UHURU 02.11.2005

 

Ni Karume tena Zanzibar

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

RAIS Amani Abeid Karume, anaendelea kuwa Rais wa Zanzibar kwa miaka mitano ijayo.

Karume ambaye alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliyofanyika Jumapili iliyopita, ameshinda uchaguzi huo kwa kumbwaga mpinzani wake mkuu, Seif Shariff Hamad wa CUF.

Anaapishwa saa tatu asubuhi leo katika viwanja vya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Mnazi Mmoja mjini hapa.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo alasiri jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Masauni Yussuf Masauni, alisema Karume ameshinda kwa tofauti ya kura 32,059. Amepata kura 239,832 ambayo ni sawa na asilimia 53.2 ya kura 460,581 zilizopigwa katika uchaguzi huo. Watu 507,225 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Karume kumbwaga Seif Shariff katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar. Mara ya kwanza alimbwaga mwaka 2000 katika uchaguzi wa pili wa vyama vingi nchini.

“Kwa kufuata masharti ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, kifungu cha 34, na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 42(4), natamka na kumtangaza rasmi Mhe. Amani Abeid Karume, kuwa amechaguliwa kihalali na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,” alitangaza Masauni.

Seif Shariff Hamad ambaye amegombea nafasi hiyo kwa mara ya tatu mfululizo, alipata kura 207,773, sawa na asilimia 46.1. Aligombea pia bila mafanikio katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, alipopambana na rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour.

Vyama sita vya siasa vilisimamisha wagombea katika uchaguzi huo wa juzi. Mbali ya CCM na CUF vyama vingine ni Jahazi Asilia, Sauti ya Umma, NRA na DP.

Mgombea wa Jahazi Asilia, Mussa Haji Kitole amekuwa mshindi wa tatu kwa kupata kura 2,110 ambayo ni asilimia 0.5 ya kura zote, akifuatiwa na Abdulla Ali Abdulla wa DP, aliyepata kura 509, Simai Abdulrahman Ali wa NRA aliyepata kura 449, na Maryam Ahmed Omar wa Sauti ya Umma aliyeambulia kura 335. Wote hao kura zao ni asilimia 0.1 ya kura zilizopigwa.

Masauni alisema kuwa kura zote zilizopigwa katika uchaguzi wa rais Jumapili iliyopita, zilikuwa 460,581 ambazo ni asilimia 90.8 ya wapiga kura wote waliyoandikishwa kwa ajili ya uchaguzi huo 507,225.

Alisema kuwa asilimia 2.1 ya kura zilizopigwa ambazo ni 9,613 ziliharibika.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, alisema Chama cha Mapinduzi kimeyapokea na kuyakubali matokeo hayo.

Alisema matokeo yaliyokipa ushindi chama chake yameonyesha matakwa ya Wazanzibari wengi, ambao wameipa ridhaa CCM iwaongoze.

Amewataka wana CCM na wananchi kusherehekea na kuufurahia ushindi huo, kwani huo ndiyo wakati wao wa kufurahi, na wasiwe na wasi wasi wote.

Nacho Chama cha National League for Democracy (NLD), kimekipongeza Chama cha Mapinduzi na Rais Amani Abeid Karume, kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Oktoba 30, 2005.

“Uongozi wa NLD unaamini kwa kutangazwa Mhe. Amani kuwa Rais wa Zanzibar kuiongoza Zanzibar kwa kipindi kingine cha miaka mitano, ikizingatiwa ameshakuwa mzoefu wa migogoro iliyoikumba Zanzibar kisiasa, kutampa nafasi ya kumuwezesha kuwajumuisha Wazanzibari wote kukaa pamoja kuangalia mustakabali wa Zanzibar,” alisema.

Sherehe za kuapishwa kwa Rais karume leo zitahudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Benjamin Mkapa, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Sheni, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula na viongozi wengine wa chama na serikali.

 

CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kimempongeza Rais  Amani Abeid Karume kutokana na kushinda nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita.

Taarifa  iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu CCM (Zanzibar), Saleh Ramadhani Feruzi kwa vyombo vya habari, CCM imempongeza Karume kutokana na ushujaa wake uliomuwezesha kuwavuusha Wana-CCM katika uchaguzi huo mkuu kwa kipindi kingine.

Sambamba na hatua hiyo, CCM pia imeitaka CUF kuheshimu matokeo hayo ambayo ni kauli ya Wazanzibari.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita na matokeo yake kutangazwa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Rais Karume ameshinda kwa asilimia 53.2 katika nafasi ya urais pamoja na majimbo 30 katika nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

" Tunampongeza Rais Karume kwa ushindi huo na kumtakia mafanikio katika kipindi chake cha  pili cha uongozi wake," ilisema taarifa hiyo na kuzipongeza juhudi za Rais Karume pamoja na wanachama wengine kwa kuiwezesha CCM kuibuka mshindi.

Feruzi alisema katika tathmini yake kupitia kwa mawakala wake imeridhika kuwa uchaguzi huo uliendeshwa kwa kuzingatia misingi ya sheria na inaungana na waangalizi wa Umoja wa Afrika kuipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kufanikisha uchaguzi huo muhimu.

 

 

 

…Zanzibar yalipukwa kwa nderemo

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MJI wa Zanzibar, ulilipuka kwa shangwe, nderemo, hoi hoi na kila aina ya furaha jana alasiri, mara tu baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kumtangaza Rais Amani Abeid Karume kuwa ameshinda urais katika uchaguzi wa Jumapili iliyopita.

