UHURU 23.09.2005

 

Watanzania waishio Afrika Kusini watoa rai kwa rais ajaye

Na Maura Mwingira, Pretoria, Afrika Kusini

WATANZANIA wanaoishi nchini Afrika Kuisni, wameelezea matumaini yao kuwa uongozi wa awamu ya nne, utaendeleza misingi imara na mizuri ya uchumi iliyowekwa na Rais Benjamin Mkapa ili kuongeza kasi ya maendeleo.

Wametoa kauli hiyo juzi wakati walipokuwa wakiagana na Rais Mkapa wakati wa hafla iliyofanyika katika hoteli ya Sheraton Pretoria.

Rais Mkapa akiwa amefuatana na Mama Anna Mkapa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Hemedi Mkali yuko nchini hapa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

“Tumekuja hapa kusema asante kwa kazi yako kubwa na nzuri ulioifanya katika uongozi wako wa serikali ya awamu ya tatu. Unaondoka ukiicha nchi katika hali nzuri kuliko ile ulioikuta wewe katika kila eneo.

“Rais tunafurahi kusema umeongoza nchi kwa umakini mkubwa, juhudi na maarifa… ulijituma, ulithubutu na ukawa muwazi na mkweli. Ni matumaini yetu kuwa uongozi wa awamu ya nne utaendeleza yale yote uliyoyaanzisha,” alisema Professa Katabaro aliyesoma risala kwa niaba ya Watanzania wenzake.

Wakiainisha mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wa Mkapa, Watanzania hao walisema kuwa, katika sekta ya uchumi, mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 30 hadi chini ya asilimia tano, pato la Taifa limekuwa kutoka asilimia 3.6 hadi asilimia 6.7

Watanzania hao ambao kabla ya kuanza mazungumzo na Rais waliimba wimbo wa ‘Tanzania, Tanzania nakupenda’, walisisitiza kuwa mafanikio yote hayo yametokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji na uejnzi wa miundombinu, hususan barabara na mawasiliano.

 

“Umewezesha nchi kuanzisha ujenzi mkubwa wa barabara kwa kutumia fedha zetu wenyewe bila kutegemea sana misaada ya wafadhili, jambo ambalo hakuna Watanzania waliowahi kuliota kabla hujachukua uongozi wa nchi, na hii imewezekana kutokana na kuongezeka kwa mapato ya ndani kutoka sh. bilioni 25 hadi bilioni 150, na pia juhudi zako za kupiga vita rushwa,” walisema.

Waliongeza kuwa wanaona fahari kubwa kuagana na kiongozi wao ambaye amewafanya wajisikie fahari sana na kutembea kifua mbele kwa kuwa uongozi wake wa mfano sio tu umeleta mabadiliko makubwa nchini Tanzania, lakini pia umemfanya atafutwe kutoa mchango wake katika taasisi mbalimbali za kimataifa.

Akizungumza na Watanzania hao pamoja na kujibu maswali, Rais aliwashukuru kwa kutambua mchango wake alioutoa katika kuliongoza taifa.

Rais Mkapa aliwaambia anafarijika sana pale anapopata pongezi kwa yale aliyoyafanya, kwani wakati mwingine na kutokana na kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani amekuwa akijiuliza hivi ni kweli hajafanya lolote katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wake.

“Nashukuru kuwa nyinyi na wenzenu wengi mnatambua na kukiri kwamba kuna jambo ambalo nilifanya katika uongozi wangu, nawashukuru sana.”

Kuhusu nini angeweza kufanya kama angepata nafasi zaidi ya kuongoza nchi, Rais alisema kuwa hana jibu la moja kwa moja na kuwa yale yote aliyoyafanya katika kipindi chake cha uongozi, kama vile kufufua uchumi, kubana matumizi, kubinafsisha mashirika ya umma na kuweka mazingira  imara ya ukuaji wa uchumi na kuvutia wawekezaji aliyatekeleza kwa kuwa hakuna njia mbadala.

