Na Khatibu
Suleiman, Zanzibar
WAMILIKI wa boti
na ngalawa zinazovusha watu katika maeneo mbali mbali ya visiwa vidogo kisiwani
Pemba, wameanzisha mgomo wa kuwavusha watu wanaotofautiana nao kiitikadi.
Habari
zilizopatikana hapa jana kutoka Pemba, zilisema kuwa wenye boti hao hawataki kuwavusha
wananchi wasiyo wanachama wa chama wanachokishabikia. Inaaminika wengi wa
wamiliki hao ni wana CUF.
Kufuatia mgomo
huo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Kassim Tindwa, ametoa siku siku mbili
kurejesha huduma bila ubaguzi wa kiitikadi, vyenginevyo atafuta leseni za
biashara za vyombo vinavyobagua watu wa kuwavusha.
Kisiwa cha Pemba
kina visiwa vidogo vidogo kadhaa ambavyo wakazi wake wanalazimka kuvuka kwa
kutumia vyombo hivyo vya usafiri kutoka ama kuingia kwenye visiwa hivyo. Miongoni
mwa visiwa hivyo ni Kisiwa Panza, Fundo na Kojani.
“Natoa muda wa
siku mbili wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini kusitisha mgomo wao huo
mara moja, vyenginevyo nitafuta leseni zao za kutoa huduma ya usafiri,” Tindwa
alikaririwa na Sauti ya Tanzania Zanzibar akisema.
Mgomo huo huo wa
wenye vyombo vinavyovusha watu kwenda ama kutoka kwenye visiwa vidogo,
inaaminika umeanzishwa baada ya chama cha CUF kushindwa katika uchaguzi mkuu wa
Zanzibar, uliyofanyika Oktoba 30, mwaka huu. Wengi wa wanaoathirika ni wafuasi
wa Chama cha Mapinduzi.
Hali hiyo katika
kisiwa cha Pemba inaashiria kuibuka tena kwa siasa za chuki na uhasama, ambazo
miaka mitano iliyopita zilichukuwa nafasi kubwa kiasi ya watu wa familia moja
kushindwa kuzikana ama kuhudhuria shughuli za kifamilia.
Hali hiyo
iliondoka baada ya kutiwa saini Muafaka wa kisiasa mwaka 2001, kati ya vyama
vya CCM na CUF, ambapo wananchi wa Pemba walishiriki kikamilifu katika shughuli
za kijamii na maendeleo bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Hali ya kuwepo
kwa mgomo huo wa vyombo vya baharini umewakumba wananchi wanaoishi katika
kisiwa Panza ambao kwa muda wa siku tatu wameshindwa kuja ng’ambo ya pili
kupata huduma mbali mbali zikiwemo matibabu, kufuatia mgomo huo.
Kisiwa cha Pemba
ni moja ya ngome kubwa ya chama kikuu cha upinzani Zanzibar cha CUF, ambacho
katika uchaguzi wa Oktoba 30, kilizoa viti
vyote 18 vya
ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kisiwani humo.
Na Mbazigwa Hassan
MAMLAKA ya Reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA) imekubali kufanya mazungumzo na Kampuni ya Majisafi
na Majitaka mkoa wa Dar es salaam (DAWASCO) ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo la
uchafuzi wa mazingira katika eneo la Temeke-Sokota jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo inafuatia
mgogoro uliopo kati ya DAWASCO inayodaiwa kutaka kulipwa sh. milioni moja kila
mwezi kutokana na TAZARA kumwaga kinyesi katika kituo cha Sokota, kutoka kwenye
nyumba zake zilizopo Temeke kwa Maganga jijini.
Meneja wa Fedha na
Uhusiano wa TAZARA, Pascal Mulenga, alisema wameomba kulizungumzia suala hilo
kutokana na DAWASCO kushindwa kutoa huduma hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.
Alisema DAWASCO wanadai
sh. milioni 40 kwa madai ya kutoa huduma ya majitaka ya nyumba hizo, lakini
ukweli ni kwamba kampuni hiyo haijatoa huduma kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Mulenga alisema huduma
huyo inakosekana kwa sababu pampu ya kusukuma majitaka iliharibika siku nyingi.
“Ni kweli suala hilo lipo
na sisi hatupati huduma kutokana na kuharibika kwa mashine ya kusukuma
majitaka, hivyo kulazimika kutumia gari letu la majitaka. Hata hivyo,
tunafikiri jambo zuri ni kukaa nao ili tupate muafaka,” alisema.
