UHURU 21.10.2005
TUME YA UCHAGUZI YAWAAMBIA WAANGALIZI:
Muwe huru, lakini msiingilie taratibu
Watakiwa pia kutoshabikia upande wowote
Na Mwandishi Wetu
WAANGALIZI wa uchaguzi kutoka nje na ndani wametakiwa kuwa huru, lakini bila kuingilia taratibu za uchaguzi au kushabikia upande wowote katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajab Kiravu, katika mkutano kati ya NEC na baadhi ya waangalizi kutoka nje ambao wamewasili nchini.
Mkutano huo wa ndani uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Dar es Salaam, ulilenga kutoa maelekezo ya namna ya kuendesha shughuli za uangalizi kwa kuzingatia taratibu na sheria zinazosimamia uchaguzi nchini.
“Tumewaeleza (waangalizi) wawe huru, lakini wasishabikie au kupendelea upande wowote,” alisema Kiravu na kuongeza pia wametakiwa kuheshimu taratibu na sheria zinazosimamia uchaguzi.
Kwa mujibu wa Kiravu wanatarajia kupokea timu zizopungua 20 za waangalizi kutoka nje ya nchi, idadi aliyosema inaweza kuwa kubwa ikilinganishwa na mwaka 2000.
Alisema hilo linatokana na ukweli kwamba mataifa na taasisi nyingi duniani zimekuwa zikivutiwa na jinsi uchaguzi unavyoendeshwa nchini.
Pia, alisema wengine wanatumia fursa hiyo kuja kujifunza siasa za Tanzania ambazo zimekuwa zikiendeshwa katika mazingira ya amani na utulivu.
Kiravu alisema waangalizi wa awali ambao walishawasili hadi jana ni kutoka Norway, Umoja wa Afrika na Jumuia ya Afrika Mashariki.
Wengine ni kutoka Sekretarieti ya Uchaguzi ya Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Sekretarieti ya Wabunge wa SADC, Sekretarieti ya Nchi za Jumuiya ya Madola, na ya Taasisi ya National Democracy ya Marekani.
Alisema mkutano na waangalizi hao ulipangwa kufanyika Oktoba 27, mwaka huu, lakini kutokana na majukumu waliyonayo baadhi ya waangalizi hao wamelazimika kukutana na NEC ili waendelee na shughuli zao.
Kiravu alisema wanatarajia kuendelea kupokea waangalizi wengine wakiwemo mabolozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini.
Kuhusu usambazaji wa vifaa, alisema shughuli hiyo inaendelea vizuri na vifaa vya mwisho zikiwemo karatasi za kupigia kura zitakuwa zimefika vituoni ifikapo mwishoni mwa wiki hii.
Akizungumzia upigaji kura kwa watu wasioona, alisema katarasi maalum kwa ajili ya makundi hayo zimewasili na mafunzo kupitia viongozi wao ya jinsi ya kupiga kura zao, yanaendelea.
Hata hivyo, alisema watu wa kundi hilo wanaweza kupiga kura kwa kutumia utaratibu wa zamani wa kwenda na mtu kwenye kituo cha kupigia kura ambaye atamsaidia katika kutekeleza haki hiyo ya kidemokrasia.
Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini watapiga kura katika uchaguzi mkuu, kuchagua viongozi wao wa awamu ya nne Oktoba 30 mwaka huu. Uchaguzi huo hufanyika kila baada ya miaka mitano.
Tumekuwa wavumilivu mno kwa wapinzani, asema Mkapa
Na Idefonce Mgimba, Mbeya
Rais Benjamin Mkapa amesema serikali imekuwa na uvumilivu mkubwa kwa viongozi wa vyama vya siasa wanaotoa matamshi yanayoshawishi uvunjaji wa amani kwa nia ya kutafuta kuingia Ikulu.
Rais Mkapa alirudia kuwaonya baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanaotamka kwenye mikutano ya hadhara kuwa wasiposhinda katika uchaguzi ujao, damu itamwagika kuwa matamshi hayo ni matamshi yanayokaribia kuwa ya kigaidi na ya kichochezi, ambayo mtu anastahili kushughulikiwa.
Rais Mkapa alitoa kauli hiyo jana mjini hapa, wakati akiwaaga wakazi wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe.
Alisema akiwa rais wa serikali iliyoko madarakani anawajibika kutetea mafanikio yaliyofikiwa na serikali yake, kwa kuhakikisha anawashawishi wananchi waichague serikali ya chama chake iweze kuendeleza mafanikio yaliyofikia.
Akiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Mkapa alisema anawajibika kutetea mafanikio makubwa yaliyofikiwa na serikali ya CCM, ambayo alisema wapinzani hawayaoni kwa kuwa tu wanaitaka Ikulu hata kwa kumwaga damu ya Watanzania.
