UHURU 24.09.2005

 

VURUGU ZINAZOFANYWA NA WAPINZANI:

Wana-CCM waaswa kutojibu chokochoko

Mangula asema inaonyesha ni dalili za mfamaji

Na Mwandisi Wetu

WANACHAMA, wafuasi na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi kamwe wasiingie katika mtego wa kujibu chokochoko na mapigo ya watu wanaochochea fujo na ghasia.

Taarifa ya CCM iliyotiwa saini na Katibu Mkuu, Philip Mangula na kutolewa jana mjini Dar es Salaam imesema CCM haina sababu ya kufanya fujo wala ghasia kwa kuwa ina hakika ya kupata ushindi mkubwa wa kupigiwa kura nyingi na wanachama, wafuasi, wapenzi na wananchi wote wanaopenda maendeleo ya nchi hii.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, fujo na ghasia hizi zinazochochewa na baadhi ya vyama vya upinzani ni sawa na kutapatapa kwa mfamaji.

Taarifa kamili ya Chama ni kama ifuatavyo:

            Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, zilianza Agosti 21, 2005 kwa vyama vya siasa kunadi wagombea wao na sera zao. CCM kwa upande wake ilizindua kampeni zake kitaifa kwenye viwanja vya Jangwani Jijini Dar es Salaam siku hiyo hiyo. Kampeni zitandelea hadi Oktoba 29 na upigaji kura utakuwa Jumapili Oktoba 30.

            Katika siku za mwanzo, kampeni hizo ziliendeshwa kwa amani na utulivu, lakini hivi karibuni katika baadhi ya maeneo kumezuka vitendo vya matusi, fujo na ghasia. Miongoni mwa matukio ya fujo na ghasia ni yale yaliyotokea majuzi na jana huko Bukoba katika mkoa wa Kagera na Tarime katika mkoa wa Mara, katika mikutano na mara tu baada ya mikutano ya kampeni ya CCM. Aidha, katika jimbo la Ubungo, tawi la Midizini (Manzese) jijini Dar es Salaam, katibu Mwenezi wa CCM alichomwa moto na kuuawa akiwa ndani ya nyumba yake na familia ya watoto wanne.

            Tathmini imeonyesha dhahiri kuwa baadhi ya vyama vya upinzani ndivyo chanzo cha fujo na ghasia hizi. Vyama vya upinzani vinajua fika kuwa havitashinda katika uchaguzi ujao na hivyo vimekata tamaa, vinachochea na kufanya fujo na ghasia ili kujenga mazingira ya kuvuruga uchaguzi. Nia hasa ni kuwachokoza wanachama, wafuasi na wapenzi wa CCM ili wajibu chokochoko hizo na hatimaye yatokee mapigano yatakayoitumbukiza nchi katika maafa makubwa yatakayosababisha kuvuruga uchaguzi.

            CCM haina sababu ya kufanya fujo wala ghasia. Ina hakika ya kupata ushindi mkubwa kwa kupigiwa kura nyingi na wanachama, wafuasi, wapenzi na wananchi wote wanaopenda maendeleo ya nchi hii. Kwa sababu hiyo CCM kamwe isingependa uchaguzi uvurugike. Kinyume chake wapinzani wa CCM, kwa kuwa wanajua watashindwa, hawana chochote cha kupoteza uchaguzi ukivurugika. Kwa hiyo, fujo na ghasia hizi zinachochewa na baadhi ya vyama vya upinzani ni sawa na kutapatapa kwa mfamaji.

            Hivyo kwanza, natoa pole kwa wote walioumizwa na pia wito kwa wanachama wa CCM, wafuasi na wapenzi wa Chama hiki, kamwe wasiingie katika mtego wa kutaka kujibu ovyo mapigo ya watu wanaochochea fujo na ghasia. Kwa kufanya hivyo tutainusuru nchi isitumbukie katika maafa makubwa yatakayovuruga uchaguzi.

