TAZARA iendeshwe kibiashara - Mkapa

  • Atoa changamoto hiyo akiwa ziarani Zambia

Na Maura Mwingira, Lusaka, Zambia

TANZANIA na Zambia zimepewa changamoto ya kuhakikisha kuwa zinabuni mipango na mikakati mipya itakayoifanya Reli ya Uhuru (TAZARA), kufanya kazi kwa ufanisi na tija.

Changamoto hiyo ilitolewa juzi usiku na Rais Benjamin Mkapa, alipokuwa akizungumza katika dhifa ya kitaifa aliyokuwa ameandaliwa na mwenyeji wake, Rais Levy Mwanawasa.

Rais Mkapa ambaye alikuwa nchini hapa kwa mwaliko wa Rais Mwanawasa akiwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 41 ya uhuru wa nchi hiyo, na pia kuwaaga wananchi wa Zambia, alisema reli ya Tazara ilijengwa kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kwa msaada mkubwa kutoka serikali ya China kwa malengo makubwa mawili.

Aliyataja malengo hayo kuwa, kwanza ni kusaidia katika shughuli za ukombozi katika nchi za Kusini mwa Afrika, na la pili ni kuzikomboa kiuchumi nchi mbili hizo.

“Lengo la kwanza lilishafanikiwa, lakini hili la pili bado halijafanikiwa vya kutosha. Hata hivyo, ni matumaini yangu kuwa lengo hili la pili nalo litafanikiwa, siyo katika maana ya kujiondoa kutoka ubaguzi wa rangi wa Afrika ya Kusini, bali katika kujenga uwezo wa kikanda katika kuhimili changamoto za utandawazi,” alisema Rais.

Aliongeza kuwa hilo litawezekana tu endapo nchi hizo mbili zitakapokuja na mipango na mikakati mipya ya kuifanya reli hiyo itelekeze lengo hilo.

Katika dhifa hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na muasisi wa Taifa hilo, Rais Mstaafu Dk. Keneth Kaunda, na Mama Anna Mkapa, Rais alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi wa Zambia kwa kutimiza miaka 41 tangu wapate uhuru.

Mimi na wewe wote ni Marais wa awamu ya tatu katika nchi zetu. Tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika uchumi unaoendeshwa na sekta binafsi, misukosuko ya kisiasa haikukosa, na vyombo huru vya habari vimekuwa huru kuelezea misukosuko ya mabadiliko hayo,’’ alisema.

Aliongeza kwamba pamoja na mabadiliko na misukosuko hiyo ya kisiasa, Zambia imeweza kubaki nchi imara na wananchi wake wameungana, na nchi hiyo imebaki kisiwa cha amani.

Akizungumzia uhusiano kati ya Tanzania na Zambia, Mkapa alisema anafurahi anaondoka madarakani huku ushirikiano na uhusiano kati ya nchi hizo na watu wake ukiwa katika misingi imara sana.

Akizungumza katika dhifa hiyo, Rais Mwanawasa alimshukuru Rais Mkapa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 41 ya uhuru wa nchi yake.

Alimpongeza kwa uongozi uliotukuka, ambao umeiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi, na kudumisha demokrasia na utawala wa sheria.

Katika bara la Afrika tutakukumbuka kwa mchango wako mkubwa katika juhudi za kutegeneza amani barani humo, sauti yako katika mikutano mbalimbali ya kimataifa ilikuwa yenye nguvu kubwa katika kupigania haki sawa kwa bara la Afrika, ulitetea vyema hoja za kufutiwa madeni yetu na usawa usio wa haki katika biashara za kimataifa na mambo mengine mengi,’’ alisema.

Ni kutokana na kazi zako hizo za kutukuka, leo hii sisi wananchi wa Zambia tunajisikia fahari kubwa kuwa nawe katika sherehe hizi za kutimiza miaka 41 ya uhuru wetu, aliongeza Rais Mwanawasa.

Akizungumzia TAZARA, kiongozi huyo wa Zambia aliunga mkono hoja ya kutaka kubuniwa mikakati ya kuifanya reli hiyo ijiendeshe kwa tija, akasema kuwa hivi sana mkazo ungetiliwa zaidi katika kuboresha na kuiwezesha reli hiyo badala ya kufikiria kuibinafsisha.

