UHURU 26.09.2005
Sumaye: Kikwete chaguo la watu
Asema wapinzani hawachaguliki, wanaiga sera za CCM Vyama vyao havina ilani na vinatumia ya CCM
Awataka walioenguliwa kura za maoni kuacha kinyongo
‘Hivi mimi baada ya kushindwa Chimwaga na kutoka si mngeniona chizi?’
Na Serafina Sungusia, Hanang
WAZIRI Mkuu Frederik Sumaye ‘amewaponda’ wagombea urais wa Jamuhuri ya Muungano kupitia vyama vya upinzani hawafai kuchaguliwa, kwani hawana hata ilani ya vyama vyao na kuishia kutumia ilani ya CCM katika mikutano yao ya kampeni.
Alisema mgombea pekee anayechagulika ni Jakaya Kikwete wa CCM, ambaye chama chake kina ilani inayoeleweka na inayoweza kumletea maisha mema kila Mtanzania.
Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wakazi wa Endagau kata ya Endasaki, jimbo la Hanang, wakati wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge jimboni humo kwa tiketi ya CCM, Dk. Mary Nagu, na mgombea udiwani, Hashim Mohamed.
Sumaye ambaye ni mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo, alisema wagombea wa upinzani wamekuwa wakitembea na ilani ya CCM kwa kuwa wanajua imekamilika katika nyanja zote, na ndiyo mwongozo wa utekelezaji wa mambo yote ya nchi hii.
Alisema ilani hiyo anayoamini kila mwananchi akiisoma na kuielewa ni lazima akubali kuwa CCM ndiyo chama pekee kitakachoweza kumtoa mwananchi katika hali duni na kumweka kwenye hali ya maendeleo ya kisasa, ikiwa ni pamoja na kuiongoza serikali ya awamu ya nne kutekeleza kila hitaji la Mtanzania.
“Wapo wanaotembea na ilani ya CCM...wakija muwaulize yao iko wapi...hawana, na ndiyo maana hata sera zao haziridhishi. Hawana muongozo, kazi ni kupiga kelele tu. Wasikilizeni lakini Oktoba 30 mwaka huu wekeni historia kwa kuwaangusha vibaya katika ngazi zote za uongozi,” alisema Sumaye.
Akimwombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete, Sumaye aliwataka ‘watoto wake’ wa jimbo hilo kuwa na ujasiri kama wake na kuhakikisha mgombea huyo anapata kura zote katika jimbo hilo na mkoa wa Manyara kwa ujumla, ili walio na hisia tofauti wajue kuwa umoja na mshikamano uliopo ndani ya CCM hautavunjika na watashinda kwa kimbunga.
“Nitampigania Kikwete kwa nguvu na hoja nzito, jimboni Hanang na kwingine kote. Hata wapinzani wanajua rais ni Kiwete, ila basi wanajaribu kuonyesha wapo...nawaomba wote walioanguka katika kura za maoni ngazi zote kuvunja makundi, tuelekeze nguvu kwa mgombea aliyepitishwa, msiingize tamaa,” alisisitiza.
Aliwataka wagombea na wale walioanguka katika mchakato wa kura za maoni, kutambua kwamba uongozi ni dhamana na siyo kitu cha kukimbilia, na aliwataka pia kujua ya kuwa wananchi ndiyo wenye maamuzi ya kumuweka na kumng’oa kiongozi yeyote asiyewajibika au kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Hivi mimi nilipoanguka pale Chimwaga ningejiengua kwenye chama si mngeniona chizi? Sasa iweje hata walioanguka udiwani kuwa na roho ya kwa nini kiasi cha kuhamia kwa hao wasio na sera?” Alihoji na kusema ‘mwisho wake mtauona’.
Akinadi sera za CCM baada ya kutambulishwa, Mary Nagu aliwaahidi wakazi wa hapa kuwa atahakikisha barabara kuu inajengwa kwa kiwango cha lami ili kutatua tatizo la kusafirisha mazao ya wakulima kwenda kwenye masoko makuu, akiamini kuwa kilimo ndiyo kazi tegemezi ya eneo hilo.
Pia aliwahakikishia kupata huduma ya maji haraka kupitia shirika la ADRA, na kuwajengea shule ya sekondari na zahanati ili kupunguza tatizo la wanawake wajawazito na watoto.
