YALIYOJIRI ZIARA YA MGOMBEA URAIS WA CCM 

Apewa heshima ya uchifu na kuitwa Mwene-Kikwete

MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, alifanya ziara katika mkoa wa rukwa kwa ajili ya kuomba wananchi wamchague pamoja na Chama kuendelea kuiongoza nchi. Mwandishi Wetu EPSON LUHWAGO aliyekuwa katika ziara hiyo anaelezea yaliyojiri katika ziara hiyo.

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete alifanya ziara ya kampeni katika mkoa wa Rukwa na kuwavuta wananchi wengi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Ziara ya Kikwete mkoani Rukwa ilikuwa Agosti 31 na Septemba Mosi, mwaka huu baada ya kumaliza kampeni zake kwenye mkoa wa Mbeya.

Katika mkoa wa Mbeya, kabla ya kuingia Rukwa,  alifanya mikutano katika maeneo ya Rujewa, Kyela, Mbalizi, Tukuyu, Uwanja wa Sokoine Mbeya, Mlowo, Vwawa na Tunduma.

MAPOKEZI MAKUBWA

Msafara wa mgombea katika mkoa wa Rukwa ulipokewa katika eneo la Mkutano wilayani Mbozi mkoani Mbeya ambapo viongozi wa mkoa wa Mbeya waliukabidhi kwa uongozi wa Rukwa chini ya Mwenyekiti wa Mkoa, Charles Kabanga.

Viongozi wengine waliokuwa katika mapokezi hayo ni Mjumbe Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM. Dk. Chrisant Mzindakaya; Mbunge wa Kalambo Ludovick Mwananzila; Mjumbe wa NEC na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti na viongozi wengine wa Chama na serikali.

Baada ya makabidhiano, alihutubia wananchi waliojitokeza katika eneo hilo ambapo aliwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi kwa kumlaki.

Aliwaomba wananchi kuendelea kuichagua CCM kwa vile imefanya mengi kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Pia aliahidi kuendeleza yaliyofanywa na uongozi wa serikali ya awamu ya tatu pamoja na kukuza uchumi.

Kikwete na msafara wake aliendelea na safari ya kwenda Sumbawanga kwa kupita Tunko, Miangula hadi Laela alikofanya mkutano wa kwanza wa hadhara katika mkoa wa Rukwa.

MANENO YA MATUMAINI

Katika ziara ya mkoa wa Rukwa, Kikwete alifanya mikutano ya hadhara Laela jimbo la Kwela, Matai jimbo la Kalambo na Sumbawanga Mjini kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.

Katika mikutano yote hiyo, umma wa wananchi uliohudhuria, ulikuwa na furaha kusikia maneno yanye faraja na matumaini ya kuendelea kupata neema ya maisha chini ya serikali ya awamu ya nne ya CCM.

Mgombea urais alisema lengo la serikali ijayo chini ya CCM ni kuboresha maisha ya wananchi kwa kuinua uchumi na ajira kwa vijana.

Alisema katika kilimo, mapinduzi makubwa ya sekta hiyo yatafanywa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nyenzo bora za kilimo, pembejeo na kuwepo kwa soko la uhakika la mazao.

"Wananchi wanalima kwa shida kutokana na kutokupata pembejeo kwa wakati na pia kutumia nguvu nyingi wakati tija wanayopata ni kidogo. Umefika wakati wa kubadilisha hali hii ili wananchi watumie nguvu ya damu na badala yake watumie nguvu yas mashine," alisema.

Mbali na kilimo, alisema uimarishaji wa miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara, utapewa kipaumbele kwa kuhakikisha barabara kuu ya Tunduma hadi Sumbawanga inajengwa kwa kiwango cha lami.

Alisema kazi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 200, uko katika hatua za mwisho na kwamba itajengwa kwa fedha za serikali.

Vile vile alisema licha ya barabara, serikali itafanya juhudi za kupanua bandari ya Kasanga ziwa Tanganyika ili kuwanufaisha wananchi kuuza bidhaa zao Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. 

