CHAMA CHA
MAPINDUZI
MADA: CHAMA CHA MAPINDUZI NA SERIKALI ZAKE WAFANYE NINI ILI KUFAIDIKA NA MFUMO WA UTANDAWAZI
Makala kwa ajili ya semina ya Wenyeviti
na Makatibu wa CCM wa Mikoa na Wilaya
Prof. D.S. KAPINGA
24 AGOSTI, 2004
_______________________________________________________________________________
“Katika kipindi kati ya
uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 na sasa, mabadiliko yaliyotokea duniani ni kuiimarisha zaidi kwa dhana ya kuwa na dunia
inayofuata itikadi moja, siasa moja,
uchumi na utamaduni mmoja ambamo dunia ni kama
kijiji”
(Ilani ya Uchaguzi Mkuu, 2000, ibara ya 8, mkazo umeongezwa).
_____________________________________________________________________________________________________________
1. UTANGULIZI
Nukuu hii kutoka Ilani ya
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2000 ina umuhimu wa pekee
katika mjadala kuhusu utandawazi na hasa maneno yaliyotiliwa mkazo. Utandawazi
unaipa dunia sura inayofanana na mahusiano katika kijiji. Teknologia ya habari na mawasiliano (teknohama)
ndiyo hasa iliyoifanya dunia iwe kama kijiji.
Katika kitabu: Jubilei ya Miaka Ishirini na Tano ya Chama cha Mapinduzi, 1977
– 2002, tunasoma:
“Uundaji wa
mazingira ya uchumi wa soko huru unafanyika katika mazingira ya utandawazi ambao sifa yake kubwa ni
ushindani katika soko la dunia ambayo kutokana na mapinduzi katika teknolojia
ya upashanaji habari (Information and Communication Technology – ICT) imekuwa
kama kijiji. Hivi sasa, wazalishaji, walaji na wadau wengine waliotenganishwa
kijiografia na makontinenti wanaweza kuwasiliana katika dakika chache
bila kuonana” (uk. 3).
Umuhimu mwingine wa nukuu
kutoka Ilani ni hii dhana ya utandawazi kama jitihada
ya nchi za magharibi kuwa na dunia inayofuata
itikadi moja, siasa moja, uchumi na
utamaduni mmoja, dhana ambayo mara nyingi haijitokezi katika mijadala kuhusu utandawazi. Soko huru
linalozungumzwa kuhusu utandawazi siyo
la fedha na bidhaa tu, bali pia siasa, itikadi, utamaduni, mawazo, fikra n.k.
Vyote hivyo havina mipaka ya kijiografia.
2. MAMBO YA MSINGI KATIKA UTANDAWAZI
2.1 Utandawazi ni mfumo
unaozipendelea nchi zilizoendelea. Na hali imekuwa hivyo tangu mahusiano na
maingiliano ya kiuchumi kimataifa yaanze zaidi
ya karne tano zilizopita. Uhusiano
kati ya nchi za Ulaya na Marekani na nchi za Dunia ya Tatu umekuwa ni wa uporaji tu. Ukoloni ndio ulioimarisha mfumo
huo wa uporaji kwa kuamua makoloni
yazalishe nini na kwa soko gani na kwa bei gani. Baada ya uhuru, hali hiyo haikubadilika; mfumo wa uchumi ulibaki ule ule.
2.2 Utandawazi ni
mfumo ambao hatuna budi kuishi nao kwa:
(a)
Kutumia
vizuri fursa unazotoa.
(b)
Kuyatumia
hata mabaya yake kwa manufaa yetu.
Tunajifunza
kuhusu utandawazi ili tutumie hata athari zake kwa manufaa yetu.
2.3 Nini kimeusukuma
utandawazi
(i)
Msukumo wa kibepari wa faida.
Uchu wa mabepari wa kupata faida umesababisha mapinduzi makubwa katika uchumi.