Mgogoro wa Kiwanda cha Karatasi Mgololo:
CCM yaitaka serikali ifikie muafaka na wafanyakazi kuepusha mgomo
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Iringa, Tasili Mgoda, ameishauri serikali kutatua tatizo la wafanyakazi wa Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo kwa misingi ya amani bila kutumia nguvu ili wafanyakazi wapate haki zao wanazostahili na kuelimishwa mambo ambayo hawatapata, anaripoti Lauden Mwambona kutoka Iringa
Mgoda alisema hayo juzi alipoelezea msimamo wa CCM juu ya mgogoro wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, ambao wamegoma tangu Julai mpaka sasa, na hakuna dalili za kupatikana ufumbuzi wa tatizo hilo.
Wafanyakazi wa kiwanda hicho waligoma, na baadaye serikali ilipeleka askari wa kikosi cha kuzuia fujo 150 kuwatimua maeneo ya kiwanda, na mpaka sasa askari hao wanakilinda kiwanda hicho.
‘’CCM inasikitishwa na jinsi serikali inavyosuasua kushughulikia matatizo ya wafanyakazi wa Mgololo, ambao wanadai haki zao za msingi,’’ alisema na kuongeza kwamba kinachotakiwa ni serikali kukaa pamoja na wafanyakazi kutatua tatizo hilo.
Alisema madai halali ya wafanyakazi yasikilizwe na mengine wafafanuliwe ili wajue ukweli, na kwamba kitendo cha serikali kukaa kimya kinawavunja nguvu wafanyakazi waaminifu wa kiwanda hicho ambao wamedumu kwa kipindi kirefu.
Mwenyekiti kwa niaba ya CCM, alisema wafanyakazi hao wanadai mafao yao ya utumishi kabla ya kubinafsishwa kiwanda hicho mwaka jana, na pia wanadai mmiliki wake mpya amefuta utaratibu wa tiba kwa wafanyakazi, na ameongeza muda wa kazi kutoka saa 40 kwa wiki hadi saa 45 bila kujadiliana kwanza na wafanyakazi.
Kiwanda cha Mgololo kilibinafsishwa mapema mwaka jana, ambapo mmiliki wake mpya ni kampuni ya Rai kutoka Kenya.
Mmiliki huyo anadaiwa kuwafukuza kazi wafanyakazi 119 bila sababu za msingi, na hakuwalipa mafao yao jambo ambalo limesababisha hofu kwa watumishi wengi.
Mgoda alitoa wito kwa serikali kusuluhisha haraka tatizo hilo ili kiwanda kiweze kuendelea na kazi sambamba na wafanyakazi nao wapate haki zao wanazostahili.
Kuhusu tatizo jingine la wafanyakazi wa mashamba ya chai nchini ambao wamepanga kugoma kazi kwa siku tatu kuanzia Oktoba 11 mwaka huu, wakiwemo wa mashamba ya chai Mufindi, Unilever na Luponde mkoani Iringa, Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa wamiliki wa mashamba wakiwemo waajiri na wafanyakazi wote, kujadili zaidi tatizo hilo ili mgomo usifanyike.
Alisema amepata taarifa kwamba wawakilishi wa wafanyakazi wa mashamba ya chai walikaa pamoja na wamiliki wa mashamba, jambo ambalo hadi sasa zimebaki sh. 500 tu kuafikiana ili kuepusha mgomo.
‘’CCM mkoa wa Iringa inawasihi wamiliki wa mashamba na wafanyakazi waendelee na mazungumzo ya kufikia muafaka, na siyo kuruhusu mgomo kwa vile migomo inakwamisha maendeleo,’’ alisema.
Mkapa atunukiwa nishani ya heshima ya juu Lesotho
Na Maura Mwingira, Lesotho
MFALME wa Lesotho, Letsie III, amemtukunu Rais Benjamin Mkapa, nishani ya kwanza na ya juu kabisa katika nchi hiyo ya ‘Knight Commander The Most Courteous Order of Lesotho’.
