Dk. SHEIN Ngombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya CCM ya awamu ya nne ikiingia madarakani itahakikisha upatikajani wa masoko kwa bidhaa za kilimo na viwanda. Dk. Shein aliyasema hayo jana (25/09/2005) alipokuwa akihutubia mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu kwa nyakati tofauti katika majimbo ya Chalinze na Bagamoyo Mkoni Pwani. Alisema serikali itawasaidia wakulima na wazalishaji wa viwandani kupata masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuinua mchango wa sekta hizo katika kukuza uchumi na maendeleo ya taifa. Lengo la serikali ya CCM, Dk. Shein alisema ni kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi kutoka kiwango cha asilimia 6.7 kwa sasa, hadi kufikia asilimia 10 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. "Serikali itahimiza uanzishaji wa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ikiwemo matunda," alisema na kuwataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kuongeza uzalishaji wa mananasi na mazao mengine yanayolimwa Mikoa ya Pwani. Dk.Shein akiwa amefuatana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Pwani Bw. Mwinshehe Mlao, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Bw. Jumanne Mangara na viongozi wengine wa CCM alihutubia mikutano ya hadhara kata ya Kiwangwa, jimbo la Chalinze na Bagamoyo Mjini, jimbo la Bagamoyo. Katika mikutano hiyo, Dk. Shein aliwaomba wananchi wamchague Mgombea Urais kupitia tiketi ya CCM Bw. Jakaya Kikwete,Wabunge na Madiwani waliosimamishwa na CCM kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Wagombea Ubunge waliotambulishwa na kuombewa kura ni Bw. Ramadhani Maneno wa jimbo la Chalinze na Dk. Shukuru Kawambwa wa jimbo la Bagamoyo. Wakati huo huo, Dk. Shein amesema viongozi wa vyama vya upinzani hawana ubavu wa kushindana na CCM katika sera na masuala mengine ya kitaifa. Akihutubia mikutano ya kampeni mwanzoni mwa ziara yake katika vijiji vya Bungu na Muhoro Wilaya ya Rufiji, Mkoani Pwani Dk.Shein alisema CCM ndicho Chama chenye historia ya uongozi wa taifa toka enzi za kudai uhuru. Dk.Shein alisisitiza kuwa misingi ya umoja, upendo na maendeleo ya Tanzania ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na CCM ambayo ilirithi majukumu hayo kutoka kwa vyama TANU na ASP vilivyopigania uhuru wa kitaifa. Aliwataka wananchi wasiyubishwe na vyama vinavyotumia dini kueneza masuala ya kisiasa na kusisitiza kuwa vyama vinavyojipenyeza kwa kuhubiri siasa misikitini vitayumbisha taifa. " Mkimchagua kiongozi kwa misingi ya dini, mtapata matatizo," alisema na kuongeza kuwa kiongozi anayeeneza siasa kwa kutumia dini ni mfilisi, hafai. Katika mikutano yake Wilayani Rufiji Dk. Shein aliwapokea wanachama 35 wa vyama vya upinzani waliojitoa kutoka kwenye vyama hivyo na kujiunga Chama Cha Mapinduzi. Wanachama hawaliojitoa upinzani walitoka vyama vya CUF-32,CHADEMA wawili na UDP mmoja. Mbali ya wanachama hao Dk. Shein alitoa kadi kwa wanachama wapya 489 wa CCM kwenye mikutano hiyo. Kesho (27/09/2005) Dk. Shein anaendelea na ziara ya kampeni Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara.

Abihudi Saideya, Bagamoyo, 26/09/2005