YALIYOJIRI KAMPENI ZA CCM

ZIARA ya Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa ilikuwa ya aina yake kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata kila alipofika kwa ajili ya kuomba ridhaa kwa wananchi kuichagua CCM iendelee kuongoza nchi. Mwandishi Wetu EPSON LUHWAGO aliyekuwa kwenye ziara hiyo, anatanabaisha yaliyotokea katika makala hii.

 

Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete alifanya ziara ya siku mbili ya kampeni mkoani Iringa Septemba 3 na 4, mwaka huu.

Kabla ya ziara hiyo, Kikwete alihutubia mikutano ya hadhara katika wilaya ya Njombe maeneo ya Kifanya, Njombe Mjini, Makambako na Wanging'ombe mkoani humo, alipokuwa akipita kwenda Mbeya kwa ziara kama hiyo.

ZIARA RASMI

Kikwete alipokewa saa 4.30 asubuhi na viongozi wa Chama na Serikali, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa, Tasil Mgoda, katika Uwanja wa ndege wa Ngwazi nje kidogo ya mji wa Mafinga.

Viongozi wengine waliokuwepo katika mapokezi hayo ni Katibu wa Mkoa, Constantine Malyagili, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mkoa wa Iringa, Joseph Mungai, Mjumbe wa NEC, William Lukuvi na Mjumbe wa Kamati Kuu Pindi Chana.       

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa Lediana Mng'ong'o, Mbunge wa Iringa Mjini Monica Mbega, viongozi wa kampeni ya kanda, Peter Siyovelwa na Mustafa Songambele na mgombea ubunge wa Mufindi Kusini, Benito Malangalila.

Baada ya kuwasili alivalishwa skafu na vijana wa chipukizi wa CCM huku vikundi mbalimbali vya ngoma vikitumbuiza kwa nyimbo zenye asili ya kihehe.

Msafara wa mgombea urais uliondoka uwanjani hapo kwenda Igowole ambako alipangiwa kufanya mkutano wa kwanza wa kampeni.

Kikwete aliwasili Igowole saa 4.55 asubuhi na kupokewa na watu lukuki waliofika katika viwanja vya Shule ya Msingi Igowole kwa ajili ya kumsikiliza.

Mgombea alizunguliwa na salamu za Chama kwa lugha ya kihehe zilizosema: "CCM Kuchanya... kuchanya, kuchanya hilo mbaka pa lunepo (maana yake CCM Juu...juu, juu zaidi na zaidi).

Baada ya salamu hizo, Mwenyekiti wa Chama Mkoa alimkaribisha mgombea kuzungumza na wananchi. Kabla  hajamruhusu, aliwaambia wananchi kwamba CCM haikufanya makosa kumpitisha Kikwete kugombea urais.

Kiwete alisimama na kuwahutubia wananchi huku akitoa ahadi mbalimbali ambazo alisema zitatekelezeka bila wasiwasi wowote.

Kumalizika kwa mkutano huo kulimfanya mgombea kuendelea na safari kuelekea Mafinga mjini ambako alifanya mkutano uliojaza umati wa watu kwenye uwanja wa Mashujaa.

Alifika Mafinga  mchana na kukutana na umati wa watu ambao hakutarajia kutokana na mji wenyewe kuwa wa kawaida.

Msafara wa Kikwete kuingia uwanjani hapo ulisindikizwa na pikipiki 15 na magari madogo takriban 20 kuingia kwenye uwanja wa Mashujaa.

Mara baada ya kufika hapo, aliduwazwa na wananchi waliokuwa wakimsubiri kwa hamu, wengine wakiwa juu ya miti na mapaa ya nyumba zinazozunguka uwanja. Hali hiyo ilitokana na uwanja kuwa mdogo kulinganisha na idadi ya watu.

Kabla ya kupanda jukwaa maalum lililoandaliwa kwa wageni mashuhuri, Kikwete alikagua ngoma za asili kama vile livangala pamoja na kwaya kutoka vikundi mbalimbali vilivyokuwa vimejipanga sawia kupamba mandhari ya eneo la mkutano.

