UCHAGUZI WA VIONGOZI WA VITONGOJI, MITAA NA SERIKALI ZA VIJIJI, TANZANIA BARA, 2004

 

(Mada iliyowasilishwa na Mhe.  Brig. Jen. (Mstaafu) Hassan Ngwilizi (Mbunge, Naibu Katibu Mkuu, CCM, kwenye Semina ya Wajumbe wa NEC, Wenyeviti na Makatibu wa Mikoa na Wilaya  iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Chimwaga  Dodoma, tarehe 24/8/2004)

 

UTANGULIZI:

 

1.         Mwaka huu utafanyika Uchaguzi katika ngazi za vijiji, mitaa na vitongoji.  Kama ilivyokuwa kwa chaguzi zilizotangulia za mwaka 1993 na 1999, uchaguzi wa mwaka  huu utafanyika kwa kuzingatia mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ambao unazingatia mambo yafuatayo:

 

·        Ushindani wa kidemodrasia wa vyama vya siasa;

·        Utawala wa kikatiba na kisheria;

·        Misingi ya kijamii ambapo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote ya Serikali;

·        Ustawi wa wananchi;

·        Uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi; na

·        Ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za Serikali.

 

  1. Chimbuko la mfumo huu ni mabadiliko ambayo yanaanzia mwaka 1992 ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanyiwa mabadiliko ili kuanzisha rasmi mfumo wa vyama vingi vya siasa.  Marekebisho haya ya Katiba yalielekeza mambo yafuatayo:

 

·        Kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama vingi vya siasa;

 

·        Kutungwa sheria za kusimamia  uendeshaji wa vyama vingi vya siasa;

 

·        Kutungwa sheria na/au kurekebishwa kwa sheria zilizopo kusimamia uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa;

 

·        Kuwa na utaratibu unaotoa haki kwa kila raia kushiriki katika kupiga kura na katika kuchaguliwa katika nafasi za uongozi.

 

  1. Kufuatia marekebisho hayo ya Katiba sheria zifuatazo zilitungwa na/au kuekebishwa ili kuweka kanuni, taratibu na mazingira mazuri ya kuendesha uchaguzi katika mfumo wa vyama vya siasa.

 

 

 

 

 

4.         Mabadiliko hayo yaliweka mazingira mazuri ya kuendesha uchaguzi wa ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngazi za vijiji, mtaa na vitongoji.  Uchaguzi  katika ngazi ya vijiji, mitaa chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1993 na kurudiwa mwaka 1999.  Chaguzi zote   2 yaani uchaguzi wa mwaka 1993 na uchaguzi wa mwaka 1999 uliendeshwa kwa mafanikio ya kuridhisha kwa vile ulitoa fursa kwa vyama vya siasa kushiriki kwa

haki; uhuru na demokrasia licha ya kutokuwepo kwa uzoefu wa kutosha.

 

5.         Sheria zinazoongoza uchaguzi wa Serikali za Mitaa zimegawanyika katika makundi mawili makubwa.  Kundi la kwanza, ni Sheria ya Uchaguzi katika Serikali za Mitaa – “The Local Authoririties Election Act. No. 4 of 1979” ambayo inahusika na uchaguzi wa Madiwani.  Uchaguzi wa kundi hili utafanyika mwaka kesho 2005 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge.  Kundi la pili, ni Sheria za Serikali za Mitaa yaani sheria na. 7 na 8 za 1982, ambazo zinaongoza uchaguzi katika ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji.  Uchaguzi wa kundi hii ndio utafanyika mwezi Novemba mwaka huu.

 

6.         Chini ya Sheria za Serikali za Mitaa na 7 na 8 za 1982, Waziri Mwenye Dhamana na Serikali za Mitaa amepewa madaraka ya kutunga kanuni zitakazoongoza uchaguzi katika ngazi ya kijiji, mtaa na kitongoji.

 

7.         Maandalizi muhimu kwa uchaguzi wa mwaka huu yameanza na yanaendelea vizuri.  Kanuni za uchaguzi za mwaka 1999 zimefanyiwa mapitio na kanuni mpya zitakazoongoza uchaguzi wa mwaka huu zimeandaliwa.  Rasimu za kanuni hizo zimetangazwa kwenye magazeti na kutolewa maoni na mapendekezo katika mikutano ya  wadau wafuatao:

 

·                    Vyama Vyote vya Siasa Vyenye Usajili wa Kudumu.

 

·                    Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa.

 

·                    Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya.

 

·                    Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mistaa, Tanzania  - ALAT.

 

·                    Halmashauri zote, Tanzania Bara.

 

·                    Wananchi kwa ujumla.

 

8.                  Maoni na mapendekezo yaliyotolewa yamegawanyika katika mafungu mawili makubwa:

 

Moja ni maoni na mapendekezo yanayolenga kuziboresha kanuni.  Mbili ni maoni na mapendekezo ambayo yakikubaliwa itabidi uchaguzi uahirishwe hadi hapo mabadiliko yatakapofanyika katika Katiba na Sheria mbalimbali.