Barabara za Michenzani, Madema na Maisara ambazo kabla ya matangazo ya matokeo ya uchaguzi wa rais kutangazwa zilikuwa tupu, ghafla zilijaa maelfu ya wana CCM na wananchi.

Wana CCM bila ya kujali kuwa wamefunga katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, wakiwa wamevalia sare za Chama cha Mapinduzi na fulana zenye picha wa Karume, mgombea urais wa Muungano, Jakaya Kikwete na wagombea wengine wa uwakilishi wa CCM, waliingia barabarani kufurahia ushindi huo wakiwa na kila aina ya vibweka.

Magari ya abiria maarufu kwa jina la daladala, malori na gari ndogo nazo zilifurika mabarabarani zikiwa zimepambwa kwa bendera za CCM, zikiwa zimejaza mashabiki wa Chama cha Mapinduzi, ambao walikuwa wakiimba na kucheza kuonyesha furaha yao kwa mgombea wao wa CCM, Amani Abeid Karume, kumshinda Seif Shariff wa CUF kwa mara ya pili mfululizo.

Alimshinda mara ya kwanza mwaka 2000, wakati karume alipogombea kwa mara ya kwanza nafasi hiyo, wakati Maalim Seif akigombea kwa mara ya pili.

“Ushindi huu tulikuwa tukiusubiri kwa hamu, na madhali tumeshinda acha tusherehee kadiri tuwezavyo na kwa namna tuitakayo,” alisema mwana CCM mmoja, aliyejitambulisha kwa jina moja la Salum.

Sherehe hizo zilipata sura ya aina yake baada ya baadhi ya wananchi hao waliokuwa wamejazana kwenye mzunguko wa Michenzani, mbele ya maskani maarufu ya Kizota, walipokuja wakiwa wamepanda mikokoteni inayovutwa na punda.

Baadhi ya waliyokuwa na magari madogo waliendesha magari yao kwa kasi huku wakipiga honi mfululizo, kuonyesha furaha yao kwa ushindi huo.

“Tunamtaka mwari wetu, tunamtaka mwari wetu,” zilikuwa baadhi ya nyimbo walizokuwa wakiimba wana CCM hao maeneo ya Michenzani, huku wengine wakiwa wamebeba picha za mgombea urais wa CUF, Seif Shariff Hamad, zikiwa zimerembwa.

Wakati sherehe hizo zikipambana moto, ulinzi ulikuwa mkali karibu kwenye barabara zote za Michenzani, Kariakoo, Mkunazini na Mlandege, ambako polisi wenye silaha na mabomu ya machozi walikuwa macho kulinda doria.

Magari yalikuwa yakizuiwa yasivuke Michenzani kwenda Mkunazini, maeneo ya Mji Mkongwe, ikiwa ni tahadhari ya kuzuia uwezekano wa kuzuka ghasia kati ya wafuasi wa CCM na CUF. Jimbo la Mji Mkongwe lina wakazi wengi wafuasi wa CUF.

Hali ya kuimarishwa ulinzi ilionekana kuchukuliwa tokea asubuhi jana, ambapo magari, hasa ya daladala yalizuiwa kuingia maeneo ya Darajani.

Maduka mengi jana yalikuwa yamefungwa, na hata soko la Darajani halikutoa huduma. Hali ya kufungwa maduka imeshuhudiwa hapa tokea siku ya uchaguzi Jumapili iliyopita, na hali bado haijarejea katika hali ya kawaida.

 

DONDOO MUHIMU:

Waliojiandikisha katika Daftari la

Kudumu la Wapigakura 507,225

Waliopiga kura ya urais 460,581 ambao ni asilimia 90.8

Kura zilizoharibika 9,613 sawa na asilimia 2.1

Kura alizopata kila mgombea:

Amani Abeid Karume (CCM) 239,832 sawa na asilimia 53.2

Seif Shariff Hamad (CUF) 207,773 sawa na asilimia 46.1

Haji Mussa Kitole (Jahazi Asilia) 2,110 sawa na asilimia 0.5

Abdalla Ali Abdalla (DP) 509 sawa na asilimia 0.1

Simai Abdulrahman Abdulla (NRA) 449 sawa na asilimia 0.1

Maryam Ahmed Omar (Sauti ya Umma)  335 sawa na asilimia 0.1

SADC: Uchaguzi Zanzibar ulikuwa huru na wa haki

Na Mwandishi Wetu

WAANGALIZI wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamesema uchaguzi mkuu uliofanyika Zanzibar Jumapili iliyopita, ulikuwa wa huru na haki na umewaachia na funzo kubwa la demokrasia.

Kama ilivyo kwa SADC, wenzao wa Jumuiya ya Madola katika ripoti yao iliyotolewa juzi, nao wameungana kutamka: "Ni uchaguzi mzuri ulioonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa."

Uchaguzi huo ulikuwa wa kumpata Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Kiongozi wa kundi ka wanagalizi wa SADC, John Pandeni, aliwaambia waandishi wa habari jana katika hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam, kuwa pamoja na hilo, uchaguzi huo umeonyesha ukomavu wa hali ya juu na uvumilivu wa kisiasa.

Alisema, uchaguzi huo umeonyesha amani kubwa, uwazi katika kazi nzima ya kupiga kura, kitu ambacho kina mchango mkubwa katika kujenga amani si Zanzibar au Tanzania pekee yake, bali katika suala zima la dekmokrasia.