Rais Benjamin Mkapa alitunukiwa nishani hiyo jana wakati wa hafla ya chakula cha usiku alichokuwa ameandaliwa na Mfalme huyo kwa heshima yake. Rais Mkapa alikuwa na ziara rasmi ya siku mbili nchini hapa kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Profesa Pakalitha Mosisili.
Akizungumza kabla ya kumvisha nishani hiyo, Mfalme Letsie III ambaye alisoma wasifu wa Rais Benjamin Mkapa, alisema ameamua kumtunuku nishani hiyo ya juu kabisa, kutokana na nchi yake na yeye binafsi kutambua mchango mkubwa alioutoa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.
Alisema Rais Mkapa pia ameshiriki kupigania haki na usawa wa Waafrika kupitia kamisheni mbalimbali za kimataifa, pamoja na kutambua uongozi wake uliotukuka alioutoa kwa maendeleo ya Watanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
“Rais Mkapa ambaye yuko mbele yetu, wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , alijitolea sana na alikuwa mstari wa mbele katika vita vya ukombozi dhidi ya ukoloni, ubaguzi wa rangi, ubeberu na ukoloni mambo leo katika nchi za kusini mwa Afrika.
“Alitetea haki na usawa wa bara la Afrika na watu wake, kwa sababu hiyo na kwa uongzi wake uliotukuka ndani ya Tanzania na Afrika na je ya Afrika, ninakutunuku nishani ya kwanza na ya juu kabisa ya taifa letu,” alisema Mfalme huyo.
Aliongeza kuwa uongozi wa Rais Mkapa ni uongozi uliotukuka, wa kujituma, kujitolea, wa uwazi na ukweli na uwajibikaji, akiwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya umasikini na kusisitiza kuwa ni uongozi unaofaa kuigwa na viongozi wengine katika bara la Afrika.
Alisema ametoa mchango mkubwa katika Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), na ni wakati wa uenyekiti wake, jumuia hiyo ilipitisha programu mbalimbali na muhimu za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuitisha mkutano maalum uliojadili kwa kina suala la kilimo na uhifadhi wa chakula.
Mfalme Letsie III, alisema Lesotho na Afrika nzima ina deni kubwa kwa Tanzania, nchi ambayo ilitoa mwana wa Afrika, na kiongozi mashuhuri katika karne ya 21, aliyekuwa na dira, msimamo, na asiyetetereka, muasisi wa vita vya ukombozi na mpigania haki, na usawa wa Mwafrika, mwanampinduzi halisi na mwanzilishi wa Umoja wa Nchini Huru za Afrika (OAU), Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema ziara ya Rais Mkapa nchini humo ni muhimu na imekuja wakati muafaka, kwani imelenga kudumisha na kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati ya serikali za nchi mbili hizo na watu wake, na kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano.
“Lesotho na Tanzania zinahitaji kuwa karibu ili kuunganisha nguvu zake pamoja na zile za nchi nyingine barani Afrika, ili kwa pamoja tuweze kukabiliana na changamoto za utandawazi na kupigania na kutetea nafasi ya bara la Afrika katika siasa, uchumi, biashara na kisiasa,” alisema.
“Wakati tunakupongeza na kusifu uamuzi wako wa kuachia madaraka ya uongozi katika nchi yako , kustaafu kwako kutakuwa na pengo kubwa sana katika Afrika, lakini tunajifariji kwa kuamini kuwa bado utaendelea kutuongoza kwa kutoa mchango wa mawazo na busara zako, kwani umekuwa mtetezi na msemaji mkubwa wa Waafrika na bara la Afrika,” alisema Mfalme Letsie III.
Akizungumza baada ya kuvishwa nishani hiyo, Rais Mkapa alisema ziara yake hiyo ilikuwa ya kuwaaga wananchi wa Lesotho na uongozi wa nchini hiyo, na kushukuru kwa ushirikiano mkubwa ulikuwapo kati yake na uongozi wa nchi hiyo.
Alisema hakutarajia kuwa angetunukiwa nishani hiyo ya juu kabisa nchi humo.
Alimshukuru Mfalme huyo kwa uamuzi huo wa kumtunuku nishani hiyo, na kwa kutambua mchango wake, pamoja na sifa alizozitoa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nrerere.
