UHURU 22.10.2005

 

 

 

Rais Mkapa ataka BoT ichochee maendeleo

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kusimamia kikamilifu juhudi za kuhuisha mitaji mfu ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa wanyonge.

Aliyasema hayo jana katika hutuba yake ya uzinduzi wa majengo mawili ya kisasa ya Benki Kuu katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa taasisi na mabalozi wa nchi mbalimbali wanaofanya shughuli zao hapa nchini.

“Naamini wananchi wengi wameshuhudia na kuguswa na matokeo ya mageuzi ya kiuchumi na huduma za kijamii katika ngazi ya familia… benki zetu lazima zihakikishe zinahuisha mitaji mfu na kwamba Benki Kuu inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inaendeleza mali za wanyonge,” alisema Mkapa.

Aidha, Rais ameipongeza Benki Kuu kwa kusimamia kikamilifu mageuzi ya kiuchumi nchini ambayo kwa kiwango kikubwa yamechangia katika juhudi za kupambana na umasikini katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Alisema mageuzi hayo mbali ya kuimarisha uchumi, pia yameongeza pato la taifa kutoka asilimia 6.7 katika miaka ya 1990 hadi asilimia saba hadi kufikia mwaka huu.

Rais Mkapa alisema mafanikio hayo pia yalijitokeza katika ukusanyaji wa mapato ya taifa ambapo hadi kufikia mwaka huu serikali imeweza kukusanya wastani wa sh. bilioni 150 kwa mwezi, kiwango ambacho kimekuwa kikichangia katika bajeti ya nchi.

Alisema mafanikio hayo yamesaidia katika kuongeza kiwango cha misaada ya wafadhili kutoka nje na kupunguziwa madeni, na hivyo kusaidia katika kuimarisha huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na umasikini.

Pia mafanikio hayo yameiwezesha serikali kuongeza akiba yake ya fedha za kigeni kutoka dola za Marekani 270 mwaka 1995 hadi dola bilioni mbili.

Mapema katika hotuba yake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Daudi Ballali, alisema kutoka na sera nzuri za kiuchumi, Tanzania imekuwa kivutio kwa wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Alisema hilo linaashiria mwelekeo mzuri wa uwekezaji nchini na hatimaye kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.

Pia, alisema katika kipindi cha miaka kumi, mfumuko wa bei umedhibitiwa kwa kiwango kikubwa kutoka asilimia 28 hadi asilimia nne.

Kuhusu ujenzi wa majengo hayo, alisema mbali ya kuongeza ufanisi, pia utapunguza adha ya wafanyakazi wa benki hiyo kufanya kazi katika majengo tofauti na yaliyo sehemu mbalimbali jijini.

 

 

Nyota ya Kikwete yang’ara zaidi Dar

Na Khamis Hamad

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, amezidi kuwa kivutio kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam, kutokana na azma yake ya kuendeleza mafanikio ya serikali ya awamu ya tatu.

Hali ya Kikwete kuwavutia wananchi iliendelea kudhihirika jana baada ya mamia ya wananchi kujitokeza kumpokea uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, wakati akitokea mkoani Pwani, na kutembea kutoka uwanjani hapo hadi Ofisi ya CCM mkoa wa Dar es Salaam, safari ambayo ilichukua saa moja.

Sambamba na wasindikizaji hao, pia wananchi kadhaa walijipanga barabarani bila kutarajiwa, hali ambayo ilimvuta Kikwete na kulazimika kusimama kwenye gari la wazi kwa lengo la kuwasalimia.

Akizungumza baada ya kuwasili Ofisi ya CCM mkoa kwa ajili ya kuanza ziara yake ya kampeni mkoani Dar es Salaam, Kikwete alisema 'nimevutiwa na mapokezi yenu na nimepokea ujumbe wenu' akimaanisha uamuzi wao wa kumsindikiza masafa marefu wakiwa wanatembea.

Mvuto huo ulizidi wakati mgombea Kikwete alipoondoka ofisi ya mkoa kwenda wilayani Kinondoni kuendelea na mikutano yake ya kampeni, ambapo alipofika eneo la Jangwani, wananchi wa wilaya ya Kinondoni waliunga msafara huo na kutembea hadi Manzese ambako kutokana na umati mkubwa wa watu aliyokutana nao, alisimama na kuusalimia kwa dakika chache.