Kama ilivyo ada Kikwete alipanda jukwaani kuwahutubia wananchi waliofurika uwanjani hapo huku wakishangilia kwa kila aina mambo aliyokuwa akiwaeleza wananchi hao.

APEWA TAFSIRI YA JINA

Licha ya kuhutubia wananchi kuomba kura, Kikwete alipewa maana ya jina lake. Maana ya jina hilo ni

K-    King (Mfalme)

I- Intelligent (Mwenye Akili)

K- Kind (Mwema)

W- Wise (Mwenye Busara)

E- Educated (Mwenye Elimu)

T- Trusted (Anayeaminika) na,

E-      Employer (Mwajiri)  

Tafsiri ya jina hilo ilitolewa na aliyekuwa Katibu wa NCCR- Mageuzi, jimbo la Mufindi,  Boniface Mliga alipokuwa akitangaza rasmi kujiunga na CCM baada ya kuchoshwa na ahadi hewa za kambi ya upinzani.

Baada ya mkutano wa Mafinga, Kikwete aliendelea na safari ya kuomba wananchi kuichagua CCM kuongoza nchi kwa kwenda Iringa.

Katika safari ya kuelekea Iringa, alifika Ifunda katika eneo la Kibaoni, jimbo la Kalenga ambao ulikuwa na watu wengi wa marika yote.

Tofauti na maeneo mengine, mbali na viongozi, Kikwete alipokewa na wazee wanne waliokuwa wamevalia rasmi kichifu. Ifunda iko katika jimbo la kalenga ambalo ni asili ya Chifu wa zamani wa Wahehe, Mkwawa.

Kwenye mkutano huo pia, alimnadi mgombea Ubunge wa Kalenga, Stephen Galinoma na wagombea udiwani wa wilaya ya Iringa Vijijini.

 Mkutano wa Ifunda ulikuwa hitimisho kwa siku ya kwanza ya kampeni za mgombea urais. Aliondoka Ifunda kwenda Iringa mjini kwa mapumziko.

HODI IRINGA

Msafara wa Kikwete ulipokewa katika kijiji cha Uyole, manispaa ya Iringa ambapo kulikuwa na wananchi waliojazana kwa shauku ya kumwona mgombea huyo.

Kama ilivyo ada aliwashukuru wananchi wa Iringa kwa mapokezi  makubwa na hatimaye kueleza nia hasa ya CCM kutaka kuendelea kuongoza nchi.

Baada ya maneno hayo, msafara rasmi ulianza ukisindikizwa na magari ya wakereketwa, teksi na pikipiki zilizokuwa na bendera za CCM.

Msafara huo ulikuwa mkubwa na pengine ulivunja rekodi ya mapokezi yaliyokuwepo awali kwenye miji mikuu ya mikoa aliyotangulia.

Kwa wanaoijua manispaa ya Iringa, wakati gari la kwanza likiwa limeshamaliza mlima kuingia eneo la Mshindo, magari mengine yalikuwa bado hayajaingia hata Ipogoro.

Kuanzia eneo la Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora hadi Gangilonga kulikuwa na umati wa watu waliokuwa wamejipanga kando ya barabara kuulaki msafara huo.

Mgombea mwenyewe baada ya kuona umati wa watu kuanzia Samora, aliamua kutokeza juu ya gari na kuwapungia mkono, hali iliyoamsha bashasha na shamrashamra za aina yake.

SARAFI YA KILOLO

Siku iliyofuata (Septemba 4), Kikwete alikwenda Kilolo alikofanya mkutano wa hadhara katika jimbo hilo kijijini Boma la Ng'ombe.

Safari ya kutoka Iringa mjini kwenda huko, ilianza saa 3.15 asubuhi kupitia vijiji vya Tagamenda, Igula, Nyabula, Kitayawa, Ndiwili na Utengule hatimaye Kilolo.

Aliwasili Kilolo saa 4.00 asubuhi na kusalimiana na viongozi wa Chama Wilaya wakiongozwa na Mwenyekiti Valentine Msuva, Mbunge Venance Mwamoto na Mgombea Ubunge wa jimbo hilo, Profesa Peter Msolla.

