UHURU 23.11.2005

 

 

Kikwete asema CUF isubiri kipigo Des. 14

Asema baada ya kushindwa Zanzibar imechanganyikiwa

Na Rashid Zahoro, Kibiti

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete

amesema hivi sasa CUF imechanganyikiwa na kwamba isubiri kipigo cha dhoruba

ifikapo Desemba 14.

"CUF imechanganyikiwa, baada ya kushindwa Zanzibar sasa wajiandae kupata kipigo

kikubwa na cha dhoruba nzito katika uchaguzi mkuu wa Desemba 14.

"Desema 14 ikifika hakuna cha Lipumba wala cha Mbowe, mimi ndiye nitakayeibuka

mshindi baada ya uchaguzi wa siku hiyo... safarini tupo wengi, lakini wengine

wananisindikiza mimi," alisema.

Kikwete aliyasema hayo jana alipoanza kampeni zake wakati aliposimama kuwasalimia

wananchi wa vijiji vya Jaribu Mpakani, Bungu na Hanga, akiwa njiani kwenda

kuhutubia mikutano ya kampeni katika maeneo ya Nyamisati na Kibiti mkoani Pwani.

Kuhusu wanasiasa wanaotumia nyumba za ibada kuendesha kampeni, Kikwete alisema

wanasiasa wa namna hiyo wamefilisika kisiasa na kwamba kamwe wasichaguliwe.

"Hawa watu hawana kitu ndio maana wanakimbilia misikitini… misikiti ni sehemu ya

kusali na kumwabudu Mungu siyo siasa. Anayekimbilia huko siasa imemshinda,

amefilisika, hana mbele wala nyuma," alisema Kikwete.

Akizungumzia bei ya korosho, mgombea urais huyo wa CCM, aliwaahidi wakazi wa

vijiji vya Bungu na Hanga kuwa atahakikisha bei ya zao hilo inakuwa nzuri ili

waweze kufaidika na zao hilo.

Kikwete alisema serikali ya awamu ya nne imepania kuinua kilimo na kukuza uchumi

wa Tanzaania na pia kupanua masoko ya mazao ili wakulima wawajue wanunuzi.

"Sio leo anakuja Fidha Hussein kesho Mohamed Enterprises... tunataka mkulima awe

na soko la uhakika na amjue mnunuzi wake," alisema Kikwete.

Kikwete alikiri kufahamu kuwepo kwa wanunuzi wa korosho ambao huwapunja wakulima

kwa kushusha bei za zao hilo na kwamba atahakikisha hali hiyo inakoma mara moja.

Kuhusu vijana wa vijiji hivyo, Kikwete aliahidi kuwatatulia tatizo la ajira kwa

kuwapatia mitaji kwa njia ya mikopo ili waweze kujiajiri wenyewe.

Kikwete katika msafara huo pia alizungumza na wananchi katika vijiji vya

Nyamtonga, Minjeti na Nachiga kabla ya kufanya mkutano mikubwa Nyamisati na

Kibiti.

Katika mikutano hiyo, Kikwete alimtambulisha pia mke wake, Mama Salma Kikwete na

kwenye mkutano wa Kibiti alimnadi Mgombea ubunge wa jimbo hilo, Abdi Malombo.

 

 

'Upinzani kuiona Ikulu kwa mialiko ya dhifa'

Dk. Sheni asema bado havina hadhi

Na Dunstan Bahai, Tanga

VYAMA vya upinzani bado havijafikia hadhi ya kwenda Ikulu na badala yake wataiona

kwa mialiko maalumu watakayopewa kwa ajili ya kuhudhuria dhifa za kitaifa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Sheni

wakati akihutubia mikutano miwili tofauti katika wilaya za Mkinga tarafa ya

Maramba na Pangani katika ziara ya mkoani hapa inayomalika leo.

Leo anaendelea na ziara yake mkoani Arusha, lakini akiwa njiani kuelekea huko,

kila wilaya atakayopita atasimama kidogo kuwasalimia wananchi.

"Kutokana na kutokuwa na uwezo kwa vyama vya upinzani, Ikulu watafika kama

waalikwa wa shughuli maalum kama vile kukiwa na sherehe au mambo mengine ya

kitaifa," alisema Dk. Sheni huku akishangiliwa na maelfu ya mashabiki, wanachama

na wafurukutwa wa CCM.

Alisema vyama vya upinzani bado ni wachanga, havina uwezo, havina uzoefu, havina

ujuzi, "hata ubwabwa wa shingo haujawatoka," aliongeza.

