UHURU 04.10.2005

 

 

 

Zikataeni ahadi hewa za wapinzani - Kikwete

Na Bakari Mnkondo, Karatu

MGOMBEA wa urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania kuwa macho na ahadi hewa za wagombea wa vyama vya upinzani, wanazotoa kwa lengo la kuwayumbisha.

Kikwete alitoa kauli hiyo jana alipohutubia mikutano mbalimbali ya kuomba kura kwa ajili ya wagombea udiwani, ubunge na urais kupitia CCM katika wilaya ya Karatu, iliyofanyika katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Mikutano ya Kikwete ilifurika watu na wanachama zaidi ya 300 wa CHADEMA, akiwemo katibu mwenezi wa wilaya, walikihama chama hicho na kujiunga na CCM jana hiyo hiyo.

Akihutubia wananchi kwenye uwanja wa Mang'oli, alisema wapinzani wanaahidi mambo ambayo kimsingi hawawezi kuyatekeleza kwa sababu hawana uwezo wa kupata fedha za maendeleo, na hata za matumizi ya serikali.

"Serikali ya Chama tawala iliyopo madarakani ndiyo inayoweza kutekeleza miradi ya maendeleo kwa uhakika," alisema.

Kikwete alisema baadhi ya vyama vya upinzani vinadai kwamba vinajenga barabara za lami jambo ambalo alisema siyo kweli, bali ni serikali ya CCM ndiyo inayojenga barabara hizo.

Alitoa mfano wa taarifa alizopata mjini Arusha kwamba CHADEMA inadai ndiyo iliyojenga barabara ya lami kutoka Ngorongoro hadi Makuyuni, jambo ambalo alisema ni uongo.

"Barabara hiyo ilijengwa kwa msaada wa mtoto wa mfalme wa Japan, ambaye ni rafiki wa serikali ya CCM na nilimleta mimi mwenyewe huku," alisema na kufuatiwa na vigelegele kumshangilia.

Mgombea huyo alisema CCM ikipata ushindi kwenye jimbo la Karatu, ambalo lilikuwa linashikiliwa na CHADEMA, itatengeneza barabara iliyoharibika vibaya kutoka Karatu hadi Mang'oli ndani ya miaka miwili.

Akiwa Karatu, Kikwete aliwapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa jitihada wanazofanya kuzalisha mazao mbalimbali, likiwemo la vitunguuu.

Alisema CCM ikipata ushindi itahakikisha mazao kadhaa hapa nchini yanauzwa moja kwa moja nchi za nje badala ya kupitia nchi jirani.

Kikwete alisisitiza nia ya serikali ya awamu ya nne kuboresha sekta ya kilimo cha umwagiliaji, na kwamba lengo ni kuhakikisha nchi inafanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

Mgombea huyo pamoja na msafara wake leo wanaendelea na mikutano ya kampeni wilayani Monduli.

 

 

 

Waeleze watakavyoboresha sekta ya uchukuzi - Mwandosya

WAZIRI wa Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Mark Mwandosya, amewataka wananchi kuwauliza watu wanaoomba uongozi katika nafasi mbalimbali za serikali wataboresha vipi sekta ya uchukuzi.

Profesa Mwandosya alisema hayo jana wakati wa sherehe za ufunguzi wa Wiki ya Taifa ya Uchukuzi zinazofanyika kwenye Viwanja wa Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Alisema hivi sasa wagombea wa vyama mbalimbali wamekuwa wakiomba kuchaguliwa katika nafasi za uongozi huku wakijinadi kwa wananchi kuwa watafanya mambo mbalimbali baada ya kuchaguliwa.

“Ninaomba kuchukua fursa hii kuwaombeni muwaulize wagombea hao wataboreshaje sekta ya uchukuzi na kuwasaidia wananchi katika kujikwamua na matatizo yanayowakabili,” alisema.

Sambamba na rai hiyo, Waziri Mwandosya aliwataka wananchi ambao ndio wadau wakuu wa sekta ya uchukuzi kutoa maoni kwa kuchambua na kukosoa matatizo yanayoikabili.

Alisema hali hiyo itaboresha sekta ya uchukuzi na hivyo kufanya vizuri kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa jumla.

Kuhusu maadhimisho ya mwaka huu, Profesa Mwandosya alisema yamezidi kuboreshwa ambapo washiriki wameongezeka kulinganisha na miaka miwili iliyopita.

