SAFARI ZA KAMPENI YA KIKWETE:

  • Kutoka Geita hadi Mahenge bila kulala
  • Ni zaidi ya kilometa 800 na zaidi ya saa 72
  • Imenifunza mengi nisiyoyatarajia maishani

Na Dunia Mzobora

WATU wa kale walituachia misemo mingi, ambayo leo imebaki kuwa funzo kubwa kwetu. Misemo hii unapoichunguza kwa makini, utagundua kuwa inakwenda sambamba na maisha yetu ya kila siku hapa duniani.

Moja ya misemo ya kale ambayo imebaki kuwa na mafundisho makubwa hata katika maisha ya sasa ni ule usemao: “Tembea uone”.

Kama ambavyo nimekuwa nikieleza katika makala zangu zilizopita, nilikuwa mmoja wa waandishi wa habari za uchaguzi katika kampeni, nikifuatana na mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete.

Ngwe yangu ilikuwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, yaani Tabora, Shinyanga na Mwanza pamoja na sehemu kadhaa za mkoa wa Morogoro.

SAFARI INAANZA

Tuliondoka Dar es Salaam kwa msafara wa magari matano kwenda Tabora, tukiwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali - magazeti, redio na televisheni.

Ilikuwa safari nzuri, kwani kama ujuavyo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma barabara ni nzuri kwa kuwa ni ya lami. Tulilala mjini Dodoma.

Kesho yake, yaani Oktoba 7, tulianza safari yetu kwenda Tabora kupitia barabara ya Manyoni na Itigi. Ni barabara ya vumbi, lakini inayopitika katika kipindi chote cha mwaka. Imo katika mkakati wa kuijenga kwa kiwango cha lami.

Tulifika mjini Tabora majira ya jioni na kisha kumsubiri mgombea wa CCM, Kikwete ambaye alikuwa anafika kesho yake kwa ndege akitokea jijini Dar es Salaam.

Kimsingi, tulimaliza kampeni za mikoa ya Tabora na Shinyanga kwa mafanikio makubwa, na kisha kuingia mkoani Mwanza.

Kikwete alianza kampeni za mkoa huo kwa kuhutubia jimbo la Sumve, baada ya kupokewa eneo la Malya mkoani Shinyanga, na kisha kwenda Kwimba, jimbo atokalo Naibu Waziri wa Elimu na Utamaduni, Bujiku Sakila.

Baada ya kumaliza mkutano wa kampeni katika jimbo hilo uliofanyika katika mji wa Malampaka, msafara wa Kikwete uliendelea na azma yake ya kupita maeneo mbalimbali mkoani Mwanza ambapo safari hii ulielekea wilayani Magu. Katika wilaya hiyo Kikwete alifanya mkutano wa kampeni, na ndipo tulipolala.

Asubuhi, msafara uendelea hadi Busega, jimbo linalowaniwa na Dk. Raphael Chegeni, ambako Kikwete alifanya mkutano wa kampeni. Baada ya hapo tukwenda Geita kupitia kivuko cha Busisi na Sengerema.

Kivukoni hapo, tulikuta maandamano makubwa ya vijana waliokuwa kwenye mitumbwi kama 20 hivi iliyokuwa ikipeperusha bendera za CCM. Tukio hilo lilikuwa la aina yake, kwani mbali ya kuvutia, hasa kutokana na jinsi vijana wale walivyokuwa wakipiga makasia, pia lilipendezesha macho.

Mitumbwi hiyo ilikuwa ikienda sambamba na pantoni iliyokuwa imembeba Kikwete na msafara wa wake hadi ng’ambo ya pili, ambako pia tulikuta umati mkubwa wa wananchi ukimsubiri.

Baada ya kuwasalimia, msafara huo ulielekea moja kwa moja Geita bila kusimama Sengerema. Tulikwenda hadi uwanja wa michezo ambako tulikuta umati wa watu ukisubiri, ambako alihutubia. Hiyo ilikuwa Oktoba 14.

