UHURU 22.09.2005
WAGOMBEA URAIS UCHAGUZI MKUU 2005:
Warioba, Wassira wasema Kikwete ndiye bora zaidi
Waongeza ni mchapakazi hodari, mfuatiliaji wa mambo
Na Bashir Nkoromo, Bunda
WANASIASA wakongwe nchini, Jaji Joseph Warioba na Stephen Wassira wamemmwagia sifa mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete kuwa ndiye mgombea bora zaidi kulinganisha na wengine.
Jaji Warioba ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu na Wassira, aliyepita bila kupingwa katika ubunge wa Bunda, walisema hayo jana wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa soko, kwenye jimbo la Mwibara mkoani Mara.
Warioba alisema Kikwete ni kiongozi bora miongoni mwa wateule wa CCM ambaye ni mchapakazi hodari na mfuatiliaji wa mambo. Kutokana na sifa hiyo, aliwaomba wananchi kumchagua ili awe Rais wa nne wa Tanzania.
Mbali na sifa hiyo, alisema Kikwete ni mtu mwenye upeo mkubwa katika kuongoza kwa kuwa ni mtu mwenye kufanya kazi bila kujali dini, rangi, kabila wala aina yoyote ya ubaguzi.
“Ni mtu asiyechoka katika kufanya kazi kwa maslahi ya taifa. Kutokana na haya upo ushahidi kwamba huyu ndiye Rais wa nne wa Tanzania,” alisema huku akishangiliwa na umati wa watu waliokuwepo uwanjani hapo.
Wassira kwa upande wake alisema wananchi hawana budi kumchagua Kikwete ili awe kiunganishi baina yao na serikali.
“Mkimchagua Kikwete mtakuwa mmefanya kazi nzuri, kwani atawaunganisha vyema katika kuwaletea maendeleo. Lakini mkichagua wapinzani hamtawasiliana naye,” alisema.
Warioba na Wassira waliungana na Mlezi wa CCM Mkoa wa Mara, Pius Msekwa kuwaomba wananchi kumchagua Kikwete kuwa Rais wa Tanzania.
Mbali na Kikwete, waliwaomba wananchi wa Mwibara kumchagua Charles Kajege kuwa Mbunge wa Mwibara. Jimbo la Mwibara kwa sasa liko chini ya TLP ambapo mbunge wake ni Muttamwega Mgahywa.
Waliwataka wananchi wa Mwibara kumpa likizo Mgahywa kwa kumchagua Kajege, kwani kuendelea kumchagua mpinzani ni sawa na kupoteza bahati ya maendeleo.
Msekwa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi, kwa upande wake alisema wapinzani Bungeni wamekuwa wakipinga tu mipango ya Chama na Serikali.
Kutokana na hali hiyo, aliwaomba wananchi kuichagua CCM ili kufanikisha kupitishwa kwa mipango mingi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wake, Kikwete aliwaomba wananchi kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani kutoka CCM ili kuunda timu bora ya kazi.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha maslahi ya watumishi yanaboreshwa. Pia, alisema wanawake na vijana watawezeshwa kimtaji ili kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Kabla ya kuhutubia Mwibara, Kikwete alipita katika vijiji vya Kukirirungu, Kerita na Guta. Katika kijiji cha Guta alizuiwa na wanafunzi ambao walimtaka azungumze nao.
Baada ya Mwibara, Kikwete alikwenda Bunda kwa ajili ya mkutano mwingine wa kampeni na baadaye kwenda Tarime na Sirari kwa mikutano mingine.
Hatimaye wastaafu wa EAC kulipwa leo
Malipo kufanywa benki za NMB na CRDB
Na Lauden Mwambona
WALIOKUWA wafanyakazi wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) nchini wataanza kulipwa mafao yao kupitia katika benki za CRDB na NMB jijini Dar es salaam kuanzia leo.
Majina ya wanaolipwa leo yamo ndani ya gazeti hili wakati mengine yataendelea kutolewa kesho.
Taarifa hiyo ilitolewa na viongozi wa wastaafu hao mbele ya wenzao karibu 1,000 waliokusanyika eneo la Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kusubiri kauli ya mwisho kufuatia malumbano yaliyojitokeza tangu Septemba 19, mwaka huu, ambapo ilikuwa siku ya kuanza kulipwa mafao hayo.
Ulipwaji wa mafao hayo ulikwama juzi baada ya wastaafu waliofungua kesi mahakamani kusita kutia saini makubaliano ya kufuta kesi ili serikali iweze kuwalipa mafao yao.
