MWISHONI mwa wiki iliyopita Mgombea Mwenza wa kiti cha urais kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Sheni, alihitimisha ziara yake ya kampeni katika wilaya tatu za mkoa wa Lindi kwa mafanikio makubwa kutokana na kuzoa zaidi ya wanachama 500 kutoka kambi ya upinzani. Mwandishi wetu RAMADHANI MKOMA anayefuatana na Dk Sheni, anaeleza zaidi katika makala hii yaliyojiri.
Dk. Sheni akiongozana na mkewe Mama Mwanamema Sheni na ujumbe wake wakiwemo waandishi wa habari, waliwasili katika uwanja wa ndege wa Nachingwea majira ya saa
4.05asubuhi na kupata mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi wa wilaya hiyo wakiongozwa na viongozi wa chama na serikali.
Viongozi hao ni pamoja na mkuu wa Mkoa wa Lindi Nicodemus Banduka na Mwenyekiti wa mkoa huo, Mzee Ali Mohammed Mtopa. Kama ilivyo ada Mgombea huyo alivishwa skafu na chipukizi na baadaye kusalimiana na viongozi mbalimbali waliofika kumpokea kabla ya kuanza safari kwenda wilayani Liwale.
Wengine waliokuwepo kwenye msafara huo ni Mbunge wa zamani wa Nachingwea, Edgar Maokola Majogo ambaye pia ni Waziri wa nchi ofisi ya Makamu Rais, anayeshughulikia umasikini na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Mbali na Majogo ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni wa Kanda ya Kusini, wengine waliokuwa kwenye msafara ho ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Kate Kamba na Mkuu wa Wilaya ya Liwale, David Holela.
Msafara wa mgombea huyo ulianza safari ya Liwale saa 5:30 ukipita kupitia vijiji kadhaa vya wilaya ya Nachingwea ambako nyumba nyingi za wakazi wa maeneo hayo zilikuwa zimepambwa kwa picha za wagombea wa CCM.
MSAFARA WAZUIWA
Katika maeneo yote, hayo msafara huo ulikuwa ukipungiwa mikono na wanavijiji waliojitokeza barabarani kumlaki mgombea huyo wa CCM na ujumbe wake.
Alipofika katika kijiji cha Nangano kilichopo maeneo ya mpakani mwa wilaya ya Nachingwea na Liwale, alilazimika kusimama ili aongee na wananchi waliokuwa
wamefurika kando kando ya barabara hiyo.
Akizungumza na wananchi hao Dk. Sheni alisema licha ya safari ndefu aliyonayo amelazimika kusimama na kusalimiana nao. Katika Salamu zake, Dk. Sheni mbali na kuwashukuru kwa mapokezi hayo, aliwaomba wananchi hao kutoyumbishwa na kauli na ahadi za wapinzani zisizotekelezeka.
Dk. Sheni aliwaambia wananchi hao kwamba CCM hakina mbadala kutokana na umakini wa viongozi wake wanaoongozwa na sera na Ilani sahihi za uchaguzi.
Aliwaambia tofauti na vyama vingine CCM pekee ndiyo chama chenye sera zinazolenga kumletea maendeleo mwananchi.
Hata hivyo aliwaambia wako huru kuwasikiliza (wapinzani) lakini linapokuja suala la kura wasiyumbe na wakipe kura CCM ili kiendelee kushika dola na hatimaye kuendelea kufanikisha mipango mizuri ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005-2010.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwaombea kura wagombea wengine wa CCM akiwemo wa kiti cha Urais, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye amekuwa aking'ara katika kampeni zake za kuomba ridhaa kwa wananchi kukichagua kwa mara nyingine Chama cha Mapinduzi.
Dk. Sheni pia alitumia nafasi hiyo kumuombea kura mgombea ubunge wa jimbo hilo, Hassan Kigwalilo na diwani wa kata hiyo, Abbas Matulilo.
Kizuizi kama hicho alikumbana nacho tena katika vijiji vya Kibutuka na Kiangara ambako nako alilazimika kusimama kuomba kura na kutoa msisitizo kwa wananchi hao juu ya umuhimu wa CCM kuendelea kuwa madarakani.
Alisema serikali ya awamu ya tatu chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa imefanya mengi mazuri kwa wananchi wake na kwamba kutokana na hilo hakuna chama kinachoweza kujilinganisha na CCM kisera au kwa Ilani yake ya uchaguzi.
Dk. Sheni aliwaambia wananchi hao kwamba wasisite kuwauliza wapinzani wamefanya nini na wana sera zipi za kuwaletea maendeleo. Pia aliwaeleza wasisite kuwahoji uwezo wa kufanya hayo yote utatoka wapi?
MKUTANO WA LIWALE
Katika mkutano wake wilayani Liwale uliofanyika katika viwanja vya Elimu na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, Dk. Sheni mbali ya kuinadi vilivyo Ilani ya uchaguzi kwa kuizungumza bila kusoma kitabu, pia alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha wananchi n a wanasiasa wanaoomba kura kwa misingi ya kidini.
