UHURU 14.10.2005

 

John Cheyo amfuata Kikwete hotelini kumsalimu

Na Dunia Mzobora, Bariadi

MWENYEKITI wa UDP, John Cheyo, jana alikwenda kumsalimia mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete na kumponda mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Freeman Mbowe kwamba utumiaji wa helikopta katika kampeni zake unamkosesha kuona matatizo mengi ya wananchi.

Kwa upande wake, mgombea urais kupitia TLP, Augustine Mrema, amewataka wananchi wasimchague Mbowe “kwa kuwadanganya na helikopta”.

Cheyo, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Bariadi Magharibi kwa tiketi ya chama chake, alitoa kauli yake alipokwenda kumsalimia Kikwete katika hoteli ya FM Complex, ambako alilala.

Mwenyekiti wa UDP alisifu mbinu za Kikwete za kutumia gari kuwa ni nzuri na bora zaidi kwa kuwa zinampa fursa ya kushuhudia kwa kina matatizo ya wananchi na nchi kwa jumla katika maeneo mbalimbali.

Cheyo alisema kwa kutumia gari baadhi ya matatizo makubwa ambayo Kikwete anapata fursa ya kuyaona ni ubovu wa baadhi ya barabara, shida ya maji, ukame na pia anapata fursa ya kusimama katika maeneo mengi na kuzungumza na wananchi kujua matatizo yao akiwa njiani, hivyo kuweza kupanga mikakati ya kuyatatua akipata Urais.

"Nimefurahishwa na kampeni za Kikwete kutumia barabara...hiyo inampa fursa ya kujua matatizo ya wananchi kiundani kuliko Mbowe" alisema na kuongeza: “Kwa helikopta unatua mji hadi mji.”

Cheyo alisema Mbowe hawezi kutambua kwa undani matatizo ya wananchi kwa sababu helikopta inamfanya asikutane na wananchi wengi.

Akieleza sababu zilizomfanya kwenda kumsalimia Kikwete hotelini, Cheyo alisema amefanya hivyo kwa kuwa ni utamaduni mzuri ambao hata yeye aliwahi kufanyiwa na mbunge wa Sumbawanga, Paul Kimiti alipokwenda huko kufanya kampeni za kusaka kura wakati akiwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Cheyo alisema akiwa Sumbawanga, Kimiti licha ya kuwa ni kada wa CCM, asubuhi alikwenda kumsalimia alikofikia na kwamba jambo hilo hakulisahau kwa kuwa ni zuri linalopaswa kufanywa na viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa.

Kuhusu fujo zilizofanywa na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa UDP, Cheyo alilaani tukio hilo na kueleza kwamba anaamini sheria itachukua mkono wake ili kuwachukulia hatua waliohusika.

Katika fujo hizo, gari la msafara wa Kikwete lenye anamba T 366 AJL aina ya Land Cruiser lilivunjwa kioo cha pembeni, huku gari la aina hiyo lenye namba T362AJL lilipondwa ubavuni.

Hata hivyo, vurugu hizo yalifanyiwa magari hayo wakati yakipeleka waandishi wa habari sehemu ya kulala wakati tayari Kikwete akiwa ameshafika hotelini.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinyanga, Abdallah Msika alithibitisha kutokea vurugu hizo na kwamba kijana mmoja anayesadikiwa kuhusika amekamatwa.

Katika mkutano uliofanyika Bariadi, CCM ilipata wanachama wapya 312, kati yao 128 wakiwa ni waliovikimbia vyama vya upinzani.

Kutoka Kigoma, Fadhili Abdallah, anaripoti kuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwanga Community Centre, mjini Kigoma juzi, Mrema aliwaasa wananchi wasifanywe kama watoto wadogo kwa kudanganywa na helikopta kwani watakujajuta baadaye iwapo watampa kura mgombea huyo na helikopta yake.

Mrema alisema kuwa kama ni helikopta chama chake kinaweza kununua mbili na malori 20 kwa sababu uwezo wa kufanya hivyo wanao, lakini wameamua kufanya kampeni kwa kutumia magari ili kuwafikia Watanzania na kukaa nao wakaongea vizuri.

 

Mkapa: Katika uchaguzi tushindane bila kupigana

Na Maura Mwingira, Butiama

RAIS Benjamin Mkapa amewataka wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kushindana bila kupigana ili kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye katika uhai wake alisisitiza sana hali hiyo.

Alitoa rai hiyo jana alipokuwa akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Butiama, muda mfupi kabla ya kufungua barabara ya lami ya Kiabakari hadi Butiama, mkoani Mara, yenye urefu wa kilomita 12 iliyogharimu sh. bilioni 2.6.

"Siwezi kumaliza salamu zangu bila kuunganisha hoja hii ya umoja wa taifa hili la upendo na udugu aliokuwa akiueleza Baba wa Taifa bila kuwataka wananchi kuwa tunapokwenda katika uchaguzi tuonyeshe kweli tunamuenzi Baba wa Taifa kwa kushindana bila kupigana kama alivyotuasa katika mfumo huu wa vyama vingi vya siasa," alisisitiza Rais.

Alisema kuwa kunaanza kuzuka vurugu za hapa na pale na kwamba hali hiyo si ya kumuenzi vizuri Baba wa Taifa.

"Wanandugu mnagombana kwa sababu gani? Tunawania nafasi ya kuwaongoza wananchi, kwa nini tupigane? Tunawania nafasi ya kuwa mstari wa mbele katika kuchangia miradi mbali mbali ya maendeleo, fikra za kuwanasua wananchi kutokana na umaskini, kwa nini tupigane? Kwa nini damu imwagike?” alihoji Rais Mkapa.

