UHURU 15.11.2005

 

 

Nahodha awaasa Wawakilishi waache malumbano yasio na faida kwa wananchi

Na Khatib Suleiman,Zanzibar.

WAZIRI Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha

 

amewataka Wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kuwatumikia katika maeneo ya

 

majimbo ya uchaguzi na kuacha kuendeleza utashi wa kisiasa wa malumbano

 

yasiyokuwa na faida yeyote.

Akiliahirisha Baraza la Wawakilishi hadi Januari 18 mwakani, Shamsi alisema

 

Wawakilishi wanapaswa kuyafahamu vyema majukumu yao yanayowapa uhalali wa kuwa

 

Wawakilishi katika majimbo ya uchaguzi Unguja na Pemba.

'Huu sio wakati tena wa kuendeleza utashi wa kisiasa wa malumbano yasiyokuwa na

 

msingi,” alisema Shamsi na kuwa kazi kubwa inayowakabili wajumbe hao ni

 

kuwahudumia wananchi kwa kuwapelekea maendeleo.

Alisema tabia ya kambi ya upinzani ya chama cha CUF kususia vikao vya Baraza la

 

Wawakilishi pamoja na kutangaza kutomtambuwa Rais wa Zanzibar aliyechaguliwa

 

kutokana na ridhaa ya wananchi wa Unguja na Pemba ni kwenda kinyume na dhana

 

nzima ya demokrasia ya utawala bora na katiba.

Aliongeza kuwa katika dhana ya demokrasia na utawala bora, siku zote imekuwa

 

ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu nguvu ya umma inayotokana na ridhaa ya wengi na

 

kitendo cha kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu yanayotokana na ridhaa ya wengi ni

 

sawa na udikteta.

Shamsi aliwataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kufuatilia kwa karibu matatizo

 

na shida zinazowakabili wananchi katika majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya

 

kuyapatia ufumbuzi.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka katika kambi ya CUF walihudhuria kikao na

 

walikuwepo muda wote wa hotuba hiyo ya kuahirisha kikao cha Baraza la

 

Wawakilishi.

Mapema Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho alimuapisha mjumbe wa

 

Baraza hilo aliyeteuliwa na Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume kupitia nafasi

 

kumi za rais ambaye ni Hasnuu Mohammed Haji kutoka Pemba.

 

Maofisa wa polisi mipakani wapatiwa mafunzo maalum

Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi, Arusha

MAOFISA wa polisi wanaofanya kazi katika maeneo ya mipakani hapa nchini wameanza

 

kupatiwa mafunzo maalumu juu ya madhara yatokanayo na mionzi na jinsi ya

 

kukabiliana na matukio yatokanayo na nguvu za Atom.

Mafunzo hayo ambayo yanafanyika mjini Arusha na kufadhiliwa na Shirika la Polisi

 

la Kimataifa (Interpol) na kamisheni ya nguvu za Atom ya Uingereza pia

 

yanawashirikisha baadhi ya waendesha mashitaka na maofisa wa Jeshi la Wananchi wa

 

Tanzania.

Akifungua mafunzo hayo jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini

 

Kamishna Adadi Rajabu, alisema mafunzo hayo yatawezesha wapelelezi kubaini jinsi

 

ya kukabiliana na matukio ya mionzi hasa katika maeneo ya mipakani.

Alisema mionzi imebainika kuwa inaweza kutumiwa na magaidi kama silaha za

 

maangamizi hivyo polisi imeonelea ni muhimu kutoa mafunzo kwa watendaji wake ili

 

kuweza kukabiliana na matukio kama hayo pindi yanapotokea.

Hii ni mara ya pili kwa mafunzo kama hayo kutolewa kwa watendaji wa vyombo vya

 

ulinzi na usalama hapa nchini.

Mafunzo ya awali yalifanyika Septemba mwaka huu na kuwashirikisha maofisa wa

 

vyombo vya ulinzi na usalama kutoka nchi za Afrika Mashariki.

Wakitoa maoni yao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema yatawasaidia sana

 

kuelewa aina ya mionzi na jinsi ya kukabiliana nayo.

Washiriki wa semina hiyo ni kutoka mikoa ya Rukwa, Kigoma, Kagera, Dar e s

 

Salaam, Mtwara, Kilimanjaro, Tanga na Arusha.

 

Mbinu za kutafuta soko kikwazo kwa wafanyabiashara nchini

Na Solomon Mwansele, Rungwe

BIDHAA zinazozalishwa nchini zinakidhi mahitaji na viwango vya kuweza kushindana

 

katika soko la kimataifa, lakini tatizo linalowakabili

wazalishaji wa Tanzania ni ukosefu wa mbinu za kutafuta masoko.

Hayo yalisemwa na meneja wa SIDO mkoani Mbeya Tresphur Mubito, wakati wa kufunga

 

mafunzo ya wiki tatu ya usindikaji wa vyakula na matunda katika wilaya ya Rungwe

 

mkoani Mbeya.

Mubito alisema uchumi wa Tanzania hauwezi kukua kama inavyotarajiwa endapo

 

wazalishaji hawatapatiwa mbinu na mafunzo ya kutosha jinsi ya kuingia katika soko

 

la kimataifa kwa ajili ya kuuza bidhaa wanazozalisha hapa nchini.

"Zikizalishwa bidhaa bora ni rahisi kupata masoko ya uuzaji wa bidhaa hizo nje ya

 

nchi, wafanyabiashara wanapaswa kutengeneza bidhaa kulingana na mahitaji ya soko

 

katika nchi jirani," alisema Mubito.

Aliwataka wahitimu hao kuwa wabunifu wanapotengeneza bidhaa zao kulingana na

 

mahitaji ya soko badala ya kung'ang'ania kutengeneza aina moja ya bidhaa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Rungwe Masanga Buliga,

 

alisema kuwa usindikaji huo utaongeza thamani na kuhamasisha uzalishaji wa mazao

 

ya kilimo ambayo yatapata soko la uhakika kwa wakulima kutokana na mazao hayo

 

kuhitajika katika usindikaji.

Buliga alisisitiza usindikaji huo ufanyike kwa makini na kuhakikisha bidhaa hizo

 

zinatengenezwa kwa viwango bora kwa kuzingatia afya ili zisilete madhara kwa

 

watumiaji hali ambayo inaweza kuharibu soko.

Mkurugenzi huyo alisema mikopo kwa ajili ya vikundi vya vijana, wanawake, watu

 

wenye ulemavu na wazee inatolewa na halmashauri hiyo.

Alibainisha kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa watu waliojiunga katika vikundi na

 

walio na nia ya dhati ya kuanza uzalishaji kwa lengo la kuondokana na umasikini.

Kwa upande wao, wahitimu wa mafunzo hayo walisema ukosefu wa mitaji unachangiwa

 

kwa kiasi kikubwa na masharti magumu ya kupata mikopo na kuwa wazalishaji wadogo

 

wengi wanashindwa kumudu kukopa hivyo kushindwa kuanza uzalishaji.

Walisema inahitajika elimu ili waweze kuzithamini na kununua bidhaa za ndani ili

 

kukuza na kuinua pato la mwananchi wa kawaida na hatimaye taifa.

