UHURU 30.09.2005
KIKWETE AWAONYA WATANZANIA: Amani si hulka, ni misingi ya waasisi
Asema wao ndiyo walioijenga, ikichezewa itavunjika
CUF yakimbiwa na wanachama wake zaidi ya 2,600
Na Bakari Mnkondo, Mkinga
MGOMBEA wa Urais Kupitia CCM Jakaya Kikwete amesema amani na utulivu wa Tanzania hautokani na hulka ya Watanzania bali unatokana na misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa TANU na ASP na hatimaye CCM waliosisitiza umoja na mshikamano wa kitaifa.
Kikwete alisema hayo jana alipohutubia mkutano wa kampeni uwanja wa Moa wilayani Mkinga mkoa wa Tanga ambako umati mkubwa wa wananchi ulifurika kumsikiliza.
Alisema wapo baadhi ya wapinzani wanaokebehi kwamba amani na utulivu uliopo nchini ndiyo asili ya Watanzania, jambo ambalo siyo kweli, na kwamba ikichezewa inaweza kuvunjika.
Alisema kama viongozi wa CCM tangu mwanzo wangeendekeza ubaguzi wa rangi, ukabila, chuki kati ya kabila na kabila au hata chuki za rangi nchi ingejaa vurugu.
Mgombea huyo aliwahakikishia wakazi wa wilaya ya Mkinga na mkoa wa Tanga kwa jumla kwamba amani na utulivu uliopo unaweza kuvurugika wakati wowote ikiwa vyama vya upinzani vitaendelea kufanya kampeni za chuki na kuhamasisha vijana kufanya fujo.
Aliwasihi Watanzania wote kuwachagua wagombea wote wa udiwani, ubunge wa CCM akiwemo yeye anayewania Urais ili nchi iendelee kuwa ya amani na utulivu.
‘’CCM inapenda amani, utulivu na mshikamano, ndiyo maana inao wazee ambao wanaweza kuwakanya vijana wake wanaopotoka, wana uwezo wa kuwaonya vijana wake wanaokosea,’’ alisema na kuongeza kwamba vyama vya upinzani havina utaratibu huo.
Kikwete ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliwasihi Watanzania kuhakikisha wanawachagua wagombea wote wa CCM Oktoba 30, mwaka huu.
“CCM inaahidi inachotenda na inatenda ilichoahidi,’’ alisema na kuongeza kwamba serikali ya CCM imedhamiria kuboresha elimu, maji, barabara, kuongeza ajira, kuondoa matatizo ya wavuvi na kulinda amani na usalama wa Taifa.
Wakati huohuo, Watanzania wametakiwa kuwa macho na chama cha CUF kwa ahadi zake za kuboresha maisha ya Zanzibar kwa muda wa siku 100.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Salum Msabaha ambaye aliwahi kuwa Mwanachama wa CUF huko Zanzibar akiwa na kadi namba 150.
Alisema CUF kwa kawaida iliundwa kwa dhamira ya upinzani Zanzibar pekee yake ikisaidiwa na watu wa nje ambao tayari wanaahidi kurudi kuitawala Zanzibar tena.
“Ndugu zangu, nawaambieni mtambue kwamba mwana CCM mmoja ni bora kuliko wanachama 10 wa upinzani,’’ alisema.
Wakati huo huo, ngome ya CUF mkoani Tanga juzi na jana ilivunjwa baada ya wanachama wa vyama vya upinzani zaidi ya 4,700 wakiwemo 2,605 wa tawi la CUF lililofunguliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuhamia CCM wakati wa ziara ya Mgombea wa Urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete.
Wimbi la kuvikimbia vyama vyao lilianza juzi ambapo wanachama 2,174 wa vyama mbalimbali vya upinzani walipovikimbia vyama vyao na kurudi CCM na kuahidi kukipigia kampeni na kura za wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba 30, mwaka huu.
Kikwete aliwakabidhi kati za CCM baada ya kuwapokea na kutoa sababu za kuhama kwao kutoka CUF, TLP, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI na TADEA.
Huko Pangani juzi, Kikwete aliwapokea wanachama wapya zaidi ya 1,000 wakiwemo wa vikundi vya hamasa vya CUF vilikuwa vikitumbuiza muziki wa kizazi kipya kwenye kampeni za CUF.
Akiwa Korogwe, Kikwete alifanikiwa kulipokea tawi lote la CUF la Korogwe Mjini ambalo lilifunguliwa mwaka 2000 na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba.