Karume aonya wafanyabiashara kuacha magendo Zanzibar
Na Mwandishi Maalum
WAFANYABIASHARA wa Zanzibar wameonywa kuacha mara moja biashara ya magendo, kwa kuwa licha ya kuikosesha serikali mapato pia inazorotesha maendeleo ya nchi.
Onyo hilo lilitolewa hapa juzi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, alipozungumza na wafanyabiashara wa Pemba katika ukumbi wa ZSSF, Chake Chake, Pemba.
Rais Karume alisema biashara ya magendo imekuwa ikiikosesha serikali mapato mengi kwa ajili ya kuhudumia shughuli mbalimbali muhimu kwa huduma za jamii, na kuongeza kuwa hata vitabu vya dini vinakataza aina hiyo ya biashara.
Alisema serikali wakati wote inapenda kuwaona wafanyabiashara wakiendelea, na ndiyo maana imeandaa sera za biashara ndogo ndogo na sekta binafsi kwa ajili ya kuwaandaa wafanyabiashra katika uchumi wa soko huria.
Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM inasema wazi kuwa biashara lazima iwe huru na uchumi wa nchi ujengwe kwa kushirikisha sekta binafsi, ushirika, wawekezaji wa ndani na nje, lakini ikiwa hakuna budi, serikali ifanye biashara katika maeneo ambayo makundi hayo hayawezi au hayathubutu kutokana na maslahi yao.
Hata hivyo, Rais Karume alisisitiza sana juu ya umuhimu kwa wafanyabiashara kulipa kodi ambayo ndiyo inayowezesha serikali kutoa huduma za kijamii kama za ulinzi, elimu na matibabu.
Aliendelea kusema kuwa ulinzi ni muhimu kwa ajili ya kulinda amani nchini, na kunukuu maneno ya Kiarabu yanayosema, “Penye matatizo, fedha haikai na kama kuna fedha basi ujue kuna amani”.
Alisema kodi inaisaidia serikali kujenga miundombinu kama barabara, umeme, mawasiliano na kutoa mfano wa barabara zilizojengwa visiwani humo kwa kutumia fedha zinazotokana na mapato ya ndani ikiwemo kodi.
Pia Rais Karume aliwataka wafanyabiashara hao kuacha kuridhika na biashara ya kuagiza bidhaa ziziotengenezwa kutoka nje, au kununua na kuuza tu, na badala yake waanze kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo ambavyo vitaongeza thamani ya bidhaa wanazouza, kama vile usindikizaji wa matunda.
Aliwataka kuanza kufikiria kuagiza vitambaa na kisha kushona nguo wenyewe kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watakuwa wanaongeza na kutoa ajira mpya kwa vijana na wanawake ambao wengi wao sasa wana matatizo ya kiuchumi.
“Kutofanya hivyo na kung’ang’ania biashara ya kununua na kuuza, mtawakosesha vijana ajira,” alisisitiza Rais Karume.
Akizungumzia uwekezaji na biashara mpya, aliwataka wafanyabiashara kutumia taasisi za fedha zilizopo kupata mikopo itakayowawezesha kuanzisha biashara mpya na kubwa, hasa ikizingatiwa kuwa soko la bidhaa nyingi limepanuka baada ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Rais Karume ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya CCM, alisema katika kuendeleza biashara ndogo ndogo, serikali ya Watu wa China ilitoa fedha kidogo ambazo hata hivyo hakuzitaja ni kiasi gani kwa ajili hiyo.
Hata hivyo, alisema kiasi fulani cha fedha hizo zimetumika kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na nyingine ndiyo zitatumika kwa ajili ya kuanzishia viwanda vidogo vidogo, ambazo masharti yake ni kuagiza mashine kutoka China.
Matumizi ya fulana za kampeni hakuathiri demokrasia - UVCCM
Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya wana-CCM waliohudhuria semina ya vijana yenye kuwaandaa kuelekea uchaguzi mkuu ujao, wamepinga fikra za wanaobeza matumizi ya fulana na mavazi mengine, eti yanakiuka demokrasia.
Wana-CCM hao akiwemo mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Mussa Mnyeti, na kada Hadija Faraji, walisema kutumia fulana na mavazi mengine ya kampeni ni sehemu ya mchakato wa kisiasa.