“Niliingia katika uongozi wa nchi nikiwa nimekabwa sana, na ilinipasa kuyatekeleza niliyotekeleza ili nchi yetu iwe na mahali pa kuanzia. Lakini kama ningepata muda mwingine, pengine ningaliangalia upya baadhi ya mambo katika masuala ya uchumi,

“…Na katika siasa ningalikuwa mkali zaidi kuliko nilivyokuwa, na pengine hata baadhi ya watu nisingaliwachagua kuwa viongozi,” alisema Rais na kuwafanya Watanzania waangue kicheko.

Akizungumzia suala la uraia wa nchi mbili, Rais Mkapa alisema kuwa anasikitika kuwa hakuweza kulishughulikia jambo hilo yeye mwenyewe, lakini ana uhakika Rais ajae atalifanyia kazi.

Alisema kuwa suala hilo la uraia wa nchi mbili linatakiwa kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa ili kuepusha matumizi mabaya ya nafasi hiyo na kufafanua kwamba katika dunia ya sasa ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni rahisi sana kwa watu wenye nia mbaya kuutumia uraia wa nchi mbili kufanya vitendo vya hujuma kama vile ugaidi, ujambazi na biashara haramu zikiwemo za dawa ya kulevya na hasa kama tahadhari hazitachukuliwa.

Hata hivyo, alisema kuwa hoja hiyo inazungumzika na atamwachia Rais ajaye ashughulikie, pamoja na ile hoja ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuwezeshwa kushiriki katika upigaji wa kura wakati wa uchaguzi mkuu katika miaka ijayo.

Kuhusu hali ya kisiasa na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu, Rais aliwaeleza kuwa safari hii Tanzania Visiwani kuna uwezekano mkubwa wa kila upande kuridhika na matokeo ya uchaguzi kutokana maandalizi makubwa yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na kuwapo kwa taratibu za upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo yake.

“Tatizo la kule ni kwamba kila upande unataka ushinde na hakuna anayekubali kushindwa, hivi sasa kuna kelele kutoka pande zote mbili (CCM na CUF) kwamba kuna watu wamejiandikisha zaidi ya mara moja, sasa kazi ya kuhakiki daftari hilo imeanza na  nina hakika kuwa pande zote zitafikia muafaka kwa hiyo natumaini uchaguzi utakuwa huru na haki na hakutakuwa na machafuko yoyote,” alisisitiza.

Kuhusu kupigwa kwa waandishi wa habari na kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Rais alisema kuwa asingeweza kutoa tamko lolote kwa vile suala hilo hivi sasa linashughulikiwa na vyombo vya dola na uchunguzi bado unaendelea.

 

 

 

 

VURUGU ZA WAFUASI WA CUF BUKOBA:

Na Angela Sebastian, Bukoba

WATU 14wanaohisiwa kuwa ni wafuasi wa CUF akiwemo aliyekuwa mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya fujo na kuwaumiza wananchi 24 ambao wanasadikiwa kuwa ni wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa Ignas Mbinga, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambalo lilitokea juzi jioni ambapo watu kadhaa walijeruhiwa na baadhi yao wamelazwa katika hospitali ya mkoa mjini Bukoba.

Watu waliojeruhiwa walikuwa wakitokea katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea ubunge kupitia tiketi ya CCM, Khamisi Kagasheki katika kata ya Nyanga nje kidogo mwa mji wa Bukoba.

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Mkoa, Dk. John Madukwa aliwataja waliojeruhiwa na kulazwa hospitalini hapo kuwa ni Jeneva Laurent, Evanjelina Karani, Vanessa Peter na Geofrey Mutashobya.

Aliwataja waliotibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani kuwa Khadija Juma, Rutasitara Magezi, Happines Deus, Julietha Jakson, Dikson Elumani, Christian Mutembei, Janepha Laurent, Nelia Wilson, Bashir Rushaka, Elias Boniface na Amini Abdu,

Wengine ni Libent Kazimoto, Jakson Lukamba, Nemsalaha Rugakingira, Kahabi Kabengwa, Philbert Wilbard, Evagrinsa Boniface, Namala Mathanka, Erick Bernado, Hamduni Abdalah na Idd Pascal.

