UHURU 18.10.2005
Dk. Sheni asema CCM itaboresha mikopo kwa wasomi wa vyuo vikuu
Na Peter Orwa, Bukoba
MKUTANO wa kampeni ya Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Sheni mwishoni mwa wiki ulikuwa kivutio kwa umati wa wakazi wa mji huu, ambapo aliwaambia kuwa serikali ijayo ya CCM, imepania kuboresha mikopo kwa wasomi wa vyuo vikuu, ili itolewe kwa wakati.
Dk. Sheni alisema hayo katika mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Uhuru mjini hapa, ambao
pia ulihudhuriwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Dk. Diodorus Kamala na mgombea ubunge wa Bukoba
Mjini, Khamis Kagasheki, aliyekuwa akishangiliwa kila alipotajwa. Dk. Kamala ni mgombea wa ubunge Nkenge.
"Tutahakikisha mikopo ya wanafunzi inatolewa kwa wakati, ili wanafunzi wa vyuo wasome bila yawasiwasi," alisema Dk. Sheni.
Pia, Dk. Sheni aliahidi wananachi kuwa serikali ijayo imepania kuboresha hospitali ya mkoa wa Kagera iliyopo mjini hapa, kuhakikisha huduma walizokuwa wanafuata wagonjwa katika hospitali za rufaa, ziwe zinapatikana hapohapo. Alitaja huduma hizo ni vifaa na madaktari bingwa katika hospitali hiyo.
Alisema mabadiliko hayo katika huduma za hospitali, ni miongoni mwa mikakati ya taifa, ambapo hospitali ya mkoani hapa ni moja ya walengwa, ambapo hoja ya matatizo ya afya yaliyolengwa kushughulikiwa kupitia mkakati huo ni maradhi ya moyo.
Kuhusiana na sifa za mgombea Urais, Dk. Sheni alimtaja mgombea Urais wa CCM Jakaya Kikwete kuwa uwezo wake ni mkubwa ukiandamana na ufanisi wa kazi.
"Ukimuona yuko kimya kama anakunywa uji wa maji kwa tende. Amekuwa waziri kwa miaka 17 na tangu amalize
Chuo Kikuu, ametumikia katika uongozi, na mimi tunafahamiana sana sana tangu nikiwa waziri huko Zanzibar, " alisema.
Alivishangaa vyama vya upinzani kuibeza CCM kuwa haijafanya chochote, wakati kuna mengi yanajionyesha, na kutoa mifano katika sekta za elimu, kilimo na afya hasa huduma za chanjo kwa watoto.
Dk. Sheni alisema CCM mara zote haiendi kujinadi mikono mitupu kwa wananchi, badala yake huwa na ilani ya uchaguzi inayotekelezeka juu ya yote yanayotarajiwa kufanywa.
"Wapinzani watake wasitake, CCM itashinda," alisema na kuongeza wapinzanihawana uwezo wala uzoefu wa kuongoza, hali iliyofanyaumati uliofurika uwanjani kushangilia huku wakitamka jina la Kagasheki aliyekuwa kivutio uwanjani na kutamka kwa lugha ya Kihaya, "Lwakatare (Wilfred) wa CUF achapwe viboko vya kura na aondoshwe". Lwakatare alikuwa mbunge kwa kipindi kilichopia.
Msisikilize uchochezi wa wapinzani
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MGOMBEA wa Chama Cha Mapinduzi nafasi ya Ubunge katika jimbo la Uzini, Unguja Muhammed Seif Khatib amewataka wananchi kutosikiliza maneno ya uchokozi kutoka kwa wapinzani wanaosema kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijafanya chochote katika kuleta maendeleo.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni katika jimbo la Uzini, Khatib alisema serikali imefanya mambo makubwa tangu kufanyika kwa mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 yaliyouondowa utawala wa kisultani na wazalendo kushika hatamu ya kuongoza nchi.
Alisema utekelezaji wa miradi mbali mbali ikiwemo wa usambazaji
umeme vijijini awamu ya nne ni ushahidi tosha jinsi Chama ChaMapinduzi kinavyotekeleza ilani yake kwa vitendo, huku lengo lake kubwa ni kuweka hali na maslahi ya wananchi kuwa bora.
“Leo hii wananchi wa vijijini vyote vya jimbo la Uzini wanapata umeme pamoja na maji safi mambo yote haya hayakupatikana katika kipindi cha utawala wa kisultani”, alisema Khatib ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshungulikia habari na siasa.
Alisema jimbo la Uzini sasa limepiga hatua kubwa za maendeleo ambapo huduma zote muhimu za jamii ikiwemo shule na hospitali zinapatikana, hatua ambayo imesaidia sana kuondosha shida mbali mbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi katika kusaka huduma hizo zaidi wakiwemo watoto na akinamama.
Mapema Khatib ambaye anagombea jimbo hilo kwa muda wa vipindi vitatu sasa, aliwataka wananchi kumchagua mgombea urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye ameonyesha uwezo mkubwa katika uongozi wa nchi hii.
Alitoa mfano katika kipindi cha kampeni zinazoendelea nchini kote mgombea wa CCM Kikwete ameweza kuzisambaratisha ngome za wapinzani wakiwemo wa CHADEMA na CUF katika sehemu mbali mbali za mikoa ya Tanzania Bara.
Aidha aliwataka wananchi hao kumchaguwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar Amani Abeid Karume ili amalize kazi aliyoibakisha ya kuwahudumia wananchi wa Unguja na Pemba pamoja na kusambaza maendeleovijijini.