Semina hiyo iliandaliwa na asasi ya Tanzania Youth Vision Association (TYVA) ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana, ambapo miongoni mwa washiriki ni pamoja na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki katika semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa UNICEF, Upanga Dar es Salaam, walishutumu dhana ya kutumia haiba ya mgombea, matumizi ya fulana na takrima kama pingamizi kwa demokrasia, huku baadhi wakielekeza shutuma kwa chama tawala-CCM.
Hadija, aliyejitambulisha kama mwanachama wa CCM, huku akimnukuu mwanafalsafa Marchiaveli, alisema katika kinyang’anyiro cha siasa, dhana ya ushindi ni lazima upatikane kwa njia yoyote na msingi ni sheria zifuatwe.
Alitaja njia hizi za kupata ushindi, ni pamoja na kujivunia haiba, kufanya matangazo na promosheni za kisiasa kama njia ya kujinadi na kupata kura za wananchi.
Aidha, wote kwa nyakati tofuati waliunga mkono matumizi ya takrima, ila walichokipinga ni matumizi mabaya ya takrima hiyo na kwa maana hiyo inastahili kuwepo.
“Wapiga kura ni watu wa hali ya chini ni lazima tu utawakirimu kwa kuwapa fulana au mengineyo,” alisema Hadija.
Naye Mnyeti, ambaye ni mjumbe kupitia Vijana mkoa wa Mwanza, aliwashangaa watu wanaojitokeza kuwabeza baadhi ya wana-CCM waliopitishwa kuwania ubunge kwa ngazi ya Viti Maalum, kuwa si sahihi kwani wana haki.
Alisema walikuwa na sifa sawia na kutumia mbinu zote za kisiasa za kujinadi kwa wapiga kura wa vikao husika hadi wakakubalika na haelewi ni jinsi gani minong’ono hiyo inaibuka.
Mnyeti alisifu CCM kama chama chenye kujali usawa, ndio maana katika nafasi za uwakalishi wa viti maalum iliangalia sehemu zote ikiwa ni pamoja na kad
Mvungi ahutubia mkutano uliohudhuriwa na watu wachache
Na El-hadji Yuusuf, Tabora
Mambo yamekuwa magumu kwa mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi, baada ya kujikuta akihutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na watoto na watu wazima wachache.
Katika mkutano huo uliofanyika katika mtaa wa Kiyungi mjini hapa, mgombea huyo alijikuta akianza kuhutubia watu wasiozidi 20, ambapo pia walikuwepo watoto waliokadiriwa kufikia 30 walioonekana kumshangaa.
Hali hiyo ilipelekea mwanachama mmoja wa chama hicho amuulize swali Dk. Mvungi, ni kwa nini mkutano huo umeendeshwa katika mtaa huo badala ya kuendeshwa katika maeneo mengine ya wazi ambayo yangeweza kuvuta watu zaidi wa kumsikiliza.
Mvungi alikataa kujibu swali hilo, kwa madai kuwa yeye ni mgeni hawezi kujua ni sehemu ipi angeweza kupata watu wengi wa kumsikiliza, bali yeye hupangiwa na wenyeji wake sehemu ya kuhutubia.
Alimtaka Murugenzi wa Uhaguzi wa chama hicho ajibu swali hilo, lakini naye katika majibu yake alionekana kubabaisha, kwa sababu hakutaja sababu rasmi iliyofanya mgombea huyo ahutubie eneo la Kiyungi.
Hali hiyo ilionekana kumsononesha mgombea huyo wa urais, kwani pamoja na yeye kuwa katika hali hiyo, wanachama wa chama hicho pia walionyesha hali ya kukata tamaa.
Akihutubia watu hao wachache waliojitokeza kumsikiliza, mgombea huyo aliwataka wakazi wa kata hiyo wampigie kura ili awe rais wa nne wa Tanzania na kueleza kuwa akishika madaraka atahakikisha elimu inaboreshwa kwa kiwango kikubwa.
Alisema chama chake kinatambua kuwa elimu ya msingi ni ile inayotolewa katika ngazi ambayo itamfanya mtu aweze kujitegemea na hivyo akiingia ikulu elimu ya msingi itakuwa mpaka kidato cha nne.
