HOJA YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MUUNDO WAKE WA SERIKALI MBILI

(Omar R. Mapuri)

 

 

UTANGULIZI

 

Hoja ya Muungano wa Tanzania inasimama juu ya msingi wa sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Sera ya  CCM kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa Tanzania ina ncha mbili; yaani kuulinda na kuudumisha Muungano wenyewe kwa upande mmoja na muundo wa Muungano huo kuwa wa Serikali mbili kwa upande wa pili.

 

CCM inaushabikia Muungano na kupania kuulinda na kuudumisha kwa sababu kwanza inaamini kuwa Muungano huu ni wa watu wenyewe na pili, uliasisiwa na vyama wazazi wake, yaani TANU na ASP.  Zaidi ya hivyo, CCM yenyewe ni matokeo ya Muungano huo na chachu ya kuziimarisha kwani tendo la kuviunganisha vyama vya TANU na ASP kuunda CCM lilitokana na utashi wa kukamilisha hatua za kuunda Muungano.

 

CCM inaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili kwa sababu kwanza ndio ulioamuliwa na waasisi wa Muungano, Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume, na pili umezingatia vya kutosha uhalisi wa mambo wa nchi kubwa na ndogo kuungana.  Muundo huo ndio unaohakikisha umadhubuti wa Muungano wenyewe bila ya nchi ndogo (Zanzibar kwa muktadha huu) kumezwa na nchi kubwa (Tanganyika).

 

CCM inajivunia Muungano huu na muundo wake wa Serikali mbili kwani hata baada ya miaka 40 ya kuundwa kwake bado ndio mfano pekee wa Muungano uliofanikiwa wa nchi huru zilizoungana katika Bara la Afrika.  Zaidi ya yote, Muungano huu umeweza kuhimili misukosuko yote ya ndani uliyokumbana nayo ambayo ingeweza kuudhofisha au hata kuuvunja.

 

Pamoja na makelele mengi ya kisiasa yenye kuulalamikia, Muungano huu na muundo wake wa Serikali mbili unaungwa mkono na Watanzania walio wengi.  Ushahidi wa kitakwimu utatolewa katika makala haya kwamba muundo wa Serikali mbili ndio unaotakiwa na Watanzania walio wengi, na muundo wa Serikali tatu unaopigiwa debe sana na vyama vya upinzani na baadhi ya wasomi ndio unaokataliwa na Watanzania wengi kuliko muundo mwingine wowote.

 

Kabla ya kuendelea na hoja, inafaa katika hatua hii kutazama maandiko rasmi ya kisera ya CCM kuhusu Muungano na muundo wake, kama yalivyo katika Ilani za Uchaguzi za CCM za 1995 na 2000.

 

Ibara ya 47 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 1995 inasomeka ifuatavyo:

 

47.            Sera ya Kuimarisha Muungano

Muundo wa Muungano, ambao unakubaliwa na CCM, ni Muungano wenye Serikali mbili:  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Sera hii imethibitishwa mwaka 1994 wakati wanachama wetu walio wengi walioshiriki katika kura za maoni kote nchini walitaka sera hii iendelee.  Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM itaendelea kudumisha Muungano wa Tanzania katika muundo wa Serikali mbili.

 

Kwa upande wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2000, ibara zinazozungumzia kuimarisha Muungano ni za 116 na 117 ambazo zinasomeka ifuatavyo:-

 

116.   Umoja wa kitaifa wa Watanzania ambao umedumu kwa kipindi kisichopungua miaka 36 unatokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ulizaa Tanzania.  Katika kipindi chote hicho muundo wa muungano ambao umeendelea kukubaliwa na Chama Cha Mapinduzi ni muungano wenye Serikali mbili:  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.  Sera hii imeendelea kuthibitishwa na wanachama wa CCM na wananchi kwa jumla.

 

117.       Katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2000 – 2005) Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhakikisha kuwa mafanikio yaliyorithiwa kutoka kwa Waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa, Mwalimu J.K. Nyerere na Makamu wake wa Kwanza Sheikh Abeid Aman Karume yanaendelezwa na kulindwa kwa kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa huru, Taifa lenye Umoja, Udugu na Mshikamano na nchi yenye amani na utulivu.  Aidha, muundo wa Muungano utaendelea kuwa wa Serikali mbili: yaani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

Hivyo ndivyo inavyosema Sera ya CCM kuhusu Muungano na muundo wake.  Ni muhimu hili kuwekwa sawa kwani wapinzani wa CCM, hasa kule Zanzibar, hupenda kujichukulia uhuru wasiopewa wa kuisemea CCM wapendavyo wao.  Hupenda sana kuipotosha sera hii kwa kuinukuu kilaghai kwamba eti “ni ya Serikali mbili kuelekea moja”.  Kauli hiyo imewahi kutoka katika vikao vya CCM kama kauli nyingi nyenginezo zilivyowahi kutoka.  Kwa mfano, Bunge, likiwa na Wabunge wa CCM watupu liliwahi kupitisha azimio la kutaka kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano”.  Lakini baada ya yote hayo na kauli zote zilizosemwa na/au kuandikwa, ulipofika wakati wa kutunga sera rasmi, Chama kiliamua bila ya kigugumizi kuendelea na sera ya Muungano wa Serikali mbili na kuiweka kwa uwazi na bila ubabaishaji katika Ilani za Uchaguzi.

 

NGUZO ZA MUUNGANO

 

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulijengwa juu ya msingi wa kijiografia na kihistoria uliowafanya watu wa maeneo haya kuwa wamoja, ndugu, wenye tamaduni zilizoingiliana na hata wenye utashi wa kisiasa uliofanana.

 

Juu ya msingi huo, zimesimama nguzo nne zinazouhimili Muungano huo.  Nguzo ya kwanza ambayo imejengeka kwa muda mrefu katika historia ni kwamba Muungano huu ni wa watu wenyewe.  Nguzo hii inaupa Muungano uhalali wa kijamii na hata wa kisiasa.  Nguzo ya pili ni msukumo wa kujenga umoja wa Afrika.  Nguzo hii inaupa Muungano uhalali wa kisiasa za kimataifa.  Nguzo ya tatu ni Hati ya Muungano ambayo iliujengea Muungano uhalali wa kisheria ambao unaendelezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984.  Nguzo ya nne inayouhimili Muungano na ambayo inaendelea kujengeka ni ya uendelevu wa Muungano wenyewe.  Muungano wa Tanzania umeshatimiza miaka 40 ukiendelea kuimarika.  Umeweza na unaendelea kuhimili misukosuko mingi, ambapo kila unapoingia kwenye tanuri la misukosuko, unaibuka ukiwa imara zaidi.  Nguzo hii inaupa Muungano uhalali wa kisiasa za ndani.

 

Sasa tuzitazame nguzo hizi moja moja.

 

Nguzo Ya Umoja wa Watu Wenyewe

 

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umejengeka kutokana na mahusiano ya dahari na karne baina ya watu wa visiwa vya Zanzibar na mwambao wa Afrika ya Mashariki, hasa Mrima ambayo ni sehemu kubwa ya Tanzania Bara ya sasa.

 

Kabla ya Kuja Kwa Wageni Toka Nje ya Afrika

 

Wanahistoria (mfano Ingrams) wakijenga hoja kutokana na maandiko ya kale ya Periplus (karne ya kwanza AD) na ngano za watu wa kale, wanakubaliana kwamba watu wa kwanza kabisa kufika katika visiwa vya Zanzibar ni Waafrika kutoka Mrima katika harakati za uvuvi.  Ushahidi wa kiakiolojia wa hivi karibuni umethibitisha usahihi wa imani hiyo.

 

Wakati wa Himaya ya Zenj

 

Lakini hata baada ya kuja kwa wageni kutoka nje ya Afrika, mahusiano ya watu wa pande hizi mbili siyo tu yaliendelea, bali yalizidi kuimarika hasa kutokana na kuongezeka kwa ubora wa teknolojia ya usafiri wa baharini.  Himaya ya Waajemi (Washirazi) katika eneo hili ambayo baadhi ya wanahistoria wanaiita Himaya ya Zenj (Zenj Empire) ilipojengeka kutokana na ujio wa wale Ndugu saba wa  El-Hasa mnamo karne ya 13 ambao walianzisha tawala katika vituo mbali mbali vya mwambao wa Afrika Mashariki (mfano Kilwa, Barawa, Lamu, Unguja, Pemba, n.k.), maingiliano ya watu wa maeneo haya yaliendelea bila ya vikwazo.

 

Wakati wa Himaya ya Biashara ya Zanzibar

 

Mnamo karne za 16 hadi katikati ya 19, ilijengeka Himaya ya Kibiashara ambayo kitovu chake kilikuwa Zanzibar.  Himaya hiyo iliyojumuisha biashara ya watumwa, vipusa na viungo, ilienea hadi maeneo ya Maziwa Makuu kwa upande wa Kaskazini Magharibi na maeneo ya Ziwa Nyasa na Mto Ruvuma kwa upande wa Kusini mwa Tanzania ya leo.  Katika kitabu chake cha Slaves, Spices & Ivory in Zanzibar Profesa Abdul Sheriff anazungumzia dhana ya Bara ya Zanzibar (The Hinterland of Zanzibar) akiwa na maana ya eneo la Bara lililokuwa chini ya ushawishi wa Zanzibar (bila shaka na Sultani wake), ambalo kwa kiasi kikubwa ni hili hili eneo la Tanzania Bara ya leo.  Dhana hiyo ilipewa methali maarufu ya: “Inapopigwa ngoma Zanzibar, wanacheza katika Maziwa Makuu”.

 

Maelezo haya yanajaribu kujenga hoja kwamba eneo ambalo leo linaitwa Tanzania, kwa kiasi kikubwa ndilo lililokuwa Himaya ya Kibiashara ya Zanzibar ya enzi hizo.  Kwa maneno mengine nchi hii ilikuwa moja toka enzi hizo ingawa yenye mipaka hafifu.  Watu wa eneo lote hili waliunganishwa na harakati za biashara.  Biashara ya utumwa iliwafanya wa huku waende kule na wa kule waje huku, ingawa katika mazingira ya uchungu.  Watumwa walichukuliwa Bara na kupelekwa visiwani Zanzibar ambako vizazi vyao vimeendelea hadi leo na kufanya sehemu kubwa ya Wazanzibari.  Kwa upande mwengine, wako wafanyabiashara ya watumwa walioanzia Zanzibar na kuhamia Bara na kufanya maskani yao huko.  Vizazi vyao vinaendelea hadi leo na wamekuwa sehemu ya jamii ya Watanzania Bara.  Hivi sasa, katika mazingira ya uhuru, watu wa kila upande kati ya pande mbili hizi wanaendelea kuhamia na kuweka maskani katika upande wa pili bila ya vikwazo.