Jimbo la Uzini wilaya ya kati ni miongoni mwa majimbo yanayofaidika na mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya nne unaofadhiliwa na serikali ya Norway kupitia shirika la kimataifa la NORAD ambao hadi kumalizika kwake jumla ya vijiji 36 vitafaidika na huduma hiyo Unguja na Pemba..
Nahodha asema ni ndoto Z’bar kuwa na serikali ya mseto
Na Khatib Suleiman,Zanzibar
WAZIRI Kiongozi wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha amesema ni ndoto kwa Zanzibar kuwa na serikali ya mseto kutokana na vyama viwili vya CCM na CUF kuwa na sera zinazotofautiana huku mmoja akihubiri amani na mwingine fujo.
Akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mkuu katika jimbo la uchaguzi la Mwanakwerekwe nje kidogo ya mji wa Unguja,Shamsi alisema CUF ni waongo ambao wanajidai wanataka serikali ya umoja mseto ili kuweza kuwarubuni wapiga kura tu.
“Zanzibar ni ndoto kuwa na serikali ya mseto. Wenzetu hawa wanahubiri fujo na uhasama wakati Chama Cha Mapinduzi kinahubiri amani na utulivu kwa wananchi”, alisema Shamsi na kusisitiza kwamba hivyo ni vitu viwili tofauti.
Alisema viongozi wa chama cha CUF waliwahi kuwemo katika serikali ya Chama Cha Mapinduzi lakini kutokana na matatizo yao yanayotokana na uroho wa madaraka walitimuliwa, hivyo siyo rahisi tena kuunda serikali ya mseto itakayovikutanisha vyama viwili vya siasa.
Mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha CUF,Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa akisema kwamba kama chama chake kitafanikiwa kushinda uchaguzi mkuu basi kitaunda serikali ya umoja wa kitaifa..
Mapema Shamsi aliwataka wanachama na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi kuwachagua wagombea wa nafasi za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kulivusha jahazi la Tanzania kwa amani na utulivu.
Shamsi alisema nyota njema huonekana asubuhi ambapo mgombea huyo zimekuwepo kila aina ya dalili za kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu kutokana na kukubalika kwake na wananchi katika kila maeneo anayokwenda kwa ajili ya kuomba kura.
Aidha Shamsi aliwataka wanaCCM kumchagua tena Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume katika kipindi kingine cha miaka mitano ili aweze kumaliza kazi mbali mbali ambazo amezianzisha ikiwemo miradi ya jamii.
Alisema Karume ameonesha kukubalika kutokana na uwezo wake mkubwa wa uchapa kazi pamoja na kusimamia miradi mbali mbali ambayo katika kipindi chake imeanzishwa tena na wafadhili ukiwemo mradi wa usambazaji umeme vijijini Unguja na Pemba.
Ngawaiya amnadi Keenja Manzese na kusema upinzani umekwisha
ALIYEKUWA Mbunge wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya TLP na baadaye kujiunga na CCM, Thomas Ngawaiwa amesema upinzani umekwisha na kwamba wanaoushabikia ni sawa na watu wachezao ngoma wasiyoijua.
Ngawaiya aliyasema hayo juzi katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea wa kiti cha ubunge wa jimbo la Ubungo, Charles Keenja uliofanyika katika viwanja vya Bakhressa Manzense mjini Dar es Salaam.
“Upinzani umekwisha wenzetu mnaoendelea kuwa CUF hamjui ngoma mnayoicheza, “ alisema Ngawaiya na kuongeza kwamba anajuta kupoteza muda wake mwingi akiwa katika kambi ya upinzani.
Alisema kukubali wapinzani ni sawa na kukubali kurudi nyuma na kukaribisha watu ambao waasisi wa taifa hili walipambana kuwaondoa na hatimaye kupatikana kwa uhuru ambao umekuwa ukitolewa mfano sehemu mbalimbali duniani.
Ngawaiya alisema kushabikia upinzani ni sawa na kukaribisha ghasia na vurugu kwani vyama hivyo havihubiri amani na utulivu kama ilivyo kwa CCM.
Alisema mbali na kupoteza muda pia hakuwatendea lolote wapiga kura wake katika kipindi cha miaka 10 akiwa katika kambi ya upinzani.
Ngawaiya alisema akiwa upinzani hakuweza kufanya lolote la maendeleo zaidi ya kushuhudia matukio ya ghasia yaliyoambatana na uchomaji moto wa magari na nyumba na utekaji wa nyara.
Kulingana na Ngawaiya kilichobaki kwa viongozi hao wa upinzani ni kuchukua ruzuku na kukaa huku wanachama na wapiga kura wao wakiendelea kuwa nyuma kimaendeleo.
Alisema hilo linatokana na ukweli kwamba vyama hivyo havina serikali na hivyo kuviwia CHARLES KEENJA
vigumu kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo tofauti na CCM ambacho kimekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Sera na Ilani yake ya uchaguzi.
Ngawaiya aliwataka wana- Manzese kutofanya makosa na kumchagua Keenja na diwani Eliam Manumbu ili waendeleze mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tatu.
Alisema chini ya uongozi wa CCM, sura ya Manzese imebadilika kwa kipindi kifupi na majengo yameshamiri mithili ya uyoga, ikiwa ni kielelezo cha maendeleo katika eneo hilo maarufu mjini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, CCM kilipokea wanachama watatu kutoka CUF na wengine wapya 34.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Hemed Mkali na
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kinondoni ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Dk. Asha Rose Migiro.