Idadi ya watu ilizidi kuongezeka kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika Boko, nje kidogo ya jiji la Dar es Saalam, na kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni.

Hali ya kuvutiwa na mgombea urais Kikwete, pia iliwakumba wanachama wa vyama vingine wakiwemo wagombea ubunge katika majimbo mbali mbali.

Wagombea ubunge waliojitokeza na kumthibitishia Kikwete kuwa wamevihama vyama vyao na kujiunga na CCM, majimbo waliyokuwa wakigombea yakiwa kwenye mabano ni Livingstone Alusinde (Mtera), Lucky Mdemu (Mufindi Kaskazini) wote kutoka Chadema, na Lipiyana Mlewa wa UDP, aliyekuwa akigombea jimbo la Ukonga.

Pamoja na wabunge hao, Kikwete pia alivuna wanachama 1,014 kutoka upinzani na wengine wapya 1,798.

Wakati huo huo, Kikwete ameihakikishia familia ya marehemu Mwajuma Nyanza kuwa nyumba yao iliyochomwa moto na kusababaisha kifo cha kada huyo wa CCM na wajukuu zake, itajengwa kwa gharama za chama.

Alitoa ufafanuzi huo jana baada ya kutoa pole kwa familia hiyo, Manzese Midizini jijini, ambapo alisema ilichomwa kutokana na misingi ya kisiasa.

Hata hivyo, alieleza kuwa waliochoma nyumba hiyo kwa matarajio ya kudhoofisha nguvu ya CCM wamekosea, kwani silaha iliyoachwa na kada huyo inaendelea kutumiwa na makada wengine kufanikisha malengo ya CCM, ambayo ni pamoja na kutetea umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Boko na kwenye viwanja vya Biafra, Kikwete aliwataka wananchi kuichagua CCM, kwani ndiyo chama pekee kinachopaswa kupewa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia.

Alisema katika historia yake, CCM imekuwa ikihubiri amani, upendo na ushirikiano, hali ambayo imesababisha kuwepo kwa Tanzania.

"Bila umoja hakuna Tanzania, kwani hakuna shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanywa na kuleta tija katika nchi iliyogubikwa na migogoro," alisema na kuongeza kuwa kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana Baba wa Taifa, Hayati Mwalim Nyerere alitumia muda wake mwingi kujenga utaifa.

Kikwete alisema wapinzani hawapaswi kupewa ridhaa ya kuongoza nchi kwa vile ni vikundi vilivyoundwa kwa lengo la kutetea maslahi ya makundi fulani, yakiwemo ya kidini, na kutokana na kushindwa kutimiza malengo yao hayo vimebakia kuwa vikundi vya walalamikaji na siyo vyama vya siasa.

Kikwete alianza ziara mkoani Dar es Salaam, jana, baada ya kutumia miezi miwili kuzunguka sehemu nyingine baada ya kampeni hizo kuzinduliwa rasmi Agosti 21, mwaka huu, kwenye viwanja Jangwani, mjini Dar es Salaam.

 

Wafuasi wa CHADEMA wilaya Karatu washambulia wana-CCM

Na Omari Shaaban, Karatu

VURUGU za kisiasa zimezuka wilayani Karatu, baada ya kundi la wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwashambulia kwa mawe na marungu wafuasi wa Chama cha Mapinduzi.

Wanachama watatu wa CCM wamejeruhiwa vibaya na wamelazwa katika hospitali ya Kanisa Katoliki ya Kata ya Mang'ola, ambako tukio hilo lilitokea.

Majeruhi hao wamejeruhiwa vichwani, miguuni na mwanamke mmoja amevunjika uti wa mgongo.

Mmoja wa majeruhi hao, Steven Lusiana (22), akizungumza kwa shida hospitalini hapo, alisema vurugu hizo zilitokea juzi saa mbili usiku.