Dk. Sheni alisema kutokana na amani na utulivu na mafanikio katika huduma za

kijamii kuboreka, hasa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ili yaendelee

kuboreshwa, wananchi wanaaswa kuichagua CCM.

"CCM itashinda watake wasitake, kwa nguvu ya wananchi. Ushahidi halisi ni katika

uchaguzi wa Zanzibar. CCM iko nchi nzima na ina nguvu ya ushindi wa kishindo

kutokana na wananchi kuwa na imani nayo," alisema na kukebehi sera za baadhi ya

vyama vya upinzani kuwa ni za vitisho na kunoa mapanga hali yenye lengo la

kuwagawa Watanzania.

Mgombea mwenza huyo ambaye pia ni Makamu wa Rais, alisema wapinzani wanapanga

mipango mingi kwa kutumia sera za Chama Cha Mapinduzi. "Domo utindi maziwa kwa

mwenye ng'ombe," alitoa msemo huo ambao uliangua vicheko kwa mashabiki

waliohudhuria mkutano uliofanyika Maramba.

Akiwa wilayani Pangani, Dk. Sheni alisema serikali ya awamu ya nne inakusudia

kuwaondolea kero zinazowakabili Watanzania na kwa upande wa wilaya ya Pangani

alibainisha kero kubwa kuwa ni barabara na kivuko.

Dk. Sheni alisema kwa upande wa kivuko, serikali yake itatoa ufumbuzi wa muda

mfupi kwa kununua kivuko kipya na kwamba ufumbuzi wa kudumu utafuatia kwa kujenga

daraja linalounganisha Pangani mjini na kijiji cha Bweni wakati upande wa barabara

alisema upo mradi unaojenga barabara ya kutoka Saadani Bagamyo kupitia Pangani

hadi Horohoro.

Alisema pia kuwa kitajengwa chuo cha ufundi stadi (VETA) ili kuwaandaa vijana

wanaomaliza shule ili waweze kujitegemea.

Mgombea mwenza alisikitishwa na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vyama vya

upinzani na kufafanua kuwa kuwepo kwa vyama vingi si fujo bali ni kushindanisha

hoja ambazo zitawashawishi wananchi kujiunga na chama wanachokipenda kulingana na

sera zake.

Akiwa Maramba, Dk. sheni alipokea wanachama 526 kutoka vyama vya upinzani ambao

wamejiunga na CCM. Wanachama hao ni kutoka CUF (405), TLP (56), CHADEMA (30) na

NCCR-Mageuzi (35) wakati Pangani aliwapokea 502 kutoka CUF (380), TLP (62),

NCCR-Mageuzi (48) na CHADEMA (12).

Wanachama hao walifananishwa na mwana mpotevu aliyepotea njia na baada ya kugundua

hali hiyo alirudi haraka nyumbani kwa baba yake.

 

 

Rais Mkapa awataka Majaji, Mahakimu kupiga vita rushwa

  • Asema hali hiyo itawajengea imani kwa wananchi

Na Mwandishi Wetu

 

RAIS Benjamin Mkapa

 

RAIS Benjamin Mkapa amewataka mahakimu na majaji kujenga imani kwa wananchi kwa

kupiga vita rushwa na kukubali kuwajibika kwao.

Hayo yamo kwenye hotuba ya Rais Mkapa aliyoitoa jana kwenye uzinduzi wa majengo ya

'Uwanja wa Haki Iringa' katika hafla iliyofanyika mkoani Iringa na hotuba yake

kupatikana mjini Dar es Salaam.

"Kama mnataka wananchi wawaheshimu, na wawe na imani na mahakama, lazima mkubali

kuwajibika kwao na mpige vita rushwa kwa nguvu zenu zote.

"Si kwamba mahakama ina ukiritimba wa rushwa, la hasha. Lakini rushwa ikijipenyeza

kwenye mahakama ubaya wake unakuwa maradufu maana juhudi za wengine wote kupiga

vita rushwa zitakwama zikifika mahakamani," alisema Rais Mkapa katika hotuba yake.

Rais Mkapa alisema kuna haja ya kuwa waangalifu kwa siku zijazo ili kuwezesha

Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ziweze kufikiwa na watu wengi kwa maana ya

umbali na gharama.

Alisema kuwa matarajio yake ni kwamba kuwe na Mahakama Kuu katika kila mkoa ili

kuwezesha kila mwananchi kuweza kuitumia huduma ya mahakama hiyo.