 

Utenganishi wa Wakoloni wa Kizungu

 

Kitendo kilichowatenganisha watu wa pande hizi ni kile cha wakoloni kutoka Ulaya (Wazungu) kugawana makoloni katika Bara la Afrika, katika nusu ya pili ya karne ya 19.  Baada ya kinyang’anyiro baina yao, wakoloni hao walikutana katika Mkutano wa Berlin wa 1887 ambapo waligawana Afrika.  Katika mgao huo, sehemu ya Bara (ukiondoa ukanda wa mwambao wa pwani ulioitwa Mrima) walipewa Wajerumani.  Koloni hilo ambalo lilijumuisha Burundi na Rwanda ya sasa liliitwa Deutsche Ost Afrika (yaani Afrika Mashariki ya Wajerumani).  Sultani wa Zanzibar aliachiwa visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia na ukanda wa Mrima.  Miaka mitatu baadae, chini ya Mkataba wa Heligoland wa 1890, Sultani alilazimishwa kuuza kwa Wajerumani ukanda wa Mrima na kisiwa  cha Mafia, na hivyo kubakiwa na visiwa vya Unguja na Pemba tu, na yeye mwenyewe kuwekwa chini ya Himaya ya Mwingereza.  Watu wa Bara na Visiwani wakawa wametenganishwa.

 

Kuanza Kurejeana

 

Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1915 – 1919), majaaliwa yalianza kuwakurubisha tena watu wa pande hizi mbili.  Kufuatia kushindwa kwa Wajerumani katika vita hivyo, Rwanda na Burundi walipewa Wabelgiji na sehemu iliyobaki ya Deutsch Ost Afrika iliitwa Tanganyika Territory na kupewa Waingereza.  Kwa hivyo watu wa Zanzibar na Tanganyika ingawa waliendelea kuwa na nchi mbili tofauti, lakini angalau wakawa chini ya mkoloni mmoja.

 

Hali hiyo ilijenga mazingira ya kuweza kurejea kwa mawasiliano baina ya watu wa Bara na wa Visiwani ambayo yalikuwa yameathirika vibaya kwa kipindi cha kiasi cha miaka 30.  Mwamko wa kudai uhuru wa kijamii na baadae wa kisiasa ulipoanza kujengeka, watu wa pande hizi mbili, hususan wenyeji wa asli (yaani Waafrika) hawakusita kuitumia fursa hiyo kushirikiana na kusaidiana katika azma hiyo.

 

Mwaka 1927, Waafrika wa Dar es Salaam walianzisha jumuiya yao iliyoitwa “African Association” kwa ajili ya kupigania maslahi yao ya kijamii.  Mwaka 1934, Waafrika wa Zanzibar nao walianzisha “African Association” yao, pengine kutokana na ushawishi wa ndugu zao wa Dar es Salaam.  Nao Waafrika wa Zanzibar wakawashawishi wale wa Dodoma na kupelekea kuundwa kwa “African Association” ya Dodoma.  Jumuiya tatu hizi zilijenga umoja wa kufanya mikutano mikuu ya pamoja ya mwaka kwa zamu baina ya miji hiyo, na zilikuwa chachu ya kufunguliwa kwa matawi ya “African Association” katika miji mbali mbali Tanganyika na Zanzibar.

 

Ziara za Michezo

 

Sambamba na ushirikiano huo wa kijamii, wananchi wa Tanganyika na Zanzibar walianzisha utamaduni wa kubadilishana ziara za kimichezo.  Ziara hizo zilikuwa zikifanyika wakati wa mapumziko ya Pasaka, kwa utaratibu wa zamu ambapo kama mwaka huu wanamichezo wa Zanzibar wanakwenda Tanganyika, mwaka ujao wa Tanganyika watakwenda Zanzibar.  Utamaduni huo unaendelea hadi leo na umezidi kupanuka kwa kujumuisha wasanii na hata wananchi tu wa kawaida.

 

Ushirikiano wa Kisiasa

 

Upepo wa harakati za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni ulipofika maeneo haya, watu wa Tanganyika na Zanzibar walihamasishana, kushirikiana na kusaidiana katika jukumu hilo la kudai na kupigania uhuru wa nchi zao.  Mwaka 1954, chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilianzishwa Tanganyika kutokana na Tanganyika African Association, kwa ajili ya kudai uhuru wa Tanganyika.  Zanzibar nako mwaka 1957 ilianzishwa Afro-Shirazi Party (ASP) kutokana na kuungana kwa African Association na Shirazi Association (iliyokuwa imeundwa 1938).  Kuundwa kwa ASP kulishuhudiwa na Rais wa TANU, Mwalimu Julius K. Nyerere.

 

Ushirikiano wa TANU na ASP katika mapambano ya kudai uhuru hadi ulipopatikana Uhuru wa Tanganyika Disemba 9, 1961 na kufanikiwa kwa Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964 unajulikana na hauna haja ya kuufafanua hapa.  Dhamira angalau ya ASP (wakati wa kupigania uhuru) ya kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika baada ya uhuru haikuwa siri.  Hiyo inadhihirishwa na maelezo yafuatayo ya Marehemu Sheikh Thabit Kombo kama yalivyonukuliwa na Rais Benjamin Mkapa katika hotuba yake ya kihistoria aliyoitoa Zanzibar kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano tarehe 26 Aprili, 2004:-

 

Mafisadi wanalalamika, kwa nini muungano umefanyika haraka haraka;  Mapinduzi Januari na Muungano Aprili, miezi mitatu tu!  Wako wanaodhani kuwa Mwalimu Nyerere ndiye aliyelazimisha Muungano.

         

Wazo la Muungano ni wazo la Afro-Shirazi tokea mwanzo.  Utakumbuka katika Manifesto yetu tulisema kuwa tukipata Uhuru azma ya ASP ni kuona kuwa Afrika yote inakuwa moja yenye nguvu.  Lakini kwa Tanganyika na Zanzibar ahadi ya muungano ni ahadi ya wanachama wenyewe waliyokuwa wanaitoa katika mikutano yao yote…  Watu wa Tanganyika na watu wa Zanzibar ni wale wale, tofauti ni sisi wa Zanzibar kutawaliwa na Sultani….  Mazungumzo yalikuwa mafupi sana, yalichukua siku moja tu; maana hakukuwa na swali kama tuungane au tusiungane.  Hoja ilikuwa tu muungano wetu uwe na sura gani…..

 

Muungano Kama Tukio la Kimantiki

 

Kutokana na ukweli huo wa kihistoria wa umoja, udugu na ushirikiano wa muda mrefu baina ya watu wa pande hizi, na kufuatia TANU na ASP kushika madaraka baada ya Uhuru na Mapinduzi, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa Tanzania uliokamilishwa rasmi tarehe 26 Aprili, 1964 lilikuwa ni tukio la kimantiki na halipaswi kuwa la kushangaza.

 

Ni ukweli wa kihistoria kwamba pamoja na kwamba watu wa Tanganyika na Zanzibar wamekuwa wamoja katika zama zote za kihistoria, lakini Tanganyika na Zanzibar hazikuwa nchi tulizoziunda.  Ziliundwa na wakoloni na mipaka yake ilikuwa ikipangwa na kupanguliwa na wakoloni kwa maslahi yao.  Tanganyika na Zanzibar pamoja na mipaka yake tuliirithi tu kutoka kwa wakoloni baada ya uhuru.  Lakini Tanzania tumeiunda wenyewe..  Katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere anasisitiza kwa fahari:  Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru.  Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka katika Ukoloni.  Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu zake mbili kutoka katika Ukoloni.  (uk.57).

 

Pamoja na hayo, kama itakavyofafanuliwa baadae, wapo watu wanaoshangaa na kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa hoja kwamba eti hayakutafutwa maoni ya wananchi kwanza.  Katika kuwabeza watu hao, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake hicho hicho cha “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania anasema ifuatavyo kwa kejeli:-

 

Pwani ya Tanganyika na Zanzibar ya sasa zilikuwa pamoja kwa muda mrefu sana kabla ya kutengwa na Wakoloni Waingereza na Wajerumani.  Kama zingebaki zimetengana, kwa “wazalendo” hao hiyo ingekuwa ni halali, maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya bunduki za Mabwana.  Lakini uamuzi wa Tanganyika huru na Zanzibr huru kuungana, na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa wametengwa na Mabeberu, tendo hilo kuna … wanaosema kuwa halikuwa halali.  Hatukutafuta maoni ya watu kwa njia ya demokrasia wanayoijua wao.  Wajerumani na Waingereza walitafuta maoni ya wazee wetu kwa mtutu wa bunduki!  Hiyo ilikuwa halali.  Nchi walizounda kwa njia hizo zilikuwa halali.  Tunatakiwa tujivunie Utanganyika na Uzanzibari uliopatikana kwa njia hizo; lakini tuuonee haya Utanzania, tunda la uhuru wetu wenyewe.  Sikuamini kuwa Wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha kasumba na kuzitawala akili za baadhi yetu!.  (uk.58).

 

Tarehe 5 Februari, 1977 vyama vya TANU na ASP viliungana na kufanya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika tukio ambalo lilikuwa na maana ya kuzidi kuuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  Tena kuundwa kwa CCM kulitanguliwa na mashauriano ya kutosha.  Aidha, ilifanywa kura ya maoni ya wanachama ambayo matokeo yake yalikuwa kama yanavyoonekana katika Jedwali Na. 1 na 2 hapa chini:-

 

 

JEDWALI Na. 1:   MATOKEO YA MAONI YA WANACHAMA WA TANU KUHUSU KUUNGANISHWA TANU NA ASP

Matawi

Idadi

Asilimia

Idadi ya Matawi Yote ya TANU

6,639

100.00

Yaliyokutana

6,427

96.81

Yasiyokutana

212

3.19

Yaliyokubali

5,424

99.95

Yaliyokataa

3

0.05

Idadi ya Matawi Madogo ya TANU

38

100,00

Yaliyokutana

38

100.00

Yaliyokubali

38

100.00

Yaliyokataa

0

0.00

Chanzo:       Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, 1977 – 1997

 

JEDWALI Na. 2:    MATOKEO YA VIKAO NA WANACHAMA WA ASP KUHUSU MAONI YA KUUNGANISHWA TANU NA ASP

Matawi

Idadi

Asilimia

Idadi ya Matawi ya ASP

257

100.00

Yaliyokubali

257

100.00

Yaliyokataa

0

0.00

Idadi ya Wanachama Wote Walioshiriki

103,983

100.00

Waliokubali

103,574

99.06

Waliokataa

409

0.04

Chanzo:       Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, 1977 – 1997.

 

Yaani wanachama wa TANU katika katika 99.95 ya matawi yao  yaliyotoa maoni na matawi yote madogo waliafiki chama chao kuunganishwa na ASP.  Kwa upande wa Zanzibar, wanachama wa ASP katika matawi yao yote waliafiki chama chao kiunganishwe na TANU.  Na kwa wanachama mmoja mmoja walioshiriki katika kura hiyo ya maoni, ni 409 tu kati ya wote 103,983, yaani sawa na asilimia 0.04 tu ndio waliokataa.