Waziri wa Fedha, Basil Mramba alitangaza mapema wiki hii kwamba serikali ilitenga sh. bilioni 117 ili kuwalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa Jumuia hiyo walioacha kazi mwaka 1977 baada ya Jumuia kuvunjika.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake jana, mmoja wa viongozi wa wastaafu hao, Stephen Kivuma alisema maamuzi ya kuanza kulipwa leo yalitolewa alasiri kufuatia kumalizika kwa malumbano yaliyokuwepo juu ya umuhimu wa wastaafu wote kukubali kuondoa kesi mahakamani ili serikali iweze kulipa fedha zilizotengwa.
Kivuma alisema wastaafu wametia saini kukubali kufuta kesi na kwamba serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha imeahidi kuanza kulipa leo saa tatu kupitia benki zilizotajwa hapo juu.
Alisema benki ya NMB ina uwezo wa kuwalipa wastaafu 2000 kwa siku wakati CRDB ina uwezo wa kuwalipa wastaafu 400 kwa siku jambo ambalo alisema kazi ya kupokea fedha inaweza kuendelea kwa siku kadhaa.
Kwa kuanzia, alisema NMB tawi la jengo la NSSF Water Front maarufu kwa jina la jengo la NASACO itatoa malipo kwa waliokuwa wafanyakazi wa Bandari na wale wa Cargo na baadaye watafuatia wa Reli wakati CRDB itaanza kuwalipa waliokuwa wafanyakazi wa Shirika la Posta na Simu enzi za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Awali, Waziri wa Fedha, Mramba alipoulizwa jana juu ya msimamo wa wastaafu hao kusita kutia saini, alisema hadi saa sita mchana wa jana, wawakilishi watatu kati ya saba walikuwa wametia saini makubaliano hayo na kwamba kilichotakiwa ni mjumbe mmoja zaidi.
Naye Wakili wa wastaafu hao, Jonathan Lukwaro alipoulizwa alisema wateja wake hadi saa nne asubuhi walikuwa wameonyesha nia ya kutia saini makubaliano hayo na alisisitiza mgogoro huo ungekwisha jana hiyo.
Baadhi ya wastaafu walipoulizwa juu ya msimamo wa kukataa kutia saini makubaliano ya kufuta kesi mahakamani, walionyesha kusikitishwa na msimamo huo wakidai hauna maslahi kwao.
“Sisi tunataka mafao, hivyo ni bora tupokee kwanza yanayotolewa na serikali ili tujue ni kiasi gani na baadaye tudai mengine tutakayopunjwa,” alisema mmoja ambaye hakutaka kuandikwa jina lake.
Hata hivyo, wastaafu wengi waliohojiwa ili kujua kiasi wanachodai kama mafao yao, walisema hadi jana walikuwa hawajui kiasi kamili kwa kila mmoja.
Lakini walidai serikali iliahidi kuwalipa sh. bilioni 50, baadaye iliongeza hadi sh. bilioni 400 na sasa imetangaza kwamba itawalipa bilioni 117 na kwamba kwa kauli hizo inaonyesha zipo fedha nyingi.
Wastaafu wengine waliwanyooshea vidole waliokuwa wafanyakazi wa Bandari kwamba ni wabishi wa mambo ya kweli na ndio waliosababisha hata kucheleweshwa kwa suala la utiaji saini makubaliano ya kufuta kesi mahakamani.
Lakini wastaafu wengine walisema walishangaa kuona baadhi ya wenzao wakiuingiza mgogoro huo kwenye masuala ya kisiasa kwa kutishia kuinyima kura CCM, jambo ambalo hata wakichagua chama kingine ndio kwanza uhakika wa kupata utapotea.
“Tatizo la baadhi ya wenzetu wanachanganya mafao na siasa, na ndio maana wanazusha mabishano makali ili watu waichukie CCM,” alisema mmoja wa wastaafu hao.
Habari kutoka Wizara ya Fedha zilisema, suala la mafao ya wastaafu hao limepewa msukumo na Rais Benjamin Mkapa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM ikiwa ni moja ya malengo ya CCM kupunguza kero za wananchi.
‘Pimeni uwezo wa vyama kwa kusoma katiba zao’
Segamba asema CCM itaboresha maisha ya wananchi
Na Prosper Kulita, Morogoro
WATANZANIA wametakiwa kupima uwezo wa vyama kwa kusoma katiba na sera ili kujua zinasemaje kabla ya kuamua wachague chama gani katika uchaguzi mkuu ujao.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM mkoa wa Morogoro, Aluu Segamba alipokuwa akiwanadi mgombea ubunge wa jimbo la Morogoro mjini na baadhi ya madiwani wa kata mbalimbali za manispaa ya Morogoro kwa tiketi ya CCM.