Alisema amekuwa akifuatilia kwa makini sana kampeni za uchaguzi nchini Liberia, nchi ndogo, maskini yenye taabu kabisa ambayo wananchi wake wamepigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi, lakini baada ya kupata mtazamo mpya katika mfumo wa vyama vingi vya siasa na msingi wa mustakabali wa taifa lao, wameweza kufanya uchaguzi katika hali ya amani na utulivu.

Katika uchaguzi wa Liberia, alisema, hakuna aliyepigwa mawe, wala hakuna aliyepigwa mshale wala kupoteza maisha.

"Halafu nikiwasha redio yangu nasikia Watanzania wameanza kupigana mawe, wameanza kurushiana mishale mpaka inapasa vyombo vya amani vitumie nguvu ya dola. Wale Watanzania, watoto na wajukuu wa Mwalimu Julius Nyerere mnataka kuleta chuki na uhasama, vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya uchu wa madaraka na si kuwania nafasi ya kuwatumikia wananchi, itakuwa aibu sana," alisema Rais kwa masikitiko.

"Kwa hiyo natoa rai kwa Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa ambaye sera zake ni kuwa na utaifa, umoja, upendo, udugu na Watanzania, kuheshimiana, kudai haki, lakini kuheshimu haki za wengine vile vile, na kwa kweli kuwasaidia wengine wafurahie haki. Tushindane bila kupigana tunapoelekea kwenye uchaguzi tarehe 30 mwezi huu," alisisitiza Rais.

Aliwahimiza wananchi wa Butiama kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuendelea kuchangia nguvu zao katika uboreshaji wa elimu na ujenzi wa makazi ya kisasa, mambo ambayo Mwalimu aliyapa umuhimu wa pekee wakati wa uhai wake.

Katika kipindi chake cha uongozi, alisema, serikali yake ilijitahidi sana kuchangia maendeleo ya kijiji hicho chenye historia ya kipekee nchini na Afrika kwa ujumla na kuwa kazi ya kukisaidia kijiji hicho inaendelea na kwamba atamshauri Rais ajaye kuhakikisha kuwa serikali inaendelea kukisaidia.

Alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mama Maria Nyerere na wanakijiji hao kwa kuonyesha moyo wa ukarimu kwa watu mbalimbali wa ndani na nje ambao wamekuwa wakikitembelea kijiji hicho, na hasa makazi ya Baba wa Taifa.

Kabla ya kuzindua barabara hiyo, ambayo imejengwa kwa fedha za serikali, Rais Mkapa na mkewe waliweka mashada ya maua kwenye kaburi la Baba wa Taifa, ambapo pia ilisomwa sala fupi iliyoongozwa na Padre Andrcej Madry wa parokia ya Butiama.

Pia waliweka mashada ya maua kwenye kaburi la Chifu Edward Wanzagi Nyerere.

Mama Maria alimkabidhi Rais Mkapa zawadi ya ng'ombe 11 wakati wanakijiji wa Butiama walimkabidhi ng'ombe 13.

Awali, akimkaribisha Rais kusalimiana na wananchi, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli pamoja na kuelezea juhudi za serikali katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami nchi nzima, aliwaomba wananchi hao wachague wagombea wa CCM ili iweze kuendeleza mipango hiyo ambayo amesema vyama vingine hawana.

Alisema kuwa maendeleo yanaweza kuletwa na mtu yeyote yule, lakini maendeleo bora yataletwa na CCM peke yake.

Wananchi wa kijiji wameahidi kuitunza barabara hiyo ili ichangie katika kuupiga vita umaskini na kujiletea maendeleo yao.

 

 

Nyerere akumbukwa

LEO ni siku ya mapumziko kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Idara ya Habari (Maelezo), ilisema maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali, ikiwemo ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika kitaifa mkoani Singida.

Pia maadhimisho hayo yatahusisha misa za madhehebu mbalimbali zitakazotolewa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwalimu Nyerere alizaliwa mwaka 1922 na alifariki dunia Oktoba 14, 1999 akiwa katika matibabu katika hospitali ya St. Thomas mjini London.

Naye Lauden Mwambona, anaripoti kutoka Singida kwamba mkoa wa Singida leo unafanya misa maalum ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere itakayofanyika kanisa la Jimbo Katoliki la Singida na kuhudhuriwa na Rais Benjamin Mkapa kuanzia saa moja asubuhi.

Rais Mkapa aliwasili Singida jana jioni na kupokewa na viongozi wa CCM na serikali wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Halima Kasungu.

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara yake mkoani Singida, Rais atahudhuria misa hiyo itakayoongozwa na Askofu Desiderius Rwamo.

Ratiba hiyo inaonyesha pia kwamba baada ya misa Rais atakwenda uwanja wa maonyesho ambako zaidi ya washiriki 200 wanaonyesha bidhaa mbalimbali wanazotengeneza baada ya kuratibiwa na Shirika la Vinwada vidogovidogo nchini (SIDO)

Baadaye Rais Mkapa atakwenda kwenye sherehe za kilele cha mbio za Mwenge kwenye uwanja wa Namfua.

 

Sumaye azindua mtandao wa mawasiliano wa kukabili maafa

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Frederick Sumaye, amezindua mtandao wa mawasiliano yakiwemo ya radio, simu za dharura utakaoiwezesha ofisi yake kuwasiliana moja kwa moja na ofisi za wakuu wa mikoa yote na hospitali zikiwemo za rufani nchini ikiwa ni juhudi za kukabiliana na maafa.

Uzinduzi huo, ulifanyika katika Idara ya Maafa iliyoko chini ya Ofisi yake ikiwa ni sehemu za maadhimisho ya siku ya upunguzaji wa maafa duniani ambayo hufanyika kila wiki ya pili ya mwezi Oktoba.