Dk. Sheni alisema serikali haina dini na kwamba wananchi wako huru katika suala zima la imani na hivyo kuwataka wananchi kuwakwepa wanasiasa na vyama wenye mtazamo huo.
Mgombea huyo pia aliwataka wananchi kukipa kura CCM kutokana na mengi mazuri iliyoyafanya lakini vile vile kwa kutambua michango ya baadhi wa waasisi akiwemo Simba wa Vita Mzee Rashidi Kawawa.
Alisema Mzee Kawawa ametumia muda na nguvu zake nyingi katika kuleta maendeleo ya wilaya hiyo na hivyo si busara jimbo hilo kwenda kabi ya upinzani.
Katika mkutano huo, Dk. Sheni aliwaambia wananchi jinsi serikali chini ya uongozi wa CCM ilivyofanikiwa katika kukuza uchumi sambamba na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
Akitoa mfano katika sekta ya Afya, Dk. Sheni alisema katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 hadi 2010, serikali imelenga katika kupunguza vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kutoka 154 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai hadi 79 ifikapo 2010.
Pia imelenga kupunguza vifo vya uzazi kutoka 529 kati ya wazazi 100,000 hadi 265 ifikapo mwaka 2010.
Hali kadhalika alisema iwapo CCM itarejea madarakani itafanya mapinduzi makubwa ya kilimo, kupitia mipango mbalimbali ya kuimarisha kilimo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kilimo cha jembe kinaondoka na wakulima kutumia Plau.
Dk. Sheni aliendelea kuinadi Ilani hiyo kwa kusema kwamba kilimo cha zao la korosho kitapewa kipaumbele hatua itakayokwenda sambamba na uanzishwaji wa viwanda vya usindikaji ili mazao mbalimbali yaweze kusindikwa na kuuzwa katika masoko ya nje.
WAPINZANI KUJIUNGA
na CCM
Katika mikutano yake wilayani Ruangwa na Nachingea, mbali ya kuhudhuriwa na watu wengi mikutano hiyo ilikuwa pigo kwa kambi ya upinzani kutokana na hatua ya wanachama wake wakiwemo viongozi kijitoa na kujiunga na CCM.
Pigo la kwanza lilijitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Ruangwa ambapo wanachama 321 wa vyama hivyo walijiunga na CCM, akiwemo Mwenyekiti wa wilaya wa chama cha Chausta, Hamisi Chawawa.
Mwingine ni Kuku Ali Juma ambaye ni Mweka hazina wa wilaya wa chama cha CUF. Wote walisema kwamba waliamua kujitoa kwenye vyama hivyo baada ya kubaini kuwepo kwa ubabaishaji.
Vyama hivyo na idadi ya wanachama wake kwenye mabano ni CUF (89), CHADEMA (34), CHAUSTA (24), UDP (19) na NCCR Mageuzi (146).
Wimbi la kujiunga na CCM kwa wanachama kutoka kambi ya upinzani liliendelea hadi wilayani Nachingwea, ambako katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Sokoine, wanachama 258 walijiunga na CCM.
Wanachana hao wanatoka CUF (70), Chedema (30), CHAUSTA (114), UDP (1) NCCR Mageuzi (17) na TLP (25). Wote hadithi yao ni kutokana na vyama hivyo kutokuwa na mwelekeo na sera sahihi zenye kulenga katika kumletea maendeleo mwananchi wa kawaida.
Mbali na wanachama kutoka kambi ya upinzani pia CCM kilipokea wanachama wapya 152 ambao walikula kiapo mbele ya mgombea mwenza.
Katika mkutano huo, Mzee Mtopa aliwakumbusha wananchi wa Nachingwea historia ya wilaya hiyo, katika harakati mbalimbali za kudai uhuru na ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika na kuwataka kutolitoa jimbo hilo kwa vyama visivyokuwa na mwelekeo.
Wakati huo huo, mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 30 Ambaye mwaka huu hawanii tena kiti hicho, Maokola Majogo alimpigia debe mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mathias Chikawe kwa kumuelezea kuwa ni kijana atakayekwenda sambamba na kasi ya serikali ya awamu ya nne katika kuliletea jimbo hilo maendeleo.
Katika mkutano huo, mbali na kuinadi Ilani ya Uchaguzi, Dk. Sheni alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi hao kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujiletea maendeleo yao, wakati serikali nayo ikiendeleza juhudi zake katika kuboresha mazingira ya uzalishaji katika sekta zote.
Pia Dk. Sheni aliwaeleza umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kuondokana na utaratibu mbaya wa upaliliaji mashamba kwa kuchoma moto. Alisema mipango mizuri imeandaliwa katika kuwainua kiuchumi chini ya utaratibu wa kurasimisha mali ili waweze kukopesheka na hatimaye kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi katika zama hizi za utandawazi.