UHURU 12.11.2005

 

Maregesi asema uchaguzi si vita, bali ni demokrasia

Wanawake nchini watakiwa kubuni miradi ya maendeleo

TRA yaasa wafanyabiashara kuacha tabia za ‘kimachinga’

Nchi za Maziwa Makuu zapongezwa kwa kusuluhisha migogoro

Klabu za waandishi wa habari zatakiwa kuanza kuitenga CUF

Hawa wanasakwa na Polisi Dar

CUF wanavunja Katiba - Karume

Wana-CCM wote ni wagombea katika uchaguzi mkuu-Mangula

 

 

Maregesi asema uchaguzi si vita, bali ni demokrasia

Na Thomas Mtinge, Kilolo

MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abiud Maregesi, amesema kwamba uchaguzi si vita, bali ni sehemu ya kutimiza demokrasia kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wowote. Aliyasema hayo juzi kwa nyakati tofauti wakati akiwahutubia wananchi katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji mbalimbali vilivyoko katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.Maregesi alisema mtu au chama kinaposhiriki katika uchaguzi Fulani, lazima

kikubali kushindwa au kushinda kwa kuwa huo ni utaratibu wa uchaguzi.

 

Alisema anasikitishwa na kauli ya CUF kukataa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar

 

wakati walijua kabisa kwamba katika uchaguzi huo wameshindwa na kuongeza

kuwa kukataa kwao kuutambua ushindi huo kuna lengo la kuwahadaa wananchi.

Alishangaa CUF kutoitambua serikali ya Rais Karume wakati huku tayari wajumbe wa

 

Baraza la Wawakilishi walioshinda katika uchaguzi huo wameapishwa na kuahidi

 

kuilinda katiba ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Maregesi, endapo CUF itakataa kukubali serikali ya Karume, basi

 

isingekubali wawakilishi wake kuapishwa.

 

Wanawake nchini watakiwa kubuni miradi ya maendeleo

Na Pendo Mangala, Dodoma

WANAWAKE nchini wametakiwa kuwa wabunifu katika kuanzisha miradi mbalimbali ya

 

maendeleo ambayo itawasaidia kuwaongezea vipato na kuondokana na umaskini.

Wito huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Luteni mstaafu Shabani

 

Muyombo wakati alipokuwa akiongea na wafanyabiashara wa mkoa huo katika mafunzo

 

ya siku tano ya udhibiti wa ubora wa vyakula na uongozi wa biashara

 

yaliyoendeshwa na shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) yaliyofanyika mjini

 

hapa.

Muyombo alisema ni lazima wanawake wawe wabunifu katika kuanzisha miradi

 

mbalimbali ya maendeleo ambayo itawasaidia kuwaongezea kipato ikiwa ni pamoja na

 

kuondokana na umaskini.

Alisema miradi ambayo wanaweza kubuni na kuianzisha ni pamoja na kusindika

 

vyakula mbalimbali ambapo watajipatia soko zuri kwa ajili ya kuuzia bidhaa zao.

Hata hivyo, alifafanua kwamba hivi sasa mifugo ni moja ya rasilimali tosha, kwani

 

kuna mazao mengi yatokanayo na mifugo hiyo na mifugo yenyewe, hivyo wafanye

 

juhudi katika kuyanadi mazao hayo.

Alitoa mfano wa mazao yanayostawi vizuri kwa mkoa wa Dodoma ambayo ni zabibu,

 

mahindi uwele na alizeti na kuwataka wayatumie kwa kuanzisha viwanda vidogo kwa

 

kushirikina na taasisi mbalimbali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.

Mkuu huyo wa wilaya aliwashauri wanawake wa mikoa mingine kuanzisha miradi

 

kulingana na mazao yanayopatikana katika mikoa husika.

Naye Meneja wa SIDO mkoani Dodoma, Iskanda Tenga alisema kuwa mafunzo hayo

 

yanatolewa na shirika kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali wadogo waweze kupata

 

elimu ya kuweza kusindika vyakula mbalimbali vyenye ubora unaotakiwa kwa afya za

 

binadamu.

Tenga alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yamekuwa yakiyatolewa

 

kwa kipindi cha miaka mitatu na yameshatoa elimu hiyo katika wilaya zote za mkoa

 

wa Dodoma.

 

TRA yaasa wafanyabiashara kuacha tabia za ‘kimachinga’

Ni kwa kufanya biashara bila leseni

Na Ghati Msamba, Tarime

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Mara imewataka wafanyabiashara kuachana

 

na tabia za kuendesha biashara za kimachinga bila lesseni.

Hayo yalisemwa katika warsha ya wafanyabiashara na Ofisa Elimu Kitengo cha

 

Walipakodi mkoa, John Mahundi katika kijiji cha Nyamongo wilayani Tarime.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakifanya biashara zao kwa wasiwasi na

 

kuhamahama ili kukwepa kodi, jambo ambalo haliwanufaishi kibiashara.

Alisema njia pekee ya kumwezesha mfanyabiashara kufanya shughuli zake bila hofu

 

na kumnufaisha ni kulipa kodi, badala kukwepa kwa kuhamahama.

Kwa upande wa wafanyabiashara walidai kuwa wamekuwa wakiogopa kuchukua fomu za

 

kujiandikisha na kutambulisha biashara zao kutokana na kutokujua viwango na

 

gharama za ulipaji wa kodi.