Maadhimisho ya Wiki ya Uchukuzi kwa mwaka huu ambayo ni ya tatu, yanashirikisha wadau wa sekta mbalimbali za umma na binafsi zinazohusika na masuala ya uchukuzi.

Idara na taasisi nyingi zinazoshiriki maonyesho hayo ni kutoka Wizara za Mawasiliano na Uchukuzi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mambo ya Ndani ya Nchi, Ujenzi na Viwanda na Biashara.

Kauli mbiu ya wiki ya uchukuzi kwa mwaka huu ni Uchukuzi Salama na Mazingira Bora kwa Maendeleo ya Uchumi na Jamii.

 

Mwana-CCM ajeruhiwa na wapinzani Manzese

Na Mwandishi Wetu

MKEREKETWA mwingine wa Chama Cha Mapinduzi ametolewa ngeu Manzese mjini Dar es Salaam na watu wanaohisiwa kuwa ni wafuasi wa chama cha CUF.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni ambapo mkereketwa wa CCM, Frank Semfukwe, alijeruhiwa na kupasuliwa na jiwe kichwani. .

Hali hiyo ilitokea wakati wana-CCM hao wakienda katika eneo la Mkunduge, Tandale kuhudhuria mkutano wa kampeni wa diwani wa kata ya Tandale, Dk. Mwilima Ahmed na mgeni rasmi alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Salum Londa.

Eneo hilo lina wafuasi wa CUF, ambapo katika kata hiyo chama hicho imechukua viti vinne kati ya sita katika uchaguzi wa wenyeviti wa mitaa.

Semfukwe alisema, wakati akiimba na wenzake kumsindikiza Dk. Mwilima, ambaye alianza kwa ziara ya kufungua mashina ya wakereketwa, ghafla liliibuka kundi la vijana kwenye uchochoro na kuanza kuwashambulia na yeye kupigwa jiwe kichwani.

Kijana huyo ambaye ni mjumbe wa tawi la Mwendo, alisema waliwatambua baadhi yao kuwa ni wakereketwa wa CUF na kumtaja mmoja kwa jina la Mustapha. Tukio hilo limeripotiwa Polisi.

Dk. Mwilima alizungumzia suala hilo akisema, CCM ilipata taarifa siku moja kabla mkutano, juu ya azma ya kufanyika vurugu kwenye mkutano huo, uliofanyika umbali wa nyumba mbili tu, kutoka tawi la CUF.

Alisema baada ya taarifa hiyo walitoa taarifa polisi kuomba ulinzi mkutanoni na kuandaa vijana wa CCM kuboresha ulinzi.

Londa ambaye alikuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni na kutangaza azma yake ya kuwania kiti hicho alilaani hujuma za CUF, ambapo alisema imezuia ujenzi wa daraja kuunganisha Tandale na Mwananyamala.

Londa alisema Manispaa ya Kinondoni ilitenga sh. milioni 75 kwa upendeleo maalum ili iweze kujenga daraja hilo, lakini vijana wa CUF wamekuwa wakimfanyia fujo za kumzuia mkandarasi, kiasi cha kuchelewesha kazi kwa muda aliopangiwa.

Kwa mujibu wa Dk. Mwilima, lengo lilikuwa ni kuiunganisha Tandale na njia kuelekea Hospitali ya Mwanayamala, kupitia daraja hilo, kutokana na zahanati ya Tandale kuboreshwa na kuwa na huduma za kujifungua. Zahanati hiyo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa na iko mbioni kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya.

Dk. Mwilima alisema, sasa hivi kuna mawasiliano yanafanyika na uongozi wa manispaa ili nguvu ya dola zitumike, kuhakikisha daraja hlo linajengwa bila ya pingamizi. Mjenzi ni kampuni ya Mwananchi Enterprises.

Daktari huyo wa tiba ya binadamu, alisema pingamizi hiyo ilitokea mwanzo wa ujenzi wa daraja mapema mwaka huu, lakini nguvu ya dola ilitumika na ndio ujenzi ukaendelea.

Dk. Mwilima alipinga madai kuwa anakula ruzuku ya sh. milioni 54 akisema ni kichekesho na kushangaa kauli hiyo inatolewa na anayewania udiwani, akisema hajui hata majukumu ya kazi anayoiomba.

 

Wapinzani wanawadhalilisha wananchi -Nnauye

Na Thomas Mtinge

MADAI yanayotolewa na wapinzani kwamba CCM haijafanya kitu katika kipindi cha utawala wake yanawadhalilisha wananchi, imeelezwa.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Mabomba Matatu, Kipawa, Dar es Salaam.