Wanachama 606 wa tawi hilo namba 59 walisema waliamua kuachana na chama hicho kutokana na kueneza falsafa za ‘mapanga shasha shaa’ ambazo kimsingi zinaongeza chuki katika jamii.
Mgombea wa CCM aliteremsha bendera ya CUF na kupandisha bendera ya CCM kwenye tawi hilo ambalo lilibadili jina na kuitwa tawi la Kikwete wa CCM.
Akiwa Wilaya ya Mkinga jana, Kikwete aliwapokea wanachama wapya 2,006 ambao walisema wanavikimbia vyama vyao baada ya kugundua ukweli kwamba havina mwelekeo wa kuiongoza Tanzania.
Vyama vilivyopoteza wanachama hao ni CUF ya wanachama 383, CHADEMA (167), UMD (260), UDP (292), NCCR-MAGEUZI (252), na TADEA iliyopoteza wanachama 104.
Vyama vingine vilivyopoteza wanchama ni TLP wanachama 227, PPT wanachama 140 na SAU wanachama 160.
Mgombea wa CCM leo anaendelea na kampeni mkoa wa Kilimanjaro.
Na Yassin Kayombo, Simanjiro
MGOMBEA mwenza wa Urais kwa tiketi ya Dk. Ali Mohamed Sheni amesema endapo CCM itachaguliwa kuunda serikali itahakikisha uchumi unakuwa kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2010 kutoka asilimia 5.6 ya sasa.
Uchumi huo utakuwa kutokana na mkakati uliowekwa na CCM wa kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wakulima na wafugaji ili shughuli zao ziwe za kisasa zitakazowapatia tija kubwa tofauti na ilivyo hivi sasa.
Dk. Sheni aliyasema hayo alipohutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Mwenge mjini Orkesumet, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara juzi na kufafanua kuwa wakulima watapatiwa mafuzo ya ukulima wa kisasa wa mazao
husika kaika maeneo yao ili wavune mazao mengi zaidi na yaliyobora.
Aliema kwa upande wa wafugaji pia wataalamu watasambazwa katika maeneo ya wafugaji na kutoa mafuzo kuhusu ufugaji bora utakaozingatia kuzingatia idadi ya mifugo na lishe bora ya mifugo hiyo.
Katik ziara hiyo anayofuatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuuu ya CCM, Grace Soka ambaye pia mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Uaratibu wa kampeni za CCM kanda ya Kaskazini, Dk. Sheni alisema serikali za CCM zitahakikisha shughuli za kilimo na ufugaji zinaendeshwa kisayansi zaidi.
Sambamba na utoaji wa mafunzo ya kilimo na ufugaji ka wananchi, serikali ya CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo itahakikisha viwanda vya mbolea vinafufuliwa na inasambazawa kwa wakulima kwa wakati muafaka na
kwa bei nafuu ambapo serikali itandeleza kutoa ruzuk kwenye pembejeo za kilmo ikiwemo mbolea.
Dk. Sheni alisema serikali za CCM pia zinahakikisha inahamasisha ujenzi wa viwanda vidogo vidogo na vya kati vya kusindika mazao ya kilmo na mifugo ili kuongeza thamani yake katika soko la ndani na nje.
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali za CCM zitaendelea na jitihada zake za kuboresha maisha kwa wananchi wote bila kujali tofauti zao za iikadi za siasa,dini, jimbo na jinsia kwa kuboresha huduma za jamii zikiwemo miundombinu, afya, maji, elimu na umeme.
Mgombea mwenza aliwataka Watanzania kupuuza maneno yanayotolewa na viongozi wa vyama vya upinzani kuwa CCM haijafanya llote la maendeleo kwa wananchi katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 44 uongozi wake.
Dk. Sheni alisema serikali za CCM zimefanya mambo makubwa ya maendeleo kwa wananchi wake wakiwemo viongozi hao w vyama vya upinzani ambao wamefikia viwango vya elimu walivyonavyo kwa kusomeshwa bure na serikali za CCM katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.
Aliwataka Watanzania wawasikilize na kuwaadhibu kutokana na siasa zao za hadaa viongozi hao wa vyama vya upinzani ambao ni wababaishaji kwa kuwanyima kura katika uchaguzi mkuu Oktoba 30, mwaka huu.
Baadaye, Dk. Sheni na msafara wake walikwenda katika Kijiji cha Naberera nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Erasto Losioki na kuweka shada la maua kwenye kaburi lake. Losioki alifariki
dunia Agosti 26, mwaka huu Kabla ya kuwasalimia wananchi katika Vijiji vya Terrat, Komolo na Hamalulu.