Segamba alisema kuwa moja ya kipimo cha mwananchi kwa vyama ni katiba ambazo zinaeleza undani wa shughuli za vyama husika na kwamba wananchi wakizisoma wataweza kupata uamuzi wa wakipigie kura chama gani.
Alisema kutokana na katiba hizo, mwananchi watajua namna chama kinavyojiendesha sambamba na kinavyoshirikiana na wananchi kuleta maendeleo.
Aliongeza kuwa wananchi wakiyafahamu yote yaliyoainishwa katika vitu hivyo, watakuwa katika nafasi nzuri ya kutambua chama hicho kitafanya nini kikipata madaraka ya nchi.
Hata hivyo, Segamba alisema chama kilichoweka msingi imara wa kisera kupitia Ilani ya Uchaguzi ni CCM ambacho sera zake ni tofauti na vyama vingine, kwani zimelenga kuwaletea wananchi wote maendeleo.
Akitoa mfano, alisema moja sera iliyomnufaisha Mtanzania kwa sasa ni ya elimu ambayo imewezesha kutoa elimu kwa watu wote, hata wale wasioipata kupitia mpango wa MEMKWA.
Mbali na sera hiyo, CCM imesimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2000/05 kwa kiwango kikubwa, kwani imeimarisha miundombinu ya barabara, sekta ya afya na elimu, mambo ambayo yanalenga kumwondolea mwananchi umasikini.
Akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2005, Segamba alisema imeainisha maeneo mbalimbali ambayo yanalenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini.
Dk. Mzeru kuhakikisha Morogoro inapata hospitali ya wilaya
Na Prosper Kulita, Morogoro
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Morogoro mjini kwa tiketi ya CCM, Dk. Omary Mzeru amesema iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo atahakikisha wilaya ya Morogoro inapata hospitali ya wilaya.Alisema hospitali hiyo itasaidia kupunguza kero mbalimbali wanazozipata wananchi, hasa wanapokwenda kupata huduma katika hospitali ya mkoa.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dk. Mzeru alisema kuwa kutokana na idadi ya wakazi wa Morogoro kuongezeka, kuna ulazima wa kupata hospitali ya wilaya ili kwenda sambamba na mahitaji ya ongezeko hilo.
Alisema anatambua kuhusu adha wanazopata wakazi wa jimbo hilo, hasa kinamama hivyo amedhamiria kuboresha hospitali ya Sabasaba iliyoko eneo la CCM mkoa wa Morogoro kuwa na hadhi ya hospitali ya wilaya ambayo kwa sasa inatoa huduma katika vitengo vya macho na meno.
Pamoja na kuifanya kuwa hospitali ya wilaya, pia mgombea huyo wa CCM alisema amedhamiria kufanya mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya barabara, afya na elimu.
Kuhusu afya alisema wananchi watafaidika kutokana na mpango wake endelevu wa kujenga zahanati katika kila kata za jimbo la Morogoro Mjini ambapo kwa kuanzia anatarajia kushirikiana na wananchi kuziboresha zahanati zote zilizopo na pia kuanza ujenzi katika kata ambazo hazina zahanati kwa sasa.
Akizungumzia sekta ya elimu, Dk. Mzeru alisema anatarajia kuendelea kuongeza idadi ya shule za sekondari na msingi ambazo kwa sasa alisema idadi yake haijakidhi hali ya ongezeko la wakazi wa jimbo hilo.
Alisema kuwa katika kutekeleza hilo, atahakikisha katika kipindi cha miaka mitano hakuna kata ambayo haitakuwa na shule za sekondari.
Alisema kuwa pamoja na kuwa na shule za msingi, lakini bado mahitaji yake ni makubwa ambapo kwa kushirikiana na wananchi atahakikisha idadi ya shule inaongezeka ili kuondokana kabisa na tatizo la uhaba wa madarasa ya shule za msingi.
Katika kuboresha barabara za manispaa ya Morogoro, mgombea huyo alisema mpango wa serikali ya awamu ya nne ni kuhakikisha kuwa barabara zote zinazounganisha mji zinakuwa katika kiwango cha lami na pia zile zinazoingia katika mitaa mbalimbali kuwa katika kiwango cha changarawe ili kukabiliana na uharibifu wa barabara hizo.