"Mbali na kupanua bandari hii, pia barabara ya kutoka Sumbawanga hadi bandarini hapo lazima ijengwe kurahisisha usafirishaji mazao," alisema.

Mkoa wa Rukwa pia una matatizo ya maji, jambo alilosema litashughulikiwa kwa ukaribu ili kuwaondolea wananchi adha ya kuifuata huduma hiyo umbali mrefu.

MKUTANO LAELA

Mgombea alikutana na umati wa watu uliojitokeza katika tarafa ya Laela, ikiwa ni ishara ya kuingia rasmi katika shughuli za kampeni mkoani Rukwa.

Msafara wa Kikwete ulipata mapokezi yaliyotiwa nakshi na maandamano ya baiskeli na pikipiki, na bendera za Chama.

Kabla ya Laela, alikutana na umati wa watu katika kijiji cha Miangula wakiwa na mabango ambapo hakusita kuwapa neno juu ya azma yake.

Hata hivyo, wananchi hao walitoa kilio chao juu ya kuuzwa kinyemela  kwa ghala la kuhifadhia mazao. Kikwete aliwaahidi kulitafutia ufumbuzi.

Katika eneo la Laela, alipokewa na kuvishwa skafu na vijana wa chipukizi na baadaye kuzindua shina la wakereketwa wa CCM.

Wakati wa kuzindua shina la wakereketwa, aliwataka vijana kujishughulisha na uzalishaji kwa kuwa bila kufanya hivyo watakuwa wakipiga majungu  tu.

Baadaye alipanda jukwaani kusubiri muda wa kuwahutubia wananchi. Kabla ya kuhutubia alivishwa mgolole na kumpa silaha za kimila ikiwa ishara ya kukubaliwa kiuongozi.

Kufuatia kusimikwa huko, Kikwete alikaribishwa rasmi kuhutubia wananchi kwa nia ya kuomba kura ili wananchi waichague CCM iendeleze mema ya maendeleo kwa wananchi.

Alipmaliza kuhutubia, Kikwete aliendelea na safari katika maeneo mengine hadi alipofika Sumbawanga mjini kwa mapumziko ya jioni kabla ya kuendelea na ziara siku iliyofuata.

SIKU YA PILI RUKWA

Siku ya pili ya ziara ya Kikwete mkoani Rukwa ilianza kwa safari ya kwenda Matai katika jimbo la Kalambo ambako alihutubia mkutano mkubwa wa hadhara.

Kabla ya kufika huko alipita maeneo ya Matanga, Katuka, Msanzi na baadaye Singiwe. Katika kijiji cha Katuka, wanafunzi waliacha masomo na kukimbilia barabarani baada yas kusikia msafara wa mgombea unapita.

Kutokana na hali hiyo hakuacha kutoa neno ambapo aliahidi kuwa serikali ya awamu ya nne chini ya CCM, itahakikisha inaendelea kuboresha elimu ya msingi kwa kujenga nyumba za walimu.

Maneno hayo yaliwafanya wanafunzi, walimu na wananchi wengine waliofika kumshangilia na hatimaye kurejea madarasani na sehemu za kazi, baada ya msafara kuendelea na safari.

Licha ya kujitokeza kwa wingi, wananchi wa maeneo hayo katika jimbo la Kalambo walitundika kanga zenye picha za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  kando ya barabara ikiwa ishara ya kumpokea kiongozi mtarajiwa wa nchi.

KIVUMBI MATAI

Umati wa watu aliokutana nao njiani akiwa safarini kwenda Matai ulikuwa kama rasharasha kwani alipofika eneo hilo, alishangazwa na wananchi lukuki waliofika kumwona na kumsikiliza.

Wananchi kutoka sehemu mbalimbali za jimbo la Kalambo, walikuwa na shauku kubwa ya kumsikiliza Kikwete ambaye tangu kuanza kwa ziara zake za kampeni, alikuwa akivuta umati wa watu.

Kufurika kwa watu hao, kulimfanya Kikwete kupata hamasa ya 'kumwaga' sera za CCM juu ya azma ya kutaka kuendelea kuchaguliwa ili kuiongoza Tanzania kutoka katika pwani ya umaskini hadi bandari ya neema.