Mtandao huo pia unahusisha mfumo wa kompyuta wa rasilimali za kukabili maafa na maktaba ndogo na direktori ya anuani za wadau muhimu katika kukabiliana na maafa.

Mawasiliano yatakayohusisha matumizi ya 'radio call' yatakuwa kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na mikoa 21, Wizara ya Afya, Mambo ya Ndani, Tamisemi na hospitali zote za Rufani ikiwemo Muhimbili, Bugando, KCMC na Mbeya.

Nyingine zilizoko kwenye mtandao huo ni hospitali za mikoa ya Dodoma, Morogoro, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Tabora, Bukoba, Iringa na Tumbi.

Akitoa maelezo ya mtandao huo, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Beatha Swai, alisema mtandao huo umegharamiwa na Serikali za Tanzania na Marekani kupitia mradi ya 'Kuimarisha Uwezo wa Tanzania Kukabiliana na Maafa' ambao ulibuniwa kufuatia tukio la ulipuaji wa bomu katika Ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam.

Tukio hilo, lililotokea mwaka 1998 lilisababisha maafa makubwa ikiwa ni pamoja na vifo watu 12 na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa licha ya uharibifu wa mali yakiwemo magari na majengo.

Alisema katika kukabiliana na maafa ya tukio hilo, Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Kimataifa la Maendeleo (USAID), lilitoa msaada wa dola za Marekani milioni 9.2 (sawa na sh. bilioni 9.2), ambazo pia zililenga katika kuimarisha uwezo wa taifa kukabiliana na maafa.

Kulingana na Beatha kati ya fedha hizo, sh. milioni 5 zilitumika kama msaada wa kibinadamu kwa waathirika ambapo sh. bilioni 2.8 katika ujenzi na ukarabati wa majengo yaliyobomolewa na sh. bilioni 5 kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na maafa.

Alisema kati ya hizo, sh. bilioni 2.2 zilitumika kununulia vifaa vya hospitali na sh. bilioni 2.8 kwa ajili ya mradi wa kujenga uwezo ikiwemo Idara ya Maafa na zingine milioni 7 zilikwenda Chama cha Msalaba Mwekundu ukiondoa zilizotumika kwa ajili ya uratibu.

Chini ya mradi huo, kilianzishwa kituo cha Kitaifa cha Mafunzo ya maafa katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu wa Majengo (UCLAS) ambacho hadi sasa kimetoa mafunzo kwa wakufunzi 500 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Akizungumza baada ya kuzindua mtandao huo, Sumaye alisema hizo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kukabiliana na maafa.

Pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kuepukana na maafa yanayotokana na uharibifu wa mazingira na amewataka wananchi kutumia wataalam katika masuala yakiwemo ya umeme ili kuepuka ajali zinazotokana na hitilafu za umeme.

Alisema kwa kutumia mtandao huo, wakuu wa mikoa wataweza kuwasiliana na kufikia maamuzi kama ya kusaidiana iwapo mkoa mmoja utakuwa umekumbwa na njaa na hivyo kupunguza mlolongo wa taratibu zisizokuwa za lazima.

 

 

 

Wakulima watahadharishwa kuwa makini na propaganda za wapinzani

Na Dunia Mzobora, Kisesa

WAKULIMA wametakiwa kuachana na propaganda ambazo zimekuwa zikitolewa na wapinzani eti CCM ikishinda katika uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa mwezi huu, itatoza kodi za mashamba.

Hayo yalisemwa juzi na mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika jimbo la Kisesa Wilayani Meatu mkoani Shinyanga.

"Nimekuwa katika Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kwa kiasi cha miaka 18 mfululizo, hatujawahi kuzungumza hilo hata siku moja," alisema Kikwete.

Kikwete alilazimika kutoa ufafanuzi huo kufuatia baadhi ya wapinzani hasa mgombea ubunge wa CHADEMA Erasto Tumbo kueneza propaganda kwamba CCM ikishinda itawatoza wakulima kodi za mashamba.

Kikwete alisema kauli hizo ni propaganda zisizo na msingi kwa kuwa jambo hilo halijawahi kuzungumzwa hata siku moja katika vikao vya CCM au serikali zake.

"Nimekuwa Waziri miaka 17, huko pia hatujawahi kuzungumzia jambo hilo" alisisitiza.

Aliwataka wananchi kumpuuza mgombea huyo wa CHADEMA na wenzake wanaoeneza uongo huo dhidi ya CCM na badala yake wawaadhibu wapinzani hao kwa kuwanyima kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwishoni mwa mwezi huu.

Kuhusu zao la pamba, Kikwete alisema analifahamu tatizo katika uzalishaji hususan katika upatikanaji wa mbegu bora na kwa wakati na kueleza kuwa akiwa rais atalisimamia tatizo hilo ahadi aliyoitoa pia wakati akihutubia katika jimbo la Kishapu na Maswa.

Alisema, Uganda hupata wastani wa mavuno ya pamba kiasi kilo 1,000 kwa hekta moja na kuhoji kwamba kama Uganda wanafanikiwa kwa nini ishindikane Tanzania.

Katika mkutano huo aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Meatu, Kimanga Jackson alirejea CCM pamoja na wengine 157 kutoka vyama vya upinzani.

Pia katika mkutano huo aliyekuwa meneja wa kampeni ya Erasto Tumbo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 1995 wakati huo akiwa UDP, Philip Charles naye alirejea CCM.

 

Maandalizi ya ujenzi barabara ya Minjingu-Babati yapamba moto

SERIKALI imesema usanifu wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Minjingu kupitia Babati hadi Singida, utaanza baada ya kuwekwa saini mkataba na kampuni ya usimamizi ya Carl-Bro COWI ya Denmark, inaripoti PST kutoka Babati.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, alipokuwa akizungumza na wananchi wilayani Babati, baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Kanali mstaafu Anatoli Tarimo, kumtaka waziri huyo kutoa tamko la kujengwa kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 223 kutoka Minjingu hadi Singida.

