyo kwa kuwa utulivu na amani vinapatikana CCM  na kamwe si vyama vingine.

Salma ambaye aliwasili juzi mkoani Mbeya akitokea Rukwa na kupokewa kwa shangwe na mamia ya wana-CCM wengi wao wakiwa ni wanawake alisema kitendo cha Serikali ya CCM ya awamu ya tatu ya kuazimia kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi  hasa bungeni kufikia asilimia 30 ni ushahidi tosha kuwa CCM ni Chama kinachojali maslahi ya wanawake na kufaa kupigiwa kura za ushindi.

Alisema Chama pia kimeahidi kitatoa nafasi nyingi zaidi za uongozi katika awamu ya nne ya uongozi wake ikiwa kitapewa ridhaa na wananchi sera ambayo haiwekwi wazi na vyama vingine vya upinzani.

Kwa hiyo alisema wanawake hawana budi kutoa ushindi wa kishindo kwa wagombea wa CCM wa ngazi zote ili azma ya kutekeleza kwa ukamilifu Ilani inayotoa kipaumbele kwa wanawake iweze kufikiwa.

Aliwahamasisha wanawake kuwachagua wanawake wenzao hasa wanaogombea nafasi mbalimbali kupitia CCM ili waweze kuwawakilisha ipasavyo katika vyombo vya maamuzi.

Salma alisema wakati huu si wa malumbano wala makundi kwani mchakato ulishapita na kusiwe na wapambe: “Kinachotakiwa sasa ni kuunganisha nguvu na kuwa kitu  kimoja hakuna kuangalia itikadi tuangalie maslahi ya CCM.”

Alisema Chama kimeonyesha uwezo mkubwa katika kutekeleza kwa vitendo ahadi zake zilizomo kwenye llani ya Uchaguzi ya mwaka 2000 ambao ni ushahidi tosha kuwa itatekeleza kwa  ari mpya, nguvu mpya  na kasi mpya yale yaliyomo kwemye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 ambayo kimsingi imetoa ahadi ya kuboresha nyanja mbalimbali ikiwemo ya mikopo kwa wanawake kuangalia suala la kuwapunguzia riba na unafuu katika urejeshaji wa mikopo.

 

 

 

 

Wanawake wanaowania ubunge kukutana Dar kesho

Na   Mwandishi   Wetu

ZAIDI ya wanawake 50 wanaowania ubunge kwenye majimbo katika  Uchaguzi Mkuu ujao watakutana Jijini Dar es Salaam kuanzia kesho  hadi Jumamosi  kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa  jinsi ya kutumia vyombo vya habari wakati wa kampeni, taarifa iliyotolewa na TAMWA imesema.

Taarifa ilisema wanawake hao wanatarajiwa  kuelezea uzoefu wao kutokana na kampeni za mwaka huu pamoja na kuimarisha ujuzi wao kuhusu mbinu za kutoa hotuba za kampeni zinazolenga kuimarisha demokrasia, amani, umoja wa kitaifa na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Warsha hiyo ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na wagombea ubunge wanawake kutoka vyama vyote vya siasa itafanyika katika ukumbi wa Red Onion ulioko kwenye jengo la Haidary Plaza.

TAMWA imeandaa warsha hiyo  ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa shughuli zake za kuwajengea uwezo wanawake ili washiriki kikamilifu katika uongozi kama Serikali ilivyoridhia kwenye mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa kuhusu jinsia na maendeleo.

Mikataba ambayo Tanzania  imeridhia ni pamoja na Azimio la Umoja wa Nchi za Afrika linalohimiza nchi zote za bara hili zihakikishe kuwa idadi ya wanawake katika vyombo vyote vya maamuzi inakuwa sawa na wanaume.

Azimio lingine ni  la nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo  ya  Kusini mwa Afrika (SADC) ambalo linasisitiza nchi wanachama kuwa na angalao asilimia 30 ya wanawake katika vyombo vya maamuzi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, 2005.

 

 

 

 

Viongozi wa TLP Pwani mbaroni kwa kufanya maandamano haramu

Na Selina Wilson, Kibaha

VIONGOZI watatu wa chama cha Tanzania Labour (TLP), wametiwa mbaroni na polisi mkoani Pwani, baada ya kufanya maandamano bila kibali na kusababisha vurugu katika barabara kuu ya Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Ally Mbilikila alisema tukio hilo lilitokea juzi eneo la

Mailimoja Kibaha baada ya mgombea urais wa chama hicho Augustine Mrema kumaliza mkutano wa hadhara na kuanza kusukumwa na wafuasi wake kwa gari.

Mbilikila aliwataja viongozi hao kuwa ni Katibu wa TLP wa Wilaya ya Kibaha Francis Tarimba (49), Ally Mchumo (44), Cosmas Kisanga (42) wote wakazi wa Mailimoja mjini Kibaha.

