YALIYOJIRI KAMPENI ZA MGOMBEA URAIS WA CCM

·        Kikwete aacha gumzo Mbeya

·        Apata mapokezi makubwa, wananchi 'wapagawa'

·        Vijana wafunga barabara ili awapoze kiu yao

·        Wamwambia akapumzike Urais ni wake

MGOMBEA Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, katika mkoa wa Mbeya ilidhihirisha wazi kuwa ndilo chaguo la wananchi wa Tanzania katika kushika kijiti cha uongozi wa serikali ya awamu ya nne. Makala hii ya Mwandishi Wetu EPSON LUHWAGO aliyekuwa katika ziara ya mgombea katika mkoa huo inabainisha hali hiyo.

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapindizi (CCM), Jakaya Kikwete, hivi karibuni aliuteka mkoa wa Mbeya katika ziara yake ya kampeni ya kuomba ridhaa ya kuichagua CCM iendelee kuiongoza Tanzania.

Kikwete aliingia Mbeya baada ya kuhutubia mikutano Kifanya, Njombe Mjini, makambako na Wanging'ombe wilayani Njombe mkoani Iringa akitokea mkoa wa Ruvuma.

Katika ziara hiyo iliyofanyika kuanzia Agosti 28 hadi 30, mwaka huu, Kikwete aliwafanya wananchi wa mkoa wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kumlaki na pia kumsikiliza katika mikutano yake aliyoifanya katika maeneo ya Mbarali, Kyela, Mbalizi, Tukuyu na Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Mbali na maeneo hayo, Kikwete alifanya mikutano na kuwasalimia wananchi katika maeneo ya Mlowo, Vwawa, Tunduma, Mpemba, Mpui, Myunga wilayani Mbozi akiwa njiani kwenda mkoani Rukwa.

Kwenye mikutano hiyo, maelfu ya wananchi walimiminika siyo kukata kiu tu ya kumwona, bali kumsikiliza nini anachokusudia kukifanya yeye na CCM baada ya kuingia madarakani kufuatia uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 30, mwaka huu.

MAPOKEZI MAKUBWA

Kila mahali alipofika, Kikwete alipata mapokezi makubwa hali iliyoashiria kwamba anapendwa na wananchi wana imani naye.

Dalili kwamba hali ya mapokezi ingekuwa kubwa, ilianza kujionyesha wakati wa mapokezi mpakani mwa Iringa na Mbeya mjini Rujewa. Katika mapokezi hayo, umati wa watu ulijitokeza kumlaki mgombea huyo kipenzi wa Watanzania.  

Viongozi wa mkoa wa Iringa chini ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tasil Mgoda, maarufu kama 'Babu Mgoda' wanavyomwita wananchi wa mkoa huo, waliukabidhi msafara wa Kikwete uliokuwa chini ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kanali Abdulrahman Kinana, kwa viongozi wa mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Mkoa, Julius Nswila.

Viongozi wengine wa mkoa, waliokuwepo kwenye mapokezi ya mgombea kuingia Mbeya ni Katibu wa Chama Mkoa, Sylvester Kikungwe, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Mbeya, Profesa Mark Mwandosya na Kamanda wa Vijana wa Mkoa, Nawab Mulla.

Katika mababidhiano hayo, kulikuwa na utani baina ya viongozi hao ambapo Mgoda alimwambia Nswila:"Nakukabidhi mgombea akiwa salama, lolote likitokea juu yako".

Nswila bila ajizi, alimjibu Kigoda kuwa mgombea na msafara wake watakuwa salama zaidi, hali iliyofanya kuwepo na furaha ya aina yake iliyotokana na utani. Wananchi wa Mbeya na Iringa ni watani wa jadi.

Baada ya makabidhiano hayo, msafara ulikwenda hadi Uwanja wa Barafu, Rujewa ambako Kikwete alifanya mkutano mkubwa wa kwanza wa kampeni mjini hapo.

Katika mkutano huo, Kikwete pia alimnadi mgombea Ubunge wa Mbarali kupitia CCM, Esterina Killasi pamoja na wagombea udiwani.

WATU WACHENGUKA

Katika mkutano wa Mbarali, wananchi walionekana kuwa 'walevi' wa CCM kwani walimwagika kwa wingi kumlaki na kumsikiliza Kikwete.

