UHURU 28.09.2005

 

 

MIKUTANO YA KIKWETE KILIMANJARO: CHADEMA yapanga kupandikiza mamluki

Na Rodrick Makundi, Moshi

CHAMA Cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro, kimebaini njama zilizopangwa na CHADEMA kupandikiza watu kuzomea mikutano ya mgombea urais, Jakaya Kikwete atakapofanya ziara kuanzia keshokutwa.

Imebainika kwamba watu hao wameandaliwa na Chadema kupiga kelele za kuwakataa wagombea wa CCM kwenye mikutano ya hadhara wakati wa ziara hiyo ya mgombea Kikwete.

Njama hizo kwa mujibu wa Katibu wa CCM mkoa, Simon Nchimbi zimepangwa kufanywa na watu waliopandikizwa katika jimbo la Moshi Mjini.

Katika taarifa yake, Katibu wa Mkoa ametoa wito kwa Chadema kurejea makubaliano yaliyofikiwa na vyama vya siasa ya kuendesha kampeni za kistaarabu na kwamba hatua ya chama hicho inakwenda kinyume na makubaliano hayo na inaweza kuhatarisha amani.

Hata hivyo, alisema CCM inatambua kinachoendelea na kuwa haipendi kuwa sehemu ya vurugu inayoweza kuhatarisha amani na utulivu wa wananchi wake.

Badala yake, Nchimbi alivitaka vyama kutambua wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inalindwa na sio kupanga njama za kuvuruga amani.

Kikwete anatarajiwa kuwasili mkoani Kilimanjaro Ijumaa kwa ajili ya kuendelea na mikutano ya kampeni mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu huyo wa CCM wa mkoa, mgombea huyo wa CCM atawasili mkoani hapa akitokea mkoani Tanga.

Alisema CCM mkoani imekamilisha maandalizi ya mapokezi pamoja na maeneo yote atakayohutubia mikutano ya kampeni akianzia maeneo ya Ndugu katika jimbo la Same Mashariki, Mwanga na jimbo la Moshi Mjini, shughuli ambayo itafanyika Ijumaa.

Aidha, kampeni hiyo itaendelea Oktoba Mosi, kwa kufanya mikutano mitatu katika majimbo ya Rombo, Vunjo na Hai ambapo baadaye ataendelea na ziara yake hiyo mkoani Arusha.

 

 

 

 

Vyombo vya habari vyatakiwa kutokuwa chanzo cha machafuko

Na Grace Msovela, Arusha

WAZIRI Mkuu Frederick Sumaye ameviasa vyombo vya habari kutokuwa chanzo cha machafuko yatakayosababisha ukosefu wa amani na utulivu ndani ya jamii katika nchi za Afrika.

Sumaye alitoa changamoto hiyo juzi jijini Arusha alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 13 wa Umoja wa Vyombo vya Utangazaji vya Umma,vilivyopo katika nchi za Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika hoteli ya Impala.

Aliwataka wadau wa sekta hiyo kuzingatia maadili na miiko ya uandishi wa habari ili kuepuka matatizo yanayoweza kusababishwa na ukiukwaji wa taaluma ya utangazaji.

Sumaye aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba, vyombo vya habari katika bara la Afrika vina nafasi pekee na maalum katika kukuza demokrasia na kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika katika hali ya utulivu, amani na usalama.

Alisema hayo yatawezekana ikiwa vyombo vya habari vitazingatia maadili na miiko ya kazi ya uandishi, hasa wakati wa uchaguzi katika nchi hizo.

Sumaye alitoa wito kwa viongozi barani Afrika kutumia vyombo vya habari katika kusikia vilio vya wananchi na kuweza kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya wananchi na yanayoikabili jamii kwa jumla kupitia vyombo hivyo.

Hata hivyo, alivipongeza vyombo vya habari kwa kuwezesha kukuza demokrasia na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi hizo.

"Demokrasia inaweza ikawa na maana tu ikiwa italenga na ikitumika kubadilisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa bara la Afrika, vinginevyo demokrasia hiyo itakuwa imepoteza maana yake," alisema Sumaye.