Kamanda Mbinga alisema kuwa watu hao waliokamatwa wako chini ya ulinzi huku karibu kutwa nzima jana polisi ikiendelea kumhoji Lwakatare.

Alisema kuwa katika fujo hizo, wananchi waliumizwa na magari mawili yaliyokuwa yamebeba watu hao wanaosemekana kuwa ni wafuasi wa CCM yalipigwa kwa mawe na chupa na kuvunjwa vioo.

Aliyataja magari yaliyovunjwa vioo kuwa ni Pick-Up yenye namba za usajili T 773 AAC mali ya mama Apronia Lugarabamu na Scania MZN 567 mali ya Emil Baruti.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Faustine Fisoo ambaye ni msimamizi wa uchaguzi alipohojiwa juu ya fujo hizo alikiri kuwepo kwa tukio hili na kusema kuwa CCM wamepeleka malalamiko kwake ambapo ameahidi kuwaita wahusika wa CUF na CCM na kuzungumza nao ili kukekmea vitendo hivyo ambavyo vinaweza kuhatarisha amani.

Inasemekana wananchi hao ambao walikuwa wakitokea katika mkutano wa kumnadi mgombea wa CCM wa jimbo la Bukoba Mjini, Kagasheki walipofika katika eneo la kituo kikuu cha mabasi walikutana na wafuasi hao wa CUF wakiwa na bendera za chama chao, marungu, mawe, chupa za bia huku wakiwa wamejipanga barabarani.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Bukoba Vijijini, Cosmas Kasangani alisema kuwa walipokaribia katika eneo hilo wakiwa ndani ya magari, wafuasi wa CUF walisikika wakianza kutoa matusi na vitisho dhidi ya wana-CCM hao kabla ya kuwashambulia.

“Kwakuwa sisi tuliona wanaanza kutoa maneno ya kashfa na kuziba njia tuliamua kupitia barabara ya hospitali ambapo walitufuata na kuanza kuturushia mawe na chupa wakisema kuwa watahahakikisha wanatudhibiti na kudhoofisha nguvu ya Chama Cha Mapinduzi,” alidai Kasangani

Alisema kuwa wao baada ya kuona hali imekuwa mbaya waliamua kukimbiza magari mpaka kwenye jengo la CCM mkoa huku wafuasi hao wakiwafuata nyuma na kuzidi kurusha mawe na chupa.

Alisema huku wafuasi wa CUF wakiendelea kufanya fujo viongozi wa CCM waliamua kupiga simu polisi ambapo walikuja askari wa FFU kusaidia.

 

 

 

 

Adaiwa kuigiza sauti za viongozi kutapeli

Na Saada Matiku, Mbeya

MKAZI wa Soweto jijini hapa, Sunday Muhagama (25) ametiwa mbaroni na polisi kwa tuhuma za kuigiza sauti za viongozi wa serikali wa idara mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kujipatia fedha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi baada ya kutafutwa kwa muda mrefu kuhusiana na matukio ya utapeli.

Inadaiwa  alishawatapeli baadhi ya wakuu wa mikoa mbali mbali na viongozi wengine wa idara za fedha huku akijifanya ni waziri serikalini.

Akifafanua, Kamanda Kova alisema kuwa mtuhumiwa alikuwa akiigiza sauti ya waziri yeyote kwa kuwapigia simu wakuu wa mikoa na kuwaamuru kumsaidia wakati akijifanya yuko katika msafara wa kusindikiza maiti na amekwama porini, hivyo anahitaji dola ili kupata mawasiliano.

Kova  alisema mtuhumiwa baada ya kuhojiwa na polisi alikiri kuwa amewahi kufanya matukio mengi kwa njia hiyo na ana namba zote za simu za viongozi mbalimbali, pia sauti hizo huziiga kwa kuzisikiliza kwenye redio na televisheni.