Rais Mkapa pia alisema katika mahakama hizo kuna tatizo la gharama ya kutafuta

haki na kuongeza kuwa iwapo gharama hizo itakuwa nje ya uwezo wa mwananchi wa

kawaida basi hataweza kupata haki yake.

Aliongeza kuwa mawakili nao gharama zao zimekuwa kubwa na kuhoji iwapo kuna

wananchi wengi wanaoweza kumudu gharama za mawakili ambazo ni mamilioni ya fedha.

Rais Mkapa alisema katika siku zijazo kuna haja ya kuchangia mawazo ya namna ya

kuwasaidia wananchi ambao wanakosa haki kwa sababu ya unyonge wao na uduni wa

mapato yao.

Kuhusu masuala ya amani, alisema kuwa utawala wa sheria ni jukumu la kila

serikali, kila jamii, kila mtu na kila asasi na kwamba penye utawala wa sheria

hakuna ruhusa kuhalalisha au kufumbia macho uhalifu unaofanywa na vyama vya siasa.

 

 

Hakuna uchunguzi kuhusu uchaguzi Z'bar-SMZ

Na Khatib Suleiman, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema uchaguzi mkuu wa Zanzibar umekwisha na

hakuna mwenye uhalali na mamlaka ya kudai kufanyika uchunguzi juu ya uchaguzi huo.

Kauli hiyo ilitolewa hapa jana na Naibu Waziri Kiongozi, na Waziri wa Habari,

Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna. Alikuwa akizungumza alipokuwa

akimkabidhi ofisi Waziri mpya wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Amina Salum Ali.

Alisema Katiba na sheria za uchaguzi za Zanzibar hazitoi nafasi ya mtu ama chombo

cho chote kuhoji ama kutaka uchunguzi ufanywe juu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais.

Alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeshamtangaza Rais Karume kuwa mshindi wa

urais wa Zanzibar, na kwa mujibu wa Katiba na sheria ya uchaguzi, hakuna mwenye

uwezo wa kuhoji hilo kwa sasa kama chama cha CUF na baadhi ya nchi na taasisi za

kimataifa zinavyotaka.

Shamuhuna alisema kitendo cha kudai kufanyika kwa uchunguzi kwenye suala hilo

hakikubaliki.

Alisema kupitiwa tena matokeo ya urais baada ya kutangazwa rasmi na Tume ya

Uchaguzi kwa nafasi za urais, udiwani, na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,

hakukubaliki.

"Katiba ya Zanzibar iko wazi, hakuna chombo chochote kitakachohoji matokeo ya

urais wa Zanzbar baada ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzbar," alisema.

Chama cha CUF ambacho kilishindwa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30,

mwaka huu, kimepinga ushindi wa Chama cha Mapinduzi, na kukataa kumtambua rais

halali aliyepo madarakani, Amani Abeid Karume.

Chama hicho kikisaidiwa na baadhi ya nchi na taasisi za nje ya nchi zimekuwa

zikitoa madai ya kutaka kufanyika kwa uhakiki wa kura zilizopigwa katika uchaguzi

mkuu huo, kikidai ili kuondoa 'utata' wa matokeo ya uchaguzi huo.

Shamuhuna alisema matokeo yaliyotangazwa na ZEC ni halali ambapo rais

aliyetangazwa amekwishakula kiapo na kuunda serikali, hatua ambayo inakamilisha

muhimili mmoja wapo wa dola ambao ni serikali.

Alisema kitendo cha Rais Karume kuteuwa baraza la mawaziri, ni kitendo

kinachoashiria kuwepo madarakani na kutekeleza majukumu yake kama ilani ya CCM

inavyoelekeza baada ya kupata ushindi mkubwa.

Shamuhuna alisema Rais Karume ameunda Baraza la Mawaziri zito ambalo limezingatia

uwiano wa uwakilishi mkubwa wa wanawake kwa kuteuwa mawaziri wanne wanawake

akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi nchini Zainab Omar ambaye anakuwa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalumu.

Mapema, Waziri Amina Salum Ali aliwataka wafanyakazi na watendaji wa Wizara hiyo

kumpa kila aina ya ushirikiano ambao utafanikisha kutekeleza pamoja na kusimamia

majukumu yake muhimu ya ujenzi wa taifa.

"Ninachokitaka kwenu ni kupata ushirikiano wa kufanikisha majukumu tuliyokabidhiwa

yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi," alisema Amina ambaye

pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake nchini UWT.