Walisema hali hiyo ilitokana na ufahamu mdogo, na kwamba baada ya kuelimishwa,

 

wameahidi kukata leseni zao ili kuepuka usumbufu.

Warsha hiyo ilihusu ulipaji kodi, uanzishaji na uendeshaji biashara nchini,

 

uandikishaji majina ya biashara, kujua umuhimu wa kulipa kodi na utunzaji wa

 

kumbukumbu.

Iliandaliwa na TRA kwa kushirikiana na kampuni ya PLACER DOME na kuhudhuriwa na

 

wafanyabiashara 50 wanaouzunguka mgodi wa Nyamongo.

 

 

Nchi za Maziwa Makuu zapongezwa kwa kusuluhisha migogoro

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limewapongeza viongozi wa nchi za Maziwa

 

Makuu kwa jitihada wanazofanya kusuluhisha migogoro katika nchi za Burundi,

 

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Rwanda.

Mwenyekiti wa Baraza hilo Balozi Jean Marc dela Sabliere alitoa pongezi hizo juzi

 

jioni alipojibu maswali ya waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Moven Pick baada

 

ya kumaliza ziara ya siku 10 iliyowashirkisha wajumbe 15 wa Baraza hilo katika

 

nchi za Maziwa Makuu.

Ujumbe wa Baraza hlo ulianzia ziara yake katika nchi ya DRC na kufuatia katika

 

nchi za Rwanda, Burundi Uganda na Tanzania kwa lengo la kuangalia hali halisi.

Sabliere alisema katika ziara hiyo waligundua kwamba viongozi wa nchi za Maziwa

 

Makuu wakiongozwa na Rais Benjamin Mkapa walifanya kazi kubwa ya kusuluhisha

 

migogoro na kwamba mafanikio yanaonekana.

'Hali ya usalama ya mwaka juzi ni tofauti sana na usalama wa mwaka huu, hivyo

 

kuna mabadiliko makubwa,'' alisema na kuongeza kwamba ni jambo la kujivunia kuona

 

Burundi ilifanya uchaguzi na tayari wakimbizi wanakubali kurejea makwao kutoka

 

Tanzania.

Wakimbizi 15,000 wa Burundi waliopo Tanzania wamepangiwa kurudi nchini mwao kila

 

mwezi.

Hata hivyo alisema jitihada zaidi zinahitajika kuvishawishi baadhi ya vikundi

 

vinavyosita kushirikiana na serikali kama cha PALIPEHUTU -FNL na kikundi cha

 

waasi cha lililokuwa jeshi la Rwanda na kule Uganda.

Awali, ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ukiwa nchini ulifanya

 

mazungumzo na Rais Benjamin Mkapa ambaye alisisitiza kwamba kikundi cha

 

PALIPEHUTU kikiendelea kukaidi mazungumzo ataiambia serikali ya awamu ya nne

 

isikiruhusu kutumia ardhi ya Tanzania.

Ujumbe huo pia ulifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa

 

Kimataifa Jakaya Kikwete, na kuzungumza na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es

 

Salaam na uliondoka juzi hiyo usiku kuelekea New York Marekani.

 

Maregesi ataka wanaohujumu CCM wazomewe

Na Thomas Mtinge, Iringa

MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abiud Maregesi

amewataka wana-CCM kuwazomea viongozi na wanachama wanaokihujumu Chama kwa

 

kuisaidia kambi ya upinzani ili CCM ishindwe katika uchaguzi mkuu unaotarajia

 

kufanyika Desemba 14 mwaka huu. Maregesi alitoa kauli hiyo wakati akihutubia

 

wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM uliofanyika juzi katika

 

kijiji cha Mgoma, Wilaya ya Iringa Vijijini mkoani hapa.

Kauli hiyo ya Maregesi imekuja muda mfupi baada ya kupewa taarifa kwamba baadhi

 

ya viongozi na wanachama wa CCM akiwemo kiongozi mmoja wa kata ya Mgoma,

 

kumfanyia kampeni mgombea wa chama cha Jahazi Asilia badala ya Steven Galinoma wa

 

jimbo la Kalenga kupitia CCM.

Maregesi alionya kwamba viongozi na wanachama wa aina hiyo hawafai kuwemo ndani

 

ya CCM kwani ni hatari kwa Chama na kwamba hakiwezi kuwavumilia.

Alisema maendeleo ya kweli katika jimbo hilo yanaweza kupatikana kwa haraka

 

endapo wananchi hao wataichagua CCM na si vinginevyo, kwa kuzingatia ukweli

 

kwamba serikali ya CCM kamwe haitatupa nguvu zake katika majimbo au kata

 

zinazotawaliwa na wapinzani.

Maregesi alisema njia pekee ya wananchi hao kutatua kero zinazowakabili na

 

kujiletea maendeleo ya haraka ni kumchagua Steven Galinoma.

Kwa upande wake Galinoma alisema kwamba endapo atachaguliwa kushika wadhifa huo

 

atahakikisha kwamba anashirikiana na wananchi katika kuzitatua

kero zinazowakabili.

 

CUF mmeshindwa kwa kivuli chenu wenyewe

HIVI karibuni matukio makubwa kadhaa ya kisiasa yalijitokeza hapa nchini.

