Wajibu wa NGO, taasisi za dini katika uchaguzi

UCHAGUZI katika nchi yoyote ni hatua muhimu kwa utekelezaji wa demokrasia. Ufanikishaji wake huhusisha wadau mbalimbali zikiwemo asasi zisizo za kiserikali (NGO) na taasisi za dini. Pamoja na asasi na taasisi hizo kuwa wadau, hata hivyo, hazitakiwi kufungamana wala kujihusisha na masuala ya kisiasa kama anavyoainisha Mwandishi Wetu EPSON LUHWAGO katika makala hii.

MASHIRIKA ya kijamii na asasi zisizo za kiserikali zina wajibu na umuhimu wake katika maendeleo ya kijamii ikiwa ni pamoja na uchaguzi mkuu wa nchi katika kuwapata viongozi bora watakaoongoza wananchi kufikia malengo yaliyopangwa.

Mashirika ya kijamii yanayozungumziwa katika makala hii ni vyama vya kidini kama vile Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).

Mbali na vyombo vya kidini, mashirika hayo ni pamoja na vyama huru vya wafanyakazi na vya kitaaluma ambavyo huanzishwa na makundi mbalimbali ya wasomi wa kada mbalimbali kwa nia ya kutetea maslahi yao.

Mbali na mashirika ya kijamii, kundi hili pia linaunganisha asasi zisizo za kiserikali (NGOs) ambazo hushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya jamii.

Asasi hizi hushughulikia masuala kama vile elimu ya uraia, ukimwi, afya, watoto yatima na wa mitaani na mengine mengi.

Zipo zingine ambazo hujishughulisha na utetezi wa maslahi ya watu, hususan haki za binadamu, usawa wa jinsi, misaada ya kisheria na mazingira.

NGOs na mashirika ya kijamii ni asasi ambazo hazina ufungamano wowote na chama chochote cha kisiasa licha ya kwamba yanaweza kufanya kazi zinazohusiana na siasa. Kwa maneno mengine, mashirika haya hayafungamani na chama chochote cha kisiasa.

HAKI, USAWA NA MAENDELEO

Kazi kubwa ya mashirika ya kijamii na NGOs ni kuhamasisha na kuharakisha maendeleo ya taifa na watu wake. Wakati mwingine huwa ni kichocheo katika kuzonga na kuzengea ili kuwezesha vyombo vya utungaji sheria kupitisha sheria au sera inayotakiwa.

Mfano mzuri katika hili ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), ambapo mwaka 1999 kilisimama kidete kuhakikisha sheria ya makosa ya kujamiiana inapitishwa na inafanya kazi barabara.

Tangu kuanzishwa kwa sheria hiyo, watu wanaopatikana na makosa ya kujamiiana kama vile kulawiti na kunajisi watoto na wanawake wanahukumiwa vifungo vya maisha jela.

NGOs na asasi za kijamii, kwa mantiki hiyo, huwa mstari wa mbele kupigania kupitishwa au kukwamishwa kwa sheria yoyote iliyo katika mchakato kwa manufaa ya jamii.

Kwa kutumia uzongaji na uzengezi, asasi hizi huwafuata watunga sera au sheria kuhakikisha kuwa sera na sheria hizo zinapitishwa kwa kufuata maslahi ya jamii husika.

Asasi zinazoshughulikia watu wenye ulemavu, mathalan, hupigania maslahi yanayohusu watu wenye ulemavu ili kuwezesha kupata haki zao zikiwa ni pamoja na za uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi.

Hivi sasa, kutokana na janga kubwa la ukimwi, zipo asasi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanapata huduma stahiki kama vile lishe bora, dawa za kurefusha maisha na kushirikishwa katika masuala ya maendeleo badala ya kutengwa na kunyanyapaliwa.

Mashirika ya aina hiyo ni kama vile Mtandao wa Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (TANEPHA), Shirikisho la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (SHIDEPHA+) na Walio Katika Mapambano ya Ukimwi Tanzania (WAMATA).

Kwa upande wa usawa wa kijinsia, Watanzania wameshuhudia asasi kama Chama cha Wanawake Tanzania (TAMWA), Mtandao wa Wanaharakati wa Masuala ya Jinsia (FemAct) na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) zikiwa mstari wa mbele katika kupigania haki za binadamu yakiwemo makundi yaliyosahauliwa katika jamii.

TAMWA, FemAct na TGNP kwa kushirikiana na kikundi cha Uhakika wa Chakula (KIHACHA) yamekuwa yakifanya utafiti juu ya masuala ya kijamii ili kuiwezesha jamii ya Tanzania kupata huduma kwa misingi ya usawa bila ubaguzi.

Asasi hizo pia zimekuwa zikipigania kuwepo kwa mgawanyo sawa wa rasilimali kwa nia ya kupunguza umaskini miongoni mwa jamii ikiwa ni pamoja na huduma kwa watu walioathirika na wanaougua ukimwi.

Mashirika na madhehebu ya  dini kwa upande wao kazi yao ni kuwahubiria wananchi kuwa na mwenendo mwema katika maisha ili jamii iweze kuwa na amani, umoja na mshikamano.

Viongozi wa dini wakiwemo maaskofu, mashehe, mapadri, wachungaji na wengineo wanapaswa kuombea amani ili taifa wakati wote liwe katika hali shwari bila misukosuko yoyote ya vita, uhasama wa kidini au kikabila na ugomvi wa aina yoyote ambao unaweza kuhatarisha usalama wa taifa.

WAKATI WA UCHAGUZI

Wakati wa uchaguzi, NGO na taasisi za dini haziruhusiwi kabisa kufanya kampeni au kushabikia au kukiunga mkono chama chochote cha siasa.