SAFARI YA MWANZA MJINI

Alipomaliza mkutano wa kampeni hapo, tulilala na kesho yake asubuhi, tulianza safari ya kwenda Mwanza mjini kupitia Sengerema ambako Kikwete alifanya mkutano.

Mkutano huo ulipomalizika, ndipo safari ya kuelekea Mwanza ilipoanza kupitia kivuko cha Busisi hadi njia panda ya Busagara katika barabara kuu itokayo Shinyanga, tulikokuta umati mkubwa wa wananchi ukitusubiri hapo.

Mbali na mamia ya wananchi waliokuwepo hapo kumlaki Kikwete, pia kulikuwa na zaidi ya magari 100, pikipiki na baiskeli lukuki.

Tuliondoka njia panda ya Busagara saa 6.30 mchana na kupita katika vitongoji vya Buhongwa, Nyegezi, Mkuyuni, Igogo hadi Soko Kuu la mjini Mwanza na kisha kuingia barabara ya Nyerere ambako kulikuwa na maelfu kwa maelfu ya wananchi wakimshangilia Kikwete.

Tulipofika Benki Kuu ya Mwanza, msafara ulisimama kidogo kwa takriban dakika 40 hivi, ili kumpa fursa mgombea kujiweka sawa kabla ya kuingia Uwanja wa CCM Kirumba ambako alihutubia mkutano mkubwa wa kampeni, ambao haujawahi kutokea katika historia ya siasa ya nchi yetu.

Msafara uliondoka eneo hilo kama saa 9.00 hivi hadi uwanja wa CCM Kirumba, ambapo njiani tulimopita kulikuwa na watu wengi kupita kiasi wakimshangilia Kikwete na msafara wake hadi ulipofika Kirumba.

TUNAINGIA CCM KIRUMBA

Nje ya uwanja wa CCM Kirumba kulikuwa na watu ambao idadi yake si rahisi kuielezea, ambao bila shaka, hao walishindwa kuingia ndani kutokana na uwanja huo wakati huo kuwa umejaa pomoni.

Tulipoingia ndani ya uwanja huo, ndipo nilipoelewa nguvu ya Chama cha Mapinduzi na mgombea wake wa nafasi ya Urais. Umati ule ndani ya uwanja huo ni ushahidi tosha kwamba uteuzi wa CCM ulikuwa sahihi.

Umati wa watu uliokuwemo ndani ya uwanja huo wa CCM Kirumba ulikuwa mkubwa kupita kiasi, kwani kwenye maeneo ya kukaa, hakukuwa hata na nafasi ya mtu kutema mate!

Katikati ya uwanja kulikuwa na umati mwingine mkubwa wa watu, ambao idadi yao inaweza kulinganishwa na ile iliyokuwemo katika nafasi ya kukaa. Kirumba ilikuwa imefurika kupita kiasi. Uwanja huo una uwezo wa kuchukua watu 45,000 kwa kukaa vitini.

AVAMIWA JUKWAANI

Hata hivyo, msafara wa Kikwete baada ya kuzunguka uwanjani huku akiwapungia wananchi, hatimaye ulifika jukwaani ambapo alishuka na kwenda kukaa kwenye jukwaa kubwa, shughuli za burudani zilianza kwa vikundi mbalimbali kuburudisha wananchi.

Walioanza kutoa burudani uwanjani hapo lilikuwa kundi la Wanaume (TMK Wanaume) chini ya kiongozi wao, Sir Juma Nature, kisha Rutta Bushoke na K-Lyn, Vicky Kamata na kisha Tanzania One Threate (TOT Plus).

Baada ya tukio hilo, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Mujuni Kataraia aliwakaribisha viongozi mbalimbali wa ngazi ya juu wa CCM kutoa salamu zao kwa wananchi na wana-CCM uwanjani hapo.

Miongoni mwa waliosalimia ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa (Bara), John Malecela, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula.

Kataraia pia aliwatambulisha viongozi wengine wa CCM, wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, wakiwemo Waziri Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Katibu wa Fedha na Uchumi wa NEC, Salome Mbatia.