            Pili, CCM inavitaka vyombo vya dola viimarishe ulinzi na vitimize wajibu wake, kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, kuhakikisha kuwa kuna amani, usalama na hakuna vitisho wakati huu wa kampeni na siku ya kupiga kura ili uchaguzi uwe huru na wa haki. Wote wanaochochea na kufanya fujo na ghasia wachukuliwe hatua za kisheria bila ya woga.

            Tatu na mwisho, nawakumbusha tu viongozi wa vyama vya siasa kuwa tulikwishakubaliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa tuchukue hatua za dhati kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani na usalama kwa kuepuka vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani. Vitendo hivi vya fujo na ghasia vinavyotokea sasa katika kampeni, ambavyo ni dhahiri vinafanywa dhidi ya CCM, ni kinyume na makubaliano hayo.

 

 

 

15 wanaodaiwa wafuasi wa CUF watinga kortini

Ni kwa vurugu za kuwapiga wana-CCM Bukoba

Na Angela Sebastian, Bukoba

WATU 15 wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa

chama cha CUF wanaodaiwa kufanya vurugu zilizosababisha mapigano yaliozuka mjini hapa juzi kati ya wana CCM na CUF, wamefikishwa mahakamani.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamni jana  wakikabiliwa na mashitaka matatu tofauti mbele ya mahakimu watatu tofauti.

 Katika kesi ya kwanza inayowakabili wafuasi hao wa CUF, 12 kwa pamoja, wanatuhumiwa kumchangia John

Linakile (29), mkazi wa mjini hapa kwa kumshambulia kwa kumpiga mawe.

Watu hao walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Ignatius Bashemela.

Wakisomea maelezo ya makosa yao na Mwendesha Mashitaka wa polisi, Shaweji Alawi, alidai watuhumiwa  kwa pamoja wanashtakiwa kumshambulia Linakile kwa  kumpiga mawe na kumsababishia maumivu makali

Linakile kufuatia kushambuliwa huko alidai, amelazwa katika hospitali ya mkoa kufuatia tukio hilo la Septemba 21, mwaka huu, saa 1.45 jioni mjini hapa.

Wanaokabiliwa na shitaka hilo ni David Kyazile (28), Mathias Petro (27) wote wakazi wa Kibeta, Rwegoshora Philipo (27) mkazi wa Buyekela, na Deusdedidh Oliva Mayanga (19) mkazi wa Kashai.

Wengine ni Ubeth Peter (18) mkazi wa Kashabo, Edward Petro (18) mkazi wa Matopeni, Edgar Gabriel (23) mkazi wa Rwamishenye, Mganda Audax (18) mkazi wa Kashai, Mohamed Charles (29) mkazi wa Buyekela, na Amos Clement (20) mkazi wa Uzuri wote wa mjini hapa.

Washitakiwa hao kwa pamoja walikana shitaka hilo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 6 mwaka huu, itakapotajwa. Walirudishwa rumande baada ya kukosa

wadhamini.

Katika kesi nyingine inayohusiana na tukio hilo, ilifikishwa katika mahakama ya mkoa, ikimkabili Abdul Selemani (46) ambaye ni dereva, mkazi wa Hamugembe, akituhumiwa kumjeruhi Isaa Juma, kwa kumpiga mawe sehemu za tumboni na kichwani, na kusababisha maumivu makali.

Alifikishwa mbele ya Hakimu wa Mkoa wa Kagera, Clophace Wanne.

Akisomewa mashitaka yake na mwendesha mashitaka wa polisi, Deusdedith Masanja, alidai kuwa mtuhumiwa

alitenda kosa hilo Septemba 21, mwaka huu saa 1.45 mjini hapa.

Mtuhumiwa alikana shitaka na yuko rumande baada ya kukosa mtu wa kumdhamini na kesi yake imepangwa kutajwa Oktoba 10, mwaka huu.

Wakati huo huo, Johannes John (26), mkazi wa Mafumbo mjini hapa amefikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa

Mkoa, Moses Muzuna, akikabiliwa na kosa la kuharibu mali ya Alpronia Rugarabamu kwa makusudi, yenye thamani ya sh. 400,000.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Erick Peter, alidai mahakamani kuwa John aliharibu gari la Garabamu lenye namba T 614 ACG aina ya Fuso kwa makusudi kwa kupasua vyoo vyake kwa mawe.

Alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Septemba 21, mwaka huu saa 12.45 kati kati ya mji wa Bukoba.

Mtuhumiwa alikana shtaka hilo na yuko rumande baada ya kukosa mdhamini.

Katika kesi nyingine iliyofikishwa mbele ya Hakimu Muzuna ilimkabili Juvent Wilson (18) mkazi Kashabo kwa tuhuma ya kuharibu gari lenye thamani ya sh. 500,000.

Akisomewa shitaka mbele ya Hakimu Moses Muzuna, Mwendesha mashitaka Erick Peter, alidai mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Septemba 21, mwaka huu saa 12.45 jioni katika vurugu zilizozuka mjini hapa wakati wafuasi wanadhaniwa kuwa wa CUF walipowashambulia wana CCM. Aliliponda gari hilo kwa mawe.

Mwendesha mashataka huyo alidai kuwa Wilson aliharibu gari la Erick Garabamu aina ya Nissan T 773 AAC kwa kuvunja vioo vyake kwa mawe.

Wilson alikana shtaka hilo na yuko rumande kwa kukosa mtu wa kumdhamini.

 

 

 

 

Sumaye: Kikwete ni chuma cha pua

Asema amepita kwenye matanuru yote

Na Bashir Nkoromo, Katesh

WAZIRI Mkuu Frederick Sumaye, amemfananisha mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete, na chuma cha pua kilichopita katika matanuru yote, tofauti na wapinzani ambao alisema ni mabati.

Sumaye alitoa kauli hiyo wakati akimnadi Kikwete katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika uwanja wa Katesh, na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa mji huu.

Alisema Kikwete anastahili kupewa kura kwa kuwa ana sifa za kuwa rais kutokana na uzoefu alionao kitaifa na kimataifa ikilinganishwa na wagombea wengine ambao hata majina yao hayajulikani.

“Kikwete ni kingozi mwenzetu, tuna matumaini naye kutokana na uchapakazi wake, uaminifu wake ndani ya CCM na serikali kwa miaka mingi,” alisema Sumaye.

Alisema kutokana na uchapakazi wake, Kikwete ameifanya Tanzania kujulikana nje ya nchi na kuheshimiwa kutokana na kazi yake nzuri akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mbali na hilo, alimuelezea kuwa ni kiongozi anayejua matatizo yanayolikabili, na ni mtu ambaye taifa halina wasiwasi naye kwa kuwa ni mtu ambaye yuko makini katika kuimarisha amani na uchumi wa nchi.

Aliwataka wananchi wa jimbo la Hanang kumpa kura zote Kikwete na kwamba atakayefanya vinginevyo ni mchawi.

Akizungumza katika mkutano huo, Kikwete aliwaomba wananchi hao kumpa kura ili aweze kuendeleza mengi mazuri yaliyofanywa na viongozi waliopita katika serikali za awamu tatu zilizopita.

Mbali na hayo alisema yeye pia ana mapya ya kuyaanzisha kwa faida ya Watanzania iwapo atachaguliwa kuongoza dola.

Alisema hayo yatakwenda sambamba na uboreshaji wa sekta ya elimu, nishati, miundombinu ikiwemo ya barabara ambayo ndiyo msingi wa uchumi wa taifa lolote.

Kikwete alizitaja baadhi ya barabara zitakazokamilishwa kuwa Dodoma hadi Mwanza, ikifuatiwa na ujenzi wa barabara itakayounganisha Babati na Singida kwa kiwango cha lami.

Alizitaja barabara nyingine zitakazojengwa kuwa ni ya kutoka Babati - Dodoma hadi Iringa.

Sekta nyingine zitakazoimarishwa katika awamu ya nne ya uongozi ni kilimo na ufugaji, ambazo zitakuwa za kisasa zaidi ili ziweze kuchangia kikamilifu katika kuongeza mapato ya taifa.