 

9.         Kanuni zimefanyiwa marekebisho mbalimbali yanayozingatia maoni na mapendekezo yaliyotolewa.Maoni na mapendekezo yanayohitaji marekebisho ya katiba na sheria yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa utaratibu tofauti.  Zogo linaloendelea kutoka kwa wapinzani linatokana na madai ya kutaka mapendekezo yao ya kurekebisha katiba na sheria mbalimbali yatekelezwe kwanza kabla ya uchaguzi wa mwaka huu kufanyika, jambo ambalo halikubaliki kwa vile litavuruga ratiba ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

 

Misingi ya kisheria ya kutunga Kanuni za Uchaguzi katika ngazi ya Kijiji, Mtaa na Kitongoji:

 

10.       Sheria za Serikali za Mitaa na. 7 na 8 za mwaka 1982 kama zilivyorekebishwa ndizo zinazohusika na uanzishaji na uendeshaji wa vyombo vya Serikali za Mitaa katika vitongoji na vijiji katika maeneo ya  vijijini na katika mitaa katika maeneo ya mijini.  Katika hali hiyo, kifungu cha 30 (4) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Na. 7 ya mwaka 1982 kinaelekeza kuwa kila kitongoji kitakuwa na  Mwenyekiti ambaye atachaguliwa na Mkutano wa wakazi wa Kitongoji.  Kifungu cha 14 (4) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Na. 8 ya mwaka 1982 kinaelekeza kuwa kila Mtaa utakuwa na Mwenyekiti na Kamati yenye wajumbe wasiozidi 6 na wajumbe wasiopungua wawili ni lazima wawe wanawake.  Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Mtaa watachaguliwa na Mkutano wa Wakazi wa Mtaa.

 

11.             Kwa upande wa Kijiji, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) katika kifungu cha 25 inaelekeza kuwa kila kijiji kitakuwa na Halmashauri ya Kijiji. Kifungu cha 56 (1) kinaelekeza kuwa Halmashauri ya Kijiji itakuwa na wajumbe wasiopungua 15 na wasiozidi 25 kama ifuatavyo:

 

 

 

(a)          Mwenyekiti wa kijiiji atakayechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.

 

(b)         Wenyeviti wa Vitongoji katika Kijiji.

 

(c)         Wajumbe wengine watakaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji wakiwemo wanawake ambao idadi yao haitapungua robo ya wajumbe wote wa Halmashauri ya Kijiji.

 

12.    Sheria imempa Waziri Mwenye Dhamana ya Serikali za Mitaa jukumu la kuandaa Kanuni zitakazofuatwa katika kuwachagua viongozi wa Vitongoji, Mitaa na Serikali za Vijiji.  Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji zimetungwa chini ya kifungu cha 30 (4) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Na. 7 ya mwaka 1982.  Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti na Kamati ya Mtaa zimetungwa chini ya kifungu cha 70 (c) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Na. 8 ya mwaka 1982.  Kanuni za Uchaguzi wa Halmashauri ya Kijiji zimetungwa chini ya kifungu cha 56 (3) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Na. 7 ya mwaka 1982.

 

Misingi iliyozingatiwa Katika Kutunga Kanuni:

 

13.       Ipo misingi ya Kikatiba, Kisheria na Kiutawala ambayo imezingatiwa katika kutunga Kanuni hizi.  Misingi hiyo ni pamoja na:

 

·        Kutumia demokrasia katika kuwapata viongozi ambao kweli ni wawakilishi wa wananchi;

 

·        Kutoa fursa kwa kila mwananchi kushiriki katika kuchaguliwa kuwa kiongozi na pia katika kuchagua viongozi;

 

·        Kurahisisha utaratibu wa uchaguzi;

 

·        Kuepuka gharama zisizo za lazima.

 

·        Kuwa na utaratibu wa uchaguzi ulio wazi na wa haki wenye kumwezesha mgombea kukata rufaa ikiwa atakuwa na malalamiko dhidi ya mwenendo wa uchaguzi.

 

·        Kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

 

·        Kuhakikisha kwamba kwa kutumia demokrasia tunampata kiongozi mwadilifu na anayezingatia maadili ya utawala bora.

 

 

14.       Vile vile ipo misingi iliyozingatiwa ili kuhakikisha kuwa uchaguzi katika ngazi ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji unakuwa wa haki, huru na wa kidemokrasia.  Misingi hiyo ni pamoja na:

 

·                    Kuwepo kwa mfumo madhubuti wa uandikishaji wa wapiga kura, kama ibara ya 5 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza.  Misingi hiyo ni pamoja na kuhakikisha uandikishaji wa wapiga kura, kuwepo kwa taratibu rahisi za uandikishaji n.k.

 

·                    Kuwepo kwa utaratibu mzuri wa uandikishaji wa vyama vya siasa na wagombea, ambapo vyama vinakuwa na uhuru wa kuteua wagombea kwa kuzingatia katiba za vyama vyao.

 

·                    Kuwepo kwa uhuru wa vyama na wagombea kufanya mikutano ya kampeni ambayo inaendeshwa bila vitisho, fujo, woga na njia nyingine za vitisho.

