UHURU 15.10.2005

 

Mkapa: Chama chochote kisithubutu kutangaza ushindi kabla tume

Na Lauden Mwambona, Singida

RAIS Benjamin Mkapa amevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30 mwaka huu, kutothubutu kujitangazia ushindi kabla ya Tume husika kutoa matokeo hayo.

Hali kadhalika Rais Mkapa amewataka watazamaji wa uchaguzi wa ndani na nje pamoja na vyombo vya habari kutodiriki kuotea na kutangaza ushindi kwa chama chochote la sivyo chama au mtu atakayetangaza ushindi ataona cha mtema kuni.

Mkapa alitoa kauli hiyo nzito jana alipohutubia wananchi wa mkoa wa Singida waliofurika kwenye uwanja wa Namfua kusherehekea kilele cha mbio za Mwenge wa UHURU mwaka huu ambapo Radio Tanzania ilitangaza moja kwa moja.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Rodney Phillips. Rais Mkapa pia alitumia muda huo kuwaaga wakazi wa mkoa wa Singida katika nafasi yake ya Urais.

‘’Baada ya uchaguzi, wananchi tunapaswa kuwa watulivu na kuyapokea matokeo ya uchaguzi yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar,’’ alisema Rais Mkapa na kuongeza kwamba hao ndio pekee wenye madaraka kisheria ya kutangaza matokeo ya uchaguzi.

Alisema kila chama na kila mgombea wameingia kwenye uchaguzi huo wakijua sheria hiyo na utaratibu huo.

Rais alionya kwamba serikali haitapenda kusikia sauti ya mtu yeyote akitangaza matokeo ya uchaguzi kinyume cha sheria, kwa sababu hali hiyo inaweza kuwa chanzo cha kuleta vurugu kubwa nchini.

‘’Ni jambo la hatari sana, Ni shimo kubwa lililo mbele yetu ambalo hatuna budi kulikwepa hasa kwa vile tumeliona mapema’’ alisema .

Rais alitoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa kuwaasa wafuasi wao wakwepe mizengwe, hila na njama za kuwazuia watu kupiga kura kwa kutishia usalama hususan kwa wazee na wanawake.

‘’Naagiza vyombo vya ulinzi vijiweke tayari kumuwahi yeyote atakayeandaa au kujaribu kutekeleza mipango ya namna hiyo’’ alisema na kusisitiza kwamba anataka uchaguzi uwe huru na wa haki katika mazingira ya utulivu.

Lakini alisisitiza kwamba kauli yake hiyo ni nasaha, lakini hatasita kuigeuza amri itakapoonekana umuhimu wa kufanya hivyo.

Alisema suala la kufanikisha uchaguzi mkuu ni la kila mdau vikiwemo vyama vya siasa, taasisi, vyombo vya habari, serikali, dini na mashirika ya ndani na nje.

Akizungumzia umuhimu wa Mwenge wa UHURU, Rais Mkapa alisema Mwenge huo ni mali ya Watanzania wote vikiwemo vyama vya siasa vyote, wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara na kwamba lazima uenziwe na utakimbizwa kila mwaka.

Alisema Mwenge wa UHURU ni alama muhimu kwa taifa na kwamba ndio maana umewekwa kwenye nembo ya Taifa, Nembo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki Kuu ya Tanzania, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na katika Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

‘’Duniani Kote Mwenge unachukuliwa kama ishara ya matumaini, ndio maana upo mwenge wa amani na mwenge wa Olimpiki ambayo inakimbizwa na kupewa heshima duniani kote’’ alisisitiza.

Alisema kwa Tanzania Mwenge wa UHURU unapokimbizwa unasaidia kuhamasisha wananchi kuongeza kasi ya kutekeleza miradi yao ya maendeleo na kujenga mshikamano wa kitaifa. 

Ujumbe wa Mwenge wa UHURU mwaka huu ulikuwa kuhamasisha masuala ya uchaguzi na kuendeleza vita dhidi ya ukimwi.