Katika mafunzo hayo ya wiki tatu,baadhi ya mambo yaliyofundishwa ni pamoja na

 

ujasiliamali, makundi ya vyakula, usindikaji wa unga wa lishe, sosi ya pilipili

pamoja na afya na ubora wa vyakula.

Mafunzo hayo yalikuwa na washiriki 25 kutoka kata za Bulyaga, Bagamoyo, Katumba,

 

Mpuguso, Masoko na Kandete.

 

 

 

Karume: SMZ kuwa makini katika utekelezaji wa Ilani ya CCM

Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Zanzibar) Rais Amani Abeid Karume

 

amesisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itakuwa makini katika

 

utendaji na utekelezaji wa sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka

 

mitano ijayo kuanzia mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu mjini Zanzibar ilisema Rais Karume ameeleza hayo

 

jana alipofanya mazungumzo na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM Zanzibar,

 

huko Ikulu.

"Utendaji wa majukumu ya viongozi serikalini pamoja na utekelezaji wa sera na

 

Ilani ya Uchaguzi ya 2005-2010 ya CCM ni changamoto kubwa ilinayokabili Serikali

 

hivi sasa," alisema Makamu Mwenyekiti huyo.

Alikumbusha kuwa wawakilishi wana dhamana kubwa waliyokabidhiwa na wananchi

 

ambapo wanatakiwa kutekeleza Ilani iliyotokana kwa mujibu wa mkataba kati ya CCM

 

na wananchi.

Akihimiza suala hilo katika mkutano huo, Rais Karume alisema: " Tuna dhamana

 

kubwa tuliyopewa na wananchi... kila mmoja mkiwa katika nafasi za uongozi, ndani

 

au nje ya baraza tujitahidi kama inavyowezekana kusimamia utekelezaji wa sera na

 

Ilani ya CCM."

Alisisitiza kuwa wajumbe wa baraza wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwafunza

 

na kuwaelimisha wajumbe wa kambi ya upinzani kutokana na udhaifu wao katika

 

baraza hilo ambapo upinzani unaendeleza tabia ya kususia vikao jambo ambalo

 

linapingana na taratibu na misingi ya demokrasia.

Karume alisema ni muhimu kuelewa kuwa nguvu kubwa ya ushindi na uimara wa CCM

 

unatokana na utekelezaji wa sera za umoja, mshikamano, amani na utulivu, pamoja

 

na ushirikiano kati ya wananchi na viongozi na kwamba hiyo ndiyo sababu kubwa ya

 

ushindi wa CCM kwa miaka yote.

"Tuchukue dhamana ya kuwasomesha wapinzani wetu na kuwafahamisha taratibu za

 

demokrasia kwa kutumia busara na hekima bila ya malumbano na kuweza kuimarisha

 

ushirikiano ndani ya baraza," alisisitiza Karume.

"Katika utawala wa demokrasia mambo muhimu ya kuyadumisha ni utekelezaji wa

 

shughuli za serikali kwa mujibu wa Katiba, sheria za nchi na kuheshimu dhamana ya

 

taasisi za demokrasia zilizoanzishwa nchini, aliongeza Rais Karume.

Alieleza kuwa pamoja na juhudi zilizochukuliwa na chama tawala za kuanzisha

 

mazungumzo ya Muafaka wa kwanza na wapili, bado upinzani haujabadilika na

 

unaendelea na tabia ile ile ya kususia na kukiuka taratibu za msingi za mfumo wa

 

demokrasia.

 

 

Mgombea Mwenza wa CHADEMA atambulishwa rasmi

Ni Anna Valeria Komu

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kilimtambulisha rasmi mgombea

 

mwenza wake, Anna Valeria Komu kwa waandishi wa habari.

Utambulisho huo ulifanyika mbele ya viongozi wa chama akiwemo Mwenyekiti na

 

Mgombea Urais, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, katika makao makuu

 

ya chama hicho, Kinondoni Dar es Salaam.

Anna ni mzaliwa wa Kwabijokha Zanzibar, mwaka 1950 na jina lake la awali lilikuwa

 

ni Maulida Abubakary. Alibadili dini na jina na kuwa Anna, baada ya kuolewa na

 

Valerian Komu, mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa muhtasari wa wasifu wake, Anna ni miongoni mwa waasisi wa chama

 

hicho na alianza na uongozi katika ngazi ya chini kabisa, akiwa katibu wa tawi

 

huko Mawela, Uru Moshi.

Baadaye alipanda na kuwa katibu wa wilaya ya Moshi na kukwea ngazi hadi Katibu wa

 

mkoa wa Kilimanjaro na akateuliwa kuwa Kaimu Katibu Mwenezi wa CHADEMA Taifa.

Ameshashika vyeo vya Naibu Mkurugenzi wa Wanawake, pia kukaimu nafasi hiyo mwaka

 

jana.

Akizungumzia malengo yake iwapo atabahatika kuingia Ikulu kama Makamu wa Rais,

 

Anna alisema lengo lake ni kuona mapinduzi makubwa katika suala la maendeleo ya

 

wanawake.

Pamoja na malengo hayo, ameeleza kuridhika na hatua iliyofikiwa sasa hivi, ambapo

 

wanawake wengine wamejitokeza katika kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa.

Mgombea mwenza huyo anayesubiri kuthibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),

 

alisema hali ya wanawake wa kawaida bado wana maisha magumu mno na kuna haja ya

 

kuwepo kwa mikakati ya kuwainua.

Kabla ya kujiunga na CHADEMA alikuwa mwana CCM mwanzilishi na kabla ya hapo,

 

harakati za siasa alianza akiwa katika kundi la vijana chipukizi wa chama cha ASP

 

na baadaye akawa mwanachama kamili.

Ameolewa na ana watoto wanane. Alisema mumewe ni mwajiriwa katika ofisi moja huko

 

Visiwani, lakini si mwanasiasa.

 

 

TACAIDS yashauriwa Kushirikisha halmashauri

Na Pendo Mangala, Dodoma

TUME ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) imetakiwa kuwashirikisha watumishi wa

 

halmashauri za wilaya katika mapambano dhidi ya ukimwi ili kusaidiana nao katika

 

kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na

 

Watoto Hilda Gondwe alipokuwa akifungua warsha kuhusu ukimwi kwa waratibu wa

 

kamati za kudhibiti ukimwi iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Veta mjini

 

hapa.

Gondwe alisema TACAIDS inatakiwa ishirikiane na watumishi wa halmashauri za

 

wilaya katika mapambano dhidi ya ukimwi ili kusaidiana nao katika kupunguza kasi

 

ya maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Alisema Tume imekuwa ikiwasahau watumishi wa halmashauri hizo za wilaya katika

 

kuwashirikisha kwenye mapambano dhidi ya ukimwi na hivyo kushindwa kufikia

 

malengo waliyoyaweka.

Katibu Mkuu alisema watumishi wa halmashauri za wilaya nchini ni moja ya sehemu

 

kubwa katika TACAIDS kwani ni wahusika wakubwa katika kutekeleza mapambano ya

 

udhibiti wa ukimwi katika jamii na nchi kwa ujumla.

Alisema endapo viongozi husika wa Tume hiyo watawashirikisha watumishi hao

 

wataweza kufikia malengo waliyoyaweka.

Hata hivyo alifafanua kwamba masuala ya udhibiti ugonjwa huo wa ukimwi ni magumu

 

kutokana na kuambatana na matatizo mbalimbali katika jamii.