 

·                    Kuwa na utaratibu mzuri wa kupiga kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi.  Chini ya utaratibu huu lazima kuwepo na mahali pa kufaa pa kupigia kura ambapo panafikika na wapiga kura wote.  Vile vile utaratibu wa kupiga kura lazima uhakikishe kwamba kura zinahesabiwa na kutangazwa katika mikutano ya uchaguzi na hati za matokeo zimetolewa na kuthibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi mbele ya wagombea au wawakilishi wao.

 

·                    Kuwepo kwa uhuru wa wagombea na vyama vya siasa na vyombo vya habari wa kujieleza;

 

·                    Kuwepo kwa uhuru wa kupata taarifa kuhusu uchaguzi na uendeshaji wake ikiwa ni pamoja na kanuni na taratibu zinazotumika.

 

·                    Kuwepo uhuru wa kuuliza na kupeleka malalamiko na haki ya kukata rufaa endapo taratibu hazikufuatwa.

 

MAPITIO YA KANUNI ZA UCHAGUZI KATIKA NGAZI YA KIJIJI, MTAA NA KITONGOJI

 

Uandikishaji Wapiga Kura:

 

15.       Kama ilivyo kawaida  ya uchaguzi wowote inafaa kuwa na kumbukumbu za wapiga kura katika kila Kitongoji, Kijiji na Mitaa.  Rasimu za kanuni zinaweka utaratibu wa kuandaa orodha ya wapiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa umri wa miaka 18 au zaidi na wenye sifa za kupiga kura.  Utaratibu utakaotumika wa kuandaa orodha hiyo ya wapiga kura ni tofauti na ule unaotumika katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

 

16.       Chini ya kanuni hizi uandaaji wa orodha ya wakazi wa vijiji, mtaa na vitongoji itafanywa na Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji.  Utaratibu utakaotumika sio wa wakazi kwenda katika vituo kujiandikisha kama ilivyo kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani bali ni kwa maafisa husika kuwaandikisha wapiga kura (compilation) kutoka katika Daftari la Wakazi wa Kijiji, Mtaa au Kitongoji na kutoa fursa kwa pingamizi endapo kuna mkazi hakuandikishwa au asiyestahili ameandikishwa.

 

17.       Yapo mapendekezo na madai kwamba uchaguzi wa vijiji, mitaa na vitongoji uahirishwe ili utaratibu wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ndio utumike badala ya utaratibu uliofafanuliwa.  Zipo sababu za kimsingi za kuendelea kutumia utaratibu tulioufafanua.  Kwanza uchaguzi katika ngazi ya kijiji, mtaa na kitongoji unafanyika katika mikutano ya wakazi hivyo wananchi wote wanajuana.  Pili, kumbukumbu za kudumu za wakazi husika zipo katika madaftari ya wakazi wa vijiji, mitaa na vitongoji, ambayo ndio yatatoa orodha ya wapiga kura.  Tatu, wakazi wa maeneo husika watapata fursa ya kutoa pingamizi ili kuhakikisha kwamba watakaopiga kura ni wale tu wenye sifa na wanaostahili.  Mwisho, endapo uchaguzi utaahirishwa ili kusubiri Daftari la Wapiga Kura utakuwa na athari kubwa katika  ratiba ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani

 

Mipaka ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji:

 

18        Jukumu la kuandikisha wakazi wa vijiji, mitaa na vitongoji ili washiriki katika mikutano ya uchaguzi linakwenda sambamba na suala la kuweka na kutangaza majina na mipaka ya maeneo husika. Kila Mkurugenzi anapaswa kutangaza majina na mipaka husika ili itambulike sio tu kwa wasimamizi bali pia kwa wakazi wa kawaida wa vijiji, mitaa na vitongoji.  Jukumu la kuweka mipaka hii ni la Halmashauri husika.  Kabla ya kuandikisha vijiji na kuweka mgawanyo wa vitongoji na kugawa kata za mijini katika mitaa, Halmashauri husika inapaswa kuweka na kutunza kumbukumbu ya mipaka ya maeneo husika.  Kanuni zinawaelekeza Wakurugenzi kutangaza kwa majina, mipaka na maeneo ya vijiji, mitaa na vitongoji wakati wa uchaguzi ili iweze kufahamika kwa wasimamizi, wagombea na wakazi wa maeneo husika.

 

HATUA ZA AWALI YA UCHAGUZI:

 

Tangazo la Waziri

 

19.       Waziri Mwenye Dhamana ya Serikali za Mitaa atatoa tangazo la uchaguzi kwa umma katika magazeti ya Kiswahili na Kiingereza siku 90 kabla ya siku ya uchaguzi.

 

 

Maelekezo ya Uchaguzi:

 

20.       Baada ya Tangazo la Waziri, Mkurugenzi wa Halmashauri atatoa maelekezo kuhusu uchaguzi siku 28 kabla ya siku ya uchaguzi itakayotaja masuala yafuatayo;-

 

(a)               Tarehe ya kufanyika mikutano ya uchaguzi;

 

(b)               Tarehe, muda na mahali pa kufanyika mikutano ya uchaguzi (ambayo itafanyika muda wowote kati ya saa 2.00 asubuhi na saa 10 jioni).

