UHURU 07.10.2005

 

 

 

 

Kikwete, Karume wang'ara

UTAFITI uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania - REDET, umebaini kuwa wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi, wanaongoza kwa asilimia kubwa kuungwa mkono na wananchi kulinganisha na vyama vingine.

Akizungumza kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), mjini Dar es Salaam, mwenyekiti wa REDET,  Profesa Rwekira Mukandala alisema utafiti huo wa kura za maoni ulifanyika  kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Visiwani, ambapo kila mkoa ilitumika wilaya moja kufanya utafiti.

"Kwa upande wa Bara asilimia  75.4 walisema watampigia kura mgombea wa CCM, asilimia 13.2 CUF, Chadema asilimia 0.8  ambapo asilimia 9.4 walisema hawajui watampigia kura nani," alisema Mukandala

Alisema kwa Visiwani asilimia  45.8 walisema  watampigioa mgombea wa CCM, asilimia 42 CUF, Jahazi Asilia  asilimia 1, Chadema asilimia 0.2, NCCR Mageuzi asilimia 0.2 wakati vyama vingine havikutajwa kabisa.

Mukandala alisema  pamoja CCM kuonekana kuongoza kwa asilimia kubwa kwenye kugombea urais, lakini inaonekana kushuka kidogo kwenye ubunge na udiwani, lakini akaongeza kuwa kulikuwa na asilimia kubwa ya watu waliosema hawajaamua watampigia kura nani.

"Upande wa urais asilimia 9.4 wanasema bado hawajafahamu wamchague nani,  wakati wabunge ni asilimia 11.7 na udiwani ni 13.2, hivyo vyama bado vina nafasi kubwa ya kuwashawishi wapigakura wakati huu wa kampeni kwa hiyo asilimia iliyobaki," alisema.

Kwa mujibu wa REDET, kwa wagombea urais wa Tanzania, kwa Bara, Jakaya  Kikwete amepata asilimia 75.1, Ibrahimu Lipumba asilimia  13.5, Freeman Mbowe asilimia 0.7, Augustino Mrema asilimia 0.5, Anna Senkoro asilimia 0.2, Sengondo Mvungi asilimia 0.2, Paul Kyara asilimia 0.1,  na wasiofahamu wampigie nani ni asilimia 9.5.

Kwa Zanzibar upande wa Rais wa Tanzania, Kikwete asilimia 45.6, Lipumba asilimia 40.6, Anna Senkoro asilimia 0.4, Freeman Mbowe asilimia 0.2, Sengondo Mvungi asilimia 0.2 na asilimia 13.0 hawajui watampigia kura nani.

Kuhusu Rais wa Zanzibar, Amani Karume (CCM) asilimia 45.8, Seif Shariff Hamad (CUF) 42.6, Mussa Haji Kitope (Jahazi Asilia) asilimia 1.0 na asilimia 10.2 walikuwa bado hawajui wampigie kura nani.

 

 

Hakuna mgawanyiko Zanzibar, asema Dk. Bilal

Na Khatib Suleiman, Zanzibar

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amesema Chama Cha Mapinduzi upande wa Zanzibar ni imara na hakuna mgawanyiko wa makundi ya viongozi kama inavyoelezwa na wapinzani.

Dk. Bilal alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni za CCM zinazoendelea katika jimbo la MJI MKONGWE mjini hapa, kwa ajili ya

kuwatambulisha kwa wananchi wagombea wa nafasi za ubunge na uwakilishi wa jimbo hilo.

Alisema vipo vyama vya upinzani vimeanza kuchukua ajenda kwamba ndani ya CCM upo mgawanyiko unaotokana na viongozi waliokosa kuteuliwa kugombea nafasi za uongozi, jambo ambalo sio kweli.

“CCM ni moja na imara, hakuna mgawanyiko katika suala hilo. Kipindi cha kuteuwa wagombea kimekwisha na sasa tunaelekea katika uchaguzi mkuu ambapo lengo ni kushinda na kushika hatamu ya kuongoza dola,” alisema Dk. Bilal.