Alisema mtuhumiwa alijifunza kazi hiyo Kitwe, nchini Zambia na kuifanya baada ya kujigundua kuwa ni mwathirika miaka miwili iliyopita, hivyo alidai kuwa  hataweza kufanya kazi yoyote ngumu.

Aliongeza kuwa kwa kupitia mtego wa polisi mtuhumiwa alikamatwa alipokuwa akijaribu kutapeli katika benki ya Stanbic mjini hapa.

Inadaiwa katika tukio hilo alimpigia simu Meneja wa TRA mkoani hapa, akijifanya waziri huku akimuamuru amtafutie kazi mtoto wa waziri na baada ya kukata simu muda mfupi hujitokeza kana kwamba yeye ndiye yule kijana aliyeagizwa na waziri.

Katika mtego huo, polisi walifanikiwa kumkamata pamoja na simu yake ya mkononi ambayo alikuwa akiitumia katika shughuli zake za kutapeli viongozi hao.

 

 

 

 

 

Kikwete kuipa Rorya hadhi ya wilaya akichaguliwa

Na Bashir Nkoromo, Tarime

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete ameahidi kulifanya jimbo la Rorya mkoani Mara kuwa wilaya iwapo atachaguliwa kuwa Rais.

Kikwete alitoa ahadi hiyo juzi alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Shirati katika jimbo la Rorya, wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Mgombea huyo alisema hayo baada ya wananchi kumweleza kuwa hawana kero yoyote inayowasumbua, bali wanaomba jimbo hilo kuwa wilaya.

“Nimewauliza viongozi wenu juu ya kero zinazowakabili wakaniambia hawana tatizo zaidi ya kuomba jimbo hili kuwa wilaya. Nimesikia kilio hiki na naahidi kukifanyia kazi.

Alisema pamoja na ombi hilo, tayari mipango ya kufanya Rorya, ambayo ni sehemu ya wilaya ya Tarime kuwa wilaya kamili iko serikalini na inafanyiwa kazi. Alisema ana matumaini Rais Benjamin Mkapa atamwachia kazi hiyo na kuifanya kwa haraka baada ya kumkabidhi madaraka.

Pamoja na ahadi hiyo, aliwataka Watanzania kuwa na imani naye kwa kuwa siyo kwamba ataendeleza tu mema yaliyofanywa na serikali za awamu tatu zilizopita, bali anayo mapya ya kuyafanya.

Katika mkutano huo, Kikwete alimnadi mgombea ubunge wa Rorya, Profesa Philemon Sarungi ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Kikwete aliwaomba wananchi kumchagua Profesa Sarungi ili aendelee kuwaletea maendeleo kama alivyofanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kabla ya mkutano huo wa Shirati, Kikwete alipita na kuhutubia mikutano mingine katika maeneo ya Utegi, Masara na Bukema.

Katika mikutano yote hiyo, Kikwete alisema serikali ijayo chini ya CCM itakuwa makini katika kukuza uchumi, malengo makuu yakiwa mapinduzi katika kilimo na uwezeshaji wa wanawake na vijana ili kuboresha maisha yao.

Pia, alisema serikali ijayo itaendeleza kupanua elimu kuanzia ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu.

Jana, Kikwete aliendelea na mikutano ya kampeni mkoani Singida ambapo alihutubia mkutano mkubwa katika Uwanja wa CCM Manyoni.

Kwenye mkutano huo, aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la maji, ambalo linaikabili sana wilaya hiyo. Katika mkutano huo, wanachama 300 wapya wengi kutoka vyama vya upinzani walijiunga na CCM.

 

 

 

 

 

Moro wahimizwa kuongeza uzalishaji wa matunda

Dk. Sheni asema ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya usindikaji

Na  Ramadhan Mkoma, Morogoro

WAKULIMA mkoani Morogoro wametakiwa kuongeza uzalishaji katika kilimo cha matunda ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya usindikaji vinavyotarajiwa kuanzishwa nchini hivi karibuni.