Baadaye ndipo lilipofuata tendo la mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Kikwete kutawazwa kuwa Chifu wa Wasukuma.

Kikwete alishuka kutoka katika jukwaa kubwa alipokuwa ameketi na kwenda katikati ya uwanja ambako kulikuwa kumejengwa majukwaa mengine mawili, moja kwa shughuli hiyo ya kumtawaza na lingine kwa ajili ya kuhutubia.

Wakati akitoka jukwaani kwenda kwenye majukwaa hayo, Kikwete alifuatana na baadhi ya viongozi wa Chama, ambapo huko aliwakuta baadhi ya wazee wa Kisukuma waliomtawaza kuwa Chifu wa kabila hilo kubwa hapa nchini waliokuwa wamevalia migolole yenye rangi nyeusi.

Kikwete alipandishwa jukwaani na kuketishwa kwenye kigoda. Wakati shughuli hiyo ikiendelea, ndipo kijana aliyekuwa amevalia mgolole mweusi, alipomvamia Kikwete na kuukumbatia mguu wake wa kulia akitaka kumdondosha chini kutoka jukwaani alipokuwa ameketi kwenye kigoda!

Kutokana na ushupavu wake, Kikwete aliweza kujinasua kutoka mikononi mwa yule kijana, na wakati huo huo ndipo kijana huyo ‘aliposhukiwa’ na kundi la zaidi ya askari 30 waliokuwa wamezunguka jukwaa alilokuwepo Kikwete.

Kusema kweli, kitendo hicho kilitokea katika muda wa sekunde chache, kiasi kwamba wapo baadhi ya watu waliokuwemo uwanjani humo hawakujua nini kilichokuwa kimetendeka.

Kutokana na jinsi kijana yule alivyokuwa amevalia, haikuwa rahisi kwa wanausalama au kwa mtu yeyote kumshuku kwamba alikuwa amedhamiria kuleta fadhaa ile pale uwanjani.

Kijana yule, mbali na kupewa mkong’oto wa nguvu, alizolewa na kuchukuliwa juu kwa juu na askari polisi walimpakia kwenye karandinga na kumpeleka kituo kikuu cha polisi mjini Mwanza anakoendelea kuhojiwa zaidi.

Hata hivyo, baada ya tukio hilo, shughuli ziliendelea kama kawaida uwanjani hapo na baadaye Kikwete kuwahutubia wananchi katika mkutano wake huo wa kampeni.

SAFARI YA MAHENGE

Baada ya Kikwete kumaliza kuhutubia mkutano huo wa kampeni ambao rekodi yake haijawahi kutokea katika mikutano yake hapa nchini, sisi waandishi tulitakiwa kuondoka mjini Mwanza jioni ile kuelekea Mahenge wilayani Ulanga.

Kimsingi, Kikwete alikuwa hajamaliza ziara yake ya mkoa huo, kwani kesho yake asubuhi alikuwa amepangiwa kwenda wilayani Ukerewe ambako alikuwa na mkutano mwingine wa kampeni. Jimbo hilo linawaniwa na Balozi Getrude Mongella ambaye ni mgombea wa CCM.

Tuligawanywa katika makundi mawili. Moja ni la waandishi ambao wangeandamana na mgombea kwenda Ukerewe na wengine kuelekea Mahenge, ili kumpokea keshokutwa yake, yaani Oktoba 17, ambako angemalizia ‘kiporo’ cha wilaya za Ulanga na Ifakara, mkoani Morogoro.

Msafara wa magari yaliyokuwa yamepangwa kwa safari ya Mahenge yalikuwa saba, yakiwemo manne yaliyokuwa yamewabeba waandishi wa habari na wapigapicha. Safari ilianza kama saa 2.00 usiku hivi, baada ya kuwa tumepata chakula cha usiku pale Mwanza Institute.