Hata Katibu wa CCM Mkoa, Kikungwe alipokuwa akiwasalimu kwa salamu za Chama (Kidumu Chama Cha Mapinduzi, wananchi hao waliitikia: "Ndiyo, Kidumu, Maisha Bora kwa Watanzania".

Hali hiyo ilimfanya Kikwete kufurahi zaidi kwa salamu hizo ambazo zilikuwa hazijapata kutokea tangu kuanza kwa ziara zake za kampeni mkoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini.

Kabla ya Mbeya, Kikwete alifanya ziara ya mikutano ya kampeni katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, na Njombe mkoani Iringa.

Si hivyo tu, wananchi wa Mbarali hawakuisha kuonyesha furaha yao kila mgombea alipokuwa akizungumza  matumaini kwa Watanzania wakati akiwaomba waichague CCM kuendelea kushika hatamu ya uongozi wa nchi.

HOTUBA NZITO

Licha ya kuendelea kusisitiza sababu za CCM kuomba kuendelea kutawala ikiwa ni kuendeleza mafanikio yaliyopatikana awamu tatu zilizopita.

Kikwete pia aliwaeleza wananchi mambo atakayofanya na timu yake baada ya kuchaguliwa, Kikwete aliwakuna zaidi alipozungumzia mapinduzi katika kilimo na ufugaji.

Wananchi wa Mbarali ni wakulima hodari wa Mpunga pamoja na ufugaji wa ng'ombe katika bonde la Usangu.

"Ni lazima tutoke kwenye ufugaji wa kuzunguka nchi nzima ambao si ufugaji bali ni uchungaji. Ufugaji umemfanya mwananchi aitumikie mifugo badala ya kumtumikia mwananchi.

"Hali hii ni lazima tuibadili haraka sana ili wafugaji wafaidike na jasho lao," alisema na kuwafanya wananchi kumshangilia.

Wafugaji wengi walioko katika bonde la Usangu ni wahamiaji kutoka mikoa ya Arusha, manyara, Mwanza na Shinyanga ambao wamefika mahali hapo baada ya kutembea umbali mrefu kwa minajili ya kutafuta malisho na maji.

Zaidi ya mapinduzi katika ufugaji, Kikwete aliwakonga nyoyo wananchi  wa Mbarali alipozungumzia ruzuku katika pembejeo na zana za kilimo ili kuwawezesha wakulima kulima kwa ubora na kupata tija.

Hali hiyo iliwafanya wananchi kuzidi kuwa na imani na CCM kuwa ina mpango kamambe wa kuwaondolea kero za muda mrefu katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Baada ya wananchi kumshangilia, alijitokeza mkereketwa na kusema: "CCM Yee..." na wananchi kuitikia: "Yee Inasonga Mbele na Kikwete hadi Ikulu".

Kibwagizo hicho kilimpa hamasa zaidi mgombea ambaye alizidi kumwaga sera za CCM na kuwataka wananchi waendelee kuichagua CCM.

Kikwete katika maeneo yote, aliwasisitizia Watanzania kuendelea kuichagua CCM kwa kuwa ndiyo iliyodumisha amani na utulivu na hivyo kusababisha maendeleo kuonekana.

Pia alisema agenda kuu ya kwanza ambayo serikali ijayo itashughulikia ni kufanya mapinduzi makubwa kwenye kilimo ili kuwawezesha wananchi ambao wengi ni wakulima kupata unafuu wa maisha.

Mbali na kilimo, Kikwete aliwasisimua vijana kila alipokuwa akizungumzia ajira kwa vijana. Vijana walionekana kukunwa zaidi na maneno hayo yenye matumaini.

Alifafanua kwamba suala la ajira kwa vijana litatiliwa mkazo kwa kuongeza vitegauchumi pamoja na kutoa mikopo kwa vijana ili waweze kupanua biashara zao na kujiajiri.

Hali bora ya maisha kwa kinamama ilikuwa gumzo kila sehemu ambapo mgombea urais alisema serikali ijayo itatilia umuhimu wa pekee kuhakikisha wanainuka kimaslahi tofauti na ilivyo sasa.

Kwa hakika hotuba zote alizozitoa, ziliamsha ari kwa kila rika la watu lililohudhuria mikutano hiyo na kupata matumaini kwamba CCM imepania kuondoa umaskini wa Watanzania na kuleta maendeleo kwa kasi zaidi.