Alisema reli hiyo ambayo ilijengwa kwa msaada wa nchi rafiki ya China, ni zawadi kwa nchi hizo mbili, kwa hiyo itakuwa si vyema, zawadi hiyo ikabinafshwa.

Naye Rais Mstaafu wa Zambia, Dk. Kaunda, alimwambia Rais Mkapa kuwa ingawa anastaafu katika kuiongoza Tanzania, lakini ajue kuwa bado hajastaafu kwa kuwa bado nchi za Afrika na hata Watanzania wenyewe wataendelea kuhitaji huduma zake.

 

 

 

 

 

 

 

CCM yaridhishwa na wagombea wanawake - Mangula

  • Ni kwa jinsi wanavyoungwa mkono na wananchi

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi kimeeleza kuridhishwa kwake na wananchi wanavyowaunga mkono wagombea ubunge wanawake waliosimamishwa na Chama Cha Mapinduzi.

Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, amesema mwenendo huo ni kielelezo kinachoonyesha kukomaa kwa Watanzania katika dhana nzima ya kukua kwa usawa wa kijinsia.

Mangula alisema Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilifanya uamuzi wa makusudi kuwateua wanawake 19 kugombea ubunge majimboni, ili kukidhi matakwa ya Katiba ya nchi na kutekeleza makubaliano ya nchi za SADC.

Katibu Mkuu alisema hayo jana mjini Songea, alipokuwa akizungumza katika mikutano ya kampeni kumnadi mgombea ubunge wa CCM jimbo la Songea mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, asilimia 30 ya wabunge wanatakiwa wawe wanawake. Vile vile makubaliano yaliyofikiwa na Marais wa nchi za SADC, kwenye makubaliano hayo ya miaka ya hivi karibuni ni kwamba asilimia 30 ya wabunge katika mabunge ya nchi zao wanatakiwa wawe wanawake.

Pia, marekebisho ya Katiba ya Tanzania ya hivi karibuni, yameweka utaratibu wa uchaguzi wa viti vya uwiano ambao kiutekelezaji vitakuwa ni vya wanawake na idadi yake ni 75, ambapo wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa watagawana kulingana na asilimia ya ushindi wa vyama vyao katika uchaguzi mkuu.

Mangula alisema Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilichukua uamuzi wa kuwateua wanawake 19 kugombea majimbo, baada ya kubaini kwamba nafasi 75 za viti vya uwiano hazitaliwezesha Taifa kufikia lengo la asilimia 30 ya wabunge wanawake bungeni.

Katibu Mkuu wa CCM alisema kutokana na dhamira hiyo ya CCM, ametoa rai kwa wananchi wa majimbo ambayo CCM imesimamisha wagombea wanawake wawaunge mkono ili washinde.

Alisema kama wanawake wote 19 waliosimamishwa na CCM watashinda, itakuwa imesaidia sana kukaribia lengo la asilimia 30 baada ya kuunganisha na zile nafasi za viti vya uwiano, na hivyo kutekeleza matakwa ya Katiba na kuijengea heshima Tanzania mbele ya macho ya kimataifa kwa kutekeleza makubaliano ya SADC.

Mmoja kati ya wagombea ubunge wanawake kupitia tiketi ya CCM ni Jenista Muhagama wa jimbo la Peramiho, Songea Vijijini. Tathmini zinaonyesha ana asilimia kubwa ya ushindi.

Katibu Mkuu wa CCM yuko mkoani Ruvuma kukagua maendeleo ya kampeni za CCM katika uchaguzi mkuu utakofanyika Jumapili wiki hii.

 

Katibu Mwenezi wa CCM Iringa afariki

  • Alitarajiwa kuzikwa jana Njombe

Na Bahati Alex, Iringa

Chama cha Mapinduzi mkoani hapa kimepata msiba mkubwa kufuatia Mwenyekiti wa Wazazi na Katibu Mwenezi wa Chama, Lazaro Mamba, kufariki dunia.

Akizungumza hapa jana, Katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoani hapa, Lotari Mbawala, alisema Mwenyekiti huyo alianza kuumwa wakati akitokea Mbeya kumuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Mbawala alisema baada ya kuona hali yake siyo nzuri, aliamua kutibiwa katika zahanati ya Mbeya na baadaye kurudi nyumbani kwake.