Rais Mkapa alisema vyama vya upinzani vimeshindwa kuandaa sera na kuzinadi kwa wananchi na badala yake vinazunguka na kubeza rekodi ya utekelezaji wa sera za CCM na serikali yake.
Alisema CCM katika ilani yake ya mwaka 1995 ilitamka wazi kuwa inaunda mfumo mpya wa vyama vingi vya siasa na kutoa uhuru wa kupingana pasipo kupigana, lakini alisema vyama vya upinzani vinataka kupingana kwa kupigana.
"Kama uhuru huu wa kupayuka ovyo ovyo, wa kutoa tathmini isiyothibitika juu ya hali ya Watanzania, matarajio yao, imani yao ya kisiasa na nguvu zao za kujiendeleza, kama uhuru huu siyo kielelezo kwamba chama tawala na serikali yake imeimarisha mfumo mpya wa vyama vingi vya siasa unataka uthibitisho gani?" aliuliza Rais Mkapa.
"Wanatoa kauli ambazo mara nyingi zinakaribia kuwa za ugaidi au uchochezi wa kuvunja amani. Tungeweza kabisa kuwashughulikia, kuwatia ndani, lakini tumewavumilia pamoja na kauli zao hizo ambazo siyo tu zinakebehi maendeleo ya Watanzania, lakini zinachochea uvunjaji wa amani. Tumewavumilia, unataka ushahidi gani zaidi kwamba tumetimiza ahadi yetu ya kuimarisha mfumo wa vyama vingi vya siasa," alisema.
Alisema wapinzani wanabeza matunda ya sera za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere juu ya elimu, ambazo ni sera zilizowawezesha wao kupata shahada wanazojivunia.
"Nasema tumewavumilia sana sana mwenendo wao, kauli zao, matamshi yao hata vituko vyao vinavyotaka kudhuru wananchi, vinavyotaka kuchochea vurugu ndani ya nchi, na wengine wako kimbelembele kabisa kwenye mikutano ya hadhara wanasema wasiposhinda damu itamwagika," alisema.
Aliwataka Watanzania kuwa macho na wanasiasa wanaoutafuta uongozi kwa njia ya kumwaga damu.
Alisema moja ya sababu ya kuwavumilia wapinzani wanaotoa matamshi yanayoshawishi vurugu nchini ni kuamini kuwa Watanzania wana mwamko mkubwa wa siasa unaowafanya wasiweze kuwapa madaraka watu wa namna hiyo.
Rais Mkapa alisema serikali ya awamu ya tatu imefanya mengi na kupata sifa kutoka nchi mbalimbali duniani, na hivyo vyama vya upinzani havina haki ya kuyabeza maendeleo hayo ambayo yametokana na sera nzuri na ahadi za CCM.
Alisema Chama cha Mpinduzi kimefaulu kutekeleza kwa makini na mafanikio makubwa ahadi za kutoa huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo mafanikio ya miundombinu, elimu, afya, maji na mengineyo mengi, ambayo kila mwananchi anayaona na hivyo alisema kubeza mafanikio hayo ni kuwadharau wananchi.
Aliwataka wananchi kutokubali kutoa ridhaa ya uongozi wa nchi kwa vyama ambavyo bado havina uwezo wa uongozi na vinavyotegemea kubebwa na wajomba kutoka nchi za nje.
Msipoteze kura zenu kwa upinzani – Kikwete
Asema yeye ndiye mwenye nafasi ya kushinda urais
Na Selina Wilson, Kisarawe
JAKAYA Kikwete ameendelea kuwaomba Watanzania wakichague Chama cha Mapinduzi kwa vile wakichagua vyama vya upinzani, kura zao zitapotea bure, kwani kwa nafasi ya urais yeye ndiye mwenye uhakika wa kushinda kwa ushindi wa kimbunga.
Alisema wagombea urais wa vyama vya upinzani wataambulia patupu na hawana chao katika nafasi ya urais, kwani ametembea nchi nzima na Pwani ni mkoa wa 25, ambapo huko amekuwa akipata mapokezi ya kihistoria jambo linalomfanya aamini kwa asilimia kubwa kuwa anaungwa mkono na wananchi wengi zaidi.
Kikwete anayegombea urais kwa tiketi ya CCM, alisema kuna baadhi ya vyama vya upinzani havina hata anuani, hivyo makao makuu ni hapo utakapokutana na kiongozi wa chama husika, tofauti na CCM ambayo mtandao wake ni mpana na wenye kueleweka kuanzia ngazi ya shina hadi uongozi wa kitaifa, na ni chama chenye mipango madhubuti ya kuendeleza Watanzania.
Mgombea huyo ambaye jana alifanya kampeni katika mkoa wa Pwani, aliyasema hayo akiwa katika maeneo tofauti ya jimbo la Kisarawe ambako alipokelewa na umati wa wananchi kila alikopita kuomba kura. Uchaguzi mkuu wa rais na wabunge na madiwani, utafanyika Oktoba 30, mwaka huu.