Mbali na kuhutubia umati mkubwa wa wakazi hao, Dk. Mzeru pia aliwataka wananchi kuachana na propaganda zinazoendeshwa na vyama vya upinzani kwamba CCM haina nia ya kuboresha maisha ya Watanzania.
Karume asema upinzani uliopo Z’bar ni wa mafisadi wa maendeleo
Na Mwandishi Wetu, Wete, Pemba
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) Amani Abeid Karume amesema Zanzibar hakuna vyama vya upinzani kwani vilivyopo ni mafisadi wa maendeleo ya nchi.
Akihutubia katika mkutano wa kampeni huko Kangageni jimbo la uchaguzi la Ole Wete, Karume alivionya vyama vya upinzani kwa tabia yao ya kutisha wananchi zaidi pale wanapovikimbai vyama hivyo na kujiunga na CCM.
“Serikali haitoshi kutumia nguvu za dola kudhibiti tabia hiyo kwa mujibu wa sheria navitaka kuacha tabia hiyo mara moja,” alisema Karume.
Alisema wananchi wanao uhuru wa kuchagua kujiunga na chama chochote hivyo ni makosa kutumia udikteta kuwatisha.
Rais Karume alisema tabia yakutishana imekwisha tangu mwaka 1964 baada ya wananchi wazalendo kuuondowa madarakani utawala wa kisultani.
Aliwataka wananchi wa Pemba kukichaguwa Chama Cha Mapinduzi ambacho kimeonyesha uwezo mkubwa wa kuongozi nchi na kuleta maendeleo.
Alisema maendeleo yaliyopatikana katika kisiwa cha Pemba ni mengi ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, bandani pamoja na sekta ya maji na elimu.
apema Rais Karume alipokea wanachama kutoka CUF ambao kwa hiari yao wameamua kujiunga na CCM baada ya kuridhishwa na sera zake tofauti na upande wa upinzani ambao una ahadi hewa. Katika risala yao walisema daima watakuwa wana Chama waaminifu na watiifu.
Karume: Zama za uongo wa kisiasa zimepita
Asema Pemba ya sasa sio ile ya zamani
Na Khatib Suleiman,Chake Chake Pemba.
RAIS wa Zanzibar Amani Abeid Karume amesema zama za kusema uongo katika siasa zimepitwa na wakati kwani wanachotaka wananchi sasa ni maendeleo ya kweli ambayo yatasaidia kuinua uchumi na hali zao za maisha.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Wesha muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la bandari ya Wesha, Rais Karume alisema wananchi wa Pemba wamejionea wenyewe jinsi Serikali ya awamu ya sita ilivyotekeleza Ilani yake ya uchaguzi katika kuleta maendeleo kisiwani Pemba.
“Ujenzi wa bandari ya Wesha kisiwani Pemba ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2000 ambayo lengo lake kubwa ni kuimarisha miundombinu katika sekta ya mawasiliano,” alisema Karume na kuongeza haya ni maendeleo ambayo wananchi wanayaona.
Karume alisema Pemba ya leo sio ya mwaka 1970 na hatua ya maendeleo iliyofikiwa ni ya kupigiwa mfano ikiwemo ujenzi wa barabara za mjini na vijijini pamoja na mafanikio katika sekta ya elimu na maji safi na salama.
Alisema utekelezaji wa mafanikio ya Ilani ya mwaka 2000 ni ushahidi tosha kwamba sasa wapinzani hawana maneno ya kusema kwani wamekatwa kile kidomodomo walichokuwa wakiwatisha wananchi kwa kusema uongo.
Rais Karume aliweka jiwe la msingi ujenzi wa bandari ya Wesha, Chake Chake Pemba ambayo hadi kumalizika kwake itasaidia kwa kiasi kikubwa kwa meli kuweza kutia nanga na kushusha bidhaa na abiria.
Mapema Meneja Mkuu wa Shirika la Bandari la Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha miundombinu katika kisiwa cha Pemba ikiwemo ujenzi wa bandari ya Mkoani na ile ya Wete ambazo zote hizo ni muhimu katika mawasiliano na uchumi.
Alisema wanatazamiwa kutumia jumla ya sh. milioni 576 kwa kukamilisha kazi za miundo mbinu katika kisiwa hicho, ambapo fedha zote hizo zinatoka katika Mfuko wa Shirika la Bandari bila ya kutegemea wahisani. Ujenzi wa gati hiyo utatumia sh. milioni 120.