Alisema matatizo hayo ambayo yamekuwa yakichangia udhibiti wa ukimwi kuwa mgumu

 

ni matatizo ya usiri, ukimya, unyanyapaa, aibu na kulinda haki za binadamu.

Warsha hiyo ya wiki moja imeandaliwa na TACAIDS na kuwashirikisha waratibu wa

 

Halmashauri za Tanzania bara.

 

 

TRA Mbeya yakamata sukari ya magendo

Na Solomon Mwansele, Mbeya

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mbeya imekamata sukari ya magendo tani

 

nne yenye thamani ya sh. milioni 2.2 iliyokuwa imeingizwa nchini kutoka nchi

 

jirani ya Malawi bila ya kulipiwa ushuru.

Sukari hiyo imekamatwa na maofisa wa TRA eneo la Simambwe ikiwa imepakiwa katika

 

gari lenye namba za usajili T 765 ABX aina ya Fuso, likiendeshwa na Charles

 

Hilary baada ya raia wema kutoa taarifa juu ya

kuingizwa kwa sukari hiyo nchini. Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini

 

kwake, Kaimu Meneja wa TRA mkoa Alphonce Mahende alisema mhusika wa sukari hiyo

 

hajakamatwa, lakini TRA inamshikilia dereva ili amtaje mfanyabiashara aliyemkodi

 

kubeba sukari hiyo.

Mahende alisema baada ya TRA kupewa taarifa hiyo, ilituma maofisa wake

 

kulifuatilia gari hilo na walikutana nalo eneo hilo la Simambwe lakini

 

walipolisimamisha dereva alikaidi na kuligeuza kurudi lilikokuwa linatoka.

"Walikaidi kusimama na kurudi kuelekea njia ya Tukuyu na walijaribu kuwazuia

 

maofisa wetu

wasifanye kitu kutokana na eneo hilo kutokuwa na mawasiliano na walijua kuwa

 

hawataweza kupiga simu kuomba msaada," alisema Mahende.

Aliongeza kuwa maofisa hao wa TRA walipoachiwa baada ya gari hilo kutoweka ndipo

 

walipoweza kutafuta eneo ambalo walifanikiwa kuwasiliana nao na kuwaeleza hali

 

halisi iliyotokea.

Kaimu Meneja huyo alisema kabla ya kuondoka waliomba msaada wa askari watatu

 

kutoka kituo kidogo cha polisi Uyole na kuelekea eneo hilo na walipolifuatilia,

 

walilikuta likiwa limewekwa kando ya barabara mpya ya kuelekea Inyala huku sukari

 

ikipakuliwa.

Alibainisha kuwa vijana waliokuwemo katika gari hilo walijaribu kuwazuia maofisa

 

hao bila ya kuwaogopa

askari ambao hawakuwa wameenda na silaha na kuendelea kupakua sukari kutoka

 

katika gari hilo na kwenda kuificha katika nyumba za majirani.

"Kuona hivyo ilitubidi tuombe tena msaada wa askari kutoka kituo cha Inyala ambao

 

walikuja na silaha kitu

kilichopelekea vijana wale wakimbie na kuliacha gari, dereva na utingo wake,"

 

alisema Mahende.

Mahende alisema hawakuweza kujua gari hilo lilikuwa na sukari tani ngapi, kwani

 

sukari nyingine

iliyoshushwa ilikutwa ikiwa imefichwa katika migomba.

Sukari iliyofanikiwa kufikishwa ofisi za TRA mkoa ni katoni 200 za kilo 20 kila

 

moja ambayo ni sawa na tani

4 yenye thamani ya sh. milioni 2.2.

 

Sh. milioni 463 zatumika kwa ujenzi kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dodoma

Na Pendo Mangala, Dodoma

 

Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere

 

JUMLA ya sh. milioni 463.8 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza wa

 

jengo la kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere (Nyerere

 

Square) lililopo mjini hapa.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu

 

(CDA) Abdullahaman Mbwambo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mjini hapa.

Mbwambo alisema fedha hizo zimetolewa na Serikali Kuu kwa mamlaka hiyo kwa ajili

 

ya ujenzi wa jengo la kumbukumbu hiyo.

Alisema jengo hilo litakuwa ni moja ya kumbukumbu katika kumuenzi hayati Baba wa

 

Taifa kwani ni jengo la kihistoria katika vizazi vijavyo kuweza kujua umuhimu wa

 

Mwalimu Nyerere pamoja na shuguli alizofanya katika nchi hiyo .

Hata hivyo alisema Nyerere ni mtu ambaye amefanya mambo mengi mbalimbali na yenye

 

manufaa kwa umma na kwa nchi ya Tanzania kwa ujumla na kwamba ndiye mwasisi wa

 

kutoa wazo la Makao Makuu ya nchi kuhamia Dodoma.

Alisema mji wa Dodoma ndiyo kitovu cha nchi hivyo wazo hilo la hayati Baba wa

 

Taifa liko sahihi na halina budi kutekelezwa na viongozi wa Serikali.

Aliwataka wananchi kumuenzi Baba wa Taifa kwa kwa yale yote mema aliyoyafanya

 

enzi za uhai wake ili kuweza kuyaendeleza na kukuza sifa ya nchi kama alivyokuwa

 

akifanya

Pia alisema kampuni ya simu za mikononi Vodacom nchini kwa kushirikiana na

 

serikali imejitolea kujenga bango kubwa ndani ya jengo hilo ambalo litakuwa

 

likirusha hotuba mbalimbali katika redio na kuonyesha picha za mwalimu kwenye

 

televisheni tofauti za hapa nchini kwa lengo la kumuenzi.

Mbwambo alisema kampuni hiyo imesema inatambua mchango mkubwa uliotolewa na

 

hayati baba wa Taifa enzi za uhai wake hivyo wao kama kampuni ya simu hawana budi

 

kuyaendeleza yale yote aliyoyafanya kwa kuyaenzi.

Alisema kampuni hiyo ya Vodacom imeahidi kuwa bega kwa bega na serikali

 

kuhakikisha wanajenga bango hilo kubwa ndani ya jengo hilo la kumbukumbu ili

 

kuwezesha wananchi kuangalia na kusikiliza matangazo ambayo yatakuwa yakirushwa

 

ndani ya jengo hilo.

Ujenzi wa jengo la kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere unatarajiwa kukamilika Septemba

 

mwakani.

 

Wadau wa bonde la Wami Ruvu kukutana

Na Prosper Kulita,Morogoro

WADAU wa maji zaidi ya 45 katika Bonde la Wami Ruvu (WRBWO) linalojumuisha wilaya

 

19 za mikoa mitano ya Tanzania bara wanatarajia kukutana mjini hapa ili kujadili

 

usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji zilizoko katika bonde hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa wa maji wa bonde hilo, Julius Sarmett

 

alisema katika warsha hiyo inayotarajiwa kufanyika leo na kesho na kuwahusisha

 

wadau wa maji kutoka wizara za serikali, watoaji huduma za maji safi na taka

 

mijini na vijijini, taasisi za utafiti, halmashauri za miji na wilaya, taasisi

 

zisizo za kiserikali, viwanda na wamwagiliaji.