 

Huu ulikuwa ni ushahidi madhubuti usio shaka wa kitakwimu wa imani ya wananchi kwa Muungano.  Kwa kura hiyo, watu wa Tanganyika na Zanzibar kupitia vyama vyao vya TANU na ASP ambavyo vilikuwa pekee wakati huo, waliuthibitishia Ulimwengu kwamba Muungano ni wao na haukuwa wa viongozi tu kama inavyodaiwa na wapinzani wachache wa Muungano.

 

Kabla ya kuunganishwa kwa TANU na ASP, Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliitaja Jamhuri hiyo kuwa ni ya mfumo wa chama kimoja ambapo kwa Tanganyika Chama hicho ni TANU na kwa Zanzibar chama hicho ni ASP.  Kwa maneno mengine, Jamhuri ilikuwa chini ya chama kimoja kwa viwili, jambo ambalo lilileta dosari kubwa katika uimara wa Muungano.  Baada ya TANU na ASP kuungana na kuwa CCM, dosari hiyo iliondolewa na hivyo kikawa ni kitendo cha kuimarisha Muungano.  Zaidi ya yote, tukio hilo ndilo lililochochea kutungwa rasmi kwa Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

 

Kwa hivyo, kwa majumuisho, inasisitizwa tena kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa watu wenyewe.  Waasisi wa Muungano huo, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume kupitia Serikali zao, waliwezesha tu kufikiwa kwa matarajio ya wananchi wenyewe.  Mzee Karume alilielezea tukio hilo kwa maneno yafuatayo kama alivyonukuliwa na Rais Benjamin Mkapa katika hotuba yake ya tarehe 26 Aprili, 2004:-

 

Napenda mfahamu wananchi wote, kazi hii si kazi ya Abeid Karume.  Jambo hili, jambo la wenyewe Waafrika wote.  Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume wao ni watumishi wa wenyewe wana wa nchi, na sisi tumekubali kuwatumikia wenyewe wananchi.  Tunawatumikia wananchi kwa utumishi wao maalum, ule walioona wao wenyewe bora.  Basi jambo hili la kufanya Union, Tanganyika na Zanzibar, ni jambo ambalo lililofikiriwa na wenyewe wananchi wa Tanganyika na Zanzibar

 

Hatimaye, mwaka 1977, watu wenyewe, kupitia vyama vyao waliithibitisha hatua ya Waasisi ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.

 

Hiki ni kielelezo cha wazi cha umadhubuti wa nguzo hii ya Muungano ya kwamba Muungano ni wa watu wenyewe, na jinsi nguzo hii inavyoupa uhalali wa kijamii na hata wa kisiasa Muungano wetu.

 

Nguzo Ya Msukumo wa Kujenga Umoja wa Afrika

 

Nguzo ya pili inayouhimili Muungano ni utashi wa kujenga umoja wa Afrika.  Manifesto (Ilani za Uchaguzi) za TANU na ASP toka enzi za mapambano ya kudai uhuru zilikuwa na vipengele vya kutaka umoja wa Afrika.  Aidha, vyama vyote vilishiriki kikamilifu katika majukwaa yote yaliyowaunganisha Waafrika wa nchi mbali mbali katika kudai uhuru kwa lengo la kuja kuziunganisha nchi hizo baada ya uhuru.  Kwa mfano, TANU na ASP zilikuwa wanachama wa PAFMECA na baadae PAFMECSA, vyombo ambavyo viliviweka pamoja vyama vilivyokuwa vikidai uhuru kutoka nchi mbali mbali za eneo la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.  Katika hili, hata Chama cha Hizbu (ZNP) cha Zanzibar kilikuwa kikishiriki.

 

Katika jitihada za kufikia ndoto hiyo ya umoja wa Afrika, nchi za Afrika Mashariki (yaani Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar) zilijaribu kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki baada ya uhuru wa nchi hizo.  Baada ya kuona dalili za kukawia kufikiwa kwa lengo hilo katika upeo wa Afrika Mashariki, Rais Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar walikubaliana zianze Tanganyika na Zanzibar ili kuonyesha njia na kuendeleza shauku ya kutafuta umoja wa Afrika.  Dhamira hiyo inajieleza katika maneno ya Mwalimu Nyerere katika hotuba yake katika Mkutano Maalumu wa Bunge la Tanganyika, tarehe 25 Aprili, 1964, lililoitishwa kujadili na kuridhia Hati ya Muungano.  Mwalimu anajinukuu katika kitabu chake cha “Uhuru na Umoja kama ifuatavyo:-

 

Ikiwa, basi, nchi ambazo ni marafiki na ni jirani, na hasa zile ambazo zilipata kuwa moja bali zikagawanywa na wakoloni wapya; ikiwa hizo zitashindwa kuungana, kushindwa huko kunaweza kukaleta wasi wasi katika bara letu la Afrika na shauku yake ya Umoja.  Bali ikiwa nchi hizo zaweza kuungana, muungano huo waweza ukawa ni thibitisho la vitendo kwamba matumaini ya bara letu si ya bure. (uk.292).

 

Miaka miwili baadae, wakati wa sherehe za Muungano kutimiza miaka miwili zilizofanyika Dar es Salaam mwaka 1966, Mzee Karume naye aliithibitisha dhamira hiyo.  Kama alivyonukuliwa na Rais Benjamin Mkapa katika hotuba yake ya kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano tarehe 26 Aprili, 2004 mjini Zanzibar, Mzee Karume alisema yafuatayo:-

 

Muungano wa Tanzania unaonyesha mithali katika Afrika.  Mithali yenyewe (ni) kuthibitisha nini viongozi wa Kiafrika kabla ya hawajapata independence walikuwa wakisema.  Neno lililokuwa likisemwa ni hili hapa – Tanzania (Muungano).  Ya kwamba kila mmoja akijitapa, “mara tu nikipata Serikali yangu katika nchi yangu lazima nilete uhusiano na Muungano wa Uafrika, tuzidi kuendelea kwa maendeleo yaliyo bora.”  Lakini si bahati mbaya (kuwa hawajatekeleza).  Watanzania mjue kuwa si bahati mbaya.  Bahati nzuri, Muungano ndiyo huu hapa.  Watanzania tena mnataka nini? …

Muungano wa Tanzania ndiyo hatua ya mwanzo. Na msife moyo wananchi wa Tanzania.  Wenzetu wako jirani watakuja unga.

 

Muungano wa Tanzania ni kani inayoendeleza uhai wa dhamira ya kuwaunganisha Waafrika na hivyo umeijengea heshima kubwa nchi yetu.  Uhai wa dhamira hiyo inayopata msukumo kutokana na Muungano wetu, unajidhihirisha katika kuingia hatua ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (African Union) wenye nguvu zaidi kutoka hatua ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU).  Na katika eneo letu la Afrika Mashariki, hatua za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki zimefufuliwa kutokana na uhai wa dhamira hiyo.

 

Kwa hivyo, nguzo hii ya msukumo wa kujenga umoja wa Afrika imeupa pia Muungano wetu uhalali wa siasa za kimataifa, hasa Barani Afrika.  Watanzania wanajivunia heshima hii na wanapenda iendelee.  Heshima hiyo itaendelea tu kwa kuudumisha Muungano na kamwe si kwa kuudhofisha au kuuvunja.

 

Nguzo ya Kisheria

 

Nguzo ya tatu inayouhimili na kuupa uhalali Muungano wa Tanzania ni ukweli kwamba Muungano huo umesimama juu ya msingi wa sheria za nchi na za kimataifa.  Ulijadiliwa, ukatungiwa mkataba wa kimataifa (Hati ya Muungano) ambao ulitiwa saini tarehe 22 Aprili, 1964 na Wakuu wa Nchi (Marais Nyerere na Karume) na hatimae kuridhiwa na Mabaraza ya kutunga sheria ya nchi zote mbili (yaani Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar) kwa niaba ya wananchi wao.

 

Kama itavyoonekana baadae, wapo waliowahi kudhani kwamba kwa upande wa Zanzibar, hatua za kuuhalalisha Muungano kisheria hazikutimia kwa madai eti kwamba Hati ya Muungano haikuridhiwa na baraza la kutunga sheria kwa niaba ya wananchi.  Lakini hoja yao ilinyauka pale walipozinduliwa kwamba wasilitazame Baraza la Mapinduzi kwa sura yake ya Baraza la Mawaziri tu, bali walione pia katika sura yake ya pili liliyokuwa nayo wakati huo ya Baraza la Kutunga Sheria.

 

 

 

 

Nguzo ya Uendelevu

 

Nguzo ya nne inayouhimili na kuupa uhalali wa kisiasa Muungano wa Tanzania na ambayo inaendelea kuimarika kila kukicha, ni uendelevu wa Muungano wenyewe.  Hadi sasa, miaka arobaini baada ya kuasisiwa kwake, Muungano huu unabaki kuwa mfano pekee Barani Afrika wa muungano wa nchi zilizo huru uliodumu.  Kama ilivyokwishagusiwa kabla, juhudi za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki mara tu baada ya uhuru, zilivia.  Ulijaribiwa pia Muungano wa Misri, Libya na Syria (ulioitwa Jamhuri ya Umoja wa Kiarabu) katika miaka ya sitini, lakini haukufika mbali.  Senegal na Gambia nazo zilijaribu Senegambia katika miaka ya themanini lakini bila ya mafanikio.

 

Kama itavyofafanuliwa baadae, Muungano wa Tanzania umefaulu majaribu mengi.  Badala ya kuudhofisha, majaribu hayo yamekuwa yakiuimarisha zaidi. Muungano ulianza na mambo 11 tu katika orodha ya mambo ya Muungano, lakini hivi sasa yamefikia 22.  Wasioutakia mema Muungano wamekuwa wakidai kwamba eti mambo yaliyoongezwa yaliingizwa kinyemela na kwa kuiburuza Zanzibar.  Lakini madai kama hayo ambayo hayana chembe ya ukweli, mara nyingine yamekuwa yakiambatana na unafiki.  Kwa mfano, waliosimamia na kuhakikisha Usalama wa Taifa wa Zanzibar unawekwa chini ya Serikali ya Muungano mwaka 1984, ndio hao hao sasa wanaoongoza kampeni ya kutaka Watanzania na hasa Wazanzibari waamini kwamba eti mambo yanaingizwa kiholela tu na kwa kuwaburuza Wabunge wa Zanzibar kutokana na uchache wao Bungeni.

 

Ukweli ni kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayalinda vya kutosha maslahi ya Zanzibar kwani inatamka wazi kwamba hakuna jambo litaloongezwa au kupunguzwa katika orodha ya mambo ya Zanzibar ila kwa thuluthi mbili ya kura za Wabunge wanaotoka Zanzibar na thuluthi mbili za Wabunge kutoka Bara.  Kwa hivyo, wingi wa Wabunge wa Bara hauna nafasi ya kuwaburuza wenzao wa Zanzibar.

 

Itoshe tu kusisitiza kwamba uendelevu wa Muungano ni nguzo madhubuti ya kuuhimili Muungano huu ambayo pia inaupa uhalali wa kisiasa za ndani.