 

Wagombea ubunge wawili Chadema wajitoa

Wadai hakiwajali huku Mbowe akiranda na helikopta

Na Omari Shaaban, Arusha

CHAMA cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kubomoka baada ya wagombea wake wawili wa ubunge wa majimbo ya Monduli na Mtera kuondoka kwa sababu chama hicho hakiwajali huku Mwenyekiti wao Freeman Mbowe akiranda na helikopta.

Mgombea Ubunge huyo ambaye alithibitisha mwenyewe kujiengua Chadema na kuhamia CCM mbele ya mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Monduli jana, ni Keloi Ole Mandoru, ambaye alikuwa nguzo ya Chadema jimbo hilo.

Diwani wa Chadema kata ya Engutoto Amos Saruni Mollel, aliungana na madiwani wenzake wawili wa chama cha wananchi CUF, Sapuru Kairo (Monduli Juu) na Jamhuri Mollel (TLP) (Monduli mjini), kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza sababu za kujiengua Chadema na kuingia CCM, aliyekuwa mgombea ubunge wa Chadema jimbo la Monduli, Mandaro alisema kuwa Chadema haiwajali wagombea wake wa ubunge, udiwani na wananchi.

Alisema kuwa mgombea urais wa chama hicho, Freeman Mbowe, anazunguka na helkopta angani badala ya kutembelea wananchi, hali inayosababisha chama hicho kutokubalika kwamba kitaweza kuwasaidia wananchi.

Alitaja sababu nyingine kuwa sera nyingi za Chadema hazitekelezeki, na hivyo kuungana na CCM, ambako sera zake zinaeleweka na kutekelezeka na kutolea mfano sera za CCM zilikuwepo kwenye awamu ya tatu ambazo zimetekelezeka, kama vile elimu na mengineyo.

“Hatuwezi kuendelea kuwa hoi…na kuumia zaidi kwa kitu ambacho hakina manufaa kwa wananchi…kwa hiyo narudi kwa wazazi CCM….kutekelezeka mema kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema Mandaro.

Akizungumzia suala hilo mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Monduli, Onesmo Nangole alisema kuwa hiyo inaonyesha ni kiasi gani sera za CCM zinavyowavutia wengi na sababu kubwa ni kwamba zinatekelezeka.

Alisema kuwa CCM itashinda kwa kishindo kwa mbunge wa jimbo hilo, Edward Lowassa kutokana na kukubalika kwake kama ‘mtu wa maendeleo jimboni humo’ na pia katika nafasi ya urais wananchi wa Monduli watampa kura zote Jakaya Kikwete wa CCM.

Naye mwenyekiti wa kampeni Monduli, David Pero alisema kuwa mpaka sasa CCM inayo madiwani wa tano ambao wamepita bila kupingwa, ambao ni wa kata ya Monduli Juu, Engutoto, Mto wa Mbu, Esilalei, Loksale kati ya kata kumi na moja za jimbo hilo.

Naye Esther Katua, anaripoti kuwa mgombea Ubunge Jimbo la Mtera mkoani Dodoma kwa tiketi ya Chadema Lusinde Joseph, amejitoa kugombea kiti hicho na kujivua uanachama kwa kile alichodai mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe anakiendesha kibabe.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwenye ofisi za Uhuru jana, Joseph alisema aliamua kwa hiari yake kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kutumia katiba ya chama chake ya mwaka 2004 ukurasa wa 7 kifungu cha 5.4.1 kinachotoa haki ya mwanachama kujiuzulu mwenyewe kwa hiari yake.

“Nachukua uamuzi huu mzito kwangu na kwa taifa maana nimepoteza haki kuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Mtera. Inauma sana, ni kama mgonjwa anayefanyiwa upasuaji hujisikia maumivu makali lakini baada ya ugonwja kutolewa hupona na kurudi kwenye hali nzuri ndivyo nilivyo sasa,” alisema Joseph.