Kwa mujibu wa mkuu wa msafara, Mzee King’wande msafara huo ulitakiwa kulala mjini Nzega, kabla ya asubuhi yake kuelekea Mahenge kupitia Igunga, Sindida hadi Mikumi. Nilikuwa kwenye gari namba T 364 AJL lililokuwa likiendeshwa na dereva aliyejulikana kwa jina moja la Ben.

Tulifika Nzega kama saa 8.00 usiku, ambako tulilala kwa wastani wa saa mbili hivi kabla ya saa 11.00 alfajiri kuanza safari ya kuelekea Mahenge kupitia Ifakara ambako tungevuka Mto Kilombero.

Ilikuwa safari ngumu, iliyohitaji uvumilivu wa hali ya juu, kwani tukiwa Nzega usiku huo wapo walioamua kutolala kabisa kwa kuhofia kwamba iwapo wangejilaza tu, basi ingekuwa vigumu kuamka!

Hata hivyo, kwa wale waliolala ilikuwa kama kuegesha mgongo kitandani na kuamka kwa msemo uliozoeleka kwa wale waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa enzi hizo! Unawezaje kulala kwa saa mbili, huku ukiwa umechoshwa na safari ya karibu saa 18!

Kulipopambazuka tu, safari ilianza na msafara ulianza kwa ari, nguvu na kasi mpya hadi Singida ambapo watu walipata chai ya asubuhi kabla ya kujipakia tena na kuendelea na safari hadi njia panda ya Kilosa eneo la Dumila tulipofika saa 11.00 hivi.

Mkuu wa msafara aliamuru kwamba safari inaendelea kwenda Mikumi kupitia njia panda hiyo, ambayo kusema kweli japokuwa barabara ilikuwa siyo mbaya, lakini kutokana na uchovu, na kwamba barabara ilikuwa ya vumbi tulijikuta tunafika Mikumi kama saa 2.30 usiku hivi.

Watu walipata chakula cha jioni hapo Mikumi na kisha kuendelea na safari hadi Ifakara, ambako tulifika saa 7.00 usiku. Ilikuwa safari ngumu, lakini yenye hamasa kubwa, huku ikifungua milango zaidi ya fahamu na jiografia.

Tuliendelea na safari hadi kivukoni, ambako tulivuka Mto Kilombero kwa pantoni saa 7.30 usiku na kisha kuelekea Mahenge, umbali wa zaidi ya Kilometa 100. Tuliitafuta Mahenge na kufika huko karibu saa 10.00 usiku.

Hata hivyo, safari ilikuwa kwenda kwenye kijiji cha Mwaya, ambako kuna uwanja mdogo wa ndege katika Hifadhi ya Taifa ya Selous, ambako Kikwete angewasili asubuhi yake akitokea Musoma mkoani Mara kupitia Dodoma.

Tulifika Mwaya asubuhi ya saa kumi na mbili, huku wenyeji wakitushangaa! Inasemekana ukiwa Selous, ni rahisi zaidi kufika katika miji ya Songea mkoani Ruvuma na Liwale mkoani Lindi.

Kadri muda ulivyokuwa ukienda ndipo wananchi wa kijiji hicho walivyokuwa wakimiminika uwanjani hapo, huku vikundi mbalimbali vya kwaya na ngoma za Umoja wa Vijana wa CCM vikiburudisha wananchi waliofika uwanjani.

Tulikaa hapo mpaka karibu saa sita mchana, ndipo ndege ndogo iliyombeba Kikwete ilipotua katika uwanja huo na shamrashamra za wananchi na wana-CCM zilipopamba moto na kisha msafara wa kuelekea Mahenge katika mji wa Ulanga zilipoanza.

Tulifika Ulanga kama saa nane hivi mchana ambako alihutubia mkutano mkubwa wa kampeni ikiwa ni pamoja na kumnadi mgombea wa jimbo hilo la Ulanga Mashariki, Celina Kombani na baadaye Ulanga Magharibi kwa Dk. Juma Ngasongwa katika mji wa Lupiro.