Wito huo, ulitolewa juzi na Mgombea Mwenza wa kiti cha Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohammed Sheni, katika mikutano ya kampeni iliyofanyika katika kata ya Kisemu, Matombo na Mkuyuni katika jimbo la Morogoro Kusini Mashariki.

Alisema hadi sasa tayari wawekezaji kadhaa wamejitokeza na taratibu zimekamilika kwa ajili kuanzisha viwanda vya usindikaji wa matunda mkoani Morogoro na Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk. Sheni, kuanzishwa kwa viwanda hivyo kutainua kwa kiwango kikubwa soko la matunda nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza ubora wa mazao hayo.

Alisema uanzishaji wa viwanda hivyo unakwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 hadi 2010 ambayo imelenga katika kufanya mapinduzi makubwa katika sekta hiyo.

Dk. Sheni alisema mazao mbalimbali ya matunda yatasindikwa ikiwa ni pamoja na nazi ili kuyaongezea ubora na soko la mazao hayo ndani na nje. Mkoa wa Morogoro ni moja ya mikoa inayozalisha matunda kwa wingi nchini.

Alisema mikakati hiyo imelenga katika kuimarisha zaidi sekta hiyo na hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo katika kuendesha maisha yao.

Dk. Sheni alisema chini ya mikakati hiyo, kilimo kinatarajiwa kukua kutoka asilimia 5.6 hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2010, na hivyo kukiwezesha kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Pia, alisema jitihada hizo zitakwenda sambamba na kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinaimarishwa sambamba na ufugaji kuwa wa kisasa na wenye tija.

 

 

 

Mgombea wa CUF aomba apewe ubunge kabla hajafa

Na  Didas Kaswamila, Musoma 

MGOMBEA wa ubunge wa CUF katika jimbo la Musoma Mjini, Mustapha Wandwi amewaomba wananchi wamhurumie kwa kumpigia kura awe mbunge angalau kwa miaka mitano tu kwa kuwa kwa umri alionao sasa anakaribia kufa.

Wandwi alitoa kauli hiyo mjini hapa juzi alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika mtaa wa bondeni kata ya Kamunyonge ambapo alisema kuwa akichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu hatagombea tena katika uchaguzi ujao.

“Naomba mnihurumie mnipigie kura katika uchaguzi huu, kwani kwa umri wangu nilionao, nachungulia kaburi, na sitagombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2010,” alisema bila ya kutaja umri alionao.

Katika mkutano huo, Wandwi alisema kuwa ingawa amekuwa akiwaomba wananchi wa jimbo la Musoma Mjini kumchagua kuwa mbunge ili aweze kuibana serikali ya CCM kuwaondolea kero zao, lakini mara mbili amepuuzwa na sasa anaomba wananchi wasimpuuze tena katika uchaguzi wa mwaka huu.

Alisema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakitafsiri vibaya kauli zake anazozitoa katika mikutano ya kampeni kwa kumgeuzia maneno na kuonekana amekashifu baadhi ya wapiga kura na kusema hatakuwa akisema maneno mengi katika hotuba zake za kampeni ya mwaka huu.

“Ndugu zangu kuna mafundi wa kubadili maneno nionekane mbaya na nimewaona wapo hapa, sitakuwa nasema maneno mengi katika hotuba zangu za mwaka huu ili yasije yakabadilishwa na kuwa kashfa kwa wapiga kura wangu,” alisema.

Ingawa Wandwi hakutaja maneno ambayo alidai kuwa yamekuwa yakigeuzwa, lakini ilidaiwa kuwa katika kampeni za ubunge mwaka 1995, alikaririwa akiwaita wanawake magodoro ya Panju na kuwaita wapiga kura kuwa ni Mijusi (Bhutuku) kwa lugha za Kijita na Kikwaya).

Kauli hiyo inapingana na iliyotolewa mjini hapa hivi karibuni na mgombea mwenza wa Urais wa Chama hicho, Juma Duni Haji aliyesema CUF ikiingia madarakani itahakikisha shule nyingi za sekondari zinajengwa ili kuongeza idadi ya wasomi.