Akifafanua kile anachodai kuwa ni ubabe wa Mbowe, Joseph alisema kuwa ni pamoja na kutumia nguvu kupitisha hoja alizoziita za hatari kama kupunguza muda wa kukaa madarakani hivyo kuwafanya viongozi wote wa chama hicho kuwa wa muda.

Alidai kwa mujibu wa hoja hiyo ambayo imepitishwa kwenye kikao cha Baraza Kuu la chama lililofanyika Agosti 11 na 12 kwenye ukumbi wa P.T.A, Chadema haina mgombea uchanguzi katika ngazi yoyote kwani viongozi wake wote ni wa muda na sheria hairuhusu chama chenye viongozi wa muda kushiriki uchanguzi mkuu.

 

Wandwi ahojiwa na polisi Musoma

Adaiwa kuongoza maandamano ya CUF

Na Peter Orwa, Musoma

MGOMBEA ubunge wa jimbo la Musoma Mjini kwa tiketi ya CUF, Mustapha Wandwi na wafuasi wake 17, wanahojiwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na ghasia zilizotokea mjini hapa mara baada ya mkutano wake wa kampeni juzi jioni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Kapita Mwaruka alisema jana kuwa, sambamba na Wandwi, kati ya waliokamatwawamo viongozi wengine wawili ambao hakuwataja, ambapo wanaendelea kuhojiwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni.

Mwaruka alisema ghasia hizo zilitokea katika eneo la Kitangi baada ya wafuasi wamgombea kuanza kuandamana naye huku polisi ikiwa imeshapiga marufuku maandamano baada ya mikutano ya kampeni Hili ni tukio la pili, ambapo Jumanne wiki hii kulitokea ghasia kama hizo katika eneo la Nyasho napolisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kama ilivyokuwa katika tukio la juzi.

Mwaruka alisema katika tukio la kwanza wafuasi hao wa CUF waliingia mitaani na kuandamana baada ya mkutano wa kampeni, licha ya kuamriwa wasifanye hivyo.

Siku hiyo Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM Dk. Ali Mohamed Sheni alihutubia katika mkutano uliofurika mamia ya wakazi wa mji huu.

Alisema baada ya tukio la kwanza Jumatano iliyopita, Mkuu wa Mkoa Balozi Nimrod Lugoye alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mjini, Ernest Kahindi, kuitisha mkutano wa vyama vya CCM na CUF, ambavyo vinaonekana vina mvutano mkubwa mjini hapa, ambapo walikubaliana kuridhia maadili ya kampeni za uchaguzi.

Mwaruka alisema, siku moja tu baada ya maridhiano hayo yaliyohudhuriwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Musoma, Vitus Molele,CUF waliamua kukaidi, ambapo Wandwi aliamuru mkutanoni wafuasi wake waandamane.

Alisema, licha ya Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), kuwakataza kuandamana, Wandwi ambaye ni Kamanda wa

Polisi wa Mkoa mstaafu na alishawahi kuwa kiongozi wa NCCR-Mageuzi aliwaongoza kukaidi amri hiyo.

Wakati Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) wakidhibiti ghasia hizo, baadhi ya wafuasi wa CUF walitupia mawe gari la FFU, ambao walitumia mabomu ya machozi kuwadhibiti kabla ya maandamano hayajaenda mbali.

Mwaruka alisema baada ya tukio la Jumanne iliyopita, Wandwi alishikiliwa na kisha kuachiwa kwa dhamana, ili aweze kuendelea na kampeni zake za kisiasa.

Kamanda alisema, Polisi inashangazwa na utetezi uliojitokeza kwa baadhi ya waandamanaji waliodai mara

ya kwanza kuwa walifanya hivyo kumsindikiza mgombea wao, wakati kwake ni jirani umbali wa mita 500, eneo la Nyasho.