Magufuli alisema mkataba wa makubaliano ya uwekaji wa saini kati ya Serikali na kampuni hiyo ambayo ndiyo itakuwa mshauri wa ujenzi, utafanyika kabla ya mwisho wa mwezi huu, na usanifu wa barabara hiyo utakamilika baada ya miezi 10.

"Nataka kuwahakikishieni wananchi wa Manyara, ujenzi wa barabara hii utakwisha baada ya msanifu ujenzi Carl Bro COWI kuwekeana saini ya makubaliano ya usanifu mwezi huu...hivyo karibuni mtaondokana na tabu ya miaka mingi," alisema.

Aliongeza kuwa katika ujenzi huo, awamu ya kwanza ya kilomita 60 za barabara hiyo itaanza kujengwa kutoka Minjingu hadi Babati, wakati awamu ya pili ya kilomita 164

itajengwa kuanzia mjini Babati hadi Singida.

Magufuli aliwahakikishia wananchi hao kuwa ujenzi huo utaanza baada ya bajeti ya mwaka kesho kutolewa, ingawa Benki ya Dunia imeonyesha nia ya kusaidia ujenzi huo, hivyo baada ya kukamilika kwa barabara hiyo hatua inayofuata itaelekezwa katika barabara ya Babati kwenda Dodoma hadi Iringa.

Akifafanua alisema pamoja na mkopo kutoka Benki ya Dunia, Serikali inao uwezo wa kujenga barabara zake kwa kiwango cha lami kutokana na makusanyo ya fedha zake za ndani bila ya kuwategemea wafadhili.

Kwa upande mwingine, waziri huyo alisema katika bajeti mwaka huu, zimetolewa sh. milioni 500 zitumike kufungulia barabara mbaya ya Simanjiro hadi Kiteto, ili kupunguza adha ya usafiri hasa katika kipindi cha mvua ambacho barabara hizo hazipitiki.

Alisema utekelezaji wa kukamilisha barabara hiyo ni tamko la Raisi Benjamin Mkapa mwaka 2002 alipotembelea barabara hizo na alitoa ahadi ya kukamilika kabla ya kuondoka madarakanai.

Katika kukamilisha miundombinu hiyo, amemtaka mkuu wa mkoa kusimamia barabara za ndani kati ya Babati kupitia Simanjiro hadi Kiteto kuanza kuchongwa kwa kiwango cha moram badala ya kusubiri wataalamu wa mazingira.

 

 

'Mapinduzi ya 1964 yaliyofungua milango ya demokrasia'

Na Khatib Suleiman, Zanzibar

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, Mansoor Yussuf Himid, amesema Mapinduzi Matukufu ya 1964 ndiyo yaliyofungua milango ya demokrasia visiwani hapa.

Akihutubia wafuasi na wanachama wa CCM katika jimbo la Kiembesamaki, huko Buyu Wilaya ya Magharibi Unguja, Mansoor alisema Mapinduzi hayo ndiyo yaliyotoa fursa ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu katika mfumo wa vyama vingi.

"Bila ya Mapinduzi tusingelikuwa na uchaguzi wa vyama vingi...utawala wa kisultani haukutoa nafasi wala usingetoa nafasi kama hiyo hata siku moja," alisema Mansoor.

Alisema Mapinduzi ya mwaka 1964 yameondoa utawala wa kisultani na kuruhusu utawala wa kidemokrasia, hayo yakiwa moja ya matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo Wazanzibari hawana budi kuyatunza na kuyalinda kwa faida ya wote.

Alisema hadi sasa wapinzani hawana maneno baada ya kuona kuwepo kila aina ya dalili za kushindwa katika Uchaguzi Mkuu, hivyo wameona ni bora kukimbilia kwa mabalozi ili kujihami kabisa, wakati mambo yatapokwenda kombo.

Mansoor ambaye ni mgombea wa nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Kiembesamaki na Mweka Hazina wa CCM Zanzibar,

alisema ni kawaida kwa viongozi wa CUF kulalamika kwa mabalozi wakati wakiona mambo yameanza kwenda kombo na wakiona dalili za kushindwa.

"Wenzetu wapinzani wanadhani ridhaa ya kuongoza nchi hii hutolewa na mabalozi, sio kweli, maamuzi ya nchi hufanywa na wananchi ambao ndiyo nyie na wanaowategemea mabalozi kutoa maamuzi ya nchi hii wamechelewa sana," alisema.

Mapema, Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Rufeya Juma Mbarouk aliwataka wananchi kuacha kuwachagua wapinzani ambao wakati walipokuwa na nyadhifa serikalini walishindwa kuwatumikia wananchi.

Rufeya alisema anawafahamu vilivyo wapinzani kwa sababu alipata nafasi ya kufanya kazi nao, ambapo walitumia muda mwingi kufanya ubadhirifu katika Serikali ya awamu ya Hayati Idriss Abdull Wakil na kufikia hatua ya kufukuzwa kazi.

"Hawa watu msiwachaguwe niulizeni mimi nawafahamu sana tulikuwa pamoja katika serikali lakini wao walionesha wazi ubabaishaji na uroho wa madaraka," alisema Rufeya ambaye alikuwa mwakilishi wa kuteuliwa na rais katika Baraza la Wawakilishi lililomaliza muda wake.