 

(c)               Kuwataka wakazi wote wenye sifa za kupiga kura wahudhurie mkutano wa uchaguzi siku ya uchaguzi;

 

(d)               Kuwataka wakazi wenye umri wa  miaka 21 au zaidi wanaotaka  kugombea nafasi za uongozi katika kijiji, mtaa na kitongoji wajaze fomu za kugombea zinazopatikana kwenye ofisi za msimamizi msaidizi wa uchaguzi.

 

(e)               Tarehe na muda wa kuchukua na kurudisha fomu za maombi  ya kugombea uongozi kwa msimamizi wa uchaguzi na kuagiza kwamba muda wa kuchukua na kurudisha fomu za kugombea hautazidi siku (7).

 

(f)                 Siku ambayo uteuzi utafanyika na mahali pa matangazo ambapo fomu za wagombea zitabandikwa ili wapiga kura wazione;

 

(g)               Muda wa kutoa pingamizi dhidi ya uteuzi na kusikilizwa kwa pingamizi;

 

(h)               Tarehe ya kusikiliza rufaa dhidi ya uamuzi wa msimamizi msaidizi wa uchaguzi;

 

(i)                 Kipindi cha kuendesha mikutano ya kampeni za uchaguzi ambacho hakitazidi siku saba na masuala mengineyo yanayohusiana na uchaguzi.

 

Sifa za Wapiga Kura:

 

21.       Watu  watakaoruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa vijiji,  mitaa na vitongoji ni wale tu wenye sifa zifuatazo:

 

(a)     Raia wa Tanzania;

 

(b)         Wakazi wa kawaida wa eneo linalohusika (kitongoji/mtaa/kijiji);

 

(c)         Wenye umri wa miaka 18 au zaidi;

 

(d)         Wasio na ugonjwa wa akili.

 

Sifa za Wagombea:

 

22.       Wagombea wa nafazi zote za uongozi katika kitongoji, mtaa na kijiji wanatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:

 

(a)       Wawe raia wa Tanzania;

 

(b)       Wawe wametimiza umri wa miaka 21 au zaidi;

 

(c)       Wawe na kipato halali cha kuwawezesha kuishi;

 

(d)         Wawe na uwezo wa kuandika na kusoma Kiswahili au Kiingereza;

 

(e)         Wawe wanachama na wadhaminiwa wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria;

 

(f)           Wawe wakazi wa kawaida wa maeneo yanayohusika (kitongoji/mtaa/kijiji);

 

(g)         Wasiwe wanadaiwa kodi yoyote ya Serikali Kuu au Serikali za Mitaa;

 

(h)         Wasiwe wamehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupewa adhabu ya kifo au kifungo cha miezi 6 au zaidi kwa makosa ya jinai.

 

(i)           Wasiwe na ugonjwa wa akili.

 

23.       Pengine itakuwa vema kutoa ufafanuzi wa kisheria ya

baadhi ya sifa za wagombea na wapiga kura:

 

(i)                 Raia wa Tanzania:  Ibara ya 5 ya Katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kwamba raia yeyote wa Tanzania anaweza kushiriki katika uchaguzi wowote kama  mpiga kura au mgombea wa nafasi ya uongozi.  Ili mtu yeyote aweze kuipata haki ya kikatiba ni sharti awe raia wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, (The Citizenship Act No. 6 of 1995”).

 

Sheria ya Uraia – “The Tanzania Citizenship Act. No. 6 of 1995 inatambua aina zifuatazo za kupata uraia wa Tanzania:

 

 

 

(a)                     Raia wa Tanzania kwa Kuzaliwa:

 

             Sheria ya Uraia kifungu cha 5 inaelekea kwamba mtu yeyote aliyezaliwa Tanzania siku ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar atakuwa raia wa Tanzania endapo wazazi au mojawapo wa wazazi wake ni raia wa Tanzania.

 

(b)                     Uraia wa Tanzania kwa tajinsi (nasturalization)

 

              Kwa mujibu wa kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Uraia, raia wote wa kigeni wanaoishi nchini wanaweza kuomba kutangazwa kuwa raia wa Tanzania.

 

(c)                     Uraia kwa kuandikishwa:

 

              Sheria ya auraia inatambua vile vile kupata uraia kwa kuomba kuandikishwa.

 

(ii)               Mkazi wa kawaida wa eneo husika:

 

Neno mkazi wa kawaida limefafanuliwa kisheria katika kanuni hizi.  Aya ya ufafanuzi inaelekeza kwamba mkazi ni raia wa Tanzania mwenye kaya au anayeishi katika kaya iliyopo katika eneo husika. 

Hata hivyo kwa madhumuni ya kanuni hizi mkazi yeyote atakuwa na haki ya kugombea nafasi ya uongozi au kupiga kura katika Kijiji, Mtaa au Kigongoji kimoja tu.

 

24.       Utaratibu wa uteuzi: 

 

Kanuni za uchaguzi katika ngazi ya Kijiji, Mtaa na Kitongoji zinaelekeza utaratibu ufuatao wa uteuzi:-

 

·                    Siku ya uteuzi:-          Msimamizi wa uchaguzi atafanya      uteuzi wa wagombea siku zisizopungua kumi na tano (15) kabla ya tarehe ya uchaguzi.