Kufuatia matukio hayo, Kamanda huyo ametoa onyo kwa mashabiki na wapenzi wote wa kisiasa kuendesha kampeni za kistaarabu zenye kuzingatia sheria na maafikiano ya maadili ya uchaguzi wa vyama kitaifa.

"Atakayeleta fujo tutamshughulikia kikamilifu, bila ya kujali anatoka chama gani," alionya Kamanda Mwaruka.

Kuhusu hali ya kampeni za kisiasa kimkoa, alisema ni shwari na amezunguzia tukio la kuuawa kwa balozi mmoja wa CCM huko Tarime, kuwa ni tukio linaloendana na mazingira ya ulevi kwani lilitokea kilabuni na walikamata lita 25 za pombe haramu ya gongo.

 

 

 

 

Huu ndio msimu wa mwisho wa CUF - Kikwete

Na Dunia Mzobora, Kwimba

MGOMBEA Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, amewataka wananchi kuachana na chama cha CUF kwa kuwa huu ndio msimu wake wa mwisho.

Alisema hayo jana katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Ngudu kwenye makao makuu ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Alisema CUF ni chama cha msimu kama ilivyo fasheni za mitindo mbalimbali, na kwamba wananchi hawana budi kuachana nacho kwa kuwa kitapita.

“CUF ni chama cha msimu kama fasheni, achaneni nacho,” alisema Kikwete na kuongeza kiko wapi NCCR-Mageuzi chini ya Augustine Mrema?

Alisema kwa kuwa CUF ni chama cha msimu, na CCM ina uhakika wa ushindi katika uchaguzi mkuu ujao, Lipumba hana budi kurudi darasani akafundishe.

Aliuambia umati wa wananchi waliojitokeza kumpokea katika jimbo hilo kwamba wananchi wasibabaike wala kubabaishwa na vyama vya upinzani ambavyo vingine havina hata tarehe yake ya kuanzishwa wala anuani zake hazijulikani.

Mgombea ubunge jimbo la Kwimba, ambaye pia ni Nibu Wziri wa Elimu na Utamaduni, Bujiku Sakila alisema wananchi wa jimbo hilo wana imani kubwa na mgombea urais wa CCM na kwamba wataichagua CCM kwa heshima zote.

“ Wananchi wengine walidhani mgombea Urais Kikwete amekuja na karatasi za kupigia kura ili wamhakikishie imani yao kwake na CCM,” alisema Sakila.

Wakati huo huo Katika mkutano wa kampeni juzi katika jimbo la Magu, Kikwete aliwataka wananchi kuachana na chama kilichoazima mwenyekiti.

“Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ameazimwa…chama si chake, mwenye chama ni Katibu Mkuu Seif Shariff Hamad,” alisema Kikwete.

Alisema kwa kuwa chama ni cha Seif, Lipumba anaweza kung’olewa wakati wowote tofauti na CCM ambayo si chama cha mtu mmoja ni cha watu wote.

Kikwete aliwaambiwa wana Magu kwamba chama kitakachohakikisha maslahi na maendeleo yao kwa ari, nguvu na kasi mpya ni CCM, na kwamba kuchagua vyama vya upinzani ni kurudisha nyuma maendeleo kwa ari, kasi na nguvu mpya.

Kuhusu ufugaji, sekta ambayo inachukua nafasi kubwa katika Kanda ya Ziwa, Kikwete alisema serikali ya awamu ya nne itahakikisha inamuondoa mwananchi, hasa mfugaji kutoka kwenye uchungaji kwenda ufugaji.

“Tunataka tutoke kwenye maisha ya uchungaji ili tuwe wafugaji…kwenye kuchunga mfugaji hanenepi wala ng’ombe hanenepi”.

Lengo ni kuwawezesha wananchi wafuge katika maeneo wanayoishi badala ya kusafiri umbali mrefu kutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao.