 

CCM tayari imejipatia madiwani watano Mtera

Malecela asema Wapinzani walie tu

Na Thomas Mtinge, Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi kimejihakikishia ushindi wa madiwani watano kwa wagombea wake wa kata zilizoko katika jimbo la Mtera kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Ushindi huo umetokana na wagombea hao kupita bila kupingwa baada ya vyama vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea kwa kile kinachodaiwa kukubaliana na sera za CCM kutokana na kuwa nzuri.

Hayo yalithibitishwa na mgombea ubunge wa jimbo la Mtera kwa tiketi ya CCM. John Malecela wakati akihutubia mamia ya wananchi waliofurika katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliyofanyika juzi katika kijiji cha Chiboli mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Malecela, majinana ya wagombea hao na kata zao zikiwa katika mabano ni kama ifuatavyo; Alfred Mwakibinga (Handali), Chomola (Makulu), Ruth Mpali (Makang'wa), Meshack Songo (Fufu) na Ainea Mnyajila (Huzi).

Malecela alisema uamuzi wa vyama vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea udiwani katika kata hizo umewadhihirishia wananchi kwamba CCM ni Chama kinachotekeleza ahadi zake za kuleta maendeleo inazozitoa kwa wananchi tofauti na za vyama vya upinzani.

Alisema CCM ni Chama chenye sera madhubuti hivyo kitaendelea kuwaomba waomba wananchi ili kiendelee kuwaletea maendeleo ya kweli.

Hata hivyo amejigamba kwamba wapinzani katika jimbo hilo wanajisumbua bure kwani katika uchaguzi mkuu ujao wasitegemee kuambulia hata kiti kimoja cha udiwani pamoja na ubunge kwani hawana uwezo huo.

"CCM ina uhakika kushinda viti vyote vya udiwani na ubunge katika jimbo hilo la Mtera, hivyo kuwepo kwa wagombea wa upinzani katika jimbo hili kunaheshimu demokrasia ya kuwepo kwa vyama vingi," alisema.

Katika jimbo hilo kuna kata 16 zinazogombaniwa za nafasi ya udiwani ambapo vyama vilivyojitokeza kuwania nafasi ya ubunge na udiwani ni pamoja na CCM, CHADEMA na CUF.

 

 

CCM Z'bar yakana kutengeneza fulana za ushindi wa Karume

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kwamba hakijatengeneza fulana za kusherehekea ushindi wa mgombea wake Rais Amani Abeid Karume kabla ya kufanyika uchaguzi.

Katibu wa Idara ya Uenezi ya CCM Zanzibar, Vuali Ali Vuai, alisema taarifa zilizotolewa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba hazina ukweli wowote.

Alisema kiongozi huyo alitakiwa kufanya utafiti kabla ya kuita vyombo vya habari na kutoa tuhuma hizo.

Vuai alisema kiongozi huyo wa CUF alitakiwa kuainisha ni wapi fulana hizo zimechapishwa na nani aliyegharamia ili kuthibitisha madai hayo.

Alieleza kwamba hivi sasa ni kipindi cha kampeni na chama chochote kinaweza kikachapisha fulana na kusingizia Chama Cha Mapinduzi.

"Chama hicho kimeishiwa na sera za kuwaambia waandishi wa habari kwani inawezekana chama hicho kikachapisha fulana hizo na baadaye kikasingizia CCM ndiyo ilifanya hivyo," alisema Vuai.

Pia alisema CCM ina wasiwasi fulana zilizooneshwa kama ushahidi zikawa fulana za mwaka 2000, kwa vile mgombea huyo ndiye aliyemshinda mpinzani wake Seif Sharif Hamad wa CUF.

Alisema kwamba ni kitendo cha kushangaza kuona CUF ikilalamika waketi wao wamekuwa wakiwahimiza wafuasi wao kujipamba ikiwemo kujipaka hina hata kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Wakati huo huo, Umoja wa Vijana wa CCM umekitaka chama cha CUF kuomba radhi kutokana na viongozi wake kudai CCM imeanzisha kundi la vijana wanaoitwa Janjaweed.

Akitoa taarifa maalum ya umoja huo, Katibu Mkuu wa Umoja huo, Machano Othman Said alisema CCM haina vijana wanaoitwa Janjaweed kama inavyodaiwa na kambi ya upinzani.

Alieleza kwamba CCM ina umoja wa vijana ambao umeanzishwa kwa kufuata sheria na umekuwepo hata kabla ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Alisema kwamba vijana hao hukusanywa na kupewa mafunzo ya itikadi ili wakijue chama chao.

Hata hivyo hakusema hatua gani watachukua iwapo chama cha CUF kitashindwa kuomba radhi, lakini alisema CCM imeshitushwa na taarifa hizo.

Vyama vya upinzani Zanzibar vimekuwa vikilalamika kuwa CCM imekusanya vijana na kuwaweka katika kambi ambapo hufundishwa uharamia.

Chama cha CUF kimekuwa kikiwahusisha vijana hao na baadhi ya matukio ya watu kushambuliwa kwa silaha za kienyeji ikiwemo mapanga, nondo pamoja na kupora vitu katika maduka.

 

Donge kumpongeza Karume kuongoza kura za maoni

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

WAZEE wa vijiji kadhaa katika jimbo la Donge wamesema wanatarajia kukutana na mgombea urais wa Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume, kumpongeza kutokana na kuongoza katika kura ya maoni iliyoitishwa na Taasisi ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (REDET).

Hayo yameelezwa katika kikao cha Kamati ya Wazee wa jimbo la Donge ambayo ilikutana juzi kujadili masuala mbalimbali ikiwemo vurugu zilizojitokeza wiki iliyopita na watu kupigwa risasi huko Mahonda katika jimbo hilo.

Matokeo ya utafiti uliofanywa na REDET mwezi uliopita yameonyesha mgombea wa CCM, Rais Karume aliongoza kwa kupata asilimi 45.8 na mgombea wa CUF, Seif Sharif Hamad alipata asilimia 42.6 na asilimia 10 ya wananchi walisema bado hawajaamua watampa nani.