Kikwete aliahidi endapo atachaguliwa atahakikisha kabla ya mwaka mpya barabara ya kilomita 6 Pugu hadi Kisarawe ambayo iko katika matengenezo kwa kiwango cha lami, inakamilika na wana Kisarawe watapita kwenye lami wakati wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya, kwani moja ya mambo atakayofanya ni kukamilisha yale ambayo Rais Mkapa ameyaanza.
Alisema anaamini yeye ndiye atakayekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo ataunda serikali itakayozingatia maslahi ya wananchi, ikizingatia sekta zote muhimu kama elimu, afya, maji, kilimo, mawasiliano na kuboresha miundo mbinu, mambo ambayo katika serikali ya awamu ya tatu yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Akiwa katika tarafa ya Mzenga, mgombea huyo wa urais kupitia CCM alisema endapo wananchi wataichagua CCM kuongoza serikali katika awamu ya nne, itahakikisha tatizo la maji ambalo linaikabili wilaya ya Kisarawe linatatuliwa ili kuwawezesha wananchi kuishi maisha bora bila kero.
Alisema serikali ijayo itazingatia kuboresha huduma mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku katika bei ya mbolea, zana za kilimo na dawa za mifugo, ili vipatikane kwa bei nafuu ambayo mwananchi wa kawaida atamudu kununua na kuongeza uzalishaji wa mazao, na kwamba mikakati itawekwa kuhakikisha bidhaa zote zinapatiwa masoko ya uhakika.
Kikwete alisema endapo atapata ridhaa ya wananchi kuongoza serikali, shabaha yake ni kuhakikisha Watanzania wanaondoka katika matumizi ya damu kwa maana ya nguvu nyingi, na watumie mashine zaidi katika shughuli zao za uzalishaji mali ili waweze kuishi maisha bora na salama.
Alisema CCM ndicho chama pekee kinachoweza kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwa ina uzoefu na uwezo wa kuongoza, tofauti na vyama vya upinzani ambavyo ni vichanga na havina mtandao wa kuwawezesha Watanzania kufikia kilele cha maendeleo kwa vile sera zimelenga kuwasambaratisha wananchi na kuvuruga amani.
Aliwataka wananchi kuhakikisha hawafanyi makosa katika nafasi za ubunge na udiwani wote wachague wa CCM na kwamba mafiga matatu ndiyo yatakayoweza kufanikiwa kupika chakula, lakini wakichagua mbunge au diwani wa chama kingine viongozi wao watakuwa kama ‘wakiwa’ kwani hawataweza kuwaletea maendeleo kwani hawatakuwa tayari kushirikiana naye kwa vile ni wapinzani na kazi yao ni kupinga serikali iliyoko madarakani.
Akiwa njiani kuelekea Maneromango, mgombe huyo wa urais msafara wake ulisimamishwa na wananchi wakiwemo wa wafuasi wa vyama vya upinzani vya CUF na TLP ambao walikuwa wakirejesha kadi za vyama vyao na kumuunga mkono kwa kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Mgombea huyo wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi alilazimika kusimama na kusalimiana na wananchi katika vijiji vya Mzenga B, Kurui na Masaki ambako alikabidhiwa kadi saba toka kwa wafuasi wa CUF ambao waliamua kurudi CCM.
Akizungumza na wananchi mjini Kisarawe katika viwanja vya Chanzige, Kikwete alilakiwa na umati mkubwa wa watu na alipopanda jukwaani kuomba kura alikatizwa na wana TLP watano waliolazimika kumkabidhi kadi za chama chao baada ya kuvutiwa na kuridhishwa na ahadi zenye neema kwa Watanzania.
Aliwaambia wananchi kuwa wapinzani wakiwapa bendera kupeperusha kwenye maeneo yao, wazipeperusha kwa sababu wanalipwa kufanya hivyo, lakini sku ya uchaguzi waichague CCM kwa sababu hakutakuwa na mtu atakayewasimamia wakati wa kupiga kura.
Katika mikutano miwili mikubwa aliyoifanya katika maeneo ya Maneromango na mjini Kisarawe, Kikwete alipokea wanachama wapya zaidi ya 2,000 na kuwakabidhi kadi za chama chake, ambapo alimuombea kura mgombea ubunge Athumani Janguo, na kuwanadi madiwani.
Idadi hiyo inafanya jumla ya wanachama wapya waliongia Chama cha Mapinduzi mkoani Pwani kutoka upinzani kufikia 13,000.
Wanyarwanda wamwuliza Rais Mkapa siri ya amani Tanzania
Na Maura Mwingira, Kigali
WABUNGE wa Bunge la nchi hiyo wamemwomba Rais Benjamin Mkapa awaeleze ni siri gani inayoifanya Tanzania iwe na amani na utulivu.