Aliwaelezea mambo mengi yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tatu ya CCM na yale yanayokusudiwa kufanywa katika serikali ijayo, pindi akichaguliwa kuwa jemadari wa mipango inayopangwa kuiendeleza nchi.

Baada ya mkutano wa Matai, msafara wa Kikwete  uliokuwa chini ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdulrahman Kinana na waasisi wa Chama, Peter Siyovelwa na Mustafa Songambele, ulirejea Sumbawanga.

VIFIJO SUMBAWANGA

Kikwete aliingia kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga saa 7.32 mchana, msafara wake ukiwa na zaidi ya magari 30.

Msafara huo, licha ya kuwa na viongozi wa kitaifa, mkoa na wilaya, ulihanikizwa na teksi, pikipiki na baiskeli  zilizokuwa zikisindikiza kwa nyuma.

Baada ya kufika lango kuu la uwanja, Kikwete alitokeza juu ya gari hali iliyowafanya wananchi waliofurika kulipuka furaha isiyo kifani.

Mgombea huyo, alizunguka uwanja mzima akiwapungia wananchi. Aliposhuka alipokewa kwa salamu za chipukizi na kuvishwa skafu na hatimaye kwenda kukaa.

KINANA AMPA SIFA

Kabla ya kupanda jukwaani kuhutubia, Kinana alimmwagia sifa mgombea kuwa ni hazina kwa taifa na anakubalika ndani na nje ya nchi.

Kinana katika kuelezea sifa za mgombea, alisema Kikwete viongozi wa Afrika hasa nchi jirani wamempongeza na kuonyesha dhahiri atakuwa kiungo cha maendeleo katika Umoja wa Afrika.

"Hali hii inatokana na kuwepo kwenye wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 10. Kuwepo kwa kipindi hicho kwenye wizara hii kumesababisha ayajue mengi ya ndani na nje ya nchi," alisema.

Kinana alisema akiwa katika wizara hiyo, Kikwete amekuwa kiungo muhimu baina na Tanzania na nchi zingine duniani na amesaidia kuifanya Tanzania iheshimike na mataifa mbalimbali duniani.

Baada ya sifa hizo, alikaribishwa rasmi jukwaani kuhutubia lakini kabla ya hapo alivishwa mavazi rasmi na kutawazwa kuwa chifu wa Wafipa. Kutokana na hadhi hiyo alipewa rasmi jina la Mwene-Kikwete.

Katika kupewa heshima hiyo, alivalishwa mgolole wenye rangi ya kijani na mistari mraba myekundu kwa mbali na kupewa fimbo iitwayo 'ulwazi' kwa kifipa ambayo hupewa watu wanapokabidhiwa dhamana ya uongozi.

Kazi ya kumtawaza Kikwete ikiwa ishara ya kukubalika kwake kuwa kiongozi, ilifanywa na mzee Abdallah Maufi na Mama Eva Ndwenya chini ya usimamizi wa Paul Kimiti.

AWANADI WAGOMBEA

Kikwete hakusita kuwaomba wananchi kuichagua CCM kwa mithili ya mafiga matatu ili kuendelea kushika dola. Katika staili hiyo, aliwaomba wananchi kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani wote kutoka CCM.

Katika hali hiyo aliwanadi wagombea Ubunge, Dk. Chrisant Mzindakaya (Kwela) katika mkutano wa Laela, Mwanzazila (Kalambo) kwenye mkutano wa Matai na Kimiti (Sumbawanga Mjini) uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.

Licha ya kuwanadi Mzindakaya, Mwananzila na Kimiti, Kikwete aliwanadi wagombea udiwani katika mikutano hiyo ambayo ilikuwa na mvuto wa aina yake kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuonyesha wana matumaini na CCM kuwa itaendeleza amani na utulivu kwa maendeleo.

Mbali na kuwanadi, Kikwete alimwagia sifa Kimiti kuwa ni kiongozi mzoefu na mwenye busara katika serikali na Chama.