Alidai vurugu hizo zilitokea eneo la Mang'ola Barazani, baada ya wafuasi wa Chadema wakiwa na diwani wao, Jacob Pius, kushambulia kundi la CCM, ambalo nalo lilikuwa likitokea kwenye kampeni za udiwani wakiwa na diwani wao Emmanuel 'Meta' Gidahudu.

Alidai kuwa kundi la Chadema likitokea kwenye kampeni katika kijiji cha Laghangareli, lilianza vurugu hizo baada ya kukaa barabarani lilipofika eneo hilo, na kukataa kuwapisha wafuasi wa CCM ambao walikuwa wakirudi majumbani mwao.

Lusiana alidai ghafla walimwagiwa mchanga na kuanza kupigwa mawe, fimbo na marungu na kuumizwa vibaya.

Alidai baada ya dakika 10 za vurugu hizo, wafuasi wa Chadema walitoweka huku yeye akiwa hawezi kutembea kutokana na kuvunjwa mguu wa kulia, na hivyo kupelekwa hospitali akiwa na majeruhi wengine.

Tukio hilo limeripotiwa kituo cha polisi.

Majeruhi mwengine mwanamke, Martha Masudi (18), alidai alipigwa mawe na fimbo hadi kupoteza fahamu na kujikuta amelezwa hospitalini hapo, huku akiwa hawezi kunyanyuka kutokana na kuumizwa vibaya mgongoni.

Alidai wakiwa wanatokea kwenye kampeni za diwani wao wa CCM kijiji cha Mibuyu Miwili, walipokuwa wakirudi majumbani walikutana na kundi la wapenzi wa Chadema katika eneo hilo na kushambuliwa kwa kupigwa vibaya.

Alidai waliwatambua kuwa watu hao ni wafuasi wa Chadema kwa kuwa walikuwa na bendera ya chama hicho ya rangi ya buluu ya bahari.

"Jamani sisi tulikuwa tunarudi nyumbani tumetoka kwenye kampeni za CCM. Tulipofika hapo (Mang'ola) tulikuta kundi la wafuasi wa Chadema wakiwa na bendera yao na kuanza kutupiga bila sababu... mimi sijui naomba serikali itusaidie," alidai Martha ambaye alisema alipoteza fahamu kwa kipigo.

Daudi Hirga (36), amepasuliwa kichwani na ameshonwa. Aliomba serikali, hasa vyombo vya dola kuongeza ulinzi katika eneo hilo katika kipindi hiki cha kampeni.

Wauguzi wa hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki (hawakutaka majina yoa yatajwe), walisema walipokea majeruhi zaidi ya 20, na wengine walitibiwa na kuruhusiwa kwa kuwa walikuwa na majereha madogo ya kawaida.

Wanachama wengi na wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na vurugu hizo, walidai kuwa hizo ni njama za Chadema za kutaka kuvuruga uchaguzi katika jimbo la Karatu, baada ya kuona hali inawaendea vibaya kwenye kampeni kwa kukosa watu kwenye mikutano yao.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Novatus Makunga, alisema kitendo cha wapinzani kuwapiga wafuasi wa CCM, kinaonyesha kushindwa kisiasa kwa wapinzani.

Makunga alisema kitendo hicho kinatakiwa kulaaniwa kwa nguvu zote na wapenda amani wote wa Tanzania, na hiyo inaonyesha kuwa Chadema imefilisika kisera na kuanza sera hiyo mpya ya kupiga wananchi wasiokuwa na hatia.

Alisema suala hilo lilisharipotiwa kituo cha polisi wilayani Karatu, na watakaobainika kuhusika nalo ameomba wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa, James Kombe, alisema uchunguzi unafanyika kubaini chanzo cha vurugu hizo, na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati huo huo, Katibu Tarafa wa Eyasi, Langanyi Ole Sipuk, kutokana na vurugu hizo, amepiga marufuku mikutano ya kampeni kufanyika baada ya saa 12.30 jioni.

Alisema kundi lolote litakalokutwa limeweka vikao vyake vya siasa usiku na kuweka 'vigenge' ambavyo vinaashiria vurugu ama uchochezi, vitachukuliwa hatua kali za kisheria.