Watanzania wanaoishi nje wahakikishiwa pasi mpya
Na Maura Mwingira, The Hague, Uholanzi
MKURUGENZI wa Idara ya Uhamiaji, Kinemo Kihomano amewahakikishia Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuwa serikali itafanya haraka kuwapatia pasipoti mpya.
Alitoa ahadi hiyo juzi wakati alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na Watanzania wanaoishi katika nchi za Uholanzi na Ubelgiji, ambao walifika The Hague kusalimiana na kuagana na Rais Benjamin Mkapa.
Katika mazungumzo hayo, Watanzania hao ambao wengi wao walikuwa ni wanafunzi na wachahce wakiwa ni wafanyakazi, walisema kuwa ucheleweshwaji wa pasi mpya unawafanya kuishi katika mazingira ya wasiwasi, kwa kuwa wenyeji wao wanatishia kuwafukuza wasipokuwa na pasi mpya.
Kihomano alisema kuwa si nia ya serikali kuchelewesha pasipoti hizo, isipokuwa ucheleweshaji huo umetokana na maombi mengi ya wananchi wanaotaka kuwa na pasi hiyo.
Alisema kuwa Idara ya Uhamiaji inarudia tena kuwaomba wananchi ambao hawana mahitaji ya haraka na pasipoti hizo kusubiri kwanza ili kipaumbele kitolewe kwa wananchi walioko nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanahitaji pasipoti hizo kwa kuwa ndio kitambulisho halali kinachowezesha kuendesha shughuli zao kaitka nchi wanazoishi na serikali inalitambua hilo.
Wakati huo huo, Serikali imesema kuwa itafikiria upya kuhusu kuufungua tena ubalozi wake nchi Uholanzi, baada ya kufungwa mwaka 1994 kutokana na matatizo mbalimbali mengi yakiwa ni ya uchumi.
Kauli hiyoilitolewa na Rais Mkapa wakati alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa Watanzania hao, ambao baadhi yao waliiomba serikali kuangalia upya suala la kuwa na ubaozi nchini humo.
Walisisitiza kuwa kuna kila sababu ya kuwa na ubalozi wa Tanzania nchini hapa, hasa kwa kuzignatia uhusiano mzuri uliopo katika ya nchi hizo mbili na watu wake.
Hivi sasa Watanzania wanaoishi na kuendesha shughuli zao nchini hapa wanahudumiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.
Mangula kuzindua kampeni za uchaguzi jimboni Kibaha leo
Na Selina Wilson, Kibaha
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Phillip Mangula anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu jimbo la Kibaha Mjini kesho.
Katika uzinduzi huo, Mangula anatarajiwa kupokea na kugawa kadi kwa wanachama wapya zaidi ya 200 na kuwapokea wanachama lukuki kutoka vyama vya upinzani wanaorejea CCM.
Katibu wa CCM wilayani Kibaha, Verena Shumbusho alisema shughuli hiyo ya uzinduzi wa kampeni itafanyika katika viwanja vya Maili Moja mjini hapa kuanzia saa tatu asubuhi.
Alisema Mangula anatarajiwa kuwasili mjini Kibaha saa tano asubuhi na kuelekea katika viwanja hivyo ambako atapokewa na wananchi na viongozi wa CCM mkoa na wilaya.
Verena alisema katika uzinduzi huo wa kampeni Mangula atawanadi wagombea wa nafasi ya Urais Jakaya Kikwete, Ubunge jimbo la Kibaha mjini Dk. Zainab Gama.
Aidha, Katibu mkuu huyo wa CCM pia atawanadi wana-CCM wanaowania nafasi za udiwani wa kata nane za wa Chama cha Mapinduzi katika jimbo hilo.
Viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi wa ngazi ya mkoa na wilaya wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo wa kampeni za uchaguzi utakaopambwa na burudani za aina yake.
Jimbo la Kibaha mjini lina kata nane ambazo ni Tumbi, Maili Moja, Kongowe, Kibaha, Misugusugu, Visiga, Pangani na Mkuza.
Mgombea asema ubinafsishaji ni chanzo kikubwa cha ajira
Na Prosper Kulita, Morogoro
SERA ya kubinafsisha mashirika ya umma imeelezwa kuwa ni moja ya chanzo kikubwa cha ajira katika sekta isiyo rasmi ambayo imemuongezea mwananchi kipato kinachompunguzia umaskini.