Wazee hao walisema wanataka kuonana na Rais Karume kumpongeza kutokana na uongozi wake bora na kumpongeza juu ya hotuba zake mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa tangu kampeni za Uchaguzi Mkuu kuanza.

Pia walisisitiza kwamba hawako tayari kuona mkutano wa chama chochote cha siasa ukifanyika katika jimbo la Donge, kwa vile bado wanakumbuka matukio ya nyuma ya vurugu za wapinzani.

"Baada ya kuona yale yaliyotokea tunasisitiza kuwa hatutaki kufanyika mkutano wa chama chochote kijijini kwetu, lengo ni kulinda maisha yetu na watoto wetu", alisema mzee Ussi Haji Pandu (65).

Jimbo la Donge ambalo linasadikiwa kuwa ni ngome ya CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, mgombea wake wa uwakilishi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna na ubunge ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Ameir Mohammed.

Habari zilizopatikana zinasema juzi baadhi ya waandishi wa habari waliongozwa na Ali Ameir kwenda kupokea msimamo wa wazee wa jimbo hilo kuhusiana na vurugu za hivi karibuni na mustakabali wa mikutano ya wapinzani.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema ataendelea kuchukua juhudi za kuhakikisha mkutano katika jimbo hilo unafanyika kwa vile ni haki ya kidemokrasia.

Hamad alisema kwamba wazee wa CCM haiwezekani wakawa juu ya mamlaka ya sheria kwa vile vitendo wanavyovifanya kuwazuia wapinzani wasifanye mikutano ni kinyume na misingi ya demokrasia.

Alisema kwamba CUF inaendelea kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ili kuhakikisha mkutano unafanyika katika jimbo hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 30.

 

Singida ngome mojawapo ya CCM

Na Lauden Mwambona, Singida

WAKAZI wa Mkoa wa Singida wamejiandaa kukipatia ushindi Chama cha Mapinduzi kwa asilimia 99 katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30 mwaka huu, ili kiunde serikali.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoa huo, Maryam Mohammed, alisema hayo jana alipoelezea hali ya kampeni mkoani humo inavyoendelea.

Maryam alisema kimsingi mkoa wa Singida ni wa CCM kwa vile serikali zote za vitongoji, vijiji na mitaa zinaongonzwa na serikali ya CCM na kwamba wananchi wa mkoa huo bado wanayo imani kubwa na Serikali ya CCM.

Alisema mgombea wa wa Urais kupitia CCM Jakaya kikwete atazoa kura zote Singida kwa sababu ni kipenzi cha Watanzania wengi na pia aliwahi kufanya kazi ya Chama mkoani humo wakati akiwa kijana.

"Hata wagombea wa ubunge wa CCM mkoani kwetu, Mgana Msindai wa Iramba Mashariki, Juma Hassan wa Iramba Magharibi, Mohammed Dewiji wa Singida mjini, Mohammed Bisanga wa Singida kusini, Lazaro Nyirandu wa Singida kaskazini, John Chiligati wa Manyoni Mashariki, na John Lwanji wa Manyoni Magharibi, watapata kura nyingi kwa vile wanauzika na pia ni wachapakazi," alisema.

Maryam ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM mkoa huo tangu 1997, alisema CCM mkoa ipo pamoja na wananchi na kwamba ndiyo maana ina uhakika wa kupata ushindi mkubwa.

 

 

 

Mzumbe wamkumbuka Baba wa Taifa

CHUO Kikuu cha Mzumbe, Morogoro, juzi kiliandaa

kongamano la kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere ikiwa ni miaka sita tangu kufariki kwake mwaka 1999. Katika makala hii Mwandiashi Wetu EPSON LUHWAGO aliyehudhuria kongamano hilo amaelezea yaliyojiri na ushauri uliotolewa katika kumuenzi kiongozi huyo mwasisi wa taifa la Tanzania.

KWA mara ya nne mfululizo, Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichoko Morogoro, juzi kiliandaa kongamano la nne la kumkumbuka Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere lililofanyika chuoni hapo, kilomita 25 kutoka Morogoro mjini.

Katika kongamamo hilo, washiriki walipata uhondo wa mada mbalimbali zilizotolewa na wasomi wakiwemo wanazuoni bingwa waliobobea katika taaluma mbalimbai kama vile siasa, utawala, elimu na sosholojia.

Waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na mwanasiasa mkongwe nchini, Ibrahim Kaduma; Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine, Profesa David Mwayusa; Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Moses Warioba.

Wengine ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa; Mrajisi wa Chuo, Profesa Hamisi Mahigi; Mrajisi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Uswege Mwinga na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Profesa Saidi Iddi.

Pia walikuwepo maporofesa, wahadhiri waandamizi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, wanafunzi na wanajamii ya chuo kikuu hicho kwa jumla.

Katika kongamano hilo lililokuwa na kaulimbiu “Uongozi na Maadili kwa Mtazamo wa Nyerere”, jumla ya mada tano ziliwasilishwa na kujadiliwa.

Mada hizo na waliotoa kwenye mabano ni Mfumo wa Siasa wa Vyama Vingi na Maendeleo ya Uongozi wa Demokrasia Tanzania (Profesa Gaudens Mpangala), Mwalimu Nyerere Kiongozi Mwenye Shujaa na Mfano wa Kuigwa (Dk. Christopher Sotta), na Maadili na Uongozi kwa Mtazamo wa Kijinsia: Wajibu wa Mashirika ya Kijamii iliyowasilishwa na Dk. Simeon Mesaki.