 

Katika sehemu hii, zimezungumziwa nguzo nne zinazouhimili Muungano wa Tanzania na hata kuupa sura mbali mbali za uhalali.  Ni kutokana na umadhubuti wa nguzo hizo ndiyo maana umehimili na unaendelea kuhimili misukosuko mbali mbali kama itavyofafanuliwa baadae.  Katika hotuba yake ya kuliaga Bunge tarehe 28 Julai, 1995, Rais Ali Hassan Mwinyi ambae alikuwa anastaafu wakati huo alisema kwa fahari kubwa:-

         

Katika kipindi hiki Muungano wetu umepita katika tanuri la moto na kutokea upande wa pili ukiwa bado imara na wenye nguvu.  Matatizo yaliyojitokeza yalishughulikiwa kwa ukamilifu na katika hali ya maelewano baina ya pande zote mbili.  Tumefanya pia marekebisho katika Katiba ambayo nina imani yatazidi kuimarisha Muungano wetu katika kipindi hiki cha mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.

 

 

SABABU ZA MUUNGANO

 

Kwa kadiri CCM inavyohusika, sababu kubwa na za msingi zilizowaongoza Waasisi wa Muungano katika kuuanzisha  ni hizi tatu zifuatazo:-

1.                 Kuurejesha na kuuthitibisha umoja wa watu waliokuwa wametenganishwa.

2.                 Kutekeleza azma ya kujenga umoja wa Afrika.

3.                 Kulinda Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Sababu mbili za kwanza zimekwishajadiliwa kwa kina hapo kabla na hivyo hapana haja ya kuurejea mjadala huo.  Kwa sababu ya tatu, ufafanuzi unapatikana kutokana na maelezo ya Sheikh Thabit Kombo kama alivyonukuliwa na Rais Mkapa katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano.  Maelezo hayo yaliyotolewa kama faida ya Muungano ni kama yafuatavyo:-

 

  Matumaini ya kudumu kwa amani na usalama yamekuwa makubwa kwa nchi zote mbili; wasiwasi mwingi wa usalama umeondoka.  Fikiri mwenyewe kusingekuwako muungano, na maadui wa Zanzibar wakazidisha vitimbi vyao, kusingekuwako usalama wala amani; si Bara wala si hapa Zanzibar.  Lakini kwa nguvu za muungano wakorofi wanasita kidogo …

Lakini usingekuwako muungano tungekuwa na hasara kubwa, kwa Tanganyika na kwa Zanzibar pia.  Zanzibar pamoja na mapinduzi yake, ingedumu katika wasiwasi kwamba mbinu zingeweza kutumika kumrudisha Sultani.  Na Tanganyika nayo pamoja na ukubwa wake, isingekuwa salama kabisa kama kungekuwako vurugu visiwani hapa.  Maadui wangeweza kuitumia Zanzibar kuihujumu Tanganyika kwa urahisi sana

 

Pamoja na kwamba kauli hiyo ya hadharani ilitoka muda mrefu baada ya Mapinduzi, ipo kila sababu ya kuamini kwamba suala la usalama wa Mapinduzi ya Zanzibar na hata Uhuru wa Tanganyika ni miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa wakati wa mazungumzo ya Muungano.  Na pengine ndilo lililochangia katika kuharakisha Muungano hasa ikizingatiwa ukweli kwamba watawala waliopinduliwa Zanzibar walikuwa wamekimbilia nje ambako wangeweza kupanga mbinu za kujaribu kurudisha utawala wao.  Hao ni maadui wa Mapindizi ambao wasingeweza kupuuzwa.  Na hofu hiyo ilithibitishwa na majaribio 17 ya mapinduzi yaliyofanywa bila ya mafanikio na maadui wa Mapinduzi ya 1964.  Muungano bila shaka una mchango wake katika kuyaviza majaribio hayo.

 

Kumekuwa pia na hoja kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulipata msukumo kutokana na vita baridi vya wakati huo kati ya Marekani na Urusi na kambi zao.  Hoja ni kwamba eti Marekani ndiyo iliyoshawishi ufanyike Muungano kwa lengo la kuidhibiti Zanzibar eti isiwe “Cuba ya Afrika”.  Wana-CCM hawaafikiani na hoja hiyo.  Mtazamo wao ni kwamba kama kweli Wamarekani walikuwa na mawazo hayo, hawakwenda zaidi ya kuomba Mungu tu tukio hilo litokee.  Lakini wenyewe Watanganyika na Wazanzibari waliungana kwa utashi wao na kwa maslahi yao.  Hawakuwa na habari na ndoto za Marekani na maslahi yake.

 

Katika hili, Rais Mkapa alitoa msisitizo ufuatao katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano:-

  wapo wanaodhani Muungano wetu ulikuwa lazima wakati ule kwa sababu tu ya vita baridi duniani, na mapambano ya mataifa makubwa kutafuta himaya barani Afrika.  Swali linabaki.   Vita baridi vilikwisha, na harakati za wakubwa kujenga himaya Afrika nazo zimekwisha.  Lakini Muungano unaendelea, kwa nini?  Kwa sababu msingi wa Muungano haukuwa vita baridi, bali shauku kubwa – iliyozuiliwa na wakoloni kwa miaka mingi – ya watu wa Tanganyika na Zanzibar kuungana kama walivyokuwa zamani.

 

KWA NINI SERIKALI MBILI?

 

Muundo wa Muungano wa Tanzania ni wa Serikali mbili; yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo inashughulikia mambo ya Muungano na mambo yote ya Tanzania Bara (baada ya Serikali ya Tanganyika kufa) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoshughulikia mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Zanzibar.

 

Muundo huu umekuwa jambo la mjadala mkubwa na wenye kuendelea miongoni mwa Watanzania.  Wapo wanaouona muundo huu kuwa haufai kwa kuwa ni tofauti na miungano mingine inayojulikana duniani.  Wapo wanaoamini kuwa unasababisha kero nyingi na hivyo haukidhi matarajio ya Watanzania.  Wapo wanaoamini kuwa haupendwi na Watanzania.  Wapo pia waliojaribu kujenga hoja kwamba eti Waasisi wa Muungano walipokuwa wanaunganisha nchi hizi mbili, lengo lao la baadae lilikuwa ni muungano wa Serikali moja na kwamba huu wa  Serikali mbili ulikusudiwa uwe wa muda tu.  Wapo wengine waliojaribu kujenga hoja kwamba eti Waasisi hao walichounda ni Shirikisho la Serikali tatu ambapo Serikali ya Tanganyika “imefichwa” ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

 

CCM inatofautiana na mawazo yote hayo.  Kufaa au kutokufaa na kukubalika au kutokubalika kwa muundo huu kwa Watanzania kutajadiliwa baadae chini ya Misukosuko Iliyohimiliwa Na Muungano. 

 

Katika sehemu hii, inatazamwa dhamira halisi ya Waasisi katika kufikia uamuzi wa Muundo huu.   CCM inaamini kwamba Waasisi walikusudia muundo wa Serikali mbili na walikuwa wanakijua walichokuwa wanafanya.  Wao wenyewe ndio walioijua zaidi dhamira yao kuliko wale wanaojaribu kuitafsiri.

 

Kwa mnasaba huo, tunaanza na kuwanukuu kauli zao kama walivyosema wenyewe.

 

Katika “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Mwalimu Nyerere anaifichua dhamira yao na sababu za kuamua muundo wa Serikali mbili kama ifuatavyo:-

 

Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi Moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili:  Muungano wa Serikali Moja, au Shirikisho la Serikali Tatu.  Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta Serikali yake, na Nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni Nchi Moja yenye Serikali Moja.  Katika mfumo wa pili kila Nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na Serikali ya Shirikisho, na itakuwa Serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki….

 

Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida.  Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika.  Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000).  Muungano wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar.  Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya1  Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja.  Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika.  Zanzibar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo.  Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha Serikali yake ya watu 12,000,000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000.  Ni watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo.  Gharama ya Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari) na wala Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo, hata bila gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho.  Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.

 

Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika?  Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na Serikali yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar?  Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar.  Basi na tutafute muundo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikali mbili zenye uzito unaolingana.

         

Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa Muungano wa Serikali Mbili.  Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazama hali halisi yetu ilivyokuwa na tukabuni mfumo utakaotufaa zaidi.  (uk.15 – 16).

 

Mzee Abeid Amani Karume kwa upande wake aliielezea kwa ushupavu zaidi dhamira ya kuunda Muungano kwa kutumia neno la Kiingereza la Union ili kuziba mwanya wa kubabaisha na shirikisho.  Katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano, Rais Mkapa alimnukuu Mzee Karume kutokana na hotuba yake maarufu aliyoitoa siku za mwanzoni za Muungano ambayo husikika sana katika redio.  Katika nukuu hiyo Mzee Karume alitamka yafuatayo:-

 

Leo tumekuja kuonana na nyinyi wananchi wote.  Na ikiwezekana kuusia mambo.  Sababu baadhi ya watu wengi, wanataka kufahamu (kuhakikishiwa kwamba) Serikali ya Unguja (kwa maana ya Zanzibar) na Serikali ya Tanganyika zimechanganyika, zimekuwa Union moja tu. …

 

Kwa hivyo, ni dhahiri kabisa kwamba walipoamua muundo huo wa Muungano walikuwa wanajua walichokuwa wanakifanya na walichokuwa wanakitaka.  Na wala haina maana kwamba labda walipoamua muundo huo walidhani hautokuwa na matatizo.  Matatizo walijua yatakuwepo lakini waliamua kwa makusudi wakabiliane nayo ndani ya Muungano badala ya kusubiri yamalizike kwanza ndio waunganishe nchi.  Ukweli huo unadhihirishwa katika kitabu cha ASP cha Maendeleo ya Mapinduzi ya Afro-Shirazi Party  1964 – 1974kama ifuatavyo:-

 

Nchi mbili huru, kama zilivyokuwa Zanzibar na Tanganyika, zinapoungana, kuna njia mbili za kuunganisha.  Njia ya kwanza ni kuungana kwa yale wanayokubaliana, hata yakiwa ni machache, madamu tu nia ipo, ni kuitekeleza ile nia na halafu zikaendelea kutanzua matatizo yao na kujenga juu ya ile nia iliyokwisha kutekelezwa.  Njia ya pili ni kukaa na kutanzua matatizo kwa makubaliano mpaka kifikilie kima cha makubaliano kiwezacho kuleta muungano.  Zote hizi njia mbili si rahisi na kila moja ina matatizo yake yanayoweza kuchukua muda mrefu kutanzuliwa.  Tanganyika na Zanzibar zilichukua njia ya kwanza, siyo kwamba ndiyo iliyokuwa rahisi, bali kwa sababu nchi mbili hizi zilikubaliana na kutekeleza nia yao ya kuungana na kutanzua matatizo yaliyosalia ya muungano huku zimo katika Muungano.  (uk.33).