Alisema washiriki mbali ya kubadilishana uzoefu pia watajifunza dhana ya

 

usimamizi wa pamoja wa raslimali za maji kimataifa kutoka taasisi ya In Went

 

yenye makao yake makuu Ujerumani.

Akifafanua, Sarmett alisema rasilimali za maji ni moja ya nyenzo muhimu katika

 

mpango wa serikali wa kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini (MKUKUTA).

Alisema kulingana na changamoto zinazojitokeza katika usimamizi wa matumizi bora

 

ya rasilimali za maji mfano kuongezeka kwa mahitaji ya rasilimali za maji,

 

serikali iliamua kuweka mfumo wa usimamizi wa rasilimali za maji kimabonde na

 

kuigawa nchi katika mabonde tisa likiwemo la Wami Ruvu.

Pia aliongeza kuwa kufuatana na sera ya maji (NAWAPO 2002) usimamizi wa

 

rasilimali za maji utatekelezwa katika ngazi tano ambazo ni ngazi za watumiaji,

 

mabonde madogo, halmashauri za wilaya, mabonde na Taifa.

Alisema ngazi hizo zimewekwa ili kuwezesha na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa

 

pamoja wa rasilimali za maji.

 

Tanzania yasema kamwe ardhi yake haitatumiwa na waasi

Na Jumanne Gange, Kigoma

SERIKALI katika wilaya Kigoma imeihakikishia serikali ya Burundi kuwa haina

 

sababu na wala haitoruhusu chama cha waasi cha PELIPEHUTU - FNL na wakimbizi wa

 

nchi hiyo wanaohifadhiwa nchini kutumia ardhi na mpaka wa Tanzania kuivamia

 

serikali na wananchi wa Burundi.

Akizungumza katika kikao cha ujirani mwema kati ya wilaya ya Kigoma na wilaya za

 

Nyanza Lake na Mabanda za nchini Burundi zinazopakana na wilaya ya Kigoma, Mkuu

 

wa wilaya ya Kigoma, Henry Clemens alisema, kimsingi, mafanikio ya amani

 

yaliyofikiwa hivi sasa nchini humo ni jitihada za za kimataifa kwa mchango mkubwa

 

wa serikali ya Tanzania.

Alisema Tanzania inaheshimu maamuzi ya wananchi wa nchi hiyo katika kuiweka

 

serikali iliyopo madarakani kwa misingi ya kidemokrasia ikwa ni jitihada

 

zilizoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mkuu wa wilaya ya Kigoma alilazimika kutoa msimamo huo kutokana na tahathari

 

iliyotolewa na serikali ya Burundi kupitia Msaidizi wa Gavana wa mkoa wa Makamba,

 

katika kikao cha siku moja kilichiofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe,

 

mkoani Kigoma kuimarisha usalama, mahusiano ya kijamii na ya kiuchumi baina ya

 

pande mbili hizo

Gavana Deo Niyonzima ambaye aliongoza ujumbe wa Burundi katika mazungumzo hayo,

 

alikiambia kikao hicho kuwa serikali ya Burundi inayo taarifa kuwa kikundi cha

 

PALIPEHUTU -FNL kupitia Congo Mashariki na hatimaye ardhi ya Tanzania wilaya ya

 

Kigoma kimepanga kuushambulia mkoa huo wa Makamba nchini Burundi.

Niyonzima, aliongoza ujumbe wa watu 13, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu wa jeshi

 

nchini humo, wakuu wa wilaya za Nyanza Lake na Mabanda, wataalamu na

 

wafanyabiashara wa mkoa huo.

Alisema Burundi inazo taarifa pia za kikundi hicho kutaka kuwashawishi na

 

kuwatumia baadhi ya wakimbizi wa nchi hiyo katika kambi za wakimbizi mkoani

 

Kigoma kujiunga nao katika azma yao hiyo.

Aidha, kikao hicho chini ya uenyekiti wa Clemens ambaye aliambatana na kamati ya

 

ulinzi na usalama na wataalamu kadha ndani ya wilaya yake, kilikubaliana kwa

 

kauli moja kuweka maazimio 12 kama dira mpya ya mahusiano ya kiulinzi, kiuchumi

 

na kijamii.

Maazimio hayo ni pamoja na kuwapo kwa vikao vya ujirani mwema kila baada ya miezi

 

mitatu, kuanzishwa na kuundwa kwa kamati za pamoja za ulinzi, usalama na masuala

 

ya kibiashara.

Vilevile, kikao hicho kiliazimia kuweka utaratibu wa kisheria wa kubadilishana

 

wahalifu na mali zilizoibwa baina ya pande mbili hizo.

 

Vyama na mabaraza ya wafanyakazi yakuze tija

Na El-hadji Yuusuf, Tabora

WAFANYAKAZI nchini wametakiwa wavitumie vizuri vyama, pamoja na mabaraza yao

 

katika sehemu za kazi kwa ajili ya kuleta ufanisi na siyo kuwa chanzo cha

 

migogoro na kuwatetea wafanyakazi wazembe.

Kauli hiyo imetolewa mjini hapa na Mkuu wa mkoa wa Tabora, Abbas Kandoro,

 

alipokuwa akifungua rasmi baraza la wafanyakazi wa mamlaka ya majisafi na

 

majitaka katika manispaa ya Tabora (TUWASA).

Alisema kuwa ni makosa kwa vyama vya wafanyakazi na mabaraza ya wafanyakazi

 

nchini, kuwa chanzo cha migogoro na hatimaye kusababisha ufanisi wa kiutendaji

 

kushuka katika sehemu zao za kazi jambo ambalo alisema kuwa linawaumiza wananchi.

Aliwataka wafanyakazi wawe makini katika utumishi na kuhakikisha kuwa wanayafikia

 

malengo ya ajira zao, ili kuifanya mamlaka yao iweze kutoa huduma bora za maji

 

hapa nchini.

Alisema kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wake, pale ambapo kuna migogoro mingi ya

 

kiutendaji katika sehemu za kazi ni kwamba viongozi wa vyama vya wafanyakazi na

 

mabaraza ya kazi huwa na kasoro kubwa.

Alisema kuwa viongozi kama hao ndiyo wanaosababisha utendaji duni na kutofikiwa

 

kwa malengo katika sehemu zao za kazi na hatimaye kusababisha utendaji mbovu,

 

ambao huzua minong'ono na malalamiko kutoka kwa wateja ambao katu hawawezi

 

kulipia huduma mbovu.

Aliwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutambua kuwa mabaraza ya wafanyakazi ya

 

sasa yanakwenda na wakati na kwamba yenyewe ndiyo yawe kichocheo kikubwa cha

 

maendeleo katika sehemu za kazi kwa kuhimiza ufanisi na juhudi kwa wafanyakazi na

 

utawala ili kuwezesha kupatikana kwa maslahi mazuri.

Alisema kuwa hali hiyo inaweza kuepukwa iwapo kama watu wanaochaguliwa kuongoza

 

vyama vya wafanyakazi na mabaraza ya wafanyakazi wanakuwa na elimu bora na uwezo

 

wa kuongoza ikiwa ni pamoja na kuishauri menejimenti ifanye nini kuongeza tija.

Alisema kuwa kinyume na hali hiyo ni kukaribisha ubabaishaji katika vyama hivyo,

 

sambamba na kuwa na vyama vibovu ambavyo viongozi wake ni wapenda majungu na

 

kulalamika kwa kila jambo na hivyo kuzifanya sehemu za kazi kuwa sehemu zisizo na

 

amani.