Alidai kuwa elimu inayotolewa sasa nchini ni ya ‘manamba’ na Watanzania wengi wana elimu hiyo ambayo haiwezi kuwasaidia, hivyo ni vyema wamchague yeye ili ashike madaraka na kuiboresha elimu hiyo.
Sambamba na elimu, Dk. Mvungi alisema NCCR ikiingia ikulu itahakikisha kuwa mikataba yote inayohusu rasilimali za kitaifa inavunjwa na kungaliwa upya ili kuwawezesha Watanzania wanufaike na rasilimali hizo.
Alidai kuwa katika kufanya hivyo atahakikisha anapambana na rushwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Watanzania wanalipwa mishahara minono.
Hata hivyo, alisema kuwa atawashangaa Watanzania iwapo watashindwa kumpigia kura, kwani anajua kuwa ana kila sifa ya kuwa rais wa nchi katika serikali ya awamu ya nne, na kwamba wasipompigia kura atakuja kuwasuta.
Kampeni za CCM zaelekezwa kuibomoa ngome ya CUF Zanzibar
Pemba yatikiswa na kimbunga cha Kikwete, Karume
Watu wahoji kwa nini Seif azindulie kampeni Nairobi?
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepania kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani visiwani Zanzibar. Makala hii ya ALLY MWINYIKAI inatathmini mkakati huo ambao unaonyesha huenda ukakisambaratisha chama kikuu cha upinzani visiwani humo-CUF.
TATHMINI iliyofanywa ndani ya kipindi cha wiki mbili za kampeni za Uchaguzi Mkuu Zanzibar zinaonesha Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume anakubalika zaidi ikilinganishwa na wagombea wa vyama vingine.
Jumla ya vyama sita vya siasa vimejitokeza kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar. Vyama hivyo ni CCM, CUF, Jahazi asilia, DP, Demokrasia Makini na NRA.
Pamoja na wingi wa vyama kujitokeza kugombea nafasi hiyo, vyama viwili tu – CCM na CUF – ndivyo vinavyoonekana kuwa na ushindani mkali kiasi kwamba wananchi wamekuwa wakifuatilia zaidi kampeni za vyama hivyo kuliko vingine.
Wakati takriban mwezi mmoja umebaki kabla ya Watanzania hawajatumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaowapenda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu, ushindani unaendelea kwa vyama hivyo viwili kila kimoja kuwania kukishinda kingine.
Viongozi na wagombea wa vyama hivyo wamekuwa katika hekaheka kubwa za kutangaza ilani zao kwa ajili ya kuwashawishi wananchi kuwachagua wagombea waliosimamishwa na vyama vyao. Kila chama kikijinadi kuwa na ilani ya uhakika.
Kampeni za uchaguzi zimeshika kasi kubwa tangu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilipotangaza kuanzwa kwa shughuli hiyo Septemba 5, mwaka huu.
Kampeni hizo zinaonekana kutoa mvuto na hisia maalumu zaidi katika mikutano inayohutubiwa na wagombea wenyewe wa nasafi ya Urais.
Kigezo kikubwa cha tathmini iliyofanyika kinachukuliwa kutokana na mahudhurio ya wafuasi wa vyama hivyo katika mikutano ya hadhara ya kampeni inayoandaliwa na vyama hivyo. Hadi sasa, CCM inaongoza kwa kuwa na watu wengi wanaohudhuria kwenye mikutano yake.
Jambo lililojitokeza katika uendeshaji wa kampeni hizo ni kuanza kwa vyama hivyo viwili kujipima kwa kiasi gani vinakubalika katika ngome za wapinzani wao. CCM imekuwa ikijipima nguvu zake katika ngome ya CUF iliyoko kisiwani Pemba na CUF ikifanya hivyo katika kisiwa cha Unguja kwenye ngome kuu ya CCM.
Katika kufanya hivyo, CCM iliamua kuzindua kampeni zake hizo kwenye uwanja wa Gombani ya Kale ulioko Chake Chake, Pemba. Uzinduzi huo ulifanyika Sepemba 5, siku iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya kuanza kampeni hizo.