Baada ya kutia saini kitabu cha wageni, aliwahutubia wananchi waliofika kwenye ofisi za CCM Kilolo zilizoko Luganga, juu ya azma ya Chama kuomba ridhaa kwa wananchi.

Kumalizika kwa hotuba hiyo, kuliashiria kuiva kwa safari ya kwenda Boma la Ng'ombe kupitia Lusinga, Ilamba, Kidabaga, Ng'ang'ange na hatimaye kituo cha mkutano.

Katika maeneo yote aliyopita, Kikwete alilakiwa na umati wa watu uliokuwa ukimsubiri kwa hamu kumwona na hatimaye kusikia neno la matumaini kwa maisha yao.

Wananchi katika vijiji vya Ilamba, Kidabaga na Ng'ang'ange,  walizuia msafara wake kwa nia ya kutaka awape neno. Hakusita kusimama na kuwasalimia, kuwapa neno na hatimaye kuomba wafunge njia ili aendelee na safari.

UMATI BOMA LA NG'OMBE

Baada ya kuwasili Boma la Ng'ombe  asubuhi hiyo hiyo, Kikwete aliduwazwa na umati wa watu kutoka kata mbalimbali za wilaya ya Kilolo waliofika kuhudhuria mkutano wa kampeni.

Mkutano wa Boma la Ng'ombe ulipambizwa na kila aina ya ngoma za wahehe kama vile livangala na kiduo ambazo huchezwa na wananchi wa wilaya hiyo- wadzungwa na wahehe.

Kama ilivyo ada, Kikwete alisimama na kuwafanya wananchi 'kupagawa' baada ya kumwona alipotambulishwa na kukaribishwa kuzungumza nao.

Bila kusita alisimama juu ya gari lake lililokuwa na spika na kuanza kuwamwagia sera wananchi, ambazo kwa hakika,  walionekana kuzikubali.

Katika mkutano huo Kikwete alimnadi mgombea Ubunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla na kuwaomba wananchi kumchagua kwa kuwa ni msomi, kiongozi shupavu na tegemeo katika utekelezaji wa ahadi za CCM katika serikali ijayo.

"Wana-Kilolo mmempata Profesa Msolla mtaalam katika kilimo. Ni raha iliyoje kumpata mtu kama profesa ambaye ndiye bingwa katika kilimo ambacho tunakitilia mkazo," alisema huku akishangiliwa na umati wa watu waliokuwepo katika mkutano huo.

Baada ya kumaliza mkutano huo, mgombea na msafara wake walirejea Iringa kwa mapumziko mafupi na baadaye  mkutano uliofanyika jioni kwenye uwanja wa Samora.

MSAFARA SAMORA

Msafara wa mgombea kwenda uwanja wa Samora ulianza saa 9.05 Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (zamani Chuo cha Benki) na kuwasili uwanjani dakika saba baadaye.

Baada ya kuingia Samora, alitokeza juu ya gari lake na kuwapungia mkono wananchi ambao walijawa na furaha kumwona mgombea huyo.

Alipewa mapokezi na heshima zote, alipanda jukwaani na kuwahutubia wananchi waliofika hapo pamoja na kumnadi mgombea Ubunge wa Iringa Mjini Monica Mbega na wagombea udiwani.

MUNGAI KUVUTIO

Waziri wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai ambaye ni Mjumbe wa NEC mkoa wa Iringa, alikuwa kivutio cha aina yake katika mikutano ya kampeni mkoani Iringa hasa katika wilaya za Mufindi, Kilolo na Iringa Mjini.

Mungai ambaye ni Mbunge wa Mufindi Kaskazini, alikuwa akivutia kutokana na uchezaji wake hodari wa ngoma ya Livangala iliyokuwa ikichezwa maeneo mbalimbali wakati wa kampeni hizo.

Kiongozi huyo wa siku nyingi, alianza kuonyesha manjonjo yake Igowole alipojiunga na kikundi kilichokuwa kikicheza ngoma ya Livangala.