Wabunge hao walimwuliza swali hilo kwa nyakati tofauti Rais Mkapa wakati wa kipindi cha maswali na majibu baada ya Rais kulihutubia Bunge hilo hapo jana. Rais alikuwa nchini Rwanda kwa ziara ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine aliagana na wananchi kupitia Bunge hilo.
Mbunge Ayubu Omari aliuliza: “Kwanza nakupongeza kwa hotuba yako nzuri na yenye mafunzo makubwa. Tanzania inasifika kuwa nchi ya mfano bora kwa kuenzi utamaduni wa amani, utulivu na demokrasia. Lakini tunakuomba utueleze ni siri gani hiyo ambayo imeifanya Tanzania iwe kama iliyvo, yaani kisiwa cha amani”.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, nchi nyingi za Afrika zimetetereka kwa njia moja au nyingine, lakini Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani, utulivu na wananchi wake wakiwa na mshikamano mkubwa jambo linalowafanya wajiulize kuna siri gani ya ziada inayoifanya Tanzania na Watanzania wawe kama walivyo.
Alisema kuwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika kwa jumla zinaweza kujifunza mambo mengi kutoka ‘kisiwa hicho cha amani’ na kuongeza kuwa Tanzania inaweza kuwa Taasisi muhimu sana kwenye kutoa msaada mkubwa kwa nchi ambazo zilijaribu kuwa na amani, lakini zikatetereka na kwa zile ambazo hazijatetereka zikajitahidi kutetereka.
Mbunge Kilambo akimshukuru Rais Mkapa kwa kuitembelea nchi yao na kulihutubia Bunge, alisema kuwa Tanzania inabaki kuwa tumaini pekee la Afrika na kuendelea kudumisha amani na utulivu.
“Mheshimiwa Rais, tunakuomba utupatie elimu zaidi kuhusu umuhimu wa utulivu kwa kiasi katika kanda yetu ya nchi za Maziwa Makuu na katika Afrika kwa jumla,” alisihi mbunge huyo.
Mbunge Rugemamiki, alitaka kufahamu ni lini Tanzania itarejea kenye COMESA na vile vile alitaka uthibitisho kama ni kweli Rwanda itajiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki mwishoni mwa mwaka huu.
Akijibu hoja hizo na nyingine, Rais Mkapa alisema kuwa hakuna siri yoyote ya ziada ambayo imeifanya Tanzania na Watanzania kuwa kama walivyo.
Alifafanua kuwa matumizi ya lugha ya Kiswahili yamewafanya Watanzania waungane na kuwa kitu kimoja na kwamba juhudi za kupiga vita vitendo vya ukabilia, udini na ubaguzi wa rangi yaliyotekelezwa baada ya kupata uhuru ndiyo hasa miongoni mwa mambo yanayoifanya Tanzania kuwa kama ilivyo.
Aliongoza kuwa baada ya uhuru serikali ya Tanzania ilirithi baadhi ya mambo ya kiutawala yaliyokuwa yakifanywa na serikali ya kikoloni ya Kiingereza.
Mkapa alizitaja taratibu hizo ni kuwa zile za mtumishi wa serikali kupangiwa kazi mahali popote nchini. Kwa mfano, alisema mtu aliyezaliwa kusini, alipangiwa kwenda kufanya kazi kaskazini na wa kaskazini alipelekwa kusini.
Rais alisema utaratibu huu uliwawezesha Watanzania kuchanganyika na kujiona kuwa ni watu wamoja
Kuhusu Tanzania kurejea COMESA, Rais alisema kuwa jambo hilo linaendelea kujadiliwa ndani ya serikali na huenda uamuzi ukatolewa hivi karibuni.
Nendeni mkapige kura, msiogope - Polisi
Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi nchini limewataka wananchi wenye shahada za kupiga kura kutokuwa na hofu na wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi kwa kuwa ulinzi utaimarishwa kwa kiwango kikubwa.
Taarifa ilitolewa kwa vyombo vya habari jana kutiwa saini na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Aden Mwamunyange, ilisema jeshi hilo litahakikisha kunakuwa na hali ya amani na utulivu wakati wa upigaji wa kura.
Pia, lilisema halitasita kuvunja maandamano yatakayofanywa kinyume cha na maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sheria na makubaliano yaliyofikiwa baina ya vyama vya siasa nchini.
Taarifa hiyo inafuatia vurugu zilizojitokeza hivi karibuni katika majimbo ya Musoma Mjini na Tarime ambapo polisi ililazimika kutumia mabomu ya machozi ili kutuliza ghasia zilizojitokeza katika maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa vyama mbalimbali mkoani Mara.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilifafanua kwamba hakuna mtu aliyeumia au kufa kama ilivyodaiwa na baadhi ya wagombea.
Ilisema vurugu hizo, zilijenga chuki miongoni mwa wafuasi na wafuasi wa vyama vya siasa na hasa katika jimbo la Musoma Mjini na vile vile jimbo la Tarime.