Alisema madai hayo yanawadhalilisha wananchi kana kwamba hawaoni wala kuwa na ufahamu wa kujua kwamba maendeleo mbalimbali yaliopo sasa yamaeletwa na serikali ya CCM.

Nnauye alisema madai hayo yanaonyesha wazi jinsi wapinzani wanavyowadhalilisha wananchi na kuwataka wawape adhabu ya kuwanyima kura ili siku nyingine wasirudie kusema hivyo.

Hata hivyo aliwataka wananchi waichague CCM kwa sababu ahadi zake zinatekelezeka, tofauti na wapinzani ambao ahadi zao hazitekelezeki.

Akizungumzia utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi cha awamu ya tatu, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoani Dar es Salaam, Michael Nyaruba alisema serikali ya CCM imetekeleza ilani hiyo kwa kiwango cha asilimia 85.

Alisema katika awamu hiyo CCM imeleta maendeleo mbalimbali ambayo yanaonekana wazi ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na utulivu kwa wananchi wake.

Nyaruba alisema ili maendeleo yaliyopatikana yaweze kudumishwa na kuendelezwa, wananchi hawana budi kuichagua tena CCM ili izidi kuendeleza mafanikio hayo.

Mgombea udiwani wa kata ya Kipawa Victus Stambuli, aliwaomba wananchi wa kata hiyo wamchague ili aweze kushirikiana nao katika maendeleo.

Alisema endapo atachaguliwa kushika wadhifa huo atahakikisha kero zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi cha uongozi wake.

Stambuli alizitaja baadhi ya kero hizo ni pamoja na bara bara, maji safi, elimu, afya na mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake, vijana na wazee.

Katika mkutano huo wa hadhara kambi ya upinzani ilipata pigo baada ya wanachama wake kuihama kambi hiyo na kujiunga na CCM.

Vyama vilivyopata pigo ni pamoja na cha CUF ambapo wanachama wake 30 walijiengua na kujiunga na CCM na CHAUSTA wachama wake 25 nao pia walijiunga na CCM.

 

 

 

 

Keenja aomba kuchaguliwa akamilishe miradi aliyoanza

Na Ferdinand Ngowi

MGOMBEA wa Ubunge jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CCM Charles Keenja, amewaomba wananchi wa kijiji cha Msumi B kilichoko Mbezi Luis na jimbo lake kumchagua tena ili aweze kukamilisha baadhi ya miradi aliyoanzisha.

Alisema kuna miradi ameianzisha lakini bado haijakamilika kutokana na kipindi chake cha miaka mitano kukamalizika huku akiwa na kiu kubwa ya kuigeuza Ubungo ‘paradiso’.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kijijini hapo juzi aliwaambia wanachama wa CCM pamoja na baadhi ya wanachama wa chama cha upinzani wa CUF waliohudhuria mkutano huo kuwa, katika kipindi chake cha ubunge amejitahidi sana kuleta mageuzi makubwa katika elimu, barabara, maji, afya na hata kujenga ofisi za Chama Cha Mapinduzi pale ambapo zilikuwa hazipo au zimechoka.

“Msumi mlikuwa hamna barabara sasa hivi mnaserereka kama mpo kwenye lami…maji lilikuwa ni tatizo kubwa sana hapa tukachimba kisima na sasa umeme huo unakuja tutaweka pampu ...nawaomba Msumi hasa ninyi CUF muipe CCM kura zenu ili mnapokunywa maji haya ya CCM muwe huru moyoni yasiwapalie,” alisema Keenja.

Alisema wapo baadhi ya watu wanawadanganya wenzao kwamba mbunge wenu hajawahi kuuliza swali bungeni, kitu alichosema ni uelewa mdogo wa baadhi ya wapinzani kwani yeye akiwa kama Waziri kazi yake ni kujibu maswali bungeni na sio kuuliza.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti baadhi wanachama wa CUF waliohudhuria katika mkutano huo walikiri kuwepo na juhudi kubwa za mbunge huyo za kuwachongea barabara na kisima, lakini wakasema kura yao watampa akiwahakikishia kuleta pampu ya maji na kukarabati sehemu korofi za barabara hiyo ambazo ni kero wakati wa mvua, mambo ambayo Keenja alishayasemea katika hotuba yake.