Karume aahidi kuimarisha sekta ya uwekezaji na kukuza ajira kwa vijana
Na Mwandishi Maalum, Zanzibar
MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume, amesema akichaguliwa kuendelea kushika wadhifa huo serikali yake chini ya CCM itaendelea kujenga miundombinu ya kutosha na kuimarisha sekta ya uwekezaji ili kutoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana nchini.
Karume alitoa maelezo hayo jana alipozungumza na wananchi na wana-CCM wa mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mikutano ya ndani ya kampeni zinazoendelea katika matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30, 2005.
Katika uongozi wake, Rais Karume ambaye anamaliza kipindi chake alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itaendelea na juhudi za kuongeza nafasi za ajira hasa katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, na kuhakikisha kuwa vijana wengi wanapata fursa ya kuajiriwa na kujiajiri.
Mgombea huyo wa urais Zanzibar alisema serikali imeshachukua juhudi kubwa ya kuimarisha sekta binafsi ambayo ni moja ya taasisi inayoweza kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wananchi nchini, ikiachwa sekta ya umma na sekta isiyo rasmi.
"Sekta binafsi tutaikuza kwa kuipalilia kwa sera nzuri za kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani. Sera zetu zinawapa nafuu wawekezaji wote...malengo na madhumuni ya kufanya hivyo ni kutaka kujenga miundombinu ya kutosha, tujenge uwezo wa kutosha wa uzalishaji ambao hatimae utazalisha ajira kwa wananchi wenyewe," alisema Rais Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.
Alisema kuwa lengo kubwa la SMZ kuchukua hatua hiyo ni kuimarisha uchumi, kuongeza kipato cha wananchi na kuondosha tatizo la ajira. "Mwekezaji wa ndani akijenga hoteli na anapohitaji wafanyakazi basi atachukua wafanyakazi wazalendo humu humu nchini, ukosefu wa ajira utakuwa amepunguzwa makali yake," alifafanua Rais Karume.
Mfano hai wa juhudi hizo za serikali, Rais Karume alieleza, ni kiwanda cha Sukari cha Mahonda ambacho kimepata mwekezaji ambaye atachukua wafanyakazi wa ndani nchini na hatimaye kupunguza tatizo la ajira kwa wakazi wengi wa eneo la Mkoa wa Kaskazini.
Mpango wa Maendeleo wa SMZ na Dira 2020 umezungumzia mipango mbali mbali ya kuinua uchumi na kuongeza kipato cha wananchi, na kuzidisha harakati za maendeleo ili wananchi wote waweze kuishi maisha bora zaidi, alisema Rais Karume.
Serikali imewekeza katika elimu ya msingi na mpango wa kuwasomesha vijana kuanzia skuli ya msingi hadi sekondari - darasa la 12, ambayo ni elimu ya lazima kwa wote na wengine kufika elimu ya chuo kikuu ili kuwawezesha vijana kujitegemea kimaisha hapo baadaye.
Hata hivyo, Rais Karume alisema msingi mkubwa wa mafanikio hayo yanatokana na kuwepo kwa amani na utulivu nchini ambapo pia Rais Karume aliwaasa vijana kufahamu kwamba tofauti kubwa ya sera za CCM na Sera za CUF, ni kwamba CCM inalenga na kutilia mkazo maendeleo ya vijana jambo ambalo haliwezekani kwa sera za CUF.
Sera ya CCM ya Uchaguzi ya 2005-2010 imetiliwa mkazo mkubwa suala la wananchi kuishi maisha bora, aliendelea Rais Karume.
Aidha, Rais Karume amesema kuwa CCM itaendelea kusimamia suala la Utawala Bora na shabaha kubwa ya kufanya hivyo ni kwamba Serikali ya SMZ inathamini sana maslahi, matakwa pamoja na kuheshimu mila, desturi za wananchi wake.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya atamba na kusema...
Namtumbo ngome ya CCM
Asema hakuna chama kitakachopata hata udiwani
JIMBO la Namtumbo mkoani Ruvuma ni jimbo pekee linaloogopwa na viongozi wa upinzani kutokana na msimamo wa wananchi wake kuwa imara na wasiotetereka na ahadi za kiinimacho za wapinzani. Mwandishi Wetu NOOR SHIJA hivi karibuni alizungumza na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Namtumbo, Maurice Nchimbi na anaeleza kwanini jimbo hilo ni ngombe ya CCM.
MWENYEKITI Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, Maurice Nchimbi ametamba kuwa jimbo la Namtumbo ni ngome ya CCM na kamwe hakuna chama cha upinzani kinachoweza kuibomoa.
Kiongozi huyo mkuu wa CCM wilayani humo alitoa kauli hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam alipokuja kwa shughuli zake binafsi.
KWA NINI DAR SASA?
Kabla ya kutoa tambo hizo, Nchimbi anaeleza sababu za yeye kuwepo Dar es Salaam katika kipindi hiki cha kampeni ambapo kila chama kinang'ang'ana kujaribu kutwaa uongozi katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani.
Baada ya kuulizwa swali hilo, Nchimbi hakuficha ukweli aliposema yeye ni miongoni mwa waastaafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki kwa upande wa posta na alikuja kufuata mafao yake.