Wananchi hao waliamini kuwa neema ya Watanzania katika kujikomboa kutoka kwenye lindi la umaskini, itapatikana kwa kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya kama ilivyo kauli mbiu ya mgombea huyo aliyoitoa alipotangaza nia ya kugombea nafasi hiyo Februari, mwaka huu mjini Kibaha.

 WAZUIA MSAFARA

Kumalizika kwa mkutano wa Rujewa kulikuwa kama mwanzo wa wananchi wa Mbeya 'kupagawa' na msafara kwani wananchi maeneo mengi barabarani waliuzuia kwa kufunga barabara.

Kufungwa kwa barabara hakukuashiria vurugu wala fujo bali ilikuwa shauku iliyowajaa wananchi kutaka kumwona na hatimaye kukata kiu yao ya muda mrefu kuhusu Kikwete.

Hali hiyo ilianza baada ya Kikwete kufika Chimala ambapo wananchi waliojitokeza, wake kwa waume, watoto kwa vijana, walionekana dhahiri walikuwa na shauku ya kumwona na kumsikiliza.

Kikwete hakuwaangusha wananchi hao, kwani alisimama na kuwapa 'neno' wananchi hao na hatimaye kumruhusu kuendelea na safari.

Ziara ya Kikwete iliendelea kukumbana na hali hiyo katika maeneo ya Igurusi, Ilongo, Uyole, Mwanjelwa hadi Iyunga alikokweda kujipumzisha baada ya safari kabla ya kuendelea na kazi siku iliyofuata.

MWANJELWA 'VICHAA'

Siku iliyofuata, Kikwete alianza safari kutoka Iyunga kwenda Kyela kwa ajili ya mkutano wa kampeni. Lakini alikumbana na watu 'waliopagawa' katika eneo la Mwanjewa waliozuia msafara wake.

Kikwete ilibidi akubaliane na hali hiyo. Alianza kuwaomba radhi kwa kutokusimama jana yake kutokana na kupita kukiwa kumeshachwea na hivyo kushindwa kuwahutubia au kuwasalimu.

Kama kawaida yake, aliwamwagia maneno yaliyowachanganya zaidi. Baada ya kusikia maneno yake, roho zao zilibaki 'kwatu' na hatimaye kumruhusu aendelee na safari.

Aliondoka na kukutana na hali kama hiyo Uyole, Kiwira, Tukuyu, Busale kabla ya kufanya mkutano mkubwa kwenye uwanja wa Mwakangale mjini Kyela.

Akiwa mjini Kyela, mgombea alipata mapokezi makubwa yaliyoambatana na kila aina ya bashasha na mashamshamu kutoka kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Aliwahutubia wananchi kwa kuwaeleza nia mahsusi ya CCM kutaka kuendelea kuongoza nchi. Pia alimnadi mgombea ubunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Baada ya mkutano wa Kyela, Kikwete alirejea Mbeya kwa ajili ya kufanya mkutano mwingine mjini Mbalizi katika jimbo la Mbeya Vijijini.

Hata hivyo, kabla ya kufika Mbalizi, alikumbana na umati wa watu katika eneo la Mwanjelwa waliokuwa wamefurika kutaka kumwona na hatimaye kupata maneno ya kukata kiu yao. 

Wananchi hao walizuia msafara mara tatu katika eneo hilo la umbali chini ya kilomita mbili. Licha ya hali hiyo, Kikwete hakusita kusimama na kuwapa maneno mawili matatu na hatimaye kuendelea.

Akiwa katika eneo hilo, baadhi ya wananchi hawakusita kuonyesha mapenzi yao kwa Kikwete ambao bila kificho walimwambia: "Mzee usisumbuke nenda kapumzike urais wako tu".

Maneno hayo yaliwafanya watu waliokuwa eneo hilo kushangilia kwa furaha na kuimba: "Rais, Rais, Rais".

Mkutano wa Mbalizi nao kama ilivyokuwa Kyela, ulijaa watu hali iliyozidi kuashiria kuwa wananchi wa Mbeya wameshikwa na 'muwashawasha' wa kumwona mgombea wa Urais wa CCM na kipenzi cha Watanzania.

Katika mkutano huo, Kikwete alimtambulisha mgombea Ubunge wa jimbo hilo, Richard Nyaulawa na wagombea udiwani.

Siku iliyofuata, msafara wa mgombea uliondoka Mbeya mjini kwenda Tukuyu wilayani Rungwe kwa ajili ya mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa CCM mjini humo.