Naye mkurugenzi wa wa Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT), Samwilu Mwaffisi alisema kuwa vyombo vya habari vimetumika kikamilifu katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika pamoja na kupiga vita ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini.

Mwaffisi alitoa mfano wa vyombo vya habari vya umma nchini Rwanda vilivyochangia kuchochea mauaji ya halaiki yaliyoikumba nchi hiyo mwaka 1984.Alisema kuwa vyombo vya habari vya umma vilitakiwa kuhakikisha hali kama hiyo, haijitokezi tena na kutumika kama silaha ya kuendeleza mauaji ya watu katika baadhi ya nchi za Afrika.

“Ni lazima vyombo vya habari barani Afrika vihakikishe kuwa utangazaji unabakia kuwa silaha ya ukombozi, umoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi badala ya kutumika kama vyombo vya kuliangamiza bara hili,” alisisitiza Mwaffisi.

 

Polisi: Marufuku kuandamana baada ya mikutano ya kampeni

Na Mwandishi Wetu

WAFUASI wa vyama vya siasa watakaoandamana baada ya mikutano ya kampeni watakamatwa, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, ameonya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Tibaigana alisema baadhi ya viongozi wa vyama wamekuwa wakiibua maandamano mwishoni mwa mikutano yao ya kampeni.

Alisema mikutano inapomalizika saa 12.30 jioni kwa mujibu wa sheria, baadhi ya viongozi wa vyama wamekuwa wakiwakusanya tena wanachama na mashabiki wao na kuingia mitaani kwa maandamano.

Katika kufanya hivyo alisema, baadhi ya viongozi hao hubuni visingizio vya aina nyingi ikiwa ni pamoja na kujidai wanafungua matawi ya wafuasi wa vyama vyao.

Tibaigana alionya polisi haitaweza kuvumilia hali hiyo kwa sababu inalenga kuvunja amani.

Alisema kwa kawaida polisi hujiandaa kuweka ulinzi kwenye mikutano yote ya kampeni kwa sababu inakuwa tayari inafahamika kuwa katika wakati na mahali fulani.

"Lakini utakuta viongozi wa vyama baada ya kuwahutubia kwenye mikutano yao, wanawaingiza mitaani wafuasi wao kwa kisingizio cha kufungua matawi ya vyama, huku wakifahamu kwamba sisi (polisi) hatukujiandaa kuendelea na ulinzi huko," alisema Tibaigana.

Alisema ni wajibu wa viongozi wa vyama kuwatawanya wafuasi wao kila mikutano yao ya kampeni inapomalizika.

Tibaigana alisema mbali na kasoro hiyo, kampeni za vyama mbalimbali vya siasa katika kuwania nafasi za urais, ubunge na udiwani, zinaendelea vizuri.

 

 

Kampeni za CCM zaingiza wanachama zaidi ya 1200

Na Prosper Kulita, Morogoro

CHAMA Cha Mapinduzi mkoa wa Morogoro kimeingiza wanachama wapya 1,260 kutoka vyama mbalimbali vya siasa vya upinzani na kufanikiwa kuvunja baadhi ya matawi muhimu ya vyama hivyo.

Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Catherine Ndahani, alimweleza mwandishi wa habari hii kuwa wanachama hao wamepokelewa kwa nyakati tofauti katika mikutano mbalimbali ya kampeni inayoendelea nchini kote.

Alisema wanachama hao wamepokelewa na viongozi mbalimbali wakiwemo mgombea mwenza wa urais, Dk. Ali Mohammed Sheni, Katibu Mkuu wa CCM, Phillip Mangula, na mke wa mgombea urais wa CCM, Salma Kikwete.

Catherine alivitaja vyama vilivyopoteza wanachama katika kipindi hicho ni pamoja na NCCR-Mageuzi, CUF, TLP, UDP na CHADEMA.

Akielezea zaidi alisema katika jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na Morogoro Kusini, wanachama wa upinzani 560 walihama na kuvunja ngome imara ya UDP. Wanachama hao walipokewa na Dk. Sheni, wakati katika jimbo la Kilosa na Mikumi mama Kikwete alipokea wanachama 200.

Katibu Mkuu wa CCM, Phillip Mangula, alipokea wanachama 500 katika jimbo la Ulanga Magharibi, ambao ni kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa hapa nchini.