Kwa upande wa wapinzani wao CUF, uzinduzi wa kampeni zake ulifanyika Nairobi, Kenya siku hiyo hiyo na kufuatiwa na mkutano wake wa kwanza wa hadhara uliofanyika Septemba 8 kwenye kiwanja cha Kibanda Maiti mjini Unguja.
Uzinduzi huo wa CUF ulianza kwa watu kujiuliza kilichofanya chama hicho kuzindua kampeni zake hizo nje ya nchi ingawa wapiga kura ni Wazanzibari na sio wa Kenya.
Tathmini iliyofanywa imedhihirisha kwamba katika uzinduzi wa kampeni hizo CCM imefanikiwa sana kuingia kisiwani Pemba kwa nia ya kuiteka ngome ya CUF ambayo inasadikiwa ilikuwa haiingiliki.
Mafanikio ya chama hicho ni kutokana na idadi kubwa ya watu waliohudhuria kwenye mkutano huo wa uzinduzi. Wingi wa watu uliokuwepo wakati wa uzinduzi, unaelezwa kwamba umeweza kuwatia hofu na wasiwasi hata viongozi wa CUF walioshuhudia umati huo wa watu. Lilikuwa tukio la kihistoria ambalo halikupata kuonekana ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Hata hivyo, baadhi ya wafuasi na viongozi wa upinzani walijijengea matumaini mapya kwamba idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye mkutano huo walikuwa kutoka Unguja na kuendelea kuamini kwamba Pemba hakuna wana-CCM.
Dhana hiyo imekuwa ikikataa kadiri kampeni zinavyozidi kushamiri kwani kinachojitokeza hivi sasa ni kuwepo mwamko mkubwa wa wananchi wa Pemba katika kukikubali Chama Cha Mapinduzi na wagombea wake wa nafasi ya Urais wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Upande wa CCM umezichukulia dhana hizo za CUF ni za kujipa matumaini yasiyoweza kutekelezeka na unaamini kuwa hayo yalikuwa mafanikio kwa upande wao.
CCM inayaeleza madai yaliyotolewa na viongozi wa CUF kwamba umati huo ulichukuliwa kutoka Unguja yalikuwa ni ya kujipa moyo.
Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema idadi ya watu waliokwenda Pemba kutoka Unguja hawakuzidi 1,000 kwa kutumia meli ya m.v. Mapinduzi watu 750 na Sepideh 250.
“Isingewezekana kwa hali yoyote kusafirisha zaidi ya watu 30,000 walioshiriki kwenye mkutano wa uzinduzi huo,” alifahamisha.
Wakati wana harakati za kisiasa wakitathmini hali hiyo, CUF nayo ilijitahidi kutunisha misuli yake katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni uliofanyika Kibanda Maiti ambapo mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad alizungumzia mambo mawili – upunguzaji wa kodi na uongezeko la mishahara iwapo atashinda uchaguzi huo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na watu wengi lakini haukuwa na idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na CCM iliyofanya mkutano wake wa kampeni kwenye kiwanja hicho hicho siku moja tu ya mkutano wa CUF.
Matamshi ya Maalim Seif yalitoa matumaini kwa wafuasi wa chama hicho kwa kiasi fulani kutokana na ahadi zilizotolewa.
Kilichoahidiwa na mgombea huyo ni kwamba CUF ikifanikiwa kuingia madarakani kitahakikisha kodi zote za bidhaa zinazoingizwa nchini hazitozidi asilimia 10 ya bei halisi ya bidhaa hizo.
Maalim Seif pia alisema watumishi wa Serikali watapandishiwa mishahara yao kwa kima cha chini kulipwa sh. 100,000 badala ya sasa sh. 50,000.
Hata hivyo, matamshi hayo yalionekana kupungua nguvu zake kufuatia uchambuzi uliofanywa baadaye na kuonekana kuwa ahadi zilizotolewa na mgombea huo wa CUF haziwezi kutekelezeka.
Ilimchukua siku mbili tu mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM, Amani Abeid Karume kuwaeleza wafuasi wake kwamba maelezo yaliyotolewa na mpinzani wake ni ahadi za njozi na ni danganya toto.