Sipuk alisema amesikitishwa na vurugu hizo, na jana aliwatembelea majeruhi kuwafariji na alikemea vitendo hivyo vilivyofanywa na Chadema na kuomba uchunguzi ufanywe haraka na watakaobainika washitakiwe.

 

Mkapa kuzindua Chuo Kikuu cha Wasilamu Morogoro

Na Furaha Omary

RAIS Benjamin Mkapa leo anatarajiwa kukizindua rasmi Chuo Kikuu Cha Waislamu cha Morogoro.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu, (MDF), Kitwana Kondo imeeleza kuwa kwa kuanzia chuo hicho kitaendesha mafunzo ya shahada za aina tatu.

Katika taarifa yake hiyo iliyosomwa kwa niaba yake kwa waandishi wa habari na mmoja wa viongozi waandamizi wa MDF,Said El- Maamry, Kondo alisema shahada hizo ni katika fani za mawasiliano, elimu ya kiislamu na elimu ya jamii.

Alisema katika mkupuo huo wa kwanza jumla ya wanafunzi 165 wamesajili kuendelea na masomo ambayo yatakuwa ya miaka mitatu.

Kada watakazosomea wanafunzi hao na mgawanyo wake katika mabano ni mawasiliano ( 55), elimu ya jamii (90) wakati elimu ya kiislamu itajumuisha wanafunzi 20.

"Katika kuwahudumia wanafunzi hao, hatukuangalia suala la dini, wala makabila yao, tulichofanya ni kuangalia uwezo wao wa kielemu," alisema.

Kati ya wanafunzi hao, 59 ni wanawake. Pia chuo hicho kina jumla ya walimu wa kudumu watano na wengine tisa.

Azma ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu Cha Waislamu na Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu mapema mwaka huu ni kwa lengo la kutoa elimu itakayowezesha kupatikana kwa wataalamu wa fani mbali mbali.

 

Watoto Yatima wahudumiwa

Na Rodrick Makundi, Moshi

WATOTO yatima waishio maeneo ya vijijini mkoani Kilimanjaro, wameanza kupatiwa huduma mbalimbali za kijamii na asasi zinazojihusisha na elimu ili kujiendeleza zaidi kielimu.

Utoaji wa elimu kwa yatima mkoani hapa umefanywa na Chuo cha Mafunzo cha Intel ambacho kimejitolea kusomesha wanafunzi wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha inayofanya washindwe kujilipia ada ili kuendelea na masomo ya juu.

Mkuu wa Chuo hicho, Zephania Gabush alibainisha kuwa chuo chake hadi sasa kimefanikiwa kuwasomesha watoto yatima wapatao 20 ambao watasomea masomo ya fani mbalimbali katika chuo hicho.

Alisema mpango wa kuwasomesha wanafunzi hao ni moja ya sera za chuo hicho ambazo zimelenga juhudi za serikali za kutokomeza umaskini kwa kuwawezesha wananchi wake kupata elimu ya kutosha ili kujikimu katika masoko ya ajira.

Gabush alisema aliamua kutoa kipaumbele kwa yatima wa maeneo ya vijijini, kwani asasi nyingi zimekuwa zikijisahau kutoa michango yao kwa wale wa maeneo hayo jambo ambalo limezidi kuwarudisha nyuma kielimu yatima wa vijijini.

Hivyo aliwataka wananchi, asasi na serikali kuhakikisha kwamba watoto yatima, hasa wale wasio na uwezo wanafadhiliwa na kupatiwa elimu ili kuwa na usawa wakati wa kutafuta ajira hivyo kuondokana na adui ujinga kulingana na mpango wa serikali wa kutokomeza maadui ujinga, maradhi na umaskini.

Pia aliomba serikali kusaidia baadhi ya vyuo vinavyojihusisha katika kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali katika jamii na akazitaka asasi nyingine zisizo za kiserikali kuzingatia umuhimu wa utoaji wa misaada kwa yatima.

Yatima waliofadhiliwa na chuo hicho wanapatiwa masomo kwa kozi mbalimbali ikiwemo uhasibu, ualimu wa chekechea, ukarani, mafunzo ya kompyuta pamoja na elimu kwa ajili ya maandalizi ya kujiunga na elimu ya sekondari.