Mulenga alisema wanafanya
utaratibu wa kuzungumza na wafanyakazi walionunua baadhi ya nyumba zao katika
eneo la Temeke-Maganga ili baadaye wahusike moja kwa moja kulipia ankara za
majitaka badala ya TAZARA, kwa sababu nyumba wanazoishi ni mali yao binafsi.
Alisema utaratibu huo
utafanywa baada ya kulipa deni la DAWASCO ili wasiwalipishe watu hao deni
lisilowahusu, na kuongeza kwamba baadhi ya nyumba wanazoishi askari wao ndizo
zitakazolipiwa.
Meneja Uhusiano wa
DAWASCO, Shyrose Bhanji, alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa uchafuzi huo wa
mazingira alikiri na kuongeza kuwa tatizo ni TAZARA ambao imekuwa hailipi deni
kwa muda mrefu na kuwafanya washindwe kutoa huduma kama inavyopaswa.
Wananchi wa eneo la
Temeke -Sokota walilalamika kwamba kinyesi cha binadamu kinafurika katika
mfereji ulio kando ya barabara ya Mandela na kusababisha harufu kali, jambo
linaloweza kusababisha kuenea kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Na Mwandishi Wetu, Iringa
MKUU wa wilaya ya Iringa,
Tatu Ruta, amewataka Watanzania kuacha tabia ya kuchoma moto mapori ili
kuepusha usumbufu kwa wanyamapori na wadudu wanaoishi kwenye mapori hayo.
Tatu alitoa wito huo
katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya
Iringa, wakati wa kuzindua maonyesho ya picha za wanyamapori yaliyodhaminiwa na
mtaalamu wa wanyamapori, Godwin Van Lawick.
Alisema Watanzania lazima
waheshimu mapori na misitu kwamba ni makazi ya viumbe wengi walio hai, na
kwamba kitendo cha kuchoma moto misitu ni sawa na kuchoma moto nyumba anayoishi
mtu.
Aliwasihi wachoma mkaa
nchini kutafuta ajira nyingine badala ya kuangamiza miti kila siku na
kusababisha kero kwa viumbe wengine.
Mdhamini wa maonyesho
hayo ya siku 20, Van Lawick, alisema Tanzania ina utajiri mwingi wa maliasili,
hususan miti na wanyama, lakini asilimia kubwa ya Watanzania hawana upendo kwa
wanyamapori.
Alisema wanyamapori ni
viumbe wanaostahili kuishi kwenye mapori yao bila bughudha na kwamba iwapo
mapori yataharibiwa, wanyama watavamia makazi ya watu.
Alisema wapo watu wazima
ambao hawajawahi kumwona mnyama wa porini kama tembo, ingawa wapo tele hapa
Tanzania.
"Nimeamua
kuwaonyesha picha mbalimbali za wanyama na kuwapa mafunzo ya kuwatambua wanyama
na kufahamu faida zao ili wawatunze na kupata faida mbalimbali," alisema
Na Mwandishi
Wetu, Mtwara
WANANCHI
wametakiwa kuuenzi ushindi wa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, kwa
kuichagua CCM katika uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano unaotarajiwa
kufanyika Desemba 14, mwaka huu, ili iweze kuendelea kuwaletea maendeleo.
Rai hiyo
ilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abiud Maregesi, wakati
akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika mwanzoni
katika Kijiji cha Mkangaula, Masasi mkoani hapa.
Maregesi alisema
matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar ni kielelezo tosha kwamba wananchi wa Zanzibar
wanaziamini serikali za CCM kutokana na utekelezaji makini wa ahadi zake
zinazotolewa kupitia Ilani za Uchaguzi.
Alisema CCM
ndicho chama pekee kinachotekeleza ahadi zake kwa wananchi na kikichaguliwa
tena kitahakikisha kinawaletea mafanikio makubwa zaidi kwa kushirikiana na
wananchi, na marafiki wa nje na ndani ya nchi.
Maregesi alisema
vyama vya upinzani kikiwemo CHADEMA na CUF bado vinajifunza uongozi ndani ya
vyama vyenyewe na havifai kupata kura za kuongoza nchi.
Aliwataka
wananchi wasidiriki kuwachagua wapinzani, kwani kuwachagua wapinzani ni sawa na
kujifunga kitanzi cha kuua maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mwenyekiti huyo
alisema vyama vya upinzani havina sera inayolenga kuwaletea maendeleo wananchi
wake na badala yake vimehubiri matusi na kuvuruga amani nchini.