"Subira yavuta kheri. Nilijua ipo siku moja tutalipwa mafao yetu japokuwa wengine wamekwisha fariki dunia," alisema.
Alisema pamoja na kutokea hali hiyo kwa wengine kutangulia mbele ya haki, anatumaini utaratibu upo kwa ajili ya warithi wao kulipwa na aliwaomba wawe na subira katika kufuata taratibu hizo.
Nchimbi alisema baada ya kustaafu kazi Desemba 1994 alimua kurudi nyumbani kwao Namtumbo ili akajiendeleze na shughuli za kilimo.
Hata hivyo, alipofika huko jamii ilimkubali kutokana na hekima na busara zake na mwaka 2002 aliombwa kugombea uenyekiti wa CCM wa wilaya alikubali ombo hilo na hatimaye kuchaguliwa kuwa kushika wadhifa huo.
NAMTUMBO NI CCM
Anasema hata kabla ya kuwa mwenyekiti Chama wilaya hakuna chama chochote cha upinzani kilichowahi kufurukuta na kujenga ngome yake jimboni na wilayani humo.
Nchimbi anabainisha kuwa hali hiyo inatokana na wananchi wa jimbo hilo wamezikubali zaidi sera za CCM kwa jinsi inavyosimamia na kuendeleza la amani na utulivu.
Nchimbi anasema kuwa wilaya ya Namtumbo ipo mpakani na Msumbiji hivyo wananchi wa eneo hilo wana uzoefu wa masuala ya vita yaliyotokea nchi jirani ya Msumbiji wakati wa kupigania uhuru.
Alisema kuwa suala la amani na utulivu ni jambo linalotiliwa umuhimu wa pekee na wananchi wa eneo hilo kwa kuwa panapokuwepo hali ya utulivu na usalama pia utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo nao unakuwa mkubwa.
Nchimbi alisema jimbo hilo ambalo lina Kata 12 tangu upinzani uanze hawajawahi kupata hata diwani mmoja pamoja na viti vyote vya serikali za mitaa na vitongoji.
Hata hivyo alisema kuna wapinzani wachache ambao hawana nguvu na mgombea urais wa Tanzania kwa Chama Cha Mapinduzi Jakaya kikwete alipokwenda kwenye jimbo hilo wapinzani wengi hasa wa CUF na TLP walirejea CCM.
Mwenyekiti wa CCM wilaya alisema hali hiyo pia ilijitokeza hata wakati wa mikutano ya kampeni ya mgombea mwenza wa CCM Dk. Ali Mohamed Sheni.
Mgombea pekee wa urais wa upinzani aliyekwenda jimboni hapo ni Profesa Ibrahim Lipumba ambaye hata hivyo alipata idadi ndogo ya watu kwa kuwa wengi walimpuuza na kwamba vyama hivyo vya upinzani havina nguvu ya kuweza kupata hata nafasi ya udiwani.
Nchimbi alisema kuwa jimbo hilo ambalo mgombea wa nafasi ya ubunge, Vita Kawawa, ana nafasi kubwa ya kushinda na kwamba jimbo hilo limepania kutoa kura nyingi kwa mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
VIKWAZO KIDOGO
Pamoja na kujikita kwa CCM, Nchimbi alisema kuna matatizo ya udiwani katika kata mbili ambazo baadhi ya wagombea katika kura za maoni ambao walishindwa wameonekana kutokubali matokeo.
Kuwepo kwa watu hao, alisema kunawafanya baadhi ya wana CCM kuamini kuwa wagombea hao walifanyiwa fitina na uobgozi wa Chama jambo ambalo siyo kweli.
Hata hivyo alisema Chama wilaya kimejitahidi kuyasawazisha kwa kuongeza nguvu za ziada katika kila kata ili kuhakikisha ushindi.
Kuhusu maendeleo ya jimbo, Nchimbi alisema katika wilaya au jimbo la Namtumbo, kuna shule nyingi zikiwepo za sekondari ambapo hakuna mtoto anayeshindwa kwenda shule ya msingi kwa sababu ya kukosa nafasi na kwamba kuna vituo vya kutosha vya afya.
Alisema kuwa wanachofanya hivi sasa ni kuhamasisha wananchi kutumia vyema fursa ya ukanda wa Mtwara kwa kujenga pembezoni mwa barabara ili waweze kufanya biashara na kuboresha maisha yao.
Nchimbi anasema kuwa jimbo hilo limekuwa na utaratibu wa
kushirikisha wananchi na kwamba kuna mikopo inayotolewa na vyama vya kuweka na
kukopa (SACCOS) na kwamba wanahamasisha wananchi kuunda vikundi vya maendeleo
ili wafaidike na mikopo ya serikali inayotolewa kwa vijana na wanawake.
'Arusha itazidi kung'ara chini ya CCM'
Na Omari Shaaban, Arusha
WANANCHI wa jiji la Arusha wametakiwa kuwachagua wagombea wa CCM, kwa kuwa ndiyo wenye mipango madhubuti ya maendeleo ya kuliweka jiji hilo, kimataifa zaidi na wananchi kupata ajira na elimu safi endelevu.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Katibu wa CCM wilaya ya Arusha Mohamed Monde, kwenye mkutano wa kampeni wa kamnadi mgombea Ubunge wa CCM, jimbo la Arusha, Felix Mrema kwenye Kata ya Kimandolu.