Katika mkutano huo CCM ilizoa wanachama wapya 456 wakiwemo 222 kutoka kambi ya upinzani. Wanachama hao na idadi yao kwenye mabano ni kutoka CUF (142), Chadema (64) na TLP (18).

 

 

 

 

Wagombea wa CCM kata 19 Mufindi wapita

Na Lauden Mwambona, Mafinga

CHAMA Cha Mapinduzi Wilaya ya Mufindi kinaendelea kupeta baada ya kupata kata 19 bila upinzani kutoka vyama vingine katika kuwania udiwani kwenye kata zote 28 za wilaya hiyo.

Katibu wa CCM wa wilaya, Getrude Lupola, alisema kata zilizopatikana zipo katika majimbo yote mawili ya uchaguzi ambayo ni Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini.

Getrude alitaja kata zenye wagombea pekee wa CCM zilizoko jimbo la Mufindi Kusini kuwa ni Mbalamaziwa, Bunilayinga, Mtambule, Mninga, Ihowanza, Idunda, Mtwango, Malangali, Kiyowela, Igowole na Makungu.

Kwa upande wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Kata ambazo wananchi wote waliikubali CCM ni Ihanu, Rungemba, Mpanda Tazara, Kibengu, Mafinga, Ikweha, Ifwagi na Mapanda,

Katibu wa CCM wilaya hiyo alisema kupatikana kwa kata hizo kunafuatia msimamo thabiti wa wananchi wa kukataa kuyumbishwa na vyama vya upinzani kwa vile serikali ya CCM imetekeleza kazi za maendeleo kwa ufanisi mkubwa.

Alisema mpaka sasa ni kata tisa tu ambazo wapinzani walijitokeza kusaka udiwani na kwamba kata hizo ni Kasanga, Itandula, Nyololo, Igombavanu, Isalavanu, Ihalimba, Mdabulo, Sadani na Luhunga.

Kuhusu maendeleo ya kampeni ya ubunge na Urais, Getrude alisema  mpaka sasa wananchi wengi wa Mufindi wameahidi kupiga kura za ndio kwa wagombea wa CCM.

"Mgombea ubunge wa CCM kwenye jimbo la Mufindi Kaskazini, Benito Malangalila na Mgombea wa ubunge jimbo la Mufindi Kusini, Joseph Mungai, wanaendelea vizuri na kampeni," alisema.

Alisema CCM wilaya ya Mufindi imejipanga vizuri kuhakikisha Mgombea wa Urais Jakaya Kikwete anapata kura nyingi siku ya Oktoba 30, mwaka huu.

Naye Katibu Msaidizi wa CCM wilaya hiyo, Godson Stephen, alisema vyama vya upinzani vinapata pigo kila siku kwa wanachama wao kuvikimbia na kurudi CCM kwenye mikutano ya kampeni.

Stephen alisema tangu kampeni ianze wilayani Mufindi hadi juzi,  zaidi ya watu 400 waliokuwa upinzani wamerudi CCM kwenye mikutano mbalimbali ya kampeni inayofanyika katika majimbo yote mawili.

 

 

 

...asema atamaliza ujenzi uwanja wa Namfua Singida

Na Mwandishi Wetu, Singida

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, amesema akiwa rais atahakikisha ujenzi wa uwanja wa Namfua mjini hapa unakamilika.

Kikwete alisema hayo jana, wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja huo, mkutano ambao ulihudhuriwa na mamia ya wananchi waliojawa bashasha na hamu ya kuona na kumsikiliza mgommbea huyo.

Hata hivyo, alisema kazi ya kukamilisha ujenzi wa uwanja huo itakuwa nyepesi na ya uhakika kama wananchi wa jimbo la Singida Mjini watamchagua mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM, Mohammed Dewji, ili ashirikiane naye katika mchakato mzima wa ujenzi huo.