Aliongeza kuwa mara baada ya kufika nyumbani kwake Ijumaa iliyopita, Mwenyekiti huyo alifariki dunia na mwili wake kuhifadhiwa katika hospitali ya mkoa hapa.

Alisema marehemu alitarajiwa kuzikwa jana katika makaburi ya Yakobi wilayani Njombe, ambapo CCM ingewakilishwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Tasili Mgoda.

Katika uhai wake, marehemu alikuwa mwalimu wa shule za msingi wilayani Njombe na baadaye kufundisha chuo cha Ihemi wilaya ya Iringa Vijijini.

Mwaka 2003 marehemu Mamba alikuwa mwenyekiti wa wazazi mkoani hapa. Mbali ya kuwa mwenyekiti wa wazazi, pia alikuwa Katibu Tarafa wa wilaya ya Kilolo.

Kifo cha mwenyekiti huyo kimeacha pengo kubwa kwa Chama cha Mapinduzi na jamii nzima, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili ijayo.

 

Ishara ziko wazi CCM kuibuka na ushindi wa kishindo, asema Dk. Sheni

  • Mjumbe wa baraza kuu CUF Zanzibar arejea CCM

Na Peter Orwa, Zanzibar

MGOMBEA mwenza wa kiti cha urais kupitia tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohammed Sheni, amewahutubia wakazi wa mjini hapa na kuwaambia ishara ziko wazi kwa CCM kuibuka na ushindi wa kishindo.

Wakati Dk. Sheni ambaye yuko katika mzunguko wa ziara za kampeni anatangaza ubashiri huo, chama cha CUF kilipigwa kumbo kwa kiongozi wake, Abeid Issa Juma, ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho kutangaza kujiunga na CCM.

Hali hiyo ilizua mlipuko wa hoihoi na nderemo kutoka kwa wana-CCM, ambapo walimzingira na kumvalisha fulani mbili za chama na kofia kichwani, wakati alipopita mbele kwenda kusema machache.

Akihutubia mkutano huo, Dk. Sheni alisema vyama vya upinzani vina udhaifu mkubwa wa ubinafsi, kutokuwa na sera zinazotekelezeka, hali inayofanya visikubalike mbele ya wananchi.

“Hawawezi na wala hawana ubavu, kwa sababu CCM si chama cha mtu mmoja,” aliwaambia wakazi hao wa mkoa wa Mjini Magharibi waliojiunga na wenzao wa mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja.

Alisema viongozi wa Chama cha Mapinduzi wanatokana na wananchi na wana maadili ya kuheshimu watu, ndio maana wanaheshimiwa hata kupewa ridhaa ya kuongoza nchi.

Dk. Sheni alisema CCM inayaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na ndio maana inadumisha mazuri yote kwa kuwatendea mema wananchi kupitia pande mbili za Muungano.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ramadhan Ferouz, alisema CUF imekuwa ikiwarubuni wananchi wa wilaya ya Magharibi kuwa serikali iliyopo ya CCM haiwatendei haki kwa kutotengeneza barabara ya Mazizini hadi Fumba.

Alisema tayari serikali imeshachukua hatua ambapo imekopa Benki ya Maendeleo ya Afrika, na ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuanza Desemba, mwaka huu, kwa kiwango cha lami.

Abeid akielezea kisa cha kuhama chama cha CUF, alisema amechoshwa na hadaa za ruzuku kutumiwa vibaya ambapo zilikuwa hazifiki wilayani, na viongozi wa huko kulazimishwa kuandika ripoti kama wakubwa wa chama wanavyotaka, kwamba pesa zimewafikia.

Pia alilalamika kuwa CUF kimeelemewa na maamuzi na nafasi nyeti kuelekezwa kwa wanachama wanaotoka visiwani Pemba.

Mimi nimefunga Ramadhani na nisingependa kuharibu saumu yangu,” alisema Abeid ambaye kabla ya kuingia CUF miaka 13 iliyopita, alikuwa Katibu wa CCM wilaya ya Magharibi, na alimtaja Jakaya Kikwete kuwa ndiye mwalimu wake wa siasa mwaka 1978.

Alipokuwa CUF, alikuwa kiongozi wa ngazi ya wilaya na mpiga debe maarufu wa chama hicho.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi, Yusuff Mohammed, alisema Abeid ana wenzake aliowashawishi kujiunga na CCM, ambao atawatangaza siku chache zijazo. Yeye alijiunga na CCM kuanzia Oktoba 20.