Mbonde alisema kamwe wapinzani hawataweza kulitwaa jiji la Arusha, kutokana na siasa zao za chuki na ugomvi na hawana mipango ya maendeleo kwa ajili ya wakazi wa jimbo la Arusha kama ilivyo CCM.
"Kamwe maendeleo ya nchi na jimbo hili hayawezi kuletwa na wapinzani, ndugu wananchi wasiwadanganye kwa nyama za mbuzi na ng'ombe ili muwape kura, ni waongo hao hawana sera na wababaishaji...kazi yao si mnaona ni kutukana tu," alisema Mbonde.
Alisema siyo kazi ya CCM, kuzungumza majungu bali CCM ni watu wachapakazi tena kwa vitendo ambavyo vinaonekana machoni mwa jamii ya kitanzania na wageni kama alivyo Felix Mrema katika jimbo la Arusha.
Naye mgombea ubunge, Mrema alisema kuwa kazi ya kuleta maendeleo kwenye jiji la Arusha na kutengeneza mipango ya ajira ni ya kwake na hivyo apewe nafasi ya kuliongoza jimbo ili mikakati iliyowekwa itekelezwe.
Mrema alisema wananchi hawana budi kuichagua CCM, kwa mtindo wa mafiga matatu ili mambo yaenda 'chapchap'.
Katika kuwaletea wananchi maendeleo alisema kwanza lazima wananchi wenyewe wawe na ari ya kujiletea maendeleo kama walivyofanya katika miaka mitano iliyopita ambapo mambo mengi ya maendeleo yamefanyika na yanaendelea kufanyika.
Mrema alisema shule nyingi za sekondari na msingi zimejengwa kwenye kipindi cha miaka mitano iliyopita na wananchi ni mashahidi ambapo mpaka mwanzoni mwa mwaka 2006, kata 11 zitakuwa na shule za sekondari katika kata 17 za jiji la Arusha.
"Lengo ni kila kata kuwa na shule ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na tunafanikiwa kwa kuwa wananchi mnaniunga mkono, hilo la shule kwa kipindi kijicho kitakwenda sambamba na kuwepo kwa vituo vya afya kwenye kila kata," alisema Mrema na kushangiliwa.
Alisema kuwa maendeleo ya kweli yanaletwa na CCM nchini, na siyo vinginevyo na kuwaomba wananchi kuwabomoa wapinzani ifikapo Oktoba 30, mwaka huu.
Mwapachu: Mazingira ya uwekezaji kuimarishwa
Na Hamida Khalid,Tanga
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Tanga kupitia CCM, Bakari Mwapachu amesema akichaguliwa tena kuliongoza jimbo hilo atahakikisha anaboresha na kuimarisha zaidi mazingira ya uwekezaji.
Mwapachu aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wake wa kampeni uliyofanyika kata ya Mabawa jijini hapa.
Alisema tayari ameshafanya mazungumzo na watu mbalimbali kutoka nje wenye nia ya kuja kuwekeza, njia itakayosaidia kufufua uchumi wa mkoa na hivyo kuboresha maisha ya watu wa Tanga.
Akizungumzia zaidi nia yake ya kuwania kiti hicho cha ubunge kwa mara nyingine, Mwapachu alisema hafanyi hivyo kwa lengo la kuboresha maslahi yake ila aweza kuwainua wananchi wa Tanga kiuchumi.
Alisema kuwa akipata ridhaa ya wananchi kumpa kura ya kuliongoza jiji hilo atazitumia kikamilifu rasilimali nyingi katika kuhakikisha kuwa Tanga inapiga hatua za maendeleo kwa haraka.
Mwapachu aliwataka wananchi kutofanya makosa kwa kuinyima kura CCM na kuwapa wapinzani watu aliowaita kuwa hawana uzoefu na uongozi.
"Hawa watu wamezoea kubeza na kuropoka tu lakini masuala ya uongozi hawayajui...hivyo wala msipate tabu na blablaa zao, siku ya kupiga kura ikifika msifanye makosa kura ni kwa Kikwete kwa urais, Mwapchu kwa ubunge na madiwani wa CCM,"alisema Mwapachu.
Kinondoni watakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura
Na Gabriel John
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Kinondoni Iddi Azani, kupitia Chama cha Mapinduzi amewataka wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kutotishika na kelele za wapinzani.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika tawi la Kwa Biyuda, kata ya Kinondoni Shamba.
Katika mkutano huo, aliyekuwa kaimu Katibu Kata wa CUF, tawi la Kumbukumbu Amida Megene alirejea CCM na kusema kuwa wapinzani hawana sera za kujenga bali zaidi ya kubomoa amani na utulivu uliopo.
Mgombea huyo aliwataka wana CCM kutotishika na kelele za chura ambazo hazimzuii tembo kunywa maji kwa kujitokeza kwa wingi katika siku ya kupiga kura.
Azani alisema CCM kimekuwa kikiwajali wananchi bila ubaguzi wowote katika kuwaleta maendeleo yao. Alisema sera madhubuti za CCM ndiyo mhimili mkubwa wa maendeleo ambapo mambo mengi yamefanywa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi.
Hata hivyo, Azani alisema serikali ijayo itahakikisha kuwa elimu inazidi kuboreshwa kuanzia sekondari hadi awali ili kila Mtanzania apate elimu iliyo bora.
Alisema kwa hivi sasa serikali ya awamu ya tatu imefanya mambo mengi hususan huduma za afya kwa kuweka vifaa vya kisasa na kupanua hospitali kadhaa nchini.