Akielezea hali ya kampeni katika mkoa wa Morogoro kwa upande wa CCM, Katibu huyo alisema kazi hiyo inaendelea vizuri na kuongeza kuwa wana uhakika na ushindi katika majimbo yote 10 ya mkoa huo, ambapo aliwataka wana CCM kuongeza nguvu katika kuzinadi sera za chama.

Kuhusiana na madai ya kuwepo makundi katika mkoa wa Morogoro yanayosababisha kugawanyika kwa wanachama wa CCM, Catherine alisema mpaka sasa wameshamaliza tofauti zilizokuwepo na wana-CCM wote wamekuwa kitu kimoja kuhakikisha Chama chao kinapata ushindi katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.

 

Karume: Wapuuzeni wapinzani wanaotaka kuleta mfumo hodhi

Agawa vifaa vya uvuvi vya zaidi ya sh. milioni 300

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, amewatahadharisha wananchi kuwapuuza viongozi wanaotaka kuleta mfumo wa uchumi hodhi.

Rais Karume alitoa tahadhari hiyo jana alipozungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya kukabidhi vifaa vya uvuvi kwa jumuiya na ushirika mbalimbali huko Maisara mjini hapa.

Alisema hatari ya mfumo wa uchumi hodhi hauwezi kuendelea kwa sababu umepitwa na wakati na duniani haupo tena hivi sasa, na kwamba viongozi wanaotaka kuurejesha ni hatari kwani mara nyingi huwa madikteta na wanaotaka kuhodhi kila kitu.

"Viwanda vikiwa chini ya serikali, basi vyote vitakuwa vyake yeye na atachagua nani akae kiwanda hiki," alisema.

Viongozi kama hao wanataka kuhodhi serikali, si viongozi tunaowahitaji katika karne hii, alisisitiza Rais Karume na kusema karne hii inahitaji viongozi wataoweka sera nzuri, na njia nzuri za utekelezaji, zitakazo wawezesha wananchi wenyewe kuendesha na kufanya shughuli hizo.

Rais Karume ambaye ni mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya CCM, alisema sera za CCM ni kuwasaidia wananchi kuendesha maisha yao na kuongeza kipato chao na kuishi maisha bora zaidi.

Aliwaeleza wananchi kuwa wasikubali kunyimwa uhuru wao, lazima wajisikie wako huru na kufanya maamuzi yao kwa nafasi na uwazi.

"...hata siku moja msikubali ule uhuru wa kubanwabanwa, hapana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitakubali hayo... na siku zote mtu anayependa uhuru wake siku zote ataheshimu uhuru wa mwenziwe," alisema Rais Karume.

Rais Karume alisema: “nchi haiwezi kujengwa kwa siku mia moja... sasa wenzetu mahodari wa kuuza maneno na mahodari wa kutembeza sera hewa zisizotekelezeka, wanatupa maneno tu na maneno yao wanapoyatupa kwanza wanaanza kuponda kile kilichopo, wao chao hakipo, ili kuwadanganya wenye akili ndogo kwa kutegemea kwamba watawafuata kwa kutegemea hicho kikubwa ambacho hakipo.”

Rais Karume aliendelea kueleza kuwa CUF inadai eti ikipewa madaraka watajenga viwanda vikubwa vya thamani, na kuhoji serikali itakuwa na wakati wa kujenga viwanda, kujenga na kuendesha maduka, kujenga mitandao ya biashara? Wakati huo upo, alihoji.

Aliwataka wananchi wasikubali wakati huo wa kuhodhi kurejea tena kwa sababu kujenga viwanda, kujenga maduka na kuendesha biashara hiyo si kazi ya serikali, hizo ni kazi za wananchi wenyewe.

"Eti watajenga viwanda vikubwa, kwanza uwezo huo wataupata wapi," alisema Rais Karume na kuongeza: “msidanganyike na sera ambazo anazo mtu mmoja kichwani... wakati wa kudanganywa umekwisha," alieleza.

Rais Karume alisisitiza kuwa wananchi wasikubali kudanganywa kuwa serikali ya upinzani itaweza kufanya kila kitu.

