UHURU 01.11.2005

 

Mkapa awataka Watanzania wasiogope kukopa

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa amewataka Watanzania wasiogope kukopa fedha kwenye mabenki mbalimbali na mifuko ya fedha iliyoidhinishwa kukopesha ili waweze kubadili maisha yao.

Mkapa amesema umaskini wa Watanzania utapungua ikiwa watakopa pesa za mitaji na kwamba ndio maana serikali imeamua kuanzisha mpango wa kurasimisha mali zao ili wapate dhamana wanapotaka kukopa fedha.

Alisema mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge nchini utawawezesha wahusika kupata hati watakayoitumia kama dhamana wanapohitaji mikopo kwa vyombo mbalimbali vinavyotoa mikopo.

Mkapa alitoa kauli hiyo jana usiku katika hotuba yake ukiwa ni utaratibu aliojiwekea kulihutubia taifa kupitia vyombo vya habari kila mwisho wa mwezi.

Rais Mkapa aliwataka viongozi au wanasiasa uchwara kuacha kuwatisha wananchi juu ya suala la mikopo na kwamba kinachotakiwa ni kuwasaidia kuwaambia ukweli juu ya umuhimu wa mikopo kutumika kwa malengo ya maendeleo.

Alisema Watanzania hawana budi kujenga tabia ya kukopa na kulipa madeni yote ili vyombo vya fedha na mabenki yawe na imani na wananchi.

Katika hotuba yake, Rais Mkapa pia amewataka Watanzania kushirikiana vizuri na serikali ijayo katika kuyatunza na kuyaendeleza mafaniko yote yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake hadi sasa.

“Wapo wanaopinga mpango wa kurasimisha rasilimali za wananchi, ati wananchi wakikopa kwa kuweka rasilimali hizo dhamana watazipoteza pale watakaposhindwa kulipa," alisema na kuongeza kwamba wananchi upotoshaji huo kwa vile kimsingi mikopo ndiyo chanzo cha mitaji duniani kote.

Alisema hapa Tanzania wapo wananchi wengi waliotajirika baada ya kukopa kutoka kwenye mifuko au benki zinazokopeshwa na kwamba Watanzania wasikubali kudanganywa na wapotoshaji.

"Msidanganywe wananchi, hata wawekezaji wakubwa, wakiwemo wanaokuja kuchimba madini hapa kwetu, wote wanakopa, tusiogope kukopa, tusipokopa hatuwezi kupanuka kiuwekezaji na kuiuzalishaji," alisema katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja na Radio Tanzania na Televisheni ya Taifa.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba kinachotakiwa ni kwa Watanzania kukopa fedha kwa busara na baada ya kufanya upembuzi wa kutosha na kuridhika na faida ya mradi unaohusika na kwamba wakiridhika na faida itakayopatikana wasisitie kukopa.

Alitoa mfano wa mikopo mizuri aliyoiona Afrika Kusini ambako alisema wakulima wanakopeshwa na vyombo vinavyokopesha mahitaji muhimu yanayohitajika katika kuzalisha.

“Kwanza mkulima anatafuta soko la mazao atakayolima. Akishaingia mkataba na wanunuzi wa mazao yake, anautumia mkataba ule kukopa mtaji, lakini kama mahitaji yake ni trekta basi atakopa trekta na kama mbegu basi atapewa mbegu,” alisema.

Alisema kipindi kijacho cha uongozi wa awamu ya nne ni cha kufurukuta kwa nguvu zaidi katika kupambana na umaskini na kwamba lazima kila Mtanzania ajiweke tayari kutekeleza wajibu wake.

"Narudia, uchumi wa soko una kanuni zake. Tusipozitambua na kuzifuata tutabaki kulalamika tukiona wivu wa Watanzania wenzetu wachache na wageni wakitumia fursa na kanuni za kukopa na zinginezo kujitajirisha,” alisema.

Alisema serikali tayari imeanzisha mpango wa kuharakisha maendeleo ya Tanzania kwa kuzingatia uzoefu wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia na kwamba maandalizi ya sera tayati na utekelezaji umeanza jambo ambalo Watanzania wote wanatakiwa kulitambua.

Mpango huo unalenga kukuza uchumi hadi asilimia kati ya 8-10, kukua kwa pato la Mtanzania kutoka dola 286 za Marekani hadi dola 1,000 sawa na kutoka sh. 286,000 hadi sh. 1,00,000 kwa mwezi, na kwamba mchango wa sekta ya viwanda inatarajiwa kukua hadi asilimia 15 kutoka asilimia saba ya sasa.