 

·                    Uteuzi utafanywa kutokana na fomu zilizowasilishwa;

 

·        Baada ya uteuzi msimamizi wa uchaguzi atabandika mahali pa matanagazo  majina ya wagombea wenye sifa na wasio na sifa za kugombea nafasi za uongozi katika ngazi ya kijiji, mtaa na kitongoji.

 

·        Ikiwa hakuna mwombaji hata mmoja aliyejitokeza au waombaji wote waliojitokeza au kumetokea kifo au sababu nyingine yoyote basi utaratibu wa uteuzi utarudiwa;  ambapo msimamizi wa uchaguzi atatengua uteuzi na kupanga tarehe nyingine ya uchaguzi ambayo sio zaidi ya siku 10 tangu tarehe ya kutengua uteuzi uliofanyika.

 

·        Pingamizi dhidi ya uteuzi:  Pingamizi kwa kuteuliwa au kutoteuliwa mgombea litawasilishwa kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi masaa 24 tangu uteuzi ulipofanyika ili kumtaka akangalie upya uamuzi wake na kutoa uamuzi katika muda wa siku 2 tangu siku ya kupokea pingamizi;

 

Kamati ya Rufaa:

 

25.       Kanuni zinaelekeza kwamba kutakuwepo na kamati ya rufaa ambayo jukumu lake ni kusikiliza malalamiko ya uteuzi wa uchaguzi katika kila Halmashauri.  Kamati hii ya Rufaa itateuliwa na kupewa maelekezo na Katibu Tawala wa Mkoa na itajumuisha wajumbe wafuatao:-

 

(i)           Katibu Tawala wa Wilaya ambaye atakuwa Mwenayekiti;

 

(ii)         Viongozi wawili (2) wa dini kutoka madhehebu tofauti ambao watateuliwa na Katibu Tawala wa Mkoa baada ya kupokea mapendekezo kutoka madhehebu yaliyomo katika eneo la Halmashauri.

 

(iii)       Afisa wa umma kutoka eneo la Halmashauri husika atakayeteuliwa na Katibu Tawala Mkoa.

 

(iv)        Katibu ambaye atateuliwa na Katibu Tawala Mkoa kutokana na maafisa wa umma waliopo katika eneo la Halmashauri husika.

 

Utaratibu wa Kampeni za Uchaguzi:

 

26.       Mgombea au mtu yeyote aliyeruhusiwa na mgombea au Chama cha Siasa cha mgombea anaruhusiwa kuitisha na kuhutubia mikutano ya kampeni itakayofuata ratiba zilizoratibiwa katika utaratibu ufuatao:

 

·              Kampeni zitaanza siku moja baada ya siku ya uteuzi wa wagombea na zitamalizika siku moja kabla ya siku ya uchaguzi.

 

·              Mgombea , chama cha siasa, au mwakilishi wa mgombea wataandaa na kuwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi ratiba ya kampeni za uchaguzi.

 

·              Ratiba za mikutano ya kampeni ambayo imeratibiwa na msimamizi wa uchaguzi, zitakuwa taarifa rasmi za mikutano ya kampeni na zitawasilishwa kwa Jeshi la Polisi ili kuhakikisha ulinzi na usalama katika mikutano hiyo ya kampeni za uchaguzi.

 

Siku   ya Uchaguzi:

 

27.             Kazi ya kwanza ya mkutano wa uchaguzi itakuwa ni kumchagua mjumbe mmoja ambaye siyo mgombea wa nafasi yoyote, kuwa Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo.  Baada ya kuchagua Mwenyekiti mpangilio wa uchaguzi utaendelea kwa utaratibu ufuatao:

 

(a)       Kwanza utafanyika uchaguzi wa Wajumbe wa Kamati ya Mtaa/Halmashauri ya Kijiji kutokana na kundi la wagombea wote, wanawake na wanaume.

 

(b)       Kura zitahesabiwa ili wagombea wanawake ambao hawatapita waweze kuingia katika uchaguzi wa kundi la viti maalum;

 

(c)       Utafanyika uchaguzi wa viti maalum vya wajumbe wanawake.

 

(d)       Mwisho utafanyika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa/Kijiji.

 

Kwa upande wa uchaguzi wa kitongoji utafanyika uchaguzi wa Mwenyekiti wa kitongoji tu.

 

Utaratibu wa Uchaguzi:

 

28.       Uchaguzi wa Mwenyekiti utakuwa kama ifuatavyo:-

 

·                    Iwapo mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji, Mtaa au Kijiji ni mmoja tu, basi atapigiwa kura za siri za “NDIYO” au “HAPANA” na ikiwa kura za “NDIYO” zitakuwa zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa basi atatangazwa kuwa Mwenyekiti.

 

·                    Ikiwa kura za “NDIYO” zitakuwa chini ya nusu ya kura zilizopigwa basi utaratibu wa uchaguzi utaanza upya (yaani kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi, kujaza fomu, kufanya uteuzi n.k.).

 

·                    Endapo hakuna mgombea hata mmoja aliyejitokeza au kama wagombea wote waliojitokeza hawana sifa zinazostahili kugombea utaratibu wote wa uchaguzi utaanza upya.