Naye mgombea udiwani wa kata ya Kinondoni Shamba, Michael Lupiana alisema wapinzani wana ubaguzi na hasa katika uongozi wa juu.
Alitoa mfano kuwa tangu mwaka 1995 nafasi za kuwania Urais Zanzibar zimeshikiliwa na Seif Sharif Hamad na kwa upande wa bara Profesa Ibrahim Lipumba jambo ambalo halitoi haki sawa kwa wanachama wake kama kauli mbio yao inavyosema.
"Nashangaa wanaposema haki sawa kwa wote, mbona hadi sasa
hawatoi usawa kwa wanachama wengine kwa nafasi za urais bara na visiwani kama si
ubabaishaji", alihoji Lupiana.
Mkapa aaga mikoa ya Kusini na kusema:
Nchi isikabidhiwe wenye kuhubiri sera za majimbo
Na Rashid Mussa, Mtwara
RAIS Benjamin Mkapa amewataka wananchi wasiwakabidhi nchi watu wenye sera za kimajimbo.
Rais alitoa mwito huo jana wakati alipowaaga wananchi wa mikoa ya Kusini kwa kuwaomba kutowakabidhi nchi watu watakaousambaratisha umoja wa kitaifa kwa kugawa rasmali ya taifa kimajimbo ama mikoa.
Alisema anawashukuru wananchi waliompa ridhaa ya kuongoza nchi katika awamu yake kwa kusimamia na kulinda muungano wa nchi kwa amani na utulivu.
Rais alisema wakati anaingia madarakani wapo waliodhani kuwa katika kipindi chake CCM ingesambaratika na kuvunja umoja na muungano uliopo, na kuifikisha nchi kwenye vurugu.
Lakini sasa alisema anafarijika kuona kuwa rasilimali hizo zimeimarika na kuendelezwa, na kuwaomba Watanzania kutowapa viongozi wanaotafuta wajomba wa nchi kutoka nje, wanaotumia lugha za uchochezi na kumwaga damu.
Alisema watu hao wanataka kuweka kizingiti cha kasi ya maendeleo yaliyofikiwa ambayo yanahitaji viongozi wa kuiendeleza, na kuomba wasiruhusiwe.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa mkoa huu na viongozi wa mikoa mitatu ya Mtwara Lindi na Ruvuma, Rais alisema anaamini kuwa Watanzania watawakataa kuwapa madaraka watu hao na kuwapa watu na chama kitakachoendeleza na kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika awamu yake ya utawala.
Alisema anashukuru kwa kuungwa mkono na wananchi katika kipindi chake cha uongozi ambacho amejitahidi sana kuwa mfuasi na mwanafunzi wa kweli wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa kufanya yale yaliyokuwa azma yake ya kulijenga taifa hili.
Alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na kampeni yake ya kufutiwa madeni makubwa yaliyokuwa yanamkera sana, ambapo yeye katika uongozi wake wamefanikiwa kupata msamaha wa madeni hayo kwa kiwango kikubwa na umesaidia katika kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na maji.
Rais ambaye katika hotuba yake alionyesha kukerwa na wanaopita pita katika kutafuta kura wakibeza mafanikio yaliyopatikana kudai kuwa wao watafuata nyayo za Mwalimu wakishika madaraka, alisema mashirika makubwa ya fedha IMF na Benki ya Dunia yameahidi kuifutia Tanzania sehemu kubwa ya madeni yake Januari na Julai mwakani.
Alisema watu wanaomtumia leo Mwalimu kupita kwa watu wakitafuta madaraka kwa kudai watamuenzi, baadhi yao ndio hao hao miaka mitano iliyopita walikuwa wakidai kuwa serikali ilitumia gharama kubwa kumuuguza, kumzika na mengine mengi, lakini sasa wanamtumia kutafutia kura.
Mkapa ambaye kabla ya kuanza kuhutubia alipokea risala za mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma zilizoelezea hatua kubwa iliyopigwa ya maendeleo katika sekta zote na kufanya hali ya maisha katika mikoa hii kuboreka ukilinganisha na miaka ya nyuma, alisema anaamini mafanikio hayo yamepatikana kwa wananchi kufanya kazi.
Alisema wapo wanaopitapita wakidai kuwa katika kipindi chake hakuna cho chote kilichofanyika katika mikoa ya Kusini, ambapo aliwajibu kuwa yeye hakuchaguliwa kwa ajili ya maendeleo ya mikoa hii ila ni kwa nchi nzima na anaamini kazi hiyo ameifanya kikamilifu kwa kushirikiana na wananchi wenyewe.
Rais alisema anawashukuru sana wananchi kwa kumpa nguvu ya kuongoza kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa ilani zote za uchaguzi za CCM kwa vipindi viwili vya utawala, hata kufanikiwa kufikia hapa ambapo kila mwananchi ameguswa na hatua hiyo ya maendeleo iliyopatikana.
Aliwaaga wananchi kwa kuwaahidi kuwatumikia hata kama hatakuwa na madaraka ama nafasi za utawala, lakini atashirikiana na wananchi katika yale ambayo atahitajika na kuwaomba wampe zawadi moja ya kisiasa ya kumchagulia rais na wabunge watakaounda serikali itakayoendeleza mafanikio haya.