Ili kufikia malengo hayo alisema lazima Watanzania wajenge mazingira ya kuvutia kwa wingi wawekezaji, wazalishe bidhaa ambazo zinahitajika katika soko, kuweka utaratibu mzuri wa kutatua matatizo yanayojitokeza na kuboresha masuala ya kisheria, taratibu za nguvukazi na utawala.

“Kwa wale wasio tayari kujituma na wale wanaoingojea serikali iwafanyie kila kitu, hao wataachwa nyuma jambo ambalo siyo lengo la serikali,” alisema na kuongeza kwamba kinachotakiwa ni kila mtu na ajitume na kujibidisha zaidi.

 

Wakati kura zikiendelea kuhesabiwa…

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi kinaelekea kupata ushindi wa kishindo kwa kunyakua majimbo mengi katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika juzi.

Ingawa matokeo rasmi ya majimbo yalikuwa hayajakamilika kutolewa hadi jana jioni, habari zisizo rasmi zilisema kuwa Chama cha Mapinduzi kitazoa majimbo 31, kati ya 50 ya uchaguzi Unguja na Pemba.

Hadi jana jioni mawaziri watatu walitetea viti vyao huku watoto wa waasisi wawili wa Mapinduzi wakishinda kwa kishindo katika majimbo yao.

Hali ya uchaguzi huo inaonyesha kuwa CCM imeshinda karibu viti vyote Unguja, ambapo chama cha CUF kimeshinda viti vyote 18 Pemba na kimoja Unguja, ambacho ni cha Mji Mkongwe. Unguja ina majimbo 32 na Pemba 18.

Chama cha Mapinduzi kwa mujibu wa habari zisizo rasmi, Pemba kimeambulia ushindi wa diwani mmoja tu, ambaye inaaminika ni wa wadi ya Mkoani, katika mkoa wa Kusini.

Kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliyoshirikisha vyama vingi wa 1995 na 2000, chama Tawala cha CCM kinaendelea kushikilia ngome yake katika kisiwa cha Unguja, wakati CUF ngome yake inaendelea kuwa kisiwani Pemba.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa jana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), mtoto wa mwanasiasa mashuhuri wa Zanzibar, Hayati Thabit Kombo, Mahammoud Thabit Kombo, ameshinda kwa kishindo ujumbe wa Baraza la Wawakilishi katika jimbo la Mpendae.

Mahamoud amepata kura 6,183, akifuatiwa kwa mbali na Juma Said Sanani wa CUF, aliyepata kura 2,844, Suleiman Mohammed Abdalla wa NRA kura 45, Ahmed Abdulatif Ahmed wa Chadema kura 43, Mahammoud Ali Mohammed wa Demokrasia Makini kura 28 na Mohammed Ahmad Khamis wa SAU kura 18.

Mansoor Yusuff Himid, ambaye pia ni mtoto wa mwanasiasa mashuhuri wa hapa, Hayati Yusuff Himid, amenyakua uwakilishi wa jimbo jipya la Kiembesamaki kwa kupata kura 4,718, akifuatiwa na Manzi Ibrahim Juma wa CUF, kura 1,198 na Khalid Omar Mahawi wa UPDP kura 35.

Waziri wa Elimu na Utamaduni katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayomaliza muda wake, Haroun Ali Suleiman, ametetea kiti chake katika jimbo la Makunduchi kwa kupata kura 8,876. Amewashinda vibaya Jihad Hassan Issa wa CUF aliyepata kura 979 na Madai Ali Madai wa Jahazi Asilia, aliyeambulia kura 115.

Mawaziri wengine wawili, Suleiman Othman Nyanga na Burhani Saadat Haji, pia wameshinda katika majimbo ya Jang’ombe na Kikwajuni, yote ya mjini hapa.

Nyanga ambaye ameingia katika kinyang’anyiro hicho kwa mara ya kwanza, ameshinda Jang’ombe kwa kura 8,780, akifuatiwa na mgombea wa CUF, Haji Ameir Muhunzi aliyepata kura 2,644, Abdalla Shamte Mketo wa NRA kura 39 na Njuma Kombo Mohammed wa NLD kura 92. Nyanga alikuwa mwakilishi wa kuteuliwa.

Burhani ametetea kiti chake cha Kikwajuni kwa kura 7,209 na kumwacha mpinzani wake wa pekee Hassan Hamad Sued aliyepata kura 3,315.