Hizo zilikuwa kama salamu tu, kwani alipofika Mafinga, alikwenda moja kwa moja kwenye kikundi kimojawapo na kuanza kucheza ngoma hiyo mkononi akiwa ameshika 'usinga'.

Kufuatia hali hiyo, wananchi waliokuwepo mahali hapo walianza kumshangilia na hivyo kutia nakshi ya aina yake katika mkutano.

Mungai aliendelea na uchezaji wa ngoma hiyo na kuonyesha kuwa ni hodari kwenye mikutano ya Boma la Ng'ombe na Iringa Mjini.

MANENO YA KIKWETE

Katika mikutano yote mkoani Iringa, Kikwete aliwahimiza wananchi kuenzi amani na utulivu vilivyodumu nchini tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi.

Alisema vitu hivyo ni tunu kwa Watanzania na kamwe wasivichezee. Aliwataka kujifunza nchi jirani ambazo zimekosa vitu hivyo kutokana na kupigana kila uchao.

"Amani na utulivu vilivyopo nchini ni vina umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi. Bila amani na utulivu hakuna maendeleo. CCM imefanya yote haya ndiyo maana nchi imetulia," alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kutokuwachagua viongozi wanaohubiri shari katika mikutano kwani alisema kuwachagua ni sawa na kuiweka nchi reheni na kuhatarisha amani na utulivu.

Mbali na amani na utulivu, Kikwete alisema lengo la serikali ijayo chini ya CCM ni kuhakikisha kunakuwepo mapinduzi ya kweli katika sekta ya kilimo.

Alisema katika kufanya mapinduzi hayo, serikali itahakikisha wananchi wanaondokana na matumizi ya nguvu ya damu kwa kutumia jembe la mkono na badala yake kutumia nguvu ya mashine.

Licha ya kilimo, alisema ukuzaji wa viwanja utapewa kipaumbele kwa kuweka mazingira bora na endelevu ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo.

Pia aliahidi kutengeneza barabara ya lami kutoka Minjingu- Babati-Dodoma hadi Iringa kwa kiwango cha lami ili kuifanya barabara kutoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo, Misri ijulikanayo kama 'Great North Road' iwe ya lami.

Mbali na barabara hiyo, aliahidi kuboresha barabara zingine ikiwemo ya kutoka Iringa hadi Dabaga ili kuwawezesha wananchi kunufaika na usafirishaji wa mazao yao hadi kwenye masoko.

Kwa upande wa elimu, alisema lengo la serikali ijayo ni kuendeleza elimu ya sekondari na chuo kikuu ili kuwawezesha wananchi wengi kupata nafasi.,

"Elimu ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya nchi. Hata mataifa yaliyoendelea yanatilia umuhimu katika elimu. Uingereza wakati wa kampeni chama cha Labour ajenda kuu ilikuwa elimu.

"Na sisi hii itakuwa kipaumbele kwa maendeleo ya nchi. Katika kufanya hivi, tutapanua vyuo vikuu nchini ili kuwezesha vijana wengi zaidi kupata elimu kwa ajili ya maendeleo," alisema.

Kuhusu makao makuu ya wilaya ya Kilolo, mgombea Urais aliwapasha baadhi ya wanasiasa wanaoeneza uvumi kuwa kuna mpango wa kuhamisha makao makuu ya wilaya kutoka Kilolo kwenda Ilula.

Aliwaambia wanasiasa hao kuwa hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuhamisha makao makuu hayo na kusisitiza kwamba uamuzi wa Rais juu ya suala hilo ni wa mwisho na hauna mjadala tena.

Kikwete alisema hayo kufuatia baadhi ya wanasiasa wakati wa kura za maoni kudai kwamba Profesa Msolla alikuwa na mpango wa kuhamisha makao makuu kwenda Ilula.