 

 

 

 

Wanachama 149 wa CUF Chake Chake wahamia CCM

Na Khatib Suleiman, Chake Chake, Pemba

MGOMBEA wa Chama Cha Mapinduzi katika nafasi ya urais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume ameivunja ngome ya CUF ambapo jumla ya wafuasi wake 149 wamekihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Karume akizungumza na wanachama pamoja na wafuasi wa CCM katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu katika jimbo la uchaguzi la CHONGA kijiji cha Pujini Chake Chake Pemba, alisema hilo ni pigo kubwa kwa CUF ambacho sasa kinaonesha wazi kupoteza dira na muelekeo wa siasa kisiwani Pemba.

“Wakati wa majigambo kwa chama cha CUF kisiwani Pemba sasa zimefikia kikomo chake na hali hii inaonesha wazi kwamba CUF sasa sio tishio tena katika kisiwa cha Pemba,” alisema Karume muda mfupi baada ya kuwapokea wanachama hao wa CUF.

Jumla ya wanachama 106 wamekihama chama cha CUF na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi katika jimbo la Uchaguzi la CHONGA huku wanachama wapya wapatao 32 wakijiunga CCM, ambapo juzi katika jimbo la OLE, Kangagani, Wete jumla ya wanachama 43 wa CUF walijiunga na CCM.

Rais Karume alisema pigo hilo kwa CUF ni ishara kwamba wananchi wa kisiwa cha Pemba wamekichoka chana hicho baada ya kuwadanganya wananchi kwa muda mrefu kwa ahadi zisizotekelezeka.

Alisema upo wakati unaweza kumdanganya mtu akakufahamu, lakini sio kila siku, kwani itafika wakati watu watagunduwa uongo huo.

“Watu sasa wamechoshwa na ahadi na udanganyifu wa chama cha CUF na ndio maana kinapoteza kila siku wanachama wake wanaojiunga kwa wingi na

Chama Cha Mapinduzi,” alisema Karume na kuwataka viongozi wa chama hicho kuacha kuidanganya dunia kwamba kisiwa cha Pemba ni ngome yake.

Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar aliwataka wananchi wa kisiwa cha Pemba kuwapa kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi ili wapate nafasi nyingine ya kuleta maendeleo kisiwani hapo.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano CCM imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusimamia na kutekeleza ilani yake kwa vitendo kwa kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya

barabara na sekta ya elimu, maji safi na salama.

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi ya urais wa Zanzibar yupo katika kisiwa cha Pemba kwa ajili ya mikutano ya kampeni zinazoendelea nchini kote ambapo alifanya mikutano yake miwili katika wilaya za Kusini na Kaskazini Pemba.

 

 

 

 

 

Wastaafu Jumuiya ya Afrika Mashariki waanza kulipwa

Na  Mwandishi  Wetu

WASTAAFU  wa mashirika yaliyokuwa  chini Jumuia ya Afrika Mashariki, walianza kulipwa mafao yao jana mjini Dar es Salaam katika benki mbili tofauti.

Hata hivyo baadhi walianza   saa 9 alasiri, baada ya kusota tangu asubuhi wakisongamana nje benki ya NMB, tawi la Water Front.

Lakini kundi jingine la wastaafu waliopangiwa kulipwa kupitia tawi la benki ya CRDB Mkwepu, mambo yalikuwa shwari, ambapo ilipofika saa 9 alasiri, wahusika wote waliojitokeza kulipwa walikuwa wameshalipwa.

Kwa mujibu wa matangazo ya magazetini jana  malipo  yaliandaliwa kwa utaratibu maalum, ambapo katika benki  ya NMB, ilikuwa zamu ya watumishi wa Bandari na kitengo cha mizigo.

Benki ya CRDB, ilikuwa ni kwa ajili ya watumishi wa vitengo vya GFS, vyenye kujumuisha idara kama hali ya hewa na makao makuu. Pia ilihusisha Posta, Shirika la Ndege la Afrika Mashariki, Posta na Simu. 