 

Miongoni mwa matukio hayo ni kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ambapo licha

 

ya kushindwa chama cha CUF kilitangaza kupinga matokeo na lile la wafuasi wa

 

chama hicho kuwapiga waandishi wa habari waliokwenda makao makuu ya chama hicho

 

eneo la Buguruni, Dar es Salaam. Kutokana na matukio hayo wananchi wamekuwa

 

wakijiuliza kuhusu chama hicho na viongozi wake.

"Hatukubali matokeo. Tutaanzisha janga la kitaifa iwapo tutaibiwa kura. CUF

 

tumeshinda tena kwa kishindo," hizo ni baadhi ya kauli zilizosikika baada ya

 

kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ambapo CCM iliibuka na ushindi wa jumla.

Katika uchaguzi huo, CCM imepata viti vya uwakilishi 30 na Civic United Front

 

(CUF) imeambulia viti 19 huku katika nafasi ya urais mgombea wa CCM Rais Amani

 

Abeid Karume akiwa ameibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake wa karibu Seif Sharrif

 

Hamad wa CUF.

Siku chache baada ya matokeo ya urais Zanzibara kutangazwa, Baraza Kuu la chama

 

cha CUF lilikutana makao makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam kwa ajili

 

ya kutoa tamko kuhusiana na uchaguzi huo.

Wakati 'vigogo' wa CUF wakiwa ndani wakiendelea na vikao, waandishi wa habari

 

kutoka vyombo mbalimbali waliokuwa, kama kawaida yao wakifuatilia mambo ili watoe

 

taarifa kwa umma, walianza kupata kipigo mithili ya wezi.

Matukio hayo na mengine, yamewaacha watu wakijiuliza maswali mengi kuhusu

 

uchaguzi na hatma ya Tanzania kutokana na mwenendo ulioonekana baada ya uchaguzi

 

wa Zanzibar kukamilika.

Kwa kuwa ni haki ya kila mtu kuzungumza yale anayoyaona yanafaa ili mradi havunji

 

sheria na taratibu zilizopo, nami nitalonga, kwani hiyo ni haki yangu.

Baada ya uchaguzi huo kumalizika, watu, vikundi na nchi mbalimbali zilitoa

 

maelezo yao kwa jinsi walivyoona uchaguzi wa Zanmzibar ulivyokwenda. Nchi na watu

 

wengi walisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki lakini wachache wakiongozwa

 

na Marekani walisema vinginevyo.

Kutokana na kauli ya ubalozi wa Marekani kulijitokeza watu mbalimbali waliowaunga

 

mkono na wengine kuwapiga, nilikuwa mmojawapo wa waliowapinga na nilieleza sababu

 

zangu hivyo sina haja ya kuzitaja tena. Lakini kama tukifuata misingi ya

 

demokrasia ambayo inatoa nafasi ya ushindi kwa walio wengi, kundi la Marekani na

 

wenzake wameshindwa!

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 nilipata bahati ya kuwepo Zanzibar ambapo kwa

 

kiasi kikubwa nilishuhudia na kuzungumza na watu mbalimbali kuhusiana na siasa za

 

CUF.

Yupo bwana mmoja (jina namhifadhi) alisema katika siku zijazo chama cha CUF

 

kitapoteza umaarufu na hatimaye kusambaratika kabisa kwa kuwa kimekuwa kikiwapo

 

matumaini makubwa wafuasi wake kuliko hali halisi ilivyo.

Baada ya matukio ya hivi karibuni, nilikumbuka kauli ya bwana huyo na nina imani

 

chama hicho kitapoteza umaarufu na hatimaye kusambaratika kabisa. Lakini baada ya

 

matukio ya hivi karibuni kuna kila dalili sasa CUF itakwenda na maji.

Picha inayojengeka sasa kwa jamii ni kuwa CUF ni chama cha watu wenye vurugu na

 

ambao wana malengo binafsi ambayo ni zaidi ya siasa za kawaida kwa maana hiyo na

 

kwa malezi tuliyopewa Watanzania ya kupenda amani na utulivu kuwa mwanachama wa

 

CUF ni kama kuamua vurugu. Je kwa malezi yetu nani atakubali kuwa mwanacahama wa

 

chama hicho?

Inashangaza kuona CUF wanakataa kukubalia kushindwa katika uchaguzi wa Zanzibar

 

ili hali wanajua nguvu walizonazo sio kubwa kama za CCM ambayo katika kipindi

 

chote imekuwa mstari wa mbele kujiimarisha katika maeneo mbalimbali.

Akihutubia mikutano ya kampeni kabla ya kampeni, mgombea uraia wa Tanzania

 

kupitia CCM Jakaya Kikwete alikuwa akisisitiza kuwa vyama vya upinzani hasa

 

Zanzibar vilianza kuona dalili za kushindwa ndiyo maana wafuasi wake walikuwa

 

wanabeba mawe kwenye malori.

Kikwete alisema vyama ambavyo vimeanza kutoa matusi majukwaani dhidi ya CCM ni

 

dalili kuwa vimekata tamaa ya kupata ushindi na kuwa vile ambavyo vinajihusisha

 

na kuzomea ni sawa na kukubali kushindwa. Alisema siasa si kutukana wala kuzomea.

 

Siasa ni hoja.