Matokeo ya majimbo mengine yaliyotangazwa matokeo yake jana majina ya vyama na kura yakiwa kwenye mabano ni:

MUYUNI: Ramadhan Nyonje (CCM-kura 7,244), Suha Suleiman Hassan (CUF-kura 1,244), Haji Ibrahim haji (Jahazi Asilia-kura 166) na Haji Hassan Kidogo (TLP-kura 64).

AMANI: Ali Denge Makame (CCM-kura 5,615), Dk. Muchi Juma Ameir (CUF-kura 1,645), Mganga Mmanga (Jahazi Asilia-32), Maulid Haji Ali (NCCR-kura 39), Mohammed Ali Chiwanga (TADEA-18) na Farashuu Wazir Abuobakar (UPDP-kura 37).

RAHALEO: Kamal Basha Pandu (CCM-kura 5,637), Iddi Khalifa Omar (CUF-kura 2,753) na Haji Ukindu Suleiman (SAU-kura 162). MKWAJUNI: Ali Haji Ali (CCM-Kura 3,586), Duni Machano Haji (CUF-kura 1,668) na Tahir Ali Mcha (Jahazi Asilia-kura 2,555).

BUMBWINI: Said Khelef Ali (CCM-kura 5,852), Zahran Juma Mshamba (CUF-kura 3,396), Abdulrahman Seif Nawawi (Jahazi Asilia-kura 95), Mzee Ali Mzee (TLP-kura 37), Ali Abdulrahman Badru (UPDP-73).

MATEMWE: Ame Mati Wadi (CCM-kura 4,161), Shauri Makame Mkadam (CUF_kura 2,388), na Kundi Haji Mkombe (Jahazi Asilia-kura 325).

CHAANI: Mzee Ali Ussi (CCM-kura 7,170), Khamis Amour Ali (CUF-kura 1,232), Khamis Juma Denge (Jahazi Asilia-kura 319), Bambi Ali Nassor (CHADEMA-kura 177), na Fatma Hamad Pwani (NLD-kura 25). NUNGWI: Ame Ussi Juma (CCM-kura 5,385), Yusuff Haji Khamis (CUF-kura 3,820), Simai Khamis Wadi (Jahazi Asilia-kura 179) na Ali Khamis Ali (UPDP-kura 5).

TUMBATU: Haji Omar Kheir (CCM-kura 5,078), Makame Hamad Makame (CUF-kura 4,762) na Juma Haji Rajab (Jahazi Asilia-kura 114).

 

 

WFP yamteua Mengi kuongoza kupiga vita njaa

Na Peter Orwa

MWENYEKITI Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, ameteuliwa kuongoza mkakati wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) kupiga vita njaa ya watoto nchini.

Taarifa ya WFP, ilisema kuwa mkakati huo utafanyika kupitia mikutano ya kibiashara na matukio ya kijamii ikiwemo matembezi ya hiari

“Tuna furaha kubwa kuwa Reginald Mengi amekubali kupokea hadhi ya kuwa ‘Mzee wa Kupiga vita njaa’ hapa Tanzania, ili kufikia Malengo ya Milenia ya kupunguza njaa duniani kwa nusu ya kiwango cha sasa ifikapo mwaka 2015,” alisema, Patrick Buckley, Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini.

Buckley alisema kuwa, katika kuleta mafanikio duniani kote, kuna umuhimu mkubwa wa sekta binafsi kushirikishwa katika jukumu hilo.

Miongoni mwa majukumu ambayo Mengi anatarajia kuyatumikia katika jukumu lake jipya ni pamoja na kukusanya michango ya kutunisha mfuko wa kampeni hiyo ya kuondoa njaa kwa watoto.

Njia mojawapi ya kukusanya michango hiyo ni kupitia matembezi ya mwaka ya WFP ambayo hufanyika katika kila nchi.

Taarifa hiyo ilitaja majukumu mapya ya kiongozi huyo wa kupiga vita njaa nchini kupitia mtandao wa WFP, kuwa atawajibika na kuwahamasisha wafanyabiashara kukusanya michango ya kuhitimisha jukumu hilo.

Mwaka huu nchini, WFP kwa kushirikiana na asasi ya TNT, iliandaa matembezi manane tofauti iliyowajumuisha jumla ya washiriki 1200, ilikusanya sh. milioni 24. Matembezi ya mwakani yanatarajiwa kufanyika Mei 21.

Fedha zilizokusanywa mwaka huu, zitatumika katika mambo mbalimbali, ikiwemo kununua chakula cha watoto hao, kwani kwa mujibu wa WFP, katika baadhi ya familia shule zinaonekana kuwa jambo la anasa na si watoto wote kwenye familia wanaopelekwa shule.