Aliwataka wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi kupuuza kauli na maneno hayo yanayotamkwa na wapinzani, ambayo lengo lake ni kujaribu kupunguza kasi na ari ya wanachama katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi

mkuu.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Amani Abeid Karume, imefanya mambo mengi, yote yakiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo imelenga kuimarisha maslahi ya wananchi yawe bora.

Dk. Bilal ambaye ni Waziri Kiongozi Mstaafu, aliitaja sekta ya elimu kama ni moja ya eneo ambalo limepata mafanikio makubwa katika awamu ya serikali ya sita, ikiwemo kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi ya darasa la kwanza pamoja na kiwango

cha elimu ya sekondari na vyuo vikuu.

“Haya ni mafanikio makubwa ambayo kiongozi anatakiwa kupimwa kutokana na uwezo huo wa kuongoza,” alisema Bilal ambaye aliwataka wananchi kumchagua Rais Amani Abeid Karume, mgombea urais wa muungano Jakaya Kikwete, katika uchaguzi mkuu.

Katika mkutano huo wananchi walitambulishwa mgombea CCM kwa nafasi za uwakilishi katika jimbo la MJI MKONGWE, Simai Mohammed Said, mgombea wa ubunge, Boniface Mwale, na diwani wa jimbo hilo, Ahmed Keis.

 

  

Kamati Kuu ya CCM kukutana

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inakutana leo mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Benjamin Mkapa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Dar es Salaam jana na Idara ya Itikadi na Uenezi ilisema kikao hicho cha siku moja pamoja na mambo mengine kitatathmini maendeleo ya kampeni za CCM za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.

 

Dk. Sheni: Tutashauri benki zipunguze riba za mikopo

Na Abihudi Saideya, Handeni

SERIKALI ya awamu ya nne ya Chama Cha Mapinduzi Nikiingia madarakani itahakikisha riba za mikopo inayotolewa na benki inakuwa ndogo ili kuwezesha wananchi wengi kunufaika.

Hayo yalisemwa jana na mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Ali Mohamed Sheni, alipokuwa akizungumza kwenye mikutano mikubwa ya kampeni za uchaguzi, katika wilaya za Kilindi na Handeni, mkoani Tanga.

Dk. Sheni alisema serikali itachukua hatua mbalimbali za kuwawezesha wananchi kushiriki katika uendeshaji wa uchumi.

Ili kutimiza azma hiyo, Dk. Sheni alisema serikali ya CCM ya awamu ya nne itazungumza na wenye benki na vyama vya kuweka na kukopa kupunguza viwango

vya riba.

"Kwa kuwa mfumuko wa bei umeshuka benki zitakuwa tayari kupunguza viwango vya riba kuwawezesha wananchi wengi kuchukua mikopo," alisema.

Aliongeza:"Kupitia mpango wa kurasmisha uchumi na biashara Tanzania (MKURUBITA) serikali itatoa hati zikazowezesha wananchi kutumia ardhi na nyumba zao kupata mikopo."

Kwa sasa wananchi wengi wanasita kuchukua mikopo benki kutokana na kiwango kikubwa cha riba na wanaochukua wamekuwa wakisema mikopo hiyo haiwanufaishi kutokana na kiwango kikubwa cha riba.

Wakati wa mikutano hiyo iliyofanyika kijiji cha Mgera, kata ya Kisangasa Wilaya ya Kilindi na Handeni mjini, Wilaya ya Handeni, Dk. Sheni alimwombea kura mgombea urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete na pia wagombea ubunge na udiwani.

Wabunge walioombewa kura na kutambulishwa kwa wananchi ni Betreace Shelukindo wa jimbo la Malindi na Dk. Abdallah Kigoda anayegombea jimbo la Handeni.

Huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mikutano hiyo, Dk. Sheni alisema serikali ya CCM imefanya mengi kwa maendeleo ya wananchi wa wilaya hizo na sehemu nyingine nchini.

Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuimarishwa kwa huduma za elimu, afya, maji na barabara, akisema wilaya ya Handeni imekwishapatiwa umeme na huduma nzuri za simu.

Kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, Dk. Sheni alisema, serikali itahaikikisha Wilaya mpya ya Kilindi inapatiwa umeme na barabara ya Korogwe-Handeni-Kilosa-Mikumi inajengwa kwa kiwango cha lami.

Kabla ya kuhutubia mikutano hiyo, alipokea kadi kutoka kwa wanachama 1,287 wa vyama vya upinzani waliohamia Chama Cha Mapinduzi.

Chama kilichopata pigo kubwa zaidi ni CUF ambayo ilipoteza wachahama 759 ambapo 623 kati yao walitoka Wilaya ya Handeni na 136 Kilindi.

Vyama vingine vilivyopoteza wanachama katika Wilaya zote mbili ni TLP 265, NCCR 135,CHAUSTA 86 na CHADEMA 42.

Katika ziara yake ya kampeni mkoani Tanga, Dk. Sheni alifuatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Musa Shekimweri, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa Mama Grace Shoka na viongozi wengine wa CCM wa mkoani.

 

 

Wapongeza ahadi za Kikwete kukipa kilimo kipaumbele

Na Bashir Nkoromo, Bagamoyo

CHAMA cha Wafanyabiashara wa Kilimo na Ufugaji Tanzania (TCAL) kimeeleza kufurahishwa na mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Jakaya Kikwete, kunadi katika kampeni zake kuwa akiwa rais ataipa kipaumbele sekta ya kilimo.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa TCAL, Elias Mshiu wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya wadau wa sekta ya kilimo iliyofanyika katika hoteli ya Livingstone, mjini hapa mkoa wa Pwani.

“Mwisho naomba kueleza jambo muhimu linalohusiana na kipindi hiki cha uchaguzi mkuu wa kumpata rais wa awamu ya nne ya nchi yetu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu, kwamba tumetiwa moyo na kauli za wawania uongozi, hasa kupitia Chama cha Mapinduzi, kwamba wakichaguliwa watakipa kipaumbele kilimo” alisema Mshiu.

Alisema kufuatia kauli hiyo ya kutia moyo, chama chake kipo tayari kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na kiongozi atakayefanikiwa kunyakua nafasi hiyo ya urais ili kuweza kuinua uchumi wa nchi na wananchi kwa jumla.

Katika mikutano yake mbalimbali ya kampeni ambayo amekuwa akiifanya nchini, Kikwete amekuwa akinadi kwa marefu na mapana kwamba akichaguliwa sekta ya kilimo ataipa kibaumbele kama chachu ya kusaidia kuinua uchumi wa nchi.

Mshiu alisema ni muhimu kuwepo ushirikiano baina ya sekta ya umma na ya binafsi ili kuifanya sekta ya kilimo yenye tija na nafasi zaidi katika kukuza uchumi wa taifa.

Alisema vilevile ni lazima ni lazima kilimo kiendelezwe katika sekta binafsi na kukipa nafasi maalum.

Mshiu alisema sekta binafsi haina budi kupatiwa nafasi ya kuchukua hatua za makusudi kukiweka kilimo katika mazingira ya kibiashara.

Alisema, katika hatua hizo ni lazima wakulima kupitia sekta binafsi wapate elimu ya kutosha ya namna ya kukitumia kilimo kama sehemu ya biashara.

Mapema, akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Matern Lumbanga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Rose Rugembe alisema serikali inatambua kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa.

Alisema kilimo ndiyo sekta inayoongoza kwani kinachangia karibu asilimia 50 ya mapato la ndani na kiasi cha asilimia 40 kwa pato la kigeni, huku sekta hiyo ikiwa inatoa ajira kwa kiasi cha asilimia 80 hapa nchini.

Rose alisema serikali imekuwa ikiipa kipaumbele sekta ya kilimo na ndiyo sababu viko vitengo mbalimbali katika wizara takribani tatu ambavyo vinaratibu na kusimamia masuala kadhaa kuhusu uzalishaji, ufugaji na biashara kuhusu sekta hiyo.