Kwa mujibu wa Pandeni ambaye ni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa nchini Namibia, jambo la kipekee alilojifunza ni jinsi kura zilivyokuwa zikipigwa, mbinu za maelekezo ya wasimamizi wa uchaguzi na uvumilivu wa wapiga kura.

Mambo mengine kwa mujibu wa Pandeni, ni matumizi sahihi ya daftari la kupiga kura na uhakiki wake, kama kulinganisha picha wapigaji wenyewe ni jambo lililomvutia sana na linageuka somo kwa SADC. Ni mara ya kwanza nchini kwa daftari la kupiga kura kutumika.

"Katika kipindi kabla ya kupigwa kura, ilionekana kuwa na amani, uvumilivu na mchuano mkali miongoni mwa viongozi wa vyama na wagombea" alisema Pandeni.

Aliongeza:" Wadau wote kutoka wakala wa vyama vya siasa, wasimamizi wa ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) wakala wa kusimamia sheria na waangalizi wa uchaguzi wa ndani, walifanya kazi zao kama zilivyotarajiwa".

Mambo mengi yaliyotazamwa pia kwenye uchaguzi huo, ni suala la jinsi sera wanavyozinadi, mawakala wa vyama walivyofanya kazi zao na kuwepo kwa vifaa vya kutosha.

Pia alizungumzia tatizo la baadhi ya majina ya wapiga kura amabayo hayakuonekana kwenye orodha ingawaje walikuwa na vitambulisho, ni jinsi gani wasimamizi wa uchaguzi walivyowapa ufafanuzi na kuwaridhisha.

Kiongozi huyo wa waangalizi, alisema ingawaje wanaondoka

na timu yake inaondoka kwenda nyumbani, lakini wanadiplomasia wa jumuiya hiyo waliopo nchini ndio watakaochukua jukumu la kuangalia mwenendo wa matukio hadi Desemba 18, Uchaguzi Mkuu unaohusu Rais wa Jamhuri ya Muungano na wabunge utakapofanyika. Hakufafanua kama watarudi.

Kwa upande wake, waangalizi wa Jumuiya ya Madola, walielezea dosari walizozishuhudia katika baadhi ya sehemu ambapo kulizuka ghasia na hatimaye kutulizwa na polisi, wakitaja baadhi ya maeneo kama Mtoni, Forodhani na Kiwanda cha dawa.

"Ulikuwa ni uchaguzi mzuri. Mabdiliko yamefanyika ili kutoa uwazi mkubwa, kama kuhesabu kura kwenye vituo vya kupiga kura. Kwa ujumla, mipango iliyowekwa na mazingira ilikuwa ya kuwezesha kuleta mabadiliko matakwa ya watu," ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujumbe wa Jumuiya ya Madola utakuwa nchini hadi leo kukamilisha kazi yake hiyo ya uangalizi.

 

CCM yaunguruma Z'bar

Na Mwadini Hassan, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi kimedhihirisha kukubalika kwake miongoni mwa wananchi wa Zanzibar, kwa kushinda majimbo 30 ya uwakilishi. Zanzibar ina majimbo 50.

Matokeo yaliyomalizika kutolewa mjini hapa jana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), yameonyesha kuwa majimbo yote hayo ni ya Unguja.

Chama cha upinzani cha CUF, kimeambulia majimbo 19, yakiwemo majimbo yote ya Pemba na jimbo moja la mjini Unguja. Jimbo la Unguja lililochukuliwa na chama hicho ni la Mjimkongwe. Pemba ina majimbo 18.

Kama ilivyokuwa kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa 1995 na wa pili mwaka 2000, matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Jumapili iliyopita, umedhihirisha kuwa kila chama kati ya vyama viwili vikuu vyenye upinzani mkali Zanzibar, kina nguvu katika kisiwa kimoja kati ya viwili vinavyounda Zanzibar.

Chama cha Mapinduzi kina wanachama na wafuasi wengi Unguja, wakati CUF kina ngome yake kisiwani Pemba.

Hata hivyo, wapiga kura katika jimbo la Dole wilaya ya Magharibi mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, hawakupiga kura za mwakilishi kwa kuwa karatasi zilikuwa pungufu, lakini walipiga kura za rais.

Juzi Mwenyekiti wa ZEC, Masauni Yussuf Masauni, alisema kuwa jimbo hilo litarejea upigaji kura za mwakilishi Desemba 18 mwaka huu, siku ambayo Watanzania watakuwa wanapiga kura kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, wabunge na madiwani.

Matokeo ya mwisho ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yaliyotolewa jana na ZEC, yameonyesha kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, ameshinda katika jimbo jipya la Mwanakwerekwe. Uchaguzi uliopita aligombea jimbo la Mwera, ambalo mwaka huu limegawiwa na kuundwa majimbo mapya ya Magogoni na Mwanakwerekwe.

Nahodha ameshinda kiti hicho kwa kupata kura 5,235, akifuatiwa na mgombea wa CUF Abdilahi Jihad Hassan, aliyepata kura 2,409, Aziz Mohammed Ali wa Demokrasia Makini, kura 58, Salum Hamad Faki wa NRA kura 23 na Rashid Suleiman Juma wa PPT-Maendeleo, aliyeambulia kura 19.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, Machano Othman Said, naye ametetea nafasi yake katika jimbo la Chumbuni, kwa kupata kura 6,266. Amefuatiwa na mgombea wa CUF Yussuf Issa Makame, aliyepata kura 2,933. Mossi Haji Mussa wa Jahazi Asilia alipata kura 193, Amour Ameir Muhiddin wa NCCR-Mageuzi, kura 21 na Ame Haji Mcha wa UPDP aliyepata kura 207.