Alisema kazi ya serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kisera na kiuchumi ili kuwajengea wananchi uwezo kujiendeleza wenyewe.

"Tunataka kuwapa wananchi wetu uwezo wa kufanya kazi na kujiendeleza wao wenyewe kwa kuweza kufanya kazi ili waondokane na tatizo la umasikini," aliongeza Rais Karume.

Katika sherehe hiyo Rais Karume alikabidhi bila malipo vifaa vya uvuvi kwa wavuvi kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja. Vifaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 343.6 vimejumuisha mishipi, boti 28 na injini zake zenye nguvu ya HP 40, kamba, maboya, madema na nyavu.

Boti hizo zitawasaidia wavuvi kuweza kuvua katika bahari kuu. Utoaji wa vifaa hivyo unatarajiwa kuendelezwa kisiwani Pemba hivi karibuni.

Lengo la msaada huo ni kuwasaidia wavuvi kuendesha maisha yao na hatimaye kuondokana na umasikini, sambamba na utekelezaji wa mpango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wa kupunguza umasikini uliozinduliwa mnamo Mei 2002.

 

 

CCM Mtwara yataka wapinzani wadhibitiwe

Na Rashid Mussa, Masasi

WANA-CCM mkoani Mtwara wametakiwa kutowapuza wapinzani wanaoendesha fujo za kihuni na badala yake wadhibitiwe kwa kukamatwa na kuwafikisha katika vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Katibu wa CCM mkoa, Anna Magowa alitoa wito huo juzi wilayani hapa akiwa katika ziara ya ufuatiliaji wa kampeni ya Chama zinazoendelea vizuri katika majimbo yote matatu na kuwakatisha tama wapinzani ya kuokota hata kiti kimoja cha udiwani.

Katika ziara hiyo aliambiwa kuwa katika baadhi ya vijiji na maeneo ya mji wa Masasi wana-CCM wamekuwa wakifanyiwa fujo za kutukanwa, kuzomewa na hata kupigwa.

Alitaka vijana wa CCM kwa kushirisha serikali za vijiji na mitaa kuzidhibiti fujo hizo mara zinapojitokeza ili kuepuka kuvunjika kwa amani na kujenga hofu kwa wananchi inayoweza kuathiri kampeni na hasa siku ya kupiga kura.

Alisema kaitka kuwadhibiti vijana hao, vijana wa CCM wasiwajibu kwa staili ya jino kwa jino na badala yake watumie serikali ya vijiji na mitaa kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria, pia wakurugenzi wa uchaguzi wilaya wapewe taarifa za matukio hayo.

Alisema katika kutapatapa, wapinzani baada ya kukosa watu katika mikutano yao sasa wanawarubuni vijana wachache kufanya vitendo hivyo kwa kuwabughi wananchi hasa wanawake.

Wiki iliyopita katibu huyo alitembelea wilayani hapa kuwafariji wakiwa wa mkereketwa mmoja wa CCM aliyeuwawa kwa ugomvi unaoaminika kuwa ni wa kisiasa.

Nae mwenyekiti wa umoja wa vijana wa CCM wa wilaya ya Shaibu Nemanga alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza la vijana la wilaya kuwa vijana wahuni wanaoonekana kuandaliwa na wapinzani wamekuwa wakiwazomea, kuwatukana na hata kuwapiga watu waliovaa sare za CCM wakipita maeneo mbalimbali, likiwemo la soko kuu la wilaya lililopo Mkuti mjini hapa pia misafara ya kampeni katika baadhi ya vijiji.

Katibu mwenyewe wa mkoa juzi alilazimika kusimamisha ghafla msafara wa kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Nanyumbu, Dunstan Mkapa katika kijiji cha Mkuula Nenyumbu baada ya kuzomewa na kutupiwa mawe na vijana waliokuwa wamekaa mahali ilipokuwa imetundikwa bendera ya CUF.

Kwa kushirikisha uongozi wa serikali ya kijiji hicho vijana hao walishughulikiwa kikamilifu kwa kukamatwa na kufikishwa kwa afisa mtendaji wa kijiji kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kosa la kuleta fujo katika msafara huo ambao zilihatarisha usalama wa malil na maisha ya watu.