Pia, ilibainika kwamba baadhi ya viongozi na wafuasi wa vyama husika wanaongozwa zaidi na malengo la kuvunja amani, kukiuka sheria na kuonyesha ubabe usio na maana badala ya kunadi sera zao na kuwaacha wananchi kuamua juu ya nani wampe ridhaa ya kuongoza.
Aidha, ilibainika pia kwamba lengo lao ni kuwajengea wananchi hofu ili ifikapo siku ya kupiga kura wasijitokeze kwa wingi kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.
"Kwa sababu ni jukumu la serikali kudumisha amani na utulivu nchini, Jeshi la Polisi litakuwa linavunja maandamano yafanywayo kinyume cha maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sheria na makubaliano kati ya vyama vya siasa nchini," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wazee CUF wamwambia Rais Mkapa hawataki vurugu uchaguzi mkuu
Na Eva Jeremia (RCJ) na Restuta James (DSJ)
WAZEE wa chama cha CUF wamesema hawataki vurugu zitokee kabla na baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.
Kufuatia hali hiyo wamemwomba Rais Banjamin Mkapa na serikali yake, kusimamia na kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika bila vurugu na nchi inaendelea kuwa shwari baada ya uchaguzi.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jana, walisema wameufikisha ujumbe huo kwa Rais Mkapa kupitia kwa mshauri wake mkuu, Kingunge Ngombale Mwiru.
Walisema hawapendi kuona uvunjifu wa amani ukiendelea kutokea kama inavyojionyesha sasa kufuatia vurugu zinazotokea kwenye mikutano kadhaa ya kampeni.
Katika barua hiyo iliyoandikwa na kutiwa saini na Mzee Ali Abasi, wazee hao wamemwomba Rais kutoa kauli yake kuhusiana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua pindi hali ya vurugu ikiendelea kujitokeza.
Walisema wao kama wazee kazi yao kubwa ni kuonyesha njia, kushauri, ikibidi kuonya na hata kukemea juu ya uovu wowote unaofanyika katika nchi.
Katika taarifa yao walisema kuwa pamoja na kuonyesha hali ambayo siyo nzuri katika masuala ya kisiasa bado hawajasikia kauli ya Rais Mkapa kuhusiana na hali hii.
Wazee hao walimwomba Rais Mkapa kuhakikisha uchaguzi unasimamiwa katika misingi ya uhuru na haki na kukemea vitendo vyote vya vurugu vinavyoweza kusababisha amani kupotea nchini.
Vilevile, waliiomba serikali kufikiria kwa makini usalama wa raia na mali zao, watoto, wanawake na vijana wenye ulemavu na hasa wazee.
Wanawake watakiwa kuwaenzi wenzao waasisi wa TANU
Na Njumai Ngota
WANAWAKE wametakiwa kuwaenzi na kuwakumbuka wanawake wa TANU kwa mchango wao mkubwa katika harakati za ukombozi.
Mwenyekiti wa Habari Corporation Limited, Jenerali Ulimwengu aliyasema hayo juzi katika uzinduzi wa kitabu cha 'Wanawake wa TANU' uliofanyika kwenye viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Mabibo, Dar es Salaam.
Ulimwengu alisema wanawake wanatakiwa kuwaenzi kwa kuwaandikia makala na kutumia vyombo vya habari ili wengine waweze kuwafahamu na kutambua mchango wao.
Alisema Titi Mohamed alijitolea kupigania uhuru wa Tanganyika kwa kuacha mambo yake muhimu ya kulea watoto hali iliyosababisha kupewa talaka kwa kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.
"Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na kina mama ambao wanapenda maendeleo ya nchi zao kwa kupigania uhuru, ndio maana nasema lazima kina mama ambao hawajaandikwa katika kitabu hiki waweze kuandikiwa makala na kuwatangaza katika vyombo vya habari kuonyesha mchango wao enzi TANU," alisema.
Ulimwengu alisema hatuna budi kumkumbuka Susan Geiger kwa mchango wake na maamuzi ya kuwaandikia kitabu kina mama baada ya kuona michango yao katika kipindi cha TANU.
Naye Farida Kawawa, mtoto wa Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na mwasisi wa TANU, Mzee Rashidi Kawawa, alisema alizaliwa baada ya Uhuru lakini aliona mchango mkubwa wa kina mama katika harakati za ukombozi.
Alisema TANU ilileta mabadiliko makubwa kwa sababu kina mama wengi walijiunga na chama hicho ingawa baadhi yao walikatazwa na waume zao.
Pamoja na hali hiyo, alisema wanawake ndio waliofanikisha TANU kuongoza nchi kutokana na harakati za kina mama akiwemo Bibi Titi.
"Mama yangu alikuwa wa kwanza kujiunga na TANU kutokana na hamasa ya Titi Mohammed. Wanawake tunatakiwa kujitokeza kwa wingi katika nafasi za kugombea najua tunaweza," alisema Farida.