 

Shahidi adai aliunguzwa matako kwa kuangushwa kwenye sufuria la supu

Na Mwandishi Wetu

SHAHIDI Mariamu Sadick (30), jana alidai mbele ya mahakama ya wilaya ya Ilala kuwa

alipigwa na kuangushwa kwenye sufuria lenye supu ya moto na kuungua matako, paja

na goti.

Mariamu alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu wa Wilaya Agnes Mchome, katika kesi

inayomkabili mshitakiwa Zena Seleman (41) na Rehema Said (25) wakazi wa Dar es

Salaam.

Alidai washitakiwa walikwenda katika banda la chakula maeneo ya Buguruni na

kurusha matusi ya nguoni kuwa aliiba sahani ya udongo.

Pia, Mariamu alidai washitakiwa walitoa matusi hayo ambapo mmoja wao alimvamia na

kumpiga kisha kumuangusha kwenye sufuria lenye supu ya moto.

"Mheshimiwa walinichangia wote kisha wakaniangusha kwenye sufuria la moto, kweli

niliungua matako, paja la kulia na kwenye goti," alidai Mariamu.

Aliongeza kuwa baada ya kuangushwa kwenye sufuria alitolewa na rafiki yake

aliyemtaja kwa jina la Amina na alikwenda kituo cha Polisi Buguruni.

Mariamu aliongeza kuwa baada ya kufika kituo hapo alipewa cheti cha polisi ambapo

alikwenda kutibiwa katika hospitali ya Amana, Dar es Salaam.

Washitakiwa hao wanadaiwa Mei 4 mwaka huu, saa tano asubuhi, katika maeneo ya

Buguruni relini, walimuunguza Mariamu katika sufuria lenye supu ya moto na

kumsababishia majeraha katika matako, paja na goti.

Washitakiwa walikana shitaka na wapo nje kwa dhamana hadi Januari 5 mwaka huu

ambapo kesi hiyo itaendelea kusikilizwa.

 

'Mashina yaunde vikundi vya kupambana na umaskini'

Na Furaha Omary

MGOMBEA udiwani wa kata ya Dovya, wilayani Temeke amesema mashina ya wakereketwa

wa CCM yatumike kuunganisha vijana katika masuala ya siasa na kuunda vikundi vya

kupambana na umaskini.

Mgombea udiwani huyo alisema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa shina la

wakereketwa la vijana wa kata hiyo.

Alisema mashina ya wakereketwa wa CCM pamoja na kuhamasisha masuala ya siasa

lazima yawe na mipango ya maendeleo ili kujikwamua katika umaskini.

Aliongeza kuwa mashina hayo pia yawe ya vijana wenye itikadi safi ya CCM na

wasaidie kuimarisha chama na kupambana na wanasiasa uchara bila kuyumbishwa.

Mgombea huyo wa udiwani, alisema maneno yanayotolewa na wanasiasa 'uchwara' ni ya

uongo na lengo lake kubwa ni kuchafuliana, ili Chama kisipate ushindi.

"Sikatai uchaguzi wa 2000 niliahidi kukamilisha ujenzi wa barabara, ikiwa ni moja

ya mambo niliyoyaahidi, lakini bado nina uwezo wa kukamilisha ujenzi huo katika

kipindi kijacho," alisema Mwakasindile

Katika hafla hiyo, vijana wa kata hiyo walimuhakikishia ushindi wa 'kishindo' na

kumtaka awe mlezi wa shina hilo waweze kufanikisha malengo yao.

Shina hilo lilianzishwa na vijana 15, ambapo hadi sasa lina vijana 30 ambao

wanajishughulisha na masuala mbalimbali ikiwemo muziki.

Mwakasindile aliwahakikishia vijana hao kuwawezesha kimuziki kwa kukiuza uchumi wa

nchi kutokana na shughuli zao katika kikundi hicho.

 

Ujumbe wa Chama cha Kikomunisti China wawasili

Na Mwandishi Wetu

UJUMBE wa watu 48 kutoka Chama cha Kikomunisti cha China ulitarajiwa kuwasili

nchini jana usiku kwa ziara ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine leo

utakuwa na mazungumzo na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, yatakayofanyika

hoteli ya Movenpick.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM jijini Dar es salaam jana

jioni, ilisema ujumbe huo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Kamati ya

Siasa ya Chama , Li Changchum.

Mazungumzo kati ya ujumbe huo na Katibu Mkuu wa CCM, Mangula, yanatarajiwa kuanza

saa tatu asubuhi.