Mwakilishi wa Dimani, Mwinyihaji Makame Mwadini wa CCM, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Zanzibar, ametetea jimbo lake hilo kwa kuzoa kura 7,788, akifuatiwa na mgombea wa CUF, Othman Rajab Shehe kura 3,749, Hamid Hassan Nassor wa NCCR kura 80, Hassan Hamad Fashin wa UPDP kura 76 na Said Hassan Haji wa NLD kura 39.

Jimbo la Donge, mwakilishi wake Ali Juma Shamhuna (CCM), ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, ametetea jimbo lake kwa kusomba kura 9,776 na kumtupa mbali mpinzani wake Machano Omar Masanja wa CUF, aliyepata kura 861. Ussi Juma Ibrahim wa Jahazi Asilia alipata kura 148, Jaffar Chum Haji wa TLP kura 86 na Mahammoud Ameir Muhiddin wa Chadema kura 48.

Matokeo ya majimbo mengine yaliyosalia ni kama ifuatavyo, idadi ya kura kwa kila mgombea zikiwa kwenye mabano:

CHONGA: Abdalla Juma Abdalla - CUF (4,731), Hasnuu Mohammed Haji - CCM (2,460), Abdalla Mohammed Khamis - Jahazi Asilia (83), Rashid Juma Rashid - CHAUSTA (59), Mbarouk Khamis Mbarawa - NCCR-Mageuzi (51) na Juma Saleh Juma - DP (25).

CHAKE CHAKE: Omar Ali Shehe - CUF (6,572), Suleiman Sarhan Said - CCM (1,635), Salum Kombo Feruzi - DP (43), Abass Mohammed Khatib - UDP (41), Mohammed Ali Salim - NLD (22), Maimuna Haji Kombo - SAU (22), Rashid Khamis Said - CHAUSTA (15), Saleh Seif Said - Jahazi Asilia (12), Ali Salum Khamis - NCCR-Mageuzi (41) na Makame Hilali Ame - NRA (19).

ZIWANI: Rashid Seif Suleiman - CUF (8,080), Mohammed Kombo Juma - CCM (1,003), Masoud Ali Nassor - Chadema (195), Salha Salim Khamis - Jahazi Asilia (33) na Mohammed Haji Kombo - SAU (22). WAWI: Soud Yussuf Mgeni - CUF (7,168), Mgeni Othman Juma - CCM (1,811), Salhina Nassor Suleiman - DP (141), Said Issa Mohammed - Chadema (216), Ali Juma Hassan - Jahazi Asilia (99), Maryam Saleh Juma - NCCR-Mageuzi (59), Ahmed Juma Ngwali - NRA (17), Mayasa Mussa Khamis - SAU (11) na Ali Rashid Abeid - UDP (11).

KOANI: Haji Mkema Haji - CCM (9,470), Khamis Malik Khamis - CUF (3,611) na Ramadhan Khamis - Jahazi Asilia (5,361). CHWAKA: Mohammed Kombo Mkanga - CCM (10,339), Amour Ramadhan Nassor - CUF (1,646), Ramadhan Soud Mlenge - TLP (311), Mwanakombo Maalim - UPDP (43) na Said Suleiman - Jahazi Asilia (282).

UZINI: Tafana Kassim Mzee - CCM (11,273), Khamis Seif Khamis -CUF (799) na Vuai Bai Soud - Jahazi Asilia (850). MAGOMENI: Salmin Awadh Salmin - CCM (6,384) na Ali Haji - CUF (3,660). MAGOGONI: Daud Hassan Daud - CCM (4,174), Nassor Khamis Mohammed - CUF (3,154) na Hassan Omar Khamis - UPDP (36).

FUONI: Anaclet Thobias - CCM (6,633), Sheikh Hamad Sheikh - CUF (3,034), Abdulazizi Ali Foum - Demokrasia Makini (190), Hassan Abdalla Nuhu - NCCR-Mageuzi (51), Mbarak Said Khalfan - NRA (54), na Ramadhan Vuai Mwita - TLP (88).

MFENESINI: Ali Abdalla Ali - CCM (5,228), Nassor Masoud Seif - CUF (2,050), Kipenda mabrouk - Jahazi Asilia (141) na Abdulrahman Amour - UPDP (21). KITOPE: Mshimba Makame Mbarouk - CCM (7,868), Hassan Khatib Kheir - CUF (1,703), Sihaba Amir Hassan - Jahazi Asilia (166), Fatma Masoud Kheir - Chadema (74), na Dume Khamis Makame - UPDP (60).

KWAMTIPURA: Hamza Hassan Juma - CCM (8,375), Majaaliwa Juma Seif - CUF (2,691), Mtumweni Jabir Seif - Jahazi Asilia (280), Mtumwa Ame Khamis - NCCR-Mageuzi (78), Omar Abdalla Hussein - UPDP (25) na Joyce D. Sanga - SAU (40). KWAHANI: Ali Suleiman Ali - CCM (7,537) na Haji Ame Haji - CUF (1,524).

KOJANI: Omar Ali Jadi - CUF (8,471), Makame Juma Said - CCM (711), Shaame Omar Ali - Chadema (277), Hassan Kombo Hassan - NCCR-Mageuzi (85) na Abdulla Mohammed Khamis - SAU (31). BUBUBU: Khatib Suleiman Bakari - CCM (5,229), Juma Omar Juma - CUF (4,936) na Mkubwa Omar Juma - SAU (63).