Kikwete aliwasisitiza wananchi kuwa amani na utulivu wa Tanzania hautokani na

 

hulka bali misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa TANU na ASP na hatimaye CCM

 

waliosisitiza umoja na mshikamano wa kitaifa.

Alitanabahisha kuwa tangu mwanzo viongozi wa CCM wangeendekeza ubaguzi wa rangi,

 

ukabila, chuki kati ya kabila na kabila au ugawaji wa rasilimali kutokana na

 

maeneo, nchi ingejaa vurugu.

CUF ikumbuke na kutambua kuwa kwa misingi ya kauli za Kikwete, ambazo Watanzania

 

wengi wanakubaliana nazo uwezekano wa kushinda Zanzibar ulikuwa mdogo kwa kuwa

 

badala ya kuashiria amani na utulivu, chama hicho kilijikita kwenye ubabe zaidi.

 

Chukulia mfano kauli ya kuwataka wafuasi wa CUF wasikae mbali na vituo baada ya

 

kupiga kura, iliashiria nini? Achilia mbali kauli mbiu za wanaumeee, mapanga na

 

ngangarii!

Pia kuna propaganda zinazopandikizwa hivi sasa na hata kwa baadhi ya wana habari

 

kuwa siku ya kupiga kura watu kwa makundi walikuwa wakipelekwa kwenye vituo vya

 

kupiga kura na kufanya hivyo bila hatua zozote kuchukuliwa. Inashangaza.

Hivi pamoja na teknolojia ya habari kupiga hatua kubwa mbele, alikosekanaaliyeona

 

hilo na kupiga picha hasa zile za televisheni, ukitilia maanani walikuwepo wana

 

habari wengi hata wale wa kutoka nje ya nchi ambao sasa CUF mmedai ndiyo

 

mnawaamini zaidi ya wa hapa nchini!

CUF imefika wakati wa kuamua kama ni kufanya siasa na ifanyike kwa njia ya amani

 

na utulivu, ujanja ujanja na kuwajaza matumaini yasiyokuwepo wafuasi wenu

 

hautawafikisha mbali. Mwanzo wa mwisho CUF huenda ukawa baada ya uchaguzi mkuu na

 

tusubiri tuone.

Kwa maana halisi ya kamusi ya kiswahili neno 'kivuli' lina maana ya giza

 

linalofanywa na kitu kuwa mbele ya mwanga. Lakini pia kivuli ina maana kumfanyia

 

mtu mambo ya kumdhuru na kumuendea kinyume na hali wakati mbele ya macho yake

 

unamuonyesha kuwa ni mwema. CUF mmeshindwa kwa kivuli chenu wenyewe.

 

Mafunzo kuhudumia wagonjwa wa majumbani yanahitajika

Na Rodrick Makundi, Moshi

MAFUNZO kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa majumbani yanahitajiwa zaidi ili

 

kuwezesha ubora wa huduma za kiafya kwa wagonjwa hao.

Kutokana na hali hiyo, serikali imeshauriwa kutoa mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa

 

wa majumbani hasa wenye virusi vya ukimwi, ikilinganishwa na idadi kubwa ya

 

wagonjwa hao wanaopatiwa huduma majumbani mwao.

Akiwakabidhi vyeti wahudumu wa afya wapatao 26, waliohitimu mafunzo yao ya huduma

 

za afya katika hospitali mbalimbali mkoani hapa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa

 

Kilimanjaro, Hubert Bwana alisema ametoa ushauri huo kwa serikali ili kuona

 

uwezekano wa utoaji wa mafunzo hayo kwa wataalamu wa afya walio karibu na jamii.

Alisema hivi sasa idadi ya wagonjwa wa ukimwi mkoani hapa imekuwa kwa kasi hali

 

inayosababisha wagonjwa wengi kupatiwa huduma majumbani kutokana na wingi wa

 

wagonjwa katika vituo vya afya na hospitalini.

Akitoa takwimu za wanaopima damu, Mganga Mkuu alisema kuwa kila watu 100, tisa

 

wamekutwa na virusi vya ukimwi, hali ambayo inaashiria kukua kwa ongezeko la

 

wagonjwa wa ukimwi.

Kwa mujibu wa takwimu wagonjwa 650 wa ukimwi wanapatiwa tiba katika hospitali ya

 

mkoa ya Mawenzi, huku wengi wao wakirejeshwa majumbani ili kupunguza msongamano

 

unaokuwepo.

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Mildmay International lililoendesha mafunzo

 

hayo, Lightness Kaale amesema lengo la mafunzo ni kuiwezesha jamii kupata mafunzo

 

ya utunzaji wa wagonjwa wa ukimwi majumbani.

Shirika hilo hadi sasa limetoa mafunzo kwa wauguzi 1000 tangu kuanzishwa kwake

 

mwaka jana hapa nchini, zikiwa zimetumika sh. milioni 178 katika utaoji wa

 

mafunzo hayo.

Wauguzi waliopata mafunzo na waliohitimu mafunzo hayo ni kutoka katika hospitali

 

za Kilema, KCMC, Kibosho, Marangu, Mwika, Umbwe na Mawenzi mjini hapa.

 

UVCCM yakata wananchi kuiadhibu CUF kwa kuinyima kura Desemba 14

Ni kwa wafuasi wake kuwapiga waandishi wa habari

Na Mwandishi Wetu

UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) umelaani kitendo kilichofanywa na wafuasi wa CUF

 

cha kuwashambulia waandishi wa habari na umewaomba wananchi kukiadhibu chama

 

hicho kwa kukinyima kura kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Desemba 14, mwaka

 

huu.