Soko la fedha na mitaji limekua na kujipenyeza kila
mahali, na hasa katika nchi za Ulaya Mashariki, Asia na Marekani ya Kusini.
(ii)
Maendeleo katika sayansi na teknolojia ya:-
a)
Uzalishaji na huduma
b)
Habari na mawasiliano ambayo yamerahisisha sana biashara ya fedha,
mitaji, bidhaa na huduma.
(iii)
Kuanguka kwa dola la Shirikisho la Kisovieti la Kisosholisti la Urusi
(USSR) na washirika wake (nchi za Kijamaa za Ulaya Mashariki). Kitendo hicho
kimeifanya dunia kuwa na itikadi moja, siasa ya demokrasia ya vyama vingi,
mfumo mmoja wa uchumi (uchumi wa soko) na kuenea duniani kwa utamaduni wa Marekani na washirika
wake. Nchi za Dunia ya Tatu na zilizokuwa za kikomunisti zipo katika hatua
mbali mbali za utekelezaji wa marekebisho ya uchumi, ukiwemo ubinafsishaji wa mashirika ya umma.
(iv)
Matumizi ya nguvu za kisiasa katika kuendesha uchumi wa dunia. Ilani ya
CCM ya Uchaguzi Mkuu (2000) inabaini: “….. Kutoweka kwa kambi ya Mashariki,
kuenea kwa fikra, siasa na sera za uchumi za soko, na kuimarika kwa Kambi ya
Magharibi, kumeleta mabadiliko makubwa katika diplomasia na mahusiano ya
kimataifa. Nchi za kambi ya Magharibi hazina tena woga wala haya kuyaingilia
madola mengine kwa kibali au, bila kibali cha Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa, Umoja ambao unatumiwa kama chombo cha sera za mambo ya nje ya mataifa
makubwa. Hata mabalozi wa nchi hizo
katika nchi maskini wanaingilia mambo ya ndani ya nchi hizo kwa kisingizio cha
kusimamia matumizi bora ya misaada yao. Kweli, Kujitawala ni kujitegemea” (Ibara ya 8).
Kuvamiwa na
kukaliwa kwa Afghanistan na Iraq na majeshi ya Marekani na washirika wake ni kiwango cha juu cha ubeberu
wa leo. Pia shughuli nyingi za kiuchumi husukumwa kisiasa ili kulinda na
kuendeleza maslahi yao. Kuvunjika kwa mkutano wa Shirika la Biashara Duniani
(World Trade Organization – WTO) kule Cancun mwezi Septemba 2003 kutokana na
nchi matajiri kuendelea kung’ang’ ania kutoa ruzuku kwa wakulima wao huku nchi
maskini zikikatazwa kufanya hivyo ni moja tu ya mifano ya matumizi ya hoja ya nguvu katika mahusiano ya
kiuchumi, kwani, siasa ni uchumi.
3. KWA NINI
MANUFAA YA UTANDAWAZI KWETU NI MADOGO
3.1 Uhodhi wa nchi za magharibi wa mambo muhimu ya utandawazi.
Nchi za
magharibi zinahodhi mambo yote muhimu ya utandawazi: teknolojia ya uzalishaji, huduma, habari na
mawasiliano; biashara; vyombo vya fedha; masoko ya fedha na mitaji; n.k. Nchi hizo huelekeza raslimali kule
ambako kunaleta faida kubwa. Hakuna biashara ya kijamaa.
3.2 Uwezo wetu mdogo
wa kumeneji (Kudhibiti) mabadiliko
Utandawazi ni
mchakato wa mabadiliko katika nyanja zote za mfumo wa maisha ya jamii. Menejimenti ya mchakato huo inahitaji ujuzi wa mfumo wenyewe; kuchanganua masuala yenye maslahi kwa
nchi/taifa; dhamira ya kisiasa ya
kuyakabili mabadiliko; na uzalendo.