Akimanadi Dewji, Kikwete alisema, ni kijana anayemfahamu kuwa si 'njaa kali' hivyo wananchi wakimchagua watakuwa na uhakika kwamba mgombea huyo atawasaidia kwa kuwa hatashughulikia tumbo lake kwanza.

Ujenzi wa uwanja huo unaendelea, lakini sehemu yake kubwa haijakamilika.

Akizungumzia sera, Kikwete alisema wananchi hawana budi kumchagua yeye kuwa rais na wabunge wote kwa tiketi ya CCM, kwa kuwa CCM ndiyo chama chenye anuani na cha kuaminika badala ya kuchagua vingine alivyoviita kuwa vya kilalamishi tu.

Kikwete alisema CCM inayo mengi ya kujivunia ambayo hakuna chama mbadala kinachoweza kutamba kuwa kinaweza kuyafanya au kiliwahi kuyafanya.

Alisema baadhi ya mambo muhimu ambayo CCM inajivunia kwa wananchi ni pamoja na kufanikiwa kujenga taifa lenye umoja na mshikamano uliojaaa amani na utulivu.

Kuhusu uchumi, Kikwete alisema serikali yake itaweka mpango maalum utakaowawezesha wananchi masikini kukopesheka.

Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuzirasimisha mali  za wanyonge ili ziweze kuwa dhamana ya kukopeshwa fedha lakini kwa masharti nafuu.

Alisema kupitia mpango huo wanawake na vijana kwani wataweza kujiari na kuondokana na umasikini ambao umekuwa ukiwaandama kila kukicha kutokana na kukosa mitaji ya kuendesha shughuli zao.

 

 

 

Kikwete asomewa dua kwenye kaburi la Mwalimu Nyerere

Na Bashir Nkoromo, Butiama

MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, ametembelea kaburi la baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika kijiji cha Butiama mkoani Mara, ambapo pia alifanya mazungumzo ya faragha na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere.

Kwenye kaburi la Mwalimu, Kikwete alisomewa dua ya kumtakia kheri na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi ujao, dua ambayo ilisomwa na Sheikh Mussa Muyinjwa.

Ilikuwa ni ziara ya aina yake, ambayo Kikwete aliifanya mwishoni mwa ziara yake ya mikutano ya kampeni mkoani Mara, ambapo pamoja na kuzungumza na Mama Maria, pia alipata fursa ya kuzungumza  na baadhi ya wanafamilia ya hayati Mwalimu.

Nyumbani kwa hayati Mwalimu, Kikwete pia alikutana na mama wa ubatizo wa hayati Mwalimu, Sophia Msonge (86), ambaye alimuhakikishia kuwa atashinda kiti cha urais na kuiongoza Tanzania.

Baadaye Kikwete alikwenda kwa ndege kuendelea na ziara yake mkoani Singida, ambako alilakiwa kwa shangwe na nderemo katika uwanja mdogo wa Kilimatinde wilayani Manyoni.

Akihutubia kwenye uwanja wa Namfua, mjini Singida, Kikwete alisema, pamoja na kuyaendeleza yaliyofanywa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere, Rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi na Rais Benjamin Mkapa, anayo mapya mengi ya kuwafanyia Watanzania.

Alisema moja ya mikakati yake akiwa rais ni kuinua uchumi wa taifa na wananchi kwa jumla, kuboresha elimu za msingi, sekondari na vyuo vya juu, ili hali iwe bora zaidi yenye kukidhi mahitaji.

Kikwete aliahidi kukamilika kwa kiwango cha lami ujenzi wa barabara ya Singida-Nzega-Kahama na Dodoma-Singida, ambazo hadi sasa matengenezo yake Yanaendelea vizuri.

 

 

 

 

 

Kususia kuandika habari ni kukiuka maadili ya uandishi

l Pia ni pamoja na kuvunja haki za binadamu

Na Mwandishi Wetu

IMEELEZWA kuwa siyo sahihi kwa vyombo vya habari nchini kususia kuandika habari, kwani kufanya hivyo ni ukiukaji wa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na haki za binadamu.