Tamko hilo la UVCCM lilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wake, Amos Makala

 

alipozungumza na viongozi wa Umoja huo wa ngazi mbalimbali kuanzia matawi

 

wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Makala alisema kitendo kilichofanywa na wanachama na wafuasi hao mbele ya Ofisi

 

za Makao Makuu ya chama chao, Buguruni, Dar es Salaam kimeudhihirishia umma

 

kwamba hakistahili ridhaa ya wananchi kuliongoza taifa.

Alisema kitendo cha kuwapiga, kuwajeruhi na kuharibu vifaa vya waandishi

 

wakitekeleza majukumu yao ya kutafuta habari siyo tu kimewanyima wananchi uhuru

 

wa kupata habari ni uvunjaji wa sheria za nchi na kimedhihirisha hawaitakii amani

 

Tanzania.

Makala pia amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa uamuzi wao wa Oktoba 30, mwaka

 

huu wa kuichagua CCM kuendelea kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano

 

ijayo. Katika uchaguzi huo wananchi hao walimchagua kwa kura nyingi Amani Abeid

 

Karume kuwa Rais na wagombea wa majimbo 30 wa CCM kati ya 49 kuwa Wawakilishi.

Kwa uamuzi huo wa Wazanzibari, Makala alitoa mwito kwa Watanzania wote kuwa

 

matokeo hayo yawe changamoto kwao kwa kuendelea kuichagua CCM katika Uchaguzi

 

Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Desemba 14, mwaka huu.

Uchaguzi Mkuu wa Desemba 14, mwaka huu, ambao Watanzania wote wa Bara na Zanzibar

 

watapiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na

 

Madiwani.

Aliwataka wana-CCM kuendeleza zaidi umoja, amani na mshikamano, hususan katika

 

kipindi hiki cha kampeni kwa kushindana na vyama vingine kwa hoja kwa kunadi sera

 

na ilani ya CCM badala ya kutumia nguvu, ghilba na vitisho kama vinavyofanya

 

baadhi ya vyama vya upinzani.

Mapema, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Kinondoni, Aaron Mwaikambo akimkaribisha

 

Makala kuzungumza na vijana hao alitoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi

 

kwenda kupiga kura Desemba 14, mwaka huu.

Mwaikambo alisema Desemba 14 itakuwa Jumatano ambayo serikali imeamua kuwa siku

 

ya mapumziko, hivyo wananchi hawana sababu za kushindwa kwenda kupiga kura

 

isipokuwa kwa wagonjwa mahututi.

Alisema hata kwa waumini wa dini ambao wengi wao siku za Ijumaa, Jumamosi na

 

Jumapili ni siku mahsusi kwa sala hawatakuwa na kizuizi cha kuwafanya kushindwa

 

kwenda kupiga kura.

 

 

Klabu za waandishi wa habari zatakiwa kuanza kuitenga CUF

Na Solomon Mwansele, Mbeya

KLABU za Waandishi wa habari nchini zimetakiwa kuacha kushirikiana na chama cha

 

CUF na kukataa mialiko yao.

Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na rais wa Umoja wa

 

Klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC) Ulimboka Mwakilili.

Rais huyo wa UTPC alisema CUF wasusiwe hadi hapo watakapokuwa wametekeleza yote

 

yaliyoagizwa na vyama vya waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari

 

(MOAT), asasi za kisheria na wadau wengine wote waliopatwa na majonzi.

Katika taarifa hiyo, Mwakilili alisema CUF wanatakiwa wawajibike kikamilifu

 

kugharamia matibabu ya waandishi hao na kulipa fidia zote za vifaa na mali

 

zilizopotea na athari mbalimbali.

Imeongeza kuwa viongozi wa CUF wamekuwa wakipanda mbegu mbaya za fujo, migogoro

 

na vurugu kwa wanachama wake kwa muda mrefu kwa kupinga juhudi zote zinazofanywa

 

hadi wao waingie madarakani na mbegu hiyo imeanza kuzaa matunda kwa madhara

 

yanayojitokeza sasa.

"Tunauagiza uongozi wa CUF ukubali na kukiri hadharani, kujutia na kutoa

 

ushirikiano wote kwa vyombo vya dola kuwasaka walioshiriki kutenda kitendo hicho

 

cha kinyama na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria," alisema Mwakilili katika

 

taarifa yake.

Iliongeza kuwa CUF wameendelea kuwaita na kuwatumia waandishi wa habari wakati

 

wote kwa kufikisha taarifa za mafanikio yao na matatizo kila inapobidi kwa vyombo

 

vya kitaifa na kimataifa na mambo yao kufanikiwa, lakini sasa wanawafanya

 

waandishi kuwa 'mbuzi wa kafara'.

Mwakilili alisema uongozi wa kitaifa wa UTPC kwa kuungana na wanachama wake nchi

 

nzima kwa uchungu na masikitiko makubwa unapokea kilio cha waandishi wa habari

 

wote kwa huzuni kubwa.