Alisema kuwa atarajika sana iwapo baraza hilo la wafanyakazi analolizindua leo,

 

litakuwa ni mfano mzuri wa utendaji kazi wa mabaraza ya wafanyakazi nchini, kwa

 

kusimamia vizuri wajibu wa mwajiri na wafanyakazi na kupigania maslahi ya

 

wafanyakazi na stahili zao kwa mujibu wa sheria.

 

 

Wananchi wawe macho na vyama vinavyowamurika mchana, watambue usiku vitawachoma vikishinda

Na Mwadini Hassan

BINAADAM ni mtu. Mtu ni kiumbe. Katika ulimwengu huu tunaoishi kuna viumbe vya

 

aina mbali mbali. Lakini sifa kuu ya kiumbe ni kuwa na roho kama vile binaadamu,

 

mnyama, ndege, samaki na wadudu.

Katika jamii hizo za viumbe, wanyama, ndege, samaki na wadudu ni viumbe

 

vinavyoishi bila ya kuwa na akili za kuwaza na kupambanua mambo.

Viumbe hivyo viliumbwa na kuwa na akili ya kawaida tu vinavyoweza kuitumia

 

kujitafutia chakula na namna ya kulea watoto wao. Maumbile yao na kwa akili

 

walizojaaliwa hawawezi kujua zuri na baya

Ndiyo maana wanyama kwa mfano, hawana akili ya kupambanua kuwa huyu ni mama au

 

baba yangu. Anakuwa na akili za kujua hayo anapokuwa mdogo tu ili aweze kulelewa

 

na kukua. Akishakua kwa kukosa kupambanua zuri na baya, ndiyo maana wanaweza

 

kuzaa na baba ama mama waliowazaa.

Kwao hakuna tofauti ama ubaya wa mtoto kuzaa na mzazi wake, ama dada kuzaa na

 

kaka wa kuzaliwa naye tumbo moja, au kinyume chake. Kwao vyo vyote ni sawa na

 

hakuna miongoni mwao atakayemshangaa mwenzake kwa kufanya hivyo. Ni jambo la

 

kawaida kabisa.

Kwa unyama wao, ndiyo maana kuuana ni jambo la kawaida kwao. Huyu anamuua na

 

kumla yule bila kimeme au aibu. Ni jambo la kawaida na wala hakuna jamii moja ya

 

mnyama inayoungana kupambana na ‘maonevu’ hayo.

Mnyama mmoja anamuona mwenzake wa ana ile ile anakamatwa na kuliwa na mnyama wa

 

aina nyingine, atakalofanya ni kukimbia kujisalimisha yeye tu, na mwenzake

 

akishakamatwa na kuliwa, na yeye amepona, hana habari. Yamemuishia mradi yeye leo

 

kanusurika.

Huo ndiyo unyama. Hawakujaaliwa kujua zuri na baya, au hili linafaa ama halifai

 

kutendwa katika jamii. Na kwa kweli hakuna atakewashangaa ama kuwalaumu. Na hata

 

Muumba wa mbingu na ardhi, hakuwawekea mipaka ama kanuni za maisha yao. Vyovyote

 

wanavyoishi viumbe hao ni sawa.

Lakini, hali haikuwa hivyo kwa binaadamu. Binaadamu ni tofauti na mnyama, ndege

 

ama wadudu. Anatakiwa aishi kwa nidhamu na utaratibu maalum katika maisha yake.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba mwanaadamu ni kiumbe mwenye daraja la juu kabisa

 

kuliko viumbe vyote vilivyoumbwa na Mungu. Hiyo inatokana na kwamba binaadamu

 

amepewa uwezo mkubwa wa kufikiri. Ana uwezo wa kujua zuri na baya, lipi linalofaa

 

kutendwa na lipi halifai.

Amepewa pia uwezo wa kutawala mazingira yake na mazingira ya viumbe vingine.

Ndiyo maana basi, binaadamu amepewa uwezo wa kujifanyia mambo mbali mbali

 

yanayomtofautisha maisha yake na viumbe vilivyonyimwa uwezo wa kufikiri na

 

kuamua.

Binaadamu kwa sifa hiyo, anajijengea nyumba ya kuishi, anajiandalia chakula chake

 

kwa kujipikia, anavaa nguo, anachana ama kusuka nywele na mambo mengine kadhaa.

Kwa kujua zuri na baya, hawezi kuzaa na mtoto wake, baba ama mama yake. Kwa

 

maumbile yake ya ubinaadamu, hawezi kutembea bila kuvaa nguo, na kutokana na

 

uwezo huo amejitengenezea vitu kadhaa vya kumrahisishia maisha yake. Huo ndiyo

 

ubinaadamu na huyo ndiye binaadamu.

Inapotokea binaadamu kufanya vitu kinyume cha hivyo, huwa ni kioja. Kwa kweli

 

binaadamu wenzake watamshangaa, na hata kufikia hatua ya kuamua huyo kiumbe

 

mwenzao ni punguwani au kumpa sifa ya uwendawazimu.

Na mtu anapoitwa mwendawazimu, huwa ubinaadamu wake umepungua na unaelekea katika

 

sifa za unyama. Mwendawazimu huwa hajui zuri au baya. Anafanya lolote, mahala

 

popote na huwa hana tofauti kubwa na mnyama.

Vitendo vilivyotokea hivi karibuni katika kijiji cha Ilolangulu, mkoani Tabora

 

vya binaadamu kutia vinyesi kwenye visima vya maji, ni uwendawazimu unaomtoa mtu

 

katika ubinaadamu.

Mbaya zaidi inadaiwa waliyofanya, eti walifanya hivyo kwa sababu za kisiasa.

 

Sababu yao ni kuwa wao ni wafuasi wa chama cha CUF na wanaotumia visima hivyo ni

 

wafuasi wa Chama cha Mapinduzi!

Ni unyama gani huo? Binaadamu aliyepewa heshima na sifa zote na Mungu,

 

aliyekutukuza kwa kila hali na kuwa mtawala wa viumbe na vitu vyote humu duniani,

 

uutupe ubinaadamu wako na kutia vinyesi kwenye visima vya maji, vinavyotumiwa na

 

mamia ya binaadamu wenzako!

Cha ajabu wanaotenda vitendo hivyo, hivi sasa wamo katika harakati za

 

kuwashawishi Watanzania wawachague na kuwapa uongozi wa kata, majimbo na nchi ya

 

Tanzania!

Ni Mtanzania gani baada ya wafuasi wa chama hicho kufanya ujinga na unyama huo,

 

watakaokipa chama chao kura eti wawaongoze?

Chama hicho kimeshajidhihirisha kuwa hakifai kupewa uongozi, siyo wa nchi tu,

 

bali hata wa kijiji. Waswahili husema anayekumurika mchana, usiku atakuchoma.

Chama hicho kimeshaonyesha wazi kuwa kinawamurika mchana Watanzania kwa

 

kuwafanyia visa na vitimbi vya kuwawekea kinyeshi kwenye visima. Kikipata

 

madaraka wafuasi wake wanaweza hata kuweka sumu kwenye visima vya maeneo ambayo

 

watakuwa hawaungwi mkono.