MTONI: Khamis Jabu Makame - CCM (4,414), Mazrui Nassor Ahmed - CUF (3,276), Ali Salum Ali - Chadema (40), Nassor Salum Khamis - CHAUSTA (29), Bishara Khalid Khamis - UDP (21), Ali Azan Kiongwe - UPDP (21) na Mussa Abdulkadir Mbaraka - SAU (13).

MJIMKONGWE: Fatma Abdulhabib Fereji - CUF (6,929), Simai Mohammed Said - CCM (2,431), Ali Hamad Juma - PPT-Maendeleo (30), Zaina Abdalla Mohammed - NLD (27), na Said Salum Hamad - UPDP (27). MKANYAGENI: Haji Faki Shaali - CUF (4,075), Khamis Juma Othman - CCM (2,112), Haji Bakari Omar - NCCR-Mageuzi (51) na Thabit Kombo Dadi - NRA (32).

 

Polisi waagizwa kukamata Dar

Na Esther Katua

POLISI wameagizwa kuwakamata viongozi wa ngazi za mkoa na wilaya wa CUF, ambao wamedaiwa kuhamasisha wanachama wao waandamane bila sababu za msingi na kuhatarisha amani na utulivu jijini.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Luteni mstaafu Yusuf Makamba jana ofisini kwake kufuatia maandamano yaliyofanywa na wanachama wa CUF jijini juzi.

Naye kamanda wa polisi Mkoa wa Dar es Salaam Alfred Tibaigana aliwaambia waandishi wa Habari jana kuwa wafuasi wanane wa CUF, wanashikiliwa na polisi ambapo viongozi kadhaa wa chama hicho wanatafutwa kwa kuhamasisha maandamano.

Tibaigana aliwataja waliokamatwa kuwa ni Ramadhani Salum ( 28), Sharif Kiviku (26), Harun Ali (45), Ramadhan Mfaume (22), Ali Kassim (26), Hamis Ali (53) Bernard Joseph (22) na Mwinyi Sidi (24).

Tibaigana aliwataja viongozi wengine wanaotafutwa na polisi kwa uchochezi na kuhamasisha maandamano hayo kuwa ni katibu wa CUF mkoa wa Dar es Salaam, na makatibu wa chama hicho wa wilaya za Ilala na Temeke.

Wengine ni mgombea udiwani wa chama hicho Mbagala Zakhem aliyetambuliwa kwa jina moja la Chivi .

Viongozi hao kwa pamoja wanadaiwa kuhamasisha wafuasi na wanachama wa chama hicho kuandamana kwenye maeneo mbalimbali jijini ili wakutane makao makuu ya chama hicho Buguruni kwa lengo la 'kujipongeza' kwa ushindi wa uchaguzi wa Zanzibar.

Makamba kwenye mkutano wake uliowahusisha wakuu wa wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke ambao pia ni wenyeviti wa kamati za Ulinzi na Usalama kwenye wilaya zao, alisema wanachama wa CUF hawawezi kuandamana bila kuhamasishwa na viongozi wao.

Makamba alisema kitendo cha wafuasi wa CUF kuandamana bila kuwa na kibali wala kufuata karatibu wakishangilia ushindi ni kinyume cha sheria na si cha kuvumiliwa.

" Kitendo cha juzi kimetupa wasiwasi kuwa watu hawa wanachezea amani na utulivu wa Dar es Salaam, tukiwaachia wanaweza kuleta vurugu wakati wa uchaguzi Desemba, hatuwezi kuruhusu mambo haya yafanyike hapa tunalaani na tutakuwa wakali toka sasa hawawezi kuchezea serikali kiasi hiki", alisema Makamba

Makamba alisema kitendo cha wafuasi hao kuandamana na kufanya vurugu mitaani kulisababisha hofu kwa wakazi na wafanyabiashara ambao wengi wao walilazimika kufunga biashara zao na wengine walipoteza.

Makamba aliwataka wakuu wa Wilaya kukutana na viongozi wa wilaya wa vyama vyote vya siasa ili kuwaelimisha taratibu na kanuni za nchi na sheria za kuandamana, wakati yeye atakutana na viongozi wa mikoa wa vyama hivyo.

 

...Dar yazizima kwa nderemo na vifijo

Na Mwandishi Wetu

JIJI la Dar es Salaam jana lilipuka kwa nderemo, vifijo vya shangwe kutoka kwa wanachama , wakereketwa na mashabiki wa CCM kufuatia ushindi wa kishindo wa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Aman Abeid Karume.

Wafanyakazi wa ofisi ndogo ya Mkao Makuu ya CCM na Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam walionekana wakirukaruka kwa furaha kushangilia ushindi huo

Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es salaam alisema ushindi wa CCM huko Zanzibar ni moja ya mapigo makubwa yaliyopangwa kutua kichwani mwa CUF na kwamba pigo lingine litawaangukia Desemba 18 mwaka huu ambapo CCM itazoa kura zote za ndiyo.

Chizi akiwa na picha ya Rais Karume mkononi mwake akifurahi na wanachama wengi nje ya ofisi yake huku matarumbeta ya vijana wa CCM yakitumbuiza, alisema ushindi wa CCM ni uamuzi halali wa wananchi wa Zanzibar ambao wamesikia sera na kauli mbalimbali kipindi chote cha kampeni.

Nao wanachama 72 wa tawi la CCM la wauza magari Mtaa wa Lumumba jana walikutwa wakirukaruka chini ya bendera ya CCM ikiwa ni kurfurahia ushindi wa Rais Karume.

