YALIYOJIRI ZIARA YA MGOMBEA MWEZA WA CCM:
Dk. Sheni asambaratisha upinzani Mtwara
Mamia wajiunga CCM kutoka CUF
Wananchi wapagawa na kuzuia msafara wake
MGOMBEA Mwenza wa Urais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Sheni alifanya ziara katika mikao ya kusini mwa Tanzania kwa nia ya kuwaomba wananchi waendelee kuichagua CCM kuendelea kuongoza nchi. Katika makala hii, Mwandishi Wetu RAMADHAN MKOMA aliyekuwemo katika ziara hiyo, anabainisha yaliyojiri mkoani Mtwara.
Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Sheni, hivi karibuni alitembelea mkoa wa Mtwara kwa ajili ya mikutano ya kampeni kuwaomba wananchi kuzidi kuichagua CCM na kuomba wakipe Chama ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu.
Baada ya kumaliza ziara yake mkoani Lindi, Dk. Sheni aliingia mkoani Mtwara kwa ajili ya kuinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mchakato mzima wa kampeni zinazoendelea sasa.
Mara baada ya kuingia mkoani humo, Dk. Sheni aliyekuwa ameongozana na mkewe Mama Mwanamema Sheni, alipata mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi na viongozi wa CCM mkoani humo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa, Mohammed Ndaile.
Wengine waliompokea mgombea huyo mara baada ya kukabidhiwa kutoka kwa viongozi wa mkoa wa Lindi ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Isidore Shirima.
Akiwa mkoani humo, Dk. Sheni na alifanya mikutano ya kampeni katika maeneo mbalimbali vikiwemo vijiji vya wilaya za Masasi, Lulindi, Newala, Tandahimba, Mtwara vijijini kabla ya kumalizia Mtwara mjini.
Katika mikutano hiyo iliyoambatana na matukio mbalimbali ya yakiwemo ya wapinzani kurejea Chama tawala lakini pia alitumia muda huo kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa ufasaha mkubwa.
Mbali na hilo, mgombea huyo pia alilakiwa kwa 'staili' tofauti na wapenzi wa CCM katika maeneo mbalimbali ya wilaya hizo ambako msafara wake ulipita.
Matukio hayo yaliambatanana kuombwa kusimama na kusalimia waananchi waliokuwa wamekusanyika kando kando ya barabara wakimsubiri.
Hii inadhihirisha CCM kinavyokubalika katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na ukweli kwamba ni chama pekee chenye sera na Ilani sahihi zinazotekelezeka.
Matukio hayo yalianza kujitokeza baada ya Dk. Sheni kufanya mkutano wake wa kwanza wa kampeni katika kijiji cha Chakama, jimbo la Nanyumbu na kumnadi Dunstan Mkapa anayegombea kiti cha ubunge wa jimbo hilo.
Pia katika mkutano huo, uliohudhuriwa na mamia ya wananchi, Dk. Sheni alimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Masasi, Raynald Mrope.
Baada ya mkutano huo, msafara wa mgombea huo uliokuwa na magari yasiyopungua 10, uliondoka kwenda jimbo la Lulindi na ulipofika kijiji cha Mbuyuni saa 6.55 mchana, ulisimama na Dk. Sheni kupata wasaa wa kusalimiana na wananchi waliokuwa wamekusanyika kando kando ya barabara kuu iendayo Newala.
Mbali na kusaliamiana nao Dk. Sheni alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea wa kiti cha Urais, Jakaya Kikwete, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Suleiman Kumchaya.
Saa 7:20 alasiri, msafara uliingia katika kijiji cha Namombwe,Kata ya Mchauru na Dk. Sheni kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Muungano.
Katika mkutano huo, Dk. Sheni alielezea kwa kina mafanikio ya serikali zote tangu uhuru na kumalizia kwa kuinadi Ilani ya Uchaguzi huku akielezea na mwekeleo na matarajio iwapo CCM itapewa ridhaa kwa mara nyingi kuongoza dola.
Sambamba na hilo, pia Dk. Sheni alipokea wanachama 168 kutoka kambi ya upinzani ambao waliamua kujiunga na CCM baada ya kubaini kwamba vyama vyao havina malengo wala mwekekeo wenye kutoa matumani kwa wananchi.