Mohammed aliongeza kuwa kuna vikaratasi vya ushawishi vinavyosambazwa mkoani mwake ili wana-CCM wakikatae chama chao, na aliwataka waachane navyo kwa kuipigia kura CCM kwa amani na utulivu.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, wajumbe wa Kamati Kuu, Waziri Mkuu mstaafu Dk. Mohammed Gharib Bilal, na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho.

 

Wananchi waonywa kutoenda na silaha vituo vya kupigakura

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imewaonya wananchi, kutoenda kwenye vituo vya kupiga kura wakiwa wamebeba silaha, kwani dola imewahakikishia usalama wao, imeelezwa.

Taarifa ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Omar Ramadhani Mapuri iliyotolewa jana, imewataka viongozi wa kisiasa kujiepusha na vitendo vyenye kuchochea wafuasi wao kufanya vurugu, badala yake imewasihi wawe watulivu siku ya uchaguzi.

Alisema Polisi itakuwa inafuatilia kwa karibu mwenendo wa amani na usalama katika uchaguzi na amewaonya wote watakaothubutu kufanya vurugu, kwamba watachukuliwa hatua kali.

“Jeshi la Wananchi litakuwa katika hali ya kuwa tayari wakati wote na litaweza kuingilia kati kusaidia linatakapohitajika,” alisema Waziri Mapuri katika taarifa yake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wadau wote wa uchaguzi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Polisi na vyombo vingine vya dola katika kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa amani na utulivu.

 

 

 

Tanzania kukumbwa na El-Nino tena?

Na Furaha Omary

TANZANIA huenda ikakumbwa na majanga mbalimbali yakiwemo ya mvua za El-Nino kuanzia mwaka 2007.

Hayo yalisemwa jana na Profesa Ernest Njau wa Idara ya Fizikia ya Chuo Kikuu cha ar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) alipokuwa akizungumzia majanga matatu yanayoweza kuikumba Tanzana kuanzia kipindi cha miaka miwili ijayo.

Profesa Njau ambaye ni mtaalamu katika masuala ya elektroniki na hali ya hewa aliyataja majanga hayo mbali na El-Nino kuwa ni ukame na machafuko ya hali ya hewa.

Alisema majanga hayo yameonekana kutokana na utabiri wa mabadiliko ya hali ya hewa ambao umeshachapishwa baada ya kuhakikiwa na vyombo vya kisayansi vya kimataifa.

Mtaalamu huyo alisema katika taarifa hizo, Tanzania itakumbwa na ukame mkali kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2023. Alisema ukame huo utakuwa mkali kama ulivyotokea mwaka 1973 hadi 1975

Vile vile alisema El- Nino kali itatokea mwaka mwaka 2007 hadi 2009 na kusisitiza kuwa kali zaidi itakuwa katika mwaka wa 2007/2008. El Nino nyingine itakuwa kati ya mwaka 2010 na 2013.

Profesa Njau alisema katika matukio mengine hali joto itapungua kwa wastani katika miaka ya mwanzoni wa karne hii kabla ya kuanza kuongezeka tena.

Kutokana na wasiwasi wa kutokea kwa majanga hayo, ameishauri serikali kufikiria njia za kukabiliana na majanga hayo ili kuepuka athari zinazoweza kuikumba nchi.

 

Zambia yaongezewa muda wa kuhifadhi mafuta Dar

Ni hadi siku 30 bila kutozwa ushuru

Na Maura Mwingira, Lusaka, Zambia

SERIKALI imeongeza muda wa Zambia kuhifadhi mafuta yake katika bandari ya Dar es Salaam hadi siku 30 bila kutozwa ushuru.

Uamuzi huo wa serikali umefuatia ombi lililotolewa na Serikali ya Zambia la kutaka iongezewe muda wa kuhifadhi mafuta ghafi katika bandari ya Dar es Salaam kutoka siku 15 za sasa hadi 30.

Hayo yalisemwa juzi Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Mark Mwandyosa, wakati wa mazungumzo rasmi yaliyofanyika kati ya serikali hizo mbili na ambayo kwa upande wa Zambia yaliongozwa na Rais Levy Mwanawasa na kwa Tanzania yakaongozwa na Rais Benjamin Mkapa. Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu ya Zambia.