 

 

CUF sasa wameanza kuhisi joto la kushindwa - Karume

Na Mwandishi Maalum, Pemba

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume, amesema CUF wameshabaini hawana uwezo wa kuishinda CCM ndiyo maana wameanza kutangaza vurugu.

Mgombea huyo ambaye anatetea kiti hicho, alieleza hayo jana alipofanya mazungumzo na wananchi, wapenzi na wana-CCM katika matawi na maskani mbalimbali za CCM katika Mkoa wa Kusini, Pemba.

Aliwaeleza wananchi kuwa, CUF imebaini haina uwezo wa kushinda uchaguzi ujao, hivyo wamejitayarisha kuwatisha watu na kuwazuia wasipige kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

Mgombea huyo ambaye anashikilia pia nafasi ya Makamu Mwenyekiti CCM (Zanzibar) alitoa tahadhari kwa wanaokusudia kufanya vitendo vya uhalifu wakati wa uchaguzi, kuwa Tanzania ni nchi huru na kila mtu ana haki ya maamuzi anayoyataka.

Alisema kuanzisha vitisho au kitendo chochote cha kumzuia mtu kwenda kupiga kura ni kuharibu amani na utulivu wa nchi.

Karume aliongeza kuwa CUF wamejieleza hadharani na kuithibitishia dunia kuwa wao ni wagomvi: "Lakini sisi tunasema hakuna haja ya ugomvi kwani tumeshashinda na CUF haiwezi kushindana na CCM," alisema Rais Karume.

"Kauli za viongozi wa CUF za kuwataka wanachama wake kukaa umbali wa mita 200 kutoka vituo vya kupigia kura hata baada ya kupiga kura zao, zinalenga katika kuvuruga na kuharibu uchaguzi," alisema.

Alisema CCM haina matarajio mengine zaidi ya ushindi mkubwa wa kishindo.

"Nakuleteeni ujumbe wa ushindi kutoka kwa wanachama wenzenu kutoka mikoa mbalimbali ya Unguja...ushindi kwa CCM hauna mjadala. Ushindi unaozungumziwa hapa ni ule wa CCM, ushindi wa amani na utulivu, ushindi wa maendeleo kwa wananchi wote wa Zanzibar," alisema.

Alisema ushindi kwa CCM ni lazima kwani ndiyo iliyothibitisha kuwa na uwezo wa kuhakikisha amani na utulivu nchini.

Karume aliongeza kuwataka wana-CCM kutokubali kuchokozwa na kuchokozeka, hivyo siku ya kupiga kura wasikae mita 200 kutoka vituoni, bali warudi majumbani mwao kusubiri matokeo.

Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaweka ulinzi wa kutosha ili kumuwezesha kila mtu mwenye haki ya kupiga kura anafanya hivyo.

Katika ziara yake ya kampeni ya ndani katika Mkoa wa Kusini Pemba, alitembelea maskani za Matuleni, Wazee, Mkani, Karume, Mgagadu na matawi ya Chama ya Chanjaani, Shungi, Mtambile na Makombeni.

Leo mgombea huyo wa urais anatarajiwa kuhutubia mkutano wa hadhara huko Wawi, Chake Chake.

 

Mwinyi asema wapinzani hawana sifa ya kuongoza

Ni kutokana na ubinafsi

Na El-hadji Yuusuf, Nzega

RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi amesema vyama vya upinzani nchini bado vinaghubikwa na migogoro na ubinafsi hivyo havina sifa ya kuongoza nchi.

Mwinyi aliyasema hayo jana mjini hapa, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kata ya Puge, katika wilaya ya Nzega, akiwataka Watanzania waendelee kuichagua CCM kuongoza.

Alisema vyama hivyo licha ya kuwa na umri mdogo, vimeonyesha kuyumba na kutokuwa imara kuweza kuongoza nchi yenye rasilimali nyingi kama Tanzania, bila ya kuzuka kwa migogoro.

Aliwataka Watanzania kuachana na vyama hivyo katika Uchaguzi Mkuu, kwani kuvichagua ni sawa na kuweka rehani amani na utulivu nchini.