 

·                    Endapo baada ya kupiga kura wagombea wawili au zaidi watakuwa wanaongoza kwa kura sawa, kura zitapigwa tena kwa wale wagombea ambao kura zao zitakuwa zimefungana.

 

 

 

 

29.       Uchaguzi wa nafasi za Wajumbe:

 

·                    Kama idadi ya wagombea wa nafasi za ujumbe wa Halmashauri ya kijiji au Kamati ya Mtaa itakuwa chache kuliko au italingana na nafasi zinazohitaji kujazwa, basi wagombea watatangazwa kuwa wamechaguliwa.

 

·                    Ikiwa idadi ya wagombea itakuwa kubwa kuliko nafasi zinazohitaji kujazwa, kura za siri zitapigwa na watakaopata kura nyingi watatangazwa kuwa wajumbe wa kamati ya Mtaa/Halmashauri ya Kijiji.

 

30.       Kuhesabu kura na kutangaza matokeo:

 

Kura zitahesabiwa na Msimamizi wa Uchaguzi mbele ya wagombea au wawakilishi wao ikiwa watataka kushuhudia zoezi hilo, na matokeo ya uchaguzi yatatangazwa mkutanoni kwa kuanza na wajumbe wa Kamati ya Mtaa /Halmashauari ya Kijiji na kumalizia na Mwenyekiti wa Kamati ya Mtaa/Mwenyekiti wa Kijiji.

 

31.       Malalamiko ya uendeshaji wa uchaguzi: 

 

Mgombea yeyote ambaye hakuridhika na uendeshaji wa uchaguzi atakuwa na haki ya kupeleka malalamiko yake mahakama ya wilaya katika muda wa siku 30 baada ya siku ya kutangaza matokeo ya uchaguzi.

 

32.       Kiapo na uwajibikaji wa wasimamizi wa uchaguzi:

 

Wasimamizi wa uchaguzi watatakiwa kula kiapo cha uaminifu na kutunza siri kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao.  Kanuni zinaelekeza pia kwamba msimamizi atakayekiuka kanuni za uchaguzi atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atapewa adhabu ya faini ya shs. 50,000/= au kifungo cha miezi 12 au vyote faini na kifungo.

 

33.       Watizamaji wa Ndani:

 

Kanuni zinatoa fursa kwa watizamaji wa ndani ili kuhakikisha kwamba uchaguzi ni wa haki, huru na kidemokrasia.

 

34.       Makosa ya Uchaguzi:

 

Kanuni zinaorodhesha makosa yafuatayo ya uchaguzi. Adhabu ya kila kosa itakuwa faini ya shs. 50,000/= au kifungu kwa muda usiozidi miezi kumi na mbili (12).

 

·                    Kuharibu orodha ya wapiga kura;

·                    Kutoa taarifa za uongo kuhusu makazi;

·                    Kuharibu karatasi ya wagombea;

·                    Kugushi karatasi za uteuzi;

·                    Kupiga kura mara mbili;

·                    Kutishia wapiga kura au wagombea ili kuvuruga uchaguzi;

·                    Kuonyesha ishara au mavazi yanayoashiria kumtambulisha mgombea na chama chake cha siasa siku ya uchaguzi;

·                    Kumzuia msimamizi wa uchaguzi  kutekeleza  majukumu yake;

·                    Kukiuka masharti ya kiapo;

·                    Kutenda jambo lolote linalokiuka kanuni hizi.

 

35.       Uchaguzi Mdogo:

 

Nafasi za uongozi huwa wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kifo, kujiuzulu, kukosa sifa za kuendelea kuwa kiongozi n.k. Mara tu zitokeapo nafasi hizi ni lazima zijazwe ili kuendeleza haki ya uwakilishi ya wakazi wa eneo husika.  Kanuni zinaelekeza kwamba Mkurugenzi atatangaza kutokea kwa nafasi wazi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Halmashauri ya Kijiji au Kamati ya Mtaa.  Baada ya tangazo la Mkurugenzi nafasi wazi itajazwa katika muda wa siku 60 tangu kutangazwa. Uchaguzi  mdogo utaendeshwa kwa utaratibu unaotumika kwa uchaguzi wa kawaida.

 

HOJA ZILIZOJITOKEZA KATIKA KUJADILI RASIMU ZA KANUNI ZA UCHAGUZI KATIKA NGAZI YA KIJIJI, MTAA NA KITONGOJI:

 

36.       Hoja, maoni na mapendekezo yafuatayo yalijitokeza katika kujadili Rasimu ya Kanuni hizi:

 

(a)       Uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa vijiji, mitaa na vitongoji uzingatie Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

 

37.       Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakaloandaliwa na Tume ya Uchaguzi halitatumika kwa ajili ya Uchaguzi katika ngazi ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji kwa sababu zifuatazo.

 

·                    Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatumika kwa kuzingatia masharti ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi na 1 ya 1985 na 4 ya 1979 ambazo zinaelekeza kwamba daftari hilo litatumika kuandikisha wapiga kura kwenye uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na sio katika uchaguzi wa viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji.