 

Hawa wanasakwa na Polisi Dar

Wanadaiwa kuhusika na matukio ya ujambazi kwenye benki

Na Mwandishi Wetu

POLISI imewatangaza watu watatu kama watuhumiwa sugu wa matukio ya kijambazi,

 

ikiwemo kwenye benki na sasa inawasaka kwa udi na uvumba.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Alfred Tibaigana, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni

 

Sixtus Alfred Ngowi (42), mkazi wa Dar es Salalaam, Abulkarim Mongi (37) ambaye

 

makazi yake hayajulikani na Sadik Fatee, mkazi wa Muheza ambaye umri wake

 

haujajulikana.

Alisema watuhumiwa hao wote wanaonekana mara kwa mara katika miji ya Dar es

 

Salaam, Arusha, Nairobi na Moshi, wanahusishwa na wizi wa pesa sh. bilioni 1.6

 

kutoka kampuni ya Security Group, ambayo wafanyakazi wake na watuhumiwa wengine

 

jumla yao 18 wana kesi inayoendelea katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu.

Polisi pia inamsaka mke wa Ngowi, ambaye hakutaja jina lake, kutokana na

 

kuhusishwa ma tuhuma za mumewe. Tibaigana alisema kuwa, mtuhumiwa Ngowi,

 

anamiliki kiwanda cha kutengeneza vinywaji baridi kiitwacho Cold Cap cha jijini

 

Dar es Salaam.

Alifafanua kuwa, mwanamke huyo anahusishwa na kesi hiyo, kwani kasha la fedha

 

lililoibwa kwenye kampuni ya Security Group, lilikutwa nyumbani kwake na mwanamke

 

huyo amejificha pasipojulikana na amekuwa akitoa taarifa kwenye ofisi mbalimbali

 

kwamba anatishiwa kuuawa. Hakufafanua.

Kamanda Tibaigana, alitoa wito kwa wananchi kuvifahamisha vyombo vya dola ili

 

watuhumiwa hao ambao kwa kiasi kikubwa wanahusishwa na matukio ya wizi kwenye

 

benki mbalimbali jijini Dar es Salaam, wakamatwe na kufikishwa mwenye vyombo vya

 

sheria.

Wakati huo huo, juzi jioni saa 1.30 majambazi manne yakiwa na silaha mbali

 

yalivamia na kujeruhi, pia kupora pesa na mali zenye thamani ya zaidi ya sh.

 

milioni mbili huko Tabata Segerea, Dar es Salaam, eneo la Ugombolwa.

Tukio hilo ni mwendelezo wa mikasa ya kijambazi, Tabata kwani ni siku moja tu

 

kabla ya hilo, kulifanyika uporaji wa namna hiyo katika eneo jirani la

 

Kilimanjaro, huko Tabata Chang'ombe majira ya saa 2.30. Tukio la Tabata Segerea,

 

lilitokea saa 1.30.

Kamanda Tibaigana amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kati ya saa 1.30 na saa

 

2.00 na kusema uchunguzi mkali unaendelea kuwasaka watuhumiwa hao, huku mtu

 

mmoja, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiuguza majeraha ya

 

kichwa.

Kwa mujibu wa Tibaigana, majeruhi aliyelazwa na Charles Batenga. Mwingine, Faiza

 

Batenga (30), alitibiwa majeraha na kuruhusiwa.

Mwandishi wa habari hizi aliyekuwepo katika eneo la tukio, alishuhudia maduka

 

yote huko Tabata Segerea yakiwa yamefungwa saa 2.30, tofauti na kawaida ambapo

 

baadhi huwa wazi hadi zaidi ya saa 5.00 usiku.

Akisimulia mkasa huo wa juzi, Tibaigana alisema kuwa majira kati ya saa 1.00

 

usiku na saa 2.00 usiku majambazi hayo manane yakiwa na panga na nyundo yalianza

 

kuvamia dukani kwa Faiza na yakampora pesa taslimu sh. 300,000 na kadi za simu

 

zenye thamani hiyo hiyo.

Baada ya hapo, yalihamia nyumbani kwa mkazi mwingine aitwaye Daudi Mboneka ambapo

 

walimkuta mkewe ambaye hakutajwa jina na kupora sanduku dogo (briefcase) yenye

 

nyaraka mbalimbali na simu ya mkononi.

Kwa mujibu wa Tibaigana, safari ya majambazi hayo ilihamia nyumbani kwa Leticia

 

Mwijage, aliyeporwa pesa taslimu sh. milioni 1.7. Safari ya uporaji iliishia

 

dukani kwa Ashery Kazimoto ambako dukani kwake, wateja waliokuwa wakiburudika kwa

 

kinywaji waliporwa pesa taslimu sh. 80,000 na simu ya mkononi.

Aidha, katika hatua nyingine jana asubuhi watu wenye hasira walimuua na kumchoma

 

moto kijana mmoja wa kiume anayetuhumiwa kuwa kibaka, huko Tabata Segerea, jirani

 

na kituo kipya cha polisi.

Kwa mujibu wa habari kutoka eneo la tukio, mkasa huo ulitokea saa 4.00 asubuhi

 

baada ya kijana huyo kukurupushwa akiiba nguo zilizoanikwa nyumbani kwa mtu mmoja

 

Mzungu, mkazi wa eneo hilo. Maiti iliendelewa kubakia mahali hapo hadi saa saa

 

7.40 mchana polisi walipofika kuichukua.