Sisi
tunakabiliana na utandawazi katika mazingira ya uchumi tegemezi,uliyonyuma na
wa ukoloni mamboleo (Programu ya Chama cha Mapinduzi, 1987 – 2002).
Kutetereka kwa msingi wa uchumi wetu na kukithiri kwa
umaskini ni sababu kubwa ya
kushindwa kwetu kuzitumia fursa zinazoletwa na utandawazi. Kanuni ya Siasa
Uchumi inasema kwamba kama msingi
wa uchumi ukitetereka, mahusiano yote ya kisiasa na kijamii (vikolombwezo)
yanayumba: siasa, sera, utamaduni, ulinzi/usalama, sheria, mahakama, utawala
bora, n.k. Mara nyingi sana, kwa kukosa ufahamu wa chimbuko la matatizo yetu
tumekuwa tukitupiana lawama zisizo na msingi wowote, na hasa viongozi wa vyama vya upinzani.
Viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakitoa ahadi rahisi za kilaghai kana
kwamba wana dawa ya kutibu umaskini. Wanaifanya jamii iamini kuwa jukumu la
kuleta maendeleo ni la serikali na Chama Tawala, jambo ambalo siyo kweli
kabisa. Hakuna mtu anayeweza kuondoa umaskini wa mwenzake. Anaweza kusaidia tu.
Baadhi ya mambo
ambayo yamesababishwa na kuyumba kwa msingi wa uchumi wetu na athari za utandawazi ni: (i) Kuongezeka kwa watu wasio na
kazi; (ii) Kukua kwa sekta isiyo rasmi
(wazalishaji na wafanyabiashara wadogo wadogo, machinga, mama/baba lishe,
n.k.); (iii) Kuongezeka kwa uhalifu
(na hasa ujambazi wa kutumia silaha, mauaji, biashara ya madawa ya kulevya,
ubakaji, kutupa watoto wachanga, ukahaba, utapeli), (iv) ulimbukeni na kukosa uzalendo
ambako kunasababisha fedha na mali nyingi za nchi kuporwa na
wafanyabiashara na wazalishaji wa nje,
n.k. Wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje na kuigeuza nchi yetu dampo
la bidhaa hafifu kutoka nje wakati bidhaa zetu zinakosa soko ni limbukeni wasio
na uzalendo. Au watumishi wa umma wanaotia saini mikataba inayotukandamiza kwa
sababu tu ya kupewa rushwa ni
limbukeni – hawana uzalendo. (v)
Kuibuka kwa vyama vya siasa vya kitapeli
na asasi zisizo za kiserikali.
Vyama vya siasa na asasi nyingi zisizo za kiserikali (NGOs) viliibuka
ili kuikabili hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na kuyumba kwa uchumi. Vilianzishwa ili kuganga
njaa ndiyo maana hadi leo hakuna dalili
kama kweli vina lengo la kujenga demokrasia.
4. CHAMA
CHA MAPINDUZI NA SERIKALI ZAKE WAFANYE NINI ILI KUNUFAIKA NA MFUMO WA UTANDAWAZI.
Kama tulivyoeleza hapo juu, hatuna budi kuzitumia
fursa na changamoto zote kwa
manufaa yetu. Azma hiyo inaweza
kutekelezwa kwa kutumia sera, sheria, kanuni na taratibu.
Njia kuu za Chama Tawala za uongozi ni kama ilivyo katika Mwongozo wa TANU (1971):
(a)
Kutoa lengo; yaani kuandaa sera.
(b)
Kuwaandaa watekelezaji wa sera hizo; ambao ni serikali na vyombo vyake;
asasi zisizo za kiserikali; vyama na asasi za kijamii; na wananchi, wakulima,
wafanyakazi, wafanyabiashara, wanaume, wanawake na watoto.
(c)
Kusimamia utekelezaji wa sera zake (ufuatiliaji, uhimizaji, masahihisho,
n.k.)