Alisema kwa kufanya hivyo kutawawezesha wafugaji kuwa na ng’ombe bora watakaotoa nyama na maziwa mengi, na kwamba wafugaji nao wataweza kufaidika na mifugo yao.

Sambamba na hilo alisema serikali itahakikisha malambo na mabwawa yanaongezwa na kuimarishwa pamoja na kuhakikisha dawa zinawafikia wafugaji kwa wakati.

 

 

…Nichagueni niongeze kasi ya maendeleo

Na Selema Bitala, Magu

Mgombea Urais wa Jamuhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete, amewaomba wananchi wa Magu wamchague yeye Oktoba 30 ili aweze kusafisha “mchwa” walao noti katika kuongeza kasi ya maendeleo.

Alisema wakimchagua yeye wameichagua CCM, na endapo Chama chake kitapewa ridhaa ya kuwaongoza ana wahakikishia fursa nyingi zaidi za maendeleo zitapelekwa vijijini ambako asilimia 80 ya Watanzania wanaishi, huku

mazingira ya miundombinu mingi ikiwa haijaimarishwa.

“Mkinichagua kuwa rais wenu tutapeleka fedha nyingi za maendeleo kwenye halmashauri zenu, na mfuko wa barabara utaongezewa fedha kwa sababu nimepita

mwenyewe na kuona barabara zilivyo, hali ni ngumu kwa hivyo nawaahidi tutaziboresha na hao mchwa wanaokula noti tutatafuta dawa ya kuwaua mchwa hao,” alisema.

Aliwambia awamu ya nne itazingatia kumkwamua Mtanzania wa kawaida kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwasogezea huduma za umeme vijijini, na kuhakikisha

ifikapo mwaka 2010 huduma za maji safi na salaam, mjini na vijijini zinapatikana kwa asilimia 90 nchi nzima.

“Nawashangaa hawa watu wengine wanaopitapita huko na kusema hadi sasa CCM toka uhuru haijafanya lolote huku wao wakiwa wamesoma bure na wanapobandika matangazo yao wanabandika kwenye nguzo za umeme na simu, wanapolala hoteli usiku wana mulikiwa na umeme, wanaongea na simu hata wakiwa bafuni, lakini

bado wanasema haijafanya chochote,” alisema.

Ichagueni CCM, safari hii shabaha yetu kuu inalenga kuongeza uchumi, maisha bora kwa Watanzania ambapo mapango wetu utakuwa ni kuendeleza kilimo, uvuvi

na mifugo ambayo ndiyo inayotoa ajira kwa Watanzania wengi, na kuondoa kodi kwenye dawa za kinga na tiba kwa mifugo, ushuru wa mbolea na kuwaletea pembejeo za kisasa.

Alisema CCM ina sera ambazo zinajenga utaifa, kuinua uchumi, utulivu na usalama na kuleta maendeleo ya Watanzania, lakini wapo wengine sera zao zinaangalia dini zao na za kugawana rasilimali, ambapo kama mlima Kilimanjaro upo Moshi, basi wafaidike wachaga, samaki dhahabu na almasi za Mwanza, basi wafaidike nazo wasukuma.

Kikwete alisema sera hizo ‘hazitatufaa’ kitaifa bali kutugawa kwa sababu sioni zitatufikisha wapi.

 

Rita aahidi kuwaletea Kawe Chuo cha Ufundi

Na Khalfan Hango na Sosteness Isengwa wa RCJ

MGOMBEA Ubunge jimbo la Kawe kwa tiketi ya CCM, Rita Mlaki, amesema akichaguiliwa kuwa mbunge atalipatia jimbo hilo chuo cha ufundi stadi kinachotambuliwa na VETA.

Rita alitoa ahadi hiyo wakati akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika juzi Tegeta, katika jimbo hilo jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya watu waliokuwa na shauku ya kumsikiliza, Rita alisema vilevile akichaguliwa atahakikisha anawatafutia wananchi wa jimbo hilo mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kujikwamua kutoka katika umaskini unaowakabili.