 

Kwa hivyo, matatizo ambayo yamekuwa yakiukabili Muungano ambayo mengine yamefikia kuutia katika misukosuko mikubwa hayawezi yakawa ni kioja, kwani yalitabiriwa.   Hata hivyo, kuendelea kuimarika kwa Muungano ndani ya mazingira ya matatizo hayo, ni kielelezo cha udhati wa nia ya kuungana na usahihi wa uamuzi wa kuteua muundo wa Serikali mbili.

 

Katika hotuba yake ya kihistoria iliyoimarisha hoja ya Muungano tarehe 26 Aprili, 2004 kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano, Rais Mkapa alitoa majumuisho mazuri ya suala hili kama ifuatavyo:-

 

Muungano wetu umefikisha miaka 40, na upo imara.  Nguvu yake ni Watanzania wenyewe, wengi wao – asilimia 84.8 – wakiwa hawajui uraia mwingine isipokuwa Utanzania.  Watanzania hawa waliozaliwa mwaka 1964 na kuendelea, ambao leo wana umri wa miaka 40 au chini zaidi, hawana uzoefu wa kuwa kitu kingine isipokuwa kuwa Watanzania.

 

Na hawajui mfumo mwingine wa Muungano isipokuwa mfumo wa Serikali mbili, wenye manufaa mawili makubwa ambayo ni sehemu ya msingi wa Muungano wetu.  Kwanza, mfumo huu unadhihirisha kuwa kweli sisi tumeungana,  serikali yetu ni muungano, si shirikisho.  Na, muungano ni imara kuliko shirikisho.

 

Msingi wa pili ni madaraka kamili ya Zanzibar kwa mambo ambayo si ya muungano.  Madaraka hayo yanasaidia kuhakikisha kuwa Zanzibar inahifadhi utambulisho wake na haimezwi na Tanzania Bara.  Wapo wanaoamini kuwa mfumo huu hauna haiba nzuri; ati haupendezi.  Kwao napenda kusema kuwa jambo muhimu kuliko yote katika msingi wa nyumba si sura yake, muhimu zaidi ni uimara wake.  Na mimi nakuhakikishieni, Ndugu Wananchi, kuwa mfumo wa Serikali mbili ndicho chombo imara kilichotuvusha salama katika bahari ya miaka 40 iliyopita, na Inshallah, ndicho kitatuvusha salama katika miaka ijayo.

MISUKOSUKO ILIYOHIMILIWA NA MUUNGANO

 

Kama ilivyokwishaelezewa, Muungano umeweza na unaendelea kuhimili misukosuko mingi.  Misukosuko hiyo imekuwa ni changamoto inayouwezesha kujidhatiti zaidi, kwani kila unapoishinda changamoto moja, unaibuka imara zaidi.  Hii ni kwa sababu changamoto hizo huwafanya wahusika, hasa Serikali zote mbili, kutoa ufafanuzi kusafisha upotoshaji unaotolewa au kuyafanyia kazi na kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayojitokeza ambayo hutumiwa kuutia misukosuko Muungano.

 

Awali, misukosuko ilijikita zaidi katika kuhoji uhalali wa Muungano wenyewe.  Baadae, baada ya shaka kuondolewa kuhusu uhalali wake, misukosuko imeelekea zaidi katika kuhoji muundo wa Serikali mbili.

 

Kuhoji Muungano Wenyewe

 

Hoja ya kwamba Muungano haukuwa halali kwa sababu eti haukupata ridhaa ya wananchi na haukukamilisha taratibu za kisheria zilianza kusikika hadharani Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya themanini.  Seif Sharif Hamad na wenzake ambao baadae walikiri kuwa walikuwa wapinzani ndani ya CCM na Serikali, waliitumia fursa iliyotolewa kwa nia njema na CCM ya kuanzisha mjadala wa kitaifa wa marekebisho ya Katiba kutaka kuudhofisha au hata kuuvunja Muungano.  Watu hao hao ni wale wale ambao baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi waliunda chama chao cha CUF katika miaka ya tisini. 

 

Kipindi hicho cha msukosuko wa kwanza mkubwa kuutikisa Muungano kilikuwa baina ya 1983 na 1984 na kinajulikana kwa umaarufu wa kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar.  Madai yaliyokuwa yameshika nguvu wakati huo ni ya kudai kura ya maoni ya wananchi ili eti kuupa uhalali Muungano huo na kukamilisha hatua za kisheria.

 

Imekwishaelezewa kwa kina katika sehemu ya Nguzo za Muungano jinsi Muungano ulivyo na uhalali unaotokana na watu wenyewe, na kwamba umekidhi matakwa ya sheria.

 

Mtazamo wa CCM kuhusu kura za maoni ni kwamba si jambo la lazima na wala si njia pekee ya kupima utashi wa wananchi.  Hadi wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana hakukuwa na nchi duniani zilizokuwa zimeungana baada ya kuitishwa kura za maoni.  Miungano mikubwa mikubwa iliyodumu na iliyo madhubuti kabisa kama ile ya Marekani (USA) na Uingereza (UK) haikuanzishwa kwa kura za maoni.  Na wala hadi leo haikupigiwa kura za maoni za kuithibitisha.  Kinyume chake,Marekani iliwahi kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kuulinda Muungano baada ya majimbo ya Kusini kutaka kujitoa.  Wanaolalamikia Muungano hupenda kutaja mifano ya nje kuzipa nguvu hoja zao, lakini mifano hii ya Marekani na Uingereza hawaitaji katika muktadha huu.  Kwa mazingira ya wakati ule na hasa kuzingatia usalama wa Mapinduzi ya Zanzibar, isingeweza kutumika njia nyengine zaidi ya iliyotumika.  Hata hivyo, suala hili la kura ya maoni lilikuwa agenda kuu ya uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa 1990 ambapo Dr. Salmin Amour alichaguliwa kuwa Rais wa tano wa Zanzibar.  Uchaguzi huo uliambatana na kampeni kubwa ya chini kwa chini iliyowataka watu waususie hadi kwanza itapoitishwa kura ya maoni.   Inasadikiwa katika CCM kwamba kampeni hiyo iliongozwa na kundi la wanasiasa chini ya uongozi wa Seif Sharif Hamad waliokuwa wamefukuzwa kutoka CCM kwa sababu za usaliti.  Ni watu hao hao ndio wanasadikiwa pia kuongoza kampeni ya chini kwa chini ya kutaka Sheikh Idris Abdul-Wakil apigiwe kura za HAPANA wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 1985.

 

Kampeni zote hizo hazikufanikiwa.  Kushindwa kwa kampeni ya 1990 iliyotaka kura za maoni kuliidhoofisha kwa kiasi kikubwa hoja ya kwamba Muungano eti Wazanzibari hawakuwa wameuridhia.  Kujitokeza kwa wingi kwa wananchi kupiga kura na kumchagua Dr. Salmin Amour ambae kampeni yake na ya CCM ilikuwa ya kupinga kura za maoni ulikuwa ushahidi wa kutosha kwamba Wazanzibari hawakuwa na tatizo na Muungano.

 

Kwa upande wa uhalali wa kisheria, kitendawili kiliteguliwa na Tume ya Chama Kimoja au Vyama Vingi (maarufu Tume ya Nyalali) katika miaka ya tisini.  Tume hiyo  ilijiridhisha kwamba Baraza la Mapinduzi la Zanzibar likikaa kama Baraza la Kutunga Sheria, liliiridhia Hati ya Muungano kama lilivyofanya Bunge la Tanganyika, na hivyo kukamilisha taratibu za kisheria.Profesa Haroub Othman katika makala yake ya “Forty Years of the Union: Is It Withering Away?” naye kwa njia zake amejiridhisha hivyo.  Ugunduzi huu ukawa umeimaliza kabisa hoja dhidi ya uhalali wa Muungano. Kilichoendelea kutokea baada ya wakati huo katika mjadala wa Muungano yakawa ni masuala ya muundo na kero za Muungano tu.

 

 

 

Kuhoji Muundo wa Serikali Mbili

 

Baada ya uhalali wa Muungano kuthibitika bila ya chembe ya shaka, sasa hoja zimehamia kwenye muundo, labda na kero za Muungano.

 

Kabla ya kuendelea na uchambuzi, kwanza tuwatazame hao wanaouandama Muungano, hasa upande wa Zanzibar.  Vitimbi vya wasaliti wa Chama wakati wa Chaguzi Kuu za 1985 na 1990 vimekwishaelezwa.  Lakini ni kundi hilo hilo ndilo lililokuwa mapema zaidi (mwaka 1984) limemfitini katika Chama (CCM) Rais wa pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe kwamba alikuwa anataka kuvunja Muungano kwa azma yake ya kutaka kupendekeza muundo wa Serikali tatu.  Ni kutokana na fitina hizo ndio akalazimika kujiuzulu.  Wakati huo walijifanya wapenzi wakubwa wa Muungano na wenye uchungu mkubwa nao.  Lakini kufikia 1990, wakautilia shaka kiasi cha kutaka kuuitishia kura za maoni.  Kufikia 1992, waliunda chama chao cha CUF na sera yao ya Muungano ikawa ya Serikali tatu.  La kujiuliza ni jee, inakuwaje sera ya Serikali tatu ya Jumbe iwe ya kuvunja Muungano lakini sera ya Serikali tatu ya CUF isiwe ya kuvunja Muungano?  Pamojawapo lazima pana unafiki.  Ili kupabaini, tutazame historia kidogo.

 

Kwamba muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilikuwa sera ya ASP toka wakati wa kudai uhuru, hapana ubishi.  Sheikh Thabit Kombo amethibitisha hivyo kwa uwazi.  Lakini kwa upande wa pili, inajulikana pia kwamba chama cha Hizbu kilikuwa kinaipinga vikali sera hiyo.  Kauli mbiu ya chama hicho ilikuwa “ASP itaiuza Zanzibar kwa Nyerere”.  Aidha, Hizbu ilijenga chuki dhidi ya watu wenye asili ya Bara na kuna wakati kwa ushawishi wake, Sultani alitoa meli ya kuwarejesha “kwao” Wabara.  Hata hivyo wito huo haukuitikiwa vyema kwani hao Wabara walijua kwamba Zanzibar walikuwa kwao.

 

CCM inaamini kwamba waliokuja unda CUF wana mnasaba na Hizbu, na zaidi, CUF iliundwa kutokana na ushawishi wa waliokuwa viongozi wa Hizbu.  Kama Hizbu haikutaka Muungano, hapawezi kuwa na taabu sana kuamini kwamba na CUF iliyochipua kutoka kisiki chake haijaukinai kikweli Muungano.  Ikumbukwe kwamba Ilani ya Kwanza ya Uchaguzi ya CUF ilizungumzia kuirejesha Zanzibar ya zamani.  Kwa hivyo, madai ya kura ya maoni na sera ya Serikali tatu ni visingizio tu vya kilaghai vinavyoficha nia ya CUF ya kuvunja Muungano.  Halikadhalika, Wana-CCM wengi hawaamini kwamba ile fitina dhidi ya Jumbe waliyoifanya viongozi wa sasa wa CUF walipokuwa ndani ya CCM na Serikali ilikuwa kielelezo sahihi na cha kweli cha imani yao kwa Muungano.