MSAFARA KUZUIWA
Baada ya mkutano huo, msafara mgombea huyo ulianza 'kuchanja mbunga'. Lakini mbio hizo zilikwaa kisiki baada ya wananchi wa kijiji cha Nambunga kilichopo njia panda ya wilaya za Masasi na Newala, kuuzuia msafara huo.
Wananchi hao waliokuwa wamevalia sare za CCM wake kwa waume, zikiwa na picha za Kikwete na Rais Benjamin Mkapa walimwomba Dk. Sheni aliyeongozana na mbunge mtarajiwa wa jimbo hilo, George Mkuchika kuwapa neno ili kupoza kiu yao ya kutaka kumskia.
Kama ilivyo kwa mashabiki wengine wa Chama, wananchi hao walihamasika vilivyo huku wakipeperusha bendera za CCM huku wakiimba nyimbo za kusifu CCM na viongozi wake.
Hali hiyo ilimfanya Dk.Sheni kusimama na kupewa kipaza sauti na kuanza kuwasalimu kwa kuwapa 'dozi' za mafanikio ya CCM ikilinganishwa na vyama vya upinzani.
UONGOZI SI MBOGA
Dk. Sheni aliwataharisha wananchi kutofanya majaribio kwa kufanya mabadiliko ya viongozi mithili ya mboga. Alisema kwa kufanya uchaguzi mfano wa mboga ni kulirudisha nyuma taifa ambalo limefikishwa hapo lilipo kutokana na juhudi za waasisi wake.
Pia Dk. Sheni alitumia nafasi hiyo kumnadi Kikwete kwa kumuelezea kuwa ndiye chaguo sahihi kwa wananchi kutokana na sifa alizo nazo zikiwemo za ukada, unyenyekevu, mpenda watu na msomi aliyebobea katika nyanja za kidiplomasia.
Alimuelezea Kikwete kuwa ndiye kiongozi anayeweza kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa katika serikali ya awamu ya tatu kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.
Mbali na wananchi hao kuzuia msafara nyumba zilizoko kando kando ya barabara hiyo zilikuwa zimepambwa kwa picha za wagombea mbalimbali wa CCM zikiongozwa na za Kikwete.
AZUIWA TENA
Saa 9.15 alasiri, msafara huo ulizuiwa kwa mara nyingine na wanakijiji cha Mkoma Moja ambao nao waliomba awasalimie. Kama ilivyo ada, Dk. Sheni hakusita na kupokea kipaza sauti ili kuwapa faraja wananchi hao kwa kuelezea sera maridhawa za CCM za kutaka kuendelea kuongoza Tanzania.
Baada ya hapo msafara uliruhusiwa na wananchi hao lakini ulikumbana na kikwazo kama hicho dakika 15 baadaye katika kijiji cha Nakahako.
Mgombea mwenzaalilazimika kusimama na kuwasalimia wananchi hao waliokuwa na shauku naye ambapo pasina kuchelewa, aliwaomba kuichagua CCM ili iendelee kuongoza nchi.
Hali hiyo iliendelea ambapo saa 9:45, wananchi wa walifanya hivyo kuomba neno kutoka kwake. Dk. Sheni alitumia nafasi hiyo 'kuwafunda' kutofanya majaribio katika kuchagua viongozi wa nchi.
Kizuizi kingine kilijitokeza kijijini Chihangu ambako mbali ya wananchi kumuomba Dk. Sheni azungumze nao, mmoja wa wanachama wa CUF alihamasika na kuamua kurudisha kadi yake papo kwa hapo.
Akiwa eneo hilo, Dk. Sheni alimnadi Kikwete huku akiwaonyesha picha za mgombea huyo zilizokuwa zimeshikiliwa na wananchi hao huku akiwauliza: "Mna muona ...ametulia?....basi chagua Kikwete na mimi ndiye mgombea Mwenza," matamshi ambayo yaliwafanya wananchi kuhamasika na kushangilia.
'Simama simama' hiyo ilihitimishwa na mkutano uliofanyika katika kijiji cha Kitangari kuanzia saa 10.31 ambako nako jumla ya wanachama wa upinzani 215 wakiwemo 55 kutoka CUF walitangaza kujiunga na chama tawala.