Kama ilivyo ada, aliwatambulisha wagombea wa majimbo ya Rungwe Mashariki, Profesa Mark Mwandosya na Profesa David Mwakyusa (Rungwe Magharibi).

"Ninashukuru kwamba tayari Profesa Mwandosya ameshapita bila kupingwa. Lakini ninachowaombeni wananchi wa Rungwe Magharibi, mumchague Profesa Mwakyusa.

"Ninamfahamu Profesa Mwakyusa tangu siku nyingi. Ni mchapakazi na mtu anayejituma. Ninachowaombeni nipeni hawa maprofesa. Ninawahitaji," alisema.

Alipomaliza mkutano huo aliondoka na kwenda Mbeya mjini alikofanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.

UMATI MKUBWA

Msafara wa Kikwete kwenda uwanja wa Sokoine zilianza kwa staili ya aina yake eneo la Mwanjelwa maarufu kama ma-fiat.

Akiwa katika eneo hilo, makutano ya barabara Kuu iendayo Makambako na Tunduma, alikutana na umati mkubwa uliokuwa umejipanga kando ya barabara hadi uwanjani.

Si hivyo tu, msafara huo ulipokewa na maandamano ya baiskeli na pikipiki huku mbele kabisa kukiwa na farasi, hali iliyoongeza manjonjo na nakshi.

Umma wa watu waliofika uwanjani, ulilipuka vifijo, mbinja na kila aina ya chereko na furaha msafara huo ulipofika lango kuu la uwanja.

Kikwete, kama kawaida yake, alitokeza juu ya gari alilokuwamo na kuanza kuwapungia maelfu ya wananchi, jambo lililosababisha uwanja mzima kuzizima kwa furaha.

Alikaribishwa uwanjani hapo kwa kuvikwa skafu na vijana wa chipukizi wa CCM na baadaye kukagua ngoma mbalimbali za makabila ya Mbeya.

KWA HERI MBEYA

Siku iliyofuata, Kikwete aliaga mkoa wa Mbeya na kwenda Rukwa kwa ajili ya mikutano ya kampeni kama hiyo kwa siku moja.

Kabla  ya kufanya hivyo na kupokewa mkoani Rukwa, alipita maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mbozi na kufanya mikutanop ya hadhara katika maeneo ya Vwawa na Tunduma.

Katika mikutano hiyo aliwanadi wagombea Ubunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na wa Mbozi Mashariki, Dk. Luka Siyame pamoja na wagombea udiwani.

Msafara wa mgombea ulikabidhiwa kwa viongozi wa mkoa wa Rukwa katika kijiji cha Mkutano. Nswila alimkabidhi mgombea kwa viongozi wa Rukwa chini ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Charles Kabanga.

 

 

 

 

Ni miongo miwili ya kutembea kifua mbele Mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii

SERIKALI ya Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitekeleza ilani mbili za Uchaguzi za CCM: Ilani ya 1995 na ya 2000. Mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi  chote cha miaka  hiyo kumi. Kutokana na ukubwa  wa mafanikio hayo ambayo yameweka msingi wa maendeleo ya haraka zaidi kwa nchi yetu, Awamu ya Nne itawajibika kuyaendeleza. Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa, inamaliza muda wake wa kikatiba wa kuwa madarakani, ni vyema kuelezea ilivyofanikiwa kutekeleza Ilani za Uchaguzi za CCM. Gazeti hili kuanzia leo litakuwa linachapisha mfululizo wa makala zenye kuelezea mafanikio hayo; na vilevile utekelezaji  wa Ilani ya 2000 kwa upande wa Zanzibar, chini ya uongozi wa Rais Amani Abeid Karume.

UCHAGUZI  Mkuu wa 2005 utafanyika katika mazingira ambapo Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itangia katika awamu mpya ya uongozi (Awamu  ya Nne) baada ya Awamu ya Tatu iliyoanza 1995, chini ya Rais  Benjamin Mkapa kumaliza muda wake kwa mafanikio makubwa.

Katika  kipindi  chake  cha kwanza cha uongozi cha  1995-2000, Awamu  ya Tatu  ilifanya kazi  nzuri  ya kukamilisha kwa mafanikio makubwa utekelezaji wa sehemu ya pili na mwisho ya Mwelekeo wa CCM  katika  miaka  ya tisini.