Taasisi za dini, unapofika wakati wa uchaguzi, zinapaswa kuombea uchaguzi ili mchakato mzima ufanyike kwa amani na utulivu.

Licha ya jukumu hilo, asasi za dini zinapaswa kuwaasa waumini wao ambao ndio wadau wa uchaguzi kujitokeza kwa wingi katika kila mchakato.

Wakati wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura , kwa mfano, viongozi wa dini walikuwa wakiwahimiza wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia kujiandikisha ili kupata nafasi ya kupiga kura.

Pia, wakati wa kutafuta wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani, viongozi wa dini kupitia ibada zao walikuwa wakiomba mchakato ufanyike kwa amani na utulivu.

Kwa sasa viongozi hao hao wanawasisitiza waumini kujitokeza kuwasikiliza wagombea wa nafasi za uongozi wanaojinadi na hatimaye kupata fursa ya kuwachagua viongozi wanaoona wafaa kuwaongoza miaka mitano ijayo.

Pamoja na kuhimiza huko, viongozi wa dini zote walifanya kongamano kubwa la amani kwa ajili ya kuombea uchaguzi mkuu uwe wa amani, huru na wa haki.

Kongamano hilo lilifanyika katika viwanja vya Jangwani na baadaye kwenye Ukumbi wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) baada ya Rais Benjamin Mkapa kuwaomba waombee uchaguzi.

Rais Mkapa alitoa agizo  hilo Aprili, mwaka huu wakati wa kuwekwa Wakfu kwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Alex Malasusa. Hafla hiyo ilihudhuriwa na maaskofu wa makanisa mbalimbali pamoja na mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban bin Simba.

NGO kwa upande wake, kabla ya uchaguzi, hufanya utafiti juu ya hali na mwelekeo wa siasa nchini pamoja na kutoa elimu ya uraia kuhusu wananchi kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Asasi ya Mpango wa Utafiti wa Elimu na Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa mfano, imekuwa ikifanya utafiti juu ya hali ya siasa nchini pamoja na kura za maoni kuona mawazo ya wananchi wanapenda mtu gani anafaa kuwaongoza, hasa kwa nafasi ya urais.

Kabla ya mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM, asasi hiyo ilifanya utafiti ambao ulionyesha ni kiongozi ambaye wananchi wanaona anafaa kuwa Rais wa Tanzania.

Asasi zingine kama vile Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Kamati ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO) zimekuwa zikiangalia mwenendo wa uchaguzi kwa namna tofauri.

Licha ya kuangalia mwenendo wa uchaguzi, taasisi zingine kama TGNP na FemAct kabla ya uchaguzi zilitoa Ilani ya Uchaguzi ambayo inazungumzia masuala mbalimbali yanayopaswa kuzingatiwa katika kuwapata viongozi.

Masuala hayo ni afya, mazingira, huduma bora kwa waathirika wa ukimwi, mgawanyo wa rasilimali na ushirikishwaji wa makundi maalum kama wanawake, vijana na wenye ulemavu katika nafasi za vyombo vya kutoa maamuzi na kutunga sheria.

Si hivyo tu, katika utoaji wa elimu ya uraia, NGO zinatakiwa kuwaelekeza wananchi kupiga kura na siyo kufanya kampeni kumchagua mgombea fulani.

MAMBO KINYUME

Pamoja na mashirika ya kijamii na madhehebu ya dini kutokuwa na fungamano na vyama vya siasa, kwa maana ya kufanya kampeni au kupendelea mgombea au chama chochote, baadhi yao wamekiuka kanuni hiyo.

Mwaka 1995, mathalan, lililokuwa Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA) lilikuwa likimfanyia kampeni aliyekuwa mgombea Urais kupitia chama cha NCCR-Mageuzi (wakati) huo, Augustine Mrema.

Kufuatia kufanya kitendo hicho cha wazi wazi baraza hilo lilifutwa kutokana na kukiuka masharti yaliyolisajili na hivyo kukosa sifa ya kuwa taasisi isiyo ya kijamii. Baada ya kufungiwa BAWATA, asasi nyingi zimejifunza na hivyo kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa.               

WANADINI JE?

Zimekuwapo taarifa juu ya baadhi ya viongozi wa dini kufanya kampeni kwa baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi hasa urais katika vyama fulani.

Hivi karibuni kulikuwa na taarifa kuwa Msikiti wa Mtoro jijini Dar es Salaam, umebandika picha za wagombea wa CUF pamoja na maandishi yanayokikashifu Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwenyekiti wake, Rais Benjamin Mkapa.

Baadhi ya maneno yaliyoandikwa katika moja ya kuta za choo cha msikiti yalisomeka: "CCM inawabughudhi Waislamu", "Mkapa fala", "CUF chama dume", "Lipumba mwanaume" na mengi mengine.

Suala la msikiti huo kudaiwa kufanya kampeni kwa CUF halikuanza karibuni, kwani hata uchaguzi wa mwaka 1995 na 2000 ulituhumiwa kufanya kazi hiyo.

Wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 28 ya CCM Februari 5, mwaka huu kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba alitamka kuwa baadhi ya mashehe wa msikiti huo wanafanya kampeni kutaka kiongozi fulani awe Rais wa Tanzania.

Katika salamu zake, Makamba alisema: viongozi wa msikiti huo wamekuwa wakishinikiza kwamba mtu fulani lazima awe Rais kwa sababu ana tabia kama zao na anakubali masharti yao".

Mkoani Lindi, Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Dk. Mohammed Ali Mtopa wakati wa ziara za mgombea urais wa Chama, Jakaya kikwete na mgombea mwenza, Dk. Ali Mohamed Sheni alisema viongozi wa dini wanachana picha za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na kuwatata waumini wao kuichagua CUF kwa sababu si chama cha makafiri kama ilivyo CCM.