Katika mkutano huo mikoa hiyo pamoja na kutoa salamu pia ilimzawadia jumla ya ng’ombe tisa wakiwemo wa kulimia maksai jozi moja, mbuzi wa maziwa 6 trekta dogo na vifaa vyake pamoja na tela mbili, shamba la bondeni lenye ukubwa wa ekari 50 na miche bora ya mikorosho 100.
Zawadi zingine ni vyakula mbali mbali, samani za ndani ya nyumba na mapambo ya vinyago na doti za khanga na vitenge.
Wananchi waliokuwa wamefurika katika Uwanja wa Umoja kumuaga Rais wengi walishindwa kujizuia machozi pale kwaya ya ‘Safina’ ya mjini hapa wakiongozwa na Michael Amlima ambaye aliuimba kwa hisia kali wimbo wa kumuaga katika ubeti wa ‘kwa heri’.
Kikwete aahidi atajenga daraja mto Kilombero
Na Dunia Mzobora na Prosper Kulita, Ulanga
MGOMBEA Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapunduzi, Jakaya Kiikwete ameahidi kujenga daraja la Mto Kilombero.
Kikwete alitoa ahadi hiyo alipohutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika mjini hapa jana mchana.
Mto Kilombero ndio unaozigawa wilaya za Ulanga na Kilombero katika mkoa wa Morogoro.
Alisema serikali ya awamu ya nne itajenga daraja hilo ili kuwaondolea kero kubwa wananchi wa wilaya hizo ambao hutenganishwa na mto huo.
Ujenzi wa daraja hilo utafanyika katika kipindi kisichozidi miaka mitatu na tayari usanifu na uchoraji wa daraja hilo unaendelea.
Kivuko kilichopo siyo kwamba hakifanyi kazi, ila wakati wa kiangazi maji yanapokuwa madogo hufanya kazi kwa shida.
Mgombea alisema mto huo umekuwa ukisababisha kero na maafa makubwa kwa wananchi wa wilaya hizo, ambazo kwa kiwango kikubwa zinasababishwa na matatizo ya kivuko kilichopo kwenye mto huo.
Aprili mwaka juzi (2002) zaidi ya watu 70 walikufa baada ya kivuko kinachovusha wananchi na magari katika mto huo kuzama na kusababisha maafa hayo.
Kikwete alisema ahadi hiyo ya ujenzi wa daraja hilo siyo tu kwamba itaondoa kero kwa wananchi lakini pia itakuwa kichocheo cha maendeleo ya wananchi wa wilaya hizo.
Pamba, mpunga na mahindi ni miongoni mwa mazao yanayolimwa kwa wingi katika wilaya hizo.
Katika mkutano huo aliwatambulisha wagombea udiwani wa halmashauri ya Ulanga na Ubunge, Selina Kombani.
Aidha alimsimamisha aliyeshinda mchakato wa kura za maoni katika jimbo la Ulanga Mashariki, Aziz Jawaad Kimeture ambaye ilidaiwa alikuwa amekasirishwa na uteuzi wa Selina katika mchakato huo.
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni Aziz alisema yeye hana kinyongo kwa kuteuliwa kwa Selina kugombea jimbo hilo, na kuongeza kwamba kambi iliyokuwa upande wake ilikwishavunjwa toka zamani na kwamba kilichopo ni kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo.
Katika mkutano uliofanyika katika jimbo la Ulanga Magharibi, Kikwete alimnadi mgombea wa jimbo hilo, Dk. Juma Ngasongwa ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
Mapema Kikwete aliwasili kwenye uwanja mdogo wa ndege kwenye hifadhi ya Selous ambapo alipokewa na umati mkubwa wa wananchi na baadae kwenda mjini Ulanga ambako alihutubia mkutano wa kampeni kabla ya mwingine uliofanyika kwenye uwanja wa mpira katika kata ya Lupilo.
Maandalizi ya uchaguzi yanaendelea vizuri - ZEC
Masanduku, wino vimewasili Z'bar
Na Khatib Suleiman, Zanzibar
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 30 mwaka huu, yanaendelea vizuri ambapo vifaa mbalimbali vya kupigia kura yakiwemo masanduku na wino vimeshawasili hapa.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Masauni Yussuf Masauni, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba jumla ya masanduku 6,600 ya kupigia kura yenye uwezo wa kuonyesha ndani, yameshawasili visiwani.
Alisema kazi ya usambazaji wa masanduku hayo imeshaanza kwa kupelekwa kisiwani Pemba na kwa upande wa Unguja ilianza tokea Ijumaa wiki iliyopita katika wilaya mbalimbali.
Masauni alisema masanduku hayo yametengenezwa yakiwa yanaonyesha ndani ili mpiga kura atakapotumbukiza kura yake ionekane.
"Masanduku ya safari hii yatakuwa ya aina yake, tunataka kuondoa ulalamishi ambao hujitokeza mara kwa mara katika upigaji kura," alisema Masauni na kuongeza kuwa vifaa vingine vitasambazwa katika wilaya kulingana na utaratibu uliopangwa.
Alisema kazi ya uchapishaji wa karatasi za kura imeanza mwanzoni mwa Oktoba nchini Afrika Kusini, ambako zinachapwa na kampuni ya Free State Business Product, na kuwa makamisaa wa ZEC na maofisa wao wote wanashungulikia kazi hiyo.
Alisema shehena ya kwanza ya karatasi hizo itawasili hapa Oktoba 19 na kupelekwa kisiwani Pemba, na shehena nyingine ya karatasi itawasili hapa Oktoba 21.