Viongozi waandamizi wa CCM , Makamisaa wa CCM ndani ya serikali na baadhi nya

maofisa na makada wa CCM wamealikwa kwenye mazungumzo hayo.

 

Sh. milioni 500 kukamilisha barabara ya Dabiri

Na Serafina Sungusia, Babati

SHILINGI milioni 500 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya

mlima Dabiri kwenda Bashnet wakati sh. milioni 290 zimetumika kuunganisha nishati

ya umeme kata ya Bashnet wilayani Babati mkoani hapa.

Akizungumza na wakazi wa Dareda, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Jumamosi

eneo la Seloto, mgombea ubunge jimbo la Babati vijijini kwa tiketi ya CCM, Damas

Nakei, alisema fedha hizo zinahitajika ili kuunganisha eneo dogo lililobaki kutoka

mlimani hapo hadi Bashnet mjini.

Alisema fedha hizo zitatoka kwenye Mfuko wa Barabara katika bajeti ya mwaka wa

fedha 2006-2007 na zitamalizia kazi hiyo zitakapotolewa.

Eneo la mlima huo lenye urefu wa kilomita saba, limekuwa korofi kwa muda mrefu na

tayari lilishafanyiwa matengenezo ya awamu ya kwanza yaliyogharimu sh. milioni

120. Lami hiyo ilidumu kwa miaka miwili kutokana na magari ya tani zaidi ya 10

kuitumia.

Agosti mwaka huu ukarabati wa barabara hiyo ulianza tena kwa kiwango cha juu zaidi

ili kukidhi matumizi ya magari ya mizigo na ya abiria na unategemea kukamilika

mwezxi ujao ambapo utagharimu sh. milioni 480.

Nakei alisema matengenezo ya awamu zote mbili zinaishia eneo hilo korofi la mlima

ndio sababu kabla hajanga'atuka kwenye bunge aliiomba serikali kuongeza fungu kwa

ajili ya kuunganisha barabara hiyo hadi Bashneti mjini na kuepuka uharibifu.

Ukarabati wa eneo la mlima huo unafanywa na kampuni mbili moja ikiwa ya ushauri

Crowtech Consaltant na kampuni ya ukandarasi MECCO zote za jijini Dar es salaam na

utawawezesha wanaosafirisha abiria na magari ya mzigo kutumia dakika 30 badala ya

saa tatu na nusu katika eneo hilo lenye urefu wa kilomita saba tu.

Wakazi wa eneo hilo walionyesha kufurahia huduma ya kuunganishiwa nishati ya umeme

unaotarajiwa kuwashwa wakati wowote kuanzia sasa uliogharimu sh.milioni 290

kuvutwa kutoka Dareda hadi kwenye transfoma iliyopo Bashnet umbali wa kilomita 13.

Wakazi hao waliema kuwa watanufaika na huduma hiyo muhimu na wataweza kumudu

gharama ya kuendesha viwanda vyao vidogovidogo ambapo awali walikuwa wanatumia

jenereta na kujikuta wakipata hasara kwenye biashara zao.

 

 

Cheyo ahojiwa na polisi kwa maneno ya uchochezi

MWENYEKITI wa Chama cha United Democratic Party (UDP), John Cheyo, anahojiwa na

polisi mjini hapa akituhumiwa kushawishi maasi dhidi ya serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani

hapa, Abdallah Mssika, alisema mwenyekiti huyo anahojiwa kufuatia kutoa kauli

kadhaa ambazo zinaweza kuchochea ghasia katika jamii. Cheyo anawania ubunge

Bariadi Mashariki.

Alitaja baadhi ya kauli hizo ni ‘polisi kukiona cha moto Desemba 14, wakiyagusa

masanduku ya kura’ na kundi la 'Tela 9', linalodaiwa kuwa limeandaliwa kwa

madhumuni ya kutekeleza azma hiyo ya 'watakiona cha moto'.

Pia, anatakiwa kueleza ni lini alifanya mazungumzo na Inspekta Jenerali wa Polisi

nchini (IGP), Omar Mahita, kama alivyonukuliwa akisema na baadhi ya magazeti hapa

nchini (siyo Uhuru).

Kamanda Mssika alisema polisi inahitaji ufafanuzi na mfano hai ni lini imeshiriki

kuiba kura kwa lengo la kukilinda CCM, na kuvigandamiza vyama vya upinzani.

Kwa mujibu wa Kamanda Mssika, kwenye mahojiano ya awali yaliyofanyika kati yake na

Cheyo, juzi, alizikana kauli hizo akidai kuwa vyombo vya habari vimepotosha kwa

kumnukuu tofauti na kauli zake halisi.