 

Ni kutokana na mtazamo huo ndio maana CCM inaamini kwamba CUF hawautaki Muungano, lakini maadam hawawezi kusema hivyo bayana kutokana na kuujua ukweli kwamba Muungano umekwishajikita ndani ya nyoyo za Wazanzibari na Watanzania kwa jumla walio wengi, jitihada wanazofanya ni kutafuta fursa za kuutia misukosuko kwa lengo la kuudhoofisha au hata kuuvunja.  Ndio hizo kelele za kura ya maoni na sera ya Serikali tatu.

 

Vyama vingine vya upinzani ambavyo nguvu zake ziko zaidi Bara navyo vina sera ya Serikali tatu.  Lakini kwao wao Sera hii inaelekea kuchochewa zaidi na hasira tu ya Zanzibar kujiunga na OIC; hasira waliyoidaka kutokana na kundi la Wabunge wa CCM (maarufu G 55) waliopeleka hoja Bungeni mwaka 1993 kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.  Hili litazungumziwa zaidi baadae.  Sababu nyengine ya sera ya Serikali tatu kwa vyama hivyo pengine tu ni kuwa na kitu tofauti na CCM.

 

CCM inaamini kwamba kuanzisha Shirikisho la Serikali Tatu kutoka Muungano wa Serikali Mbili ni kurejea nyuma na kuudhofisha Muungano.  Tendo hilo litajenga mazingira ya hata kuuvunja kabisa Muungano.  Maneno yafuatayo ya Mwalimu Nyerere yaliyomo katika “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania yanatoa kwa majumuisho ujumbe huo:-

 

  mimi nasema, ukifufua Tanganyika,utaua Tanzania.  Fahali wawili hawakai zizi moja.  “Yeltsin” wa Tanganyika ataua Tanzania.  (uk. 6)

 

Alipozungumzia “Yeltsin”, Mwalimu alikuwa akimaanisha jinsi Muungano wa Kisovieti ulivyosambaratika.  Yeltsin alipoingia katika madaraka ya kuwa Rais wa Russia, Jamhuri iliyokuwa kubwa kuliko zote zilizokuwa ndani ya Muungano wa Kisovieti na akaamua kujitenga, Muungano huo ulisambaratika kwa urahisi tu.  Hilo linaweza kutokea kwa urahisi pengine zaidi ya huo kama Tanganyika inafufuliwa na kuwa na Serikali yake na Serikali hiyo ikapata viongozi wasiotaka Muungano.

 

Muungano wa Serikali Mbili Ulivyoweza Kuhimili Misukosuko

 

Kama ilivyokwishaelezwa, Muungano, katika muundo wake huu wa Serikali mbili umeweza kuhimili misukosuko mingi na mikubwa, na kufaulu majaribu kadha.  Katika sehemu hii tutajaribu kubainisha misukosuko na majaribu hayo na jinsi Muungano ulivyoyashinda.

 

Kuchafuka Kwa Hali ya Hewa ya Kisiasa Zanzibar (1982 – 1984)

 

Mtikisiko uliopata Muungano katika kipindi hicho umekwishaelezewa.  Itoshe tu kueleza kwamba baada ya malumbano makali na hoja za nguvu na jazba za kuhoji uhalali wa Muungano, Katiba za Zanzibar na Jamhuri ya Muungano zilifanyiwa marekebisho makubwa.  Katiba ya Zanzibar ni kama iliandikwa upya (kutokana na ile ya 1979) ndiyo maana inaitwa Katiba ya 1984.  Katiba hiyo ilipanua upeo wa demokrasia Zanzibar na iliwiyanishwa vizuri zaidi na ile ya Jamhuri ili kupunguza migongano.  Katiba ya Jamhuri nayo iliongezewa mambo katika orodha wa mambo ya Muungano ikiwa ni mwelekeo wa kuimarisha Muungano.

 

Uchaguzi Mkuu wa 1990

 

Kampeni ya chini kwa chini ya kuwataka Wazanzibari wasusie Uchaguzi Mkuu wa 1990 hadi iitishwe kura ya maoni kwanza, imekwishaelezewa.  Itoshe tu kusisitiza kwamba Wazanzibari waliipuuza kampeni hiyo na wakajitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo na hivyo kuthibitisha imani yao kwa Muungano.

 

Mjadala wa Mfumo wa Chama Kimoja Au Vingi (1991 – 1992)

 

Kufuatia upepo wa mageuzi ya kisiasa uliokuwa unavuma Duniani wakati huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliunda Tume ya kuratibu maoni ya wananchi na hatimae kupendekeza kama Tanzania iendelee na Mfumo wa Chama Kimoja au iingie katika Mfumo wa Vyama Vingi.  Tume hiyo imepata umaarufu wa Tume ya Nyalali kutokana na jina la Mwenyekiti wake.

 

Katika kufanya kazi yake, Tume hiyo pia ilitaka na kupokea maoni ya wananchi kuhusu muundo wautakao wa Muungano.

 

Kama inavyoeleweka, Tume ilipendekeza kwamba Tanzania iingie katika Mfumo wa Vyama Vingi pamoja na ukweli kwamba asilimia 80 ya wananchi waliotoa maoni yao walitaka Mfumo wa Chama Kimoja uendelee.  Pendekezo hilo la Tume lilikubaliwa.

 

Kuhusu suala la muundo wa Muungano, Tume ilipendekeza muundo wa Shirikisho la Serikali Tatu.  Pendekezo hilo lilikataliwa na CCM na baadaye Bunge kwa sababu za kisera kama zilivyokwishaelezwa lakini pia kwa sababu haukupatikana kabisa ushahidi kwamba watu wenyewe waliutaka muundo huo.

 

Kwa mujibu wa takwimu za Tume, ni Watanzania 49 (sawa na asilimia 0.13) tu kati ya wote 36,279 waliotoa maoni yao ndio waliotaka muundo huo wa Serikali Tatu.  Uchambuzi unaonekana katika Jedwali na. 3 hapo chini:

 

 

 

 

JEDWALI Na. 3:   WATANZANIA WALIOTAKA MUUNDO WA SERIKALI TATU

 

Washiriki

Wote

Waliotaka

Asilimia

Tanzania Bara

32,279

45

0.13

Zanzibar

3,000

4

0.13

Tanzania

36,299

49

0.13

Chanzo:   Kiambatanisho cha Tume ya Nyalali (Uk.i) (pamoja na makosa ya hesabu)

 

Hakukuwa na maafikiano ndani ya Tume yenyewe kuhusu pendekezo hili kwani Wajumbe tisa walipinga na wakaandika maoni yao (dissenting opinion).  Miongoni mwa hoja nyingi zenye uzito mkubwa za kukataa pendekezo hili walizotoa wajumbe hao, ilikuwamo ifuatayo:-

 

Pamoja na kuelewa kuwa kwa baadhi ya mambo mengine ya kisiasa sio lazima uamuzi wake kutegemea wingi wa watoa maoni, lakini pia tunaona kuwa sio busara kupendekeza mabadiliko makubwa kama haya ya mfumo wa Muungano wetu kwa kutegemea maoni ya Watanzania 49 kati ya Watanzania 36,299 walioshiriki katika mjadala wote ulioendeshwa na Tume ya Rais.  Idadi hii ni ndogo isio na uzito wa kitakwimu (statistically insignificant).

 

Hoja hiyo pamoja na nyengine za wajumbe hao waliotofautiana na wenzao ziliwavutia Wabunge ambao kwa hivyo, walilikataa pendekezo la Serikali Tatu mwezi wa Aprili, 1992.

Hoja ya G 55 (1993)

 

Baada ya uamuzi wa kuingia katika mfumo wa Vyama Vingi, ilibidi baadhi ya vifungu vya Katiba vihitaji marekebisho.  Rais Ali Hassan Mwinyi, mwishoni mwa 1992, aliunda Kamati ya kupendekeza marekebisho hayo ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mark Bomani.  Miongoni mwa mambo iliyotakiwa iyatazame ni namna ya kupata Makamu wa Rais katika mfumo wa vyama vingi ambao utafungua milango ya uwezekano wa Rais wa Jamhuri na yule wa Zanzibar kutoka vyama tofauti.  Wakati huo wa mfumo wa Chama Kimoja, Rais wa Zanzibar alikuwa moja kwa moja Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.  Lakini ujio wa vyama vingi ulileta hofu ya uwezekano wa kuigawa Taasisi ya Rais (inayojumuisha Makamu wa Rais) katika itikadi zinazopingana ikitokezea Rais na Makamu wake kutoka vyama tofauti.

 

Kamati hiyo ilipendekeza kwamba Makamu wa Rais apatikane kwa utaratibu wa Mgombea Mwenza ili kuhakikisha kuwa wote wanatoka chama kimoja.  Pamoja na pendekezo jengine kwamba kama Rais anatoka upande mmoja wa Muungano, Makamu wa Rais atoke wa upande wa pili, utaratibu huu ulikuwa unamwondoa Rais wa Zanzibar katika Umakamu wa Rais wa Jamhuri.

 

Zanzibar ilisita kulikubali pendekezo hilo kwa madai kwamba haliendani na dhamira ya makubaliano yaliyomo katika Hati ya Muungano ingawa baadae iliridhia lifikishwe Bungeni ambako lilipitishwa.  Wakati mashauriano kuhusu suala hilo yakiendelea, Zanzibar ilijiunga na Umoja wa nchi za Kiislamu (OIC).

 

Ilikuwa katika mazingira hayo lilipoibuka kundi la Wabunge walioanzia 44 hadi kufikia 55 waliowasilisha Bungeni hoja ya kutaka ianzishwe Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, Agosti, 1993.  Wabunge wote hao walikuwa wa CCM na wa kutoka Bara.

 

Kabla ya hapo, mjadala kuhusu Muungano na muundo wake ulikuwa zaidi mkali Zanzibar.  Makelele mengi dhidi ya Muungano yalisikika zaidi Zanzibar kuliko Tanzania Bara.  Inaelekea dhahiri kwamba msimamo wa Zanzibar kuhusu Makamu wa Rais na OIC ndio uliochangia kwa kiasi kikubwa kuamsha hisia na hata hasira miongoni mwa Wabunge hao wa Bara na waliowaunga mkono.  Uamuzi wa Zanzibar kujiunga na OIC ulihusishwa na kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Kwa vile hoja yao ilipitishwa na Bunge, ni dhahiri kwamba Wabunge hao walipata uungwaji mkono mkubwa.  Tukio hilo ndilo lililoupa Muungano mtikisiko wa kweli na mkubwa pengine kuliko yote ya kabla na baadae.  Taifa lilikuwa katika hatari ya kweli ya kugawanyika na Muungano kuvunjika.