Waziri Mwandosya alisema kuwa serikali imefikia uamuzi huo ili kuiwezesha Zambia kukabiliana na upungufu mkubwa wa nishati hiyo muhimu katika uchumi.

Alisema serikali iliweka siku 15 za kuhifadhi mafuta ghafi kabla ya kuanza kutoza ushuru ili kukabiliana na vitendo vya ukwepaji kodi uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wafanya biashara ambao si waaminifu na ambao walikuwa wakisema mafuta hayo yalikuwa yakisafirishwa nje, ili hali yalikuwa yakiishia mitaani.

Zambia ambayo hivi sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta, baada ya mitambo yake ya kusafishia mafuta ghafi iliyoko Ndola kuharibika, ilikuwa imeiomba Serikali ya Tanzania kuiongezea muda wa kuhifadhi mafuta yake kutoka siku 15 za sasa hadi 30 ili iweze kuagiza mafuta mengi katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo linalotishia kusambaratisha uchumi wa nchi hiyo.

Kwa taratibu za bandari, mafuta yanayosafrishwa nje ya Tanzania kupitia bandari hiyo, huwa hayatozwi kodi katika kipindi cha siku 15 na kodi huanza kutozwa baada ya siku hizo ikiwa mafuta hayo yatakuwa hayajaondolewa katika kipindi hicho.

Kwa hali hiyo, kutokana na matatizo ya usafirishaji wa nishati hiyo, na ili kupunguza gharama, Serikali ya Zambia iliomba ifikiriwe kuongezewa muda wa kuhifadhi mafuta hayo kwa siku 30 kabla ya kuanza kutozwa kodi.

Pamoja na Zambia kuchukua hatua za kuagiza malighafi hiyo kwa wingi kupitia bandari ya Dar es Salaam pia imetoa kibali kwa wafanya biashara binafsi kuagiza nishati hiyo.

Uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo, pia unaweza kuathiri uingizaji wa nafaka nchi humo ili kukabiliana na tatizo la upungufu mkubwa wa chakula unaoikabili nchi hiyo kwa sasa.

Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, Tanzania pia imekubali kushughulikia tatizo la upitishaji wa bidhaa katika maeneo ya mpakani ya Tunduma na Nakonde ili kurahisisha na kuharakisha huduma katika eneo hilo.

 

 

TISCAN kizimbani kwa kukiuka mkataba na kashfa kwa mteja

Yadaiwa fidia ya mamilioni ya shilingi

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya kuondoa mizigo bandarini ya Quality Business Consultancy (QBC) Tanzania Ltd, imeishitaki kampuni ya ukaguzi wa mizigo inayoingia nchini, TISCAN Limited kwa kukiuka mkataba na kuisababishia hasara ya mamilioni ya shilingi.

Pamoja na kutaka kulipwa mamilioni ya shilingi, kampuni ya QBC ambayo hufanya kazi ya kuondoa mizigo bandarini, imetaka kulipwa fidia kwa kukashifiwa kuwa ilighushi hati ya kutolea mizigo, jambo ambalo ilidai kuwa si kweli.

Katika kesi hiyo iliyotajwa jana kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, kitengo cha Biashara, QBC kupitia wakili wake Serapius Mdamu, inaiomba mahakama kuimamuru TISCAN Limited kulipa sh. milioni 36 (dola za Marekani 30,333.40).

Mdamu alidai katika hati iliyowasilishwa mbele ya Jaji Natalia Kimaro kuwa TISCAN Ltd ilikatisha mkataba wa kuondoa mzigo bandarini uliotiwa saini na QBC na Tongfan Dragon Limited kwa ajili ya kutoa kontena la shehena lenye futi 40 kutoka bandari ya Dar es Salaam.

Wakili Mdamu katika hati hiyo alidai kuwa QBC ilipewa kazi hiyo Machi, mwaka huu, lakini TISCAN kwa kushirikiana na Tongfan zilishindwa kuheshimu mkataba huo na hivyo kuisababishia hasara.

Alidai kuwa mteja wake alipokwa kufanya kazi hiyo bila sababu za msingi na matokeo yake kudaiwa ameghushi hati ya kutolea mzigo husika. Hati hiyo inadaiwa kutumiwa na kampuni ya Global Logistics Limited.