Msingi mkubwa wa hoja ya Karume ni kwamba ahadi hizo haziendani na misingi ya kiuchumi. Hoja kubwa ya mgombea wa CCM ni kwamba haiwezekani kupunguza kodi kwa kiwango kikubwa na wakati huohuo ukapandisha matumizi kwa asilimia 100 bila ya kuwepo vyanzo vingine vya kodi. Taratibu za kiuchumi hazikubali hali hiyo.
Hoja hizo zimeanza kutawala mawazo ya wapiga kura wengi wa Zanzibar na kwa kiasi kikubwa zimeanza kuathiri fikra za wananchi ambapo kumekuwa na kutiliwa mashaka makubwa wa baadhi ya kauli zinazotolewa kwenye majukwaa ya kisiasa.
Ndani ya duru za kampeni zinavyoendelea, Mgombea Karume ameonekana kumpiku Mgombea Maalim Seif kwa taaluma ya uchumi ambapo wafuasi wa mgombea huyo wa CCM wameanza kutangaza kwamba Maalim Seif hamuwezi Karume kwa mambo ya uchumi.
Athari iliyojitokeza kuhusisha na kauli za kutilia mashaka ni kuonekana kudhoofika kwa ngome ya upinzani hasa kisiwani Pemba.
Kudhoofika kwa ngome hiyo kulijitokeza pale Maalim Seif alipofanya mikutano minne ya kampeni kisiwani Pemba iliyohudhuriwa na wafuasi wachache kinyume na ilivyozoeleka huko nyuma.
Mikutano hiyo ilifanyika katika kijiji cha Konde, Ole, Mkanyageni na Ditia Wawi. Katika mikutano hiyo kutokana na mahudhurio yake, mgombea huyo alishindwa hata kuwahutubia wafuasi wake zaidi ya kusimama kwenye jukwaa na kuwapungia mkono baada ya wapambe wake kufanya utambulisho.
Lililodhihirisha kwamba mahudhurio yamewafadhaisha viongozi wa CUF ni pale chama hicho kilipopangua ratiba yake ya kufanya mkutano mkubwa kwenye kiwanja kikubwa ilichokizoea cha Tibirizi na badala yake kuamua kufanya kiwanja kidogo cha Ditia Wawi ambapo hapo Maalim Seif alihutubia kwa dakika 10 tu.
Tathmini ya jumla ya kampeni inavyokwenda inaonekana kung’ara kwa mgombea wa CCM ikilinganishwa na mpinzani mwenzake.
Hali hiyo imekuja kwa kufuatilia kwa karibu mikutano ya kampeni inavyokwenda ambapo CCM imebainika kujiongezea nguvu ndani ya ngome ya CUF.
Nguvu hizo zimeongezeka kutokana na baadhi ya wanachama wengi wa CUF kutangaza kujitoa katika chama hicho na kujiunga CCM.
Tukio la karibu ni lile lililofanyika kwenye mkutano wa kampeni wa CCM huko Kangagani katika jimbo la Ole na Pujini jimbo la Chonga ambako wanachama 149 wa CUF yalikabidhiwa kadi za CCM na mgombea Karume.
Vitisho na vitendo vya vurugu vinavyosadikiwa kufanywa na wafuasi wa CUF vya kuwapiga mawe CCM kupigwa mawe wanapokuwa wakirejea kwenye mikutano ya kampeni na kuchanwa kwa picha za wagombea wa CCM vimeelezwa kuwa ni dalili zinazoashiria CUF kukubali kushindwa.
Aidha, CUF kuanza kulalamika mapema kwenye nchi na jumuiya za kimatifa kwa kila hatua inayotekelezwa katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi ni ushahidi wa chama hicho kutafuta hisani za kisiasa kutoka kwa taasisi hizo pale itakapofikia chama hicho kushindwa.
Pamoja na kukabidhiwa kadi kwa wanachama hao, vukuto la kutaka kumdhihirishia mgombea Hamad kwamba CUF sio mali yake pekee liko ndani ya wafuasi na wanachama wa Chama hicho na limekuwa likizungumwa hadharani.
Nini wafuasi hao walichokusudia kukifanya katika uchaguzi mkuu huo bado hakijafahamika wazi lakini hali inaonekana haiko shwari ndani ya chama hicho cha upinzani hali ambayo haitoi matumaini yoyote ya ushindi kwa mgombea huyo wa CUF.