Wakizungumza katika mkutano wa kutathmini uandishi wa habari jana katika hoteli ya Palm Beach mjini Dar es Salaam, waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walisema badala yake vyombo hivyo vinapaswa kuandika masuala yote muhimu kwa lengo la kuelimisha jamii.

Walisema jukumu muhimu la vyombo na waandishi wa habari ni kuandika mambo yote kwa kuzingatia ukweli na uwazi, na kwamba kususa kuandika habari ni kwenda kinyume na maadili yanayoiongoza taaluma hiyo.

Mkutano huo ulilenga kutathmini uandishi wa habari mbalimbali, hususan habari za kususia kuandika habari za Waziri wa Mambo ya Ndani, Omari Ramadhani Mapuri na Kamishna Mkuu wa Magereza nchini, Nicas Banzi kufuatia kauli iliyoonekana kama inatetea tukio la kupigwa kwa waandishi wa habari.

Mkutano huo ambao ulikuwa katika hali ya majadiliano zaidi uliitishwa na taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na masuala ya utafiti katika taaluma ya uandishi wa habari ya Media Research Centre (MRC) ya mjini Dar es Salaam, chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Kassim Mbegha.

Mwandishi wa habari wa siku nyingi nchini, Lawrence Kilimwiko, alisema siku zote kazi ya mwandishi ni kukusanya, kuchambua na kutawanya habari kwa ajili ya watu wengine na kwamba kususa kuandika habari ni kwenda kinyume na misingi inayoongoza taaluma ya habari.

Kilimwiko alisema waandishi wa habari hawaandiki habari kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili ya jamii na kwamba kwenda kinyume na hivyo ni kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kufahamu mambo mbalimbali yanayoendelea nchini na duniani kwa jumla.

Alisema vilevile kwamba kususa kuandika habari za maendeleo, mafanikio na matatizo kuhusu taasisi fulani ni ukiukwaji wa haki za binadamu, kwani wananchi wana haki na wajibu wa kutambua kuhusu kinachoendelea katika taasisi hizo.

Joe Nakajumo, mhariri wa habari wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo akichangia katika majadiliano hayo, alisema vyombo vya habari na hasa waandishi wa habari wanapaswa kuepuka kuandika habari zao kwa kuegemea upande wowote na ushabiki.

Nakajumo alisema uandishi wa habari unaoegemea upande mmoja au kushabikia unadumaza vipaji vya waandishi na taaluma hiyo ambayo ni nyeti katika mchakato mzima wa maendeleo ya nchi.

Alisema ni vyema waandishi wakajikita zaidi katika misingi na taratibu zinazoongoza taaluma hiyo kwa kuandika habari zilizo wazi na kazi ya kutathmini upande wa aliyekosa na ulio sahihi aachiwe msomaji wa habari hiyo.

Mabel Masasi wa Star TV alisema upo umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari kupitia vyama vyao kuwa na majadiliano na wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama ili kuwa na mwelekeo mmoja katika ujenzi wa nchi.

Mbegha katika majumuisho ya majadiliano hayo alisema yapo mambo mbalimbali yanayopaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari kuongeza ujuzi zaidi, hasa katika masuala yanayohusiana na sheria mbalimbali za nchi.

Alisema mapungufu ya kutojua sheria za nchi na maadili yanayoongoza taaluma ya habari kwa baadhi ya waandishi wa habari nchini ni kikwazo katika kukuza taaluma hiyo na maendeleo ya nchi.

 

 

 

 

Karume asema maslahi ya walimu kupewa kipaumbele

Na Mwandishi Maalum, Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, ameeleza kuwa maslahi ya walimu yatapewa kipaumbele ili kuimarisha ubora wa elimu Zanzibar.

 Rais Karume alieleza hayo alipofanya mazungumzo na walimu wa skuli wanaofanya kazi kisiwani Pemba katika ukumbi wa Chachani, Chake Chake, Pemba.

 Katika mazungumzo hayo, Rais Karume ambaye ni mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya CCM, alisema serikali inathamini sana juhudi na mchango wa walimu katika azma ya kuendeleza sekta ya elimu Zanzibar.

