UHURU 14.11.2005

 

KUFUATIA VIONGOZI WAKE KUZOMEWA:

Mwandishi Wetu, Songea

KANISA Katoliki jimbo kuu la Songea limetangaza rasmi kuacha kuhubiri siasa na

 

kuwafanyia kampeni baadhi ya wagombea ubunge katika jimbo la Songea Mjini.

Tamko la kuacha rasmi kampeni za kisiasa kanisani lilitolewa jana wakati wa ibada

 

na Mwenyekiti wa Baraza la Walei la kanisa hilo, Ernest Haule ambaye alisema

 

uongozi wa kanisa umesikitishwa na yaliyojitokeza kutokana na mahubiri na kuwa

 

haitatokea tena jimboni humo.

Mwenyekiti amewataka waumini kuacha kuwazomea viongozi wa kanisa kwa yale yote

 

wanayoaamini kuwa yanawakwaza na badala yake watumie viongozi wao wa ngazi

 

mbalimbali kufikisha malalamiko yao.

Haule alisema kwa upande wao baraza limekutana na Baba Askofu Nobert Mtega na

 

mapadre wote na wamekubaliana kimsingi kuacha mahubiri yote yenye mwelekeo wa

 

kisiasa ili kulinda maadili na umoja wa kanisa hilo na kuwataka waumini kuwa

 

katika hali yao ya kawaida kuheshimu kanisa kama mwanzo.

Imekuwa ikidaiwa kwamba viongozi wa kanisa katika jimbo hilo, hasa mapadre na

 

askofu wamekuwa wakimfanyia kampeni kanisani mgombea wa ubunge wa chama kimoja

 

cha upinzani katika jimbo la Songea Mjini.

Wananchi wamekuwa wakililalamikia Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea kwamba

 

limekuwa likimfanyia kampeni mgombea wa Chadema hali iliyosababisha kuzomewa kwa

 

baadhi ya makasisi wake kanisani hapo na katika hali ya kushindana, waumini nao

 

wamekuwa wakivaa sare za Chama Cha Mapinduzi wakati wa ibada kanisani.

Inadaiwa Padre Noel Duwe ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo Cha Radio Maria Songea

 

aliwahi kuzomewa na waumini baada ya kutamka wazi kuwa wananchi wasiichague CCM

 

na badala yake wachague CHADEMA kwa madai CCM inatoa Khanga, fulana na kofia

 

ambazo zina picha za wagombea wao.

Kwa kauli yake hiyo inadaiwa ilisababisha azomewe na waumini na kuanzia hapo

 

waumini wakaamua kuvaa sare za CCM kanisani.

Hata hivyo, hali haikuishia hapo, kwani katika ibada siku nyingine katika kanisa

 

hilo hilo la kiaskofu la Mtakatifu Mathias Mulumba Kalemba inasemekana waumini

 

waliwahi kumzomea Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea Mhashamu Norbert Mtega

 

kutokana na mahubiri yake kama ya Padre Duwe na kusababisha kuamsha hasira toka

 

kwa waumini wa kanisa hilo.

Zomea zomea haikuishia kwa viongozi hao tu, kwani paroko wa parokia ya Songea

 

Mjini Padre Paulo Chiwangu ambaye anaheshimika sana kwa waumini wa kanisa hilo

 

naye alipata adha hiyo alipokuwa na hoja ya kuwataka waumini wa kanisa hilo

 

kuacha tabia ya kuwazomea na kuwatukana viongozi wao wanapowakosea na badala yake

 

watumie utaratibu wa kuwaona viongozi wa ngazi mbalimbali ili kutatua tatizo

 

hilo.

Aidha, paroko huyo alipata wakati mgumu pale alipozomewa wakati alipowataka

 

waumini wamwombe radhi Askofu Mkuu Mtega kutokana na kitendo chao cha kumzomea

 

kwa vile ni kiongozi wao mkubwa wa kanisa, na kwamba hakupaswa kuzomewa kwa

 

kiwango kile na kwamba ni kumkosea adabu na kukosa utii kwa Mungu.

 

CUF iheshimu maamuzi ya Wazanzibari - Mapuri

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Omar Ramadhan

 

Mapuri amewataka viongozi na wafuasi wa CUF kuheshimu uamuzi wa Wazanzibari wa

 

kuichagua CCM kuendelea kuiongoza Zanzibar.