Utekelezaji huo ulifanyika kupitia ilani ya CCM ya Uchaguzi  Mkuu  wa Oktoba, 1995. Aidha katika kipindi chake cha pili na cha mwisho  cha 2000 -2005, Awamu Tatu imeweza kutekeleza kwa mafanikio makubwa ya kujivunia, sehemu kwanza ya mwelekeo wa Sera za CCM Katika  Miaka  ya 2000 Hadi  2010  kupitia Ilani ya CCM  ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2000.

Mafanikio ya Awamu ya Tatu kutokana na utekelezaji wa dhati wa Sera na  Ilani za CCM yanadhihirika katika mkakati wa urekebishaji wa uchumi  wa  nchi kutoka uchumi uliodumaa hadi kufikia uchumi uliochangamka na unaokua. Mafanikio hayo ya msingi yameweza kuzaa mafanikio katika sekta zote za kiuchumi, kijamii  na kisiasa na kuiweka Tanzania katika njia ya uhakika ya maendeleo na kupambana na umaskini.

Kwa jumla, katika kipindi  cha miaka 10 iliyopita mafanikio makubwa yamepatikana yanayoendana na matarajio ya Dira ya Taifa ya 2025, hasa katika nyanja kuu zifuatazo:-

Utulivu wa kisiasa

Utawala bora

Utulizaji wa misingi ya uchumi mkuu

Ukuaji mkubwa wa sekta ya Madini

Mafanikio hayo ni kama yafuatavyo:-

(a) Mafanikio katika uchumi

(i) Pato la Taifa limeongezeka kutoka dola (za Kimarekani) 5.6 bilioni mwaka 1995 hadi dola 9.8 bilioni mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 75.

(ii) Pato la  kila mtu limeongezeka kutoka dola 160  mwaka 1995  hadi dola 260  mwaka  2004,  likiwa  ni ongezeko la asilimia 62.5.

(iii) Ukuaji wa pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.6 mwaka 1995  hadi alimia 6.7 mwaka 2004.

(iv) Mfumuko wa bei umeshuka kutoka  asilimia 27.1 mwaka 1995 hadi asilimia 4.2 mwaka 2004.

(v) Asilimia ya Watanzania wanaoishi kwa kipato cha chini ya dola moja ilishuka kutoka 50 mwaka 1995 hadi 20 mwaka 2004.

(vi) Utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma umeweza kuiondolea Serikali mzigo mzito wa kuendesha uchumi moja kwa moja. Ubinafsishaji umeanza kujenga mazingira ya ongezeko la tija na ufanisi katika uzalishaji wa bidhaa za viwandani. Baada  ya kubinafsishwa, kampuni na mashirika hayo sasa yanaipatia Serikali mapato makubwa badala ya kuendeshwa kwa ruzuku ya Serikali.

(vii) Mauzo  ya nje ya bidhaa yameongezeka kutoka thamani ya dola 682.9 milioni  mwaka 1995 hadi dola 1,165.9  milioni mwaka 2004, likiwa ni ongezeko la asilimia 70.7

(viii) Akiba  ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagizia  bidhaa  kutoka  nje imeongezeka  kutoka uwezo wa kukidhi mahitaji ya mwezi 1.6 mwaka 1995 hadi mahitaji ya miezi 9 mwaka 2004.

(ix) Ruzuku ya Serikali Kuu kwa Serikali za Mitaa ambazo ni chombo cha wananchi wenyewe cha kusimamia  maendeleo yao kule kule waliko, imeongezeka kutoka sh. 12.3 bilioni mwaka 1995 /96  hadi sh. 392.2 bilioni mwaka 2004/05 . Hili ni ongezeko la asilimia 3,088.6 (yaani zaidi ya mara 30).

(x) Kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya kuweka mazingira mazuri ya kuvutia vitenga uchumi na kupambana  na rushwa, hivi  sasa Tanzania ni miongoni  mwa  nchi zinazoongoza  katika Afrika katika kuvutia uwekezaji. Mwaka 2004 Tanzania  ilipata  tuzo ya kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa uwekaji wa mazingira mazuri  ya uwekezaji. Uwekezaji wa moja kwa moja wa mitaji kutoka  nje umeongezeka kutoka dola 50.2  milioni  mwaka 1995  hadi  dola 247.8  milioni mwaka 2004,  sawa na ongezeko la asilimia 394.

