Vyama vya kuweka fedha na kukopa vimeaminiwa na wananchi na kuongeza wanachama maradufu
KIPINDI cha miaka kumi ya serikali ya awamu ya tatu kimeshuhudia imani ya wananchi ikiongezeka katika kuanzisha na kujiunga na vyama vya ushirika, hasa vya kuweka fedha na kukopa. Makala hii inaeleza juu ya kupanuka kwa sekta hiyo na wananchi walivyonufaika.
ILANI ya CCM katika kipindi cha 2000-2005 iliweka malengo yaliyokusudia kuimarisha na kuendeleza ushirika kama njia ya kumwezesha Mtanzania wa kawaida hupambana na umaskini. Katika utekelezaji, hatua kadhaa zilichukuliwa na mafanikio kupatikana kama ifuatavyo:-
Serikali ilibadilisha Sera ya Ushirika ya mwaka 1997 na kuifanyia marekebisho Sheria ya Ushirika ya mwaka 1991 ili kuzifanya shughuli za ushirika ziendane na mabadiliko katika uendeshaji uchumi wa soko. Sera ya Maendeleo ya Ushirika ilitungwa mwaka 2002 na Sheria Mpya Vyama vya Ushirika ilitungwa upya mwaka 2003.
Wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimba madini wadogo wadogo wameanza kuingia katika utaratibu wa kuanzisha vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS).
Vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa vimeongezeka kutoka 803 mwaka 2000 hadi 1,719 mwaka 2004, sawa na ongezeko la asilimia 114.1
Baadhi ya mikoa na wilaya imeanzisha benki za ushirika, zikiwemo Kagera Farmers Cooperative Bank, Kilimanajro Cooperative Bank na benki za wananchi za Dar es Salaam Community Bank na Mufindi Community Bank.
Hisa na akiba za wananchama zimeongezeka kutoka sh. bilioni 14.04 mwaka 2000 hadi sh. bilioni 42.98, sawa na ongezeko la asilimia 200.6.
Wanachama wa vyama vya ushirika wa akiba na mikopo wameongezeka kutoka 133,134 mwaka 2000 hadi wanachama 251,631 mwaka 2004 sawa na ongezeko la asilimia 89.
Mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka sh. bilioni 11.52 mwaka 2000 hadi sh. bilioni 54.14 mwaka 2004, sawa na asilimia 370.
Umeanzishwa utaratibu wa kutoa dhamana ya mikopo kwa vyama ushirika (na wafanyabiashara binafsi ili kununulia mazao. Dhamana hiyo imevisaidia sana vyama vya ushirika kununua mazao ya wakulima katika ushindani na kampuni binafsi. Wanachama wameanza tena kuwa na imani na vyama vyao vya ushirika. Bila ya utaratibu huo baadhi ya vyama vya ushirika vingekufa.
Vyama vya ushirika vimeruhusiwa kuuza moja ka moja mazao ya wanachama wake nje ya nchi.
Vyama vya ushirika vimepewa uwezo wa kuwashitaki moja kwa moja wanaosababisha wizi na ubadhirifu katika ushirika.
Chuo cha Ushirika Moshi kimepandishwa hadhi na kuwa Chuo Kikuu Kishiriki (cha Chuo Kikuu cha kilimo cha Sokoine).
Maendeleo ya Masoko
Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza soko la ndani na la nje kwa kupitia mikataba na makubaliano mbali mbali. Jitihada kubwa zimefanywa katika kuwaelimisha wakulima kuzalisha mazao kibiashara, na hasa kuzingatia mahitaji ya soko, hususan ubora, madaraja na ufungashaji. Katika kipindi cha 2000/2001 – 2004/2005, Tanzania imejipatia mafanikio kutokana na kuongezeka kwa uuzaji wa mazao yaliyomo katika makubaliano hayo. Tanzania ni mwanachama katika mikataba na makubaliano kama vile:-
Soko la Amerika kwa mujibu wa ‘African Growth and Opportunity Act” – AGOA
Jumuiya ya Ulaya (EU) chini ya utaratibu wa “Every thin But Arms (EBA)”.
Upendeleo maalum unaotolewa na baadhi ya nchi marafiki
Jumuia ya Afrika Mashariki.
Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Ununuzi na mauzo yanayofanywa na kampuni zinazosafirisha mazao ya biashara asilia kama kahawa, chai, tumbaku, mkonge na pamba umekuwa ukiongezeka katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, isipokuwa zao la pamba. Katika kipindi cha 1995 hadi 2000, uzalishaji wa zao la pamba ulishuka kwa asilimia 14. hata hivyo, katika kipindi cha 2000 hadi 2004, zao hilo pamoja na tumbaku yameonekana kuongezeka zaidi kuliko mazao mengine.
Matatizo yanayoendelea kuathiri uzalishaji usiwe mkubwa zaidi ni pamoja na kutegemea zaidi mvua, mabadiliko ya hali ya hewa (hasa ukame), uduni wa miundombinu ya masoko ambayo imekuwa ikiongeza gharama za usafirisaji, upungufu wa taarifa za mahitaji ya masoko, hasa ya nje, upungufu wa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje.
Katika jitihada za kupunguza matatizo na kuongeza ufanisi, hatua zifuatazo, miongoni mwa nyingine, zilichukuliwa katika kipindi kilichopita.
Kuendelea na maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane).
Kuwashirikisha wazalishaji katika maonyesho ya kimataifa kama ya mboga na matunda mjini Rostock, Ujerumani (2003/2004) na Maonyesho ya Mazao ya Chakula Moscow (2004/2005). Maonyesho ya Rostock yameanza kuwanufaisha wakulima wadogo wadogo kwa kuingia mikataba ya kuziuzia kampuni kubwa ambazo zinashughulikia biashara ya kimataifa.
Kuanzishwa kwa mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Masoko Vijijini. Mradi huu unatekelezwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa lengo la kuwa na soko la uhakika la mazao yanayozalishwa na wakulima. Mradi huu unatekelezwa katika Wilaya za Kongwa na Mvomero.
Kuanzishwa kwa Programu ya Kuendeleza Mifumo ya Masoko ya Mazao ya Kilimo. Moja ya malengo ya programu hii ni kuimarisha miundombinu ya masoko vijijini, hasa barabara na maghala ili kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, hivyo bidhaa zetu kuweza kushindana na bidhaa kutoka sehemu yoyote duniani.
Kuandaa Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo yenye mwelekeo wa kuwaunganisha wazalishaji wakubwa na wadogo kwa upande mmoja, na wanunuzi/wasindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa upande mwingine, kwa lengo la kupata soko la uhakika na bei nzuri.