Kutokana na kukosa kazi na kukashifiwa, Mdamu ameiomba mahakama kuziamuru TISCAN na Tongfan kumlipa mteja wake fidia ya zaidi ya sh. milioni 36.

Pamoja na fidia hiyo, QBC kupitia kwa wakili wake inaomba kulipwa na wadaiwa riba ya asilimia 30 ya gharama hizo kwa mwezi kuanzia Machi, mwaka huu ambazo ni sawa na zaidi ya sh. milioni 10.8 kila mwezi.

Vile vile, Mdamu ameiomba mahakama kuamuru mteja wake kulipwa riba ya asilimia 12 ya hasara aliyoipata mteja wake ambayo ni sawa na sh. milioni nne kila mwezi.

Mdamu pia ameiomba mahakama kuiamuru TISCAN kulipa fidia mteja wake kutokana na maneno ya kashfa yaliyoko katika maandishi, dhidi yake kuwa ameghushi hati ya kutolea mizigo.

"TISCAN imemkashifu mteja wangu na kusababisha akose hadhi, heshima na uaminifu mbele ya jamii kwa kuzingatia kuwa mmoja wa wakurugenzi wake ni Makamu wa Rais wa TAFFA (Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania) yenye zaidi ya kampuni wanachama 400.

Si hivyo tu, mteja wangu pia na Mjumbe wa Bodi ya Walaji ya SUMATRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Uchukuzi Majini na Nchi Kavu) chombo ambacho kimeundwa kwa sheria ya Bunge hivyo kutambuliwa kisheria," alidai katika hati hiyo.

Kwa kukashifiwa huko, Mdamu alidai mteja wake amepata pigo kubwa kibiashara kutokana na kampuni ya kimataifa ya ABB Limited ambayo imekuwa ikiipa kandarasi ya kufanya shughuli kwa niaba yake hapa nchini kukatisha mkataba baada ya kupokea taarifa hizo.

TISCAN inatetewa na kampuni ya mawakili ya M.A Ismail Advocates ya Dar es Salaam. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 17, mwaka huu itakapotajwa.

 

 

 

 

 

 

Kikwete apongeza UN kusaidia kupambana na umaskini

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Jakaya Kikwete ameushuruku Umoja wa Mataifa (UN) kwa kuweka mkakati wa kupambana na umaskini katika nchi zenye matatizo ya maendeleo ili kufikia malengo ya milenia ya maendeleo ifikapo mwaka 2015.

Kikwete alitoa shukrani hizo jana katika hotuba yake aliyoitoa siku ya kuadhimisha miaka 60 ya UN zilizofanyika viwanja vya Karimjee na kuhudhuriwa na maofisa mbalimbali wa mashirika ya kimataifa, mabalozi na viongozi wa serikali.

UN ilianza mwaka 1945 ikiwa na wanachama 51, lakini sasa ina wanachama 191.

Kabla ya hotuba yake, Kikwete alikagua gwaride rasmi la askari wa Jeshi la Wananchi nchini na kushuhudia upandishwaji wa bendera ya UN.

Alisema kitendo cha nchi tajiri duniani kufanya mkutano maalum kujadili mkakati wa kusaidia maendeleo ya nchi maskini duniani ni moja ya dhamira za UN, kwani kifungu cha 55 cha makubaliano ya Umoja huo kinasisitiza kuona kila binadamu anaishi maisha bora.

Kikwete ambaye pia ni mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM, alisema nchi zinazoendelea zinakabiliwa na kazi ya kuweka mazingira bora kuwavutia wawekezaji na kusimamia ukuaji wa uchumi, kupambana na rushwa na kutoa haki kwa watu wote.

"Ninafurahi kuona Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya hayo na kufanikiwa vizuri kutekeleza masuala ya elimu ya msingi kwa wote, kudhibiti vifo vya watoto wachanga na kuimarisha uwiano wa jinsia," alisema.

Alisema Tanzania imedhamiria kwa dhati kuongeza kasi ya maendeleo na kwamba kitendo cha nchi tajiri kuzifutia madeni ya dola bilioni 40 (sawa na zaidi ya bilioni 41) nchi maskini ikiwemo Tanzania kitaongeza kasi ya kufanikisha malengo ya milenia ya maendeleo ifikapo 2015.