 

 

 

 

CCM na mikakati ya  ushindi Temeke

KATIKA kipindi hiki cha kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao, watu wasiojua siasa za Temeke, 'wanaropoka' kwamba miongoni mwa majimbo yanayotajwa kuwa huenda yakaangukia kwa wapinzani ni pamoja na lile la Temeke, mkoani Dar es Salaam kwa madai kwamba limekuwa na  historia fupi ya kuongozwa na wapinzani. Hata hivyo wenye mwelekeo huo wanasahau kuwa kuna nafasi kubwa ya jimbo hilo kwenda CCM kutokana na siri iliyofichika. Ni siri gani hiyo? Mwandishi THOMAS MTINGE, anafafanua katika makala hii.

 

JIMBO la Uchaguzi la Temeke mkoani Dar es Salaam katika nafasi ya ubunge kabla ya Uchaguzi Mkuu wa sasa lilikuwa chini ya CCM ambapo mbunge wake alikuwa Khadija Kusaga.

Mgombea huyo wa CCM katika uchaguzi wa kura za maoni hakupata nafasi ya kuteuliwa kutetea kiti chake na badala yake nafasi hiyo imechukuliwa na Abbas Mtemvu ambaye anapeperusha bendera ya CCM katika kinyang'anyiro cha ubunge.

Wakati joto la kuwania nafasi hiyo likizidi kupanda kwa kuwa siku nazo zinakaribia kuchagua viongozi, kumejitokeza baadhi ya wanaojiita watabiri wa masuala ya siasa na watu wengine kwa ajili ya kutoa maoni mbalimbali huku wakielezea kuwa jimbo hilo linaweza kuchukuliwa na upinzani na hasa chama cha CUF.

'Watabiri' hao wanataja sababu nyingi mbalimbali lakini baadhi ni kuwa mgombea wa CUF Tambwe Hizza ambaye amewania nafasi hiyo mara tatu sasa lakini bila mafanikio, amepata ukomavu na uelewa mkubwa wa kisiasa hivyo kuwa rahisi kushinda.

Wanasema kuwa kitendo cha Tambwe kupata nafasi hiyo tena, kinampa fursa ya kuibuka na ushindi dhidi ya mgombea wa CCM.

Sababu nyingine inayotajwa ni kuwa wananchi wa jimbo hilo wameshawahi kuwapa wapinzani ushindi kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa sasa wa TLP Augustine Mrema ambaye alipata kuongoza jimbo hilo akiwa NCCR-Mageuzi.

Mrema alikuwa mbunge wa Temeke hadi alipotangaza kujiengua kutoka NCCR-Mageuzi na kujiunga na Tanzania Labour ambapo kisheria alikuwa amepoteza wadhifa wake wa ubunge.

Lakini jingine linalotajwa kuwa litachangia ushindi kwa CUF ni kuwa jimbo hilo eti lina wanachama wengi wa CUF kuliko majimbo mengine katika jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, Wilaya ya Temeke ina majimbo mawili ya Kigamboni na Temeke.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, katika mkoa mzima wa Dar es Salaam, jimbo pekee lililochukuliwa na wapinzani ni lile la Kigamboni tu ambalo mbunge wake alikuwa Frank Magoba. Kwa sasa Magoba amerejea CCM.

Majimbo mengine kama vile Kawe, alikuwa Ritha Mlaki ambaye amepata nafasi ya kutetea kiti chake, Kinondoni alikuwa Peter Kabissa ambaye safari hii naye hakuteliwa ambapo nafasi hiyo inatetewa na Iddi Azan, Ubungo alikuwa Charles Keenja,anatetea kiti chake, Ukonga alikuwa Dk. Makongoro Mahanga, anatetea tena kiti chake na Ilala alikuwa Idd Simba ambaye ameamua kupumzika na kuiacha bendera ya CCM katika jimbo hilo ikipeperushwa na Mussa Azzan 'Zungu'.

UTABIRI HAUNA NGUVU

Lakini utabiri huo unaotolewa na baadhi ya watu katika jimbo hilo unatofautiana kabisa na mtazamo wa kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM Kata ya 14, wilayani Temeke Fard Bazar.

Akieleza  mtazamo wake, Bazar anasema utabiri huo kwa sasa hauna nafasi tena katika jimbo hilo kutokana na jinsi CCM ilivyojiimarisha pande zote.