Maregesi alisema
pamoja na vurugu za mara kwa mara zinazofanywa na vyama vya upinzani, hususan
CUF kuelekea uchaguzi mkuu ujao, CCM itaendelea kuendesha kampeni zake kwa
ustaarabu, kuheshimu sheria, amani na utulivu na kuwataka wananchi kuhudhuria
kwa wingi katika mikutano yake ya kampeni, lakini kura iende kwa wagombea wa
CCM.
Kwa upande wake
mgombea ubunge wa jimbo la Nanyumbu, Masasi mkoani Mtwara, Steven Mkapa,
alisema endapo atachakuliwa kushika wadhifa huo atashirikiana na serikali
kuharakisha maendeleo.
Alisema uwezo
anao, nia anayo ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo na kwamba
anachosubiri sasa ni ridhaa ya wananchi kumchagua ili aweze kuwatumikia kwa
moyo wa dhati kabisa.
Mkapa alisema
kwamba maendeleo ya jimbo hilo yatapatikana endapo wananchi wataipigia kura CCM
kuanzia mgombea wake wa urais wa Tanzania Jakaya Kikwete, wabunge na madiwani.
Alifafanua kuwa
akiingia madarakani atahakikisha kwamba anashirikiana kikamilifu na wananchi
wake katika kuhakikisha maendeleo hayo yanapatikana haraka.
Alisema maendeleo
katika jimbo hilo yatapatikana kwa njia ya ushirikiano na mshikamano na si kwa
mtu mmoja.
“Maendeleo katika
jimbo letu yatapatikana kwa njia ya kushirikiana, kwani yeye pekee hawezi
kufanikisha chochote hata kama angekuwa na uwezo wa kifedha,” alisema.
Na Esther Katua
KAMPUNI ya simu za
mkononi ya Vodacom imezindua kampeni ya ijulikanayo kama VodaMOTO ikiwa ni ofaa
maalumu kwa wateja wake kwa kipindi cha mwisho wa mwaka.
Wakizungumza na
waandishi wa habari kwa kupokezana kwenye viwanja vya Karimjee Jijini Dar es
Salaam jana, Mkurugenzi wa Masoko wa Vodacom Junaid Munshi na Meneja Masoko
Eprahim Mafuru walisema lengo la VodaMOTO ni kuwapa zawadi wateja wao kwa kuwa
nao kwa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Kwenye VodaMOTO
kutakuwa na vitu vinne ambavyo ni droo la shinda mamilioni na Vodataarifa,
punguzo la mawasiliano ya ujumbe usiku, nyongeza ya asilimia tano kwa kila
ongezo la fedha zitakazoingizwa kwenye simu na siku ya kufurahi na familia.
Wakifafanua
kuhusu ofa hizo, walisema nyongeza ya asilimia tano ya fedha unazoingiza kwenye
simu za muda wa maongezi zimeanza jana, ambapo kila kiwango cha fedha
utakazoingiza kwenye simu yako utaongezewa muda wa maongezi wa asilimia tano.
Wakizungumzia
droo la shinda mamilioni na Vodacom walisema mteja anapaswa kutuma ujumbe
kwenye voda taarifa kwa gharama ya sh. 150 iikiwemo VAT kwenda namba 155,
ambapo ataingizwa kwenye droo la kushindaniwa.
Walisema kila
wiki kutaendeshwa droo la washindi wa wiki ambapo shindano la mwisho
litafanyika baada ya wiki sita na watachaguliwa washindi sita ambao kila mmoja
atapewa sh. milioni tano.
Wakizungumzia
punguzo la utumaji wa ujumbe mfupi walisema kuanzia saa sita usiku hadi asubuhi
wateja wataweza kutumia sh. 30 kwa kutuma ujumbe badala ya sh. 45 ofa ambayo
itaanza leo.
Kuhusu siku ya
familia walisema kampuni ya Vodacom imeamua kuandaa matamasha kwenye mikoa ya
Arusha, Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam kwa lengo la kufurahi na wateja wao na
familia zao, hasa watoto yatima.
Wakizungumzia
kuhusu watoto yatima walisema Vodacom iliamua kutenga sh. laki tano kwa kila
kituo cha watoto yatima, ambapo wanatoa msaada kulingana na mahitaji ya kituo
au watatoa fedha taslimu.