Mapuri aliyasema hayo juzi baada ya kuzindua shina la Wazee wakereketwa wa CCM,

 

Gongolamboto, kata ya Ukonga, Dar es Salaam na kuongeza kuwa baada ya matokeo ya

 

uchaguzi huo kila Mzanzibar na Mtanzania kwa jumla kuyaheshimu.

Alisema baada ya kauli ya Wazanzibar waliyoitoa kwa kupiga kura Oktoba 30, mwaka

 

huu, katika Uchaguzi Mkuu ambapo waliichagua CCM kuendelea kuunda dola, CUF haina

 

budi kuheshimu kauli hiyo.

Katika uchaguzi huo, wananchi wa Zanzibar walimchagua Rais Amani Abeid Karume

 

kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo, pia

 

waliwachagua wagombea wa CCM katika majimbo 30 kati ya 49 kuwa Wajumbe wa Baraza

 

la Wawakilishi na Madiwani.

Huku akishangiliwa na wana-CCM na wananchi waliofurika katika viwanja vya shina

 

hilo, Mapuri alisema mtu yeyote kukataa matakwa ya Wazanzibari walio wengi siyo

 

tu ni kuwanyima haki wananchi, pia ni uvunjaji wa sheria za nchi.

Mapuri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani, aliwatahadharisha wana-CCM na

 

wananchi kwa jumla wanaoitakia mema Tanzania wasibweteke na ushindi walioupata

 

katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Oktoba 30, mwaka huu.

Badala yake, aliwataka wajipange upya kuhakikisha CCM inashinda kwa ushindi wa

 

kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopangwa

 

kufanyika Desemba 14, mwaka huu.

Alisema uamuzi uliofanywa na Wazanzibari wa kuichagua CCM kuendelea kuiongoza

 

Zanzibar uwe changamoto kwa wana-CCM na wananchi kwa jumla kuhakikisha wanaweka

 

mikakati madhubuti itakayohakikisha CCM inaibuka na ushindi wa kishindo katika

 

uchaguzi huo.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Desemba 14, mwaka huu, Watanzania wote wa Bara na

 

Zanzibar watapata fursa ya kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

 

Wabunge na kwa Bara watawachagua pia Madiwani.

 

CCM haina shaka na jimbo lolote Iringa

Na Bashir Nkoromo, Njombe

CHAMA Cha Mapinduzi kimesema kwa sasa hakuna jimbo hata moja la uchaguzi mkoani

 

Iringa ambalo lina shaka nalo kwamba italikosa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula katika mikutano yake ya

 

ndani na viongozi wa CCM aliyoifanya mwishoni mwa wiki kwa nyakati tofauti katika

 

maeneo ya Ilembula na Wanging'ombe katika jimbo la Njombe Kusini.

Alisema, hata hivyo, hali imekuwa nzuri baada ya kuwa baadhi ya majimbo kulikuwa

 

na shaka zilizosababishwa na tofauti baina ya wanachama zilizotokana na mchakato

 

wa kura za maoni wakati wa kupata wagombea.

Mangula alisema, baada ya migawanyiko hiyo ambayo ni ya kawaida kutokea wakati

 

kama huo, sasa mshikamano umerejea na wana CCM wamekuwa kitu kimoja.

Aliwataka wana CCM ambao bado wanazing'ang'ania tofauti hizo mkoani humo na

 

nchini kote kwa jumla sasa kuachana nazo kabisa kwa kuwa waliokuwa wakiwashabikia

 

sasa si wagombea ila waliobaki baada ya kuteuliwa na vikao vyenye maamuzi ya

 

mwisho ya Chama ndiyo wagombea.

Mangula alisema, mgawanyiko uliokuwepo si katika ngazi za ubunge tu na udiwani

 

ila hadi katika ngazi ya mgombea Urais.

Alisema, baada ya michakato kupita hatimaye alipopatikana mgombea mmoja

 

aliyetakiwa, migawanyiko sasa haipo na wale 10 wote ambao hawakupita wameungana

 

na wana-CCM wote kumpigia debe mgombea wa kiti hicho, Jakaya Kikwete.

"Kwa mwanachama aliyeiva na mwenye moyo thabiti na Chama anatambua kuwa kura za

 

maoni ni maoni si uamuzi... hivyo baada ya vikao vyenye maamuzi ya mwisho

 

kupitisha mgombea yeye wajibu wake hubaki ni kuunga mkono aliyepatikana," alisema

 

Mangula.