Katika uzinduzi wa kitabu hicho, alikuwepo mtoto wa Bibi Titi Mohammed, Halima Mzee ambaye ni mtoto pekee wa mwanaharakati huyo wa kihistoria.
Halima alisema anakumbuka wakati Mwalimu Julius Nyerere na mama yake walipokuwa wakisafiri kwenda kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi katika mapambano ya kupigania Uhuru.
Alisema wanawake ni wapiga kura wazuri ndio maana waliweza kuikomboa nchi kutoka kwa wakoloni na kuweza kuongoza TANU.
Halima aliwasihi wanawake kina mama wajiunge na siasa na kushiriki katika uchaguzi kwani alisema ipo siku mwanamke anaweza kuteuliwa katika nafasi ya Waziri Mkuu.
Kitabu cha Wanawake wa TANU kiliandikwa na Susan Geiger ambaye alikuwa ni Muingereza, alizaliwa mwaka 1926 huko Uingereza na alifariki mwaka 2001.
Kitabu hicho kilizinduliwa na Natalie Chiume ambaye alikuwa rafiki yake Susan.
Msichague vyama vinavyohubiri sera zinazogawa watu - Sheni
Na Peter Orwa, Shinyanga
MGOMBEA mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohammed Sheni, amewaambia wananchi mkoani hapa kutovichagua vyama vyenye sera za kugawa nchi kwa kutaka kila jimbo limiliki rasilimali zake.
Akihutubia juzi katika mikutano ya kampeni mkoani hapa, Dk. Sheni alisema kuna vyama vinavyojinadi kwa sera hizo na kuwataka wananchi wasivichague, kwani rasilimali za nchi ni kwa ajili ya Watanzania wote.
"Utawala bora gani huu wa kila mtu kuwa na chake. Watanzania wote ni wamoja, tofauti ninazozijua mimi ni za kabila, dini mwanamme na mwanamke... huwezi kugawa huyu ana chake, yule ana chake, siasa hii ya chake chake inatokea wapi?” alihoji Dk. Sheni na kuongeza: "Anayekuja na sera hiyo mtazameni na mwacheni peke yake".
Katika mkutano uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Bugoye mjini hapa, Dk. Sheni alihoji tabia ya vyama ya upinzani kujinadi kwa njia ya kukashifu mazuri yaliyotendwa na CCM kwa lugha ya 'haijafanya lolote' jambo linaloonyesha kutokomaa kwao na kukosa uungwana.
"Sasa hivi si dunia ya kulalamika na kusema uongo. Nawaomba wale walioko katika upinzani, katika siku hizi 10 zilizobaki mtafakari na kufikiri vizuri ili tarehe 30 muipigie kura CCM," alisema na kusisitiza sera zinazotekelezeka zinapatikana CCM.
Aliwaahidi wananchi wa mjini hapa kuwa CCM kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya kipindi cha miaka mitano ijayo, watapatiwa maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria, na kuondokana na adha hiyo sambamba na ujenzi wa barabara za halmashauri ya Manispaa hii na barabara kuu iendayo Mwanza.
Katika mkutano huo uliofurika watu na kutumbuziwa na kikundi cha taarabu cha Zanzibar Stars, Dk. Sheni alimnadi mgombea ubunge Dk. Charles Mlingwa na madiwani 13 wa manispaa hii.
Wakati huo huo, huko wilayani Kishapu, Dk. Sheni katika mkutano wake mwingine aliyoufanya kata ya Iganzo, alimtangaza mgombea ubunge Dk. Alfred Mpendazoye, kama mtu mahiri na anamfahamu fika kutokana na elimu na uwezo wake katika kazi, kwani ni mtaalamu wa mazingira chini ya ofisi yake.
Dk. Sheni alisema mgombea huyo ni 'lulu' kutokana na uwezo wake kimataifa, kwani alishatumikia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Sambamba na hilo, aliwaahidi wananchi wa jimbo hilo ambalo ndiko uliko mgodi wa almasi wa Mwadui, kuwa serikali ya awamu ya nne ya CCM, itafanyia kazi suala la wachimbaji hasa wadogo kuinua uwezo na kupitia upya sera ya madini nchini.
Akianisha yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Dk. Sheni alisema serikali itatoa kipaumbele kwa kuongeza thamani ya madini mara 10 zaidi ya ilivyo sasa ya asilimia 0.3.
Mgombea huyo alisema wachimbaji wadogo pia watapatiwa fursa ya mikopo na kuboresha utendaji wao, huku serikali ikizingatia migongano iliyokuwa ikijitokeza kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa.
“Pamoja na kuendelea kuhamasisha wawekezaji wakubwa, wachimbaji wadogo nao watapewa kipaumbele cha elimu ili wawe na tija katia utendaji wao,” alisema
Katika mkutano huo, wanachama wapya 100 walijiunga na CCM na kukabidhiwa kadi na mgombea mwenza huyo.