Taarifa hya WFP ilisema kuwa vijana wanashindwa kuvumilia njaa wawapo shuleni na suala la kuwapa mlo wa mchana lina maana kubwa kuboresha mahudhurio.

Kwa Upande wake, Mengi alisema kuna haja ya kupambana na njaa kwa watoto, kupitia mipango ya lishe bora ya watoto na wajawazito, pamoja na lishe ya mashuleni kwa kuwathimini watoto hao kama rasilimali bora ya baadaye kwa taifa.

 

 

Sumaye ahudhuria kikao cha wakuu wan chi AU

Na Mwandishi Maalum, Addis Ababa

WAZIRI Mkuu . Frederick Sumaye jana alihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika utakozungumzia mageuzi ndani ya Umoja wa Mataifa.

Sumaye alimwakilisha Rais Benjamin Mkapa katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika ulikuwa na ajenda moja ya kupokea taarifa ya Kamati maalum ya Umoja huo yenye mapendekezo ya msimamo wa Afrika kuhusu mageuzi ndani ya Umoja wa Mataifa, hususan Baraza la Usalama la Umoja huo.

Awali, Kamati hiyo ilikutana Februari, mwaka huu, nchini Swaziland na kupendekeza kuwa nchi za Afrika zipewe viti viwili vya kudumu katika Baraza la usalama vyenye hadhi ya “Veto” kura za turufu. Kamati imependekeza Afrika ipewe viti vingine vitano visivyokuwa vya kudumu katika baraza hilo.

Utaratibu wa kupata uwakilishi wa nchi za Afrika katika baraza hilo utashughulikiwa na Umoja wa Afrika. Nchi zinazowania nafasi hizo hadi sasa ni Nigeria, Afrika Kusini, Misri, Angola, Kenya, Libya na Senegal.

Waziri Mkuu na ujumbe wake watarejea nyumbani leo.

 

 

Mikoa saba kupatiwa magari ya Zimamoto

Na Esther Katua

MIKOA saba nchini kupatiwa magari ya Zimamoto katika kipindi cha mwaka wa fedha 2005/2006, kwa lengo la kupunguza majanga ya moto.

Hayo yalisemwa jana na Kamishna wa Zimamoto nchini, Sotery Ntamuturano alipokuwa akitoa ufafanuzi baada ya baadhi ya mikoa nchini kulalamika kuwa hawana vituo vya Zimamoto hivyo kushindwa kudhibiti majanga ya yatokeapo.

Alisema mikoa kama Singida na Kagera walifunga vituo vya Zimamoto miaka mitatu iliyopita na kuwastaafisha watumishi wake kwa madai hawana kazi, lakini kwa sasa ni lazima wafufue vituo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwaajiri watumishi.

"Walifunga vituo kwa madai watumishi hawakuwa na kazi za kufanya, sasa majanga ya moto yameongezeka wanalalamika. Hata hivyo katika mwaka huu wa fedha, serikali imenunua magari saba kwa ajili ya mikoa saba nchini kwa lengo la kuboresha huduma za zimamoto katika mikoa yote," alisema Ntamuturano.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Kagera, Singida, Kilimanjaro, Dodoma, Morogoro, Lindi na Pwani.

Ntamuturano aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya ukaguzi wa vifaa vya zimamoto kwenye majengo na kuwataka wananchi kutowapatia malipo ya ukaguzi watumishi wa Idara hiyo wanapokwenda kukagua.

Akifafanua, Ntamuturano alisema kuna baadhi ya wateja ambao wanadai wamewalipa fedha za ukaguzi wa majengo watumishi wa idara hiyo (wakaguzi) hivyo hawawezi kulipa tena ofisini kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

"Ni kinyume cha sheria kwa mteja anayekaguliwa jengo lake kumlipa fedha taslimu mkaguzi, wateja wote wanapaswa kulipa fedha zao kwenye ofisi za Idara ya Zimamoto na sio kuwapatia wakaguzi," alisema Ntamuturano.

 

 

 

Sekondari zaidi zahitajika Moshi

Na Rodrick Makundi, Moshi

MKOA wa Kilimanjaro bado unahitaji shule za sekondari ili kukidhi mahitaji ya kila mmoja ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kuendelea na masomo.

Hali hiyo imetokana na idadi kubwa ya wanafunzi wapatao 8,000 waliomaliza elimu ya msingi na ambao walitakiwa kujiunga na shule za sekondari, ingawa kuna shule mpya 31 za sekondari za kutwa mpya zilizoanzishwa mwaka huu.