Mwenyekiti huyo wa ZEC alisema wakati karatasi hizo za kura zitakapowasili, watashirikishwa wadau wote wahusika vikiwemo vyama vya siasa.
"Tunataka kufanya mambo yetu kwa uwazi zaidi, hakuna siri hapa. Wakati karatasi zitakapowasili tutawashirikisha wadau wote kushuhudia," alisisitiza hali ambayo ni dalili nzuri inayoashiria kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30, katika mazingira ya uwazi zaidi.
Alisema kura zote zitahesabiwa katika vituo vya kupigia kura ambapo matokeo ya kura za rais, wawakilishi, wabunge na madiwani zitafahamika hapo hapo.
Jumla ya vituo 1,630 vya kupigia kura vimepangwa katika maeneo yote ya Unguja na Pemba, ambapo vituo vilivyotumika katika uandikishaji wapiga kura katika daftari la kudumu, ndiyo hivyo hivyo vitakavyotumika kwa kupigia kura.
Uchaguzi Mkuu wa urais wa Zanzibar na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge, wawakilishi na madiwani unatarajiwa kufanyika Oktoba 30 mwaka huu, nchini kote.
Rais Mkapa ziarani Rwanda
Na Mwandishi Wetu
RAIS Benjamin Mkapa anaondoka nchini leo kwenda Kigali, Rwanda, ambako atakuwa na ziara rasmi ya siku mbili.
Ziara hiyo inafuatia mwaliko aliopewa na Rais Paul Kagame, wakati alipofanya ziara rasmi hapa nchini Mei mwaka huu, ambapo alimwomba Rais Mkapa aitembelee Rwanda kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi.
Akiwa nchini humo, Rais atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, atatembelea Taasisi ya Sayansi na Teknolojia, atatembelea Gizozi yalipo makumbusho ya mauaji ya Rwanda. Pia atazungumza na Watanzania waishio Rwanda.
Rais atawaaga wananchi wa Rwanda na kulihutubia Bunge la nchi hiyo kesho.
Hadi sasa Rais Mkapa amekwishafanya ziara za kuwaaga wananchi wa Kenya na Uganda, na kwa upande wa nchi za SADC, rais aliagana na wananchi hao kupitia viongozi wao katika mkutano uliofanyika nchini Botswana, Agosti mwaka huu.
Pia amekwishawaaga viongozi wa Umoja wa Afrika katika mkutano uliofanyika Sitre, Libya.
Rais na ujumbe wake ambao atakuwemo mkewe, Mama Anna Mkapa, atarejea nyumbani Oktoba 10, ambapo atakwenda moja kwa moja mkoani Mbeya, ambako Oktoba 20, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Songwe.
Naye, Solomon Mwansele ameripoti kutoka Mbeya, kuwa Rais Mkapa atawaaga wananchi wa Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa, atakapokwenda huko kuweka jiwe la msingi la uwanja huo mpya wa ndege wa Mbeya.
Pia katika ziara hiyo, Rais Mkapa atawaandalia futari Waislamu wa mikoa ya Nyanda za Juu katika ukumbi wa Benjamin Mkapa uliopo jijini hapa.
Akitoa ratiba kwa waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mateo Qaresi, alisema viongozi na wananchi wa mikoa ya Iringa, Rukwa, Ruvuma na Mbeya watashiriki katika tukio hilo la kihistoria.
Wakenya wasakwa kwa uporaji wa mamilioni ya fedha
Ni katika duka la Mac Sons
Na Mwandishi Wetu
RAIA watatu wa Kenya wanatafutwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na uporaji wa fedha aina mbalimbali za jumla ya sh. milioni 150 katika duka la kubadilishia fedha la Mac Sons Bureau de Change jijini Dar es Salaam mwezi uliopita.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, jana aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Seremia Mbeo Owuor, Michael M. Kitoo na Jafari Kiusa.
Alisema, Owuor anatuhumiwa kuhusika kutokana na kupatikana katika eneo la tukio hilo lililotokea Septemba 20, pochi iliyokuwa na hati ya muda ya kusafiria iliyotolewa Kenya.
Tibaigana alisema picha za Owuor ziliweza kutambuliwa na wenye duka hilo kuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifika hapo mara kwa mara.
Alisema, Kitoo amehusishwa baada ya kupatikana hati yake ya kusafiria aliyoamua kuitelekeza pamoja na tiketi baada wakati akipekuliwa kwenye uwanja wa Dar es Salaam.
Tibaigana alisema, wakati akipekuliwa na maofisa usalama wa kiwanjani, Kitoo alitoweka baada ya kufanikiwa kondoka katika eneo la upekuzi na kwenda nje akiwaeleza wapekuzi hao kuwa alikuwa akienda kumleta shangazi yake.
Alisema, Kiusa naye baada ya picha yake kupatika na kupelekwa kwenye duka hilo walimtambua kuwa miongoni mwa majmabazi yaliyohusika katika uporaji huo.
Kuhusu matukio mengine, Tibaigana alisema, watu watatu wamekutwa wamkufa maji baharini katika eneo la Ununio wilaya ya Kinondoni.
Aliwataja waliokufa kuwa ni, Gustafu Damba (15) ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Jordan na mkazi wa eneo la Nyaishozi, Tegeta.
Wengine ni Jeka Kassim (13) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Ununio na kuishi Tegeta na Issa Ibrahim (28) aliyekuwa mfanyabiashara ndogo ndogo eneo la Tegeta.