 

Kipindi chote cha 1993-1994 kilikuwa kigumu sana kikihanikizwa na mijadala mikali mikali ndani ya Chama na Serikali na katika jamii.  Azimio la Bunge ambalo dhahiri lilikuwa kinyume na sera ya CCM lilileta mtafaruku mkubwa ndani ya Chama.

 

Baada ya mashauriano ya muda mrefu, Zanzibar ilijitoa katika OIC.   Hatimae Chama kiliamua kufanya uhakiki wa mtazamo wa wanachama kuhusu muundo wa Muungano ili kujiridhisha kama kweli Wabunge walizisoma kwa usahihi hisia za wanachama au la.  Tarehe 12 – 14 Novemba, 1993, ulifanyika Mkutano Maalumu wa Pamoja kati ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Wajumbe wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Wajumbe wa Kamati ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM, na Mawaziri wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Mkutano huo ulifanyika Dodoma.

 

Mkutano huo uliamua kwamba kwa kuwa suala la kutazama upya Muundo wa Muungano linahusu Sera ya CCM, wana-CCM waulizwe juu ya suala hili na watoe maoni yao.

 

Kura za maoni za siri za wana CCM zilipigwa nchi nzima mwezi Aprili, 1994 na matokeo yalikuwa kama inavyoonekana katika Jedwali na. 4,5 na 6 hapa chini:

 

JEDWALI Na. 4:   MATOKEO YA KURA ZA SIRI ZA WANA-CCM WA TANZANIA NZIMA

Mtazamo

Idadi

Asilimia

Waliotaka Serikali moja

394,157

29.21

Waliotaka Serikali mbili

833,285

61.75

Waliotaka Serikali tatu

112,934

8.37

Kura zilizoharibika

9,115

0.67

Jumla ya Wote walioshiriki

1,349,501

100.00

Chanzo:   CCM Makao Makuu

 

 

 

JEDWALI Na. 5:    MATOKEO YA KURA ZA SIRI ZA WANA-CCM WA ZANZIBAR

Mtazamo

Idadi

Asilimia

Waliotaka Serikali moja

452

0.52

Waliotaka Serikali mbili

85,175

98,78

Waliotaka Serikali tatu

386

0.45

Kura zilizoharibika

214

0.25

Jumla ya Wote walioshiriki

86,227

100.00

Chanzo:   CCM Makao Makuu

 

Jedwali Na. 6:   MATOKEO YA KURA ZA SIRI ZA WANA-CCM WA TANZANIA BARA

Mtazamo

Idadi

Asilimia

Waliotaka Serikali moja

393,715

31.17

Waliotaka Serikali mbili

748,110

59.22

Waliotaka Serikali tatu

112,548

8.91

Kura zilizoharibika

8,901

0.70

Jumla ya Wote Walioshiriki

1,263,274

100.00

Chanzo:   CCM Makao Makuu

 

Matokeo hayo yalionyesha kwamba asilimia 61.75 ya wanachama wote wa CCM walioshiriki katika kura hiyo ya maoni bado walikuwa na imani na sera ya Chama chao ya Serikali mbili, na hivyo kuithibitisha tena.  Imani hiyo kwa upande wa Zanzibar ilikuwa kubwa zaidi (asilimia 98.78).

 

Muundo wa Serikali Tatu waliotaka kuulazimisha Wabunge uliungwa mkono na asilimia 8.37 tu ya wanachama na ndio uliothibitika kukataliwa kabisa na wanachama ambapo ulishindwa hata na ule wa Serikali Moja kwa pande zote mbili za Muungano.

 

Baada ya kura hiyo ya maoni iliyothibitisha kwamba Wabunge walienda mchomo, Wabunge walilazimika kurudi kwenye mstari kwa kuifuta hoja yao Bungeni.  Aidha, toka wakati huo, CCM ilianza kuhakikisha kwamba sera ya Muundo wa Serikali Mbili inaingizwa bayana katika Ilani zake za Uchaguzi.  Kabla ya hapo, ilikuwa ikilichukulia tu kuwa ni jambo linaloeleweka.

 

Kabla ya CCM kuamua kuendesha kura kwa wanachama wake tu zilikuwapo hoja kwamba kura ya maoni ilipaswa iwe ya wananchi wote.  Mwalimu Nyerere aliijibu hoja hiyo kama ifuatavyo kama alivyojinukuu katika “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania:-

 

Muundo wa Muungano, pamoja na kwamba hatutaki uwe ukitibuliwa –tibuliwa mara kwa mara, ni suala la sera, si amri ya Mungu.  Vyama vya siasa mbali mbali vinaweza vikawa na maoni mbali mbali kuhusu muundo unaofaa kwa katiba ya Nchi yetu.  Muundo utakaokubaliwa na Wananchi walio wengi ndio utakaokuwa sehemu ya Katiba ya Nchi.  Muundo wa Serikali mbili unakubaliwa na Wananchi, lakini unatokana na sera ya TANU na ASP na kwa  sasa CCM. …  Maoni ya Wananchi yanaweza kukifanya Chama kibadili sera zake; lakini si lazima.  Chama chochote kinaweza kubadili sera zake bila kutafuta kwanza maoni ya Wananchi.  Siku ya Uchaguzi Mkuu maoni ya Wananchi yatajulikana.  (uk. 29)

 

Uchaguzi Mkuu wa 1995

 

Uchaguzi Mkuu wa 1995 ndio uliokuwa wa kwanza kufanyika ndani ya mfumo wa vyama vingi baada ya Uhuru na Mapinduzi.  Vyama vyote vya upinzani viliendesha kampeni ya bidii kubwa ya kupinga muundo wa Serikali Mbili na viliwaahidi wananchi kwamba kama vitachaguliwa vitaanzisha muundo wa Serikali Tatu.  Matokeo yake ni kwamba vilishindwa vibaya na huo ni ujumbe wa dhahiri kwamba sera ya Muundo wa Serikali Tatu ilikataliwa na wananchi.  Badala yake, kwa ushindi mkubwa wa CCM, Muungano wa muundo wa Serikali Mbili ulithibitishwa tena na Watanzania.

 

Kamati Ya Kuratibu Maoni Kuhusu Katiba (1999)

 

Mwaka 1999, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilitoa waraka wa mapendekezo (white paper) kuhusu mambo mbali mbali iliyokuwa inafikiria kuyazingatia wakati wa marekebisho ya Katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2000.  Rais aliunda Kamati ya Kuratibu maoni ya wananchi kuhusu mapendekezo ya Serikali yaliyokuwamo katika waraka huo.  Kama kawaida, Kamati hiyo imepewa umaarufu wa Mwenyekiti wake, Jaji Kisanga.

 

Suala la muundo wa Muungano kwa mara nyingine tena, lilikuwa miongoni mwa mambo yaliyotakiwa maoni ya wananchi.  Lakini kwa mara nyingine tena, Watanzania walioshiriki kutoa maoni yao walithibitisha imani yao kwa muundo wa Serikali Mbili kwa kiwango cha asilimia 88.87, ambapo Zanzibar ilikuwa asilimia 96.25 na Bara asilimia 84.97.  Muundo wa Serikali tatu ulipata asilimia 4.32 tu ambapo Zanzibar ilikuwa asilimia 3.48 na Bara asilimia 4.76.  Jedwali Na. 7, 8 na 9 hapo chini zinatoa uchambuzi wa takwimu za matokeo hayo.

 

JEDWALI Na. 7:  MAONI YA WANANCHI WA TANZANIA KUHUSU MUUNDO WA MUUNGANO UNAOFAA

Mtazamo

Idadi

Asilimia

Waliotaka Serikali moja

4,326

6.54

Waliotaka Serikali mbili

58,750

88.87

Waliotaka Serikali tatu

2,855

4.32

Waliotaka Miundo Mingineyo

174

0.26

Wote walioshiriki

66,105

100.00

Chanzo:   Ripoti ya Kamati Ya Kisanga

 

JEDWALI Na. 8:   MAONI YA WANANCHI WA ZANZIBAR KUHUSU MUUNDO WA MUUNGANO UNAOFAA

Mtazamo

Idadi

Asilimia

Waliotaka Serikali moja

41

0.18

Waliotaka Serikali mbili

22,017

96.25

Waliotaka Serikali tatu

797

3.48

Waliotaka Miundo Mingineyo

19

0.08

Wote Walioshiriki

22,874

100.00

Chanzo:   Ripoti ya Kamati ya Kisanga

 

JEDWALI Na. 9:   MAONI YA WANANCHI WA TANZANIA BARA KUHUSU MUUNDO WA MUUNGANO UNAOFAA

Mtazamo

Idadi

Asilimia

Waliotaka Serikali moja

44,285

9.91

Waliotaka Serikali mbili

36,733

84.97

Waliotaka Serikali tatu

2,058

4.76

Waliotaka Miundo Mingine

155

0.36

Wote Walioshiriki

43,231

100.00

Chanzo:   Ripoti ya Kamati ya Kisanga

 

Kama ilivyofanya Tume ya Nyalali, Kamati hii nayo iliyaacha maoni ya wananchi na badala yake ikapendekeza Muundo wa Serikali Tatu kwa kutumia hoja za jazba na maneno mengi.  Haishangazi kwamba na Kamati hii nayo ilikuwa  na kikundi cha wajumbe wake walioandika maoni tofauti (dissenting opinion) kwa suala hili kama ilivyokuwa kwa Tume ya Nyalali.  Pendekezo hilo la muundo wa Serikali Tatu lilikataliwa na Serikali.

 

Uchaguzi Mkuu wa 2000

 

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2000, Muungano wenye Muundo wa Serikali Mbili ulitiwa tena kwenye mtihani.  Wapinzani waliuza tena sera ya Serikali Tatu na CCM iliendelea kuuza sera yake ya Serikali Mbili.  CCM ilishinda kwa ushindi mkubwa zaidi kuliko hata ule wa 1995.  Muungano ukapasi tena mtihani huu.

 

 

MAFANIKIO YA MUUNGANO

 

Kama alivyosema Rais Mkapa kwenye kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 40 ya Muungano, kule kudumu hadi kufikia miaka 40, pakee ni mafanikio ya Muungano hata kama hakuna mafanikio mengine, hasa ikizingatiwa kwamba umeruka vihunzi vingi.  Lakini yapo mafanikio mengine mengi ya msingi.  Kwanza kurejesha na kudumisha umoja na udugu wa watu waliokuwa wametenganishwa na wakoloni ni mafanikio yasiyo kifani.  Muungano umefanikiwa kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar na uhuru wa Tanganyika, na kuhakikisha amani na utulivu wa nchi.  Hali hiyo imewezesha kushughulikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi tunayoyafaidi hivi sasa.  Muungano umesaidia kuharakisha kurejeshwa kwa demokrasia Zanzibar na umekuwa muhimili wa utulivu (stabilizing factor) kwa siasa za ndani za Zanzibar.  Muungano umefungua milango ya fursa kwa wananchi kujiendeleza kiuchumi bila ya kujali upande gani wa Muungano mtu anatoka. 