“Sisi hatuangalii chama tunachoangalia ni maendeleo…kama mtu anayaleta (maendeleo) tunampa kura bila ya kujali katoka chama gani…unajua watu wengi hufuata mkumbo lakini sisi ni tofauti tunachotaka ni maendeleo,” anasema Abdularahaman Mohamedi, mfuasi wa CUF Msumi B bila ya kufafanua jambo linaloashiria kukubalika kwa Keenja.

Keenja amekuwa kivutio kwa wapiga kura wengi wa jimbo la Ubungo hasa kutokana na maendeleo makubwa aliyowaletea wapiga kura wake katika nyanja ya elimu na barabara, ambapo inasemekana mbali na mambo mengine mengi aliyofanya, amejenga madarasa mapya zaidi ya 30 na madaraja makubwa matatu likiwemo lile la Kilungule ambalo limerudisha mawasiliano ya wananchi wa eneo hilo na majirani wakati mvua za masika.

Katika mkutano huo wanachama wawili wa CUF akiwemo mgombea aliyekuwa akiwania udiwani kwa tiketi ya CUF kata jirani ya Goba, aliyejitaja kwa jina moja la Issa, na kusema alienguliwa kwa mizengwe na ukiritimba wa chama hicho, na mwingine kusema amevutiwa na juhudi za Keenja katika kuleta maendeleo Jimbo la Ubungo.

 

 

 

Mkapa aishukuru taasisi ya Aga Khan kwa kuwekeza sekta ya afya na elimu

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa ameishukuru taasisi ya Aga Khan duniani kwa kuwekeza katika sekta za Afya na elimu nchini tangu awali hadi sasa.

Mkapa alitoa shukrani hizo jana jioni alipokuzungumza mjini Berlin kwenye hafla fupi iliyondaliwa na taasisi hiyo kuagana naye.

Katika hotuba ambayo nakala yake ilipatikana mjini Dar es Salaam, Rais Mkapa alisema historia ya taasisi ya Aga Khan inaanza miaka 100 iliyopita nchini Tanzania, ambapo shule mbili zilijengwa moja ikiwa Zanzibar na nyingine ikiwa Tanzania Bara ili kutoa huduma ya elimu.

Rais alisema baada ya hapo Aga Khan iliendelea kuwekeza pia kwenye sekta za afya kwa kujenga hospitali na sekta ya maendeleo ya jamii ambayo imesaidia Watanzania wengi kupata mbinu mpya za maendeleo.

Mkapa alisema Aga Khan imekua taasisi ya kuigwa duniani kwani mpaka sasa inasaidia maendeleo ya wananchi kwa kutoa misaada ya kuanzisha na kuimarisha miradi ya biashara.

Alisema misaada inayotolewa na Aga Khan inasaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wa mijini na vijijini, na kwamba misaada hiyo inasaidia kuboresha maisha kwa kujenga nyumba mpya au kusomesha watoto katika shule mbalimbali.

Rais Mkapa aliwahakikishia viongozi wa Aga Khan kwamba Tanzania itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia watu mbalimbali kujenga vitega uchumi vyao nchini.

 

 

 

 

Karume ashangazwa na wapinzani kujifanya wanajali amani

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, ameshangazwa na viongozi wa upinzani kujifanya wanajali amani na utulivu wakati CCM ndiyo kinara wa kuidumisha nchini.

Rais Karume alionyesha hali hiyo ya kushangazwa jana alipohutubia maelfu ya wanachama na wapenzi wa CCM huko Mpendae, mjini hapa katika mfululizo wa mikutano yake ya kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwezi huu.

Karume, anayegombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, alisema serikali ya Chama Cha Mapinduzi ndiyo iliyojizatiti katika kudumisha amani ya nchi kwa kulinda Katiba ya nchi, na pia Ilani ya CCM inayoongoza serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano na Zanzibar, zinasisitiza haja ya kulinda na kudumisha amani.

Rais Karume alisema amani na tulivu nchini itadumu hata kama wapinzani wanajitahidi kuivuruga, kwani serikali za CCM zitahakikisha zinaitetea kwa kupitia Katiba za nchi.

Kazi ya kutunza amani na utulivu ni ya serikali, alisema Rais Karume, na kuongeza:

"Wametuchokoza, hatukuchokezeka na nakuombeni wananchi mtulie hivyo hivyo. Viongozi wa upinzani wamekosa hoja dhidi ya serikali iliyopo madarakani, badala yake wanakosoa mambo ambayo yanasimamiwa kwa dhati na serikali."