Katika mikutano hiyo Mangula aliwataka wananchi wa jimbo la Njombe Magharibi

 

kuhakikisha wanamchagua kwa kura nyingi mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM

 

Charles Kevela ambaye amechukua nafasi ya mbunge wa zamani Thomas Nyimbo.

Mangula kama alivyokuwa akitamka katika mikutano yake ya Lupembe na Makambako

 

jimbo la Njombe Kaskazini, aliwataka wana CCM kutambua kwamba kwa sasa kazi

 

iliyopo mbele yao ni moja tu, kuipatia ushindi mnono CCM katika uchaguzi Mkuu

 

utakaofanyika Desemba 14, mwaka huu.

Alisema, kila mwana-CCM hana budi kuhakikisha anapiga kampeni ya aina ya kipekee

 

kuhakikisha anashawishi wasio wanachama kuipigia kura CCM siku hiyo.

Katika mikutano hiyo Mangula alionya pia kwamba kusiwepo viongozi ndumilakuwili

 

watakaothubutu kukisaliti Chama wakati huu wa kutafuta kura ili CCM iweze kuunda

 

serikali tena.

Alisema kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokutana hivi karibuni kimeagiza

 

kukusanywa kwa kumbukumbu za viongozi wasaliti ili baada ya uchaguzi watupwe nje

 

ya Chama.

Mangula alisema, kwa wale viongozi watakaoonekana kusaliti wazi wazi kama ni wa

 

kuchaguliwa wasimamishwe uongozi na kama ni wa kuteuliwa wafukuzwe.

Katibu Mkuu wa CCM ambaye anafanya ziara hiyo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya

 

kampeni na hali ilivyo kuelekea uchaguzi mkuu, jana aliendelea na ziara yake

 

katika eneo la Wemba jimbo la Njombe Kusini kabla ya kwenda Mbeya leo.

 

 

 

Kanisa kuruhusu kondom kwa wanandoa tu, iwapo Mmoja ana virusi vya ukimwi

Na Pendo Mangala, Dodoma

KANISA Anglikana nchini limesema litaruhusu matumizi ya kondomu kwa waumini wake

 

ambao ni wanandoa tu pindi mmoja kati yao atakapokuwa ameathirika na ugonjwa wa

 

ukimwi ili kumlinda mwenzake asipate virusi vya ugonjwa huo.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Mchungaji Dk.

 

Akili Mwita alipofungua semina ya mama wachungaji juu ya ukimwi katika ukumbi wa

 

Furaha Hostel mjini hapa.

Mwita alisema kanisa hilo litaruhusu matumizi ya kondomu kwa waumini wake ambao

 

ni wanandoa tu pindi mmoja kati yao atakapokuwa ameathirika na ugonjwa huo.

Alisema kwamba mtu kupata ukimwi siyo dhambi na wala siyo adhabu toka kwa Mungu,

 

na kwamba mtu yeyote anaweza kupata ukimwi, kwani ugonjwa huo huambukizwa kwa

 

njia mbalimbali hivyo kanisa na jamii kwa jumla iachane na dhana hiyo potofu.

Katibu huyo alifafanua kwamba awali Kanisa Anglikana na jamii kwa jumla walikuwa

 

wakiamini kwamba mtu ambaye ameathirika na ugonjwa wa ukimwi ni mtenda dhambi,

 

jambo ambalo siyo kweli.

Alisema wao kama kanisa hawaruhusu matumizi ya kondomu kwa waumini wake na jamii

 

nzima, kwani kitendo cha kuwaruhusu kuvaa kondomu ni sawa na kuwatuma watende

 

dhambi na kuendeleza uzinzi na hivyo wanakuwa hawajajikinga na dhambi, bali

 

wanaiendeleza.

Aidha, aliwashauri wale ambao ni watumishi wa Mungu na ambao hivi sasa

 

wameathirika na ugonjwa huo wamgeukie Mungu kwa kutubu ili aweze kuwasaidia

 

kuishi kwa matumaini.

Hata hivyo, aliwataka kinamama hao kutumia uwezo waliupata katika kuwaelimisha

 

wananchi juu ya athari za ugonjwa wa ukimwi, ikiwa ni pamoja na kuzungumza na

 

familia zao bila woga kuhusiana na ugonjwa huo.

