UHURU 27.09.2005

 

 

Kikwete: Sikubali Muungano uchezewe na wachache

Na Khatib Suleiman, Zanzibar

MGOMBEA wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amesema akichaguliwa kuwa rais hatokubali kuona Muungano unachezewa kwa faida ya wachache.

Alisema kuvunjika kwa Muungano huo kutalifanya taifa la Tanzania kufa, na hivyo kuchekwa na dunia.

Alisema kama atakuwa rais hatokubali kamwe kuona muungano unachezewa na wakorofi wachache kwa maslahi yao, kwani kufa kwa muungano ni sawa na kusambaratisha taifa na 'tutachekwa' na mataifa mengine.

Alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni huko katika kijiji cha Chwaka mkoa wa Kusini Unguja, ambapo alisema juhudi mbalimbali zimefanywa kujaribu kuondoa kero zinazohusiana na masuala ya Muungano.

Kikwete alisema akichaguliwa kuwa rais atahakikisha kero za muungano na manung'uniko yote yaliyopo yanapatiwa ufumbuzi kwa uwazi zaidi.

Alisema katika kutatua kero hizo Tume mbalimbali za kuyatafutia ufumbuzi ziliundwa katika kipindi kinachomalizika cha Rais Benjamin Mkapa.

"Nikichaguliwa kuwa rais wa Muungano kazi hiyo nitaiendeleza ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya muungano kwa ‘lilahi’ na kwa uwazi zaidi," alisema.

Alisema Muungano utazidi kuimarishwa kwa maslahi ya pande zote mbili za Zanzibar na Tanzania Bara.

Alisifu juhudi za viongozi waasisi wa taifa la Tanzania akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume, kwa kuasisi Muungano ambao umekuwa mfano wa kuigwa katika bara zima la Afrika na ulaya kwa ujumla.

Mapema, Kikwete aliwataka wananchi na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi, kuichagua CCM na wagombea wake wote ili wapate nafasi ya kuleta maendeleo zaidi.

Alisema viongozi waliopo sasa akiwemo Rais Amani Abeid Karume, wamefanya kazi kubwa katika kuimarisha amani na utulivu, na uimarishaji wa miundombinu ikiwemo ya barabara, ambayo imewasaidia wananchi kurahisisha usafiri kutoka mjini hadi vijijini.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Karume ameisimamia na kuitekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo, na matunda yake yanaonekana waziwazi na wananchi wote, pamoja na wapinzani.

"Mkimchaguwa Karume, mjuwe kuwa mmechagua mtu anayeweza kuwaletea maendeleo yenu kwa haraka," alisema Kikwete ambaye pia aliwaombea wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani kura, ili waingie katika vyombo vya kutunga sheria.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia mgombea wa Chama cha Mapinduzi kwa nafasi ya urais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ambaye aliwataka wafuasi wa CCM kuwa watulivu katika kipindi hiki, kwani kiburi cha wapinzani kitamalizwa kwa kunyimwa kura katika uchaguzi mkuu.

 

 

 

 

 

Rais Mkapa aenda Uholanzi kwa ziara rasmi ya kikazi

Na Mwandishi Wetu

RAIS Benjamin Mkapa alitazamiwa kuondoka nchini jana usiku kwenda The Hague, Uholanzi ambako atakuwa na ziara ya kikazi ya siku mbili.

Akiwa nchini humo, Rais atahutubia katika ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa ulioitishwa na Taasisi ya Maendeleo ya Uholanzi (SNV). Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake katika nchi 28 za Afrika, Ulaya, Asia na Amerika ya Kati.

Mkutano huo wa Kimataifa, utajadili na kutafakari namna gani Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) yanavyoweza kutekelezwa katika ngazi ya kitaifa na kwa kutumia rasilimali na uwezo uliomo ndani ya nchi husika.

Tanzania inatarajiwa katika mkutano huo, kuelezea uzoefu wake katika utekelezaji wa malengo hayo na pia kutoa mapendekezo ya nini kinachoweza kufanyika na nini hakiwezekani.

Mkutano pia utajadili namna gani taasisi zisizo za kiserikali, sekta binafsi na serikali zinavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa malengo hayo ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wake.

Viongozi mbalimbali kutoka nchi zinazoendelea wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo. Waziri wa Maendeleo wa Uholanzi, Agness von Ardenne, Profesa Jefferey Sachs kutoka Mradi wa Milenia na Rais wa Benki ya Dunia, Paul Wolfewitz ni baadhi ya viongozi watakaozungumza katika mkutano huo.

Mkutano huo pia unafanyika ikiwa ni wiki chache tu tangu ulipofanyika mkutano wa mwaka wa Umoja wa Mataifa ambapo ulipitia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Baada ya kuhudhuria mkutano huo, Rais Mkapa atakwenda Roma, Italia ambako pia atakuwa na ziara ya kikazi. Akiwa nchini humo, Rais anatarajiwa kwenda Vatican ambako atakutana na Baba Mtakatifu Benedictine wa XIV.

Baadaye Rais atakwenda nchini Ujerumani ambako atazungumza katika hafla ya kutunukiwa nishani Aga Khan.

Rais atafuatana na mama Anna Mkapa na balozi wa Tanzania nchini Simen Mlay katika ziara yake ya Uholanzi. Katika ziara ya Ujerumani, Rais atafuatana na Mama Anna Mkapa.

Rais na ujumbe wake anatarajiwa kurejea nyumbani Oktoba 4.