Mgombea ubunge Ulanga Mashariki aonya wananchi
Awataka kuwa macho na wapinzani
Na Prosper Kulita, Ulanga
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Ulanga Mashariki kupitia CCM, Selina Kombani, amewataka wana CCM kuwa waangalifu wakati wa upigaji kura, baada ya kubaini njama za wapinzani ambao wamepanga kuvuruga uchaguzi huo.
Selina alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika kata ya Chamange, Mahenge wilayani Ulanga.
Alisema CCM imebaini kuwa vyama vya upinzani vimepanga kuwatisha wananchi wakati wa upigaji kura Oktoba 30, mwaka huu, na kusema wana CCM wanatakiwa kuwa kitu kimoja ili kulinda ushindi wa chama chao ambao unaonekana.
Alisema kwa mantiki hiyo wanaamini vyama hivyo tayari vimeshashindwa uchaguzi, na ndiyo maana vimepanga kuwasumbua wananchi wataojitokeza kupiga kura siku hiyo.
Selina aliongeza kuwa mabalozi wa CCM wahakikishe kuwa siku ya kupiga kura wawe na watu wao bega kwa bega ili wasije wakapata matatizo, na pia wahakikishe watu wao wanapiga kura.
Akizungumzia maendeleo ya jimbo la Ulanga Mashariki, Selina alisema katika kipindi cha uongozi wake endapo atashinda, amelenga kuinua kiwango cha elimu jimboni humo na kwa kuanzia atarekebisha kasoro zilizopo katika shule za jimbo hilo.
“Kwa kuanzia natarajia kuanza katika elimu ambapo kwa sasa elimu Ulanga imeshuka, kwani unaweza kwenda katika shule unakuta walimu hakuna, wanafunzi nao watoro. Hakuna maendeleo katika jimbo bila ya kuwa na watu wenye upeo,” alisema.
Alisema katika mkakati wake wa kuinua elimu jimboni mwake, anatarajia kuanzisha mjadala wa pamoja na wazazi ili kupata mawazo yao juu ya kuwashawishi wanafunzi watoro warejee madarasani.
Alisema pia atahakikisha sheria ndogo ndogo zitazowabana wazazi wanaowazuia watoto kwenda shuleni kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kuolewa ama kulima mashamba, zinatungwa kupambana na hali hiyo.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Catherine Ndahani, aliwataka wananchi kuacha kubabaika na vyama vya upinzani ambavyo mpaka sasa havijapata mafanikio yoyote kama ilivyo kwa CCM.
Mzindakaya asambaratisha upinzani jimboni mwake
Na Oscar Simon, Sumbawanga
Mkongwe wa siasa mkoani Rukwa anayegombea Ubunge katika jimbo la Kwela kwa tiketi ya CCM, Dk. Chrisant Mzindakaya, amezisambaratisha kambi za wagombea wa vyama vya upinzani jimboni humo.
Kambi ambazo zimesambaratishwa ni za vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA katika kata za Laela, Muze na Kaengesa ambako wanachama 525 kutoka vyama hivyo walivihama na kujiunga na CCM.
Dk. Mzindakaya aliwapokea wanachama hao wapya waliyovikimbia vyama vya upinzani katika kampeni zake kwenye kata hizo, ambako mamia ya wakazi wake walijotokeza kumsikiliza katika mikutano yake.
kihutubia mikutano ya kampeni katika kata hizo, Mzindakaya alisema Chama cha Mapinduzi jimboni humo kitashinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu, kwa asilimia 85.
Alisema ana uhakika wa ushindi huo kwa sababu vyama vya upinzani vimechoka na havina wagombea wenye mvuto kwa wananchi, licha ya kwamba vyama vyao havijawafanyia lolote wananchi tokea kuanzishwa kwao.
Mbali ya CCM wagombea wengine wa ubunge katika jimbo la Kwela na vyama vyao kwenye mabano ni Didas Mfupe (NCCR-Mageuzi), Robin Simtengu (CUF) na Emil Nkulu (CHADEMA).
Alisema wagombea hao wa upinzani wamekuwa wakitoa lugha za matusi na kejeli zisizo za msingi dhidi ya Chama tawala badala ya kunadi sera za vyama vyao, hali ambayo imewakasirisha wapiga kura.
Aliwaahidi wananchi wa Jimbo hilo kuwa endapo atapita katika uchaguzi wa Oktoba 30, mwaka huu, atasimamia kikamilifu mpango wa wakulima na wafugaji jimboni mwake kwa kuhakikisha wanafaidika na mikopo ya zana na vifaa vikiwemo pembejeo za kilimo, maksai, mikokoteni na mbolea.
Mgombea huyo wa CCM aliwaambia wananchi kuwa tayari majimbo ya Kwela na Kalambo, yameshatengewa fedha zaidi ya sh. bilioni tatu na serikali kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na wafugaji kupitia benki ya NMB, ambayo itatoa maelekezo ya mikopo hiyo katika mwaka huu wa fedha wa 2005/2006.