Vitendo vyao vinathibitisha kuwa hawafai kupewa madaraka.

 

Kwa nini uchaguzi wa Zanzibar ulikodolewa sana macho na wakubwa

WACHAMBUZI wetu wa masuala ya uchaguzi wanaendelea kutuelimisha kuhusiana na

 

matukio na mambo mbali mbali yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar na

 

uchambuzi kuhusiana na hali hiyo vyanzo na malengo yake, kama inavyoeleza makala

 

hii ya pili ya mfululizo huo.

MWANAFALSAFA mmoja aliwahi kuelezea juu ya mabadiliko ya kisiasa na udhibiti wa

 

biashara na uchumi chini ya mfumo wa utandawazi wa utawala wa upande mmoja au

 

demokrasia ya mfumo mpya . Alieleza kuwa mabadiliko haya yametoa udhibiti kwa

 

mataifa ya Magharibi tokea kumalizwa kwa vita baridi na kusambaratika kwa Taifa

 

kubwa la Kisovieti.

Nilipoisoma makala ile kwanza nilikumbuka yaliyotokea mwaka 1964

Januari 12 pale ilipotoka kauli ya kuungwa mkono na Mataifa ya Mashariki

 

Mapinduzi ya Zanzibar.

Mataifa hayo yaliongozwa na Urusi, Uchina, Ujerumani Mashariki na Cuba. Urusi

 

ilitoa onyo kali kwa Taifa lolote litakaloingilia Mapinduzi halali ya Wananchi wa

 

Zanzibar. Na kila mtu aliufyata. Mapinduzi baridi yaliyotaka kuletwa na wajanja

 

yalizimwa.

Na sasa inanikumbusha kuwepo nguvu za upande wa Magharibi zinazotawala kila kitu

 

kutoka siasa, hadi uchumi. Na ninakumbuka usemi wa baadhi ya viongozi na wafuasi

 

wa Chama cha CUF pale walipokuwa wakijipongeza na kushangilia ushindi kabla kura

 

katika vituo vya uchaguzi hazijamalizwa kuhesabiwa. Walituambia hata CCM

 

ikishinda ushindi itapewa CUF kwa nguvu za Umoja wa Mataifa.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa tulishindwa kuamini kauli hiyo isiyofuata nadharia

 

za demokrasia na utawala bora. Hadi hapo tulipoanza kuulizwa masuala ya kuwepo

 

Serikali ya kitaifa, na Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (yaani NGO) kumiminiwa

 

fedha kedekede za kuendesha mafunzo ya urai , tulianza kubashiri mbinu, ujanja na

 

mikakati inaundwa na Mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani ya kuipa CUF

 

madaraka ya kutawala pole pole iwapo itashindwa katika uchaguzi. Dhana ya kuwepo

 

serikali ya pamoja ndivyo inavyoendelezwa.

Kwa CUF kutegemea nundu, walinyamaza kimya tokea kumalizika uchaguzi kwa

 

kisingizio cha kusubiri mkutano wa Baraza kuu. Kumbe kulichokuwa kikisubiriwa ni

 

kauli ya Marekani ya kutotambua matokeo ya uchaguzi iliyotolewa katika mkesha wa

 

Novemba 3, 2005. Kauli hiyo nayo ikaungwa mkono na Serikali ya Norway ambayo kwa

 

jeuri kubwa inaitaka SMZ/Tume ya Uchaguzi kurudia uchunguzi wa madai ya CUF ya

 

kasoro za uchaguzi na kuyaweka hadharani matokeo ya uchaguzi.

MASWALI

Hapa wachunguzi wa kisiasa tunaanza kujiuliza Norway wamepata wapi madaraka ya

 

kuihoji Tume au SMZ juu ya matokeo ya uchaguzi yaliyoungwa mkono na Taasisi na

 

mashirika kadhaa? Norway imebainika kuiunga mkono kauli ya uchochezi ya Marekani

 

ya kuyakataa matokeo halali ya uchaguzi yaliyotolewa na Tume huru wakati historia

 

bado inatukumbusha yaliyotokea Florida, Marekani katika uchaguzi wa Rais mwaka

 

2000 ambapo Tume ya uchaguzi ya Marekani ilifyata mkia. Na Rais Bush akatangazwa

 

Urais wake na Mahakama Kuu ya Florida. Haya ni maajabu na kweli.

Hoja gani inataka kujengwa hapa? Kuleta vurugu nchini na itakapodhibitiwa

 

serikali ilaumiwe kutumia nguvu kubwa kwa vikosi vya ulinzi. Vurugu zizagae ili

 

nchi isitawalike na hatimae utawala wa nguvu mpya uchukue mkondo wake wa

 

kumlazimisha Rais wa Zanzibar aunde Serikali ya kitaifa. Hiyo ndiyo misingi ya

 

ukoloni mambo leo unaosaidiwa na hoja mpya inayoitwa "Industrial imperialism".

Turudi katika ukweli wa kutafuta mbinu za kufuta kashfa iliyowakuta Waingereza

 

mwaka 1963-64. Waingereza kwa kebehi, dhuluma na jeuri walitoa uhuru wa Zanzibar

 

kwa walowezi wenzao kupitia vyama vya Hizbu na ZPPP. Vyama hivyo kwa pamoja

 

vilipata aislimia 45.4 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1963, wa

 

kutafuta uhuru wa Zanzibar, Chama cha ASP cha wanyonge, wakwezi na wakulima

 

kilipata kura nyingi zaidi - asilimia 54.6. Waingereza waliona demokrasia sahihi

 

ni ile ya kuwapa wachache, makabaila, madaraka ya kuitawala nchi ya Zanzibar,

 

chini ya mamlaka ya Sultan Jemshid Bin Abdulla, Bin Khalifa Bin Haroub ... Huu ni

 

ukoo mrefu wa Ma-Busaidi kutoka Oman, wavamizi wa nchi hii katika karne ya17.

 

Hatua hiyo iliwanyima haki wanyonge walio wengi, waliochoka kutawaliwa,

 

kubaguliwa, kunyanyaswa na ambao walikuwa watumwa katika nchi yao.

Wanaume hao wenye nguvu za umma kwa asilimia 54.6 dhidi ya nguvu hafifu za

 

makabaila na vibaraka vyao kwa asilimia 45.4 walisubiri Muingereza akabidhi nchi

 

aondoke ili wanaume wachukuwe nchi yao. Wanamapinduzi hao Wazanzibari halisi

 

"waliuwa tembo kwa ubuwa" wakaikomboa nchi yao, na hadi leo Wazanzibari hao

 

wanayaona mapinduzi yao ni ya kudumu na ndiyo maana yakawa "Mapinduzi Daima".

Kitendo cha wanaume kuiondoa madarakani Serikali ya Sultani na vibaraka wake kwa

 

kipindi cha mwezi mmoja tu, tokea Serikali hiyo iwepo madarakani ni kashfa na

 

aibu kubwa kwa Serikali ya Kiingereza. Na ndiyo maana inatafuta mbinu za kuifuta

 

kashfa hiyo.

Seif Sharif Hamad alikuwa (na bado anaendelea) mkereketwa mkubwa wa muungano wa

 

ZNP/ZPPP tokea awe mwanafunzi wa King George VI katika miaka ya 1960. Hivyo ni

 

muathirika mkubwa wa mapinduzi matukufu ya Zanzibar, ingawa ni mmoja

 

aliyesomeshwa na kupewa vyeo kadhaa hadi kufikia Waziri Kiongozi (1984 -88).