Mgombea ubunge wa jimbo la Morogoro Mjini kwa tiketi ya CCM, Dk. Omar Mzeru aliyasema hayo juzi wakati wa kampeni za ubunge na udiwani katika kata ya Mji Mpya manispaa ya Morogoro.
Dk. Mzeru alisema sera hiyo ambayo imeweza kuyafufua mashirika mengi ya umma ambayo yalikuwa yamekufa imewezesha vijana wengi waliokuwa hawana ajira kujipatia ajira ambazo huwaongezea kipato na kujiondoa katika lindi kubwa la umaskini.
Alisema changamoto iliyopo mbele ni kumkwamua mwananchi kutoka katika lindi la umaskini, hivyo mkakati wa serikali ya CCM ni kuona kuwa kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi anakuwa na kazi ambayo itamuingizia kipato ambacho kitamsaidia katika kujikimu maisha yake ya kila siku.
Akielezea mkakati wa kupunguza na kuondoa umaskini chini ya serikali ya awamu ya tatu, mgombea alisema moja ya mambo ambayo serikali iliyoyaona ni kuhamasisha wananchi kujikita katika sekta ya ajira ya mfumo usio rasmi ambayo kwa sasa ndiyo mkombozi wa wananchi.
Dk. Mzeru alisema kutokana na kutambua hilo na kutokana na uhaba wa nafasi za ajira katika mfumo rasmi, serikali ya CCM imeona ibebe jukumu la kuihamasisha sekta isiyo rasmi ili iweze kumkomboa mwananchi kwa kumuinua kimaisha.
Alisema sera ya vyama vya upinzani ya kuwalaghai Watanzania kuwa watapata ajira katika mfumo rasmi ni propaganda ambayo wananchi wanatakiwa waipuuze kutokana na ukweli serikali ya nchi yeyote haiwezi kuajiri wananchi wote katika vitengo vyake mbalimbali.
Naye Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM mkoa wa Morogoro, Aluu Segamba alisema kutokana na kutambua umuhimu wa kila mwananchi kuwa na kipato kitakachomsaidia kimaisha, CCM itatoa kipaumbele katika miradi mbalimbali ya maendeleo wakati wa uongozi wake wa awamu ya nne.
Msome awataka wana-CCM kuwa macho na wapinzani
Hasa wanaofika kwenye mikutano ya kampeni ili kuwakataa wagombea
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
KATIBU wa Organaizesheni wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Jackson Msome amewataka wanachama wa CCM kuwa macho na vikundi vya upinzani vinavyofika kwenye mikutano ya kampeni za CCM na kuwakataa wagombea wa ubunge kwa lengo la kumkatisha tamaa mgombea Urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
Msome alitoa wito huo hivi karibuni alipozungumza na viongozi wa CCM wa mkoa wa Shinyanga, mabalozi na Wazee wa wilaya ya Shinyanga Mjini wakati wa mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Rehema mjini hapa.
Alisema uchunguzi wa awali umegundua kwamba baadhi ya vyama vya upinzani vinatuma vijana wao kwenda kufanya fujo kwenye mikutano ya kampeni za Urais za CCM zinazoongozwa na Mgombea wake, Kikwete.
Alisema CCM imegundua njama hizo na kwamba kinachotakiwa ni kwa wana-CCM wote kuwa macho na vijana hao wanaofika kuvuruga mikutano kwa mbinu za kuwakataa wagombea, hususan wa nafasi za ubunge.
“Hakuna eneo ambalo mgombea wa upinzani atashinda bila ya kusaidiwa na wanachama wa CCM,” alisema na kuwataka Wana CCM kuachana na vitendo vya kutumiwa na wapinzani kwa vile kufanya hivyo ni kuwapigia kampeni wapinzani.
Msome aliwataka wana-CCM kushikamana katika kipindi hiki cha kampeni hadi uchaguzi mkuu na kusahau kabisa tofauti zao za kipindi cha mchakato wa kura za maoni ili kuzishinda hila za vyama vya upinzani.
Alisema CCM ina imani na wagombea wote walioteuliwa kuwania udiwani, ubunge na hata Mgombea wa Urais na kwamba ni jukumu la kila mmoja na mwana-CCM kutambua hilo na kuwatetea kwa udi na uvumba.
“Viongozi wa CCM pia hawana budi kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza vitambulisho vya kupigia kura ili wasidanganywe na watu wanaopita kutaka kununua na kuwanyima haki ya kupiga kura,’’ alisema.
Msome alisema vyombo vya dola vinawafuatilia kwa karibu watu wanaonunua au kuuza vitambulisho hivyo na kwamba wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.