Zeno Bosco wa tawi hilo akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema walipokea kwa furaha ushindi wa mgombea wa CCM huko Zanzibar na kwamba ushindi huo unadhihirisha ukamavu wa kisiasa wa Wazanzibar.

David Mwita akiwa na Martin Manyawa wa tawi hilo walisema ushindi ni wa haki na kwamba CCM imefanya mambo mengi hapa nchini ukilinganisha na vyama vya upinzani.

Katika hatua nyingine, mmoja wa wanachama wa CUF alisema kushindwa kwa mgombea wa CUF kumetokana na ukweli kwamba hachaguliki.

"Hamad alishawahi kushindwa uchaguzi mara mbili, bado alitaka kujaribu jambo ambalo haliwezi,'' alisema mwanachama huyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake.

Mapema jana hiyo baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam walilaani kauli ya mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia CUF, Seif Shariff Hamad aliyoitoa juzi ya kuyakataa matokeo kabla ya Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) haijayatangaza.

Katika tukio lingine, wasafiri wa daladala lililotoka Kariakoo kwenda uwanja wa ndege walilazimika kumteremsha mtu mmoja aliyekuwa akiwasiliana na ndugu zake waliokuwa Unguja ambapo aliwahimiza wayakatae matokeo na kuadmana.

Wakitoa maoni yao kufuatia msimamo wa Hamad alioutangaza juzi kupitia waandishi wa habari huko Zanzibar, watu kadhaa walisema kauli hiyo inalenga kuwadanganya vijana wapambane na vyombo vya sheria kwa faida zake.

Maganga Shabaan ambaye ni mkazi wa Gongo la Mboto akiwa kwenye biashara yake barabara ya Samora alisema alishitushwa na kauli ya Hamad alipowaambia waandishi wa habari kwamba hakubaliana na matokeo .

Shabaan alisema kitendo cha Hamad ni cha kuchochea ghasia nchini na kwamba lazima vyombo vya dola vichukua hatua za kudhibiti hali hiyo.

Naye Juma Mikidadi wa Mburahati anayefanya kazi ya kusafisha viatu mtaa wa Agrey mjini hapa alisema Hamad alitakiwa kukamatwa tangu juzi.

Taarifa ya awali kwa matokeo ya uchaguzi juzi zilionyesha kwamba CUF ilikuwa imeshinda viti vyote 18 vya Pemba ambako ni ngome ya chama hicho na CCM ilijizolea viti 31 eneo la Unguja ambako ni ngome yake.

Kufuatia taarifa hizo, Hamad alipata kiwewe na kuanza kuitisha mkutano wa waandishi wa habari ambapo alisema hatakubaliana na matokeo yatakayotangazwa na Tume na kushauri isitishe hadi kasoro zitakaposhughulikiwa.

Amina Usia wa Buguruni anayeuza kadi za simu mtaa wa Samora alisema kitendo cha Hamad kutaka kukataa matokeo kinatokana na dalili alizoziona kwamba alishashindwa.

''Tatizo la Hamad ni kwamba akishindwa uchaguzi huu, hatagombea tena urais 2010 kwa vile vijana wa CUF walimweleza kwenye mkutano mkuu kwamba akishindwa ajue ndio kwa heri," alisema.

Naye Mzee Omar Hashim wa soko la Kisutu alisema ipo haja kwa wanasiasa wote nchini kuhakikisha wanakubali matokeo yanapotangazwa kwa vile ni kauli ya wapiga kura.

"Taratibu za kupigaji kura zilifanyika kwa haki na usawa, lakini matokeo yanakataliwa kwa sababu zipi? " alihoji Mzee Hashim.

Wakati huo huo, juzi abiria wa daladala kutoka Kariakoo kwenda Gongo la Mboto walilazimika kumteremsha abiria mwenzao baada ya kumsikia akitoa kauli za kushawishi wakazi wa Unguja wafanye fujo alipokuwa akiongea na simu .

Mtu aliyeshuhudia tukio hilo alisema jana kwamba abiria huyo alipiga simu akiwa ndani ya daladala na kuanza kuuliza hali ya uchaguzi na kwamba baadaye alisikika akisema wasikubali CCM itaqngazwe mshindi , na kuwataka wafuasi wa CUF kuandamana hati ZEC.

"Abiria walimfokea na kumwamuru dereva asimamishe daladala , jambo ambalo lilitekelezwa na hatimaye kumtaka abiria mwenzao ateremke kwa vile ni mchochezi wa masuala ya siasa'' alisema mtu aliyeshuhudia.

 

Maazimio ya mabadiliko Baraza la Usalama yafikiwa

Ni katika mkutano uliofanyika makao makuu ya Au

Na Mwandishi Wetu

MKUTANO wa Umoja wa Afrika umefikia maazimio ya kuunda timu ya nchi 15 ya kufuatilia msimamo wa nchi za Afrika wa kutaka mabadiliko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Abdulkadeer Shareef alisema kuwa mkutano huo uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia na kuhudhuriwa na marais sita, mawaziri wakuu sita na mawaziri wa mambo ya nje ulikuwa ukijadili taarifa ya maamuzi ya nchi za Afrika ya kutaka nafasi mbili za ujumbe wa kudumu na nafasi tano za ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Dk. Shareef alisema kuwa timu hiyo ya nchi tano inaongozwa na mwenyekiti wa Umoja wa Nchi za Afrika na Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo itafanya kazi ya kupiga kampeni kwa nchi zingine zinazojiita marafiki wa Afrika kwa lengo la kuungwa mkono.