Rais Karume aliongeza: 'Kiongozi mmoja wa juu wa chama cha CUF alikuwa Waziri Kiongozi katika serikali hii hii. Na sasa tunaposema uhuru wetu

unatokana na mapinduzi sijui ubishi kwa hilo unatokea wapi.'

Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad, aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

Rais Karume alisema inasikitisha kwa kiongozi huyo anayetaka urais kuwadharau wananchi kupita kiasi kwa kudai kuwa wananchi wa Zanzibar wanachotaka ni shibe tu, na siyo zaidi.

Alisema katika mazungumzo mwishoni mwa wiki iliyopita na mwandishi wa shirika la utangazaji la Uingereza (BBC), Seif Shariff alikaririwa akisema wananchi wa Zanzibar hawahitaji barabara wala nyumba za kukaa, isipokuwa wanachohitaji ni shibe tu.

Rais alisema hiyo ni dhihaka ya mwisho, kwani wananchi wa Zanzibar wanachohitaji ni mapinduzi katika mawasiliano, kilimo na sekta zingine mbalimbali, mambo ambayo yanazidi kutekelezwa na CCM.

 

 

Mamilioni washuhudia kupatwa kwa jua

Na Mwandishi Wetu

MAMILIONI ya watu wa nchi za Afrika, Ulaya, Asia na Mashariki ya kati, jana walishuhudia kupatwa kwa jua.

Pamoja na kutangazwa tangu wiki iliyopita kwamba Jua litapatwa, wakazi kadhaa wa jiji la Dar es salaam walikumbwa na hofu kubwa juu ya tukio hilo, ambapo kivuli cha Mwezi kiliweza kufifisha mwanga wa jua kwa karibu dakika 10 mfululizo muda wa kati ya saa 7.30 na 8.00 mchana.

Baadhi ya wakazi walionekana wakiangalia juu kwa kutumia miwani mieusi na wengine walitumia 'Negative' za picha na wengine walitumia karatasi maalum za kuzuia mwanga kwenye magari.

Hata hivyo taarifa za wanasayansi duniani zilisema kwamba kupatwa kwa jua jana hiyo hakukusababisha giza la totoro maeneo mengi duniani, bali mwanga uliendelea kuwepo ukitokea eneo la theluthi moja ya jua iliyobaki bila kuzuiwa na mwezi.

Jiji la Madrid nchini Hispania lilikumbwa na giza zito kidogo na kusababisha watu wengi kujitokeza mitaani wakisubiria hatma yake.

Nchini Uingereza, kivuli cha mwezi kiliyakumba maeneo mengi na kudumu kwa zaidi ya nusu saa, lakini maeneo kadhaa yalipata giza kidogo kuliko mengine.

Siyo kila kupatwa kwa jua kunaweza kuwa giza totoro, kwa sababu imengundulika kwamba umbo la dunia siyo la mviringo usio na mabonde kwani umbali wa kutoka duniani hadi kwenye mwezi kunatofautiana mahali na mali kwa kati ya kilometa 356,000 na 407,000.

Wanasayansi wanasema Jua litapatwa tena Marchi 29 mwaka ujao na kwamba maeneo yatakayokumbwa na tukio hilo kwa uwazi zaidi ni Afrika Magharibi , Uturuki, Russia, nchi za Jangwa la Sahara na zile za Magharibi mwa Bahari ya Mediteranian.

 

 

Watoto 5000 waondolewa katika ajira ya hatari

Na El-hadji Yuusuf, Tabora

ZAIDI ya watoto 5000 waliokuwa wakitumikishwa katika mashamba ya tumbaku wilayani Urambo, wameondolewa katika ajira ya hatari.

Taarifa iliyotolewa jana na chama kikuu cha wakulima wa tumbaku mkoani Tabora (WETCU LTD) imesema kuwa sasa hakuna wakulima wanaowatumikisha watoto katika kilimo cha zao hilo mkoani Tabora.

Taarifa hiyo imesema kuwa elimu iliyotolewa na shirika la kazi Duniani (ILO) imesaidia watoto zaidi ya 5000 waweze kuondolewa katika ajira mbaya kwenye mashamba ya tumbaku.

Watoto wadogo chini ya umri wa miaka 15 walikuwa wakiajiriwa kwenye mashamba ya tumbaku, ambapo hufanya kazi kubwa na kupata ujira mdogo.

Aidha chama hicho cha wakulima wa tumbaku kimesema kuwa uzalishaji wa zao hilo umekuwa ukiongezeka katika kipindi cha miaka mitano kutokana na ushirikiano mzuri baina ya wadau wa zao hilo.