Alisema watuhumiwa hao watatu walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuongoza maandamano kutoka uwanja wa Mailimoja kupitia barabara kuu ya Morogoro na kufunga barabara hiyo jambo lililosababisha usumbufu kwa magari yaliyokuwa yanaingia na kwenda mikoani.

Mbilikila alisema licha ya kupewa tahadhari na askari wa kituo cha polisi Mailimoja kwamba watakapomaliza mkutano wao waondoke kwa amani bila vurugu lakini wao walikiuka amri hiyo.

Kamanda alisema baada ya mgombea urais  wa chama hicho, Mrema kufanya mkutano wa hadhara mashabiki walitoka uwanjani wakimsindikiza kitendo kilichosababisha kuwepo na vurugu ambazo ziliwafanaya polisi waingilie kati ili kuwazuia.

Kamanda Mbilikila ametoa onyo kwa wafuasi wa vyama vingine vinavyoendelea na kampeni za uchaguzi kufanya mikutano yao katika hali ya amani na kuacha tabia ya kujihusisha na maandamano yanayosababisha kuvunjika kwa amani.

Mapema Mrema akihutubia wakazi wa Kibaha katika

Viwanja vya Mailimoja aliwaeleza wananchi kuwa mambo yaliyofanywa na CCM wameyaona na athari zake zimeonekana hivyo ni wakati muafaka wa kuchagua chama chake kushika dola.

Mrema alisema Tanzania imekuwa chini ya mfumo wa chama kimoja kwa miaka mingi na baadae vikaundwa vyama vya upinzani ambavyo kwa sasa vina nguvu zaidi hivyo wananchi wasiige Urusi ambayo imesambaratika kwa sababu ya kushikilia chama kimoja.

Mgombea huyo wa urais alitaja sababu zinazomkwamisha kupata urais kwamba ni wapiga kura wanafiki, watu wenye chuki binafsi na wanaokubali kuhongwa na CCM na mawakala wanaodai kuwa ukiwachanja wanatoka damu ya

kijani.

Aliwataka wananchi wamchague kwa sifa alizonazo na kwamba wananchi wangekuwa wanatenda haki wasingemchagua mgombea wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba kwani alikuwa chini yake na hata sasa wagombea wenzake hawamfikii mgombea kama Lipumba hajawahi kuwa hata katibu kata.

 

 

 

 

 

Dk. Mahanga awaasa wananchi kuwapuuza wanaokashifu Serikali

Na Nashon Maingu

WANA-CCM na wananchi wapenda maendeleo wametakiwa kupuuza wapinzani wanaodai Serikali ya Chama Cha Mapinduzi haijafanya kitu katika miaka mitano iliyopita kufuatia Ilani yake ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Wito huo ulitolewa jana na mgombea ubunge wa jimbo la Ukonga kupitia CCM, Dk. Makongoro Mahanga.

Mgombea huyo wa CCM ambaye yuko katika ziara ya kujitambulisha na kutoa shukurani kwa wanachama kwa kuteuliwa tena kuwa mgombea katika jimbo la Ukonga, alisema hayo alipokuwatana na Wenyeviti na wajumbe wa matawi katika Kata ya Kitunda, Manispaa ya Ilala kwa nyakati tofauti.

Dk. Mahanga alisema CCM imefanya mambo makubwa katika Kata ya Kitunda hasa upande wa elimu.

Alisema katika miaka mitano iliyopita Kata ya Kitunda imeweza kujenga shule za msingi saba, ukilinganisha na shule moja ya msingi  (Kitunda) iliyokuwepo wakati huo.

Dk. Mahanga alizitaja shule hizo kuwa ni Kerezange, Jitihada, Magore, Kipunguni, Kivule, Mwanagati na moja ambayo imejengwa karibu na Kipunguni ambayo haijapewa jina, lakini madarasa matatu yako tayari kwa kutumika.

Alisema katika kipindi hicho Serikali imejenga barabara na darasa la kudumu kati ya Kitunda na Kivule. Pia kuna zahanati na kituo cha afya.

Mgombea huyo ambaye alifuatana na mgombea kiti cha udiwani Kata ya Kitunda, Johnes Kaseno aliwahidi wakazi wa Kitunda kuwa baada ya kupata ushindi mwaka huu, watapanga maendeleo zaidi hasa kero ya barabara katika mitaa ya Kipunguni na Mzinga.

Wakati huo huo, mgombea kiti cha udiwani Kata ya Kitunda Johnes Kaseno aliwataka wanachama wa CCM kuzidisha mshikamano na kusahau matokeo ya kura za maoni.