 Wapinzani, alisema  hawana nafasi tena ya kulitawala jimbo hilo kwa sababu walichezea bahati waliyoipata katika uchaguzi wa mwaka 1995 ambapo Mrema alichaguliwa kuwa mbunge.

Pamoja na wananchi kutupa karata yao katika kambi ya upinzani wakitarajia kupata mabadiliko ya maendeleo, bado ikaonekana kama ndoto kwao baada ya Mrema kuwatelekeza kwa kujiuzulu ghafla bila kutoa sababu za msingi.

Kitendo cha Mrema kujiuzulu wadhifa huo bila sababu za msingi, kimewachukiza wananchi na kuwafanya wasiwe na imani tena na kambi hiyo, anasema Bazar.

Akifafanua,alisema  kuwa kutokana na imani hiyo iliyojengeka kwa wananchi, kambi ya upinzani sasa imekuwa haiaminiki tena.

" Samaki mmoja akioza wote wameoza'. Hivyo kitendo alichokifanya Mrema kinaweza kufanywa pia na wagombea wengine kutoka kambi ya upinzani endapo watapewa ridhaa ya wananchi kushika nafasi za uongozi."

Kutokana na kulitambua hilo, ndio maana ulipofanyika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mrema, wananchi wakaamua kuichagua CCM.

Kamanda Bazar anasema wameamua kuichagua CCM si  kwa kubahatisha, bali  wakiwa na matumaini kwamba ni Chama chenye sera nzuri na kinachoweza kuwaletea maendeleo.

Kwa mujibu wa Bazar, katika uchaguzi huo mdogo ambapo CCM ilimsimamisha John Kibaso kuwa mgombea wake, iliibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya wapinzani.

Ushindi huo wa CCM, ndio ikawa mwanzo wa kuzika ndoto za wapinzani kuliongoza tena jimbo hilo.

Kwa kuthibitisha hilo,  wapinzani walisambaratishwa tena katika Uchaguzi Mkuu uliyofanyika mwaka 2000.

.CCM haiwezi kubishana na vyama ambavyo havina sera wala mwelekeo ambavyo hata wananchi tayari wameonyesha hali ya kutovikubali.

" kama ni mchezo wa mpira wa miguu basi naweza kusema kwa sasa CCM ndio timu ya Simba na wapinzani ni Yanga.kwahiyo hawa ni wateja wetu na wataendelea kuwa wateja wetu hadi hapo tukapoamua vinginevyo," anasema kamanda Bazar.

Litakuwa ni jambo la ajabu kwa wananchi wa jimbo hilo kuthubutu kurudia makosa waliyoyafanya mwaka 1995 kwa kuchagua mgombea kutoka kambi ya upinzani.

Endapo wananchi wataamua kuchagua wagombea waliosimamishwa na vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao, watakuwa wamejifunga kitanzi cha kujiletea maendeleo katika maeneo yao husika.

Hii ni kwa sababu kambi hiyo haijajiimarisha kisera na hivyo haina uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi.

UONGOZI SI MAJARIBIO

Wanachokifanya sasa kuhusu kushiriki kwao katika uchaguzi huo, Bazar anasema  ni kutaka kujaribu kama wanakubalika kiasi gani.

Anashauri wana-CCM na wananchi kwa ujumla wao kutofanya makosa ya majaribio ya uongozi kwa kuwachagua wapinzani.

"Uongozi kamwe haujaribiwi hata siku moja kwani kufanya hivyo ni sawa na kuchezea shilingi katika tundu la choo ambapo ikidumbukia haitapatikana tena.

" Kuwapa uongozi wapinzani kwa majaribio ni sawa na kumpa panga mwenda wazimu ambaye anaweza kulitumia vibaya wakati wote na baadaye ukajutia uamizu wako uliyoufanya," anasema.

CCM, anasema  imejiandaa vema   kukabiliana na hali ya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao. "Tuko imara kukabiliana na hali yoyote ile kwani tuna silaha za kutosha za kupambana nao na lazima CCM itashinda tu na si vinginevyo.