Hata hivyo , Kikwete alisema pamoja na kufutwa kwa deni hilo nchi maskini bado zinakumbwa na deni lingine la sh. trilioni 18 ambalo ni kubwa mno.

Alisema mazungumzo yaliyofanyika Doha, Qatar mwaka 2001 yalianza vizuri kujadili mfumo wa biashara, lakini yanahitaji kuendelezwa wakati wa mkutano wa Shirika la Biashara Duniani utakaofanyika Desemba mwaka huu Hong Kong.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambaye ni mratibu wa masuala ya UN nchini John Hendra alisema umoja imedhamiria kwamba kipindi kijacho kinakuwa cha kuleta mabadiliko ya maendeleo duniani.

Hendra alisema UN itashirikiana na nchi mbalimbali duniani kupambana na umaskini na magonjwa yakiwemo ya Ukimwi ili kufikia malengo ya milenia ya maendeleo ifikapo 2015.

Kuhusu sulala la misaada, biashara na kufutwa kwa madeni ya nchi maskini, alisema anayo matumaini kwamba mkutano utakaofanyika baadaye kuhusu masuala ya biashara utakuwa na mafanikio .

Hendra alimhakikishia Waziri Kikwete kwamba UN itashirikiana kwa karibu na Tanzania kutekeleza mpango wake wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini (MKUKUTA) ili kufanikisha malengo ya maendeleo.

Alisema pia kwamba UN imeridhia kwa dhati mkakati wa kupambana na umaskini Zanzibar (ZPRP) .

Jana hiyo, Waziri kikwete alikagua mabanda ya maonyesho yaliyoandaliwa na mashirika mbalimbali yanayopata misaada kutoka UN kupitia mashirika yake.

 

Sheikh Kasenga wa Mbeya afariki dunia

Na Furaha Omary

SHEIKH wa Mkoa wa Mbeya Adamu Kasenga amefariki dunia jana mjini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) anayeshughulikia masuala ya dini Mussa Hemed, alisema Sheikh Kasenga alifariki jana alfajiri.

Kasenga ambaye alikuwa anaumwa, anatarajiwa kuzikwa leo mkoani Mbeya.

Taarifa ilifafanua kuwa Kasenga alijiunga na BAKWATA katika miaka ya 60 na alilitumikia Baraza hilo katika ngazi mbalimbali.

 

Citibank yafurahia mazingira ya biashara

Yatimiza miaka 10 nchini

Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Citibank umesema mazingira ya biashara yalivyoboreshwa hapa nchini yanaonyesha dalili nzuri za kukua kwa uchumi.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo hapa nchini, Mayank Malik alipozungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya miaka 10 ya benki hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.

"Biashara hapa nchini zinakuwa kwa kasi, hii inachangiwa na mazingira mazuri yaliyowekwa ya kufanya biashara," alisema Malik.

Alisema katika kipindi cha miaka 10 tangu benki hiyo ianze kutoa huduma zake hapa nchini, kumekuwa na mafanikio mengi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi wazalendo.

Alifafanua kuwa wakati benki hiyo inaanza kutoa huduma, asilimia 90 ya wafanyakazi wake walikuwa ni kutoka nje lakini sasa asilimia 75 ya wafanyakazi katika benki hiyo ni kutoka hapa nchini.

Maliki alisema maadhimisho ya miaka 10 ya kutoa huduma nchini yatafanyika keshokutwa ambapo wadau na wateja wa benki hiyo watashirikishwa.

Alisema, Citibank itazidi kutoa huduma katiak maeneo mbalimbali nchini kwa njia tofauti ikiwemo ya kushirikiana na taasisi nyingine za fedha katika maeneo ambako hawana matawi au ofisi.

"Hata hivyo, tunaweza kuhudumia wateja wengi zaidi bila hata kufungua matawi kwa kuwa huduma yetu pia inapatikana kwenye mtandao wa intaneti ambao kwa sasa unazidi kuenea sehemu mbalimbali nchini," alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Alisema mbali ya kutoa huduma za kibenki, pia wanatoa misaada mbalimbali ya kijamii.

Citibank ni taasisi ya fedha ya kimataifa yenye kutoa huduma katika nchi mbalimbali zaidi ya 100 duniani kote zikiwemo 17 za Afrika.