Zingine ni Mchango wa Mwalimu Nyerere katika Kuimarisha Maadili kwenye Utumishi wa Umma Tanzania (Dk. Mujwahuzi Njunwa) na Nyerere Kielelezo katika Maadili Duniani iliyowasilishwa na Profesa Matthew Chao.

NENO LA AWALI

Kabla ya kuanza kwa mada hizo, kilitolewa hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Msaidizi Maalum wa Mkurugenzi

Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyeyrere, Gallus Abedi.

Abedi ni mwanasiasa mkongwe tangu enzi za uongozi wa Nyerere na aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali kama vile mkuu wa Mkoa wa Singida na Kilimanjaro, Katibu wa CCM Mkoa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, kabla ya Abedi kutoa hotuba yake, Profesa Mwakyusa ambaye alikuwa daktari wa Mwalimu Nyerere hadi anafariki, alimkaribisha kwa kutoa maneno machache yaliyobeba ujumbe mzito.

Katika maneno hayo, Profesa Mwakyusa alisema yapo mambo mengi ambayo Watanzania hawana budi kumkumbuka kiongozi huyo mwasisi wa taifa kutokana na kuifanya Tanzania kuheshimika ndani na nje ya nchi.

"Hii inawafanya hata baadhi ya watu walioko huko vijijini kuamini kwamba Nyerere bado yuko hai.

Wahadzabe wanaamini hivyo na wamekuwa wakisema wanamsikia kila siku kwenye redio.

Si hivyo tu hata baadhi ya watu unapofika wakati wa uchaguzi hutaka kumpigia kura Nyerere au chama cha Mwalimu Nyerere. Hii inaonyesha wazi kuwa Nyerere ni kielelezo cha taifa kutokana na mambo mengi aliyoyafanya," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema Watanzania hawana budi kuyaenzi kwa vitendo mambo aliyoyafanya wakati wa uhai na uongozi wake kwa jumla.

Kubwa katika hayo, Profesa Mwakyusa alisema Nyerere amewaachia watanzania urithi wa kudumu ambao uko katika vitabu na machapisho yake mbalimbali, hivyo hawana budi kuyasoma ili kuelewa alichokuwa akimaanisha kulinganisha na hali halisi ya maisha ya sasa ya Watanzania.

VIGONGO VYA ABEDI

Baada ya maneno hayo ya ukaribisho, Abedi ambaye wakati wa utawala wa mkoloni alikuwa mkalimani wa mahakama, alianza kwa kusema: “Watanzania hawana budi kumuenzi Mwalimu Nyerere kutokana na mchango wake katika kueleleza, kufafanua na kusisitiza imani yake katika haki, usawa, heshima, uhuru na maendeleo ya binadamu”.

Alisema Mwalimu alisisitiza suala la uongozi na maadili kwa viongozi wa ngazi zote. Katika kusisitiza kwake, alisema Mwalimu alikuwa akiweka bayana kuwa uongozi una asili mbili ambazo ni haki na watu.

Katika hilo, kwa mujibu wa Abedi, Mwalimu Nyerere siku zote alikuwa akisisitiza kwamba uongozi wa nchi katika ngazi zote lazima utokane na watu na mtu anapokuwa kiongozi hana budi kuternda haki.

Abedi alimnukuu Mwalimu akisema: "Uongozi wetu hauna budi utokane na watu wa nchi hii bila hila, bila rushwa, bila vitisho na bila ujanja wa aina yoyote. Tunapokuwa katika hali ya uongozi kwa kupitia mlango wa hila, rushwa, vitisho au ujanja wa aina nyingine yoyote, basi hatukutokana na watu wenyewe".

Katika hali hiyo, Nyerere alikuwa akihimiza na kusisitiza kwamba kiongozi yeyote hawezi kuwa kiongozi kamili kama atakuwa hajishughulishi na shida za wananchi hususan watu waliomchagua.

Kwa upande wa haki, Abedi alisema Nyerere alikuwa kiongozi wa mstari wa mbele kutaka haki itendeke kwa watu wote bila kujali nafasi au hali aliyo nayo mtu fulani.

Alisema Nyerere hata baada ya kuondoka madarakani, hakusita kutoa msimamo wake alipokuwa akiona mambo ndani ya serikali au Chama yanaendeshwa bila kufuata utaratibu.

Alitoa mfano wa mwaka 1994 alipotunga kitabu cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania. Alifanya hivyo baada ya kuona kuna hatari ya nchi kuyumba kutokana na mambo mbalimbali yakiwemo ya ukiukwaji wa sheria na katiba ya nchi.

Kiongozi huyo wa siku nyingi serikalini hakuishia hapo. Alisema Nyerere alikuwa mkali pindi alipokuwa akiona maadili yanakiukwa kwa viongozi wake. Alisema hakuwa na huruma kwa mtu aliyekuwa akienda kinyume na maadili.

VIONJO VYA MADA

Profesa Mpangala kutoka Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika

mada yake alisema Nyerere alikuwa kiongozi aliyekuwa akisisitiza demokrasia na utawala bora.

Profesa Mpangala alitoa mfano wa Mwalimu alivyosisitiza juu ya misingi ya demokrasia, uongozi bora na kuwa mtu asiyependa rushwa wala kujinufaisha.

Alisema Mwalimu Nyerere alisisitiza suala la demokrasia na uongozi bora hata wakati wa mfumo wa chama kimoja ambapo uchaguzi ndani ya chama na serikali ulikuwa ukifuata misingi hiyo. Alisema Mwalimu alikuwa akisisitiza uongozi bora lazima utokane na watu.

 

"Ingawa Mwalimu alikuwa kiongozi na mwanzilishi wa mfumo wa chama kimoja, busara zake zilimfanya kukubali kwamba mawimbi yaliyoikumba Afrika na dunia nzima juu ya mabadiliko ya kisiasa yalikuwa hayakwepeki na hivyo kushauri Tanzania pia kubadilika na kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 1990," alisema.