(d)
Kupima (kutathmini) matokeo ya utekelezaji wa sera kwa lengo la kubaini mapungufu na
kufanya marekebisho ya kisera.
Majukumu hayo ya Chama Tawala bado yana
umuhimu leo kama ilivyo kuwa
mwaka 1971. Hii ndiyo tafsiri ya Chama
Kutawala/Kuongoza.
Zaidi ya majukumu hayo ya kisera, Chama
Tawala pia kina nafasi kubwa ya kuendesha elimu
ya umma (advocacy) kuhusu masuala
nyeti kama vita dhidi ya UKIMWI,
unyanyasaji wa kijinsia, mmomonyoko wa maadili
katika jamii, ajira ya watoto, n.k. Kwa
hiyo basi, kuhusu utandawazi, Chama cha
Mapinduzi kinaweza kuongoza Serikali zake kupitia
sera na jamii kupitia elimu ya umma (advocacy).
4.1 Sera kama njia ya Chama ya Uongozi.
Vyama vya TANU, ASP na CCM vimejijengea
sifa kubwa sana ya kuwa na sera safi katika nyanja zote za maisha ya
jamii na Taifa. Hatuna sababu ya
kuziorodhesha hapa. Na Serikali za CCM
zimeandaa sera mbalimbali za utekelezaji wa Mwelekeo wa CCM katika miaka ya 1990 na 2000 – 2010 na Ilani za CCM
za Chaguzi Kuu za mwaka 1995 na 2000.
Hivi sasa serikali inakamilisha Sera
ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Tume ya Dunia Kuhusu Athari za Kijamii za Utandawazi imebaini
kwamba nchi za Dunia ya Tatu (Maskini) zimeathirika sana katika maeneo
yafuatayo:
(a)
Mfumo wa dunia wa uzalishaji ambao umezifanya ziendelee kuzalisha na kuuza nje bidhaa
ghafi ambazo bei zake huendelea kushuka katika soko la dunia.
(b)
Utegemezi
wa bidhaa za viwanda na teknolojia ya kisasa katika uzalishaji na huduma.
(c)
Ongezeko kubwa la idadi
ya watu wasio na kazi, na hasa vijana.
Katika Tanzania tumefikia hali kwamba vijana wanaomaliza elimu ya juu hawana uhakika wa ajira. Kitengo cha Kuondoa Umaskini na Ajira katika
Idara ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Ustawi wa Jamii kinakadiria kuwa vijana milioni 188, wengi wao kutoka nchi
zinazoendelea wanaishi bila kufanya kazi,
au kufanya kazi za kipato kidogo (Kaale, katika Majira Jumapili, Julai 11, 2004; Tume ya Utandawazi, uk.40).
(d)
Kuwafanyisha kazi
watoto wa chini ya miaka 15, hivyo kuwakosesha elimu na kuwaingiza katika
mzunguko usio na mwisho wa umaskini na dhiki.
(e)
Athari katika utamaduni
wetu. Ingawaje Tanzania ina Sera ya
Taifa ya Utamaduni, athari za utandawazi katika jamii, na hasa kuiga tamaduni
za Magharibi, ni za kutisha. Vyombo vya
upashanaji habari na mawasiliano (redio, magazeti, hasa ya udaku, TV, intaneti,
n.k.) vimekuwa mbadala wa wazazi na watu wengine wazima katika jamii katika
malezi ya watoto. Uhuru wa kutoa maoni
umegeuka kuwa huria (anarchy) katika kutafuta habari na kutoa maoni na hasa
kuiga tamaduni za kigeni.