 Silaha hizo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo Bazar anasema imetekelezeka kwa asilimia kubwa katika serikali ya awamu tatu.

Lengo la CCM, ni kupata tena ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu ujao, ili kuendeleza mafanikio iliyoyafanya na kuongeza mengine zaidi ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi wake.

 CCM ina uwezo wa kutekeleza ahadi zake inazozitoa kwa wananchi hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu tofauti na sera za wapinzani ambazo hazitekelezeki hata kidogo.

Ushindi huo kwa CCM, Bazar anakiri hauwezi kupatikana hivi hivi bali utapatikana kwa kunadi mafanikio yaliyopatikana kupitia ilani yake ya uchaguzi kwa wananchi.

 Akiwa kama kamanda wa UVCCM, alisema atahakikisha kwamba vijana wake wanashiriki kikamilifu katika kunadi sera za CCM kwa wanchi.

Bazar anasema kushiriki kikamilifu kwa vijana katika kunadi sera za CCM ni sehemu ya wajibu wao lakini pia kutawafanya wananchi walio wengi kutambua nini ilichokifanya CCM.

Alifafanuwa kwamba  kumekuwa na taarifa za upotoshaji zinazosambazwa na wapinzani mitaani eti CCM katika kipindi cha utawala wake haijafanya kitu chochote huku wakitembelea barabara nzuri, kupata maji safi, afya, elimu na maendeleo mengine mengi.

"Vijana ndio nguzo ya CCM hivyo lazima washiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa kuwaelimisha wananchi waachane na vyama 'uchwara' ambavyo havina sera madhubuti na badala yake waichague CCM iendelee kuleta maendeleo," anasema.

Katika kipindi hiki cha uchaguzi, Bazar alisema  atahakikisha kwamba kauli ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Benjamin William Mkapa ya kuwataka makamanda wa UVCCM washirikiane na vijana badala ya kuvaa majoho tu inatekelezwa ipasavyo kwa kuipatia ushindi CCM katika jimbo hilo.

Akielezea alivyoawaandaa vijana, alisema  tayari amekaa na vijana kupanga nao mikakati ya kuipatia CCM ushindi ukiacha ile ya kujiletea maendeleo endelevu ambayo pia ishakamilika.

Kwa mujibu wa Bazar,  anakusudia kukutana na makamanda wenzake wa UVCCM waliomo katika jimbo la Temeke ili kujenga nguvu na mawazo ya pamoja ya jinsi ya kuwahimiza vijana ili wajitokeze kwa wingi wakati wa kupigakura kuchagua viongozi na waichague CCM.

Kuna haja ya makusudi kabisa kila mwana-CCM kuunga mkono kauli ya mgombea wa CCM wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ya kuweka serikali yenye mafiga matatu, alibainisha.

Kauli hiyo, aliongeza  imejaa ukweli tupu kwamba wananchi hawawezi kupata maendeleo safi endapo serikali ijayo itakuwa na upungufu wa mafiga matatu kama alivyosema Kikwete kwa maana ya kwamba rais, wabunge na madiwani lazima watokane na CCM.

" Ilani za vyama zinatofautiana hivyo unapochagua Rais kutoka CCM na kisha ukachagua mbunge kutoka CUF, ujuwe wazi kwamba hapo maendelo yake ni sawa na 'ziro' kwa sababu kila kiongozi atataka kutekeleza sera ya ilani yake," anasema kamanda Bazar.

Kwa vyovyote vile, aliongeza  Kikwete atashinda katika uchaguzi ujao na kuwataka wananchi wamchagulie wabunge na madiwani kutoka CCM ili waweze kuchapa kazi na kuzungumza lugha moja ya kuwaletea maendeleo ya haraka.

Kamanda Bazar anaongeza kuwa serikali ijayo ya CCM inauhakika wa kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka kumi ijao kutokana na ukweli kwamba sera zake zinakubalika na wananchi.

"Ari mpya, nguvu mpya. Kasi mpya  2015," anasema Bazar akimaanisha kwamba CCM itaendelea na kasi hiyo kwa kipindi chote hicho.