Katika mkutano huo, uliofurika mamia ya wakazi wa eneo hilo, Dk. Sheni mbali ya kumwaga sera na Ilani ya Uchaguzi, pia aliwatahadharisha wananchi na watu wanaowapotosha kwa kutoa matamshi ya kutaka kuwepo kwa serikali tatu.
Alisema matamshi kama hayo yanalenga katika kuibua ghasia na vurugu na hasa ikizingatiwa kwamba tayari wananchi walishaafiki suala la kuwepo kwa serikali mbili na kudumisha muungano.
Mkutano huo ulimalizika jioni na msafara wa Dk. Sheni kuelekea wilayani Tandahimba kuanza huku giza likiwa limeingia.
Licha ya giza hilo, wananchi katika maeneo mbalimbali waliendelea kuusubiri msafara huo na kila ulipopita walipunga mkono huku wakishangilia.
Hali hiyo, iliendelea kujitokeza hadi msafara huo ulipoingia mjini Tandahimba na Dk. Sheni kupokewa katika ofisi za CCM wilayani Tandahimba takribani saa mbili usiku.
Shughuli za kuomba ridhaa kwa wananchi ziliendelea siku inayofuatia kwa Dk. Sheni kufungua shina la wakereketwa la "Wana Kikwete" kwa kupandisha bendera ya CCM.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza vijana wa eneo hilo kwa kuanzisha shina hilo, ambalo aliwataka walitumie katika kudumisha amani na mshikamano.
Aliwapongeza vijana hao kwa kuanzisha shamba la ushirika la kilimo cha korosho, kitendo alichosema kinapaswa kuigwa na wananchi wengine wilayani humo.
Katika kijiji cha Maheka, Dk. Sheni alipokewa kwa kuvikwa mgolole na wazee ikiwa ishara ya kukubalika na kupewa heshima ya mzee wa eneo hilo.
Katika mkutano huo, Dk. Sheni na Mkuchika kwa nyakati tofauti walielezea mchango wa wilaya hiyo katika harakati za kudai Uhuru na ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika licha ya kuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo TANU ilichipuka.
Kutokana na hilo, walisema wilaya hiyo kamwe haiwezi kwenda kwa wapinzani ambao hawaenzi juhudi zilizofanywa na waasisi wa taifa la Tanzania.
Akiwa katika kijiji cha Nyundo jimbo la Mtwara Vijijini, mgombea mwenza alimnadi Hawa Ghasia katika mkutano uliofurika wananchi kwa kumuelezea kuwa ni chagua la CCM aliyesimamishwa kwa ajili ya kuliletea maendeleo jimbo hilo.
Baada ya mkutano huo, msafara wa Dk. Sheni ulikumbwa kwa mara nyingine na vizuizi katika kijiji cha Nalunga, ambako mwananchi mmoja alijitokeza na bango lililosomeka kwamba 'Tunaomba Tukuone'.
Pia alisimamishwa katika vijiji vya Njengwa, Mnima na Mango Pacha Nne kabla ya kuhutubia kijijini Dihimba ambako alipokea wapinzani 43 wakiwemo 34 kutoka CUF.
Alihitimisha mikutano yake ya kampeni kwa kusalimiana na waanchi wa Mikindani na baadaye kuhutubia katika mkutano mkubwa uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa ambako nako alipokea wanachama wapya 120 wakiwemo kutoka kambiza upinzani.
PONGEZI KWA WANA MTWARA
Katika mikutano hiyo, Dk. Sheni hakusita kutoa pongezi kwa uongozi wa mkoa wa Mtwara kutokana na mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la pato la mkoa kutoka sh. bilioni 255.6 mwaka 2000 hadi sh. bilioni 430.8 mwaka jana.
Ongezeko la mazao ya chakula ukiwemo muhogo kutoka tani 300,809 mwaka 1995/1996 hadi tani 469,176 msimu wa mavuno wa mwaka 2004/2005.
Pia uzalishaji katika kilimo cha korosho uliongezeka kutoka tani 49,107 mwaka 1995/1996 hadi tani 51,219 mwaka 2002/2003.
Mavuno ya samaki nayo yalipanda kutoka tani 88,225 zenye thamani ya sh. 39,893,623 mwaka 1995 hadi tani 155,000 zenye thamani ya sh. 85,250,000 mwaka 2004/2005.