Alisema matatizo na maslahi ya walimu kisiwani Pemba yatatafutiwa ufumbuzi ili kuwajengea mazingira mazuri walimu kufanikisha malengo ya elimu yaliyokusudiwa kutekelezwa.

 Mapema katika risala yao, walimu walieleza kuwa wengi miongoni mwao wanakabiliwa na tatizo la nyumba za kuishi na usafiri, mambo ambayo yanawasababishia usumbufu.

 Alisema maslahi ya walimu, hasa kipato chao kitaongezwa, na serikali itatekeleza mpango uliokuwepo zamani wa kujenga nyumba za walimu karibu na maeneo yao ya kazi.

 Rais Karume alitoa wito kwa walimu hao kufanikisha malengo ya kuinua ubora wa elimu kwa kiwango cha juu zaidi, na kuwataka wafanye juhudi za kujiendeleza kwa kutumia fursa zinazopatikana nchini katika vyuo vikuu na taasisi nyengine za elimu kupitia miradi maalum ya kuendeleza elimu kwa walimu.

 “Endeleeni kujifunza zaidi kwa kutumia fursa za elimu zinazotolewa na serikali kupitia vyuo vikuu vyetu nchini,” alisema Rais Karume.

 Wakati akitoa ufafanuzi wa maendeleo ya elimu, Rais Karume alisema hatua kubwa ya maendeleo ya elimu Zanzibar yanatokana na kuwepo kwa mfumo mpya wa utawala, ambao umechukua nafasi ya mfumo mkongwe wa kikoloni na Kisultani. Alieleza kuwa sera ya elimu bila malipo iliyotangazwa Septemba 23, 1964, ndiyo chanzo cha maendeleo hayo chini ya mfumo mpya wa utawala.

 “Kila fursa za walimu kujiendeleza zimewekwa wazi kwa kila mwalimu... na hayo yanatokana na utekelezaji wa malengo ndani ya maana halisi iliyokusudiwa katika usemi wa Mapinduzi Daima. ... Mapinduzi Daima maana yake ni mabadiliko ya kuendeleza maendeleo yanayotokana na Mapinduzi ya 1964 yaliyoanzisha mfumo mpya wa utawala,” alisema Rais Karume.

 Serikali ya Mapinduzi ilichukua hatua ya kuwekeza katika elimu katika misingi ya usawa na elimu kwa wote na kutokana na juhudi hizo leo kila Shehia kisiwani Pemba imeweza kuwa na skuli, alisisitiza Rais Karume.

 Ili kufanikisha malengo yote ya maendeleo Zanzibar, kunahitajika umoja, amani, utulivu na mshikamano. “Walimu mna kazi kubwa ya kujenga jamii yenye amani, utulivu na mshikamano hasa kwa sababu mnakaa na vijana wafunzeni kuishi kwa amani na utulivu,” alisisitiza Rais Karume.

 Mapema katika mazungumzo hayo, Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo, Haroun Ali Suleiman, aliwaeleza walimu kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutilia mkazo suala la ubora wa elimu, wizara yake imekuwa akiajiri walimu karibu 1,000 kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya walimu na ongezeko la skuli katika shehia na ngazi mbali mbali za masomo.

 Aliendelea kusema kuwa ajira ya walimu itaendelea kupewa kipaumbele ili kuimarisha maendeleo ya elimu Zanzibar.

 Hata hivyo, Waziri Haroun aliwatahadharisha walimu kuzungumza na watu wanaotumia wanafunzi wadogo wa skuli kusambaza ‘posters’ za kisiasa mitaani. “Walimu na wanafunzi hawahusiki na shughuli za kusambaza ‘posters’ za viongozi wa kisiasa,” alisema Waziri Haroun.

 

 

 

 

Mkapa ahimiza vyuo vikuu Afrika kuzalisha wabunifu

Na Peter Orwa

RAIS Benjamin Mkapa, amesema vyuo vikuu barani Afrika ni lazima vizalishe wahitimu wabunifu na wenye uwezo wa kumudu ushindani katika soko la ajira katika sekta binafsi na za umma.