Na Mwandishi Wetu
RAIS Benjamin
Mkapa leo anatarajia kuzindua rasmi jengo jipya la Ubungo Plaza lilipo karibu
na kituo cha mabasi yaendayo mikoani, jijini Dar es Salaam.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Ubungo Plaza,
Margaret Ikongo, ilisema jengo hilo linamilikiwa kwa ubia na Shirika la Bima la
Taifa (NIC), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Pensheni kwa
Watumishi wa Umma (PSPF).
Alisema jengo
hilo linatoa huduma mbalimbali kwa wakazi wa Dar es Salaam kama vile hoteli,
sehemu za kufanyia mikutano, ofisi, maduka na upangaji wa ofisi.
Margaret alisema
katika sehemu ya hoteli kutakuwa na vyumba 154, wakati ukumbi wa mikutano una
uwezo wa kuingiza watu 800 wakati kwa wapangaji wa ofisi tayari wameingia
kwenye jengo hilo toka Mei mwaka jana.
Baada ya uzinduzi
huo kesho, Rais Mkapa anatarajiwa kuzindua majengo ya Mahakama Kuu, Mahakama ya
Mkoa wa Iringa na Mahakama ya wilaya ya Iringa.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sam
Rumanyika, ilisema shughuli hiyo itaenda sambasamba na kuwaaga majaji wote wa
Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Na Mwandishi Wetu
WANAWAKE walitia
fora kwa kuwa wahitumu wengi kuliko wanaume katika mahafali ya 29 ya Chuo cha
Ustawi wa Jamii, kilichoko Kijitonyama, Dar es Salaam.
Katika mahafali
hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo,
Profesa Juma Kapuya, kati ya wahitimu 217, wanawake walikuwa 151. Hata hivyo
wahitimu 15 wa kozi ya cheti cha kompyuta hawakuainishwa jinsia zao.
Dk.Hosea
Rwegoshora, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, alitaja idadi ya wahitimu na kozi zao
katika ngazi ya cheti ni: Rasilimali Watu (40), Uongozi wa Kazi (6) na Ustawi
wa Jamii (62).
Katika ngazi ya
Stashahada za juu kwenye fani ya Usatwi wa Jamii (40), Uongozi wa Kazi (8),
Rasilmali Watu (30) na Stashahada ya Uzamili ya Ustawi wa Jamii (5).
Kaimu Mwenyekiti
wa Bodi ya chuo hicho, Ibrahim Marwa, alifafanua kuwa idadi hiyo ya wahitimu
mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 26, kwani mwaka jana ilikuwa 171 na kila
mwaka imeendelea kuongezeka.
Marwa alisema,
chuo hicho sasa hivi kinatarajia ifikapo mwakanai kitaanza kutoa shahada katika
fani zilizopo chuoni hapo, baada ya Mamlaka ya Elimu nchini kuidhinisha mitaala
yake na ndiyo hatua kuelekea kuwa chuo kikuu ndani ya miaka mwili ijayo.
Kwa mujibu wa
Marwa, nafasi ya kozi za Stashahada za juu zitachukuliwa na kuanzishwa kwa
mafunzo ya diploma katika fani hizo, pia katika mwaka wa masomo 2007/8 chuo
kinatarajia kuanza kutoa shahada ya juu na kuwa maandalizi yote yamekamilika.
Alilalamika hali
mbaya ya makataba ya chuoni hapo kuwa ni ndogo yenye uwezo wa kuchukua
wanafunzi 31 tu, jambo ambalo halikidhi haja na kuomba Wizara ya Kazi,
Maendeleo ya Vijana na Michezo iingilie kati.
Kuhusiana na
kampeni dhidi ya ugonjwa wa ukimwi, Marwa alisema chuo kimefanya utafiti kujua
hali ya ukimwi chuoni hapo na taarifa zake karibu zitachapishwa na kuwa
wanatarajia kuanzisha kituo cha ushauri nasaha.
Kwa upande wake,
Waziri Kapuya ameunga mkono juhudi hizo na kuongeza kuwa wizara yake inalenga
kuendesha mkakati kama huo kwa kutimia wataalamu wa chuoni hapo.
Alisema asilimia
68 ya vijana kitaifa ndio nguvu kazi ambayo pia ndiyo inaathirika zaidi na
ukimwi na ametaka juhudi zifanyike kulinusuru taifa na janga hilo.
Sambamba na hilo,
chuo kinatarajia kuanzisha kozi ya usuluhishi wa migogoro sehemu za kazi na
Waziri Kapuya, ameunga mkono mpango huo.