Katibu huyo alisema mama ndiye kitovu cha familia, hivyo ana wajibu mkubwa katika

 

kukaa na kuzungumza nayo juu ya maadili mema na mienedo bora ya watoto, hasa

 

kuwaeleza juu ya ugonjwa wa ukimwi bila woga.

Alisema baadhi ya kinamama wamekuwa wakiogopa kuongea na familia zao juu ya

 

mienendo mibaya waliyonayo watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwaeleza juu ya ugonjwa

 

huo na hivyo kuwafanya waingie katika janga la ugonjwa huo.

Alisema madhumuni ya semina hiyo ni kuwawezesha wake za wachungaji kuelewa na

 

kushiriki katika huduma ya kutunza wagonjwa nyumbani pamoja na kuwapa ushauri

 

nasaha.

Semina hiyo iliandaliwa na Kanisa Anglikana la Tanzania ambapo liliwashirikisha

 

jumla ya Mama Wachungaji 35 kutoka katika wilaya za Manyoni, Kongwa, Mpwapwa na

 

Dodoma mjini.

 

Dk. Mahanga awataka wananchi kuichagua CCM

Na Nashon Maingu

WANACHAMA wa CCM na wananchi kwa ujumla wametakiwa kuiga mfano wa Wazanzibari kwa

 

kuwapigia kura wagombea wa CCM katika uchaguzi mkuu mwezi ujao ili kudumisha

 

amani.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na mgombea ubunge, jimbo la Ukonga, kupitia

 

CCM , Dk. Makongoro Mahanga, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika

 

viwanja vya Kilimani.

"Kule Zanzibar wapinzani wamenyolewa kwa wembe mkali na kuwaacha vipara, basi na

 

sisi Tanzania bara tuwakwanguwe kabisa ngozi ili wasambaratike,"alisema Dk.

 

Mahanga.

Mgombea huyo amewatoa shaka wakazi wa kata ya Kitunda katika maeneo yaliyokuwa

 

yametengwa kwa ujenzi wa viwanda kuwa sasa serikali imekubali yawe maeneo ya

 

makazi na kuwa kazi ya kupima viwanja imeishaanza.

Mgeni rasmi katika mkutano huo, J. Gasaya ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa wa Kivule,

 

kwa vipindi viwili mfululizo, amewaonya wana CCM ambao wanasemekana kuajiriwa na

 

wapinzani katika kata hiyo ili kuweka makundi.

Imebainika kuwa baadhi ya wanachama wanadanganywa na wapinzani kuwa watapelekewa

 

maendeleo, kama vile barabara, zahanti, shule na watapatiwa masoko ya uhakika ya

 

kuuza mboga na mayai.

Mwenyekiti wa mtaa aliwambia wananchi kuwa ili kuwasogezea maendeleo na pia

 

kuongeza ajira, serikali ya awamu ya tatu imeishaidhinisha kugawanya kata ya

 

Kitunda kuwa kata mbili.

Kata moja itajumuisha mitaa ya Kitunda kati na Mzinga na kata ya pili itakuwa na

 

mitaa ya Kivule na Kipunguni B.

Naye mgombea kiti cha udiwani Johness Kasema aliwataka wana CCM kuwa askari

 

mahiri wa kulinda amani na usalama uliopo.

Mwenyekiti wa CCM, wilaya ya Ilala Mikidadi Mahamud aliwakumbusha kuwa kata ya

 

Kitunda ilivunja rekodi ya taifa kumpigia kura Rais Benjamin Mkapa mwaka 2000 na

 

hivyo kuwataka mwaka huu wazidishe maradufu ya hapo na kuwapitisha wagombea wote

 

watatu wa CCM.

 

Mwenegoha: wapinzani wanaozuia uchangiaji maendeleo wapuuzwe

Na Latifa Ganzel na Prosper Kulita, Morogoro

MGOMBEA ubunge jimbo la Morogoro Kusini kupitia CCM, Hamza Mwenegoha amewataka

 

wananchi kuwa macho na vyama vya upinzani vyenye sera ya kuzuia kuchangia ujenzi

 

wa shule kwani kufanya hivyo ni kuondoa kasi ya maendeleo ya elimu.

Mwenegoha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi alisema

hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akiongea na wananchi wa kijiji cha Kibangile

 

Morogoro vijijini juu ya uchangiaji wa ujenzi wa shule za sekondari.

Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi wa vyama vya upinzani kuwarubuni wananchi

 

wasichangie ujenzi huo hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya elimu.

Aliongeza kuwa tangu kuanza kwa mpango wa kuchangia ujenzi wa shule za msingi na

 

sekondari hali ya elimu imepanda tofauti na awali.

Wakati huo huo, imeelezwa kuwa sera za CCM zilizowekwa katika kutafuta maendeleo

 

hazipo kuwabagua wanachama wa vyama vya wapinzani wala wagombea wa vyama hivyo

 

badala yake zitafanya kazi kwa malengo ya kuwatafutia maendeleo Watanzania wote

 

bila kujali itikadi zao.

Hayo yamesemwa na msemaji mkuu wa CCM jimbo la Morogoro Mjini ambaye pia ni kaka

 

wa mgombea ubunge kupitia CUF, Mbarala Mharagande, Mahiku Maharagande alipokuwa

 

akielezea sera za CCM katika uzinduzi wa kampeni za ubunge na udiwani awamu ya

 

pili zilizofanyika katika kata ya mji mkuu manispaa ya Morogoro mwishoni mwa

 

wiki.

Alisema baadhi ya wapinzani wakiwemo vijana ambao wanavishabikia vyama hivyo wana

 

mtazamo wa kubaguliwa iwapo CCM itashika madaraka na kuwa sera za CCM hazibagui

 

wala kuweka matabaka.

Mharagande alisema wafuasi wa vyama vya upinzani pamoja na viongozi wao lazima

 

watambue kuwa sera za kuwaneemesha Watanzania kiuchumi hazitalenga mwana CCM ama

 

shabiki wa CCM badala yake zitaangalia watu wote.

 

Wahimizwa kujenga mabweni katika shule za sekondari

Na El-hadji Yuusuf, Tabora

SERIKALI imewataka wakazi wa mkoa wa Tabora waanze sasa kujenga mabweni katika

 

shule za sekondari za kata kwa ajili ya kulala wanafunzi wanaoishi mbali na shule

 

hizo, ili kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha washindwe kuendelea na

 

masomo.

Wito huo, umetolewa na Mkuu wa mkoa wa Tabora, Abbas Kandoro, wakati akihutubia

 

wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kijiji cha Goweko, wilaya ya

 

Uyui.

Mkuu mkoa, aliwaambia wananchi kuwa, sekondari zinazoendelea kujengwa katika kila

 

kata ni vyema zikawa na mabweni ya kulala wanafunzi, hususan wa kike

 

ili kuwaepusha na vishawishi, ambavyo husababishia wengi kushindwa kuendelea na

 

masomo.

“Mwanafunzi anayelala bwenini ana muda mwingi wa kujisomea tofauti na yule

 

anayelala nyumbani, kwa kuwa ana muda mwingi wa kujifunza na kupata msaada wa

 

walimu wakati wote, hivyo kuwa na maendeleo mazuri ya masomo tofauti na yule

 

anayesoma na kurudi nyumbani kwao jioni,” alisema Kandoro.

Mkuu wa mkoa ambaye alikuwa katika ziara ya kukagua shughuli za maendeleo,

 

aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa shule ya sekondari ya

 

kata hiyo ili watoto wao waanze kuitumia katika muhula wa kidato cha kwanza

 

mwakani.

Alieleza kwamba jitihada za serikali za ujenzi wa shule za sekondari katika kila

 

kata zitafanikiwa haraka iwapo wananchi katika kata hizo watahamasika na

 

kuchangia ujenzi wa shule hizo kwa kutumia nguvu zao.

Katika ziara hiyo ya kukagua miradi ya maendeleo, mkuu wa mkoa aliweka jiwe la

 

msingi katika jengo la vyumba vinne na ofisi ya shule ya sekondari ya kata ya

 

Goweko na nyumba ya mwalimu ambapo majengo hayo yanatarajia kukamilika kati ya

 

mwezi ujao ili yaanze kutumika mwakani.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewaagiza watendaji kuwa ifikapo

 

Januari mwakani, watoto wote waliokusudiwa kuandikishwa kwenda shule, wawe

 

wameandikishwa, vinginevyo wazazi au walezi wakamatwe na kuwajibishwa kwa mujibu

 

wa sheria.

Akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Kandoro amewataka viongozi wa

 

serikali za vijiji kutumia sheria kuwabana wazazi wasiotaka kupeleka watoto wao

 

wakaandikishwe kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza mwakani.

Agizo hilo lilitolewa kufuatia risala ya wakazi wa kata hiyo kwa mkuu wa mkoa,

 

ambayo ilieleza kuwa hadi kufikia mwezi huu, wazazi na walezi katika kata hiyo

 

wameandikisha watoto 200 tu, wakati lengo la kata ni kuandikisha watoto zaidi ya

 

1,000.

 

Kamati za ujenzi wa shule zatakakiwa kumaliza kazi

Na Bahati Alex, Iringa

SERIKALI wilayani Njombe imezitaka kamati za ujenzi wa shule za msingi na

 

sekondari, kumaliza ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za walimu kabla

 

ya Desemba 15, mwaka huu.

Mkuu wa wilaya ya Njombe, Halima Kihemba aliyasema hayo wakati wa ziara ya wiki

 

mja ya ukaguzi wa shule za sekondari na kuzungumza na kamati za ujenzi.

Aliziambia kamati hizo kuwa, kushirikisha wananchi na serikali kwa ukaribu

 

kunaweza kuweka mipango madhubuti na mikakati itakayowezesha watoto watakaofaulu

 

kuanza kidato cha kwanza mwakani kuendelea na masomo.

Shule zilizochelewa kupokea wanafunzi mwaka jana ni Jackson Makweta, iliyopo kata

 

ya Igongolo na shule ya sekondari Uliwa iliyopo kata ya Iwungilo.

Jumla ya shule za sekondari mpya 13 zimefunguliwa mwaka huu wilayani Njombe, kati

 

ya shule 28, zilizofunguliwa mkoani Iringa.

Wakati huo huo, jumla ya viwanja 6,000 vya ujenzi wa nyumba bora vinatarajiwa

 

kupimwa katika kata ya Makambako wilayani Njombe mkoani hapa ili kukamilisha

 

ujenzi wa mji mdogo utakaojengwa kufuatia sheria za mipango miji.

Ofisa Mtendaji wa mji mdogo wa Makambako, Godwin Beeny alisema upimaji wa viwanja

 

hivyo utauweka mji huo katika ramani ya mji wa kisasa kuliko ulivyo hivi sasa.

Alisema Makambako inayokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 52,000 umepitishwa kuwa

 

mji mdogo, lakini nyumba nyingi zimejengwa holela bila kufuata utaratibu

 

unaotakiwa kufuatwa.

Katika hatua nyingine wakazi wa wilaya ya Makete mkoani hapa wametakiwa

 

kuwasaidia watoto yatima na waathirika wa ukimwi, kwani wanapata shida sana

 

kutokana na mazingira wanayoishi.

Wito huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania

 

(KKKT) Dayosisi ya Kusini-Kati, Shadrack Manyeiwa wakati akiongea na wakazi wa

 

tarafa ya Bulongwa, wilayani Makete, ili kuwahamasisha wawe na moyo wa kujitolea

 

katika kuwasaidia walio na shida.

 

 

Tupigwe na wafuasi wa CUF, kisha tulipwe fidia, hapana…!

Na Dunia Mzobora

BILA shaka, nitatofautiana kwa kiasi kikubwa na wanataaluma wenzangu wa habari

 

kutokana na hili la kupigwa, kisha tukubali kulipwa fidia.

Nitatofautiana na wengi kwa sababu yapo masuala ya mtu kupigwa na baadaye

 

mahakama au wazee wakaketi na kisha wakamwamuru muhusika alipe fidia na

 

aliyepigwa au kuumizwa kuipokea fidia hiyo.

Hili kwa namna fulani linakubalika na kwa kiasi kikubwa, fidia aliyolipa muhusika

 

huyo huweza kumpa fundisho la kutorudia makosa yake, na wakati huo huo kumpoza

 

aliyefidiwa kwa namna moja.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi

 

wa Kiswahili (TUKI) mwaka 1981, Uk. wa 55, fidia ni malipo kwa ajili ya hasara au

 

maumivu yaliyofanywa.

Ni kweli wanataaluma wenzetu wamepigwa, wameumizwa, na hivi sasa wanaugulia

 

maumivu makali mwilini mwao… vyombo vyao vya kazi, zikiwemo kamera na magari

 

navyo viliharibiwa vibaya.