Mwandishi wa habari hii aliyetembelea tawi la CRDB, alikuta hali ni shwari, kuna watu wachache kinyume na NMB kulikofurika watu wanaokadiriwa kufikia 1,000.

Ilipofika saa 7.15, katika benki ya NMB Mwenyekiti wa muda wa wastaafu hao, Stephen Kavuma, aliwataka wenzake kuunda foleni mbili tayari kwa malipo, lakini kazi hiyo ilikwama kwa saa mbili zaidi, hali iliyoifanya foleni isambaratike. Baadhi walishachoka kusimama.

Alipotakiwa kufafanua sababu za kicheleweshwa malipo hayo, mwalikilishi wa Hazina, Damian Barandagie, alisema kwa upande wake pamoja na watumishi walikuwa tayari na walikuwa wakiwasubiri watu wa benki kutekeleza jukumu.

Hata hivyo, Mohamed Njalali, ofisa pekee wa NMB aliyekuwa pale na alipotakiwa kutoa ufafanuzi, alisema kuwa taarifa zilikuwa  zimechelewa, lakini alikuwa akifanya kazi yake kwa maelekezo ya meneja wa tawi ambaye hakuwepo hapo.

Jumla ya watu 12,000 wanatarajiwa kulipwa kupitia NMB, kwa utaratibu wa watu 2,000 kwa siku.

Wakati huo huo, mmoja wa viongozi wa wastaafu hao, Hamisi Kibira, alimsifu mno Rais Benjamin Mkapa, kwa kuitikia kilio chao cha miaka 28 juu ya malipo hayo na kusema ameonyesha utu mkubwa kwa wananchi wake.

 

 

 

 

Kondom mpya za kike zaingia sokoni

Zinaitwa 'Ladya Pepeta'

Na Mwandishi Wetu

KONDOM mpya kwa ajili ya wanawake inayoitwa 'Lady Pepeta', imezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam jana sambamba na vidonge vya uzazi wa mpango.

Akizindua kondom hizo  na vidonge vya uzazi katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Masoko na Mawasiliano Tanzania (T-MARC), Rosemary Mwakitwange alisema wameamua kuleta bidhaa hizo mpya ili kupambana na ugonjwa wa ukimwi, pamoja na kufanikisha afya bora ya mama kwa upangaji bora wa uzazi.

Kuhusu kondom za Lady Pepeta, Rosemary alisema zitamwezesha mwanamke kuwa na maamuzi makubwa zaidi katika suala zima la ufanyaji mapenzi, pamoja na kumfanya awe huru pale atakapokutana na mwanaume asiyetaka kuvaa kondom.

Rosemary alisema, wameamua kuleta kondom za kike kwani katika utafiti uliofanywa wamebaini pale kunapokuwepo matumizi makubwa ya kondom hizo, maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi yanapungua.

Alisema Lady Pepeta zitakuwa mbili tu katika paketi moja ambayo itauzwa kwa sh. 100 na mtumiaji anaweza kuivaa saa nane kabla ya kukutana na mwanaume na akafanya kazi zake zote bila tatizo lolote.

"Sisi tumewalenga wale ambao wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa ukimwi na mtumiaji yupo huru zaidi katika masuala yake ya kimapenzi kwani akikutana na mwanaume ambaye hataki kutumia kinga itakuwa si tatizo tena," alisema.

Kuhusu vidonge vya uzazi vya Flexi P, alisema katika utafiti uliofanywa imegundulika asilimia 28 ya wanawake walioolewa ndio wanaotumia uzazi wa mpango, hivyo nia yao kubwa ni kuhakikisha wanaongeza idadi hiyo ili kuwawezesha wanawake wawe salama zaidi.

Rosemary alisema vidonge hivyo vitauzwa kwa sh. 150 kwa mzunguko na wanatarajia akinamama wengi watavitumia kwani ni salama zaidi na vimefanyiwa utafiti wa kina na uwezekano wa kumuathiri mtumiaji ni mdogo.