Katika tukio la Alhamisi usiku, majambazi yalipora pesa sh. 70,000 eneo Tabata,

 

Kilimanjaro wakitishia kuvunja chupa iliyotoa mlio kama bunduki na kufanikisha

 

uporaji wao.

 

CUF wanavunja Katiba - Karume

  

Na Khatibu Suleiman, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, amesema kitendo cha wajumbe wa Baraza la

 

Wawakilishi kutoka chama cha CUF kususia uzinduzi wa Baraza hilo pamoja na

 

kutomtambua yeye ni uvunjaji wa Katiba ya nchi.

Alisema mbali ya kuvunja Katiba, lakini pia ni tabia ya chama hicho kuendelea na

 

kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.

Rais Karume alisema hayo jana alipolihutubia Baraza jipya la Wawakilishi,

 

lililochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30 mwaka huu. Alikuwa

 

akilizindua Baraza hilo.

Katika uchaguzi huo Rais Karume alishinda kiti cha urais, wakati chama chake cha

 

CCM kilishinda viti 30 katika Baraza hilo.

Chama cha CUF ambacho kinadai hakitambui matokeo ya uchaguzi huo, kilishinda viti

 

19 na mgombea wake wa urais, Seif Shariff Hamad, alishindwa na Karume.

Rais alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha tano

 

A(1), kinaeleza kwamba kutakuwa na mamlaka ya nchi ambayo ni serikali pamoja na

 

Baraza la Wawakilishi, ambapo yeye rais ni sehemu ya Baraza hilo.

"Rais wa Zanzibar ni sehemu ya Baraza la Wawakilishi hivyo huwezi kumtenganisha

 

na Baraza la Wawakilishi," alisema Karume ambapo alionesha kushangazwa na tabia

 

ya wajumbe wa CUF kususia Baraza hilo ambapo juzi waliapa kulinda na kuitetea

 

Katiba ya Zanzibar, pamoja na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Karume alisema kitendo cha wajumbe wa chama cha CUF kususia kuingia katika Baraza

 

la Wawakilishi kinaonesha kwamba CUF hawapo tayari kujiheshimu wala kuheshimiwa,

 

na kuwaheshimu watu wengine.

Alisema wakati umefika kwa viongozi wa chama cha wananchi CUF kujenga tabia ya

 

kuheshimu maamuzi ya wengi, kwani ndio mfumo unaokubalika katika nchi zinazofuata

 

utawala wa kidemokrasia na Katiba ikiwemo Zanzibar.

Mapema, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alisema hana taarifa

 

yoyote kuhusu kutohudhuria kwa wajumbe wa kambi ya upinzani ya CUF katika kikao

 

cha jana, licha ya kuwapa taarifa ya ujio wa rais na shunguli za uzinduzi wa

 

Baraza hilo.

"Sina taarifa kwa nini wajumbe wa CUF hawakuja katika uzinduzi wa kikao hiki...

 

lakini nitafuatilia kwa makini kujua sababu ni zipi?" alisema Kificho, muda mfupi

 

kabla ya kumkaribisha Rais Karume kulizindua Baraza hilo.

Rais Karume katika hotuba yake alisema uchaguzi mkuu wa Oktoba 30 umekwisha kwa

 

Chama cha Mapinduzi kimekabidhiwa dola na wananchi, na sasa kazi kubwa iliopo

 

mbele yetu ni kuleta maendeleo, umoja na mshikamano wa wananchi.

Alisema serikali yake itaendelea na kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika visiwa

 

vya Unguja na Pemba bila ya kujali itikadi za kisiasa, huku utekelezaji wa ilani

 

ya Chama cha Mapinduzi itakuwa ndiyo dira ya mafanikio yote hayo.

"Maendeleo ya nchi hayana itikadi ya kisiasa...wananchi wanataka maendeleo na

 

siyo siasa tu," alisema Karume ambapo alielezea mafanikio yake mbali mbali katika

 

utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika kipindi cha

miaka mitano iliyopita.

Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, alielezea muelekeo wa serikali yake katika

 

kipindi cha miaka mitano ijayo cha 2005-20010, ambapo alisema suala la

 

uimarishaji wa sekta binafsi utapewa kipaumbele ili kuongeza ajira kwa wananchi

 

wa Unguja na Pemba.

Alisema suala la kuimarisha miundo mbinu ya barabara, sekta ya nishati pamoja na

 

maji safi na salama Unguja na Pemba, litapewa kipaumbele ili kuona wawekezaji

 

wengi wanajitokeza kuwekeza katika sekta na miradi mbali

mbali ya maendeleo.

Karume alisema tayari kitengo cha uwekezaji cha ZIPA kimezidi kuimarishwa ili

 

kuwavutia wawekezaji zaidi kuwekeza katika maeneo mbali mbali ikiwemo kuondosha

 

urasimu kwa wawekezaji katika kuwekeza.

Alisema mpango wa kupunguza umasikini MKUZA unaendelea na unafanya kazi katika

 

visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo wananchi wameweza kushirikishwa kikamilifu

 

katika utekelezaji wake bila ya kujali itikadi za kisiasa.

Alisisitiza na kuutaka upande wa upinzani wa chama cha CUF kujali na kuweka mbele

 

maslahi ya taifa kwa ajili ya kuleta maendeleo na sio ubinafsi wa watu wachache,

 

ambao hauwezi kuleta tija na maendeleo ya nchi.