 

Muungano umekuwa muhimili madhubuti wa umoja siyo wa Tanzania nzima tu, bali pia wa kila upande wa Muungano huo, yaani Tanzania Bara (Tanganyika) na Zanzibar.  Katika Hotuba yake ya kihistoria ya tarehe 13 Machi, 1995 kwenye mkutano wa waandishi wa habari Hoteli ya Kilimanjaro, Dar es Salaam wakati vumbi la hoja ya Tanganyika (ya G55) halijatulia vyema; hotuba ambayo imeandikwa katika kitabu cha “Nyufa”, Mwalimu Nyerere aliifafanua dhana hiyo kama ifuatavyo:-

 

Watu wazima wamezungumza Muungano, kwamba tuuvunje au uendelee.  Ilikuwa ipo hatari ya kuvunjika na wala haijaisha.  Watu wamezungumza Uzanzibari, baadhi ya viongozi wetu!  Nadhani wengine wanafikiria hata kujitenga.  Wapo, si wengi; lakini wapo.  Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi ivunjike tusiwe na nchi moja, tuwe na nchi mbili.  Ni jambo linalozungumzwa.  Tunataka kiongozi na viongozi watakaoelewa hivyo.  Huku kuzungumza Uzanzibari si fahari.  Si jambo la fahari.  Hatima yake itavunjika Zanzibar.  Mtu mwenye akili hawezi kufikiri anayeona Uzanzibari ni fahari ana akili.  Hawezi akautukuza Uzanzibari kwa kujiita ‘sisi Wazanzibar’ na ‘wao Watanganyika’.

 

Sidhani kwamba Uzanzibari ule una usalama ndani yake.  Hatima yake Zanzibar itajitenga; na Zanzibar ikijitenga kutokana na ule tu kuwa (sisi) Wazanzibari na wao Watanganyika, haibaki.  Wakumbuke kwamba Muungano ndio unaowafanya wanasema ‘sisi Wazanzibari’ ‘wao Watanganyika’.  Nje ya Muungano, hawawezi kusema hivyo: kuna ‘wao Wapemba’ na ‘sisi Waunguja’ …

 

Watanganyika (nao) wakiwakataa Wazanzibari kwa tendo la dhambi ile ile ya ‘sisi Watanganyika’, ‘wao Wazanzibari’, wakautukuza ‘usisi Tanganyika’ na, kwa ajili hiyo, wakawafukuza Wazanzibari, hawatabaki salama.  Hapatakuwa na Tanganyika.  Wakishajitenga tu, Wazanzibari wako kando hivi, mmewafukuza mnajidai wakubwa nyinyi:  “hawa nani hawa, wao wana Rais sisi hatuna kwa nini tusiwatimue?”.  Mkiwatimua mkabakia kwenu hapa, hambaki kweni mtasemaji?  Mtakuwa mmeshatoa sababu ya kusema ‘wale ni wao’ na  ‘nyinyi ni nyinyi’, ‘wao’ vipi Wazanzibari; halafu mbaki ‘nyinyi?’.

 

Maana kama leo wapo kabila la Wazanzibari, mmewabagua, mtaanza vijumba vya Wapemba, vipo vijumba vya Wapemba humu.  Basi watakimbia Wapemba.  Baadhi yao wamo waliokimbia wakati ulee wa zamani.  Vijumba vya kwanza  mtasema ‘Wapemba Wapemba’ kama kwa sauti ya nyinyi mliokuwa mnajiita ‘sisi Watanganyika’ mtakapoanza kuchoma nyumba za Wapemba.  Mnazichoma moto zile, mtakuta eh!  sisi wote si wamoja.  Mbona za Wapemba tulizichoma moto za Wachaga hatuchomi kwa nini?  Maana Wachaga si wazawa bwana!  Hapa kuna wazawa, sasa mnachoma za Wapemba tu za Wachaga mnaacha?  Mtakuta hakuna watu wanaitwa Watanganyika.  Mtakuta mnajidanganya tu.  Mnadhani kuna watu wanaitwa Watanganyika.  Hakuna!  Kuna Wagogo, Wanyamwezi, Wasukuma, Wazanaki, Wakuria, Wamwera eh, wengi sana siwezi kuwataja wote.  Matakuta hakuna hiki kitu kizima kinaitwa ‘sisi Watanganyika’.  (uk.  9-12)

 

Zaidi ya kuimarisha umoja wa ndani ya nchi, Muungano pia umelijengea heshima kubwa Taifa letu na unaendelea kudumisha shauku ya kujenga umoja wa Afrika.

 

MATATIZO

 

Wapinzani wa Muungano na hata wanaoutakia mema wanaweza kuorodhesha matatizo au kero nyingi kwa idadi, lakini nyingi yake zilikuwa zisizokuwa za msingi.  Kero zimekuwapo, zipo na zitaendelea kuwapo.  Zipo zinazopatiwa ufumbuzi, zipo zinazoshughulikiwa na zipo zitazoshughulikiwa kadiri zitavyojitokeza.  Kero ni sehemu ya maisha.  Ukiiondoa hii inazuka nyingine.  Kero ziko katika nchi zisizoungana, seuze zilizoungana kama yetu.  Na kama ilivyokwishaelezewa, wakati Muungano unaundwa, matatizo yalitarajiwa kuwa yatakuwapo na yataendelea kwa muda mrefu.  Na hata tungekuwa na muundo wa Serikali Tau au Moja, matatizo yangekuwapo tu ingawa ya sura tofauti.

 

Kazi ya kuimarisha Muungano ni ya kudumu kama ilivyo kazi ya kujenga demokrasia.  Haina mwisho.  Waingereza walioungana toka karne ya 18 bado hadi leo wamo katika kuimarisha.  Seuze sisi wa miaka 40 tu.

 

Kwa bahati nzuri, malumbano mengi yanayotokea hapa Tanzania juu ya Muungano na muundo wake aghlabu huwa zaidi baina ya viongozi wa Serikali na wa kisiasa, kuliko baina ya wananchi wenyewe.

 

Hivi sasa kuna Muafaka wa Serikali zote mbili uliofikiwa kufuatia mapendekezo ya Kamati ya Wataalamu ya Kushughulikia matatizo ya Muungano (Kamati ya Shellukindo) ya 1992.  Muafaka huo ambao unaendelea kutekelezwa hatua kwa hatua unatoa dira ya kuondoa kero za Muungano.  Miongoni mwa hatua zilizokwisha chukuliwa hadi sasa kufuatia Muafaka huo ni Serikali ya Muungano kuipatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar asilimia 4.5 ya faida ya Benki Kuu na misaada ya nje; kuondoa paspoti kwa Watanzania kuingia Zanzibar; kutungwa kwa sheria moja ya Uraia; kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha ambayo itashughulikia malalamiko yote yanayohusu uchumi na fedha, n.k.

 

Pamoja na wingi wa kero zinazozungumzwa aghlabu kwa kutiwa chumvi na kwa jazba, ni heri kuzungumzia kero hizo kuliko kuzungumzia historia ya muungano uliovunjika kama ambavyo pengine tungekuwa tunafanya hivi sasa kama tungekuwa na Muungano wa Serikali Tatu.  Ni rahisi zaidi kuondoa kero kuliko kufufua muungano uliovunjika.

 

HITIMISHO

 

Imedhihirika katika hoja hii kwamba uhalali wa Muungano wa Tanzania hivi sasa si suala tena la mjadala.  Mjadala uliohamishiwa kwenye kuhoji muundo wa Serikali Mbili nao unapungukiwa nguvu kutokana na wananchi walivyothibitisha imani yao kwa muundo huo kila walipoulizwa.  Baada ya kukosa nguvu ya hoja, wapinzani wa muundo huo sasa wanategemea tu mbinu ya hoja ya nguvu; maneno mengi, makelele na jazba.

 

Muungano wenye muundo wa Serikali mbili umefaulu mtihani wa nyakati (has stood the test of time) kwa kuhimili misukosuko mikubwa na kudumu kwa miaka 40 sasa, ukiwa mfano wa pekee Barani Afrika.

 

Matatizo ya Muungano yanaweza kuwa kwa idadi kwenye orodha, lakini hayauzidi uzani wa mafanikio yake.  Na mwelekeo uliopo ni kwamba mafanikio na uimara wa Muungano vinazidi kuongezeka wakati kero zinapungua.

 

Chini ya mfumo wa vyama vingi, kila chama cha siasa kina haki ya kuwa na sera yake ya muundo wa Muungano na kuiwasilisha kwa wananchi.  Kwa upande wa CCM, sera ya muundo wa Serikali Mbili inaendelea.

 

MUNGU IBARIKI TANZANIA

REJEA

 

A.S.P. (1974); “Maendeleo ya Mapinduzi Ya Afro-Shirazi Party”; Printpak

                   Tanzania Ltd.; Dar es Salaam.

 

CCM (1994)          ; “Taarifa ya Kura za Maoni Ya Wana-CCM Kuhusu Muundo Muafaka wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”; Taarifa isiyochapishwa.

 

CCM (1998); “Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, 1977 – 1997”; KIUTA;

Dar es Salaam.

 

Mapuri, O.R. (1996); “The 1964 Revolution: Achievements and

                   Prospects”;TEMA Publishers; Dar es Salaam.

 

Mkapa, B.W, (2004); “Hotuba Ya Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa

Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Kwenye Sherehe za Kuadhimisha Miaka 40 ya Muungano”; Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali; Dar es Salaam.

 

Mdundo, Minael – Hosanna O. (1999); “Masimulizi ya Sheikh Thabit

                   Kombo Jecha”; DUP (1996) Ltd.; Dar es Salaam.

 

Mwinyi, A.H. (1995); “Hotuba ya Rais Ali Hassan Mwinyi Akiagana na

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali; Dar es Salaam.

 

Nyerere, J.K. (1968); “Uhuru na Umoja”;  OUP; Dar es Salaam.

 

Nyerere, J.K. (1994); “Uongozi Wetu na Hatima Ya Tanzania”; Zimbabwe.

                   Publishing House; Harare

 

Nyerere, J.K. (1995); “Nyufa”; Taasisi ya Mwalimu Nyerere; Dar es Salaam.

 

Othman, Haroub (2004); “Forty Years of The Union: Is It Withering

                   Away?”;  Unpublished

 

Serikali ya Tanzania (1991); “Ripoti ya Tume Ya Nyalali Kuhusu Mfumo wa

Vyama Vingi au Chama Kimoja”; Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali; Dar es Salaam.

 

Serikali ya Tanzania (1999); “Ripoti ya Kamati Ya Kuratibu Maoni Kuhusu

Katiba (Kamati ya Kisanga)”; Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali; Dar es Salaam.

 

Sherif, Abdul (1987); “Slaves, Spices & ivory In Zanzibar”; Tanzania.

                   Publishing House, Dar es Salaam

 

Shivji  I.G. (1990); “Tanzania – The Legal Foundations of the Union;

                   Dar es Salaam University Press; Dar es Salaam.