Alivifananisha vyama hivyo kupewa uongozi wa Taifa ni sawa na kumpa mtoto wembe, ambao unajua kuwa hajui matumizi yake, bali wembe huo utatumika kumkata mwenyewe.

Alisisitiza kuwa nchi ni lazima iongozwe na chama chenye uzoefu wa kushika madaraka na kupigania maslahi ya umma kama ilivyo kwa CCM.

Alhaji Mwinyi alisema itakuwa ajabu iwapo Watanzania wataamua kumpa uongozi 'mwanafunzi', ambaye wanajua atawaingiza shimoni na kumuacha mwalimu ambaye wana hakika naye kuwa atawafikisha katika neema, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Alisema CCM ni chama kinachoonyesha wazi kuwa kipo kwa ajili ya kupigania maslahi ya umma na itaendelea kufanya hivyo na kamwe chama hakiwezi kutumiwa vibaya kwa namna yoyote.

Akimzungumzia mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM, Jakaya Kikwete, alimueleza kuwa ni kijana mchapakazi, mwenye upeo wa kuona mbali na ana sifa ya kuwa rais wa Tanzania katika awamu ya nne.Alisema katika watu waliojitokeza kuwania urais kupitia vyama mbali mbali, hakuna hata mmoja anayeweza kumfikia Kikwete kwa sifa za utendaji, hivyo aliwataka wampe kura.

Aliwataka Watanzania wawape kura wagombea wa ubunge na udiwani kutoka CCM ili kumuwezesha rais huyo wa awamu ya nne, aweze kutekeleza vizuri sera za CCM katika kupambana na umasikini, na waache kuwachagua wapinzani ambao alisema ni kikwazo cha maendeleo.

Katika mkutano huo, Rais mstaafu Mwinyi aliwapokea wanachama 45 wa vyama vya upinzani, waliorejea CCM baada ya kutoridhishwa na vyama hivyo, ambavyo walisema 'vimejaa ubabaishaji'. Wanachama hao wametoka vyama vya CUF, Chadema, UDP, TLP na NCCR-Mageuzi.

 

CHADEMA Muleba wafunga tawi na kuhamia CCM

Na Mwandishi Wetu, Muleba

WANACHAMA 53 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika tawi la Ngenge, Muleba mkoani Kagera, wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi na hatimaye kufunga tawi la chama hicho.

Tukio hilo lilitokea wakati wa mkutano wa kampeni ya ubunge katika kijiji cha Ngenge, kilichoko jimbo la Muleba Kaskazini, uliohutubiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk. Diodorus Kamala.

Katika tukio hilo, wanachama hao pia walikabidhi bendera, kadi, vitabu na vifaa vya ofisi walivyokuwa wakivitumia kwa ajili ya shughuli za CHADEMA.

Wanachama hao walipewa kadi mpya walizokabidhiwa na Dk. Kamala, ambaye amepita bila kupingwa katika kiti cha ubunge jimbo la Nkenge mkoani Kagera.

Akihutubia mkutano huo, Dk. Kamala ambaye ni Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, aliwataka wananchi kuchagua wagombea wa CCM ili waweze kuendeleza mema waliyoyafanya katika miaka mitano iliyopita.

Katika mkutano huo, aliokuwa akimnadi mgombea ubunge wa CCM, Ruth Msafiri, Dk. Kamala alisema kipindi kilichopita Chama kimefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kupambana na umaskini.

Alisema katika miaka mitano ijayo, nguvu zaidi itaelekezwa katika mkakati huo ambapo serikali imeshapata fedha zitakazopelekwa moja kwa moja vijijini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

"Kutokana na mambo ambayo CCM imeyafanya katika miaka mitano iliyopita, imeonyesha kuwa ndicho chama bora na chenye sera maridhawa, hivyo nawaomba wananchi kuendelea kuipa ridhaa ya kuongoza nchi ili iweze kufanya mengi kwa maendeleo ya nchi," alisema.

Dk. Kamala alisema wananchi hawana budi kuendelea kuichagua CCM kwa kuwa ndiyo iliyopanga mipango ya maendeleo na kuvichagua vyama vya upinzani ni kurudisha nyuma maendeleo na mafanikio hayo.