 

Wana-CCM wote ni wagombea katika uchaguzi mkuu-Mangula

Na Bashir Nkoromo, Makambako

KATIBU Mkuu wa CCM, Philip Mangula, amesema wanachama wa CCM wote ni wagombea na

 

kuonya kuwa mwana-CCM atakayethubutu kutompigia kura mgombea wa CCM atakuwa

 

amejinyima kura yeye mwenyewe.

Alisema hayo jana kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya ndani aliyofanya na

 

wanachama na viongozi wa CCM katika mji mdogo wa Makambako, jimbo la Njombe

Kaskazini mkoani Iringa.

"Ushindi wa mgombea urais, ubunge au udiwani kupitia CCM ni wa wanachama wote wa

 

CCM, hivyo kwa sasa wagombea ni ninyi wana-CCM. Ni lazima muhakikishe kila

mmoja wenu anapigia kura mgombea wetu kwa kuwa huyo mgombea ni mwakilishi tu,

 

wagombea hasa ni ninyi wanachama," alisema Mangula.

Alisema CCM inayo hazina kubwa ya wanachama hivyo jukumu alilonalo kila

 

mwanachama halisi ni kuhakikisha anatumia wakati huu uliobaki kuwashawishi wasio

wanachama kuipigia kura CCM, ili ipate ushindi mnono zaidi kuliko inavyotarajiwa.

Mangula aliwaasa wanachama wa CCM wasighilibike na kuamua kutompigia kura mgombea

 

wa CCM, eti kwa sababu ya ugomvi wa binafsi kati yake na kiongozi mmoja tu wa

chama.

"Ukigombana wewe binafsi na kiongozi mmoja wa chama usikiadhibu chama, hayo ni

 

makosa kwa kuwa utakuwa umejiadhibu na wewe kama mwanachama," alisema

Mangula.

Aliwataka wana-CCM kuongeza mshikamano wao katika chama badala ya wengine

 

kuendelea kukumbatia hadi sasa wagombea walioachwa katika kura za maoni.

 

Alifafanua kuwa walioachwa sasa si wagombea, wagombea ni waliopitishwa.

"Halmashauri Kuu inaheshimu sana maoni yenu mliyotoa katika kura za maoni, lakini

 

hailazimishwi kuyafuata kwa kuwa yenyewe ndiyo yenye uamuzi wa mwisho," Mangula

 

alikumbusha na kuongeza: "Sisi hufuata vigezo muhimu kuona kama mgombea anatosha

 

kwa kuwa taarifa za muhusika huwa tunaanza kuzikusanya mara tu anaponuia kuchukua

 

fomu ya kuomba".

"Mwanachama mara tu akitamka nataka kuchukua fomu kuwania nafasi fulani, basi

 

sisi mara moja tunafungua faili na kuanza kukusanya mambo yake yote. Kwa hiyo

 

hatumuonei mtu tunapomwacha hata kama alikuwa ameongoza katika kura za maoni,

 

wakati mwingine

tunaweza kuwa tumemwacha kutokana na sababu pengine zenye maslahi hata na

 

aliyeomba," alisema.

Kuhusu upinzani, Mangula alisema kwa sasa chama cha CUF kichwa chake kimeshakatwa

 

huko Zanzibar, huku Bara imebaki mikia tu mfano wa pweza, kwa hiyo

kilichobaki ni kumalizia tu hapo Desemba 14, mwaka huu.

Mangula alisema wananchi hata wale wasiokuwa wana-CCM hawana sababu ya kukichagua

 

CUF kwa kuwa tayari wamekuwa wakishuhudia au kusikia jinsi kilivyo cha

shari na chenye kutamani mauaji.

Alitoa baadhi ya mifano ya mauaji yaliyokwishatokea yakihusishwa na chama hicho

 

kuwa ni yale ya kuchinjwa kwa polisi huko Pemba wakati wa uchaguzi wa mwaka 2000

na mfuasi mmoja wa CCM kuuawa kwa nyumba yake kuchomwa moto Manzese na vitendo

 

walivyofanya hivi karibuni vya kupiga waandishi wa habari kwenye ofisi zake mjini

 

Dar es Salaam.

Mangula alisema, ukiacha CUF vyama vingine ndiyo hoi kabisa kwa sababu ndiyo

 

kwanza vinajikongoja kwa kuwa katika maeneo mengi havina hata anuani ya kuweza

kuvipata ukihitaji.

Mangula ambaye tangu juzi bado yupo katika wilaya ya Njombe alikagua hali ilivyo

 

katika majimbo, baada ya mkutano aliofanya mjini Makambako alifanya pia mkutano

wa ndani katika kata ya Mtwango.

Kabla ya kuzungumza na wananchi, Mangula alifungua shina la Wakereketwa la

 

Mtwango ambako aliwataka wana-CCM kuyatumia mashina kote nchini kutafakari

namna CCM itakavyoweza kuibuka na ushindi wa kihistoria katika uchaguzi mkuu.

Mapema, Katibu wa CCM wa mkoa wa Mbeya, Costantine Malyagira na Mwenyekiti wake

 

Tasili Mgoda walimwambia Mangula kwenye mikutano hiyo kwamba hali katika majimbo

 

hadi sasa inaashiria CCM kupata ushindi mkubwa na pia wanachama wanasubiri

 

uchaguzi kwa hamu.