Dk. Simeon Mesaki wa Idara ya Sosholojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mada yake juu ya Maadili na Uongozi katika Mtazamo wa Jinsia, alisema Mwalimu Nyerere alikuwa mfano wa viongozi walioongoza kwa kufuata misingi ya maadili na uadilifu.

Kwa masuala ya kijinsia, Dk. Mesaki alisema tangu wakati wa kupigania uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za wanawake.

Alisema katika Azimio la Arusha, mathalan, Mwalimu alielezea usawa baina ya wanawake na wanaume na kusisitiza kuwa wanawake hasa waishio vijijini wanafanya kazi kwa muda mrefu kuliko mtu yeyote nchini.

Hata katika maendeleo, kwa mujibu wa Dk. Mesaki- Mhadhiri Mwandamizi wa Socholojia, Nyerere alisisitiza kama ifuatavyo juu ya suala la usawa hasa kwa wanawake;

“ Kama tunataka nchi yetu iwe na maendeleo ya haraka, ni muhimu wanawake wakaishi katika hali ya usawa sambamba na raia wenzao ambao ni wanaume”.

Hai hiyo inaonyesha bayana kwamba Nyerere alikuwa mtu anayezingatia suala la usawa wa kijinsi hata kabla harakati za watu mbalimbali duniani hazijaanza na kuota mizizi.

Dk. Sotta, Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Utawala na Uongozi cha Chuo Kikuu cha Mzumbe alimwelezea Nyerere kuwa alikuwa kiongozi shujaa na aliyejitoa kuwatumikia watu wake.

Alisema sifa nyingine inayomfanya Nyerere kuonekana tofauti na wengine ni uwezo mkubwa wa kuchambua mambo kwa kutumia nadharia mbalimbali ambazo zilikuwa na mantiki.

Katika suala la maadili, Profesa Chao wa Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema Nyerere alikuwa kielelezo cha maadili mema duniani.

Alizitaja sababu zilkizomfanya kuwa na sifa hiyo kuwa ni uwezo wake wa kujifunza kwa kina matatizo yanayoikabili jamii, kusikiliza masuala mbalimbali, utekelezaji katika kutatua matatizo ya kijamii na kushiriki kwake katika mgawanyo wa madaraka.

Sifa ya ziada ya Mwalimu Nyerere, kwa mujibu wa Profesa Chao, katika mambo hayo ni kuwa mbunifu katika kukabiliana na chanamoto za matukio na itikadi zilizokuwa zikitokea kila wakati.

Dk. Njunwa kwa upande wake alisema Nyerere alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha maadili katika utumishi wa umma yanazingatiwa na kufuatwa ipasavyo.

ALIKUWA MKAMILIFU?

Kama ilivyo kwa binadamu yeyote asivyo mkamilifu, washiriki walieleza kwamba Nyerere alikuwa na udhaifu wake katika dhana na mambo aliyoyaanzisha, kutekeleza na hata kuyaamini. Pamoja na udhaifu huo, washiriki hao walikubaliana kwamba mambo mengi aliyoyaanzisha yameleta mafanikio tofauti na yale ambayo yameonekana kuwa hayakufaa kwa mtazamo wa watu mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, walisema Nyerere hana budi kuenziwa kwa mambo aliyoyafanya kwa taifa hili na yale ambayo yalikuwa na udhaifu yachukuliwe kama changamoto katika ujenzi wa taifa linalofuata haki, usawa, maadili na uongozi bora kama alivyokuwa akisisitiza juu wakati wa uhai wake.

MAMBO YAKE YANAFUATWA?

Tofauti na alivyohimiza Nyerere katika maadili na uongozi, viongozi wengi wa sasa, kwa mujibu wa washiriki, wameshindwa kufuata maadili ya uongozi na hivyo kwenda kinyume na dhana ya Nyerere.

Baadhi ya washiriki waliochangia kwenye kongamano hilo walieleza wazi kwamba hivi sasa watu wengi wanaingia madarakani siyo kuwatumikia wananchi bali kwa manufaa binafsi.

Walisema hali hiyo inajionyesha nyakati za uchaguzi ambapo mamalamiko mengi yamekuwa yakijitokeza juu ya watu kutumia fedha kuingia madarakani. Hali hiyo, kwa mujibu wa washiriki inaashiria kwamba maadili ya taifa yanamomonyoka kwa kasi kubwa.

Michango hiyo ya washiriki pia ilihanikizwa na igizo lilionyesha watu wanavyogombea kuingia madarakani huku wakitumia mbinu mbalimbali za kuchafuana na kupigana vita vya maneno baina yao.

WANG’ATUKE

Abedi katika hotuba wyake alitoa ‘ushuri wa bure’ kwamba waliopewa dhamana katika nafasi mbalimbali hawana budi kujiuzulu nyadhifa zao pindi wanapotiliwa shaka kuwa wamekiuka maadili ya uongozi, ikiwa ni pamoja na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Abedi alisema viongozi katika ngazi mbalimbali wamekuwa wakituhumiwa kukiu kamaadili, zikiwemo tuhuma za rushwa, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kuamua kujiuzulu.

Alisema kwa viongozi kujiuzulu pindi wanapotuhumiwa watakuwa wanatekeleza dhana halisi ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo.

"Umefika wakati watu wakafufua utamaduni wa kung'atuka kama tuhuma za ukiukaji maadili zinawaandama. Suala siyo kusubiri upatikane ushahidi kwani kiongozi anatakiwa wakati wote kuwa mfano wa kutokutiliwa shaka juu ya matendo yake," alisema.