Alisema katika miaka mitano ijayo, CCM itaendelea kuwavutia wawekezaji ili kuleta mitaji mingi zaidi ambayo itasaidia kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi.

Katika miaka mitano iliyopita, alisema, mitaji imeongezeka kutoka sh. bilioni 30 mwaka 2000 hadi sh. bilioni 450 mwaka huu.

Kutokana na ongezeko hilo, alisema serikali ijayo ya CCM imepania kuendeleza kasi ya uwekezaji ambayo itawezesha kupatikana kwa ajira na kupunguza umasikini unaowakabili wananchi.

 

Minoca Mbega kutimiza ahadi zote

Na Bahati Alex, Iringa

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi katika jimbo la Iringa mjini, Monica Mbega, amesema endapo atachaguliwa tena kuongoza jimbo hilo, atahakikisha anatekeleza ahadi zote za chama, ikiwa ni pamoja na kuwainua wakulima.

Akizungumza katika mikutano ya kampeni jimboni humo, mgombea huyo alisema katika kutekeleza ahadi hizo, atashirikiana na wananchi ikiwa ni pamoja na kupanga mipango endelevu, itakayoweza kuwakwamua kiuchumi wakulima wa jimbo hilo.

Monica amewataka wakazi wa jimbo hilo kutofanya kosa la kuwachagua wapinzani, ila wakipigie kura CCM kiweze kuendeleza shughuli za maendeleo ya nchi na wananchi ambazo tayari ilishaanza kuzifanya.

Mgombea huyo alisema kuwachagua wapinzani ni sawa na kuyarudisha nyuma maendeleo yaliyokwishapatikana.

Alisema CCM imefanikiwa kutekeleza Ilani yake katika sekta za kilimo, afya, elimu, na miundombinu.

 

CRDB yatumia sh. milioni 30 kupima wafanyakazi ukimwi

Na Lauden Mwambona, Arusha

BENKI ya CRDB imetumia zaidi ya sh. milioni 30 kuwapima ukimwi wafanyakazi wake ili iweze kuwasaidia waliopatikana na virusi.

Meneja wa Uhusiano na Mratibu wa Ukimwi katika Benki hiyo, Nicholas Kingazi alisema hayo jana alipotoa mada juu ya umuhimu wa kuanzisha mpango wa kuwatunza wafanyakazi maeneo ya kazi kwenye mkutano wa 15 wa mfuko wa Pensheni (PPF) uliofanyika mjini Arusha.

Shughuli za mkutano huo wa PPF zinatarajiwa kukamilika leo, lakini jana wajumbe karibu 200 walitumia siku nzima kujadili jinsi ukimwi unavyoathiri uchumi, maendeleo na kuua watu wengi.

Kingazi alisema CRDB Bank Ltd ilianzisha mpango wa kuwajali wafanyakazi wake kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la utafiti wa masuala ya afya (AMREEF) na kwamba iliweza kuwapima wafanyakazi wake 820.

Alisema hatua hiyo ililenga kuwasaidia kwa dhati wafanyakazi walio na virusi jambo ambalo kwa sasa linatekelezwa kwa siri kubwa.

Lakini pia benki hiyo imepanga kuwapima tena wafanyakazi wake mwaka ujao.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba matokeo ya upimaji ni siri ya mfanyakazi na kwamba mpaka sasa ni mfanyakazi mmoja tu ambaye alijitangaza kuwa anavyo virusi.

Kila mfanyakazi mwenye virusi vya ukimwi anayo namba yake aliyopewa na AMREEF ili aweze kupata huduma za dawa za kurefusha maisha kwa gharama ya benki,ƒ__ alisema.

Kingazi alisema CRDB Bank ltd inawajali wafanyakazi wake na kamwe haiwezi kuwafukuza waliona virusi vya ukimwi, bali itawalea hadi Mungu atakapopenda mwenyewe.

Takwimu za hali ya ukimwi duniani zinaonyesha kwamba watu milioni 39.4 wanaishi na virusi vya ukimwi wakiwemo watu 25.4 walioko nchi za kusini mwa jangwa la sahara.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini, (TACAIDS), Meja Jenerali (mstaafu) Herman Lupogo alifafanua jana kwamba kila idara au taasisi inayotaka kupata fedha za kusaidia mapambano ya ukimwi, lazima aishauri wizara mama iandae mpango maalum wa kazi hiyo kiwizara, idara na taasisi zake ili mpango huo usaidie kupata fedha kutoka kwa wahisani.