Kwa kiwango kikubwa, yafuatayo ama
yameletwa au kuchochewa na utandawazi:
·
mmomonyoko wa maadili katika
jamii (kutoweka kwa adabu na heshima miongoni mwa watoto, vijana na baadhi ya
watu wazima);
·
tamaa ya utajiri wa
haraka haraka ambayo imeondoa uaminifu/juhudi katika kazi na kuleta uhalifu wa
kutumia silaha, utapeli, uingizaji wa bidhaa hafifu nchini;
·
nyanja ya starehe na
burudani imetawaliwa na matendo yanayoibua hisia za ngono na kuchochea ufuska
hivyo kuyafanya mapambano dhidi ya UKIMWI kuwa kama mchezo wa kuigiza. Hata baadhi ya matangazo yenye lengo la kudhibiti
maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) yanachochea ngono kinyume na matarajio.
·
Kuibuka kwa vyama vya
siasa na asasi zisizo za kiserikali ambavyo huchochea vurugu na uvunjifu wa
sheria na mshikamano wa kitaifa.
4.2 Maeneo
muhimu kisera.
Kuhusu utandawazi, maeneo
muhimu kisera ni kama ifuatavyo:
(i) Uhusiano wa kimataifa.
Kama ilivyoelezwa, utandawazi ni mahusiano na mwingiliano wa kimataifa.
Sera ya sasa ya Taifa ya Uhusiano wa Kimataifa inakidhi mahitaji yote
muhimu ambayo yanajenga mazingira mazuri kwa Tanzania kunufaika na
utandawazi. Sera hiyo inasisitiza
umuhimu wa ujirani mwema; kukuza
ushirikiano wa kieneo (k.m. Jumuiya
ya Afrika Mashariki); kikanda (k.m. Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika SADC); na ushirikiano baina ya nchi za kusini (South – South cooperation).
Aidha, sera inazitaka ofisi zetu za
ubalozi kuwa watangazaji wa utajiri wa kiraslimali wa nchi yetu ili kuwavutia
wawekezaji, na watalii na kutafuta masoko kwa bidhaa zetu. Uhusiano wa kimataifa ulenge masoko na
vyanzo vya teknolojia ya kisasa.
(ii) Uchumi na Maendeleo.
(a) Ubinafsishaji
Jukumu katika eneo hili ni kuhakikisha
kwamba Taifa linanufaika na manufaa hayo yanawafikia walio wengi.
(b) Kupambana
na ukosefu wa ajira
Serikali zina mipango na programu
madhubuti za kuondoa umaskini. Jitihada hizo hazina budi kupongezwa.
Hata hivyo, suala la ukosefu wa ajira
halinabudi kuundiwa mkakati maalumu hasa kutokana na uhusiano wake na amani na usalama wa Taifa. Mambo ya
kisera:
·
Kuainisha ajira katika
mazingira ya Tanzania. Ajira kuu ya
Watanzania ni kilimo, siyo viwanda. “Siasa ni Kilimo” (TANU, 1972).
·
Kuwahamasisha
wanaojiajiri (kwa kuwapunguzia kodi, mikopo yenye riba nafuu).
·
Kuwashirikisha vijana wenyewe kutaka kubuni na kupanga
mikakati ya ajira.
Kaale (kama hapo juu) anamnukuu Katibu wa
Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Ajira kwa Vijana (Youth Employment Network –
YEN), Bw. Steve Miller akisema:
“Kwa mujibu wa makubaliano ya nchi
wanachama wa Umoja wa Mataifa kila nchi itaunda mtandao wa ajira kwa vijana utakaojumuisha Taasisi za
Serikali, Mashirika ya Kimataifa,
Taasisi za Elimu, vikundi vya vijana, wasomi, sekta
isiyorasmi, taasisi za fedha, asasi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari na wadau wengine
wakereketwa wa maendeleo ya vijana.”
Tanzania imekwishaunda Mtandao wa Taifa
wa Ajira kwa Vijana. Lakini, ili vijana
washiriki katika mtandao huo, wanahitaji hali ya utulivu wa kisiasa na kuamini kwamba suala hilo halina mfungamano
na itikadi za kisiasa.