 

·              Uchaguzi wa viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji husimamiwa na Serikali za Mitaa nazo zina Daftari la kumbukumbu muhimu kuhusu maeneo hayo ya vijiji, mitaa na vitongoji.  Daftari hilo ndilo litatumika kupata orodha ya wapiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji.

 

·              Uchaguzi wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji inafanyika katika mikutano ya wakazi wa maeneo husika.  Wakazi wa maeneo hayo wanajuana hivyo utaratibu uliowekwa kwenye kanuni wa kuandaa orodha ya wapiga kura kwa kushirikisha wananchi unafaa na utaepusha migogoro isiyo ya lazima.

 

·              Daftari la kudumu la wapiga kura bado halijakamilika na endapo litatumika athari yake ni kuahirisha uchaguzi, jambo ambalo litavuruga ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka 2005.

 

(b)      Uchaguzi wa Viongozi wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji Kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi Badala ya Usimamizi Chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

 

38.       Uchaguzi wa viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji husimamiwa na mamlaka za Serikali za Mitaa husika  yaani Mkurugenzi wa Halmashauri ambamo uchaguzi huo unafanyika akisaidiwa na Watendaji wa kata au kijiji  wala siyo watumishi wa Makao Makuu ya OR-TAMISEMI.  Utaratibu huu umewekwa ili kukidhi matakwa ya ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotoa jukumu kwa Vyombo Vya Serikali za Mitaa kusimamia demokrasia katika eneo lake.        Ibara hiyo inaelekza kama ifuatavyo:

 

146. (1)  “Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka   madaraka kwa wananchi.  Vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla.

 

 (2)   Bila ya kuathiri maelezo ya jumla yaliyomo katika ibara ndogo (i) ya ibara hii, hiki chombo cha Serikali za Mitaa, kwa kuzingatia masharti ya sheria iliyokianzisha, kitahusika na shughuli zifuatazo:

                 

(a)               Kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika eneo lake;

(b)               Kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi; na

(c)               Kuimarisha demokrasi katika eneo lake na kuitumia demokrasi kuharakisha maendeleo ya wananchi”.

 

 

 

 

39.       Jukumu hili la kusimamia uchaguzi ni la kiutendaji. Kazi ya

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambayo ina Dhamana ya Serikali za Mitaa, kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa ni kuweka tu Kanuni ya namna uchaguzi huo utakavyoendeshwa na si vinginevyo.

 

40.       Sambamba na hoja hiyo, ipo minong’ono kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri wana utii kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa kuwa ndiyo inayowateua.  Uteuzi wa Wakurugenzi sio wa kisiasa bali unafanywa kwa misingi ya stahili (meritiocracy) kama sera ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma inavyoelekeza.

 

41.       Uchaguzi huu hausimamiwi na Tume ya Uchaguzi kutokana sababu zifuatazo.

·        Uchaguzi huu unafanyika kwenye ngazi ya mtaa, kijiji au kitongoji.  Katika kitongoji wakazi wote waliopo wanafahamiana.  Hii ni tofauti na uchaguzi wa kitaifa ambapo wagombea wanaweza kupigiwa kura kutoka kwenye maeneo ambayo hawakuzaliwa na hawaishi na hawafahamiki.  Ni kwa sababu hii kwamba katika ngazi ya kitaifa wanahitaji chombo maalum kitakacho hakikisha kwamba haki zao zinalindwa.

 

·        Kikatiba, jukumu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, na jukumu la kusimamia uchaguzi katika vijiji, vitongoji na mitaa limepewa vyombo vya Serikali za Mitaa katika ngazi hizo husika.

 

·        Sababu nyingine ni ile haja ya kuzingatia uwezo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya jukumu hili kwa ufanisi.  Kwa mfano, kwa uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji, vitongoji na mitaa, idadi ya wagombea kutoka vyama vya siasa kumi na sita vyenye usajili wa kudumu kama vitasimamisha mgombea mmoja mmoja tu kutoka kila chama kutakuwa na wagombea karibu 1,500,000 ambao kwa uchache husimamiwa na watumishi 12,721 wa Serikali za Mitaa.  Watumishi hawa wamepatiwa mafunzo, wana utendaji wenye maadili ya Serikali na wanaweza kuwajibishwa.  Kwa kuzingatia hali kama hii, ni dhahiri kuwa huu utakuwa ni mzigo mkubwa kwa Tume kuweza kuuhimili.  Kinachotakiwa ni kuwepo kwa utaratibu utakaowezesha uchaguzi kufanyika kwa haraka, kwa urahisi na wenye kuzingatia demokrasia na haki.

 

Mwisho:

42.       Viongozi wa vitongoji, mitaa na serikali za vijiji ni muhimu sana katika mfumo wa utawala wa nchi yetu.  Utawala bora umejengwa katika ngazi hii.  Jambo lingine ambalo pia ni muhimu ni kwamba uongozi madhubuti katika ngazi hii ndio utakaosaidia katika kudumisha umoja na mshikamano wa Taifa letu na hivyo kutuwezesha kuwa na maendeleo ya kweli na yenye kudumu.