Alisema azimio lingine ni kuhakikisha uamuzi huo unapelekwa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa haraka iwezekanvyo kwa ajili ya kupigiwa kura.

Wakati huo huo, Jacob Tesha kutoka Addis Ababa, Ethiopia anaripoti kuwa Waziri Mkuu Frederick Sumaye amesema Tanzania inaunga mkono msimamo wa nchi za Afrika kutaka zipewe nafasi ya viti viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vyenye hadhi ya kura ya turufu.

Akichangia taarifa iliyotolewa jana katika mkutano wa tano usio kuwa wa kawaida wa viongozi wa Umoja wa Afrika unaojadili mageuzi ndani ya Umoja wa Mataifa, na hususan Baraza la usalama la umoja huo.

Waziri Mkuu Sumaye alisema mbali na viti hivyo viwili vya kudumu, Tanzania iko bega kwa bega na nchi nyingine barani humu kudai viti vingine vitano visivyokuwa vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Alisema Tanzania inaamini Afrika ni lazima iendelee na msimamo wake wa kudai viti hivyo kutokana na ukweli kwamba mambo mengi yanayojadiliwa katika Baraza la Usalama yanalihusu bara la Afrika.

Waziri Mkuu Sumaye alisema ni muhimu kwa nchi za Afrika kujiunga na mataifa matano yenye viti vya kudumu katika baraza hilo, yaani Ufaransa, Uingereza, Marekani, Russia na China ili kulinda maslahi ya taifa.

Alisema ni busara kwa mataifa ya Afrika kuendelea kuyashawishi mataifa matano yenye viti vya kudumu katika Baraza la Usalama kuhakikisha kwamba watakwa ya Afrika yanatiliwa maanani wakati wa mageuzi ndani nya Baraza hilo yatakayopitishwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Waziri Mkuu Sumaye katika mkutano huo amemwakilisha Rais Benjamin Mkapa, mkutano huo wa wakuu wa nchi una ajenda moja ya kupokea taarifa za kamati yake iliyopewa jukumu la kupendekeza mageuzi ndani ya Umoja wa Mataifa na jinsi ya kupanua uwakilishi katika Baraza lake la Usalama.

 

 

Mkapa apokea hati za Balozi mpya wa UAE

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa jana alipokea hati za utambulisho kutoka kwa balozi mpya wa Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Malalia Mubarak Swaid Elamri.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyolewa na Ikulu, ilisema balozo huyo ni wa kwanza kutoka Muungano wa Falme za Kiarabu kuwa makazi ya kudumu nchini Tanzania.

Akiwasilisha hati zake, balozi Elamri alimhakikishia Rais Mkapa kuwa atafanya juhudi kukuza na kuendeleza uhusiano uliopo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniana Falme za Kiarabu.

Kwa upande wake, Rais Mkapa alimhakikishia ushirikiano kutoka serikalini ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Uhusiano wa kati ya Tanzania na Falme hizo za Kiarabu ni wa kihistoria ulionza kabla hata ya nchi hiyo kuwa na uhusiano wa kidiplomasia.

Ilisema uhusiano rasmi kati ya nchi mbili hizi ulianza katika miaka ya 1970 wakati Mzee John Samwel Malecela akiwa Waziri wa Mambo ya Nje alipotembelea Falme hizo na kutia saini mkataba wa pamoja wa makubaliano ya ambao ulizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa Tume ya Ushirikiano ya Pamoja kati ya nchi mbili hizo.

Tume hiyo ilianzishwa rasmi mwaka1985 ambayo ilitilia mkazo ushirikiano katika sekta ya uchumi, biashara. Sayansi na ufundi.

Ilisema tangu kuanzishwa kwa Tume hiyo, Tanzania imekuwa ikinufaika kwa kupata misaada mbalimbali ya kimaendeleo kutoka Falme hizo.

 

Ashukuru kanisa kupatiwa majengo kwa bei nafuu

Na Bahati Alex, Iringa

MHASHAMU Askofu Mkuu Norbert Mtega wa jimbo la Songea amemshukuru Rais Benjamin Mkapa kwa kulipatia Kanisa Katoliki majengo ya Chuo cha Benki cha Amon Nsekela kwa bei pungufu ili kukifanya Chuo Kikuu cha madhehebu hayo.

Askofu Mtega alikuwa akizungumza katika ufunguzi wa masomo ya juu ya sheria na sayansi ya kompyuta yaliyoambatana na mahafali ya nne ya cheti cha kimataifa cha ufundi wa mawasiliano ya kompyuta (CISCO CERTIFIED NETWORK ASSOCIATED) katika chuo kikuu cha Ruaha.

Majengo hayo yalikuwa ya Chuo cha Benki ya Taifa ya Biashara cha Dk. Amon Nsekela na serikali iliamua kuliuzia kwa bei nafuu Kanisa Katoliki Tanzania na kuanzisha chuo kikuu chake cha Ruaha University College.

Alieleza kuwa,miongoni mwa vyuo vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki Tanzania ni Saint Augustine University of Tanzania (SAUT) kilichopo Mwanza na kingine ni cha mjini Moshi ambacho kitafunguliwa hivi karibuni.

“Kanisa Katoliki Tanzania lilikaa na kufikiria na wakaona ni vyema wakachangia elimu ya juu nchini, hivyo vyuo hivyo ni hatua chache tu walizozipiga katika mchango wa elimu ya juu nchini,” alisema Askofu Mtega.