Si hivyo tu, heshima na utu wa wanataaluma wenzetu umeporomoka mbele ya jamii

 

kutokana na kipigo kile cha ‘mbwa mwizi’, na mbaya zaidi ni kwamba wameathirika

 

kisaikoliojia.

Kwa namna yoyote ile, hili la kupigwa na wafuasi wa chama cha CUF na kisha

 

‘tupozwe machungu’ kwa kupokea fidia itakayolipwa na chama hicho ni jambo ambalo

 

halikubaliki.

Kama ni kulipwa, fidia hiyo italipwa na waajiri wao kwa sababu wanataaluma hawa

 

walipatwa na madhila hayo wakiwa kazini, na sheria za kazi zinaweka bayana kuhusu

 

suala hilo.

Vinginevyo, wanataaluma ya habari kupitia ‘majukwaa’ yetu mbalimbali tunaweza

 

kukutana na kuchangishana kidogo kidogo na kisha tukawapa ‘pole’ wenzetu hawa,

 

John Maxmillian na Salehe Masoud.

Kuikubali fidia ya CUF ni kukubali ‘kujiua’ kwa kisu chetu wenyewe. Kwamba,

 

watakuwa wakitupiga kwa makusudi kwa kutambua kwamba kesho yake watalipa fidia.

Kamwe tusikubali mchezo wa mume ‘mshenzi’ anayempiga mkewe kila mara kwa kutambua

 

kuwa kesho yake atamwangukia kwa doti ya khanga au kitenge cha Wax! Huu ni

 

upuuzi.

Tangu tukio la awali la kupigwa kwa ‘mdogo wangu’ Khalfan Said na mwenzake na

 

wafuasi wa chama hicho, CUF ilikaa kimya kabisa kana kwamba hakuna kilichotokea.

Hata baada ya kutokea hili la kupigwa kwa kina Maxmillian, CUF haikujali mpaka

 

vyombo vyenyewe vya habari vilipoichachamalia, ndipo zikaanza kujitokeza kauli za

 

‘kujikosha’.

Kimsingi, siandiki hivi kwa kuwa ni mwandishi na mhariri katika gazeti la Chama

 

tawala, la hasha, naandika kama mwanataaluma wa habari, ambaye ningeweza kuandika

 

haya katika chombo na mahali popote duniani.

Ninaomba nieleweka vyema kwamba, hapa sisukumwi na itikadi ya chama au

 

ukereketwa, bali misingi na kanuni zinazoongoza taaluma ya habari, ambayo

 

nimeisomea ndani na nje ya nchi.

Hivi mbona tukio la kupigwa kwa kina Mpoki Bukuku na Christopher Kidanka na

 

askari magereza na wafungwa wao, vyombo vya habari havikusita kuchukua hatua

 

dhidi ya wakubwa wa taasisi hizo?

Kila mmoja ameshuhudia jinsi Waziri wa Mambo ya Ndani, Omar Ramadhani Mapuri na

 

Kamishna Mkuu wa Magereza, Nicas Banzi ‘walivyosuswa’ na baadhi ya vyombo vya

 

habari vya hapa nchini.

Kumbe ni kitu gani, kama wanataaluma ya habari kinachotufanya tushindwe kuiadhibu

 

CUF kwa kususia habari zake, japo kwa kipindi fulani cha mwaka mpaka uongozi wake

 

utakapoheshimu taaluma na wanataaluma ya habari.

Kama chenyewe katika moja ya kauli mbiu yake ni ‘haki sawa kwa wote’, iweje chama

 

hicho kishindwe kuheshimu uhuru na haki ya wanahabari kuandika na kupasha habari

 

jamii?

Kwa heshima na taadhima, ninawaomba wanahabari tuache unafiki na tufuate kanuni

 

za msumeno, ambao unakata huku na huku kwa kuiadhibu CUF kwa kuacha kuandika au

 

kutangaza habari zao, achilia mbali ati kupokea fidia!

Vinginevyo, kuendelea kuandika na kutangaza habari za CUF tena kwa kuona kama

 

matukio yale yalifanywa kwa bahati mbaya, tunakifanya chama hicho kizidi kuwa

 

‘nunda’, na tusije tukashangaa ya baadaye, kwani ‘mchelea mwana kulia hulia

 

yeye’!

Alamsiki!