Kutumiwa muathirika wa mapinduzi kama Seif Sharif Hamad kuifuta kashfa ya

 

Muingereza sio ajabu hata kidogo. Lengo kuu ni kufuta historia ya Mapinduzi na

 

kuurejesha utawala wa Zanzibar kwa "mabwanyenye"chini ya nguvu za ukoloni mambo

 

leo. Historia kweli hujirudia, lakini penye haki sio penye batili.

UKOLONI MAMBOLEO

Mbinu za kurudisha nguvu za ukoloni mamboleo zilianza kupamba moto tokea pale

 

vilipomalizika vita baridi na kusambaratika kwa Taifa la Kirusi, kama

 

nilivyoeleza hapo awali. Sera mpya za utanuzi wa demokrasia kuheshimu haki za

 

binadamu, utawala bora na mbinu za kupunguza nguvu za utawala wa serikali

 

zikatawaliwa kwa kuanzisha taasisi zisizokuwa za kiserikali yaani (NGO). Hii ni

 

mikakati maalum iliyoandaliwa na Mataifa ya Magharibi ambayo yalipoteza makoloni

 

yao yaliyodai uhuru sasa katika miaka ya 1960, ikiwemo Zanzibar.

Makoloni hayo yaliyopata uhuru katika miaka ya 1960 ndiyo yaliyokuwa yakiimarisha

 

uchumi wa viwanda wa nchi za Magharibi kwa kutoa malighafi na nguvu kazi. Hivyo

 

kwa kupata uhuru wao ni kujitegemea kwa nguvu kazi zao na malighafi zao na

 

kuimarisha uchumi wa nchi za Magharibi.

Ndiyo maana sasa juhudi zinafanywa na nchi hizo kuirejesha hali hiyo kwa kupitia

 

mlango wa nyuma chini ya misingi ya utawala wa nguvu za upande mmoja. Katika

 

kutekeleza nguvu hizo juhudi zinafanywa za kuondoa madarakani uongozi wote

 

uliofanikisha ukombozi wa nchi zao, wanamapiduzi washupavu, na badala yake

 

kuuweka uongozi utakaoshinda maslahi yao.

Na kwa upande wa Zanzibar (na hata Zimbabwe) kuuondosha uongozi wa kimapinduzi na

 

badala yake kuweka uongozi utakaolinda sera za kikabaila, na kufuta kashfa

 

iliyowakuta watawala wawili, kwa mpigo, Muingereza na Sultani Jemshid na vibaraka

 

wake.

Kutokana na maelezo haya, wasomaji sasa watafahamu kwa nini uchaguzi wa Zanzibar

 

ukawa na mvuto mkubwa kwa Mataifa Makubwa, na hasa nchi marafiki za Magharibi

 

zikiongozwa na Marekani, Uingereza na nchi ya Norway.

Zanzibar ina historia ya ukombozi iliyojengeka kwa misingi imara sana. Haibomoki

 

mpaka ifutwe na historia ya Mapinduzi. Inaonekana wazi kuwa atakayeweza kuifuta

 

historia hiyo sio Karume, mwana Mapinduzi lakini Seif Sharif Hamad muathirika wa

 

Mapinduzi hayo.

Wakati Karume na watu wake wanasema "Mapinduzi Daima", Seif na wafuasi wake

 

wanasema "Mapinduzi Dhulma". Hizi ni tofauti mbili za msingi zinazosababisha CCM

 

kushinda Zanzibar. Kwani wanaoyaunga mkono Mapinduzi bado ni wengi na wataendelea

 

kukiunga mkono chama cha sasa kinachoheshimu mapinduzi na kuyalinda mapinduzi

 

hayo.

Itaendelea..

 

NGAWAIYA: Rais Mkapa amefanya mengi ya neema kwa Tanzania

Ni katika miundombinu, elimu na huduma za afya

KUTOKANA na mafanikio mengi yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya tatu, aliyekuwa

 

Mbunge wa Moshi Vijijini (TLP) Thomas Ngawaiya ambaye sasa ni mwana-CCM, amekiri

 

kwamba Rais Benjamin Mkapa amefanya mengi mazuri kwa wananchi. Katika makala hii

 

Mwandishi GABRIEL JOHN anaelezea zaidi.

Thomas Ngawaiya anaeleza kushangazwa kwake na ‘kelele’ zinazopigwa na viongozi wa

 

vyama vya upinzani kwamba tangu Chama Cha Mapinduzi kishike hatamu za uongozi

 

uongozi kutoka vyama vya TANU na ASP, kasi ya maendeleo ya nchi yetu imesimama na

 

kwamba hakuna wananchi wanachofaidi zadi ya kuonezeka kwa shida na kero

 

mbalimbali.

Katika kupinga kauli hiyo, Ngawaiya anasema kwamba mafanikio mengi yamepatikana

 

baada ya CCM kushika dola tofauti na hali ilivyokuwa miaka iliyopita ambapo sasa

 

huduma nyingi za jamii zimepatikana na zilizokuwepo kuboreshwa.

Akieleza zaidi kuhusu mafanikio ya serikali hiyo, Ngawaiya anataja kuboreshwa kwa

 

utoaji wa elimu kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu. Anasema miaka mingi

 

Tanzania ilikuwa ikijivunia kuwa na chuo kikuu kimoja tu cha Dar es Salaam,

 

lakini sasa vipo vyuo zaidi ya 10.

Mbali na elimu, mbunge huyo wa zamani wa kambiya upinzania anasifu jitihada za

 

serikali ya Rais Mkapa katika kuboresha miundombinu, huduma za afya na maji ikiwa

 

ni sambamba na upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo mengi ya Tanzania.

ELIMU

Ngawaiya anasema katika kuhakikisha kwamba elimu inakuwa bora na kwamba kila

 

mwenye sifa anafika hatua ya juu ya elimu hiyo, serikali imeweka mikakati ya

 

kuhakikisha kila mtoto mwenye sifa za kujiunga na elimu ya msingi anafanya hivyo.

Katika kusisitiza hilo, serikali ilipitisha sheria kali kwa wazazi ambao

 

watashindwa kuwaandikisha watoto wao wenye sifa za kujiunga na darasa la kwanza.

 

Hali hiyo imesaidia mno kuongeza idadi ya watoto hao hasa ikizingatiwa kwamba ada

 

na michango yote kwa kiwango hicho cha elimu imefutwa.

“Kuna mipango mingi kwenye sekta ya elimu ambayo yote ina lengo la kuiarisha

 

utoaji na upatikanaji wa elimu wa watoto wetu,” anasema.

Serikali ilibuni mpango mahsusi wa kuhakikisha kwamba elimu ya msingi inakuwa

 

boora kuanzia walimu, majengo na vifaa vya kufundishia, mpango ambao mafanikio

 

yake yanaonekana kuwa na faida kubwa. Mpango huo maarufu kwa jina la MMEM (Mpango

 

wa Maendeleo kwa Elimu ya Msingi).

Baada ya kuonekana mafanikio hayo kwa elimu ya msingi, serikali pia inaendelea

 

kuweka nguvu zake katika kuiboresha elimu ya sekondari kupitia mpango wake wa

 

MMES.