Alisema chuo kikuu cha Ruaha kwa kuanzia kitatoa shahada za sheria na sayansi ya kompyuta na kwamba vyuo vyote vya Kanisa Katoliki ni vitachukua mwanafunzi ye yote bila ubaguzi.

Wahitimu 19 walitunukiwa cheti cha kimataifa cha ufundi wa mawasiliano ya kompyuta. Akizungumza katika mahafali hayo Mratibu wa Chuo, Baby Chuma ameyaomba mashirika mbalimbali kuwaunga mkono kwa kuwapa vifaa mbalimbali zikiwemo kompyuta.

0000

 

Watakiwa kufuga kitaalamu

Na Dunstan Bahai, Dodoma

WAFUGAJI nchini wameshauri kufuga mifugo yao kitaalamu ili kwenda na wakati hasa kipindi hiki cha utandawazi ambacho kitavutia soko la nyama na kuweza kuondokana na umasikini.

Ushauri huo ulitolewa jana na Balozi Job Lusinde wakati wa hafla ya ufunguzi wa duka la nyama la kisasa lijulikanalo kwa jina la Mshikamano lililopo mjini hapa jirani kabisa la baa maarufu ya Green View au Makrisa.

Alisema kwamba endapo wafugaji watafuga kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu, watakuwa wametengeneza soko zuri la nyama ambalo litamvutia kila mteja na hivyo kukamilisha sera ya kupambana na umasikini.

Kwa mujibu wa Balozi Lusinde, mbali na kuwa na mifugo inayovutia soko, wafugaji hao watakuwa wameweza kujipatia vipato vyao ikiwa ni pamoja na kuliingizia taifa pato lake na kuuza uchumi wake.

Balozi alisema kwamba endapo wafugaji hao watafuata kanuni bora za ufugaji wa kisasa zinazo tolewa na taalamu wa mifugo wataweza kuingia katika soko la ushindani la nyama la ndani na nje ya nchi yaani la kimataifa.

Alisema mifugo ni rasilimali kubwa kwa wafugaji na kwamba wakiitumia vizuri wanaweza kunufaika nayo na kuondokana na umasikini.

Wafugaji kwa jumla wametakiwa kuachana na umaarufu wa kuwa na mifugo mingi ambayo haina ubora na kwamba badala mfugaji kunufaika nayo anazidi kujiongezea umasikini.

Balozi Lusinde aliishukuru Serikali kwa kujenga machinjio ya kisasa pamoja na chuo cha usindikaji wa nyama mkoani Dodoma, kwani itawasaidia wananchi kupata nyama bora pia kuuzwa nchi za nje na hivyo kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

Alisema kitendo hicho cha Serikali kujenga machinjio hiyo kimewasaidia baadhi ya vijana wa Mkoa huo kupata ajira.

Alifafanua zaidi, alisema uchumi wa mkoa huo unakua kwa kutegemea sana mifugo pamoja na mazao, hivyo wananchi watilie mkazo shughuli hizo ili waweze kujiongezea vipato vyao na Taifa.

Aliomba Serikali kuwawezesha vijana ambao wanaishi vijijini ambao hawana ajira ila wana mifugo ili kuweza kufuga mifugo yao kisasa ili waweze kuwa na maisha bora.

Hata hivyo, wafugaji wa mkoa wa Dodoma na ile ya jirani na Tanzania kwa ujumla kutumia chuo cha usindikaji wa nyama kilichopo mkoani hapa ili kuweza kuthaminisha zaidi mazao yatokanayo na mifugo yao.

 

Placer Dome yatumia sh. milioni 80 kukarabati shule

Na Mwandishi Wetu, Tarime

KAMPUNI ya Placer Dome inayochimba madini ya dhahabu kwenye mgodi wa North Mara wilayani hapa imetumia zaidi ya sh. milioni 80 kukarabati Shule ya Msingi Kenyangi iliyopo katika kata ya Matongo.

Hayo yalisemwa hivi karibuni shuleni hapo na Ofisa Mwandamizi wa Placer Dome, Aggrey Kassano wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea miradi mbalimbali ya huduma za jamii inayofadhiliwa na kampuni hiyo.

Alisema fedha hizo zimetumika kwenye ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ukarabati wa nyumba ya mwalimu.

Kassano alisema kampuni yake ilianza kuisaidia shule hiyo mwaka 2000 ili kuungana na juhudi za wananchi katika eneo hilo waliojenga vyumba vya madarasa vitano na nyumba mbili za walimu.

Alisema kuwa zaidi ya sh. milioni 100 zinatarajiwa kutumika kwenye mradi huo unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Yusto Yohana, alisema uandikishaji kwa ajili ya wanafunzi wapya unatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa mradi huo utakapokamilika.

"Tunao wanafunzi 208 kwa hivi sasa na tunarajia idadi hiyo kuongezeka mradi utakapokamilika," alisema.

Aliishukuru kampuni hiyo ambayo alisema imefanya kazi kubwa sana kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

"Watoto waliofikisha umri wa kwenda shule katika eneo hili wamepata faraja kutokana na msaada huu wa Placer Dome," alisema.

Kampuni hiyo imewekeza kwenye shughuli mbalimbali za kijamii kwa lengo la kuboresha maisha ya jamii zinazoishi jirani na machimbo yake.

Huduma hizo ni pamoja na uhifadhi wa mazingira, michezo, afya na uboreshaji wa miundo mbinu.

Kwa sasa, kuna mradi unaoendeshwa kwenye vijiji vya Lamboni, Muungano na Songambele kwenye kata ya Nyamwaga unaolenga kuwapatia wanawake elimu ya biashara.