Mchakato wa kupambana na tatizo la ajira
hauna budi kwenda sambamba na mapambano dhidi ya ajira ya watoto.
·
Kuheshimu haki za wafanyakazi
Tangu enzi za kupigania uhuru, vyama vya
TANU, ASP na sasa CCM vilikuwa na
mfungamano mkubwa na wafanyakazi
kupitia vyama vyao.
Ingawaje utandawazi unarembwa na lugha ya
mapinduzi ya demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria, haki za binadamu, na
kadhalika, katika hali halisi ni mfumo wa kibabe na dhuluma. Baadhi ya waajiri huwapiga marufuku
wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi.
(c) Uzalishaji na Utoaji Huduma
Mwelekeo
wa sera za CCM katika Miaka ya 2000 hadi 2010 umetamka kwamba Modenaizesheni
ndiyo mkakati wa ujenzi wa msingi
wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea (Ibara ya 20). Mkakati huo pia utaongoza maendeleo katika miundombinu ya kiuchumi na kijamii.
Katika suala la uzalishaji wa bidhaa za
kuuza nje (hata ndani), mambo ya kuzingatiwa ni:
·
kuuza bidhaa
zilizosindikwa badala ya bidhaa ghafi.
·
Aina za mazao. Kuzalisha kwa wingi mazao yenye bei kubwa
kwenye soko.
·
Ubora wa mazao. Ushindani mkubwa katika soko la dunia
unahusu ubora wa bidhaa.
·
Kuangalia mwenendo wa
bei katika soko la dunia. Haileti faida
kuzalisha mazao ambayo yana bei ndogo.
·
Utafutaji wa masoko
mapya na kuwa na mikataba ya ununuzi na uuzaji.
(d) Katika miaka ya 1970 na 1980, Tanzania
ilikuwa na sera ya maendeleo ya viwanda.
Viwanda vinavyozalisha bidhaa muhimu kama chuma, kemikali, ngozi,
karatasi, viatu na hata nguo vingi vimefungwa.
Ingawaje kwa hivi sasa kilimo ndiyo sekta kiongozi, viwanda
ndivyo vitakuwa mhimili wa uchumi wetu.
Kilimo cha kisasa kinategemea sana mazao ya viwandani. Kukuza
viwanda vya msingi vya kuzalisha mashine na vifaa kunahitaji chuma. Chuma Cha Mapinduzi hakina budi kuwa na sera
kuhusu uchumbaji wa makaa ya mawe na chuma.
(e) Masuala mengine ya kiuchumi
·
Uchimbaji wa madini;
·
Utalii;
·
Uvuvi na biashara ya
nje ya samaki;
Vyote hivyo vilenge kulinufaisha Taifa na
siyo kuwatajirisha wawekezaji tu.
(f) Huduma za
Jamii
Katika huduma za jamii, Mwelekeo wa sera za CCM katika Miaka ya
2000 hadi 2010 unaweka mkazo mkubwa katika maendeleo ya Elimu, na hasa sayansi na teknolojia
(ufundi). Mkazo uwe katika utafiti ambao utaongeza ufanisi na tija katika nyanja zote za uzalishaji na utoaji huduma. Mapinduzi katika elimu, na hasa sayansi na
teknolojia yametiliwa mkazo sana na Tume ya Utandawazi.
Hivi sasa, utafiti katika vyuo vikuu hufadhiliwa na wahisani. Wahisani hao huchagua hata aina ya utafiti na wapi ufanyike. Lazima tujikwamue kutokana na utegemezi wa aina hii unaozaa wataalamu tegemezi hata katika kufikiri.
(g) Utawala
bora
Utawala bora unaojali haki za binadamu na
kwamba kila raia ni sawa mbele ya sheria, unaoheshimu uhuru wa mahakama na
unaopambana na maovu kama rushwa,
unaelezwa kuwa msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kwamba, bila utawala bora, hakuna maendeleo.