Rita aliyekuwa akishangiliwa mara kwa mara na wananchi aliahidi pia kuwa akichaguliwa atahakikisha linajengwa soko la kisasa katika eneo la Tegeta.

"Mkinichagua nitahakikisha mnajengewa soko zuri ili muondokane na adha hii ambapo mnakaa barabarani na kuhatarisha maisha yenu kwa kuwa mnaweza kugongwa na na magari,' alisema.

Akieleza mafanikio aliyoonyesha katika kipindi chake cha Ubunge kilichopita, Rita alisema, amefanikisha kujengwa shule sita na kuongezwa madarasa 33 katika kata ya Kunduchi.

Kuhusu suala la maji, Rita alisema, tatizo lake limepunguzwa kwa kiasi kikubwa ambapo sasa jimboni zinapatikana lita milioni 25 za maji kwa siku.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea Udiwani, kata ya Kunduchi, Patrick Makoyola alisema kuwa endapo wananchi watampa kura atahakikisha anaboresha miundombinu, elimu, maji na michezo katika kata hiyo.

Makoyola ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tegeta alisema kiu yake kubwa itakuwa katika kuboressha hasa mchezo wa soka hadi kuhakikisha timu katika kata hiyo zinakuwa katika viwango vya ligi kuu na pia wanafunzi wenye vipaji kuendelezwa hadi kidato cha sita.

Alisema mfano mkubwa unaoonyesha kuwa akiwa diwani atasukuma mbele maendeleo katika nyanja mbalimbali ni jinsi alivyofanikiwa kuifanya shule yake kuwa na wanafunzi wengi wenye kufaulu vema masomo na wanamichezo bora.

 

 

Warioba asema Kikwete, Sheni ni chaguo sahihi

Na Peter Orwa, Buhemba, Mara

WAZIRI Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba, amesema anawafahamu fika mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete na Mgombea Mwenza Dk. Ali Mohammed Sheni, hivyo ni chaguo sahihi la Watanzania katika uchaguzi mkuu ujao.

Warioba alisema hayo alipowasalimia wananchi na kuwanadi wagombea wa CCM, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika juzi mchana katika kijiji cha Byatika, kata ya Buhemba jimbo la Musoma Vijijini.

Aliwaambia wananchi wa kijiji hicho alichowahi kuishi akiwa mwanafunzi, kwamba CCM imefanya mengi ya mfano

akitoa mfano wa zama hizo hakukuwa na sekondari hata moja mkoani Mara na walienda kusoma katika shule ya

Bwiru Mwanza, na sasa ziko takriban 100 na nyingine zinaendelea kujengwa.

Warioba alisema, kwa jinsi ambavyo wamempitisha bila ya kupingwa mbunge Nimrod Mkono aendelee kuwatumikia

kwa miaka mitano, pia alitaka ifanyike hivyo hivyo kwa diwani Pitalis Odero na mgombea Urais.

Naye Mgombea Mwenza, Dk. Sheni, binafsi alimtaja Kikwete kama 'mtu mahiri' na mzoefu na mwenye uwezo

wake siku nyingi tangu yeye (Dk.Sheni) akiwa Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kuhusu maendeleo ya wananchi wa Buhemba, Dk. Sheni alisema serikali ya awamu ya tatu katika kipindi cha

miaka 10 iliyopita imefanikisha maendeleo, kiasi cha kata ya Buhemba kuvuka lengo la chanjo ya watoto

kitaifa kwa kuwa na asilimia 98, dhidi ya asilimia 90 zilizolengwa.

Dk. Sheni, aliyeambatana katika mkutano huo na mkewe Mwanamwema, pia mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa,

Mwita Gachuma, alisema mwaka 1995 chanjo hiyo ilikuwa ya wastani wa asilimia 30 tu ya watoto wote.