Lupogo alisema kwa kipindi kirefu wapo watu wanaofikiri fedha ziko kwenye ofisi yake jambo ambalo siyo kweli.

Alisema Benki ya Dunia iliahidi kutoa dola za Marekani milioni 65 sawa na zaidi ya sh. bilioni 65 kusaidia mpango huo, lakini fedha hizo zinatolewa baada ya kuonekana mpango na kwamba mpaka sasa ni dola 1.5 (sawa na zaidi ya sh. bilioni 5).

TACAIDS haina fedha, mpaka sasa haijapokea hata robo ya fedha za Benki ya Dunia kwa sababu Wizara ndizo zinazotakiwa kuwasilisha mipango ya utekelezaji, alisema na kuongeza kwamba akiwa mjini Arusha tayari alifuatwa na viongozi wa dini, taasisi binafsi wakitaka fedha za kupambana na ukimwi.

Alisema serikali ilishazitaka kila Halmashauri ziwe na kamati maalum ya ukimwi , lakini zipo habari kwamba baadhi ya kamati za halmashauri hazijawahi kukaa ili kujadili mbinu za kupambana na ukimwi.

Naye Katibu Mkuu wa mtandao wa wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini (NETWO+), Theresia Kawamala aliipongeza PPF kwa kutenga siku maalum ya mkutano wake kujadili ukimwi.

Theresia ambaye ameishi na virusi kwa zaidi ya miaka mitano alisema mashirika makubwa au waajiri hawana budi kutumia muda mwingi kutoa elimu ya ukimwi.

NETWO+ yenye makao yake jijini Dar es Salaam ina watoto yatima 437 ambao alisema wanahitaji msaada wa hali na mali kwa watu wenye uwezo ili wapate elimu.

 

 

Serikali kuweka mikakati ya kuimarisha usalama viwanjani

Na Solomon Mwansele, Mbeya

WAZIRI wa Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Mark Mwandosya amesema kuwa serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama wa viwanja vya ndege nchini unaimarika.

Profesa Mwandosya aliyasema hayo juzi kabla ya kumkaribisha Rais Benjamin Mkapa kuweka jiwe la msingi katika uwanja ndege wa kimataifa wa Songwe uliopo nje kidogo kutoka jijini hapa.

Alisema kuwa Wizara yake inatambua kuwa suala la usalama wa viwanja na abiria ni muhimu na la msingi hasa ikizingatiwa kuwepo kwa matukio mengi ya kigaidi yanayoiandama sekta ya usafiri wa anga hivi sasa.

"Dhamira ya serikali ni kuhakikisha kunakuwepo utoaji huduma huduma bora kwa ngazi ya kitaifa na kimataifa katika hali ya ufanisi na usalama wa hali ya juu na kwa gharama nafuu," alisema.

Waziri alisema kuwa kuwepo kwa huduma za usafiri wa anga kunamaanisha kuwepo kwanza kwa viwanja vya ndege.

Alisema kuwa Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini (TAA)

inasimamia na kuendesha viwanja 62 nchini, ikiwa nisehemu ya viwanja 319 vilivyoandikishwa wakati vilivyobaki vinaendeshwa na Wizara ya Maliasili na

Utalii, TANAPA na watu binafsi.

Ni matumaini ya Wizara kwamba uongozi wa mkoa wa Mbeya na mikoa ya nyanda za juu kusini,taasisi mbali mbali, sekta binafsi na wananchi wataanza kupanga jinsi gani ya kuutumia uwanja huu katika kujiletea maendeleo, alisema.

Aliongeza kuwa kiwanja cha ndege cha Songwe kijiografia kiko mahali pazuri kwani kimepakana na nchi za Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine za kusini mwa Afrika.

Alisema kuwa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005, inawaahidi wananchio kuhusu kukamilisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe na kuimarisha viwanja vya ndege vya Kigoma, Tabora na Shinyanga.