Hakuna ubishi kwamba serikali ya Tanzania
inazingatia misingi yote ya utawala bora.
Rais mwenyewe ni Waziri wa Utawala Bora akisaidiwa na Waziri wa
Nchi. Pia, serikali inaandaa sera ya haki za binadamu.
4.3 Utandawazi
na kupungua kwa madaraka na mamlaka ya serikali.
Taarifa ya Tume ya Dunia kuhusu Athari za kijamii za Utandawazi imebaini
kwamba mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ndani ya utandawazi yamepunguza sana
mamlaka na madaraka ya serikali katika nchi zinazoendelea ambayo ni muhimu sana
katika kuunda na kusimamia utekelezaji wa sera. Mamlaka na madaraka ya serikali yamepunguzwa na:
·
“kujitoa” kwa serikali
katika kuendesha uchumi.
·
Makelele ya vyama vya
upinzani ambavyo havina sera lakini vina uchu
wa kutawala.
·
Asasi zisizo za
kiserikali ambazo zinajipa sauti ya kisiasa kwa ruzuku kutoka nje. Hakuna aliyepima mchango wa asasi hizo
katika maendeleo ya jamii hasa ikilinganishwa na fedha wanazopewa na wahisani,
pengine kwa shabaha za kisiasa.
·
Kampeni za wanasiasa na
asasi mbalimbali zisizo za kiserikali hasa kuhusu haki za binadamu, utawala wa
sheria ambazo zimepandisha kiwango cha utambuzi wa jamii (social consciousness)
baina ya wananchi wengi; hali inayochochea maasi
dhidi ya sheria, kanuni na taratibu.
Kwa mfano, vyama vya siasa kudai mabadiliko
ya Katiba (kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi) kwa njia ya maandamano ambayo
ni mamlaka na madaraka ya Bunge.
Serikali hazina budi kulinda haki zake za utawala wa nchi. Wanaotaka kutawala wasubiri wapewe ridhaa na
wananchi. Serikali ina kazi moja
tu: kutekeleza sera na Ilani ya CCM.
4.4 Chama na Usimamizi, ufuatiliaji wa
utekelezaji wa sera zake.
Ingawaje
mara nyingi kuna pengo kati ya sera na utekelezaji wake, vyama vyetu havina
sifa nzuri sana katika suala la usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa
sera. Hali ilikuwa hivyo wakati wa
mfumo wa chama kimoja. Ingawaje vyama vya TANU, ASP na CCM vilisimamia
utekelezaji wa sera zake moja kwa moja,
bado mapungufu yalikuwa mengi. Sera
zilibadilishwa hata bila
kufanyiwa tathmini ili kubaini mafanikio na matatizo.
Baada ya kuingia katika mfumo wa vyama
vingi, sasa usimamizi hufanywa na vyombo
vya uwakilishi ambavyo hata wakati wa mfumo wa chama kimoja vilifanya kazi hizo hizo. Vyombo hivyo ni Bunge, mabaraza ya maendeleo
ya kata, halmashauri za wilaya, miji, manispaa na jiji.
Kwa maoni yetu, Chama Tawala hakiwezi
kubaki na jukumu la kuunda sera na
kuviachia vyombo vingine kazi za maandalizi
ya umma, usimamizi na tathmini. Wakati wa utekelezaji wa Siasa ni Kilimo (TANU, 1972), uhamasishaji ulioongozwa na
kusimamiwa na Chama uliongeza uwingi na
ubora wa mazao ya chakula na biashara.
Serikali na vyombo vya uwakilishi haviwezi
kuwa mbadala wa Chama Tawala katika maandalizi ya umma, usimamizi na
tathmini ya utekelezaji. Wala chama hakiwezi kuwa karibu na wanachama
na wananchi isipokuwa kupitia kazi za
kisiasa za maendeleo, ustawi wa jamii, ulinzi na usalama. Chama cha Mapinduzi kisipofanya hayo, vyama
vya upinzani vitaziba pengo. Wapinzani
wanatoa madai ya kipuuzi kwamba viongozi wa CCM (wakiwemo wabunge) hawajafanya
kitu kwa sababu viongozi wa CCM hawasemi
Chama na Serikali zake wamefanya nini.