Baadaye tulirudi Ifakara kupitia kivukoni ambako nako alifanya mkutano wa kampeni na kumnadi mgombea wake, Castory Ligalama na baada ya hapo tukarudi Kidatu tulipoingia majira ya kama saa nne hivi usiku. Tulilala hapo.

Hiyo ndiyo safari ya waandishi wa habari za kampeni za mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete za kutoka Geita hadi Mahenge wilayani Ulanga zaidi ya Kilometa 800 na zaidi ya saa 72 bila kulala!

Kwa maneno mengine, unaweza kusema tulisafiri usiku, mchana, usiku, mchana bila kulala! Hata hivyo, ni safari niliyojifunza mengi, na kwa kweli mambo niliyoyaona sitayasahau kamwe maishani mwangu.

Pia, safari hiyo imepanua mno jiografia yangu kwa kufika maeneo na sehemu ambazo, nisingeweza kuota kuzifika katika maisha yangu, kama siyo kampeni za mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete!

Lakini kubwa zaidi, nimeshuhudia jinsi Chama cha Mapinduzi kilivyojichimbia na kuweka mizizi hadi katika maeneo ya vijijini kabisa. Ni wapi utakwenda nchini hapa ukose kuona bendera ya CCM ikiwa inapepea?

Hii inadhihirisha pia kwamba Chama Cha Mapinduzi ni Chama chenye mtandao mkubwa na wa hali ya juu, ambao kamwe wapinzani nchini wasikae na kuota ndoto za alinacha kwamba ni rahisi kuking’oa! CCM ni imara kama chuma cha pua!

 

 

IDD Azzan: Mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni anayefananishwa na Kikwete

Wengi jimboni waonyesha kuwa na imani naye

ARI mpya, Nguvu mpya na Kasi Mpya ni kaulimbinu iliyoasisiwa na Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete tangu alipotangaza kuomba ridhaa kuwania kiti hicho kwa tiketi ya CCM. Kauli hiyo hadi sasa tayari imekwishapenya masikioni mwa wananchi wengi kama si wote huku ikipewa kipaumbele pia katika kulinganishwa nayo na wagombea wa udiwani na ubunge kupima kama wana uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi.Idd Azzan ni mgombea wa Ubunge wa Kinondoni ambaye amaeonyesha kuibeba vilivyo kaulimbiu hiyo. Mwandishi GABRIEL JOHN anaeleza zaidi katika makala hii.

IDD Azzan si jina geni masikioni mwa wakazi wa Kinondoni, kwani limekuwa likivuma zaidi kwa wale wafuatiliaji wa karibu wa masuala ya michezo.

Lakini baada ya kuwika na kwa kweli kusaidia sana na kuinua medani ya michezo katika wilaya hiyo, hususan upande wa soka, Azzan sasa amejitupa katika medani ya siasa ambako bila shaka nako atafanikiwa.

Anawania ubunge katika jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa kwa upande mmoja ameiva katika kushughulikia matataizo ya wananchi, kwa kuwa inasadikiwa kuwa michezoni ni pahala ambako ni lazima mtu awe shupafu ndiyo anaweza kumudu kuiendeleza michezo.

Licha ya kuwa kiongozi wa Soka, Azzan pia ni diwani wa kata ya Magomeni ambapo wakazi wengi wa kata hiyo, wamepata maendeleo makubwa kwa kuweza kutatua matatizo yaliyokuwa yakiikabili kata hiyo.

Kukubalika kwa Azzan kunatokana na ucheshi wake alionao miongoni mwa jamii inayomzunguka, pia ni kiongozi asiye na ‘majigambo’ machoni mwa watu.

Kubwa zaidi hivi karibuni alitambulishwa kwa wananchi wa jimbo la Kinondoni katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Biafra, na mgombea Urais kupitia tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete ambapo wengi walimkubali na kumfananisha na Kikwete.

‘KIKWETE’ JUNIOR

Wakati akipanda jukwaani wananchi wengi walimshangilia kwa ‘mbwembwe’ na nyimbo mbalimbali huku wengi wakimuita ‘Kikwete junior’ kutokana na mvuto alionao kwa kufananishwa naye.