Hata hivyo amesema kuwa wakulima wa zao hilo wamekuwa wakipata hasara kutokana na kushindwa kabisa kuzingatia maadili ya kilimo.

Amesema kuwa wakulima wengi wemeshindwa kuzalisha tumbaku nyingi kutokana na kutoihudumia vizuri toka ikiwa shambani na kuitupa hovyo katika hatua mbali mbali za kuitengeneza.

Alisema kuwa iwapo kama wakulima wa zao hilo wataweza kulitambua tatizo hilo la utupaji hovyo tumbaku kwa kushindwa kuihudumia, wataweza kuzalisha tumbaku katika kiwango cha juu cha kilo 1200 kwa kwa heka badala ya kilo 600 za wanazozalisha sasa na hivyo kupata faida kubwa.

 

 

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege Mbeya yakamilika

Na Idefonce Mgimba, Mbeya

AWAMU ya kwanza ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe nje kidogo ya jiji la Mbeya kwa kiwango cha changarawe umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Prosper Tesha ameeleza kuwa uwanja huo ambao ulikuwa ukamilike kwa asilimia 100 na kukabidhiwa serikali mwezi uliopita sasa utakamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Mkandarasi aliyepewa kandarasi ya ujenzi wa uwanja huo Kundan Singh Construction kutoka Kenya alishindwa kutekeleza mkataba wa ujenzi kama ilivyokubaliwa kutokana na kukumbana na tabaka gumu la udogo pasipo kutarajia wakati wa ujenzi na hivyo kuhitaji mtambo mkubwa wa kuweza kuchimba (Grader aina ya DC 9).

Kundan Singh sasa ameagiza mtambo huo ambao utawasili katika eneo la ujenzi wiki hii pamoja na baadhi ya mitambo mingine ili kuhakikisha ujenzi unakamilishwa mwishoni mwa mwezi huu.

Tesha alikuwa akitoa taarifa kwa Waziri wa Mawasiliano na uchukuzi Profesa Mark Mwandosya, aliyetembelea uwanja huo hivi karibuni ili kukagua maendeleo ya ujenzi ambao utawekewa jiwe la msingi la ujenzi na Rais Benjamin Mkapa wakati wowote mwezi huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tesha kwa Profesa Mwandosya dola za kimarekani Milioni 11.62 sawa na zaidi ya sh. bilioni 11.5 kwa ajili ya awamu ya tatu ya ujenzi wa uwanja huo kwa kiwango cha lami na ununuaji wa vifaa mbalimbali vya uwanja ikiwemo Kamera yenye mionzi maalum kwa ajili ya kuchunguza wasafiri na mizigo yao na pia mitambo ya kusukuma mizigo zimepatikana.

Fedha hizo zimepatikana kutoka Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na mfuko wa OPEC baada ya kutiliana saini mkataba kati ya serikali ya Tanzania na maofisa wa taasisi hizo katika hafla iliyofanyika mjini Cairo Misri.

Kiasi hivyo cha fedha pia kitagharimia ujenzi wa maegesho ya ndege, jengo la kuondokea abiria, mitambo ya zimamoto, mitambo na vifaa vya kuchunguza hali ya hewa, kuweka mtambo wa kusafisha maji na mfumo wa kuyasambaza.

Tesha alieleza kuwa mitambo muhimu ya kuongozea ndege itagharimiwa na Mamlaka inayosimamia usalama wa anga (TCAA) na kwamba awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi wa uwanja huo inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 7 imegharimiwa kwa asilimia 50 na serikali kupitia mamlaka hiyo.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini alisema uwanja huo utakuwa kichocheo cha maendeleo ikiwa wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hasa Mbeya wataanza sasa kufanya maandalizi wa kuwekeza kwa kujenga miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo mahoteli ya kisasa na mashamba ya vyakula na maua kwa ajili ya kusafirisha nje.

Aliwataka viongozi kuwasaidia wananchi katika kuandaa mikakati ya kukitumia ipasavyo kiwanja hicho cha ndege chenye urefu wa kilometa 3.4 kuwezesha kutua ndege aina ya Boeing 737 ili kuinua uchumi wa taifa na mikoa ya kusini.

"Ni rai yangu kuwa mkoa uichukue changamoto ya ujenzi wa uwanja huu kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya vinginevyo mkoa utakuwa umechelewa na kutoitendea haki nchi kwa kushindwa kuutumia uwanja huu," alisema Tesha.