Aidha, alitaja mafanikio ya kiwilaya kwa zaidi ya wastani wa asilimia 50 katika maeneo mbalimbali ya

elimu ikiwa ni pamoja na uandikishaji wa wanafunzi, kutengeneza madawati, ujenzi wa madarasa na nyumba za

walimu.

"Kama alivyosema Mzee wetu Warioba, mwaka 1960 hakukuwa na shule, leo hii Buhemba kuna sekondari

mbili, haya ndio mandeleo," alisema na kuhoji kauli za wapinzani wanaoibeza CCM kuwa haijafanya lolote

akisema: "Mwaka 1960, hakukuwa na umeme hapa, leo hii kuna umeme, Mungu awape nini? Suala la umeme maana yake ni maendeleo".

Pia, mgombea huyo mwenza alitangaza azma ya serikali ijayo ya CCM, kumaliza migogoro baina ya wachimbaji wadogo na wakubwa na kuahidi azma ya serikali kuendelea kukaribisha wawekezaji katika sekta hiyo.

Aliwaambia wakazi wa Buhemba, ambako pia kuna machimbo ya dhahabu kuwa serikali kupitia sera ya madini itahakikisha kuwalipa fidia wachimbaji wadogo pindi maeneo yao yanapochukuliwa na wachimbaji wakubwa kwa njia ya mapatano.

Kwa mujibu wa Dk. Sheni, kupitia sera hiyo utawekwa mkazo wa kuboresha thamani ya madini yanayosafirishwa kutoka asilimia 0.3 ya dhahabu inayochimbwa hadi asilimia tatu. Alisema, hadi sasa nchini kuna migodi mikuu mitano ambayo inaipatia taifa fedha nyingi.

Baada ya hapo, mgombea huyo aliendelea na mkutano mwingine katika kijiji cha Kitingi, kata ya Murangi kandokando ya Ziwa Victoria, ambapo mbunge Nimrod Mkono aliungana naye na alikuwa kivutio kwa sera yake ya 'mkono kwa mkono' yaani wananchi waanze halafu yeye anasaidia kumalizia.

katika mkutano huo, Dk. Sheni aliitetea sera ubinafsishaji wa mashirika ya umma kuwa umeleta ufanisi, huku akitoa takwimu na kupinga propaganda zinazoendelezwa na baadhi ya vyama vya upinzani akisema:

"Wapinzani wanatusema tunauza nchi, hawa ni watu wa ajabu sana! Umeona wapi mtu akauza nchi? Yote hayo tuliyasema katika ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 1995."

Aliongeza kuwa, katika ubinafsishaji wa mashirika hayo asilimia 70 ya hisa za mashirika hayo yanamilikiwa na Watanzania ama kwa ubia na wageni au kumiliki sehemu ya hisa hizo.

Baada ya kukamilisha ziara yake mkoani Mara, jana aliingia Kagera kuendelea na mikutano yake ya kampeni.

 

Ali Ameir asema hahusiki

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Donge huko Zanzibar anayemaliza muda wake, Ali Ameir Mohammed, hakuwaongoza waandishi wa habari kwenda kupokea msimamo wa wazee wa jimbo lake la uchaguzi kuhusiana na vurugu za hivi karibuni na mustakabali wa mikutano ya wapinzani.

Katika habari iliyoandikwa na mwandishi Mwinyi Sadalla kutoka Zanzibar juzi, na kuchapishwa na gazeti hili jana, ilielezwa Ali Ameir ndiye aliyewaongoza waandishi hao kwenda kwa wazee hao.

“Hakuna kitu kama hicho, mimi sijafanya. Niwaongoze kama nani, mie sihusiki cho chote na vyombo vya habari,” alisema mbunge huyo jana.

Alisema kama wangesema ni mmoja wa wazee hao, ingewezekana kwa sababu ‘mimi ni mbunge wao’, lakini sikufanya hicho walichoandika.