Kauli hiyo aliitoa jana akihutubia jumuiya ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Lesotho, ambapo alitunukiwa Shahada ya heshima ya Udaktari wa Falsafa (Ph.D) katika fani ya sheria.

“Elimu ya Chuo Kikuu ni lazima iandae vijana wetu kuwa wabunifu, washindani, iwe ama kwenye sekta za umma au binafsi, kitaifa, kanda au kimataifa katika soko la ajira kwenye utandawazi wenye kuhitaji nguvu kazi zenye maarifa,” alisema Mkapa katika hotuba yake ambayo Uhuru ilipata nakala.

Hata hivyo, alishutumu vyuo vikuu vya sasa Afrika ambavyo ni chemchem ya kuzalisha wasomi wa kizazi kijacho, kuwa bado havijafanya mabadiliko ya kutosha katika changamoto ya kuondokana na mfumo wa mapokeo ya nchi tajiri za Magharibi.

Rais Mkapa alisema vyuo vikuu vingi vya Afrika bado havijalifanyia mabadiliko hilo, hasa katika maeneo ya mitaala, utafiti, na mabadiliko mengine kwa ajili ya kujenga mwelekeo mpya.

Akizungumzia uwezo wa wasomi wa vyuo vikuu, alisema kimsingi wanatakiwa kuwa na upeo wa kutosha juu ya kizazi cha sasa na kijacho kwa upana wake, na kazi ya kuwaandaa ni ya chuo kikuu, kupitia mikakati bora.

“Nchini Tanzania, ama ninaposikiliza au kusoma kile kilichoandikwa na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu au baadhi ya wahadhiri, sifurahii kuona uelewa wao uko hivyo,” alisema Rais Mkapa.

“Elimu ya vyuo vikuu tunayoipa kizazi chetu kipya, ni lazima iwaandae kiuerevu, msimamo na kitaaluma, ili wawe chachu ya mabadiliko. Tunawahitaji wahitimu wenye fikra za ubunifu na wenye kubunu vitu asilia na si anayeturudishia mtazamo, fikra na hisia za Magharibi,” alifafanua.

Alitoa mfano wa katika kipindi akisoma nadharia na kazi mbalimbali za kitaaluma, wakati akiandaa ripoti ya Tume ya Dunia kuhusu madhara ya Utandawazi, alisema mchango wa wasomi wa Afrika ni mdogo mno.

Rais Mkapa katika hotuba hiyo, akionyesha wazi kuguswa mno na uzalendo kwa bara lake, alisema wasomi wa Afrika wamebweteka kwa kutofanya utafiti wa matatizo yanayohusu Bara lao na badala yake, wanawaachia wenzao wa nchi tajiri za Magharibi, kuwafanya kazi hiyo.

“Kuna wakati nilikuwa Waziri wa Elimu ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Ninayafahamu matatizo yanayovifika vyuo vikuu vya Afrika, hasa inapofika kipengele cha kufanya utafiti, maandiko na machapisho,” alisema.

Akizungumzia Zimbabwe, alivishanga vyombo vya habari vya Afrika vikiimba wimbo wa wenzao wa Ulaya, kuwa tatizo kubwa la siasa za Zimbabwe, ni suala la ardhi, jambo ambalo si la kweli, bila ya kuzingatia undani wa suala hilo.

Alisema kimsingi anashawishika kuamini hayo yanayoitwa ‘madhambi’ yasingekuwepo iwapo tofauti za kihistoria kuhusiana na suala la milki ya ardhi lingeshughulikiwa mapema.

“Kama ni hili linaloifanya Zimbabwe kuwa ‘taifa lililoanguka’ tunapaswa kujiuliza kwanini? Je, Tanzania nayo ni taifa lililoanguka kwa sababu tu tunataka kulinda haki za msingi za wananchi kuhusu mali-ardhi?” alihoji Mkapa.