Na Omari Shaaban.
BODI za utalii za
nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, Kenya, Uganda na Tanzania, zimekubaliana
kuutangaza utalii kwenye nchi hizo kwa pamoja katika masoko ya kimataifa.
Makubaliano
yaliifikiwa Novemba 14 mwaka huu, kwenye soko la kimataifa la jijini London,
Uingereza ambapo wakurugenzi wa bodi hizo walikutana katika shughuli za
kutangaza utalii wa nchi zao.
Taarifa
iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wa jumuia hiyo, Magaga Alot, ilisema makubaliano
hayo hayatahusiana na utekelezeji wa masuala ya ndani ya utalii wa nchi
wanachama.
Hata hivyo,
alisema makubaliano hayo yataanza mwakani na katika kipindi kilichobakia, kila
nchi itakwenda kivyake kwenye masuala yanayohusiana na utalii.
Alisema katika
maonyesho ya utalii ya kimataifa ambayo yatafanyika hivi nchini Ujerumani, nchi
za Afrika mashariki zitashiriki kwenye banda moja litakaloitwa "East
African Village" lakini kila nchi itajitangaze kivyake.
Ofisa huyo
alisema makubaliano hayo ya pamoja yatatengenezewa kanuni zake na kwamba
mkutano wa kwanza wa kujadili mambo mbalimbali ya muungano huo utafanyika
mwakani na ambao utajadili masuala ya kisheria na mikataba.
Wakurugenzi wa
bodi za utalii waliokuwepo kwenye mkutano huo, nchini Uingereza ni Dk. Ongonga
Ochien wa Kenya, James Bahinguza wa Uganda na Peter Mwenguo wa Tanzania.
Wengine
waliohudhuria mkutano huo ni mchumi mwandamizi wa EAC kuhusu utalii, Dk. Nyamajeje
Weggoro, Mkurugenzi wa Utalii nchini, Selehe Pamba na Mkurugenzi wa utalii
nchini Kenya, Wanjiru Munene.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Weggoro alisema kuwa muungano huo ni mzuri kwa kuwa utaleta
ongezeko la utalii kwa nchi za Afrika Mashariki na kukua kwa ajira.
Madaktari rejeeni
kazini, komeni kujiona bora kuliko fani nyingine
MGOMO wa
madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) leo umeingia katika siku
ya tano, huku wakiwa wameshawarubuni hata wafamasia kuwaunga mkono. Madaktari
wanashiriki mgomo huo kwa wanachosema ni kuishinikiza serikali iwaongeze
mishahara kufikia sh. milioni 1.2 kwa kima cha chini, yaani kwa wanaoanza kazi.
Madaktari hao
wameahidi kuendelea na msimamo wao huo hadi serikali itakapokubali kutekeleza
madai yao kwa kuwawekea kwenye akaunti zao za benki fedha hizo, kulingana na
viwango vya kila mmoja vitakavyokuwa vinazingatia kima hicho cha chini. Wanasema
hivi sasa wanalipwa kima cha chini sh. 200,000 ambazo hazitoshi kukidhi
mahitaji.
Inawezekana
kabisa madai ya madaktari hao yakawa ya msingi na ambayo yanahitaji kufanyiwa
kazi ili kuwapunguzia makali ya maisha, na tunakubali kuwa kazi ya udaktari
inahitaji watu wenye utalaamu wa kutosha kwa maana kuwa waliokwenda shule.
Lakini
kinachoshangaza ni msimamo mkali uliochukuliwa na madaktari wetu hao wa kutaka
fedha kwanza, vinginevyo wataendelea kukaa wakishuhudia wagonjwa wakifa bila
msaada kutoka kwao. Inavyoeleweka ni kwamba katika mambo yanayohusu ugonjwa,
madaktari wana nafasi kubwa ya kuokoa maisha pale roho ya binadamu inapokuwa
haijafikia hatima yake kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Pamoja na kuwa
wameitisha mgomo, lakini tunaamini hali halisi ya maisha ya binadamu inafanya
hata hao madaktari wasutwe na hatua hiyo waliyoichukua kwa kuona au kuendelea
kusikia taarifa za vifo vya wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo. Watuambie:
Hivi kweli wanafurahia na kupiga vigelegele wanapopata taarifa kwamba wagonjwa
wengi wanazidi kupoteza maisha Muhimbili kutokana na mgomo wao?