Katika mpango huu, serikali imedhamiria kuona kwamba kila kata inakuwa na shule,

 

walau moja ya sekondari ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji wa kiwango hicho cha

 

elimu.

Mbali na jitihada hizo, serikali pia kwa kutambua kuwepo kwa idadi ya watoto

 

waliokosa elimu ya sekondari kutokana na sababu mbalimbali, ilibuni mpango wa

 

kuwapatia elimu vijana walioikosa wa MEMKWA.

Katika mpango huo, watoto hao wanapatiwa elimu kuanzia ya msingi na baadaye wenye

 

uwezo kuendelea na sekondari na hata elimu ya juu.

Akitoe mifano halisi juu ya mafanikio ya elimu, Ngawaiya anasema kwamba katika

 

jimbo la Moshi Vijijini, kata nyingi zimejengwa shule za sekondari na hiyo n

 

kuonyesha kwamba Ilani ya CCM ya Uchaguzi inatekelezeka.

Ngawaiya anasema kwamba kata ya Kibosho Mashariki, ina shule za sekondari zaidi

 

ya tano, miongoni mwa shule hizo ni Old Moshi, Kibosho Girls, Nsoo na Sungu.

Anazitaja shule nyingine kuwa ni Sahoni, Mbokomu, Meli Nane ambazo ni miongoni

 

mwa shule zilijengwa katika kipindi cha awamu ya tatu ya uongozi.

BARABARA

Ngawaiya anasema serikali ya awamu ya tatu imejenga barabara nyingi kwa kiwango

 

cha lami na zingine kuwekwa changarawe ili kuzifanya kupitika kwa mwaka mzima,

 

bila kujali mabadiliko ya hali ya hewa.

Anasema miongoni mwa barabara zilizowekwa ‘mkeka’ na kuondoa kabisa mashimo

 

kwenye barabra hizo ni barabara toka Rombo hadi Takeya (Kenya) ambapo awali

 

zilikuwa hazifai kutokana na kuharibika mara kwa mara, huku ziishindwa kabisa

 

kupitika wakati wa masika.

Barabara nyingine ni Oriri kuelekea Dar es Salaam ambazo zimewekwa lami jambo

 

ambalo hurahisisha mawasiliano katika kusafirisha bidhaa na abiria baina ya Kenya

 

na Tanzania.

Pia anasema kwamba si barabara hizo tu zinazounganisha Tanzania na Kenya, bali

 

barabara za mikoani zimeboreshwa na zinajengwa katika kuhakikisha kuwa

 

mawasiliano yanakuwa rahisi kutoka eneo moja hadi jingine.

Ngawaiya anasema kwamba yote hayo ni maendeleo makubwa yanayofanywa na Serikali

 

ambayo inamaliza muda wake baadaye mwaka huu.

HUDUMA YA AFYA

Serikali ya awamu ya tatu imewajibika ipasavyo katika kuhakikisha kuwa huduma za

 

afya zinakuwa bora zaidi na kwamba zinapatikana jirani zaidi na makazi ya

 

wananchi.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, zahanati nyingi zimejengwa, dawa

 

zinapatikana huku wataalamu wa afya wakiongezeka katika zahanati, vituo vya afya

 

na hospitali.

Ngawaiya anasema kwamba kutokana na hali hiyo, anaamini kwamba vifo vingi

 

vimepungua ikilinganishwa na wakati ambapo hapakuwa na huduma za afya jirani

 

zaidi na makazi ya watu, hasa wa vijijini.

“Nina amini kwamba idadi ya akinamama wajawazito ambao walikuwa wakipoteza maisha

 

kutokana na umbali wa vituo vya afya, sasa imepungua kwa kiasi kikubwa,”

 

anaongeza mbunge huyo wa zamani.

Mbali na kuwa baadhi ya maeneo bado yana umbali mkubwa kufia hospitali kubwa,

 

lakini kuimarishwa kwa miundombinu, limekuwa jambo jingine lenye faida kubwa

 

kwani wagonjwa wanaweza kusaidiwa kufika mapema kunakopatikana huduma hizo za

 

afya.

USHINDI KWA CCM

Ngawaiya anasema kuwa baada ya kupokea matokeo ya ushindi wa ‘Tsunami’ kwa CCM

 

Zanzibar, ushindi kwa upande wa Tanzania Bara utakuwa wa kishindo zaidi na kwamba

 

vyama vya upinzani havitaambulia matarajio yao.

Anasema ushindi wa CCM Zanzibar ni ishara ya mvua ya kubwa ya masika

 

inayotarajiwa bada ya wananchi uwa wamepiga kura Desemba 14, mwaka huu.

“Kutokana na ushindi huo wa Zanzibar, niliamua kufanya tambiko kwa kuchinja mbuzi

 

ikiwa ni ishara ya kuondoa mikosi niliyokumbana nayo nilipokuwa TLP kwa kipindi

 

cha zaidi ya miaka kumi…

Nina imani kwamba sasa yote yaliyokuwa yakijitokeza kuishambulia CCM na maendeleo

 

yake kwa wananchi yamefutika, nimekuwa mtu mpya kabisa,” anaongeza.

WAPINZANI

Ngawaiya anasema kwamba kwa sasa vyama vya upinzani havina nguvu na vinavurugwa

 

zaidi na chama cha CUF kwa kuendelea kutomtambua Rais Amani Abeid Karume ambaye

 

alipata ridhaa ya wananchi kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Anasema ni jambo la kushangaza kwa CUF kuendelea kudai kuwa uchaguzi haukuwa wa

 

huru huku watu wengi wa ndani na nje walioshuhudia uchaguzi huo wakieleza kuwa

 

huru na kwamba ulifuata misingi yote ya kidemokrasia.

Hivyo, anawataka viongozi wa CUF na wote wasiokubalina na matokeo hayo, kuacha

 

kuchochea vurugu Zanzibar.

MATARAJIO

Anasema kwamba kukosa ubunge siyo mwisho wa kushirikiana na wananchi wa Moshi

 

Vijijini kuleta maendeleo.

Ngawaiya anaeleza kuwa ataendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo

 

kuhakikisha kwamba maendeleo yanaendelea kuimarishwa kwa kuwa anatarajia CCM

 

kushinda katika jimbo hilo.

Mbunge huyo wa zamani anabainisha kwamba kurejea CCM siyo jambo la kushangaza,

 

kwani kabla ya vyama vingi alikuwa mwanachama na kiongozi ndani ya Chama na

 

kwamba amerejea tu nyumbani baada ya kutangatanga pembeni.

“Kama madaraka nimekaa ndani ya CCM tangu mwaka 1977 nikiwa Mwenyekiti wa

 

Serikali ya Mtaa Mlangede, Iringa kabla ya kuingia kwa mfumo wa vyama, anasema

 

Ngawaiya.

Ngawaiya anasema kuwa CCM haina mpinzani katika uchaguzi ujao, kwa kuwa itaibuka

 

na ushindi utakaowahakikishia wapinzani kwamba hawana chao.

Amewataka wananchi kuhakikisha kwamba kadi zao za kupiga kura wanazitunza hadi

 

siku ya upigaji kura wa rais, wabunge na madiwani ili wasipoteze haki yao ya

 

kupiga kura na kuhakikisha maendeleo ya Tanzania.