Alisema kampuni za Shelys Pharmaceutical na Kays Hygiene Products ndizo zitakazosambaza vidonge na kondom hizo nchi nzima, huku Shirika la Misaada la Marekani (USAID) likiwa limewekeza kiasi cha dola milioni 2 kwa bidhaa zote hizo kwa muda wa miaka minne ili ziweze kuwafikia kinamama wengi kwa bei rahisi na elimu kwa watumiaji wake.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na badhi ya maafisa kutoka Kamisheni ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Wizara ya Afya pamoja na taasisi nyingine.

 

 

 

 

 

Mkapa, Mbeki watia saini kuanzishwa kwa Tume ya ushirikiano wa uchumi

Na Maura Mwingira, Pretoria

MARAIS Benjamin Mkapa na Thabo Mbeki wametia saini 69.kuanzishwa kwa Tume ya Rais ya Ushirikiano wa pamoja katika masuala ya Uchumi na Biashara kati ya nchi za Tanzania na Afrika Kusini.

Pamoja na marais hao kusaini kuanzishwa kwa Tume hiyo, Mawaziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Dk. Juma Ngasongwa na Mandisi Mpahlwa nao wametia saini mikataba miwili  inayohusu kuepusha utozaji kodi mara mbili wa bidhaa zinazoingia na kutoka katika nchi hizo na mkataba wa kukuza na kulinda maslahi ya wawekezaji.

Utiaji wa mikataba yote mitatu uliofanyika Ikulu maarufu kama Union Building.

Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa mikataba hiyo, Rais Mbeki alisema na Rais Mkapa walijadiliana na kukubaliana kuwa ni vema wakaanzisha Tume hiyo itakayokuwa nchini ya uongozi wa maraisi ili kuongeza kasi ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara.

"Tulikaa na kujadiliana baada ya kuwa na uhusiano mzuri wa kihistoria, kidugu na katika ngazi ya kidiplomasia, tulikuwa tukilegalega katika uhusiano wa kibiashara na uchumi, kwa hiyo kuanzishwa kwa Tume hii tutaongeza kasi ya ushirikiano na kuweka uwiano sawa wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi zetu," alisisitiza Rais Mbeki.

Alisema wananchi wa Afrika ya Kusini ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe wanaichukulia Tanzania kama nyumbani na kwamba mchango mkubwa uliotolewa na Rais Mkapa pamoja na viongozi waliopita na  Watanzania wote unapaswa kuenziwa kwa kuongeza kasi ya ushirikiano wa kiuchumi na biashara.

Alisema kuwa Afrika Kusini itakuwa na iko tayari kutumia uzoefu wake kusaidia katika kuitangaza Tanzania katika uso wa kimataifa ili iweze kupata wawekezaji na wafanya biashara wengi zaidi.

Kwa upande wake, Rais Mkapa alisema amefurahi kushiriki katika utiaji saini wa kuanzishwa kwa Tume hiyo kabla hajamaliza muda wake wa uongozi.

Alisema kuanzishwa kwake  kutafungua milango ya uwekezaji zaidi kwa pande zote  pamoja na kukuza biashara.

Rais Mkapa alisema waliamu kuwa tume hiyo iwe chini ya uongozi wa marais ili kupunguza urasimu na kutoa maamuzi ya haraka ili mambo yaweze kwenda kwa kasi.

Baadhi ya maeneo ytakayoshughulikiwa kupitia mikataba hiyo kwa lengo la kukuza uchumi na biasahra ni sekta ya maliasili, misitu, utalii, kilimo cha umwagiliaji na usindikaji wa mazao, utamaduni na hifadhi ya mambo ya kale.

Maeneo mengine ni uwekaji, biashara na fedha, mambo ya ndani na  hususani katika kuptia upya taratibu za utoaji wa viza katika nchi hizo ili kurahisisha wananchi na bidhaa zao kutembelea bila  kipingamizi pamoja na ulinzi na usalama.