 

KIAMBATISHO “A”

 

KAZI ZA MWENYEKITI WA KITONGOJI KWA MUJIBU WA TARATIBU ZILIZOTUNGWA CHINI YA KIFUNGU CHA 112 CHA SHERIA YA SERIKALI ZA MITAA (MAMLAKA ZA WILAYA) NA. 7 YA MWAKA 1982

 

(i)               Kuitunza rejesta ya Wakazi wa Kitongoji na habari nyingine muhimu zinazohusu maendeleo ya Kitongoji kwa Jumla ikiwa ni pamoja na kumbukumbu za vizazi na vifo.

 

(ii)             Kusimamia ulinzi na usalama wa watu na mali za wanaoishi katika eneo lote la Kitongoji.

 

(iii)           Kuhamasisha ulipai wa Kodi na ushuru mbali mbali, kama utakavyoamuliwa na kuwekwa mara kwa mara na Halmashauri ya Wilaya.

 

(iv)           Kusimamia katika eneo lake suala zima la Hifadhi ya Mazingira hususan vyanzo vya maji n.k.

 

(v)             Kusimamia suala zima la Afya katika eneo lake ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Kampeni za afya za Kitaifa, Kimkoa au Kiwilaya dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.

 

(vi)           Kusimamia utekelezaji wa Taratibu za Kilimo na Ufugaji bora ili kuinua hali ya lishe na uchumi wa wakazi wa Kitongoji.

 

(vii)         Kufuatilia na kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapoatiwa nafasi, na kushirikiana na viongozi wa shule katika kudhibiti utoro shuleni.

 

(viii)          Kuhamasisha Elimu ya Watu Wazima.

 

(ix)           Kusimamia na kuwahamasisha wakzi wa Kitongoji katika kutekeleza shughuli za kujitegemea.

 

(x)             Kusuluhisha migogoro midogo isiyostahili kushughulikiwa na Mabaraza ya Kata au Mahakama.

 

(xi)              Kuwakilisha Kitongoji katika Serikali za Kijiji.

 

(xii)         Kuwaongoza na kuwahamasisha wakazi wa Kitongoji washiriki katika Sherehe za Taifa na mikutano ya hadhara itakayoandaliwa na kuitwa na Serikali au Halmashauri.

 

(xiii)       Kutekeleza kazi nyingine atakazopangiwa na Halmashauri ya Wilaya.

 

KIAMBATISHO “B”

 

KAZI ZA MWENYEKITI WA KITONGOJI KWA MUJIBU WA TARATIBU ZILIZOTUNGWA CHINI YA KIFUNGU CHA 56 CHA SHERIA YA SERIKALI ZA MITAA (MAMLAKA ZA MIJI) NA. 8 YA MWAKA 1982

 

(i)                 Kutunza rejesta ya wakazi wote wa Mtaa na habari nyingine muhimu    zinazohusu maendeleo ya Mtaa kwa Jumla ikiwa ni pamoja na kumbukumbu za vizazi na vifo.

 

(ii)               Kusimamia ulinzi na usalama wa watu na mali za  wanaoishi katika eneo la Mtaa.

 

(iii)             Kusuluhisha migogoro midogo isiyostahili kushughulikia na Mabaraza ya     Kata au Mahakama.

 

(iv)              Kuhamisha ulipaji wa kodi na ushuru mbalimbali kama utakavyoamuliwa na kuwekwa mara kwa mara na Halmashauri ya Mji, Manispaa au Jiji.

 

(v)                Kusimamia suala zima la Afya katika eneo lake ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Kampeni za afya za Kitaifa, Kimkoa au Kiwilaya dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa.

 

(vi)              Kusimamia uwekaji wa eneo la Mtaa katika hali ya usafi.

 

(vii)            Kushirikiana na Halmashauri ya Mji, Manispaa au iji kudhibiti   bughudha.

 

(viii)          Kufuatilia na kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye unri wa kwenda shule anapata nafasi ya kushirikiana na viongozi wa shule katika kudhibiti utoro.

 

(ix)              Kuhamaisha elimu ya watu wazima.

 

(x)                Kusimamia na kuhamasisha wakazi wa Mtaa katika shughuli za kujitegemea.

 

(xi)              Kuwaongoza na kuwahamasisha wakazi washiriki katika sherehe za Taifa na mikutano ya hadhara itakayoandaliwa na Serikali au na Halmashauri.

 

(xii)            Kuwakilisha Mtaa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata.

 

(xiii)          Kutekeleza kazi nyingine atakazopangiwa na Halmashauri ya Mji, Manispaa au Jiji.

 

 

 

KIAMBATISHO “C”

 

DAFTARI LA ORODHA A WAKAZI WENYE UMRI WA MIAKA 18 NA KUENDELEA

 

KITONGOJI/MTAA……………………………………………

KIJIJI……………………………………………………………

KATA……………………………………………………………

 

NA.

JINA LA MKAZI

JINSIA (KE/ME)

UMRI

TAREHE YA KUANDIKI-SHWA

SAHIHI YA ANAYEANDI-KISHWA

SAHIHI YA MWANDI-KISHAJI

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

KE =  Mwanamke

 

ME = Mwanamme