Madaktari hao
watambue kuwa katika nchi yetu si wao pekee ambao taaluma yao ni muhimu kwa
jamii. Zipo kada nyingi za taaluma zilizo muhimu. Kwa kutambua kwamba kuna
uduni wa maslahi katika sekta karibu zote, je, sasa fasheni iwe kama hiyo ya
mgomo inayotumiwa na madakri wetu?
Mathalani, kuna
walimu waliowafundisha hata hao madaktari. Wapo polisi wanaofanya kazi kwa saa
24 kuhakikisha wanalinda mali na usalama wa raia, wakiwemo hao madaktari. Wapo
wanajeshi ambao ni mahiri katika ulinzi wa usalama wa mipaka ya nchi yetu. Wapo
wahandisi wa fani mbalimbali, zikiwemo za ujenzi wa miundombinu kama barabara
na madaraja.
Pamoja na
kutambua mchango wa Watanzania wote hao, na wengine, katika kutoa huduma na
kuijenga nchi yetu, vipi madaktari ndio sasa wajione ndio bora zaidi na kutoa
masharti ambayo lazima kwanza yatekelezwe bila kujali roho za watu zinazotoweka
kutokana na hatua yao hiyo?
Tunavyofahamu ni
kwamba katika nchi inayojali kuzingatiwa kwa taratibu na utawala wa sheria,
utekelezaji wa mambo mbalimbali daima hufuata kanuni.
Na serikalini
ambako ajira ya madaktari wanaogoma sasa huangukia, utoaji wa maslahi ni jambo
linalozingatia bajeti. Je, ndugu zetu hawa madaktari wasomi, wanaelewa kwamba
fedha wanazotaka wawekewe benki mara moja kabla ya kuendelea na kazi zao,
zimeshaidhinishwa kwa mujibu wa taratibu? Kama hawaelewi, na kama hazijaidhinishwa,
shinikizo lao hilo ambalo tayari linaathiri uhai wa watu ni la nini?
Wimbi la sasa la madai
haya ya madaktari si la kwanza. Mara zote ni madai yanayoandaliwa kwa uongozi
wa madaktari hao. Pengine tujiulize: Hivi uelewa wa viongozi wa madakari hao na
madaktari wenyewe ni finyu kiasi cha kutofahamu taratibu zinazohusu utoaji wa
malipo ya serikali zinavyofanya kazi?
Kwa sababu baada ya
kuanza kwa mgomo wa sasa, serikali ilijitahidi kueleza hatua iliyokuwa
imefikiwa katika utekelezaji wa madai hayo, lakini madaktari wakasema hakuna
watakachokielewa isipokuwa tu kukuta fedha zao benki. Hoja gani isiyokuwa na
mantiki hii? Au ndugu zetu hawa wana ajenda ya siri wasiyotaka kuiweka wazi,
wakitumia unyeti wa taaluma yao, likiwa ni tishio kwa uhai wa watu? Hivi iwapo
hizo fedha wanazoziota hazipo, huu ndiyo sasa utakuwa mwisho wa utekelezaji wa
taaluma yao Muhimbili?
Tujuavyo, kulingana na
uwezo wake katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali, Serikali kwa upande wake
imejitahidi kuwawekea mazingira mazuri wananchi wake, ikiwemo kutoa fursa za
kusoma bure au kwa gharama nafuu kwa watu mbalimbali, wakiwemo hao madaktari. Nani
asiyejua kwamba madaktari wamekuwa wakifaidika na mambo mengine kama kusamehewa
kodi wanapoingiza vitu, yakiwemo magari? Hivi hatua yao hiyo ya kugoma ndiyo
ielezeke pengine kwamba ni ‘shukrani ya punda ni mateke’ kiasi cha kupuuza
kuokoa roho za watu?
Madaktari waangalie tena
uamuzi wao na kurejea kazini huku matatizo yao yakiendelea kushughulikiwa. Hakuna
fedha ambazo mtu akipewa anaweza kusema zinatosha. Madaktari wetu wasidhani wao
ni tofauti na watendaji wa fani zingine.
Wakishaelewa hivyo
hawatathubutu kila kukicha kuiona fani yao kama silaha ya kuonyeshana ubabe na
serikali, kwa kugoma kufanya kazi, hali ambayo inasababisha kero kubwa kwa
wagonjwa, huku wengi wao wakipoteza uhai kwa sababu tu wataalamu wetu hao wa
tiba wanataka kima chao cha chini mishahara kiwe sh. milioni 1.2.