Alisema mikopo hiyo itatolewa kwa mtu binafsi au vikundi vya watu watakaokuwa wamejiunga pamoja. Alisema wakopaji watadhaminiwa na serikali ya kijiji na hawatahitajika kuweka dhamana binafsi.
Wagombea Kigoma Mjini kuwekewa mdahalo
Na Fadhili Abdallah, Kigoma
CHAMA cha waandishi wa habari mkoani Kigoma (KGPC), kinatarajia kuendesha mdahalo wa wagombea ubunge
katika jimbo la Kigoma Mjini keshokutwa.
Mwenyekiti wa KGPC, Richard Katunka, alisema katika mdahalo huo utakaofanyika Jumapili, kuanzia saa tatu asubuhi katika Ukumbi wa Chama cha Msalaba Mwekundu mjini hapa, utawashasirikisha wagombea 12 wanaowania jimbo hilo.
Aliwataja wagombea hao kuwa ni Dk. Walid Aman Kabourou wa CHADEMA, Peter Serukamba wa CCM, Omari Rubibi wa CUF, Alhaji Hussein Beji wa NCCR-Mageuzi, Mvano Juma wa Sauti ya Umma na Shukuru Kondo wa DP.
Wengine ni Zakaria Kapapa wa FORD, Fube Athuman wa PPT Maendeleo, Omari Tito wa Jahazi Asilia, Tunu Jaffary wa TADEA, Juma Milembe wa UMD na Digio Hamis wa UPDP.
Katunka alisema lengo la mdahalo huo ni kuwawezesha wananchi kupata fursa ya kusikia mambo mbalimbali watakayoulizwa wagombea hao ambayo kwa kiasi kikubwa hayapati nafasi ya kuelezwa katika mikutano ya kampeni.
Aliongeza kuwa pia mdahalo huo utatumiwa kueleza kwa kirefu mambo ambayo wagombea hao watawafanyia wananchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwa mmoja wao atachaguliwa.
Wagombea hao wataulizwa juu ya mikakati yao ya kupambana na rushwa, kuboresha afya, mapambano dhidi ya maambukizi ya ukimwi na magonjwa ya mlipuko, njia za kupambana na njaa na umasikini, na nafasi ya mashirika na taasisi zisizo za kiserikali katika kuboresha maisha ya wananchi jimbo humo.
Mgombea kuimarisha sekta ya uwekezaji
Na Rashid Mussa, Mtwara
MGOMBEA ubunge jimbo la Mtwara Mjini kwa tiketi ya CCM, Mohammed Sinani, amesema akichaguliwa atahakikisha sekta ya uwekezaji ambayo imekuwa ikisuasua mkoani Mtwara inaimarishwa.
Mgombea huyo ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa ndani na nje, alitoa ahadi hiyo ya kukuza sekta hiyo katika mikutano yake ya kampeni katika maeneo ya Sokoni na Vigaeni.
Katika mikutano hiyo alisema amebuni mikakati mingi ya utekelezaji wa mpango mkubwa wa kisasa wa maendeleo ya jimbo hilo, ukiwemo wa kukuza sekta ya uwekezaji.
Mgombea huyo anayetajwa sana na kuaminika nchini Msumbiji kwa kufanikisha mpango kabambe wa kuinua sekta ya uwekezaji nchini humo alikokwenda kufanya biasahra, alisema atatumia uzoefu huo kukuza maendeleo nyumbani kwao Mtwara.
Alisema wananchi wakimpa ridhaa ya kuwa mbunge wao atatumia mbinu zote kutangaza nje na ndani ya nchi maeneo ambayo ni bikira katika ustawi wa biashara vivutio vingi vya utalii na uendelezaji wa nishati ikiwa pamoja na kuwatafuta kuwashawishi wawekezaji makini kuja kuwekeza kwa kushirikisha wazalendo.
Sinani alisema kazi hyo anaiweza ana ujuzi na uzoefu mkubwa, anachohitaji ni wananchi kumpa ridhaa ya kufanya hivyo ili kuyapeleka maendeleo ya mji huu na mkoa kwa kasi ya urukaji wa ndege angani.
Akishangiliwa kwa nguvu na umati mkubwa uliokuwa umefurika katika mikutano hiyo, alisisitiza kuwa hili linawezekana kwa kuzingatia sera na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na hasa kwa kufuatia kazi kubwa ilyofanywa na uongozi wa serikali wa mkoa wa kufungua milango ya uwekezaji mkoani hapa.
Ilisema Mtwara ni tajiri sana kwa rasilimali na vivutio vikubwa vya utalii ambavyo havijatumiwa kikamilifu kutokana na kutokuwepo wawekezaji na sababu mbali mbali za msingi ambazo sasa hazipo tena.