Pamoja na kumtambulishwa machoni mwa maelfu ya wananchi waliokusanyika katika mkutano huo, kama ilivyo kawaida kwa Kikwete- alimnadi kwa wananchi hao ambapo pia alimuita mdogo wake kutokana na kupendwa kwake kwa wananchi.

”Ndugu wana CCM wenzangu, nachukua nafasi hii kumtambulisha kwenu mdogo wangu, rafiki yangu wa siku nyingi, Idd Azzan anang’ara… hang’ari, naomba mpeni kura za NDIYO ili niweze kukamilisha yale niliyodhamiria...

“Azzan ninamfahamu kwa muda mrefu hata kama kutakuwa na tatizo hakuna wa kumzuia nitakapokuwa Ikulu, ataingia moja kwa moja na kunieleza matatizo ya jimbo lake,” alisema Kikwete.

Hata hivyo, katika mikutano yake ya hivi karibu aliyofanya katika maeneo mbalimbali ya Kinondoni, Azzan alisema kwamba atahakikisha wananchi wanapata maisha bora kwa kuboresha miundo mbinu iliyopo kwa kuzingatia Ilani ya CCM.

Ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi, aliongeza ni jambo la kawaida na kuwataka wapinzani wakae chonjo kwani kuongeza kuwa CCM imeshawasha taa ya ‘Kijani’ na hakuna wa kuzuia.

Pamoja na hayo, Azzan anasema kwamba tatizo la maji kwa baadhi ya maeneo ya Kinondoni yatakwishwa ambapo hadi sasa Serikali ya Chama Chama Mapindizi tayari imeshatenga fungu kwa ajili ya tatizo hilo.

Hali hiyo inatokana kuwepo kwa maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo mgombea ameahidi kukamilisha. Azzan amekuwa na nyota ya kupendwa na watu wa kila rika si kwa vijana tu bali pia wazee pamoja na kina mama kutoka maeneo mbalimbali ya Kinondoni.

UONGOZI WAKE

Suala la uongozi kwa Azzan halina mjadala kwa kuwa watu wengi wanamfahamu tangu akichochea maendeleo ya soka, hadi kuchaguliwa kuwa diwani katika kata ya Magomeni.

Mgombea huyu amekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha mandeleo kwa wakazi wake na hii inatokana kuwepo kwa misingi bora na imara ya uongozi.

Miaka mitatu iliyopita Azzan alipitishwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi alipokuwa nje ya nchi kwa shughuli zake. Hii inaonyesha ni jinsi gani anavyokubalika.

Azzan pamoja na mambo mengine, ameahidi kufanya mambo mengi makubwa ya maendeleo kwa wananchi ikiwemo uboreshaji wa zahanati, vituo vya afya, elimu na mifereji ambalo ni tatizo kubwa kwa wakazi wa Kinondoni wakati wa mvua.

Kuhusu michezo Azzan anasema atahakikisha vijana wapenda soka wanapatiwa vifaa bora vya michezo katika kuendeleza soka la ‘bongo’ ambalo litakua katika chati ndani na nje ya nchi.

“Kwa nini Tanzania isijulikane katika medani ya soka kama vipaji tanavyo, hilo linawezekana nchini mwetu, mbona Mataifa mengine ya Afrika ambayo hayakuwa na historia ya soka yanatambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kwa nini sisi tushindwe”, alihoji Azzan.

Akinguruma kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika hivi karibuni katika tawi la Kwa Biyuda, kata ya Kindoni Shamba, Dar es Salaam alitaja nchi zilizofuzu michuano ya kombe la dunia kuwa ni Angola, Togo na Ghana.

Mgombea huyu wa CCM pia, ni mwanzilishi wa timu ya Veterani (Tanzania Stars), ambayo iliiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya Kombe la Washindi barani Afrika kwa miaka miwilimfululizo 1997 hadi 1998.