5
MAMBO MENGINE MUHIMU KATIKA UTANDAWAZI.
5.1 Uwezo wa majadiliano (negotiation)
Kunufaika na mikataba ya kimataifa kunategemea sana uwezo wetu wa majadiliano
(negotiation). Majadiliano hayo yanahitaji ufahamu wa masuala husika na msimamo wa kizalendo (kuweka mbele
maslahi ya Taifa kabla ya binafsi).
Hatuna budi kujidhatiti katika hilo.
5.2 CCM kutumia teknohama
Mtandao wa uongozi wa Chama cha Mapinduzi
unaoanzia ngazi ya shina hadi Taifa
ungenufaika sana kama ungeunganishwa na mtandao wa mawasiliano wa
kompyuta. Tunafahamu kwamba Makao Makuu
ya CCM yameunganishwa kwenye intaneti na yana tovuti yake. Jitihada ifanyike ili mikoa na wilaya kwa kuanzia iunganishwe kwenye matandao wa
kompyuta ili kurahisisha mawasiliano ndani
ya chama.
6. HITIMISHO
Ingawaje ni kweli kwamba utandawazi wakati wote
umezipendelea nchi zilizoendelea ambazo zinahodhi
sayansi na teknolojia, bado kuna nafasi kwa nchi zinazoendelea kunufaika na mfumo huo. Chama cha Mapinduzi kina uwezo wa kuongoza mchakato wa kuifanya
Tanzania kunufaika na mfumo wa utandawazi.
Akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Afrika, Durban, 9 Julai, 2002, Rais Benjamin Mkapa,
Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Dunia kuhusu
Athari za Kijamii za Utandawazi, alimnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
ambaye alitoa maneno yafuatayo ya Kizanaki wakati wa uzinduzi wa Tume ya Kusini tarehe 20 Oktoba, 1987:
‘Wakasusu, nihe wagya?
Nagya kwita Wanzugu.
Oragya kutura?
Ndagya Kusaya-sayamu,
Ndinukira!
Maana yake:
‘Sungura, unakwenda
wapi?
Nakwenda kumwua tembo.
Utaweza?
Ah, nitajaribu na
nitajaribu tena.
Rais Mkapa alisisitiza kwamba Nchi
za Kusini zisikate tamaa. Tunasisitiza,
tusikate tamaa.
REJEA.
1. Semboja, J., Mwapachu, J. and Jansen, E. (2002), Local
Perspectives on Globalisation: The
African Case, Dar es Salaam: Mkuki na
Nyota Publishers.
2. Mkapa, B.W. “Statement at the Launching of the National
Dialogue on the Social Dimension of
Globalisation,” Golden Tulip Hotel, 19 August, 2002.
3. URT
(2002), President Benjamin William Mkapa Speaks on the Social Dimension of
Globalisation, Dar es Salaam:
Government Printer.
4. Kent,
Bruce (1991), Bulding the Global Village, Glosgow: Harper Collins.
5. Rosenan,
James, N. “Globalization and Governance:
Bleak Prospects for Sustainability,”
In: International Politics and Society, Vol.3, 2003.
6. Shao, Ibrahim, F. (2003), “Utandawazi na Nchi Maskini,” Makala iliyotolewa kwenye Semina ya Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Zanzibar 14/1/2003.
4.
Kapinga, D.S. (2003),
Globalisation: Its Evolution and
Changed Perspectives, Processed, DSI, SUA.
8. World Commission on the Social Dimension of Globalisation
(2004), A FAIR GLOBALISATION:
CREATING OPPORTUNITIES FOR ALL, Geneva: ILO.