Alisema changamoto iliyopo sasa ni kuzifanyia kazi sera na taratibu zilizopo kuhusu sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kuundwa vyama zaidi vinavyojishughulisha na masuala ya sekta hiyo kama kilivyo Chama cha Wafanyabiashara wa Kilimo na Ufugaji.

Rose alisema vyama hivyo, pamoja na kuundwa kwa wingi, pia havina budi kuwa na wanachama wa kutosha na kufanya kazi kwa mshikamano zaidi.

Warsha hiyo ya siku tatu inashirikisha wadau zaidi ya 100 kutoka ndani na nje ya nchi na imetaribiwa na TCAL.

 

 

 

Wenye ukimwi, maradhi sugu kuhudumiwa  na kituo cha kisasa Muhimbili

Na Mwandishi Wetu

KITUO kipya cha kisasa cha kuhudumia wagonjwa wa ukimwi na wenye maradhi sugu kimezinduliwa na Rais Benjamin Mkapa katika hopsitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.

Kituo hicho chenye vifaa vya kisasa vya kupima magonjwa sugu na wenye virusi vya ukimwi kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1000 kwa siku.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari ilisema kuwa kituo hicho kimejengwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na mfuko wa Abbott.

Abbott ni kampuni ya afya dunia inayotafiti, kuendeleza, kuzalisha na kutafuta soko la dawa na bidhaa zingine za kiafya, ikiwa ni pamoja na lishe, vifaa na uchunguzi.

Rais Mkapa pia alizindua maabara ya kisasa ambapo sasa inaweza kupima vipimo 8,000 kwa siku tofauti na zamani ilipokuwa na uwezo wa vipimo 75 kwa siku.

Maabara hiyo ina uwezo wa kushughulikia aina za anuai za damu kutoka 100 hadi 400 kwa siku.

Mwenyekiti wa Bodi na Mtendaji Mkuu wa Abbott, Miles White alisema Hospitali ya Taifa ya Muhimbili sasa itakuwa na uwezo wa kukabiliana na ugonjwa na ukimwi kwa kupanua mpango wa tiba wa taifa  kuwafikia Watanzania wengi wanaoishi na virusi vya ukimwi.

White alisema mfuko wa Abbott umelenga kutoa huduma bora, matunzo ya kudumu kwa waathirika wa ukimwi na magonjwa mengine.

alisema mfuko huo wenye makao yake katika hospitali ya  Muhimbili umelenga kuongeza vituo vya afya vya vijiji 82 nchini kote.

White alisema chini ya ubia wa mfuko na serikali ya Tanzania,  madaktari na wauguzi nchini wamewezeshwa kuboresha kwa kiasi kikubwa huduma kwa wagonjwa.

Alisema mfuko huo umesaidia kuweka vifaa vya kisasa, kuboresha usimamizi wa hospitali na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi.

White alisema kimsingi wamepanua uwezo wa taifa kutoa vipimo na tiba bora kwa waathirika wa ukimwi na magonjwa mengine ya muda mrefu.

"Tunaamini ubia huu unatoa mfano wa kuigwa na nchi nyingine na wafadhili, katika kukabiliana na changamoto kubwa ya ukimwi barani Afrika," alisema White.

Rais Benjamin Mkapa katika uzinduzi huo alisema kuwa nchi wafadhili zimekuwa hazitaki kutoa misaada kupitia serikali kwa kudhani haitumiwi vizuri, lakini ubia wa serikali ya Tanzania na mfuko wa Abbott ni kielele kuwa madai hayo si ya kweli.

Alisema kuboreshwa kwa huduma za afya ni kwa ajili ya wananchi kupata huduma bora za afya.

Rais Mkapa kabla ya uzinduzi wa maabara na kituo hicho alitembelea wodi ya Sewa Haji na kukagua jengo jipya ya wodi ya watoto.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Afya, Anna Abdallah, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi, mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Abdulrahman Kinana, Mtendaji Mkuu wa hospitali ya Muhimbili, David Tregoning na viongozi wengine wa serikali.