Takwimu hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Tawala wa mkoa Ndeshukurwa Sumary katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na kaimu wake Felisian Mchuluza wakati wa mahafali ya 18 ya wanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Majengo.

Kwa mujibu wa katibu tawala huyo, mkoa una shule za sekondari 200, shule 116 zikiwa ni za serikali na 84 za binafsi.

Kufuatia hali hiyo, Sumary alisema serikali inaendelea na uhamasishaji wa wananchi wake kujiingiza kwenye ujenzi wa shule binafsi ili kukidhi kiwango cha wanafunzi wanaofaulu na kukosa nafasi za kuendelea na masomo ya sekondari.

Hata hivyo, alisema wanafunzi ambao walikosa nafasi wameweza kupatiwa nafasi katika shule binafsi hivyo akahimiza wazazi kutilia mkazo katika elimu hasa ulipaji wa ada zitakazowezesha kuboresha viwango vya elimu zinazotolewa.

Mapema, akisoma risala yake Mkuu wa shule Peter Lyimo alisema shule hiyo meendelea kukua kitaaluma ambapo imeongeza michepuo kwa wanafunzi wanaojiunga na masomo ya kidato cha tano.

Katika mahafali hayo, wanafunzi 220 wamehitimu masomo yao ya kidato cha nne.

 

 

 

Wafuasi wawili wa CUF Dar mbaroni

Ni kwa kushiriki maandamano haramu

Na Mwandishi Wetu

WATU wawili wanasadikiwa kuwa ni wafuasi wa chama cha CUF, jana walikamatwa na polisi mjini Dar es Salaam kwa tuhuma za kushiriki maandamano ambayo polisi waliyazima haraka.

Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hii, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Alfred Tibaigana alisema, watu hao ambao hakutaja majina yao walikamatwa baada ya kudaiwa kushiriki maandamano katika eneo la Mbagala Kizuiani, Wilayani Temeke.

“…ndiyo kuna kundi la watu waliokuwa na bendera za CUF walijikusanya na kuanza kuandamana pale Kizuiani, Temeke. Lakini tukavunja mara moja maandamano hayo na kuwakamata wawili kwa ajili ya kuwahoji,” alisema Tibaigana.

Alisema pamoja na kuwakamata watu hao ambao hakutaja majina yao, alisema polisi inawatafuta viongozi wa CUF walioshawishi kufanyika maandamano hayo kinyume cha sheria.

Tibaigana alisema, katika maeneo mengine kama Kariakoo, Buguruni kuliripotiwa kutokea maandamano madogo madogo ambayo yalisababisha shughuli kusimama na maduka kufungwa.

Kwa mujibu wa Tibaigana wafuasi hao wa CUF walizua maandamano hayo wakitaka mambo yaende walivyotaka wao katika matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika juzi kumpata Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani.

Uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani haukuweza kufanyika nchini kote baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuusimamisha hadi Desemba 18, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chadema, Jumbe Rajabu Jumbe, mwishoni mwa wiki iliyopita.

 

 

Uchukuaji fomu kuomba Uspika Bunge la Jamhuri waahirishwa

Na Mwandishi Wetu

UCHUKUAJI fomu kwa ajili ya kuomba Uspika wa Bunge kwa tiketi ya CCM uliokuwa uanze leo umeahirishwa.

Taarifa iliyotolewa jana mjini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula ilisema, kwa upande wa utoaji fomu kwa ajili ya kuomba Uspika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia CCM utaanza leo na fomu hizo kurejeshwa keshokutwa kabla ya saa 10 jioni.

Mangula alisema katika taarifa hiyo kwamba, hali hiyo imetokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani na badala yake kupangwa ufanyike Desemba 18, mwaka huu, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya Chadema, Jumbe Rajab Jumbe.

Alisema wanaowania kugombea nafasi hizo watatakiwa kutoa sh. 500.000 wakati wa kuchukua fomu hizo.

Mangula alisema, kwa mujibu wa ratiba iliyokwishatolewa na Chama, Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) inatakiwa kukutana Jumamosi, wiki hii kuwachuja wagombea wa nafasi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Alisema, Kamati Kuu ya CCM iliyokutana Agosti 13 na 14, mwaka huu ilikasimu madaraka ya kufanya uchujaji na uteuzi wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Chama Zanzibar.

Utaratibu wa kugombea, kuchuja na kuteua wagombea wa nafasi ya Manaibu Spika hufanywa na vikao vya kamati za Wabunge/Wawakilishi wa CCM.