Katika tukio la msingi, Kamanda Mssika alisema Cheyo anadaiwa kutamka hadharani

kauli hizo za uchochezi kwenye mkutano wa kampeni za ubunge, za mgombea wa

Shinyanga Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA, Bob

Makani, Novemba 20, mwaka huu.

Mssika alisema endapo atashindwa kutoa ufafanuzi wa kuridhisha wa kauli hizo zenye

mwelekeo wa kuleta vurugu katika uchaguzi mkuu wa Desemba 14, atafikishwa

mahakamani kukabiliana na sheria za uchochezi.

 

Wazazi wenye watoto walemavu waaswa kutowaficha

Na Pendo Mangala, Dodoma

WAZAZI wenye watoto walemavu wameshauriwa kuacha kuwaficha na kuona aibu

kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kulelea watoto hao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Mussa Nkhangaa,

alipozungumza na wazazi wenye watoto walemavu, walioshiriki katika mashindano ya

michezo mkoani hapa na Marekani. Hafla hiyo ilifanyika ofisi ya mkuu wa mkoa mjini

hapa.

Alisema watoto walemavu wana haki sawa ya kupata huduma muhimu za kijamii kama

walivyo watoto wasio na ulemavu.

Nkhangaa alisema baadhi ya wazazi ambao wana watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiona

aibu na kuwaficha watoto wao, na mbaya zaidi hushindwa kuwapeleka katika vituo

maalum vya kuwalea na kuwakosesha mahitaji muhimu ya kijamii.

Aliwataka wazazi hao kuwapeleka watoto wao katika vituo hivyo ili wapate haki zao

za msingi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kumficha mtoto mwenye ulemavu ni sawa na kumpinga

Mwenyezi Mungu, kwani yeye ndiye anayepanga mipango mbalimbali, hivyo waridhike na

hali ya ulemavu waliyonayo watoto wao.

Alisema baadhi ya watoto wenye ulemavu ambao wamekuwa wakiwapeleka watoto wao

wenye ulemavu katika vituo hivyo hupatiwa huduma muhimu za kijamii ambazo ni

elimu, chakula pamoja na mavazi ambapo baadhi yao ambao hawaongei huweza kuongea

kutokana na malezi wanayoyapata vituoni humo.

Hata hivyo, alisema serikali itakuwa bega kwa bega na watoto wenye ulemavu

mbalimbali ili kuweza kuhakikisha wanapata huduma hizo muhimu za kijamii.

Jumla ya watoto wapatao 10 wenye ulemavu toka katika vituo vya Miyuji Cheshire,

Mlezi pamoja na Chinangali vilivyopo Mkoani Dodoma walipata zawadi za medali za

dhahabu, fedha, shaba pamoja na medali za kuwapa moyo watoto hao.

 

CBE sasa kufungua tawi jipya mkoani Mwanza

Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara nchini (CBE) kinatarajia kufungua tawi jipya mkoani

Mwanza ili kupanua utoaji elimu kwa wanafunzi wanaopenda masomo ya biashara.

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Chuo hicho, Serivanus Hyera alipokuwa akizungumza

na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa

kwa chuo hicho.

Hyera alisema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo ya biashara imekuwa

ikiongezeka kila mwaka hivyo uongozi umeona kuna umuhimu wa kufungua tawi lingine

mjini Mwanza ili kusaidia wanafunzi wa eneo la Kanda ya Ziwa.

Mbali ya hatua hiyo, Hyera alisema katika kuimarisha chuo hicho, mwishoni mwa wiki

hii wanatarajia kupata kompyuta mpya 150.

Kuhusu matatizo yanayowakabili, Hyera alisema ni pamoja na uhaba wa majengo kwa

ajili ya madarasa ya wanafunzi.

Hata hivyo, alisema chuo kina mpango wa kujenga madarasa mengine juu ya majengo

yaliyopo sasa ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na uhaba wa madarasa.

Alisema lingine linalosababisha usumbufu kwa wanafunzi ni ukosefu wa mabweni na

kuwa kutokana na wingi wa madarasa inakuwa vigumu kuwapatia wanafunzi wote sehemu

za kulala.

Madhimisho ya miaka 40 ya CBE yanaendelea leo kwa semina kuhusu mambo mbalimbali

ya biashara katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na zitahitimishwa

Jumamosi ijayo wakati wa mahafali ya 40 ya wanafunzi wa chuo hicho.