(xi) Kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mikakati ya  kupambana rushwa na kuziba  mianya ya ukwepaji wa kulipa kodi pamoja zoezi la ubinafsishaji wa mashirika ya umma, hatua ambayo imeboresha uzalishaji, makusanyo ya mapato ya  Serikali  yameongezeka kutoka wastani wa sh. 25  bilioni kwa mwezi, mwaka 1995  hadi wastani wa sh. 160 bilioni kwa mwezi, mwaka 2005, likiwa ni ongezeko la asilimia 540.

(xii) Tanzania ilitimiza masharti ya Mpango  wa Kuzifutia Madeni nchi zenye Madeni Makubwa (HIPC)  na hivyo kuingizwa katika Mpango huo mwaka 1999. Kutokana na hali hiyo, kuanzia  mwaka 2002/2003 hadi 2004/2005, Tanzania ilitekeleza Mkakati  wa Kupunguza Umaskini (MKU)  ambapo fedha ambazo  zingetumika kulipia madeni ya nje yaliyofutwa,  sasa zilielekezwa katika sekta teule za huduma  za jamii na kiuchumi  na miundombinu  zinazowagusa moja kwa moja wananchi  wa kawaida  kwa manufaa ya pamoja. Sekta hizo ni elimu, afya, maji, barabara za vijijini, kilimo  na utawala bora, hususan Mahakama.

(xiii) Kutokana na juhudi za makusudi za kuimarisha utalii kwa lengo la kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira, idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka watalii 295,000 mwaka 1995 hadi watalii 582,000 mwaka 2004. Hili ni ongezeko la asilimia 973. Pia, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka dola 259 milioni mwaka 1995 hadi dola 746 milioni mwaka 2004, ongezeko la asilimia 88. Nafasi za ajira kwenye Sekta ya Utalii zimeongezeka kutoka 96,000 hadi 160,750, sawa  na ongezeko la asilimia 67.4.

(xiv) Kutokana na utekelzaji wa sera za makusudi za kuvutia wawekezaji wakubwa na teknolojia ya kisasa katika uchimbaji  wa madini, hasa dhahabu , imefunguliwa migodi  mikubwa Nzega, Geita, Kahama, Mara n.k. Kutokana na maendeleo hayo, uuzaji wa madini umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka thamani ya sh. 452 milioni mwaka 1995  hadi sh. 22,786  milioni mwaka 2004 likiwa ni ongezeko la asilimia 4,941.

(xv) Kutokana na utulivu wa mazingira ya kisiasa na kiuchumi, biashara imechangamka nchini. Mchango wa Sekta ya Biashara kwa pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.4 mwaka 1995  hadi  asilimia 16.8 mwaka 2004. Mchango wa Sekta ya Fedha umeongezeka kutoka asilimia 5.9 hadi asilimia 12.1 katika kipindi hicho. Mchango  wa Sekta ya Viwanda  nao uliongezeka kutoka asilimia 4.5 hadi 8.7. Vilevile, mchango wa Sekta ya Madini kwa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 0.1 mwaka 1995 hadi asilimia 3.0 mwaka 2004.

(b) Mafanikio katika huduma za kiuchumi na Miundombinu

Barabara na Madaraja

(i) Toka mwaka 2001, Serikali imekuwa ikitenga sh. 1.8 bilioni kila mwezi kwa ajili ya ujenzi wa barabara nchini. Fedha hizo, pamoja na za Mfuko wa Barabara na za wahisani, zimewezesha uimarishaji na utanuzi wa kiasi kikubwa wa mtandao wa barabara kuu na za vijijini nchi nzima. Urefu wa barabara za lami nchini umefikia kilomita 4,837 mwaka 2004. Kwa upande wa barabara za changarawe/udongo, urefu umefikia kilomita 80,063 mwaka 2004. Pia, wakati  ujenzi wa  barabara  kwa kiwango  cha lami ukiwa unaendelea kwa kasi, barabara  za  changarawe/udongo za Taifa, Mikoa, Wilaya na za vijijini  ziko  katika hali nzuri ya kupitika kuliko  zilivyokuwa mwaka 1995  kutokana na kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara.

(ii) Ujenzi wa Daraja  la Mto Rufiji,  linalojulikana  sasa kama  Daraja la  Mkapa,  ulikamilika mwaka 2004  na hivyo  kuifungulia milango ya maendeleo ya kiuchumi Mikoa ya Kusini.